SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

Duuh hii ni nouma kwel mkufu wa malkia wa goshen n hatariii ndo umezua yote haya, Sultan na wakeze wamekufa hatar.
 
Hiii kuuana tena.!! Ya nn yote hayo. Kama kaamua kuoa acha aoe waume wapo kibao tu.!! Sultana mkubwa duuh.!!
 
Malkia na Zura wapi mbona kimya au aliporudi kumtafuta Zura naye ndo ikawa mwisho. But Malkia ni Sterling why afe mapema kabla move haijafika ukomo. Najaribu kuwaza tu.!
 
Malkia na Zura wapi mbona kimya au aliporudi kumtafuta Zura naye ndo ikawa mwisho. But Malkia ni Sterling why afe mapema kabla move haijafika ukomo. Najaribu kuwaza tu.!
Anakufaje kwa mfano alishindwa kufa mwanzo ataweza kufa sasa hivi
 
*MKUFU WA MALKIA II -- 55*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Haraka wakenda huko. Ilikuwa ni stoo. Wakamkuta Sultana mkubwa akiwa ananing'inia kitanzini!!

Ameacha ujumbe karatasini ukiwa umeandikwa na damu. Karatasi imeshikizwa na ncha ya kisu ukutani.

ENDELEA

Wakautoa mwili huo na kuuweka chini. Bibi akachukua kile kikaratasi kilichoachiwa ujumbe na kukipeleka machoni akisome.

'Kama ilivyokuwa na mwanzo, hii ndiyo mwisho. Maisha haya hayana maana tena kwangu. Na siwezi kuwaacha watu wakifurahia kwa mgongo wa maumivu yangu.'

Bibi akajawa na machozi machoni. Duku likamkaba kooni akatamani kupiga yowe. Akasaga meno yake kwanguvu akiumia sana kifuani.

Habari ilikuwa imekwisha!

Hakukuwa na Sultan tena wala Sultana zake. Wote wakawa habari ya upepo!!

**

"Amkeni!" Sauti ilifoka. Oragon na Ottoman wakakurupuka na kukaa sawa. Mbele yao walikuwa wamesimama wale wanaume wawili waliowakarimu na kuwapatia makazi.

Wanaume hao hawakuwa wamevalia vema. Wapo hovyo na wala wasiokane kujali. Mmoja wao, yule mfupi alikuwa anachokonoa meno yake na jiti kubwa. Meno yake yalikuwa na rangi ya kahawia.

Mwenzake huyu mrefu alikuwa amesimama akishikilia kiuno chake akiwatazama wakina Oragon kwa macho malegevu.

"Mnalalaje mpaka saa hii?" Akauliza huyu mrefu. "Mmeridhika na hali zenu, sio?"

Oragon na Ottoman wakatazamana wasijibu kitu zaidi ya kutazama chini. Si kwamba walikuwa wamechelewa sana. Wala. Bado jua halikuwa limesimama. Kulikuwa kuna ka-giza ka-asubuhi. Ndege wakiwa wanaimba madirishani.

"Amkeni. Leo kuna kazi kabambe ya kufanya," alisema mfupi baada ya kuchomoa jiti lake mdomoni. "Hapa hamna kula bure, lazima mfanye kazi."

Ni kweli hata maandiko yasema pasi na kazi pasi na kula. Lakini kazi hii wanayotaka kuwapatia vijana hawa majira haya ya asubuhi ya mapema hivi, ilikuwa ni ipi?

Oragon akaamka na kaka yake. Wakasimama na kuwafuata wanaume wale wenyeji wao mpaka kwenye kachumba fulani kadogo kachafu kamejawa na vitu lukuki. Humo yule jamaa mrefu akatoa kifurushi kidogo na kuwakabidhi.

"Mnaona hiyo?" Akauliza akikaza macho yake malegevu. "Mnatakiwa kupeleka kwa Rabis."

