Simulizi ya kweli: Mpaka kieleweke

Simulizi ya kweli: Mpaka kieleweke

STORY :MPAKA KIELEWEKE
MTUNZI : NIRA SAIRE
SEHEMU YA TISA

Ilipoishia.....

Nikiwa hatua chache kutoka nyumbani nikaona watu wengi sana wakiwa pale kwangu, nikashtuka na kukaza zaidi mwendo, nilipokaribia zaidi niliweza kumuona na yule paka mkubwa katikati ya wale watu..

Endelea....
Nilifika nikiwa na shauku ya kujua ambacho kinaendelea huku nikiwa na hofu pia, watu wale watanifanya nini kama uwepo wa yule paka ndiyo sababu ya kuwepo kwao pale, nilijiuliza. Mchawi ni adui mkubwa sana kwenye jamii yoyote, hakuna ambaye angeweza kunielewa kuwa nafanya jambo lile kwa nia njema kwa maana hajawahi kuonekana mchawi mwema. "Vipi jamani kwema hapa?" Niliuliza kwa sauti yenye kitetemeshi cha uoga ndani yake mara baada ya kufika na watu wote wakasitisha mazungumzo na kunipokea kwa macho. "Sio kwema sana bwana, si unajua tena mambo ya kidunia haya" aliongea bwana mmoja wa makamo kwenye lile kundi na kisha akaendelea "huyu bwana ni miongoni mwa wakazi wa eneo hili" alianza kuelezea bwana yule huku akimnyooshea kidole bwana mwingine ambaye kwa harakaharaka alionekana ana matatizo "bwana huyu, amepatwa na tatizo ambalo linafanana sana na ambalo limekupata wewe hivyo tumeelekezwa tukuone pengine tunaweza kusaidiana mawazo" alimaliza bwana yule akaweka kituo kunipa nafasi yaniingie vyema kisha akaendelea "bwana huyu amepotelewa na binti yake siku ya tatu sasa, jitihada za kumtafuta mpaka sasa hazijafanikiwa pamoja na polisi kujitahidi kadri ya uwezo wao. Mwisho tumefikia kuamini kuwa huenda amepotea kama alivyopotea mkeo na wanawake wengine wengi wenye ujauzito, sijui tunaweza kusaidianaje?" Aliweka kituo bwana yule na macho ya watu wote yakawa kwangu, muda huu mimi nilikuwa kimya nikishukuru kimoyomoyo kuwa umati ule haukuwepo pale kwaajili ya paka yule wa kichawi.. "ndugu yangu tunaomba utusaidie, niko tayari kukupa chochote kwaajili ya binti yangu...." alisema bwana yule mwenye kupotelewa na binti yake nami nikamuwahi kabla hajaongea zaidi "hata mimi sijampata mke wangu mpaka leo ndugu yangu, bado nahangaika bila mafanikio na wala sijui ni kwavipi nikusaidie" baada ya maelezo haya bwana yule alionekana kuchanganyikiwa, akasimama akitembea kama mtu ambaye anataka kuondoka lakini ghafla akanirudia "sikiliza bwana, kuna tetesi mitaani kuwa wewe umepata mbinu ya kumrudisha mkeo ndio maana hata huangaiki tena" alisema bwana yule akibaki amenitumbulia macho kama ambaye ananitaka kuthibitisha habari zile... "ni kina nani wanaeneza habari hizo, hakuna mtu ambaye amewahi kunifuatilia hata kwa kuuliza kujua habari za kumtafuta mke wangu, leo wanayajuaje hayo maendeleo? ni uzushi tu ambao wala hauna ukweli wowote" nilijitahidi kutoa maelezo yale ya kujitetea lakini bwana yule alionekana waziwazi kutoamini.. "kama utaona una chochote cha kunisaidia tafadhali nitafute, alisema huku akinikabidhi business card yake ambayo niliitupia macho haraka haraka na kujua kuwa alikuwa ni hakimu mkuu wa mahakama ya wilaya..
