Simulizi ya kweli: Mpaka kieleweke

Simulizi ya kweli: Mpaka kieleweke

STORY :MPAKA KIELEWEKE.
MTUNZ: NIRA SAIRE.
SEHEMU YA 11.

Ilipoishia..

"Abubakar Saireee, kuna mgeni wakooo" ilikuwa ni sauti ya askari ikinishtua kutoka katikati ya dimbwi kubwa la mawazo. Nikasimama na kumfuata askari yule..

Endelea..

Safari yangu na askari yule ikatuchukua mpaka kwenye chumba kidogo ambamo niliingia nikamkuta bwana Filbert Tago ambaye alikuwa ni hakimu na bwana ambaye alipotelewa na binti yake akiwa ananisubiri. Alikuwa amekaa juu ya kiti kimojawapo katika chumba kile chenye viti viwili na meza. Nikaenda na kukaa kwenye kiti kile kingine tukawa tukitizamana. "Nataka uniambie ukweli juu ya jambo hili" alisema bwana yule kufungulia maongezi. Nilibaki kimya nikiwaza, kama huyu bwana amenifuata mpaka huku basi ana nia ya kunisaidia kwa maana sio jambo la kawaida hakimu kumtembelea mshtakiwa, sidhani hata kama inaruhusiwa kisheria "sii sio kesi ndogo, iwapo utashindwa utafungwa miaka mingi sana. Na iko wazi kuwa utashindwa maana kuna ushahidi wa kutosha kuwa ulitoroka" aliongeza bwana yule nami nikamueleza kuwa nilitoroka kichawi, jambo ambalo aliliamini mara moja kinyume na mategemeo yangu.
"Sikia, mimi najua kuwa unayo mbinu ya kumpata mkeo. Unaonaje kama nitakusaidia ili na wewe unisaidie kumkumbuka binti yangu wakati wa kumsaidia mkeo?". Hii ni fursa pekee ya kuharakisha zoezi la kumpata mke wangu ambaye anakabiliwa na mambo mawili mbele yake ambayo mpaka sasa sijui lipi litampata au limekwishampata, kuna uwezekano wa kuolewa Magugi lakini pia nilielezwa juu ya kufa kwake baada ya kijifungua. "Sina muda wa kutosha hapa" niligutushwa na sauti ya bwana Tago kutoka kwenye mawazo ambamo nilipotelea humo. "Sawa bwana, tushirikiane katika hili" nilijibu kisha kumuelezea bwana yule kila kitu juu ya mipango yangu na Mnaro naye akaahidi kunisaidia ila akinitaka kuhakikisha kuwa namrudisha binti yake kutoka Muifufu, tukakubaliana ba mimi kurudi mahabusu nikiwa na matumaini mapya.
Ile siku ikaisha mahabusu ndani ya jela ile.