Kabla wakina Oragon hawajauliza Rabis ni nani, yule jamaa mfupi akadakia na kuwadadavulia:

"Rabis ni mkuu wa wahuni wote ndani ya himaya. Lazima kila mmoja atoe kodi kwake kila baada ya majuma kadhaa. Sasa hakikisheni hiyo imefika mikononi mwake. Mtajitambulisha kama wana wa mwewe!"

"Wana wa mwewe?" Ottoman akashangaa.

"Ndio," yule jamaa mrefu akajibu upesi. "Ukimwambia hivyo atawaelewa. Nyie fikisheni mikononi mwake."

"Anapatikana wapi?" Oragon akauliza. Mtu yule mfupi akampatia ramani.

"Hakikisheni mnaufikisha mzigo huu mikononi mwake ... mikononi mwake ... alafu mseme amewatuma wana wa mwewe. Tumeelewana?"

**

Baada ya kutembea kwa umbali wa muda kidogo, Oragon aliamua kumshirikisha mwenzake maswali kadhaa yaliyokuwa yanamtatiza kichwani. Mkono wake wa kuume alikuwa amebebekea kifurushi walichoagizwa. Jasho linaamchuruza.

"Kwanini wametutuma mzigo nyeti kama huu kwa mtu wao mkubwa kiasi hicho? Hawakuweza kuupeleka wenyewe?"

"Pengine walitaka tu na sisi tushughulike," Ottoman akajibu. Alikuwana anatafuma muwa.

"Sidhani, sidhani kabisa!" Oragon akakataa akitikisa kichwa. "Kupeleka kodi. Tena kwa huyo mkubwa wao, alafu watutume?"

Akamtazama kaka yake vema.

"Hatujui huko tuendako, twaenda na ramani. Hata sura ya Rabis hautuifahamu. Huoni ni hatari?"

Ottoman hakujibu kitu. Kwake hakuona tabu, akaamua kuwa bize na kutafuna mua wake.

"Na hiyo kodi ni nini haswa?" Oragon akaendelea kuuliza. "Vipi kama ni zile fedha zetu walizotukwapua?"

Hapo kidogo Ottoman akaguswa. Akamtazama kaka yake kwa macho ya tahadhari.

"Oragon!" Akaita. "Oragon, sitaki kuingia kwenye shida nyingine saa hii! Tafadhali mimi nishachoka kuishi kama digidigi!"

Akameza fundo la muwa kisha akaendelea.

"Hata kama tukikwapua hiyo kodi tutaenda kuishia wapi?"

"Nani kasema tunaikwapua?" Oragon akajishuku.

"Sasa kuniuliza maana yake nini?" Ottoman akamtambia. "Tafadhali, tuufikishe huyo mzigo unapotakiwa. Naomba tuishi kwa amani."

Kukawa kimya kwa dakika kadhaa wakitembea. Lakini wasidumu muda mrefu, mara wakasikia vishindo vya miguu nyuma yao. Walipotazama wakawaona wababa wawili wakija kwa kasi.

Kutazama vema, walikuwa ni vijakazi wa Mzee Raam!!

Lahaula!

Haraka wakaanza kukimbia. Wakipishana na watu huku na huko. Lakini hawakufika mbali wakakutana na mwingine mbele yao. Akawadaka!!

"Leo ndiyo mwisho wenu!" Akasema mbaba huyo kisha akacheka. Wakawabeba wakina Oragon na kutokomea nao mbali na watu ili wakawamalize huko!

Huko ambapo hamna mtu atajua. Wala atayejali.

Wakazama msituni. Mmoja wao alikuwa tayari ameshachukua kile kifurushi walichokabidhiwa vijana hao wakipeleke kwa Rabis. Walipozama msituni kinani wakawatenga vijana hao wakiwa tayari wamewafunga mikono na miguu.

Mmoja wao, yule mpana, jabali, akachomoa jambia lake tayari kuwanyofoa roho.

