*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II -- 43*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
"Mama!" Akaendelea kuita mpaka alipoingia ndani. Hakumkuta mtu sebuleni, na hata nyumba haikuonekana na dalili ya mtu yoyote!
Akagonga milango na kupita kila chumba. Hamna mtu. Sasa walikuwa wameenda wapi?
Akaketi sebuleni tumbo likimsokota. Jasho likimtoka.
ENDELEA
Hata hamu ya kukaa hakuwa nayo akawa ananyanyuka na kuangaza kila mara kutazama kama wazazi wake watarejea.
Haikuwa hivyo mpaka muda mrefu ulipopita, baba na mama wakaja. Sasa Tattiana akapata wasaa wa kutoa donge lake linalomsumbua kooni.
Akawaeleza ameshajua biashara wanayofanya na mzee Harid, na hivi anavyoongea tayari mfalme amewaagiza watumishi wake wakawakamate watoto wa mzee huyo baada ya kufanya jaribio la kumuua Nebukadeza!
Melkizedek akaumwa kichwa kusikia hayo. Mkewe akaumwa tumbo. Sasa ndani hakukuwa kunakalika. Wakahisi hata nao wanakuja kukamatwa.
"Sasa tunafanyaje, Melkizedek?" Mama akauliza. "Wale watoto wakikamatwa watatutaja, itakuwa ndiyo mwisho wetu gerezani!"
Hata Melkizedek alikuwa anasikia? Wala! Kichwani alikuwa anasikia sauti ya chaki mpya ikwaruayo ubao ... kriiiiiiiiii! Na kadiri mkewe alivyokuwa anapiga kelele, akahisi kuumia masikio zaidi.
"Kelele!" Akafoka akibamiza meza. Akasimama akitazama kwa hasira. Alikuwa amechanganyikiwa. Akawaita watumishi wake na kuwaagiza wafanye usafi kila eneo huko ghala, wahakikishe hakuna linalobaki!
Basi haraka agizo likatekelezeka. Melkizedek akahakikisha hakuna lililobakia, sakafu nyeupe. Akafukia na yale mabaki yote ya majani ya cedar.
Kisha sasa akaketi sebuleni. Kichwa kilikuwa chekundu. Macho yake yamefura.
"Nililikataa hili. Nilijua madhara yake. Ona sasa tumehatarisha yote!" Akalalama akishika kichwa. Majuto ni mjukuu.
Sasa kiza kilikuwa kinazidi kinaingia, Tattiana akaaga aende zake kasrini kwa mfalme akiahidi atarejea kuwapasha habari zaidi endapo akikumbana na jipya.
Akajipakia juu ya farasi na kwendaze.
Melkizedek akaendelea kuketi pale mezani kwa muda mrefu hata mke wake aende na kurudi akimkuta hapo. Alikuwa amesononeka na amejawa na woga.
Kwanza ameigharimu himaya yake ya Goshen, pili amegharimu na biashara yake aliyohangaika kuijenga maisha yake yote.
"Nisamehe mume wangu," akasema mkewe. "Nimekuwa mshauri mbaya kwako."
Melkizedek hakusema kitu, akanyanyuka na kwenda zake chumbani akimwacha mkewe hapo mezani akimtazama anaishilia.
**
Alipokaribia lango la kasri ya mfalme, akasimamisha farasi wake na kutazama. Akaona kikundi cha wanajeshi kinaingia ndani ya jengo.
Akajiuliza je wamewakamata wale vijana. Alijikuta moyo wake unakita kana kwamba yeye ndo' mzazi wa watoto hao.
Akazama ndani, kwa uoga akarusha macho. Hakumwona Oragon wala Ottoman! Angalau akahema.
"Mpenzi wangu, wapi ulienda?" Phares akauliza.
"Nilitoka kwenda nyumbani, nilikuaga," Tattiana akajitetea.
"Ooh! Nilisahau," mfalme akaweka kiganja chake kwenye paji la uso. "Nahisi mambo mengi yananichanganya.
"Vipi umewakamata?" Tattiana akauliza.
"Hapana!" Mfalme akajibu akionyesha kufadhaika. "Lakini hawana pa kwenda. Nitawakamata tu kwani mipaka imefungwa, wataenda wapi."
Tattiana akawa kimya.
"Upo sawa?" Mfalme akauliza.
"Ndio ... nipo sawa, mfalme!" Tattiana akaropoka.
"Vipi nyumbani?" Mfalme akauliza.
"Wanaendelea vizuri," Tattiana akajibu kwa uso unaomsaliti. Hakukaa sana na mfalme akaenda zake ndani akimwacha mfalme nje.
Akaketi sebuleni akishika tama. Hakuwa na raha. Unaitolea wapi na huku roho za wazazi wako zipo rehani? Akiwa hapo Lucy akaja.
"Ewe kipenzi cha mfalme, nini kinakusibu?" Akamuuliza.
Tattiana akamtazama na kumwomba ampatie faragha kwani hayupo sawa.
"Nahitaji kuwa mwenyewe kwa sasa," akasema akimtazama Lucy kwa uso wa kumaanisha.
"Sawa, malkia wangu mtarajiwa. Ila huwezi jua, pengine ningekusaidia ulipo kwama. Ujakazi wangu si ukilema."
Tattiana hakusema kitu. Akaendelea na mawazo yake kana kwamba hamna mtu. Lucy akaguna na kumshauri aende kule alipomkuta jana usiku.
"Nikiwa nimekwazika ama nina mawazo huwa narnda kule na kusimama mwenyewe. Natazama watu walivyo wengi, upepo wanipiga na jua likizama. Nikitoka hapo nakuwa na kichwa chepesi."
Lucy alipomaliza kushauri, akaenda zake akihofia kuendelea kumkera Tattiana.