"Huyu mwingine analala kama vile yuko kwake, aisee amkaaa" nilisikia mtu akizungumza huku akinitikisa kuniamsha. Nikaamka na kukutana na bwana mmoja mkubwa sana wa umbo. "Twende ukafanye kazi kumekucha" alisema bwana yule akinikabidhi fagio nami nikatii haraka kwakuwa sikutaka kujenga chuki ndani ya mahabusu ile kuhofia kuwa na maisha magumu zaidi. Nikaongozana na bwana yule hadi kwenye eneo la vyoo akanitaka kufanya usafi humo. Nilichungilia ndani ya vyoo vile na kwakweli hali ilikuwa ikitisha. Kulikuwa ni kuchafu mno, sidhani kama vyoo vile viliwahi kusafishwa. Kinyesi kilikuwa juu juu kikielea juu ya maji ambayo sikujua yametoka wapi ndani ya vyoo vile.
Nikawaza kubishia kazi ile, ila nilipomuangalia bwana yule ambaye inaelekea alikuwa kiongozi ndani ya mahabusu nilimuona fika kuwa amejiandaa kukabiliana nami iwapo nitakataa kazi ile.
Nikaamua kuwa mpole, nikainama na kuanza kukunja suruali yangu ambayo kama ningeingia bila kuikunja bila shaka ingecheza na kinyesi.
Wakati nikiendelea kukuja suruali yangu mara nikasikia sauti ikiita "Jafariii, namuomba huyo jamaa" nikageuka na kumuona askari wa magereza akimuagiza bwana yule.
"Kamsikilize afande kwanza ila mkimalizana tu urudi haraka, kazi inakungoja hii" alisema bwana yule nami nikaondoka na kumfuata askari yule tukaongozana "una bahati mbaya sana bwana" alisema askari yule nikashtuka na kujiuliza nini kilikuwa kinakwenda kunipata tena "yani umekuja jana tu leo unaondoka? Bado hujajifunza maisha wewe, ilipaswa ukae angalau miezi miwili bwana" alisema askari yule kiutani huku akicheka.
Nivuta pumzi nyingi nikaiachia yote. Nikamshukuru mungu kimoyomoyo kwa wema ambao amenitendeat.
Tuaenda mpaka mapokezi ya gereza lile ambapo nilielezwa kuwa wamepokea hati ya dhamana kutoka mahakamani hivyo natakiwa kwenda nyumbani lakini nihudhurie mahakamani tarehe ambayo ilipangwa kesi yetu isikilizwe tena.
Nikapewa vitu vyangu ambavyo walinihifadhia na kwenda nyumbani.
Nilifika nyumbani na kukimbilia bafuni kabla ya chochote, mwili wangu nilikuwa nauona kama wa ambae alilala jalalani kutokana na mazingira machafu ya ndani ya magereza.
Baada ya kuoga nikakaa nikijiuliza nawezaje kumpata Mnaro, nilikuwa nikimuhitaji sana lakini sikuwa nikijua namna ya kufika kwake ingawa nimeenda mara kadhaa, hii ni kutokana na yeye kuwa ananichukua kiuchawi kwenda huko kila wakati ambao alitaka twende, hivyo sikuijua njia ya kwenda huko.
"Hii ni mara ya mwisho kukufuata, wakati mwingine utakuwa unakuja mwenyewe" niliikumbuka kauli hii ya Mnaro nikajikuta nimetoa msonyo mkubwa sana.. alitegemea nitakuwa naenda mwenyewe ikiwa sipajui? Niliwaza nikijilaza kitandani na usingizi haukuwa na hiana, ukanipokea vizuri nikalala fofofo.

Niliposhituka ilikuwa ni majira ya saa saba usiku lakini Mnaro hakuwa amekuja. Nikaamua kutoka na kwenda kufanyia mazoezi ambacho alikwishanifundisha. Nikamchukua yule paka, ambaye sasa nilikuwa nimemuweka kwenye banda kubwa nyuma ya nyumba yangu ambalo lilitengenezwa kwaajili ya kufugia kuku lakini halikuwa likifanya kazi hiyo kwa wakati huu.
Nikaingia mitaani nikiwa namuendesha paka yule, nilikuwa nimejua kila kitu kuhusu namna ya kumuendesha paka yule na nilikuwa nikifurahia sana utendaji wake hasa uwezo wa kwenda umbali mrefu ndani ya muda mfupi tu.