"Sala zenu za mwisho?" Akauliza wakati awaulizao amewafunga kitambaa mdomoni. Ooh! Akakumbuka, akawaondolea kitambaa mdomoni na kurudia swali lake.

"Tunakuomba usituue!" Akalia Ottoman. "Tumefanya kosa gani mpaka tukastahili haya?"

"Hamjui?" Muuaji akauliza. "Mmeona hayo?" Akaonyeshea kidole mazingira yaliyowazunguka. Kulikuwa kuna mifupa na baadhi ya miili ya watu iliyooza. "Wote hao wamekufa kwasababu sawa na ya kwenu. Kosa la kujua siri ya kuhani!"

Baada ya kusema hayo, hao wanajeshi, vijakazi wa Raam, wakacheka kama mazuzu. Wakina Oragon wakapaza makelele ya kuomba msaada. Wakazidi kuwafanya wanaume hawa waangue kicheko.

"Unadhan kuna anayekusikia?" Akauliza muuaji kwa sura ya mzaha. "Hakuna anayesikia kelele zako. Na hata wale watakaosikia wanaogopa kuja!"

Akanyua jambia lake juu, lakini kabla halijatua mara muuaji akadunguliwa na mshale wa shingo. Akadondoka akitapatapa. Hawajakaa vema, na wale wawili nao wakala mishale ya vifua na kufa papo hapo!!

Mara wakatokea wale majamaa waliowatuma wakina Oragon. Mikononi mwao walikuwa wamebebelea pinde za mishale. Wakawajulia hali wakina Oragon na kuwafungua kamba zao.

Wakawaeleza kumbe walikuwa wakiwafuatilia kwa nyuma tangu walipotoka kwenye makazi yao. Lakini kuna jambo walilisikia kutoka kwa wale wajakazi wa Kuhani.

Siri.

Ni siri gani hiyo? Wakawauliza wakina Oragon. Ni siri gani inayowatia hatiani mpaka kutaka kuuawa? Na hata wengine wakiwa tayari wameshanyofolewa roho zao kwasababu hiyo?

"Kuhani ni shoga," Ottoman akawahi kunena. Wale majamaa wakaachama midomo yao wazi kwa kuduwaa.

"Anataka vijakazi wake wamhudumie, mimi nilishindwa," alieleza Oragon. "Sasa akasema hiyo ni siri, hayuko radhi himaya yote ikajua. Ndo maana anawinda roho zetu!"

Wale majamaa wakatahamaki. Alah!! Lilikuwa jambo kubwa hili? Wakatazamana na macho ya kustaajabu alafu yule mfupi akauliza:

"Ni kweli?"

"Ndio, ni kweli!" Oragon akamsisitiza.

Mara wale wajamaa wakaangua kicheko. Sasa kwanini hamkuwapatia hiyo huduma? Wakauliza. Lakini wasijali sana, wakawataka wakina Oragon waendelee na safari yao ya kwenda kwa Rabis.

"Fanyeni upesi muda unaenda!"

Wakaelekea zao.

Wale majamaa wakabaki hapo wakijiuliza cha kufanya. Lile jambo la Kuhani lilikuwa kubwa na lingeweza kuwaingizia fedha kubwa wakawa matajiri.

Akili zao za kipumbavu ziliwaza!

Twaweza uaga ufukara hapa. Wakawa wanasemezana huku wakiishilia.

**

Siku hii ikiyoyoma, wakafika mbele ya makazi ya Rabis. Nyumba kubwa chakavu. Mbao zake zilikuwa zimetoboka na zimefubaa. Mabati yake yamerendemka na kuota kutu.

Hapo nje kulikuwa na zizi kubwa la nguruwe. Zizi hili lilikuwa chafu, limejawa na nguruwe lukuki waliokuwa wamepoteza rangi za muonekano wao. Lakini walikuwa wamenona haswa.

Sijui walikuwa wanakula nini!!

