STORY: MPAKA KIELEWEKE
MTUNZI: NIRA SAIRE
SEHEMU YA SABA
ILIPOISHIA........
“huu ni mwezi wa 6, mwezi ambao Mgugi huchagua mke mwingine kila mwaka, mwaka huu kuna uwezekana mkubwa sana wa mkeo kuchaguliwa kwa maana Magugi ameonesha waziwazi kuwa anavutiwa naye” alielezea Mnaro habari ambazo sikutamani kuzisikia katika maisha yangu yote, nikajikuta napatwa na wasiwasi mara kumi zaidi ya ambao nilikuwanao.
“aisee hawezi kuthubutu kumchukua mke wanguuuuu! Sitokubaliiiii” nilisema kwa uchungu lakini Mnaro aliniangalia kisha atabasamu na kusema “akiamua huna jinsi ya kuzuia hilo, kama kungekuwa na njia basi mimi ningekuwa wa kwanza kumzuia asinipokonye Sauda wangu”.........................
pamoja na kuumizwa sana na kauli ile nilijitahidi kuvumilia kwakuwa nilikuwa najua fika hali ya kutokuwa mvumilivu ingenirudisha nyuma kama ambavyo imetokea mara kadhaa ninapokuwa na bwana Mnaro, safari hii nikafanikiwa na kushusha kabisa hasira nilizokuwanazo na kuonesha utulivu ambao najua hata Mnaro mwenyewe hakuutegemea. “tunafanyaje sasa? Nadhani muda wa kwenda Muifufu umefikia, hatupaswi kumuacha huyo Magugi aendelee kufanya atakacho, ni bora kumuwahi mapema kwamaana kadri muda uendavyo na yeye anajipanga” nilianzisha upya maongezi ili kumshawishi bwana yule nikijaribu kuonesha utulivu wa hali ya juu ili nisionekane mwenye kukurupuka.
“ni muda muafaka wa kwenda Muifufu sikatai, ila jambo la msingi zaidi ni wewe kujifunza mbinu ambazo zitakuwezesha kuwa salama ndani ya Muifufu, kama ambavyo nilikueleza awali itakubidi kuwa mchawi, na sasa niko tayari kuanza kukufundisha mbinu hizo” aliweka kituo akanitizama nami nikauliza kwa shauku “ni lini tutaanza sasa mafunzo hayo” naye akanijibu “muda wowote ukiwa tayari, hata leo kama ukitaka” nikajikuta nimeingiwa na faraja moyoni mwangu na matumaini ya kumpata mke wangu yakanijia tena kwa kasi kubwa “mafunzo haya yatatuchukua muda gani mpaka kuyamaliza?” niliuliza tena ili kujua ni muda kiasi gani ulikuwa umesalia mpaka safari ya Muifufu. “hiyo inategemea kasi yako ya kuelewa, siku tatu zinaweza kutosha kama una kasi nzuri, lakini kama huna kasi ya kutosha inaweza kutuchukua miaka” kitu pekee ambacho nilikua nikikitaka kwa wakati ule ni kwenda mahali alipo mke wangu kwa gharama yoyote kuingia kwenye mafunzo ya uchawi sikuona kama ni tatizo na nikaamini haitonichukua muda kufuzu mafunzo hayo kwa maana siku zote penye nia pana njia “naomba tuanze leo hayo mafunzo” niliomba na Mnaro akakubali na kunitaka nijiandae kwa jambo hilo usiku wa siku hiyo kisha akaondoka.
Niliendelea kujipumzisha pale kitandani baada ya kuangalia muda na kuona ni saa moja tu toka tuingie kupumzika na kuona haukuwa wakati muafaka wa kuongea na baba yangu juu ya jambo lile baadala yake nilipaswa kumuacha apumzike huku na mimi nikijipatia nafasi ya kupumzika zaidi nikiamini kazi ya usiku wa siku hiyo itakuwa sio ya kitoto, na kweli usingizi ulinichukua kama ambavyo nilitaka.
Nilifumbua macho kutoka kwenye ndoto ambayo nilikuwa nikiota kuwa Mnaro ananiita na kweli nikamkuta akiwa amesimama kando ya kitanda changu pale chumbani.. “amka haraka tuwahi kabla hakujapambazuka, na leo itakuwa mara ya mwisho kukufuata itabidi uwe unakuja mwenyewe mafunzoni” alisema Mnaro ambaye alikuwa amevalia kivazi mfano wa nguo ya ndani ila kilikuwa kimetengenezwa kwa ngozi, alikuwa ni karibu tu na mtu aliye uchi. Nikawa naomba kimoyomoyo mafunzo hayo yasiwe ya uchawi ule wa kutembea uchi ambao huwa nausikia.