Nikawa nimeenda mbali zaidi ambapo hata sikuwahi kufika kabla nikaona kwa mbali nyuma yangu kuna mtu anakuja uelekeo niliopo akiendesha mnyama ambaye kwa umbali ule sikuweza kumtambua. Nikaamua kujificha nyuma ya mti mkubwa wa mbuyu ambao niliuona mbele yangu ili kumpisha mtu huyo apite kwamaana sikujua kama alikuwa ni mwema kwangu ama laah!..
Nikiwa nachungulia nyuma ya mbuyu ule niliona mtu yule akija juu ya mnyama ambaye sasa niligundua kuwa alikuwa ni paka kama huyu wakwangu akija mpaka mbele ya mbuyu ule kisha akasimama, tukawa tumetenganishwa na mbuyu tu, mimi nikiwa nyuma na yeye akiwa mbele. Nikapatwa na uoga kidogo nikijiuliza mtu yule alikuwa na lengo gani kusimama pale? Au atakuwa ameniona? "Umejificha lakini uoga unakuumbua, unapumua kwanguvu mpaka nakusikia" ilisikika ikisema sauti ya mtu yule nyuma ya mbuyu nikagundua mara moja kuwa alikuwa MNARO.
Nikatoka nyuma nyumauyu mbuyuanikiwarahafurahao sikujusikujuakkwa maana nilkwawa nikasirishwailitoka mnharamno na mwenendo wa Mnaro na kutamani angalau ningekuwa na uwezo wa kumchapa hata kibao tutakapo onana
"Ulikuwa wapi siku zote hizi aisee? Nimekusubiri sanaaa" nilisema huku nikishindwa kuzuia tabasamu la furaha.. "mimi ndo nikuulize wewe ulikua wapi? Ulikuwa unaningoja kwani tulikubaliana kuwa nitakuja?" Aliuliza Mnaro nami nikabaki kumshangaa kwa maana wakati wote aluokua anaingia chumbani kwangu bila hodi kama kwake hatukuwa tumekubaliana kama atakuja. "Nadhani mara ya mwisho kukufuata nilikwambia waziwazi kuwa ilikuwa ni mara ya mwisho kukufuata na baada ya hapo ungekuwa unakuja mwenyewe" aliongeza maelezo Mnaro. "Sasa nawezaje kuja ikiwa sipajui pa kukupata?" Niliuliza swali ambalo nililiona ni la msingi lakini Mnaro akanitizama kama ambaye naongea ujinga "leo ndo unauliza hilo swali? Nadhani ulipaswa kuuliza wakati nakwambia kuwa sitokufuata tena. Tatizo lako unaishi kwaajili ya leo tu wala hujisumbui kuiwaza kesho" alisema Mnaro nami nikajiona kweli nilikuwa "juha" nikaamua kuwa mpole.
"Nilipatwa na matatizo bwana" niliamua kubadili mada baada ya kuona lawama zangu zinanirudia mwenyewe. "Ninajua kila ambacho kilikupata. Najua ulitegemea nikusaidie lakini sipo kwaajili ya kukusafisha kila ukijichafua, huko ni kukulemaza. Kumbuka Muifufu hautomwenda na mimi" alisema Mnaro nami nikabaki bila hoja.
"Kwakuwa tumekutana nadhani tugange yaliyopo na yajayo, bora tuanze mafunzo" nilisema kumwambia Mnaro ambaye alitabasamu na kisha akajibu "sielewi kwanini huoni kama hapa tunajifunza, maisha yote ambayo unaishi toka nianze kukufundisha ni mafunzo sio kushika matunguri tu" alisema Mnaro ambaye niliona kama leo ameamua kunionesha ni jinsi gani mimi sijui kufikiria.
"Umejifunza mambo mengi sana ndani ya muda mfupi, tena kwa vitendo. Kapumzike uyafanyie kazi hayo kisha tukutane keshokutwa kwaajili ya kumalizia mafunzo" alisema Mnaro ambaye nilianza kumuona kuwa amekwishazoea hali ya mpenzi wake kuishi Muifufu huku yeye akiwa huku. Anaachaje kuzoea ndani ya miaka yote ambayo amekuwa mbali na huyo mpenzi wake, niliwaza. Ambacho hakielewi ni kuwa mimi siko tayari kuandamwa na tatizo hili kwa muda mrefu kiasi hicho.
"Tukutane keshokutwa" alisema Mnaro akianza kuonda.. "sasa nitakupataje hiyo kesho kutwa?" Niliuliza Mnaro akaniangalia akitabasamu "unaona bwana, vitendo vinafunza zaidi ya maneno. Sasa unajua kuiwazia hata keshokutwa" alisema kisha akatoa kakioo kadogo kutoka kwenye ule mkoba wake wa ngozi na kunikabidhi.
"Sema na hicho kioo ukinihitaji nacho kitanileta" alisema Mnaro na kupotelea mbali na yule paka wake akiniacha nikikitalii kioo kile ambacho kilikuwa chakavu kikiwa kimefungwa na mipira kukizunguka.

