Simulizi: Soka Lilivyonikutanisha Na Shetani

Sehemu ya 28

Mtoto mwenye sura nzuri alikuwa amelala, hakuwa na afya nzuri, alikondeana, nguo alizovishwa, zilichakaa na kutoa harufu kali ya maziwa. Mtoto alikuwa na michubuko chubuko sehemu mbalimbali za mwili wake.

“Anaumwa?” niliuliza kwa wahaka.
“Ndio.”
“Nini zaidi?”
“Leukemia”
“Leukemia ndio ugonjwa gani?”
“Ni ugonjwa wa kupungukiwa damu!”
“Whaat!” nilimaka.

Mke wangu aliongea jambo lile katika namna iliyoonesha hana uhakika na asemacho, japokuwa hata mimi nilikuwa sijui ‘Leukemia’ ni maradhi gani lakini sikuamini tafsiri aliyonipa Pili.

“Daktari ndio alinieleza hivyo,”
“Anatumia dawa gani?” nilimuliza “Zipo tembe za maumivu, lakini hazimsaidii, ndio maana nimeamua nimelete hospitali ya Bugando.”

Sasa nikatambua sababu kubwa ya ujio wa Pili mkoani Mwanza ni kumleta mwanangu hospitali.
“Ulimpa jina gani?”
Mke wangu akatabasamu akaniambia:
“Nilimwita Maganga.”
“Dah umelenga mule mule”
Wote tukacheka.

Siku hiyo tuliongea mengi mule chumbani mwangu, akanielza mambo mengi tu ya kijijini, akaniambia namna baba yangu alivyochukizwa na suala la mimi kutimkia jijini Mwanza kwa ajili ya soka. Akasema mzee alikuwa hana radhi na mimi juu ya maamuzi yangu.

Mwisho akaniambia:
“Naona mambo yako sio mabaya mume wangu” “Kivipi?”
“Soka limekupa umaarufu wa haja, ingawa ulinitelekeza na mwanangu Ajibu” alisema. Sauti yake ilitia huruma, Pili alikuwa na mapenzi ya dhati mno juu yangu.

“Ni umaarufu Kiasi tu. Halafu sijawatelekeza, siku moja ningerudi tu kukuchukueni, ” nilimjibu ingawa ukweli ni kwamba sikuwa na mapenzi na mwanamke huyo, akili yangu yote ilikuwa kwa Lawalawa.

Asubuhi kulipokucha tukampeleka mtoto Bugando. Baada ya vipimo dokta akaniita ofisini kwake kunipa majibu:
“Mwanao anasubuliwa na Leukemia”
“Leukemia ni ugonjwa gani?”
“Leukemia ni saratani ya damu,”alisema. Moyo ukapiga kite, nikaogopa sana.
 
Sehemu ya 29

“Saratani!!”
Nilifahamu ugonjwa huo ulikuwa ni moja ya maradhi hatari mno.
“Ndio, ana saratani”
“Atapona?” nilimuliza kwa wahaka.
“Ipo njia moja tu.” Alisema. Nikatega sikio kwa makini kumsikiliza.

“Tiba ya Saratani hii ni upandikizaji wa cell kitalaamu huitwa stem cell transplant, Tiba hii hufanyika kwa ajili ya kurejesha sehemu ya supu ya mifupa iliyoharibika kwa kuweka supu mpya. Ila kabla ya kufanya hivyo, mgonjwa atapewa dawa za kuua seli za saratani ili kuua kabisa eneo lililo athiriwa kisha supu ama uboho mpya itapandikizwa.

Umenielewa?
“Ndio...Ndio dokta, najaribu kuelewa,” nilimjibu.
“Lakini kwenye mchakato huo huwa kuna tatizo moja tu...” alisema huku akaniangalia kwa makini sana.
Nilihisi mapigo ya moyo yakinienda kasi, nikaendelea kumisikiliza nikiwa na presha kubwa.