Mbali na nyumba hiyo, hakukuwa na nyumba nyingine kwa pembeni wala hatua kadhaa kwa umbali. Nyumba ilikuwa imejitenga kana kwamba ipo jangwani.

Pweke.

Kunguru kadhaa walikuwa wamesimama juu ya paa. Wanatazama huku na kule.

Kabla Oragon na Ottoman hawajapiga hatua kujongea ndani ya nyumba, wakaisikia sauti kali ya mtu akilia! Kunguru wote waliokuwa juu ya paa wakarusha mbawa zao kuruka!

Oragon na Ottoman wakatazamana.
 
*MKUFU WA MALKIA II -- 56*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Kabla Oragon na Ottoman hawajapiga hatua kujongea ndani ya nyumba, wakaisikia sauti kali ya mtu akilia! Kunguru wote waliokuwa juu ya paa wakarusha mbawa zao kuruka!

Oragon na Ottoman wakatazamana.

ENDELEA

Walikuwa na hofu mioyoni mwao. Akili yao ilitengeneza picha kubwa Rabis kama bonge la mtu anayeogopeka na hata kuua ama kutesa wanaomkosea. Penngine mawazo yao yalikuwa sahihi.

Ila ni mpaka pale walipoenda kuthibitisha kwa macho yao.

Wakabisha hodi mara mbili mlangoni na punde wakasikia kishindo kizito kikijongea mlango. Huyu ndiye Rabis! Wakatetemeka mioyo.

Mara mlango ukafunguliwa na jibaba kubwa lililoshikilia panga mkononi. Nguo zake zilikuwa chafu zimelowana damu. Alikuwa ana ndevu na nywele lukuki kichwani.

Macho makubwa ya kutisha. Pua ndefu iliyochongoka ila mdomo usionekane kisa kufunikwa na ndevu.

Aliwatazama wakina Oragon pasipo kuteta jambo. Alafu akaufungua mlango wazi waingie. Wakazama humo ndani na kukuta watu kadhaa, kwa haraka kama vile kumi na wawili, wakiwa wamesimama na kila mtu akiwa na mzigo wake, aidha ndani ya kifurushi, ama mkoba.

Lakini humu ndani palikuwa pakubwa sana. Kwa mbali kidogo na watu waliosimama kulikuwa na kama kimadhabahu kidogo. Kuna kiti hapo na mtu mmoja mfupi, miguu hata haigusi chini, alikuwa ameketi.

Alikuwa ana nywele ndefu nyeusi. Vidole vyake vimejawa pete za dhahabu na shingo yake pia. Mikufu inayong'aa!

Chini yake kulikuwa kuna vifurushi kadhaa vikiwa vimewekwa hapo.

Kushoto kwake kulikuwa kuna damu zimetapakaa. Mwili mmoja umelala hapo kimfu. Si bure alikuwa ndiye yule aliyepiga kelele muda si mrefu, kunguru wakawehuka.

Mbali na hapo humo ndani hakukuwa na kitu kingine cha maana zaidi ya samani zilizochoka, mkangafu, japokuwa palionekana ni eneo zuri likifanyiwa matengenezo.

Lile jibaba liliwaelekeza wakina Oragon mahala pa kusimama, kule walipo wenzao, kisha likaenda kusimama kando na yule mtu ambaye ameketi kwenye kiti. Ambaye bila shaka ndiye Rabis!

Akamuagiza,

"Pelekea nguruwe!" Akionyeshea maiti iliyokuwepo hapo chini. Yule jibaba likaunyanyua ule mwili, bado ukiwa unaendelea kuvuja damu, akaenda nao nje.

Si bure wale nguruwe walikuwa wanono kiasi kile. Wanalishwa nyama za binadamu!! Oragon na mwenzake wakatetemeka. Hawakujua ni kwanini mtu yule aliuawa. Pengine nao watauawa kama yule kisha wakalishwe nguruwe!!