Nikaondoka kuelekea nyumbani kwa usafiri wa paka yule ambaye hakuchukua muda kinifikisha mtaani kwetu lakini nilisita nikaangalia kwa mbali na kuona nnje ya nyumba yangu kukiwa na kikundi cha watu wakiwa busy kufanya shughuli ambazo sikuzielewa.
Nika shuka juu ya paka yule huku nikimnong`oneza kuwa nimkute hapo ninapomuacha.
Nikasogea karibu na nyumbani kwa mwendo wa kuchuchumaa kukwepa watu wale wasinione. Nikafika karibu kabisa mpaka nikaweza kuwaona watu wale.
Nimgundua mmoj wa watu wale ambaye ndiye aliyeonekana kuongoza kundi lile, alikuwa ni mwanamke yule ambaye alikuja kuniwangia nikamkimbiza na kukimbilia kwa wachawi wenzake..

Usikose sehemu ya kumi na mbili.

Kwa mswali, maoni au ushauri.. unaweza kunipata kunipata kupitia:
+255653686008
Nirasaire@gmail.com
 
Simulizi la kusisimia, una talent kubwa sana ndugu , umenikumbusha riwaya za watunzi marehemu Katallambula na Eddy Ganzel. ..Simu ya kifo na Kijasho Chembamba . Big up sana
 
STORY: MPAKA KIELEWEKE.
MTUNZI: NIRA SAIRE
SEHEMU YA KUMI NA MBILI.

Ilipoishia..
Nikasogea karibu na nyumbani kwa mwendo wa kuchuchumaa kukwepa watu wale wasinione. Nikafika karibu kabisa mpaka nikaweza kuwaona watu wale.
Nimgundua mmoj wa watu wale ambaye ndiye aliyeonekana kuongoza kundi lile, alikuwa ni mwanamke yule ambaye alikuja kuniwangia nikamkimbiza na kukimbilia kwa wachawi wenzake..

Endelea..