“Kwa hali aliyonayo mwanao lazima ‘uboho’ wa kumpandikizia mwanao itoke kwa mtu mwingine.” Alisema.
“Mimi na mama yake tuko tayari kutoa huo uboho sijui supu kwa mwanetu”nilisema harakaharaka, daktari akatabasamu kisha akaniambia:

“Tutaangalia kama itakidhi”
Mimi na mke wangu Pili tulichukuliwa vipimo, kisha tukatakiwa kusubiri majibu hadi kesho yake. Niliondoka, mke wangu Pili alibakia wodini na mtoto wetu. Japokuwa sikuwa nampenda Pili lakini uhai wa mwanangu ulikuwa kitu muhimu.

Nilitamani mno mwanangu apone, nilikuwa tayari kufanya lolote kwa ajili ya mwanangu, hata hivyo, haikuwa hivyo!!. Haikuwa hivyo kabisa. *****
Siku iliyofuati a nilirudi hospitali ya Bugando, majibu yetu yalikuwa tayari. Mimi na mke wangu, Pili, tuliingia ofisini kwa dokta na kupewa majibu:

“Kipimo nilichowafinyieni kinaitwa HLA yanii ‘Human leukocyte antigens” alisema, akaendelea “Kwa bahati mbaya, aina ya protein mlizonazo zinatofauti kubwa na za mtoto wenu, hivyo uboho wenu haufai kupandikizwa kwenye mifupa ya mwanenu. Ndio maana hata jana nilikwambieni tiba ya saratani ya damu huwa inatatiza mno.” dokta alitueleza.

“Sasa tufanye nini?”
“Ataendelea kutumia dawa za maumivu.”
“Hadi lini?” niliuliza. Dokta akawa kama anafikiria kitu fulani.

“Hadi lini dokta?” Pili naye akauliza huku machozi yakimlenga.
“Naweza kuwasidia jambo moja...” alisema dokta yule. Tukawa kimya kumsikiliza.
 
Sehemu ya 31

“Yupo binti anaitwa Lawalawa, mwezi uliopita aliwahi kumtolea uboho baba yake mzazi, na leukocyte antigens yake nahisi inaweza kumsaidia mtoto wenu. “Lawalawa!!” nilimaka. Nilishituka sana.

“Ndio Lawalawa, binti mmoja ana asili ya kiarabu, unamfahamu?” Kauli ya daktari yule ilinishitua sio kidogo, nilihisi kama daktari yule mzee kuna kitu alikuwa akijua juu yangu na lawalawa na alitaka kunichomea kwa mke wangu juu ya mpenzi wangu Lawalawa. “Unamjua?” nikaulizwa tena.

“Ndio namjua” hatimaye nilijibu. Mke wangu, alitabasamu baada ya kauli yangu, akaonekana kuwa na shauku kubwa ya kumpata mwanamke huyo.
“Basi kama unaweza kumpata anaweza kuwa mkombozi wa mwanao?”dokta alihitimisha. Hakuonekana kujua wala kuwa na hisia kama mimi na Lawalawa kulikuwa na uhusiano wa siri.

Ni Lawalawa....Hawara wangu....Huyu huyu niliyekuwa na mpango wa kumfuata mjini Tabora kabla ya ligi daraja la kwanza kuanza. Ndiye awe mwokozi wa maisha ya mwanangu. Itawezekana? Atakubali hali nilimdanganya sikuwahi kuwa na mke wala mtoto.

Leo natakiwa nimfuate nimwambie nilimdanganya. Ninaye mke na mtoto mmoja, ambaye yupo hoi kitandani kwa saratani ya damu na yeye awe ndiye mwokozi wake. Atanielewa?? Vipi kuhusu penzi langu kwake. Ndio itakuwa mwisho wake, Je mimi niko tayari kumpoteza Lawalawa.? Jibu ni hapana. Je niko tayari kumpoteza mwanangu? Jibu pia ni hapana. Nifanyeje sasa?

Nilijiuliza mambo yote hayo tukiwa tumekwisha toka chumbani kwa daktari, nilikuwa pembeni ya kitanda alichokuwa amelala mtoto wangu, Maganga.
Penzi la Lawalawa na uhai wa mtoto wangu kipi zaidi? Jibu ni rahisi tu, uhai wa mwanangu ni zaidi . Basi lazima nimkabili Lawalawa nimweleze ukweli, naye anisaidie. Niliafiki mawazo hayo.