Tena lililowapa uoga zaidi, hawakuwa wanamjua Rabis hata punje. Hawakuwa wanajua mwanaume huyo anataka nini, nini miiko yake wala laana!

Basi wakiwa wanameza mate, wakanyamaza watazame namna mambo yanavyoenda.

Wakasonga kwenye ule mstari. Mtu wa kwanza wakamwona akiwa amefikisha mbele kifurushi chake. Rabis akatazama kilichomo ndani na mara akamtikisia kichwa.

Mtu huyo akaenda zake!

Akaja wa pili na wa tatu. Wote hawakuwa na shida. Lakini mmoja aliyefuata alikuwa ameshikilia kifurushi kilichosinyaa. Uso wake ulikuwa na woga. Mikono yake ilikuwa inatetemeka.

Alimkabidhi kifurushi Rabis, Rabis akakitazama kisha akamtazama yule jabali lake la pembeni, mara jabali akamnyaka huyo jamaa na kumsukumia chini. Akamkatakata!!

Kisha kama kawaida akamnyanyua na kwenda kupeleka maiti kwenye banda la nguruwe wamtafune!

Ulipopita muda mfupi, wakina Oragon nao wakafika mbele ya Rabis. Walikuwa wanatetemeka sana. Walimkabidhi Rabis kifurushi chao kisha wakajitambulisha, wao ni wana wa mwewe!

Basi Rabis akawatazama kana kwamba anawapekua. Akatazama na ndani ya kifurushi kisha akabinua mdomo wake.

"Wana wa mwewe!" Akasema kwa kebehi. "Mnajifanya wajanja sio?"

Oragon na Ottoman wakatazamana. Kisha wakatikisa kichwa.

"Yani ushuru wote ninaowadai, muda wote huo, huu ndiyo mmeniletea?" Rabis akauliza akitoa macho.

"Hapana, sisi hata hatujui. Wametukabidhi tulete tu hapa hakuna lolote tunalolifahamu."

Rabis hakuamini. Akamuagiza yule jabali awakamate na kuwashughulikia vijana hao haraka iwezekanavyo!!

Basi wakina Oragon wakadakwa kwa mkono mmoja tu, wakatupiwa chini. Jabali akapandisha panga lake nene juu! Mara

"Msituue! Tuna kingine cha kuwapa!" Akaropoka Oragon.

Rabis akamzuia jabali kutenda kazi yake, kisha akauliza:

"Ni nini hicho?"

**

Sasa alikuwa anafahamu safari yake inaelekea ukingoni. Moyoni alijawa na furaha sana na hakutaka kungoja tena kuijaza zawadi mikono mwake.

Waheed akatabasamu. Mbele yake kulikuwa kuna lango kubwa. Lango kubwa la chuma. Na humo ndani ndimo kuna kofia ya pharao!

Akasogelea lango hilo na kuweka kiganja chake hapo. Mara lango likang'aa na kujiandika maneno kadhaa:

'Ndani mfalme amepumzika. Ni nini unataka?'

Waheed akatabasamu mwenyewe. Alikuwa ana hamu pomoni kushuhudia kwa macho yake kitu ambacho amekuwa amehadithiwa maisha yake yote.

Basi kwa kutumia kidole chake akaandika:

'Nataka kofia ya pharao'

Akangoja majibu. Kimya.

Akaweka tena kiganja chake juu ya lango. Mara maneno yale yaliyotokea awali yakajiandika tena.

'Ndani mfalme amepumzika. Ni nini unataka?'

Waheed akaandika:

"Nataka kofia ya Pharao'

Ikawa kimya tena. Hakupata majibu. Akaweka kiganja kwa mara nyingine. Mara hii akaandika anaomba kofia ya Pharao. Bado majibu yakawa yaleyale. Kimya. Akaweka tena kiganja na sasa akaandika tafadhali naomba kofia ya Pharao.

Majibu hayakubadilika. Kimya.