Umati ule ukaanza kuondoka taratibu huku nikibaki mimi na maswali mengi ambayo sikuwa na pakuyapatia majibu yake, je nilipaswa kuwaeleza watu wale juu ya safari ya kwenda Muifufu? Kwanini jamii inafikiri kuwa ninayo njia ya kumpata mke wangu? Pengine mzee Miale atakuwa amewaeleza juu ya ujio wa sauti ya Mnaro nyumbani kwake siku ile, au inawezekana ni fikra za watu tu baada ya kuona jitihada zangu za kumtafuta mke wangu zilisimama ghafla mbele ya macho yao.
Niliingia ndani nikaendelea na shughuli zangu za kawaida kisha nikaamua kutoka angalau ninyooshe miguu maana nilichoka kukaa peke yangu ndani kwa maana baba pia alikuwa ametoka.
Kabla sijatoka nikaamua tena kupaka ile dawa kwa maana nilikuwa nimeoga hivyo kuiondoa, na kuamua kuitumia safari ile kujionea ambayo yanaendelea kwa siri kwenye jamii ile.
Kumbe jamii ile ilikuwa imejawa sana na mambo ya kishirikina, hasa katika sehemu za biashara. Niliona vitu vingi sanaaa, vingine vilikuwa vikinitisha ingawa nilikuwa nikivumilia na kujifanya kama sivioni.
Nikatembea sana mpaka nikajikuta nimechoka na kuamua kukaa chini ya mti na kupumzika. Nikiwa pale nikapata wazo la kwenda kwa mzee Miale angalau nikapate kujua kama ni yeye aliyewaambia wale watu waliokuja nyumbani kuwa mimi nimepata njia ya kumpata mke wangu, nikaanza safari ya kuelekea kwa mzee Miale ambapo nilifika na kupokelewa na yeye mwenyewe, tukakaa na kuanza mazungumzo..
"Umefikia wapi kwenye jitihada zako mwanangu?" Hili lilikuwa swali la kwanza la mzee Miale ambalo sikuliona kama lilikuwa la kumaanisha kwa maana kwake na kwangu sio mbali, kama kweli alikuwa na nia ya kujua lazima angekuja na kuniuliza "bado napambana mzee" nilimjibu kwa kifupi na kisha nikahamia kwenye swala ambalo lilinileta pale "mzee kuna watu wamenitembelea nyumbani kwangu leo,..." nilianza kuongea ila mzee Miale hakuruhusu nimalizie akadakia "ninafahamu, walianzia hapa kabla ya kuja kwako" wakati mzee huyu akiendelea kuongea alikatiza paka mweusi, mbaya, na mkubwa kama yule ambaye ninaye kule nyumbani akitoka ndani kwenye vyumba kuelekea nnje ya kajumba kale kadogo, nilishangaa nikawa najiuliza kumbe mzee huyu naye ni mchawi, nilikuwa nimetoka kabisa katika mazungumzo na kumsindikiza nyau yule mbaya kwa macho akielekea nnje jambo ambalo mzee Miale aliligundua naye akaacha kuongea na kubaki akinitizama mimi, nadhani hata yeye alishangaa nimewezaje kumuona paka yule.
"hana matatizo huyo achana naye" alisema mzee yule kisha akarudi kwenye mada husika ili kulipoteza swala la paka yule "wale watu walifika mpaka hapa na lengo kubwa lilikuwa ni kujua wewe umefanikiwa kwa kiasi gani katika utafutaji wako, nami nikawajibu kuwa sikuwa nikijua lolote hivyo wakaamua kuja kwako" aliweka nukta mzee Miale. "Kwahivyo hukuwaambia jambo lingine lolote?" Niliuliza na mzee yule akatikisa kichwa kukataa nami nikabaki bila neno la ziada la kusema, nikaamua kuondoka na kurudi nyumbani kupumzika.

