SEHEMU YA 12
Kelele zilikuwa zikisikika nje, nikashtuka kutoka katika usingizi mzito. Kitu cha kwanza kabisa nilianza kujiuliza ni mahali gani nilipokuwa, baada ya akili kukaa sawa na kukumbuka nilikuwa nchini Sudan, nikainuka kitandani na kwenda dirishani kuchungulia ili kujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea huko.
Niliwaona watu wakikimbia huku na huko, wanajeshi wa Serikali walikuwa wameingia mitaani huku lengo lao likiwa ni kuwatafuta wanajeshi wa kikundi kilichojiita DLF (Darfur Liberation Front) ambacho kilikuwa kinyume na Serikali ambayo ilikuwa madarakani.
Haraka sana nikaichukua kamera yangu kwani kile kilichokuwa kikiendelea kilinivutia mno, nikaanza kurekodi kupitia dirisha la chumba changu.
Mule nilipokuwa nilihisi kama siridhiki hivyo kwa haraka sana nikavaa suruali yangu, nikachukua kitambulisho changu cha bandia ambacho kilinionyesha kuwa ni mwandishi wa habari kutoka katika Shirika la Habari la Al Jazeera na kuelekea nje huku kamba yake nikiwa nimekining’iniza shingoni.
Nilipofika nje, nikaanza kurekodi, nilikuwa nikiendelea kurekodi kimoja baada ya kingine, jinsi wanajeshi wa serikali walivyokuwa wakiwatafuta watu hao na mambo mengine mengi tu.
Hapo niligundua kwamba nilikuwa nikifanya kosa, kwa sababu ile ilikuwa ni makala ihusuyo mambo mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea nchini Sudan, yalihitaji maelezo ili kila atakayeiangalia aielewe.
Kwa haraka sana macho yangu yakaanza kuangalia huku na kule na kutua kwa kijana mmoja ambaye alishika madaftari, umri wake bila shaka nilikuwa nimemzidi kidogo.
Nikamfuata kujitambulisha kwamba nilikuwa mwandishi wa habari na hivyo nilihitaji msaada wake.
Hakufahamu Lugha ya Kingereza vizuri lakini tuliweza kuelewana.
Nilichokifanya ni kumpa kamera ile na kuanza kunirekodi kwa malipo ya paundi mia tano za Sudan.
Kazi ikawa imeanza, nilikuwa nikielezea kila kilichokuwa kikiendelea huku kijana yule aliyejitambulisha kwa jina la Majeed akiendelea kunirekodi.
Mahali pale sikuwa mimi peke yangu, waandishi wengine wa BBC, CNN walikuwahapo huku nao wakichukua habari juu ya kila kilichokuwa kikiendelea mahali pale.