Sehemu ya 37
Kwa dakika nzima nilibaki nimeduwaa, nimeganda kama niko kwenye theruji. Nilihisi uchungu mkali mno moyoni, nilijiona ni mwanaume mpumbavu, nisiyestahili kuigwa mbele ya jamii.
Kwa kiwango kikubwa nilikuwa nimesababisha kifo cha mwanangu. Nilishusha pumzi ndefu, kisha nikaendelea kumuliza daktari.
“Mazishi ya mwanangu yalifanyikia wapi ili angalau nikalione kaburi lake?” “Nitajuaje!!” dokta alijibu harakaharaka.
Sikuwa na la ziada la kumuuliza dakatri yule. Nilichofanya ni kuondoka nikiwa nimeghafirika vibaya sana, nilirudi hadi kwenye ‘lodge’ tuliyokuwa tumefikia, baada ya kufika nikaingia chumbani mwangu na kutulia humo nikitafakari kifo cha mwanangu.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nikagundua nilikuwa nimemfanyia kosa kubwa sana mke wangu Pili, pamoja na kwamba nilikuwa sina mapenzi na mwanamke huyo, ila sikutakiwa kabisa kumtelekeza hospitalini akiwa na mwanangu aliyekuwa mahututi kitandani.
siku hiyo nilishinda chumbani kama mgonjwa wa homa kali, daktari wa timu aliponihoji juu ya hali ile nilimdanganya nilikuwa nahisi homa.
Kwa kuwa nilikuwa mchezaji tegemeo katika timu ile, kila mtu aliguswa na hali niliyokuwa nayo, hata hivyo sikupenda kufungua mdomo na kuwaeleza watu ukweli wa jambo linalonisibu.
Hadi inafika siku ya mechi kwa kweli bado nilikuwa sina utimamu wa mwili na akili, nakumbuka siku hiyo nilimwomba kocha asinipange.
Nilikuwa nasumbuliwa na sana taswira ya mwanangu, kila wakati nilikuwa najutia na kujilaumu mwenyewe.
Mchezo kati ya timu yetu na Igogo Fc, timu yangu ya zamani, ulikuwa mkali sana, nakumbuka hadi dakika ya 20 kipindi cha kwanza tayari tulikuwa tumekwisha fungwa goli mbili kwa bila.
Kutokuwepo kwangu uwanjani pengo lilikuwa kubwa sana, timu yangu ya Reli Tabora ilikuwa imejengwa kunizunguka mimi.
Hadi tunakwenda mapumziko ya kipindi cha kwanza timu ya Igogo fc ilikuwa inaongoza kwa goli tatu kwa bila, naweza nikasema timu yangu ilikuwa imezidiwa vibaya sana.
“Vipi hutaweza kabisa kucheza?” kocha aliniuliza wakati wa mapumziko.
“Hapana kocha, bado sijikisii vizuri.