Ilikuwa ni majira ya saa 12 jioni ambapo nilikuwa nimejipumzisha chumbani kwangu nikiangalia filamu, nikachoka na kupitiwa na usingizi.
Katikati ya usingizi nilisikia kama kuna mtu anazungumza ndani ya chumba kile nikashtuka na kufumbua macho. Nikakutana na sura ya dada yule ambaye alitaka kuniuzia vitumbua akiwa uchi asubuhi tukashindwana akiwa amenikalia tumboni.
Dada yule alishtuka sana alipoona nimefumbua macho nadhani hakutegemea kama nitaamka, akainuka haraka na kutaka kukimbia lakini nilimvuta akaanguka chini pembeni ya kitanda nami nikaamka haraka na kumuwahi pale chini, akaniwahi na kukimbia akiuelekea ukuta huku nikimsindikiza kwa kofi zito sana la mgongo ambalo lilimfanya apepesuke ila akajikaza na kutoroka kupitia ukutani, na mimi sikusubiri nikapitia hapohapo kumfuata dada yule ambaye nilimuona kwa mbali akikimbia nami nikamfuata kwa kasi ya ajabu. Nilikuwa na kasi ambayo sikuwahi kuwa nayo kabla siku hiyo mpaka mimi mwenyewe nilijishangaa, lakini nikaendelea kumkimbiza dada yule ambaye naye alikuwa na mbio kwakweli, safari yetu ilitupeleka mpaka kwenye shule ya msingi ambayo ilikuwa jirani na dada yule akakimbia kuelekea kwenye uwanja wa shule hiyo huku mimi nikimfuata lakini nilisimama ghafla mara baada kuona kundi kubwa la watu wakiwa wamekaa wakitengeneza mduara pale uwanjani, dada yule akaenda moja kwa moja na kukaa katikati ya mduara ule huku watu wote waliokuwepo pale wakigeuza macho yao na kuangalia kule alikotokea ambako ndipo nilipokuwa nimesimama mimi. Nikaona eneo lile halikuwa salama hata kidogo hivyo nikaondoka kwa mwendo wa kasi kurudi nilikotokea. Nikitembea harakaharaka huku nikigeuka nyuma kila mara kuhakikisha kuwa sifuatwi. Nilitoka nnje ya shule ile na kushika njia kubwa ambayo ingenipeleka moja kwa moja nyumbani lakini baada ya hatua chache ilisimama gari mbele yangu ikiwa imewashwa taa kubwa na kunimulika vizuri, nikiweza kuitambua mara moja gari ile kuwa ilikuwa ya polisi.. "simama hapo mara moja" iliamuru kwa ukali sauti kutoka ndani ya gari, nami nikatii. Wakashuka askari wawili wakiwa na silaha wakawa wakija upande ule ambao nilikuwepo. Nilikuwa nimevaa suruali ya michezo na flana nyepesi lakini chini sikuwa na viatu, nitawaambia natoka wapi askari wale? Sikuwa na jibu. " wewe ni nani na unatoka wapi?" Aliuliza askari mmoja wa askari wale, akili yangu ikafanya kazi harakaharaka nikajikuta nimejibu, "natoka kumsindikiza mgeni afande" askari wale waliangaliana kwa mshangao kisha mmoja wao akauliza "unajua ni saa ngapi saa hizi?" Kwakweli hata sikuwa nikijua muda, ninachokumbuka tu ni kuwa nililala mida kama ya saa 12. Sikujaribu kujibu swali lile kwa maana nilijua naweza kuharibu zaidi. Askari mmojawapo akaangalia saa yake na kisha kusema "ni mgeni gani huyo ambaye unamsindikiza saa saba kasoro?" Duuh! Muda umeenda kiasi hiki? Nimewezaje kulala muda wote huo? Nilikuwa nikijiuliza bila hata kujibu swali la mapolisi wale.. "tunaomba kitambulisho chako" alisema askari yule mwingine, sikuwa na kitambulisho pia, jambo ambalo askari wale walilitegemea bila shaka.. "hana kitambulisho, twende naye kituoni tu huyu" alishauri askari mmoja baada ya kuona nimekuwa kimya baada ya kuombwa kitambulisho. "Jamani mimi ni mtu mwema, haina...." kabla sijamalizia sentensi yangu askari yule akafoka "unatufundisha kazi? Twende kituoni" nikabaki nimeduwaa, sikuwa na neno lolote la kusema.. "bwana tunaenda ama umegoma?" Aliuliza askari mmoja, ikanibidi kukubaliana na matakwa yao. Tukaongozana mimi nikitangulia, wao wakifuata nyuma hadi kwenye gari yao ambapo tulipanda na kuelekea kituoni.
Tulifika, wakanichukua maelezo na kuniweka mahabusu. Muda huo niliweza kukadiria kuwa ilikuwa majira ya saa saba na nusu, nikajiuliza itakuwaje kama Mnaro atanifuata kwa ajili ya muendelezo wa mafunzo yetu? Sikuwa nikitaka kupoteza hata siku moja. Nikaamua kuwa niondoke kupitia ukutani, nikafanye ya kufanya usiku huo kisha nirudi mahabusu mule kabla hakujakucha. Nikatoroka na kuelekea nyumbani ambapo nilijilaza na kumngojea Mnaro kwakuwa sikua hata nikijua namna ya kumpata, ilikuwa ni lazima aje yeye kama ulivyo utaratibu wetu siku zote.
Niliendelea kujilaza pale mpaka usingizi ukanipitia ambapo nilikuja kushtuka mlango wa chumba changu ukigongwa. Nilikurupuka na kuangalia saa ya ukutani pale chumbani ambayo ilionesha kuwa ilikuwa saa mbili na dakika kumi asubuhi.. "khaaaaaa" nilihamaki sana baada ya kugundua kulikuwa kumekucha bila kurudi mahabusu..