Alinipa kitu kama kijiti kidogo mithili ya njiti ya kibiriti akanitaka nikishike kwa kukibana katika kidole changu cha mwisho cha mkono wa kushoto na kisha kuniambia “ukiwa umekibana kijiti hicho namna hiyo unaweza kupenya kupita hapa ukutani na kutokea nnje, unatakiwa tu kuhakikisha mlango umefungwa kwa maana ukiwa wazi hauwezi kupenya, jambo lingine ni imani, unatakiwa kuamnini unachokifaya vinginevyo uchawi huwa unashindwa kukusaidia” niligeuka na kuangalia mlango wa chumba changu na kuona ukiwa umefungwa, ikabaki tukio la kupenya kupitia ukutani kutoka nnje ya nyumba! “Basi wacha nimuage baba maana anweza kuamka akanikosa kisha akapatwa na wasiwasi” nilitoa ombi nikianza kuongoza kuuelekea mlango wa chumba changu “hapana, haina haja. Lengo la uondokaji wa aina hii ni kumfanya mtu anayebakia kutojua kama haupo, ataendelea kukuona ukiwa umelala palepale mpaka utakaporudi” alielezea Mnaro maelezo ambayo yalinishangaza sana “vipi kama ataamua kuniamsha sasa? Si nitashindwa kuamka na kumtia wasiwasi uleule?” niliuliza swali lingine ambalo nalo alilijibu “unatakiwa kunuia ambavyo unataka mambo yatokee ukiwa haupo, kwa mfano unaweza kunuia kuwa iwapo mtu ataingia chumbani asikuamshe naye atakuwa mzito kufanya uamuzi wa kukuamsha na kuamua kukuacha ulale” niliyaelewa vizuri maelezo yake lakini nilishangaa kwanini anakwepa sana wazo la kumuaga baba hali ya kuwa hili sio jambo la siri kwake kwamaana anaijua mipango inayoendelea “kwani kuna ubaya wowote kama nikimuaga?” niliamua kuuliza baada ya kushindwa kujipatia mwenyewe najibu ya maswali yangu.. “wachawi huwa hawaagi wanapotoka kwaajili ya kwenda kwenye shughuli za kichawi, mafanikio huwa sio makubwa kwenye safari kama mchawi ataaga” nilimuelewa na kuamua kufanya kama ambavyo likuwa akiniagiza. “kibane vizuri hicho kijiti kisha upite hapo utokee nnje” alinielezea Mnaro akinioneshea kwenye ukuta wa chumba kile, nami nikatembea polepole kuelekea kwenye ukuta ule nikiuvaa polepole kuona kama utaniruhusu kupita baadala yake nilijikuta nikijigonga ukutani, sikufanikiwa kupenya. Nikageuka na kutizama Mnaro ambaye alikuwa akitikisa kichwa kusikitika “nimekwambia mambo mawila ambayo ni lazima yatimie ili uweze kupenya, kwanza mlango uwe umefungwa na pili uamini ambacho unakifanya, lakini wewe umeusogelea ukuta huo kwa wasiwasi mkubwa na nilijua tu kama hautofanikiwa” aliongea Mnaro na kisha akaendelea “haya bwana mimi nakuacha, kama kweli unataka kwenda kwenye mafunzo leo utaniwahi, ukinikosa hapo nnje ujue nimeshaondoka tayari” baada ya kusema hayo alitembea kwa mwendo wa kawaida akauvaa ukuta ambao ulimpokea na akapotea pale chumbani, nikapatwa na hofu ya kuchwa pale na kushindwa kupiga hatua kuelekea kumkomboa mke wangu kwa mara nyingine, nikajikuta nimepatwa na ujasiri wa ajabu kisha nikakibana vizuri kijiti kile katika kidole kile cha mwisho kisha nikauvaa ukuta ule kwa mwendo wa kasi sana, nilijikuta nimepita kupitia ukuta ule kama vile ulikuwa ni pazia na nikajikuta nnje ya nyumba ile, Mnaro alikuwaa amesimama mbele yangu akiwa amepanda juu ya paka mkubwa sana na pembeni yake alikuwepo paka mwingine mweusi sana na mkubwa kama yule wake, paka wale walikuwa na macho mekundu sanaaa na walikuwa waanatisha kwa kweli ila nilijikaza sana nikatembea kuelekea pale alipo Mnaro “usafiri wako huo hapo” alisema Mnaro akinionesha paka yule ambaye sikuwa nikitamani hata kumuangalia, lakini nikajikaza na kusogea mpaka karibu ya paka yule nikabaki nimesimama bila kusema lolote kwa maana hata sikujua pakuanzia nikawa nikingojea muongozo wa Mnaro. “ unangoja nini? Panda twende” Mnaro aliongea nami nikabaki nikiwa na bumbuwazi kwa maana paka yule alikuwa ni mkubwa sana na sikuona namna gani naweza kupanda mpaka juu ya paka yule! “mvute shingo yake chini atashuka na utaweza kupanda” Alielekeza Mnaro baada ya kuona nimebaki nikiwa nashangaa bila kujua cha kufanya, nami nikanyoosho mkono wangu juu na kuanza kuvuta shingo ya paka yule nikiwa nimefumba macho kwa uoga. Haikuwa kazi rahisi kama ambavyo nilidhani, paka yule alikuwa