SEHEMU YA 07
Maandalizi yangu yaliendelea zaidi na zaidi, baada ya miezi miwili, nikawa nimekwishagongewa viza ya kukaa kule kwa muda wa miezi mitatu.
Bado siri iliendelea kuwa siri tu, sikuwaambia wazazi wangu na wala sikumwambia mpenzi wangu, Myra kwani nilimuona msichana huyo kuwa kama wazazi wangu tu.
Kiu ambayo nilikuwa nayo katika kipindi hicho ni kuwa mwandishi mkubwa wa kimataifa, mwandishi ambaye ningeweza kufanya kazi ya uandishi katika mashirika makubwa duniani, sikutaka kuonekana kujali au kuhofia kuuawa, kwangu niliamini kwamba nafsi zote zingeonja mauti, haijalishi kama ni Mchungaji au Imamu, wote wangeonja mauti.
Ingawa nilifahamu fika kwamba nchi ya Sudan haikuwa na usalama mkubwa katika maisha yangu lakini katika kipindi hicho sikuonekana kuhofia kitu chochote kile, yaani nilijiona kwamba ningeweza kufika salama na kurudi salama nchini Tanzania ambapo ningeendelea na maisha yangu huyku nikianza kuipeleka makala yangu katika mashirika mbalimbali ya habari.
Naikumbuka sana siku hii ya tarehe 12/11/2005 siku ambayo nilianza safari yangu ya kuelekea nchini Sudan. Moyo wangu ulikuwa na furaha kubwa sana, sikuamini kama katika kipindi hicho nilikuwa nimeweza kuondoka nchini Tanzania na kuelekea nchini Sudan kwa ajili ya kutengeneza makala moja ambayo kila mtu ambaye angeiangalia basi angeonekana kushangaa sana.
Ndani ya ndege nilikuwa na mawazo mengi, nilikuwa nikiwafikiria wazazi wangu ambao nilikuwa nimewaambia kuhusiana na safari hiyo lakini hawakuonekana kuwa radhi kuniruhusu kuelekea katika nchi hiyo ambayo vita vya wenyewe kwa wenyewe vilikuwa vikiwasumbua sana.
Ukiacha na wazazi wangu, pia nilikuwa nikimkumbuka mpenzi wangu, Myra ambaye nae wala hakutofautiana sana na wazazi wangu, kwani nae hakutaka nielekee katika nchi hiyo.
Nilijiona nikiwa nimefanya maamuzi magumu sana, maamuzi ambayo baadae yangeweza kuleta lawama za kila aina, sikutaka kujali kuhusiana na lawama ambazo ningezipata, nilichokuwa nikikitaka ni kuwa mwandishi mkubwa sana ambaye ningeonekana kuifanya dunia kuelewa kwa undani kile ambacho kilikuwa kikiendelea ndani ya nchi ile.