Usikose sehemi ya kumi.

Kwa maswali, maoni, ushauri au biashara.. unaweza kunipata kupitia:
+255653686008
nirasaire@gmail.com
 
STORY : MPAKA KIELEWEKE
MTUNZI : NIRA SAIRE
SEHEMU YA KUMI

Ilipoishia...

Nikatoroka na kuelekea nyumbani ambapo nilijilaza na kumngojea Mnaro kwakuwa sikua hata nikijua namna ya kumpata, ulikuwa ni lazima aje yeye kama ulivyo utaratibu wetu siku zote.
Niliendelea kujilaza pale mpaka usingizi ukanipitia ambapo nilikuja kushtuka mlango wa chumba changu ukigongwa. Nilikurupuka na kuangalia saa ya ukutani pale chumbani ambayo ilionesha kuwa ilikuwa saa mbili na dakika kumi asubuhi.. "khaaaaaa" nili hamaki sana baada ya kugundua kulikuwa kumekucha bila kurudi mahabusu.

Endelea....
Nilikurupuka nikaenda moja kwa moja na kufungua mlango. Alikuwa ni baba akiniamsha na kunipa taarifa juu ya mama yangu kuumwa, alisema mama alikuwa amelazwa akiwa na hali mbaya sana. Tukakubaliana kuwa yeye aondoke kwenda kumuuguza mama huku akiniacha mimi nikiendelea na jukumu la kumtafuta mke wangu, baba akaondoka.
Nilibaki pale ndani nikijiuliza cha kufanya juu ya kutoroka kwangu mahabusu, mpaka sasa lazima watakuwa wamegundu kutokuwepo kwangu, lazima watakuwa wameshangazwa na jambo lile kwa maana niliondoka nikiacha chumba kile cha mahabusu kikiwa kimefungwa kama ambavyo walikiacha. Je nirudi mahabusu? Lakini nitawaeleza nini iwapo watanikuta mule ndani wakati wamegundua tayari kuwa sikuwepo?
Au niache tu kwenda? Hili pia ni jambo gumu kwa maana nilitoa maelezo yote kunihusu mimi, tena kwa usahihi kabisa, hivyo wana uwezo wa kunipata iwapo watanihitaji.. niliendelea kujiuliza maswali mwisho nikaamua kutoenda mahabusu, liwalo na liwe kwanza serikali haiutambuwi uchawi, niliwaza.
Nilipumzika pale nyumbani mpaka majira ya saa tano asubuhi kisha nikaamua kwenda benki nikatoe pesa kwa maana nilikuwa karibu kuishiwa.
Nikatoka na kwenda benki, nikachukua pesa na kisha kuamua kuingia kazini angalau nikawaone watu wangu kwa maana sasa ulikaribia mwezi toka niombe likizo ile ya bila malipo.
Nilifika kazini nikakutana na wafanyakazi wenzangu, tukaongea mengi huku wengi wakinipa pole na kunitaka nirundi kazini. Kwa muda ule mfupi wa kuongea na wafanyakazi wenzangu nilijikuta nikipata ari ya kufanya kazi. Ninaweza kufanya kazi na mambo mengine yakaendelea, isitoshe mchana nakuwa bila kazi kwa maana mambo mengine hufanyika usiku, niliwaza na kufikia maamuzi kuwa nirudi kazini.
Nikaamua kwenda kwenye ofisi ya mkuu wa kitengo ili kuzungumza naye juu ya kurudi kwangu kazini. Tukaongea na kukubaliana, kisha nikabaki tukiongea mengine kuhusu maisha kwani alikuwa rafiki yangu pia. Tulipomaliza maongezi nikatoka nikikusudia kwenda nyumbani lakini secretary wa mkuu wa kitengo akanipa taarifa "kaka Abuu, kuna wageni wako mapokezi" wageni wangu mapokezi? nani anaweza kuwa mgeni wangu ikiwa sikuwepo kazini kwa muda wote huu?, nilijiuliza huku nikielekea mapokezi kuonana na hao wageni wangu.
Sasa nilikuwa nikiutizama mlango wa mapokezi lakini kabla sijaingia ndani akili ikaniambia nimeingia mtegoni, nilipokamatwa na polisi niliwapa maelezo yote kunihusu ikiwa ni pamoja na mahala pangu pa kazi, kivyovyote baada ya kutoroka sehemu ya kwanza kutafutwa ingekuwa hapa kazini kwakuwa hawana taarifa kuwa sipo kazini.
Baada ya kupata wazo hilo nikaamua kugeuka haraka ili kutoka nnje ya ofisi lakini nilikutana na askari polisi akiwa ndani ya sare "bwana Abubakar Saire uko chini ya ulinzi" niliishiwa nguvu, mwili ukanyong`onyea na kujuhisi kama sina uzito. Askari yule akaja na kunitaka kumpatia mikono yangu kisha akanifunga pingu na kuwaita wenzake kwa simu nao wakaja kutokea mapokezi, safari ya kuelekea kituoni ikaanza huku wafanyakazi wenzangu wakibaki wamepigwa na butwaa wasielewe nimefanya kosa gani la kuwindwa na polisi.