Niliwatazama kwa muda watu wale ambao walikuwa wachawi ambao bila shaka walikuja kupambana na mimi baada ya kujenga ugomvi na mmoja wa wachawi wa kundi lile...
Wachawi wale waliendelea kuwapo pale kwa muda huku wakiihama eneo kila baada ya muda fulani, waliendelea kufanya hivyo kwa muda mpaka wakiizunguka nyumba mpaka kurudi pale ambapo walianzia. Wakatulia hapo na kuanza kuzungumza lakini sikuweza kusikia wanaongea nini, nikaamua kusogea zaidi mpaka sehemu ambayo niliweza kusikia ambacho wanaongea. "Tumeshajikinga vizuri, kama akitushinda tutakimbi nnje ambako hatoweza kutoka,zindiko tulilofanya litamzuia" alikuwa akielezea mchawi yule huku wengine wakimsikiliza kwa makini..
Wachawi wale walikuwa ni kundi lisilopungua watu kama kumi na mbili, kwanini wanafikiria kuzidiwa na mimi?, nilijiuliza na kupata jibu kuwa walikuwa ni waoga na hivyo hawana uwezo wa kunidhuru. Nikaamua kutoka pale mafichoni na kuwafuata wachawi wale pale walipo.
Wachawi wale waliponiona wote wakakimbilia kwenye ukuta wa nyumba ambapo niligudua walikuwa wamechora mstari chini mduara kuizunguka nyumba hivyo wao na nyumba walikuwa ndani duara hilo la kuchora huku mimi nikiwa nnje ya duara hilo.
Nikazidi kusogea lakini wakaanza kurusha vitu kama vitenesi ambavyo nilijaribu kuvikwepa lakini vingine vikanilenga, nikashangaa kuona vile ambavyo vilinilenga havikuwa na maumivu yoyote hivyo nikaamua kuacha vinipige mimi nikisonga na safari ya kuwafuata, jambo ambalo lilionekana kuwashangaza sana.
"hebu acheni ujinga! ondokeni haraka kabla sijavunja mtu mguu" nilichimba mkwara baada ya kufika na kusimama mbele ya mstari ambao waliuchora kuzunguka nyumba nikihofia kuuvuka kwakuwa nilikuwa nikijua kuwa walikuwa wameuchora kujikinga na mimi na sikujua madhara ya kuuvuka.
"kama unataka kutuvunja miguu we tuvunje tu, hakuna ambaye anaondoka hapa" aliongea yule mwanamke mchawi, nadhani alikuwa anajaribu kunishawishi nivuke mstari ule. Nikaamua kujita ujasiri na kuvuka mstari ule ingawa nilikuwa na hofu kidogo. nikajikuta ndani ya mstari ule bila kudhurika na chochote, wachawi wale wakaanza kukimbia kila mmoja na uelekeo wake! lakini nilifanikiwa kumkamata ambaye nilimkusudia, alikuwa ni yule mwanamke ambaye bila shake ndiye chanzo cha ujio wa wachawi wote wale. Mwanamke yule alifurukuta akipambana kujitoa mikononi mwangu lakini nilikuwa kama ambaye nimekamata panzi, hakuwa na uwezo wa kutoroka mikononi mwangu. Akawa analia akiomba nimuachie lakini nilikuwa kama simsikii "kaka naomba unisamehe, sirudi tena haki ya mungu" alijitetea mwanamke yule lakini sikujali maneno yake, nikambeba kwa mkono mmoja nikimbana kwapani kama ambavyo kuku hubebwa nikawa natembea naye kuondoka eneo lile la nyumbani kwangu.
Nikaenda moja kwa moja mpaka nilipouacha usafiri wangu (paka) nikawa napanda juu ya paka yule nikiwa nimembeba yule mwanamke ambaye alizidi kupambana, hakutaka kipanda juu ya paka yule. Baada ya kunikwamisha mara mbili nilizaba kofi zito la uso akazimia papohapo nami nikapanda juu ya paka yule na nikiwa na mwanamke yule, tukaanza safari ambayo sikuwa hata nikiijua. Nilikuwa nikifanya matendo yote kama ambaye ninaongozwa na sauti fulani ndani ya ubongo wangu nami nikawa nikitii bila kuhoji.
Safari ikaenda mpaka kwenye kijumba fulani kidogo na cha kizani kwenye eneo ambalo sikulijua kabla. Baad ya kusimama kwa sekunde kama 10 akatoka Mnaro ndani ya nyumba ile akionekana mwenye furaha sana.
"Sasa safari ya Muifufu imeiva" alisema Mnaro katika hali ya tabasamu huku akinipokea mwanamke yule ambaye nilikuwa nimembeba mapajani juu ya paka yule.
"Kwa muda mrefu nimejaribu kukutumia kama silaha yangu ila ilishindikana kwakuwa ulikuwa na hofu hivyo hukuweza kufanya kama ambavyo nilikuwa nakuagiza, ila sasa umeiva" alisema Mnaro lakini sikumuelewa vyema, hivyo nikauliza "una maana gani?" Akawa amempokea mwanamke yule tukawa tumeongozana kuingia kwenye kajumba kale "huwezi kupambana ndani ya Muifufu kama mimi sitokuwa nyuma yako, lazima nikutumie kama silaha yangu kwakuwa wewe huna mbinu za kutosha" alisema Mnaro, tukawa tumefika ndani tukakaa huku akimlaza chini yule mwanamke.
"Nimekuwa nikijaribu kuunganisha ubongo wangu na wako ili uweze kufanya kama ambavyo ningefanya mimi lakini uoga wako umekuwa ukinikwamisha, mfano nilifanikiwa kukuwezesha kumkimbiza huyu mpuuzi mpaka kule shule na nilikusudia kuwaadhibu wachawi wote waliokuwepo kule lakini uoga wako ulipelekea kushindwa kukuongoza zaidi, ukarudi" alizidi kutoa maelezo Mnaro, nikapata jibu la uwezo ambao nilikuwa naupata bila kujua ulikuwa unatoka wapi.
"Siku zote tambua kuwa niko na wewe na siwezi kuacha udhurike na chochote kwakuwa wewe ni silaha yangu, hupaswi kuwa na uoga wowote ndani ya Muifufu pia kwakuwa nitashiriki mapambano kutokea hapahapa" alizidi kunielezea Mnaro, nikawa nimeelewa vyema.
"Sasa safari ya Muifufu iko tayari, ni wewe tu kuamua unataka kwenda lini" alisema Mnaro lakini kitu cha ajabu ni kuwa siku ile sikuwa na usongo sana wa safari ile kama ambavyo ulikuwa siku za nyuma ingawa bado nilitaka kwenda na ilikuwa lazima niende.
"Hebu nieleze kidogo kuhusu Muifufu na ambacho napaswa kufanya nikiwa huko" nilisema na Mnaro akaanza kutoa maelezo "huko Muifufu yuko mwanamke anaitwa Sauda, mwanamke ambaye nimekueleza sana kumuhusu. Wakati natoroka Muifufu nilikubaliana na mwanamke yule kuwa nitaandaa mtu ambaye nitamtuma kwenda kumchukua. Mwanamke huyo amebaki akijifunza juu ya namna ambavyo yeye na mtu huyo watafanikiwa kutoroka Muifufu. Unachotakiwa Kufanya ni kuingia Muifufu na kuishi kama ambavyo wanaishi watu wengine, mpaka ambapo utakutana na Sauda ambaye atakueleza zaidi nini cha kufanya" aliweka kituo Mnaro. Nikatafakari vizuri maelezo yale kisha nikapata swali na kuuliza "sasa nitamtambuaje huyo mwanamke?" Mnaro akanijibu "sio wewe ambaye unapaswa kumtambua, yeye ndiye atakutambua wewe. Unachopaswa kufanya ni kuweka ishara kuwa umeingia Muifufu kwenye sehemu ambayo tuliku aliana kuwa ataikuta ishara hapo naye kila siku hudamka na kwenda kuangalia hapo jambo ambalo hulifanya pia kabla ya kwenda kulala" alimaliza kunieleza Mnaro nikawa nimeelewa. Sasa ilikuwa imebaki mimi kuamua ni lini niende Muifufu.
Mama yangu anaumwa na sijamuona, sijaaga pia na kupata baraka za wazazi. Siwezi kwenda kwanz mpaka niende nyumbani, niliwaza. "Leo ni jumaa nne, naomba safari iwe jumaa nne itakayofuata baada hii ijayo" niliomba nikiamini wiki mbili zingetosha kujiandaa na Mnaro akakubali bila ubishi hata kidogo. "Vipi kuhusu huyu?" Niliuliza nikimuoneshea mwanamke yule mchawi ambaye alikuwa amelala pale chini akiwa hajitambui. "Huyo niachie mimi" alijibu Mnaro kwa kifupi.
Nikaondoka kurudi nyumbani kwa usafiri ule wa paka.
Nikafika nyumbani, nikalala nikipanga kuwa asubuhi ningeanza safari ya kwenda kuwaona wazazi nyumbani.