Nilimwita mke wangu na kumtaka ajitulize pale hospitali ya Bugando mimi nifunge safari ya kumfuata mwanamke yule mjini Tabora. “Umemjulia wapi huyo Lawalawa?” mke wangu aliniuliza.
“Ni shabiki wangu wa soka uwanjani,” nilimdanganya.
 
Sehemu ya 32

“Sawa Ajibu, ila naomba uniahidi kitu kimoja.” “Kitu gani?”
“Ajibu mume wangu, niambie kama hutotuacha tena.” Mke wangu Pili aliniambia.

“Unaongea nini wewe!!” nilifoka.
“Nina maana yangu kukwambia hivyo Ajibu, nakujua wewe”
“Kwamba nitawatelekeza hapa hospitali?” Pili alinikera sana kuongea upumbavu wake mbele yangu, nilitamani hata nimtandike vibao hadharani . Sikutaka kupigizana kelele na Pili, niliondoka na kurudi hotelini kutayarisha safari ya Tabora.

Alfajiri ya siku iliyofuatia, nilidamkia stendi, nikapanda basi la Mohamedi Trans, safari ya Tabora ikaanza. Saa kumi na mbili jioni tuliingia mjini Tabora.
Kwa kuwa ilikuwa bado mapema nikaona sio mbaya nikionana naye siku hiyo hiyo.

Nilitaka siku hiyo nionane na Lawalawa ikiwezekana tutafute sehemu tulivu nimweleze juu ya maswahibu yangu.
Kwa kuwa nilikuwa na namba ya nyumbani kwa mwanamke huyo, nilichofanya ni kutafuta simu na kupiga, simu iliita kidogo, ikapokelewa na sauti tamu ya kike. Alikuwa ni mwenyewe Lawalawa.

“Lawalawa.” niliita
“Ajibu!!”
“Habari yako?”
“Nzuri, jamani leo umenikumbuka!!”
“Nipo Tabora lawalawa”
“Eeeeh upo Tabora!! Umefikia wapi?
Nikamwelekeza.
“Nakuja muda si mrefu” alisema na hapo hapo akakata simu.

Upo usemi wa Kiswahili unasema, jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza. Sikujua ni nini kingetokea siku ile Tabora baada ya kuonana na Lawalawa. Na laiti kama ningalijua, heri ningejitenga mbali na mwanamke yule. Kheri ningalibakia Mwanza na mke wangu Pili. SIKUJUA.

LISAAA LIMOJA badaye, mlango wa lodge niliyokuwa nimefikia, uligongwa. Nilipofungua, Lawalawa alikuwa wima mbele yangu. Siku hiyo alikuwa amependeza kuliko siku yoyote niliyowahi kumfahamu mrembo yule.

Alivaa sketi nzuri, ndefu iliyoburuzika hadi chini. Juu alivaa blauzi iliyombana kidogo kiasi cha kuichora picha halisi ya matiti yake. Kichwa chake kilichokuwa na nywele nyingi laini alizistiri kwa ushungi mweupe uliompendeza.

Alinirukia na kunikumbatia kwa furaha. Akiwa mwilini mwangu halufu nzuri ya manakato, ikazipa uhai tundu za pua yangu. Lawalawa alikuwa mithili ya malaika wa urembo ndani ya chumba kile.
 
Sehemu ya 33

“Mpenzi wangu nilikukumbuka mno,” alining’oneza sikioni, sauti yake ilijaa mahaba. Pumzi zake zilimtoka kwa nguvu.
Taratibu ule wahaka wa dhamira ya kumwambia ukweli ikaanza kuyeyuka. Nikajikuta nasombwa na misisimko ya huba, mapigo ya moyo yakaanza kunidunda kwa nguvu.

Sauti moja akilini ikawa inanikumbusha: Uhai wa mwanao upo mikononi mwako, fanya kilichokuleta. Mwambie ukweli kwamba una mke na mtoto, mweleze waziwazi kwamba uhai wa mwanao unamtegemea yeye. Lakini sauti hiyo ikazidiwa ushawishi na kila alichokianzisha Lawalawa.