Tulifika kituoni nikaingizwa mahabusu, lakini kilikuwa ni chumba tofauti na kile ambacho niliingizwa mwanzo.
Nilitamani sana kutoroka mule mahabusu ila nilishindwa kutoka kutokana na kutokuwa na vijiti vile ambavyo vingeniwezesha kupenya kichawi.
Nikakaa humo kwa nusu saa kisha wakaja askari watatu na kuanza kunihoji, askari wale walikuwa wakiamini kuwa kutoroka kwangu kituoni pale kulitokana na kusaidiwa na askari mmojawapo mule ndani na walikuwa wakitaka kumjua askari huyo "bwana, sisi unachotaka kujua ni kimoja tu, nani alikusaidia kutoka mahabusu na si kingine chochote" alisema askari mmoja ambaye alikuwa akizungumza lafudhi ya Kihaya na alionekana mwenye roho ya kikatili.
Kwa haraka haraka sikuwa na jibu la kutoa nikabaki nikiwaangalia tu kitendo ambacho walikitafsiri kama dharau. "Tumewahi kukutana na wajeuri kuliko wewe lakini walitii bila kupenda, hakuna ambaye huingia humu akaacha kutupa habari ambazo tunazitaka" alisema askari yule Muhaya akionekana amekasirika, "kwanini mpaka uumizwe? Bora useme mapema tu kwa maana kusema lazima utasema" aliongea askari mwingine lakini bado niliendelea kuwa kimya, niwajibu nini sasa? Kuwa nilitoroka kichawi? Kwanza hawawezi kuniamini, niliwaza.
Ghafla nilizabwa kofi kali la shavuni na yule askari ambaye hakuwa ameongea chochote toka ameingia mule ndani, lilikuwa kofi zito kiasi kwamba sikuamini kuwa lilitoka kwa askari yule ambaye nilimuona kuwa alikuwa mpole kuliko wale wengine, ama kweli umdhaniae ndie kumbe siye. Damu zilikuwa zikinitoka puani kutokana na kofi lile ambalo lilinifanya pia Nikapatwa na kizunguzungu cha hali ya juu. "Uko tayari kusema ama show iendelee?" Aliuliza askari yule ambaye aliyenizaba kofi ambaye alikuwa ni mdogo wangu kiumri, lakini kwa mara nyingine nilikuwa kimya akanizaba kofi lingine kali mpaka nihisi harufu ya damu kisha akanibaki akinikazia macho kama ambaye anangoja nitoe majibu lakini sikuwa na chakusema, nikamuona akinyanyua mkono wake ili kuninasa kibao kingine nikasimama na haraka huku nikikinga mikono kuzuia kofi lile zito ambalo lilitua juu ya mikono yangu.. askari wale wote watatu wakanikabili kunidhibiti kila mmoja akipiga alipopaona mpaka nikaanguka chini.
Askari mmoja akatoka na kurudi mara moja akiwa amebeba kiti cha mbao na kamba, wakaninyanyua na kunikalisha kitini kisha wakanifunga wakinishikanisha vyema na kiti kile kutia mikono yangu ambayo ilizungushwa nyuma ya kiti na kukazwa na kamba vizuri kisha miguu nayo ikafungiwa viziri kwenye miguu ya mbele ya kiti kile.
"Tunakuuliza kwa mara ya mwisho, nani alikutorosha kituoni jana" aliongea askari ambaye sasa nilimgundua kuwa alikuwa miongoni mwa wale ambao walinikamata usiku na kunileta pale kituoni kabla sijatoroka kichawi..
