Sehemu ya 19
nikijibwaga. katika benchi lililokuwa mbele ya kioski chake. “Nipe soda na mandazi, ” niliagiza. Jamaa haraka haraka akanihudumia.
“Jisikie upo Serena hotel, karibu sana,” jamaa yule chakaramu aliniambia. Nikatabasamu.
Nikamuuliza jambo jingine. “Hapa ni wapi nitapata gesti ya bei rahisi?”
“Zimejaa tele.”
“Ziko wapi?”
“Unaona zile ofisi za idara ya maji, pale...”alisonta kunionyesha. Majengo yaliyokuwa mita kama 100 kutokea pale.
“Ndio.”
“Pale kuna gesti moja bei rahisi sana, askari polisi wa hapa, wote huwa wanapeleka wachumba zao pale,” alisema.
Nilicheka, jamaa alikuwa na meneno mengi sana ya kufurahisha. “Nashukuru ndugu yangu, acha nikapumzike sasa.”
“Unakwenda kupiga peku kaka?
Kondomu hununui?”
“ Kwani nimekwambia nina kwenda kulala na mwanamke?”
“Unakwendaje kulala mpweke sehemu kama ile kaka?” “Una maneno mengi sana, kabila gani wewe.”
“Mimi mtu wa Kigoma, ila hapa nafahamika kwa jina la Chado” niliondoka nikimuacha Chado na uchakaramu wake.
*****
Alfajiri na mapema, nilikuwa mtu wa kwanza kuwasili katika uwanja wa mazoezi, nilifanya mazoezi mepesi ya peke yangu, Nusu saa badaye mtu mmoja mmoja wakaanza kujitokeza uwanjani.
Dakika 45 badaye timu nzima na makocha ikawa imetimia. Nilijisogeza kwa kocha, mzee Gideon na kumsalimu ili tu aniaone. Maana kwa muda mfupi tu nilimtambua mzee yule ana ugonjwa wa kusahau mambo.
Kweli mzee yule nadhani umri ulikuwa unamwacha, aliponiona, alishituka tena, akanisalimu kwa ukarimu tu kisha alinitambulisha kwa kocha wa viungo kama mchezaji mgeni ninayetakiwa kufanyiwa majaribio, kama nitafaa basi nijumuishwe kwenye timu yake.
“Jina lako?” Kocha msadizi aliuliza.
“Ajibu maganga.” Nilijibu.
“Karibu.” Alisema
Asubuhi ile tulifanya mazoezi pamoja,ingawa nilikuwa mgeni kwenye baadhi ya mazoezi, lakini nilijituma kiasi cha kuwafurahisha wale walimu.
Tulipogawa timu mbili, na kufanya mazoezi ya kucheza mpira, kocha mkuu aliniuliza namudu zaidi kucheza nafasi gani, nikamwambi kama mshambuliaji, yanii namba tisa.
Wakati huo nilikuwa nimekwisha fahamiana na baadhi ya wachezaji kadhaa, wao pia walionekana kuvutiwa na mimi.