Alisogeza mdomo wake karibu na wangu, papi zetu zikagusana, macho yake malegevu yakiniangalia kwa hisia kali. Tukaanza kunyonyana denda. Tukio hilo likachochea kuiendea hatua nyingine.

Niliingiza mkono ndani ya blauzi yake, nikawa napapasa mzunguko wa kiuno chake chembamba, mtoto wa watu akaanza kuweweseka. Kwa kweli Lawalawa alikuwa na hisia za karibu. Nilimweka kwenye kochi lililokuwa mule ndani akiwa hana nguvu.

“Tuongee kidogo.” Nilimwambia.
Hakujibu kitu, alibakia kama bubu huku macho yake yakiwa yamebadilika rangi.
“Habari za siku mpenzi?” nilimsalimu huku nikiketi kitandani.
“Ni nzuri mpenzi, nilikukumbuka tu hadi nikawa na wasiwasi Ajibu.”

“Pole sana Lawalawa, usiwe na wasiwasi tena.”
“Kuna wakati nilikuwa napata ndoto mbaya juu yako.”
“Ndoto gani tena?”
“Nilikuwa naona kama umepata manamke mwingine na umezaa naye mtoto,” alisema.

Ingawa mwanamke yule aliongea kwa hisia tu, lakini ndio hasa ulikuwa ukweli wenyewe, nilikuwa na mke na mtoto ambaye kwa wakati huo alikuwa hoi kitandani kwa ugonjwa wa saratani ya damu. Na yeye ndiye alitakiwa kumtolea uboho mwanangu ili upandikizwe kwenye mifupa yake.

“Ingetokea ndoto hiyo ikawa kweli ungeafanya nini Lawalawa mpenzi?”nilimuliza.

“Wallah ningekuacha upesi sana, katika maisha yangu huwa sipendi kusalitiwa,” alisem. Moyo wangu ulipiga kite, meneno ya mrembo huyo yalinitisha sana. Akaendelea kuniambia :
“Unajua kwa nini nataka uwe mume wangu mpenzi, Ajibu?”

“Sijui mpenzi.”
“Ni kwa kuwa wewe ni mwanaume mstarabu sana, ni mtu wa pekee, hujawahi kunichanganya na wanawake wengine, unanipenda na kuniheshimu, wewe ni tofuati na watu wengine maarufu.
 
Sehemu ya 33

Tangu umekuwa gumzo huko mwanza sijawahi kukusikia ukihusishwa na mwanamke mwingine zaidi yangu, najivunia sana wewe Ajibu, nakuomba usije kubadilika mpenzi.”

Maneno ya mwanamke huyo yalinimaliza. Uzito wa kumweleza ukweli wa maisha yangu ukawa mkubwa zaidi, pengine kauli ya Lawalawa ingeweza kuwa nzuri kama nisingekuwa na familia, kama ningekuwa mimi ni wake peke yake. Yangekuwa ni maneno matamu kwa wapenzi wapendanao.

Lakini ilikuwa tofauti, maneno yake yalikuwa ni mwiba mkali nafsini, nawezaje tena kumweleza ukweli. Uso wake unaonesha kweli ni mwanamke mwenye wivu na hasira kali pale anapochukizwa.

Labda anaweza kuniacha? Ni sawa hata akiniacha. Naweza kupata mwanamke mwingine mzuri kama yeye, ingawa sidhani kama nitampenda kama ninavyompenda yeye. Hata hivyo hitaji langu kubwa kwa Lawalawa ni yeye kumsaidia mwanangu.

Je atakuwa tayari kumsaidia mtoto wangu baada ya kubaini ukweli? Mambo yote hayo nilijiuliza kimoyomoyo. “Ajibu.” aliniita huku akinyanyuka pale kitini na kunijia pale kitandani nilipokuwa nimeketi mimi.

“Nahitaji uishi na mimi huku Tabora, nahitaji nifunge ndoa na wewe haraka iwezekanavyo, kama mtoto wa pekee, baba yangu amenikabidhi utajiri wake wote, namuhitaji mume mwema kama wewe, ambaye tutashirikiana katika kusimamia miradi yetu.

Nataka niwe na familia bora yenye tabasamu wakati wote, sioni mwanaume mwingine katika hii dunia zaidi yako Ajibu, wewe ndiye mtu sahihi kwangu.”

