SEHEMU YA 70
“Hawezi kufa akiwa kitandani, kuna siku atasimama na kutembea tena,” alisema Dickson huku akilia kwa sauti kubwa kiasi kwamba kila mmoja aliyekuwa hospitalini hapo akahisi kuwa mgonjwa wake alifariki dunia.
Siku zilikatika na baada ya miezi mitatu na nusu, hatimaye muujiza ukaonekana kwa Nandy, akayafumbua macho yake na kuanza kuangalia huku na kule.
Kitu pekee alichokuwa akikikumbuka ni kupata ajali mbaya akiwa kwenye pikipiki, baada ya hapo hakujua ni kitu gani kiliendelea.
Akaanza kuyapeleka macho yake huku na kule, mashine ya kupumulia ilikuwa puani na mdomoni mwake, kwa juu yake aliiona dripu ikiwa inaning’inia, hakutaka kujiuliza, kwa jinsi ajali ile ilivyokuwa imetokea, alijua kabisa kwamba hapo alipokuwa ilikuwa ni hospitalini.
Akajaribu kuinuka kitandani pale, akashindwa, mwili wake ulikuwa haufanyi kazi kabisa. Kiuno kilikataa kutingishika, alijaribu kuitingisha mikono yake, akashindwa kabisa, ilikuwa ni kama mtu aliyepigwa sindano ya ganzi.
Hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, mwili wake ulikosa mawasiliano na ubongo na kitu pekee alichokuwa na uwezo wa kukitingisha kilikuwa ni kichwa chake tu.
“Nini kimetokea?” aliuliza kwa sauti kubwa iliyowafanya manesi wawili kuingia chumbani hapo.
Walipomuona Nandy amefumbua macho, mmoja akatoka na kwenda kumuita daktari. Ulikuwa ni mwezi wa tatu tangu afikishwe hospitalini hapo, alikuwa kimya, alipoteza fahamu na hatimaye siku hiyo aliyafumbua macho yake na kuangalia tena.
Daktari alipofika, akatoa tabasamu pana. Alishangaa, manesi waliokuwa mbele yake walikuwa Wahindi na hata daktari aliyekuwa ameingia ndani ya chuma hicho alikuwa Mhindi pia.
“Where Am I?” (nipo wapi?) aliuliza Nandy.
“In the hospital!” (hospitalini)
“Agha Khan?” “No! Apollo, India,” (Hapana! Apollo, India) alijibu daktari huyo.
“Doctor! What is wrong with me? I can’t move my legs, hands, what is wrong with me?” (Dokta! Nina tatizo gani? Siwezi kuisogeza miguu yangu, mikono, nina tatizo gani?) aliuliza Nandy huku akiwa kitandani pale.