Story: Mpaka Kieleweke
SEHEMU YA 17
pamoja na kupata maumivu makali sana, nilivumilia na kusimama haraka kujaribu kukabiliana na huyo ambae amenisukuma!..
lakini kadri cheko zile zilivyokuja karibu yangu niligundua kuwa walikuwa zaidi ya mmoja, nikawa narudi nyuma kujaribu kuwaepuka lakini nikajikuta nimefika mwisho, tena nilinusurika kuanguka kutoka kwenye kilele kile cha mlima, nikajiweka sawa na kusimama hapohapo nikingojea hatma yangu!...
nilistaajabu kuona kuwa nilikuwa nakabiliwa na viumbe ambao hawakuwa wanadamu!. Walikuwa sokwe watatu wakinijia katika hali iliyoonesha kuwa hawakuwa na nia njema na mimi! nikabaki nikiwa nimesimama bila ujanja wa kujiokoa! sokwe wale wakazidi kunisogelia huku wakijitandaza vizuri kuhakikisha kwamba siwaponyoki na kutokea upande wa nyuma yao lakini waliacha upenyo mdogo baina ya sokwe mmoja na mwingine! nikaamua kuwa nafasi hiyo ndogo ingenitosha kupita, hivyo nikaendelea kujifanya kama ambaye nimezubaa bila mipango huku nikivizia nafasi ya kuwatoroka!, waliponikaribia zaidi nika chomoka kwa mbia za hali ya juu na kupita katikati ya sokwe wawili lakini mmoja wao akageuka kwa kasi kubwa na kunitegua mguu, nikaanguka vibaya sana kutokana na kasi niliyokuwanayo!...
sasa sokwe wote watatu wakaja kwa kasi pale nilipokuwa huku mwili wangu ukiwa mzito kufanya chochote nikigumia maumivu makali yaliyotokana na kuanguka mara kadhaa!.. nikabaki nimefumba macho nikingoja kitokee chochote ambacho kingefanywa na sokwe wale kwani sikuwa na ujanja!...
"ACHAAAAAA" ilisikika sauti kubwa ikiamuru! nami nikafumbua macho na kutazama baada ya kuona sekunde zinakatika bila kudhuriwa na sokwe wale!!..
nilishangaa kuona sokwe wengine watatu wakiwa wameongezeka, sikujua wametoka wapi na wala sikumuona ambaye alitoa amri ya kuacha kwa sokwe wale ambao walikuwa wakinishambulia!.. inamaana sokwe hawa wanazungumza? nilijiuliza baada ya kujiridhisha kuwa hakukuwa na mwanadamu zaidi yangu pale!..
sokwe wale ambao walikuwa wakinishambulia wakarudi nyuma na kisha mmoja kati ya wale ambao waliongezeka akaja mpaka nilipo na kunitizama kwa makini huku akisogeza macho yake karibu kabisa na uso wangu!..
sura yake ilikuwa mbaya na yakuchekesha mno lakini ningeupata wapi ujasiri wa kucheka katika hali ile ya hatari?..
baada ya kumaliza ukaguzi wake akarudi walipo wenzie, wakawa kama wanajadiliana jambo, kisha akaja tena mwingine na kuanza kunichunguza kama alivyofanya mwenzie ila yeye alikwenda mbali zaidi na kuanza kuninusanusa kisha akatoa kicheko kikubwa sana kilichonishtua, kicheko kile mbali na kuwa kikubwa hakikutofautiana sana na cha mwanadamu!..