Kwa mara nyingine mwanamke huyo aliongea kauli iliyonisisimua mno, maneno yake yaliniingia akilini yakawa yanajirudia rudia. Shauku ya kusema kilichonipeleka tabora ikafa!! Habari za mke wangu, Pili na mtoto wetu Maganga nikazizika.
 
Sehemu ya 34

Mbele ya malaika yule mrembo, ndani ya chumba cha Lodge sikuwa na hali. Alikilaza kifua chake kifuani mwangu, mikono yake ikawa inapapasa vinyweleo vyangu, kufumba na kufumbua, mikono yangu ikawa inafanya ziara ndefu kwenye maungo ya chotara yule.

Dakika kumi zilizofuatia tulikuwa kama tulivyozaliwa kila mmoja akikata kiu yake katika mwili wa mwenziye. Nilichokuwa nakikosa kwa mke wangu Pili ni msisimko ambao nilikuwa naupata kwa Lawalawa.

*****
SIKURUDI tena Mwanza. Sikujua tena habari za mtoto wangu Maganga aliyekuwa hoi kitandani kwa saratani ya damu, sikujua kama mtoto huyo alikufa ama alikuwa bado anahema.

Kwa kweli penzi la Lawalawa lilinifanya niwe kama shetani anayetembea, nilikuwa sina wasiwasi kabisa, nikiwa na mpenzi wangu Lawalawa nilikuwa mwenye furaha na maisha wakati wote.

Hadi wakati huo hakuwa amenipeleka kwao kunitambulisha. Aliniambia ningengojea kwanza hadi baba yake atakapomkabidhi nyaraka zote za utajiri maana hadi wakati huo alikuwa amepewa jukumu la kusimamia tu utajiri wa baba yake, ila nyaraka za kumiliki mali alikuwa bado.

Alisema hivyo kwa sababu ukoo wa baba yake ambao wengi walikuwa huko nchini Oman walikuwa na tabia za kibaguzi, hivyo kunipeleka mbele ya mzee wake kwa nyakati hizo ingekuwa ni kama kucheza kamari.

Nlikuwa nimenipangia nyumba nzima pale Ipuri, na kila siku mpenzi wangu huyo alikuwa akija na kushida kwangu wakati mwingine alilala kabisa. Kwa kweli maisha yangu na msichana huyo yalikuwa matamu asikwambie mtu.

Wakati huo huo nilikuwa nimetuma barua rasmi ya kuvunja mkataba na timu yangu ya Igogo Fc ambayo nilikuwa nimeipandisha kuingia ligi daraja la kwanza. Kwa kushirikiana na Lawalawa Nililazimika kulipa kiasi fulani cha fedha kwa kuvunja mkataba na timu hiyo ambayo kwa kweli ilikuwa inanihitaji mno.

Sikupenda kabisa kurudi Mwanza, na siyo Mwanza tu bali hata kwetu huko Maji moto, niliona nahitaji kuishi maisha niyatakayo, nikiwa huru, mimi na mpenzi wangu Lawalawa.
 
Sehemu ya 35

Kwa kuwa nilikuwa nina CV yangu nzuri tu, timu ya Reli Tabora iliyokuwa inashiriki ligi daraja la kwanza ilinisajili tayari kwa kipute cha ligi hiyo ambayo ilikuwa mbioni kuanza.

kama ilivyokuwa kawaida yangu, nilipoanza tu mazoezi na timu hiyo, haraka sana nikajikuta nakuwa nyota ninayetarajiwa kufanya makubwa. Hiyo timu ilikuwa chini ya shirika la reli la taifa, Maslahi kwa wachezaji wengi pale angalau yalikuwa mazuri ukilinganisha na timu ya Igogo fc.

Lawalawa alinipa sapoti kubwa kwenye harakati zangu za mpira, alinipenda na kuniamini. Siri ya kutelekeza mke na mtoto wangu hospitali ya Bugando ilibaki kuwa siri iliyonitesa na kunisimanga nafsini. ****

Ni karibu miezi mitatu ilikuwa imepita, ligi daraja la kwanza ikaanza, kama kawaida yangu nilikuwa nikiibeba mno timu yangu. Kila nilipopata nafasi ya kupachika mabao sikufanya makosa.