kama ambaye anapingana na nguvu ya mimi kumvuta chini na alionekana kuwa na nguvu kwelikweli nami nikajitahidi kuongeza nguvu zaidi lakini sikufanikiwa baadala yake nikamkasirisha, akatoa mlio mkali kama ambao hutokea paka wakipigana lakini huu ulikuwa mlio mkubwa zaidi, nadhani ni kutokana na paka mwenyewe kuwa mkubwa sana tofauti na paka ambao nimezoea kuwaona na kusikia wakilia. Nilishtushwa na mlio ule na kumuachia paka yule haraka sana na kuruka nikasimama mbali kidogo na paka yule macho yang yakiwa kwa Mnaro kama ishara ya kutaka msaada wake “wewe na mgumu sana kuelewa ndugu yangu, nimekwambia bila kuamini ambacho unafanya huwezi kufanikiwa” aalisema Mnaro akianza kuonesha kuchoshwa na ugumu wangu wa kuelewa, ingawa sio kweli kwamba mimi nilikuwa mgumu wa kuelewa ila nilikuwa najifunza jambo la kutisha na halikuwa jambo ambalo nilikuwa na uzoefu nalo. Sikusubiri Mnaro aongee neno lingine lolote nikakaza moyo na kumsogelea tena paka yule, safari hii kwa ujasiri wa hali ya juu, nikamshika shingo na kumvuta chini, tofauti na mwanzo mara hii paka yule alionekana mtii, akachuchumaa chini taratibu mpaka kufikia kimo ambacho kilinitosha kumpanda nikampanda naye akaanza kurudi juu, nilijikuta nikiyumba na kutaka kuanguka nikakosa pakushika na kushika manyoya ya paka yule lakini yaling'oka baadhi ya paka yule akatoa kelele ya maumivu na kuanza kukimbia ovyo ovyo, hali ilikuwa ya kutisha sana nikijitahidi kuhakikisha kuwa sianguki kwa kung'ang'ania vyema manyoya ambayo nilikuwa nimeyashika huku mengine yakiendelea kung'oka na paka yule kuzidi kuwa kuchaa “MSHIKE KWENYE MASIKIOOOOO” Mnaro alikuwa akipiga kelele huku akija kwa kasi kufuata uelekeo ambao paka yule alikuwa akielekea, nilijitahidi nikaachia manyoya ya paka yule upande wa mkono wangu wa kushoto na kushika sikio la kushoto la paka yule kisha nikaachia na manyoya ambayo nimeyashika kwa mkono wa kulia na na kushika sikio la kulia la paka yule. Paka yule akapunguza mwendo taratibu kisha akasimama kabisa. Mnaro alikuja mpaka paka yule alipo akanitizama akitabasamu.. “masikio yake ndio mjuongozo wako, ukitaka aende mbele unayavuta mbele, ukitaka asimame unayavuta nyuma, ukitaka aruke unayavuta juu na kuelekea kushoto ama kulia ni hivyohivyo, unaelekeza masiko ya paka huyu kuelekea uelekeo wowote ambao unataka aende” alimaliza kusema kisha akanivuka na kuendelea kwenda mbele, nami nikavuta masikio ya paka yule kuelekea huko ambako alikuwa akielekea yeye. Tukaenda tukikimbia juu ya wanyama wale tukipita mitaa mbalimbali mpaka nikajikuta nikimzoea mnyama yule na kuona kama naendesha tu pikipiki yangu ambayo nimeizoea sana! Nikajikuta nikifurahia kumuendesha myama yule mwendo wake ulikuwa wa kuruka ruka hivyo kwenda mwendo mrefu ndani ya muda mfupi Mno! Wakati mwingine nikawa navuta sana masikio yake naye akawa anaruka juu sana kama wafanyavyo ndege, nikawa navutiwa na usafiri ule nikizidi kumfuata Mnaro ambaye alionekana kuwa dereva mzuri sana kwenye usafiri ule.
Mara nilisikia ngurumo kubwa sana nyuma yangu, kugeuka niliona wanyama watatu wakubwa kuliko wale ambao tumepanda sisi wakija kwa kasi kubwa sana, wanyama wale walikuwa na macho ambayo yalitoa mwanga wa kutisha sanaaa! “Kimbiaaaaaaa, hao wanyama ni maadui wakubwa sanaaa” alisema Mnaro huku yeye akikaza mwendo zaidi na hatimaye kutokomea kizani, nami nikajitahidi kuvuta zaidi masikio ya paka yule mkubwa lakini hakuwa na mwendo mkubwa kama yule paka wa Mnaro, nikaona wanyama wale wakizidi kunikaribia na hatimaye mmoja wao akawa karibu kabisa, hatimaye akaja kama anakuja kunigonga! Nikamrusha paka wangu juu zaidi mnyama yule akapita lakini nikaona wanyama wawili waliokuwa nyuma yangu wakinifuata hukohuko juu, nikashuka chini nao wakaja. Wakawa wananikimbiza nikijitahidi kulazimisha mwendo wa paka yule, lakini kwa mbele nilimuona mnya yule mwingine ambaye alipitiliza aliwa anakuja kwa kasi upande ule ambao mimi nilikuwa nikitokea! Nilijaribu kuangalia huku na huko lakini sikumuona Mnaro, wasiwasi ukatanda moyoni mwangu.......
usikose sehemu ya 8