SEHEMU YA 75 •
•
•
“Dickson! Kwa nini usitafute mwanamke mwingine?”
“Siwezi! Nilianza kukupoteza Nandy! Kwa sasa, sitoweza kukupoteza tena. Kwako sihitaji watoto, sihitaji kufanya mapenzi, nikiwa na wewe tu najisikia amani, najisikia furaha, najiona kukamilika kama mwanaume,” alisema Dickson, akachukua mkono wa Nandy na kumvisha pete ya uchumba huku wazazi wao wakiwa kwa mbali wakiangalia.
Ulikuwa ni ushujaa mkubwa kwa Dickson, kwake hakutaka kujali kitu chochote kile, alichokuwa akikiangalia ni kuwa na msichana huyo tu.
Baada ya kukaa miezi miwili, wakaondoka na kurudi nchini Tanzania. Njiani walikuwa wakizungumza mambo mengi mno, walikuwa wakifurahia pamoja japokuwa kwa msichana Nandy hakuweza kufanya kitu chochote kile.
Walipofika, maisha yakaanza upya. Dickson hakutaka kuona Nandy akikaa peke yake, alichokifanya ni kumuhamisha nyumbani kwao na kuanza kuishi na yeye. Hakutaka kusoma tena, alichokifanya ni kusimamia biashara za baba yake.
Akamuajiri msichana wa kazi za ndani aliyeitwa Maria ambaye huyo alitakiwa kukaa na Nandy na kumuhudumia kwa kila kitu.
Wakati akiwa ameishi nchini Tanzania kwa siku tatu, ghafla akashtukia akipokea ugeni kutoka katika Kituo cha Polisi cha Osterbay na kuambiwa kwamba alikuwa akihitajika huko kwa kuwa kulikuwa na kesi ya kubaka iliyofunguliwa.
“Nilibaka?” aliuliza, alisahau kabisa kuhusu Amina.
“Ndiyo!” alijibu polisi mmoja na kumfunga pingu, wakaanza kuelekea kituoni.
Wakati akiwa ndani ya gari la polisi ndipo kumbukumbu ya tukio hilo lilipomjia kichwani mwake. Alikumbuka namna alivyotumiwa video akiwa anafanya mapenzi na Amina ambaye alionekana kama alikuwa akimbaka.
Moyo wake ukawa na hasira zaidi na Linda kwani aliamini kwamba msichana huyo ndiye aliyekwenda kituoni na kufungua kesi hiyo.
Alipofikshwa huko, akatupwa selo na kuambiwa asubiri kwani kesi yake hiyo nzito ilikuwa ikiandaliwa tayari kwa kupelekwa mahakamani ambapo ingeanza kusikilizwa na kama angekutwa na hatia, alitakiwa kufungwa gerezani kwa miaka isiyopungua thelathini.
JE, nini kitaendelea?