Akashika kiuno chake akiwaza. Fikra ikamjia kichwani. Akaweka kiganja tena kwenye lango, mara hii akaandika:'

'Nataka kumwamsha Pharao!'

Mara lango likaandika kuuliza:

'Unacho cha kumfanya aamke?'

Waheed akafikiri kwanza. Tamaa ikamzidi hamu akaandika kujibu:

'Ndio.'

Mara lango likafunguka. Waheed akazama ndani na lango likajifunga. Humo ndani kulikuwa na kama kauwanja. Kwa mbele, juu kidogo, kulikuwa na kiti kimoja kikubwa kilichotengenezwa kwa dhahabu.

Kwenye kiti hicho alikuwa kulikuwa kumekaliwa na mifupa ya binadamu. Haikuonyesa chembe ya uhai. Mifupa hiyo ilikuwa ni ya Pharao aliyekufa miaka lukuki huko nyuma!!

Juu ya fuvu ya mifupa hiyo kulikuwa na kofia ya dhahabu! Kofia inayometameta. Kofia ambayo kwa kuitazama ungetambua ni ya thamani kiasi gani!

Japo ilikuwa ya muda mrefu hapo nyuma, kofia hii bado ilikuwa mpya. Inavutia machoni na kushawishi kuinyakua!!

Waheed mate yakamtoka. Sasa kazi kwake ilibakia moja tu. Kwenda kuinyakua kofia ile na kutokomea zake akaitawale dunia.

Lakini kabla hajapiga hatua kuifuata kofia hiyo, akawaza. Li kwapi jeshi la wafu?? Lile alilokuwa anaambiwa habari zake za kutisha kwamba ukizama humo basi utapambana nalo??

Akatazama kando na kando, hakuona kitu! Kakiwanja haka kalikuwa cheupe, mabaki tu ya vitu vya kale hapa na pale. Mbali na mifupa ya Pharao hakukuwa na mifupa mingine ya ziada.

Basi Waheed akaanza kujongea kuelekea kitini. Moyoni alikuwa ana hofu, akawa anatazama nyuma na pembeni yake mara kwa mara.

Akafika kitini hapo. Akameza mate kwanza. Akashika kofia ile na taratibu akainyofoa kichwani kisha akatulia kusikilizia kama kuna lolote litatokea. Kimya. Hakuna kitu!!

Akatabasamu na kushusha pumzi ndefu.

Akakumbatia kofia ile na kuanza kupiga hatua za haraka kwenda langoni. Akaweka kiganja chake hapo, na mara Lango likaulizia ahadi aliyoiweka hapo awali kwa njia ya maandishi.

"Umeshamwasha mfalme?"

Kabla Waheed hajajibu, mara lango likaandika tena:

"Ahsante kwa kutimiza ahadi."

Hapa Waheed akashtuka. Ahadi gani hiyo? Mbona hakumwamsha mfalme??

Kutazama nyuma, hamaki akaona mifupa ile iliyokuwa imeketi pale kitini, imenyanyuka!!

Pharao alikuwa ameamka!

Mara Lango likafunguka, Waheed akataka kukimbia, lakini asiende popote akakutana na JESHI LA WAFU mlangoni!!

Watu hawa wote walikuwa ni mifupa tu. Mikononi mwao walikuwa wamebebelea mapanga yaliyoota kutu. Wengine wakiwa na mikufu shingoni ama pete za dhahabu vidoleni.

Waheed alipotazama vema, akashtuka, kwa kando alimuona Seth, mara akamwona na Alk - jitu la Azeth, mwishowe Fluffy!!

Watu hawa wote walikuwa wafu. Miili yao bado ilikuwa na mabaki ya damu na matundu ya visu walivyokitwa na Waheed.

Nao walikuwa tayari miongoni mwa jeshi la wafu. Macho yao yalikuwa mekundu na makali. Sura zao za kutisha. Sura za kazi!!

**
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom