Sehemu ya 31
“Yupo binti anaitwa Lawalawa, mwezi uliopita aliwahi kumtolea uboho baba yake mzazi, na leukocyte antigens yake nahisi inaweza kumsaidia mtoto wenu. “Lawalawa!!” nilimaka. Nilishituka sana.
“Ndio Lawalawa, binti mmoja ana asili ya kiarabu, unamfahamu?” Kauli ya daktari yule ilinishitua sio kidogo, nilihisi kama daktari yule mzee kuna kitu alikuwa akijua juu yangu na lawalawa na alitaka kunichomea kwa mke wangu juu ya mpenzi wangu Lawalawa. “Unamjua?” nikaulizwa tena.
“Ndio namjua” hatimaye nilijibu. Mke wangu, alitabasamu baada ya kauli yangu, akaonekana kuwa na shauku kubwa ya kumpata mwanamke huyo.
“Basi kama unaweza kumpata anaweza kuwa mkombozi wa mwanao?”dokta alihitimisha. Hakuonekana kujua wala kuwa na hisia kama mimi na Lawalawa kulikuwa na uhusiano wa siri.
Ni Lawalawa....Hawara wangu....Huyu huyu niliyekuwa na mpango wa kumfuata mjini Tabora kabla ya ligi daraja la kwanza kuanza. Ndiye awe mwokozi wa maisha ya mwanangu. Itawezekana? Atakubali hali nilimdanganya sikuwahi kuwa na mke wala mtoto.
Leo natakiwa nimfuate nimwambie nilimdanganya. Ninaye mke na mtoto mmoja, ambaye yupo hoi kitandani kwa saratani ya damu na yeye awe ndiye mwokozi wake. Atanielewa?? Vipi kuhusu penzi langu kwake. Ndio itakuwa mwisho wake, Je mimi niko tayari kumpoteza Lawalawa.? Jibu ni hapana. Je niko tayari kumpoteza mwanangu? Jibu pia ni hapana. Nifanyeje sasa?
Nilijiuliza mambo yote hayo tukiwa tumekwisha toka chumbani kwa daktari, nilikuwa pembeni ya kitanda alichokuwa amelala mtoto wangu, Maganga.
Penzi la Lawalawa na uhai wa mtoto wangu kipi zaidi? Jibu ni rahisi tu, uhai wa mwanangu ni zaidi . Basi lazima nimkabili Lawalawa nimweleze ukweli, naye anisaidie. Niliafiki mawazo hayo.
Nilimwita mke wangu na kumtaka ajitulize pale hospitali ya Bugando mimi nifunge safari ya kumfuata mwanamke yule mjini Tabora. “Umemjulia wapi huyo Lawalawa?” mke wangu aliniuliza.
“Ni shabiki wangu wa soka uwanjani,” nilimdanganya.