Kulipokucha niliamka nikiwa na mawazo mengine.
Kwanini nisafiri kwa basi safari ile ambayo ingenichukua masaa karibu kumi? Nikaamua nisubiri usiku uingie ili nisafiri kwa kumtumia paka yule ambaye bila shaka angenifikisha mapema sana.
Nikaendelea na maisha ya kawaida mpaka ukafika usiku wa kama saa tatu hivi, nikachukua begi dogo ambalo niliweka kila ambacho ningekihitaji na kuanza safari.
Ilinichukua kama masaa mawili nikawa nimefika nyumbani, nikamuhifadhi paka wangu nyuma ya nyumba na kuingia ndani ambako nilipokelewa na ndugu zangu kwa furaha sana "mbona umechelewa hivyo kaka? Uliondoka saa ngapi? Aliuliza mdogo wangu akinipokea begi langu "aaah! Niliondoka saa sita kwa magari ya kuungauunga" nilijibu nikikaa ambapo ndugu zangu wengine ambao walikuwemo vyumbani mwao, kila mmoja akitoka kuja kunilaki kwa furaha, hata baba ambaye alikuwa ameingi kulala tayari akatoka na kunipokea.
Nikauliza juu ya afya ya mama ambaye bado alikuwa hospitali akiuguzwa na dada yangu, nikaambiwa afya yake ilikuwa ikiendelea vizuri sana na walitegemea kesho yake angeruhisiwa.
Nikaongea mengi na ndugu zangu wale ambao hatukuwa tumeonana ndani ya muda wa kama miezi nane hivi lakini ilikuwa ni mingi sana kwani hatukuzoea kukaa mbalimbali kwa muda mrefu kiasi kile.
Tukaingia kulala mida ya saa saba.