Nilitamani kujieleza ili adhabu ile iondoke lakini nini niseme ndio tatizo ambalo sikujua kulitatua.
"Endelea afande" alizungumza askari aliyenifunga kamba baada ya kuona sitoi maelezo na askari yule mtaalamu wa kupiga makofi akanisogelea tayari kwa muendelezo wa adhabu ile..
"NGOJENI JAMANI NASEMAAA" nilijikuta nikisema kwa sauti kubwa yenye hofu ndani yake.. "kusema tunajua utasema tu unataka ama hutaki" alisema askari yule mdogo lakini katili huku akinizaba kofi lingine zito nikajihisi kuchanganyikiwa.. "haya sema sasa" aliamuru askari mwingine, wakati huu damu zilikuwa zinazidi kutoka puani, na mdomo wangu wa chini ulikuwa umevimba kutokana na kupatwa na kofi mojawapo, lakini nilijikaza nikaanza kujieleza harakaharaka kabla askari yule asiyerudi nyuma akiamua kupiga hajaamua tena.. "jamani mimi nilitoroka kichawi, nilipenya kwenye ukuta" nilijieleza lakini kama ambavyo nilitegemea askari wale hawakuniamini, waliangalian, wakacheka kisha wakanirudia "wewe ni mchawi? toroka sasa uende" alisema askari mmoja kimzaha huku wenzake wakicheka.
Askari wale waliona kama nimepania kutomtaja ambaye alinitorosha hivyo wakaamua kunining`niniza kweye kamba ambayo iliifunga mikono yangu ikiiunganisha pamoja na kisha askari yule mpenda kupiga akawa ananishindilia ngumi nzito za tumbo huku akisema mchezo ule ungesita iwapo nitawaeleza nilitorokaje mahabusu..
"Kama hutomtaja ambaye alikusaidia kutoka mahabusu utakufa kwa adhabu humu ndani" alisema askari ambaye alionekana yeye ndiye mwenye kuagiza wenzake lakini yeye hakuwa akifanya chochote zaidi ya kuongea.
"Kwanini unaacha niteseke ikiwa unajua ni wewe ambaye ulinitorosha, nirudishie pesa zangu basi" niliropoka kumwambia askari yule akabaki mdomo wazi huku askiri aliyekuwa akinipiga akisitisha zoezi ya kumgeukia askari mwenzao, wakawa wanamtazama bila kusema neno naye akagutuka na kutaka kuniamia lakini wenzie walimdhibiti wakamtoa mule chumbani.. "kumbe tunapoteza muda ikiwa unajua ulichokifanya" alisema askari yule aliyekuwa akinipiga wakati wakimvutia nnje askari mwenzao ambaye nilimvika kesi isiyomuhusu ili mimi nipumzike na kipigo kile.
Nikabaki pekeyangu kwenye chumba kile ambacho niligundua kuwa kilikuwa cha mateso, huku nikiwa nimening`inizwa kwa kamba nikiwa na maumivu makali.
Nikawa nikiwaza juu ya hatma yangu, nilitamani kutoroka lakini sikuwa na vifaa, Mnaro pia sikuwa nimemuona toka nipatwe na matatizo yale ya polisi na sikujua kama alikuwa anajua kama nilikuwa polisi. Mipango ya kumkomboa mke wangu itafanikiwaje kwa mimi kiwemo mule ndani, na roho iliniuma sana na nikauchukia uchawi kwakua haukua na chakunisaidia.

Baada ya kama dakika ishirini aliingia askari yule mwenye lafudhi ya Kihaya akanifungua na kunihamishia kwenye chumba kile cha mahabusu ambacho nilitoroka. "Tulikuwa tunajua yule bwana ndiye ambaye atakuwa amekutorosha, hatukua na ishahidi tu, ila hakuna askari mwingine angeweza kufanya kitu cha aina hiyo hapa" alisema askari yule akinibwaga chini, nikagumia kwa maumivu ya tumbo.. "ungetueleza haraka wala yasingekupata hayo, sisi tulikuwa tunamtaka mpumbavu huyu ambaye anataka kututia matatizoni kwaajili ya tamaa zake, alisema askari yule huku akiondoka..
"Sasa nini hatma yangu afande?" Nilimuuliza polisi yule naye akajibu "tunawapeleka mahakamani kesho, wewe ni mshtakiwa namba moja na huyo mwenzio ni mshtakiwa namba 2" alisema askari yule akatoka nnje na kuniacha nikimuonea huruma polisi yule ambaye nimemsababishia matatizo.. lakini sikuwa na jambo la kufanya zaidi ya lile, pengine mpaka sasa ningekuwa bado napigwa. Niliwaza.
Mida ya saa 8 wafanyakazi wenzangu wawili walikuja kiniona wakaniletea na chakula. Walijaribu kuniwekea dhamana nitoke ila ikashindikana, ikanibidi kulala pale bila mpango wowote juu ya kutoka kwangu.

Asubuhi tulipelekwa mahakamani nikiwa na askari yule ambaye nilimvika kesi, tukasomewa kesi ya kujaribu kutoroka nguvuni mwa polisi, tukakana shtaka..
Nilishangaa kukuta hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi yetu akiwa yule bwana ambaye alinijia nyumbani akiwa amempoteza binti yake na kuniachia business card.
Baada ya kukana shtaka tukapelekwa kwenye mahabusu ya gereza kuu huku tukipangiwa kesi ile kusikilizwa tena baada ya wiki mbili.

Niliyaona maisha ya jela yakiwa magumu ndani ya siku moja tu. Nilikuwa nimekaa muda mrefu, tena chini mpaka makalio yakawa yanauma sambamba na maumivu ya kipigo cha kule polisi hali ikawa mbaya. Nilijiona wazi wazi kuwa siyawezi maisha ya mule gerezani.. wiki mbili za kuwemo mule mpaka siku ya kusomwa tena kesi nilianza kuziona kama mwaka mzima.

"Abubakar Saireee, kuna mgeni wakooo" ilikuwa ni sauti ya askari ikinishtua kutoka katikati ya dimbwi kubwa la mawazo. Nikasimama na kumfuata askari yule..

Usikose sehemu ya 11

Kwa maswali, maoni au ushauri. Unaweza kunipata kupitia:
+255653686008
nirasaire@gmail.com
 
Back
Top Bottom