"bhebhaaa" alisema sokwe yule ambaye alionekana kuwa mzee kwa matamshi ambayo hayakusikika vizuri lakini nadhani alitaka nibebwe, kisha wakaja sokwe wawili mbele yangu halafu mmoja akanibeba na kunipandisha mgongoni mwa mwenzie kisha sokwe wale pamoja na mimi nikiwa mgongoni mwa sokwe tukaondoka aliyenibeba akitangulia huku wengine wakifuata kwa mwendo wa kukimbia kupanda kilima kile!..
sikujua safari ile ilikuwa ina lengo gani lakini nilishangaa kuingiwa na imani kwa sokwe wale na kuwaacha wafanye ambavyo walitaka!...
mwendo wa sokwe wale ulikuwa wa kutisha kiasi kwangu kwani walikuwa wakienda kwa kurukaruka huku wakipanda juu, nilikuwa nikihofia sana iwapo wangeteleza na kuanguka, nikawa najishika vizuri zaidi pale mgongoni ili nisianguke! maumivu ya kiuno na makalio pia yalizidi kwanyi sokwe yule alikuwa na vishindo vikubwa akiruka na kutua mbali hali iliyosababisha mtikisiko mkubwa wa mwili wangu pale mgongoni kwake!..
mlima ule ulikuwa wa ajabu sana, pamoja na kuonekana mfupi, kuupanda ilikuwa ni safari ndefu sana hata baada ya kupandishwa na sokwe wale ambao walikuwa wazoe fu wa kupanda mlima ule na walikuwa wakienda bila kusita!..
baada ya masaa kadhaa tulikuwa kwenye kilele cha mlima ule na sokwe yule akaniweka chini huku akionekana kuchoka sana! wenzake wakawa wamefika kisha nikabebwa na kuwekwa mgongoni mwa sokwe mwingine ambaye naye alitangulia kama ambavyo alifanya yule aliyenibeba mwanzo na safari ikaendelea!..
tulienda mbele kidogo kisha tukaanza kushuka mlimani!.
upande huu wa mlima ulikuwa mrahisi kushuka kwani kulikuwa na ngazi za kushuka kuelekea chini!.
safari ikaendelea nikiwa mgongoni mwa sokwe yule huku hali yangu ikizidi kuwa mbaya kutokana na maumivu..
Tukaendelea kushuka mpaka kukaanza kupambazuka, na kwambali nikaanza kuuona mji!..
kazi ya kushuka ikaendelea!.
mpaka tunafika chini ilikuwa tayari ni asubuhi, hata jua lilikuwa limetoka, nilikadiria kuwa ilikuwa majira ya saa mbili!.
Safari ikaendelea tukifuata njia ambayo ilikuwa ikielekea ulipo mji ambao kutokea kilimani niliona haukuwa mbali sana!..
na kweli baada ya muda mfupi tu tukawa tunakatiza kwenye nyumba za watu ambao walikuwa wakishangazwa na ujio wetu wakawa wanaitana na kukimbia wakitufuata nyuma!.
safari ikaenda kukomea kwenye nyumba kubwa kuliko nyingine zote ambazo niliziona, ikiwa imezungushiwa uzio mkubwa wa miti na kuacha eneo kubwa sana mbele ya nyumba ile!..
nikashuswa chini kwenye uwanja wa nyumba ile..
watu wote wakaja kunizingira wakinishangaa bila kusoma neno!.
watu wale walionekana kuwa na afya mbovu huku wakionekana kama ambao wamechoka sana!..
mara akatoka mzee sana ndani ya nyumba ile na kuja mpaka nilipokuwa watu wakimpisha njia! akanitizama kwa muda kisha akasema "muingizeni ndani" aliagiza mzee yule na kazi hiyo ikafanyika mara moja, nikabebwa na watu wale wasio na afya ya kuridhishwa na kupelekwa ndani ambapo nililazwa kwenye kitanda cha kamba, nikavuliwa nguo zote na kupakwa aina fulani ya mafuta ambayo yalikuwa ya moto sana kiansi kwamba nilikuwa nikitoa kelele ya maumivu wakati zoezi lile likiendelea!.
nikatokwa na jasho jingi sana, lakini baada ya muda mfupi maumivu yalinipungua, nikaachwa pale kitandani nikipumzika na hatimaye nikapitiwa na usingizi..