Nilikuwa nina nguvu, kasi na control nzuri ya mpira, katika mechi za mwanzo tu tuliongoza kundi letu. Kwa bahati mbaya katika kundi lile, tulikuwa pamoja na timu yangu ya zamani ya Igogo Fc ambayo nayo kwakweli ilikuwa inafanya vizuri.

Ligi daraja la kwanza ilikuwa ni ligi ngumu yenye rapsha nyingi uwanjani. Michezo ya kihuni na hila ilikuwa ni vitu vya kawaida. Mwanzoni nilipata tabu mno, lakini kadiri ligi ilivyozidi kwenda ndivyo nilivyozidi kuzoea. Nikawa napambana kufa na kupona, ndoto yangu ilikuwa ni kucheza ‘premier’na kuwa mchezaji wa kimataifa.

Tulikuwa na mchezo mmoja nyumbani na timu moja kutoka Kigoma, kisha tungesafiri hadi jijini Mwanza ambako tungecheza na timu yangu ya zamani ya Igogo Fc.
 
Sehemu ya 36

Hakuna kitu nilikuwa sipendi kama kwenda Mwanza, sio kwamba mji ule nilikuwa siupendi.

Laa! Ila nafsi yangu ilikuwa haipendi kupata kumbukumbu ya kitendo cha kuitelekeza familia yangu hospitali ya Bugando na kutimkia mjini Tabora kwa Lawalawa.

Tukio hilo lilizidi kunitesa kisaikolojia, kila wakati sauti ya mke wangu Pili ikinisihi nisiwaache ilikuwa ikijirudia. Picha ya mwanangu akiwa anateseka kitandani ikawa inajitengeneza kichwani mwangu.
Tulicheza mchezo wetu na timu ya Kigoma fc, mchezo huo tukashinda mabao matatu kwa bila, wakati magoli mawili nikifunga mwenyewe huku lile moja nikitoa asist.

Siku chache baada ya mchezo huo, kocha akatutaka wachezaji tujitayarishe kwa safari ya Mwanza kwa ajili ya mchezo wa na Igogo fc, siku hiyo kutwa nzima nilikosa raha. Kwa kweli sikupenda kabisa kufika katika jiji lile.

Siku ya pili tuliondoka na treni kuelekea Mwanza, wachezaji tulikuwa kwenye mabehwa ya daraja la kwanza. Wakati wenzangu wakicheza karata na kufurahia pamoja safarini, mimi nilikuwa peke yangu nikiwa nimezama kwenye lindi la mawazo.
“Unamuwa nini?” daktari wa timu aliniuliza.

“Hapana naifikiria mechi tu.” nilimdanganya
“Una presha?”
“Ndio, si unajua ni timu niliyotokea.”daktari yule ambaye pia alikuwa mtaalamu wa mambo ya saikolojia alianza kunijenga kiakili.

Tuliwasili Mwanza asubuhi ya siku iliyofuatia, tulifikia katika lodge moja nzuri tu ambayo kwa kweli jina lake sikumbuki vizuri. Baada ya kupumzika kidogo, niliomba ruhusa ya kutoka.
Kwa kuwa walitambua nilikuwa mwenyeji kwenye mji ule, hilo halikuwa tatizo kwao, viongozi wangu wa timu waliniruhusu.

Nilichukua gari hadi Bugando, nikaelekea hadi katika ofisi ya daktari aliyekuwa akimuuguza mwanangu. Kwa bahati nzuri nilimkuta hana wagonjwa wengi, alinikaribisha kitini na kunisikiliza:
“Unanikumbuka dokta?” nilimuliza.
“Vizuri sana, nakukumbuka. Wewe si baba wa yule mtoto aliyekuwa anaumwa kansa ya damu?”

“Naam!! ndio mimi dokta, tangu kipindi kile ndio narudi Mwanza leo.”
“Kwa hiyo huna taarifa ya kilichomkuta mwanao?” dokta aliuliza huku akiningalia kwa chati.
“Sina dokta. ”
“Yule mtoto alifariki dunia,”dokta aliniambia kwa ufupi.
 
Back
Top Bottom