Asubuhi tulikwenda hospitali kumuona mama ambaye alifurahi sana kuniona. Afya yake ilikuwa nzuri sana kiasi kwamba ungemkuta nyumbani ungehitaji kuambiw kuwa alikuwa mgonjwa.
Tukaongea mawili, matatu na baadae tukaongea na daktari ambaye alituruhusu kuondoka naye, tukarudi nyumbani.

Nilikaa pale nyumbani mpaka zikabaki siku mbili kwaajili ya safari ya Muifufu.
Usiku wa siku hiyo nikawaita wazazi wangu, nikakaa nao nikiwaeleza juu y safari ya Muifufu ambayo ilipaswa kuwepo siku mbili zijazo.
Pamoja na wasiwasi ambao walikuwanao, wazazi wangu walinipa baraka zao na kuniombea mafaniko katika safari ile.
Nikawaaga kuanza safari ya kurudi kwangu ambayo niliwaambia ni lazima niondoke usiku ila sikuwaambia kuwa natumia usafiri wa paka kuhofia kuwaacha kwenye wasiwasi mwingi nikiwa safarini.
Nilifika nyumbani haraka kama ambavyo ilikuwa safari ile ya kwenda.
Nikalala nikijua kuwa kesho yake nilitakiwa kuamkia mahakamani ambako kesi yetu ingesomwa.

Niliamka napema nikajiandaa na kwenda mahakamani ambapo ziliendeshwa kesi kadhaa na majira ya saa tano ndipo nasisi tukaitwa na kesi yatu kusomwa.
Nilikataa kuwa mimi sikuwahi kukamatwa na kuingizwa mahabusu kisha kutoroka kama ambavyo askari wale walieleza (melezo ambayo hakimu yule alinifundisha niyaseme). Nikaulizwa juu ya kukubali kwangu kuwa askari yule ambaye ni mshatakiwa namba mbili alinitorosha, nikajibu kuwa sikuwa na kingine cha kusema kwakuwa askari wale walikuwa wakinipiga nikubali kuwa nilitoroka.
Hakimu yule akawataka askari wale kuleta ushahidi ila askari wale wakomba wapewe muda kuendelea na upepelezi.
Ikapangwa tarehe nyingine ya kusikilizwa kesi ile ambayo ilikuwa ni miezi miwili ijayo.
Nami nikaondoka kwakuwa tayari nilikuwa na dhamana.
Nikaenda mojakwa moja nyumbani ambapo jioni ya siku hiyo hakimu yule alikuja kunitembelea tukazungumza mengi.
Nilimjuza kuwa safafari ya kwenda Muifufu ilikuwa kesho yake ingawa siijui siku ya kurudi, naye akanitaka niende kwa amani tu ya huku mahakamani nimuachie yeye hata kama nitachelewa.
"Hii kesi itakusubiri tu mpaka urudi, ukija na binti yangu nitahakikisha unakuwa huru ila usiporudi naye nitahakikisha unafungwa miaka mingi sana bwana Saire" aliongea hakimu yule akionesha msisitizo mkubwa ukiashiria kukimaanisha akisemacho. Nami nikajitahidi kumtoa hofu "usiwe na shaka bwana Waisaka, umenisaidia pakubwa sana nami lazima nilipe fadhila" nilisema.
Tukaagana na bwana Waisaka akaondoka na kuniacha nikipanga mipango ya kumtafuta Mnaro kwaajili ya mipango ya safari ya kwenda Muifufu.

USIKOSE SEHEMU YA 13 YA STORY HII.
MPAKA KIELEWEKE BY NGINIRA SAIRE.

MAWASILIANO:
+255653686008
nirasaire@gmail.com
 
Back
Top Bottom