nilipokuja kuamka nikainuka kitandani na kuelekea pembeni ambapo niliona nguo zangu zikiwa zimetundikwa kwenye kamba kwa nia ya kuzivaa lakini nilihisi bado nilikuwa na maumivu ya kiuno!..
nikaanza kuangaza huku na huko ndani ya chumba kile kujaribu kuona kama naweza kuupata mkoba wangu na kweli nikafanikiwa kuupata, nikaufungua na kuchukua dawa ile ya majani na kuitafuna kisha kuanza kujipaka maeneo ambayo nilikuwa na maumivu!..
kama kawaida ya dawa ile nikahisi maeneo yale yakiwaka moto lakini ndani ya muda mfupi mno nikawa nimepona.
Nikavaa nguo na kutoka nnje ya nyumba ile ambapo nilimkuta yule mzee mwenye nyumba ile akiwa amekaa kwenye kiti cha mbao huku pembeni yake akiwepo binti mwenye afya mbovu sana akitwanga kitu ambacho sikukijua kwenye kinu! kwa mbali niliona watu wengine kila mmoja akiwa na kazi yake!...
ujio wangu pale nnje ulionesha kuwashitua watu wote waliokuwepo eneo lile wakawa wanasogea mmoja baada ya mwingine wakiwa wameshikwa na bumbuwazi!..
"ungepumzika kwanza afya yako itengemae, kaa hapa" alisema mzee yule huku akinipisha kiti ambacho alikuwa amekalia yeye! "hapana mzee, kaa tu! mimi niko sawa" nilijibu huku nikionekana kuwa na utimamu wa kutosha wa mwili, nikasogea na kukaa chini karibu na kile kiti chake "nadhani hamnijui, ningependa kwanza mnitambue kabla ya kukijua ambacho kimenileta kwenye mjini wenu" nilianza kujieleza lakini kabla sijafika mbali mzee yule alinikatisha "tunajua kila kitu kuhusu wewe, wewe ndiye ambaye hujui mengine kutuhusu! ila leo tutakueleza" alizungumza mzee yule nami nikakaa sawa kumsikiliza "najua unafahamu historia iliyopo kati ya wakazi wa mji huu na bwana Magugi.." Alianza kuzungumza nami nikakubali kwa kichwa kisha akaanza kuelezea kama sio yeye alieanza kwa kusema kuwa anajua kama naijua historia ile!..
akanielezea kila kitu kama ambavyo nilielezewa awali, lakini yeye alielezea mpaka maisha yalivyokuwa upande wa pili wa mlima baada ya kufika kwao "maisha hayakuwa mazuri kabisa, tulikuta ni eneo kame na lisilo na rutuba, hakukuwa na chochote cha kutuendeshea maisha zaidi ya ambavyo tulikuja navyo! Magugi alikuwa ametudanganya..
baada ya chakula kubaki kidogo, ilitubidi kukitoa chote kwa vijana kumi ili wao wapate nguvu na kwenda kutafuta kingi kwaajili ya wengine lakini walitakiwa kuwa makini wasiingie eneo la Muifufu na kuvunja mwiko tuliokuwa nao, vijana wale wakaenda na kufanya kazi ambayo waliagizwa, wakatafuta sana bila kupata chochote, mwishowe wakashauriana kuwa ni bora waingie Muifufu kuliko kuacha watu wote wa huku kijijini wafe na njaa!. kukatokea mabishano makili, wengine wakikubaliana na wazo hilo huku wengine wakipinga, hatimaye uamuzi ukaafikiwa kwamba kila mmoja afanye ambalo yeye aliona ni sahihi, hivyo vijana wanne wakarudi kijijini huku sita wakielekea eneo la Muifufu kutafuta chakula kwaajili ya waliobaki kwenye kijiji hiki wakiwa na hali mbaya sana kutokana na njaa...
Usikose sehemu ya 18.