Tattiana akaendelea kuwaza. Na baadae akaona atende kama vile Lucy alivyomshauri, pengine inaweza kumsaidia. Akanyanyuka na kwenda uani mwa ghorofa, akasimama na kutazama.
**
"Mkuu, una wageni toka Goshen!" Alisema jabali.
"Toka Goshen?" Akashangaa Venim. Hakutegemea kabisa kulisikia jina hilo tangu alipoachana na wakina Rhoda ambao walimsaliti.
Akiwa anakula na kunywa damu ya kondoo, akasita kwanza. Akanyanyuka upesi na kujifuta damu kwa mgongo wa kiganja. Alikuwa amevalia joho jeusi lililofubaa. Kwa mbali alikuwa amefanana na kakaye lakini ukimsogelea karibu, alikuwa ni wa tofauti.
Kwa akili yake mara moja aliposikia Goshen alimkumbuka Rhoda. Mwanamke aliyeweka naye miadi akamtekeleza. Mwanamke aliyetokea kumpenda, akamjaza mikononi mwake lakini akaponyoka.
Basi haraka, isijulikane ametembeaje, akawasili sebuleni na kuwakuta hapo wazee wawili wa baraza. Akatahamaki na kufadhaika pia.
"Mnahitaji nini hapa? Kuuawa?" Akauliza akichezea kucha zake ndefu. Alikuwa anatisha. Kama ni mwoga ungezirai kwa uwepo wake.
"Tumekuja kukuomba msaada. Tusaidie!" Akasema mzee Harid. Venim akacheka sana akiketi. Akakunja nne na kuwatazama wazee hao.
"Goshen! Goshen! Mmeniona mpumbavu sana, wa kuja na kunisaliti? Leo mnataka mwataka nini kwangu?"
Wazee wakaeleza wanaomba msaada wa kukombolewa himaya yao dhidi ya mlozi anayetaka kuibeba. Hata wakasema hawajui huko walipoondoka, maana wametoka muda mrefu, huenda ameshaiteka tayari.
Venim akastaajabu. Ni mlozi gani huyo? Wale wazee wakamweleza hata hawamjui jinale lakini amekalia mwili wa mwana Goshen, hivyo anaweza kutoka na kuingia ndani ya Tanashe.
Ni hatari, amefanya himaya nzima ishikwe na taharuki.
Haraka Venim kusikia maelezo hayo, akahisi jambo, haraka akaendea kioo chake na kutazama. Akamwona kaka yake akiwa ndani ya shimo pamoja na mwili wa Rhoda. Akawaonyeshea wale wazee.
"Ndiye huyu?"
"Naam, huyo ndiye. Amezama ndani ya mwanamke huyo aliyemlaza kando"
Venim akamwonea huruma sana Rhoda. Kumbe ndiye amekuwa nguo ya kaka yake, Venet! Lakini zaidi akajionea huruma mwenyewe kwani kama kaka yake ametoka, basi atakuja kummaliza.
Ana kisasi naye cha damu.
Akashusha pumzi ndefu. Akawaomba wazee wampatie muda kwanza wa kuwa mwenyewe apate kufikiria.
Akawaza sana nini afanye, je arekebishe makosa yake ya awali kwa kumsaidia Venet ama amsaidie Rhoda, mwanamke anayempenda, na kwa wakati huo akijiweka salama dhidi ya kaka yake anayetaka kumuua?
Kichwa kikamuua kwa mawazo. Na anapokuwa na mawazo hunywa damu kwa wingi. Akanywa karibia ndoo nzima asiridhike!
Akiwa anawaza hivyo, mzee wa pili wa Goshen akamfuata huko uani na kumshtua akihitaji jibu. Venim kwa hasira akamkaba mzee huyo na kumining'iniza kama unyoya!
"Sikuwaambia mnipatie muda?" Akafoka. Akaminya koo la mzee huyo nusura amuue, kisha akamtupia nje!
Kwa usiku huo mzima akakesha akiwaza, kesho yake asubuhi akaonana na wazee wa Goshen apate kuwaambia alichoamua.
Mkononi alikuwa amebebelea kikombe kikubwa cha chuma kilichojaa damu. Macho yake yalikuwa mekundu na mwili wake ukifunikwa na joho rangi ya zambarau iliyokoza.
"Nimeamua kuwasaidia," akasema akiweka kituo. Wazee wakafurahi.
"Lakini kwa sharti moja," Venim akaongezea. "Kwa sharti moja tu."
"Lipi hilo?" Akauliza mzee Harid.
"Nitakapomtoa huyo mlozi nje ya mwili wa huyo mwanamke, basi huyo mwanamke atakuwa wangu. Nitaondoka naye."
Hapa wazee wakatazamana. Wakakabwa na kigugumizi. Lakini laiti wangejua hata Venim naye alikuwa anataka kumrejesha Venet ndani ya Tanashe kwa hali na mali kwasababu ya usalama wake, basi wangeweza kumtikisa kiberiti.
Lakini hawakuwa wanafahamu. Na kiu yao ya kuikomboa Goshen ilikuwa kubwa kuliko kumpata Rhoda, basi wakakubali.
"Mnaweza mkaenda!" Venim akawaambia.
"Sio twende wote?" Mzee Harid akatahamaki. "Huoni tunahitaji kwenda huko upesi?"
"Hamna haja hiyo," Venim akawatoa hofu. "Venet alizaliwa kipindi mwezi unapevuka, ni mlozi anayebadilika kuwa popo na nguvu zake zote huchepuka pindi mwezi unapokuwa kamili. Pale mezi unapoonekana mzima angani, hakuna mlozi yeyote anayeweza kupambana naye, si ardhini wala baharini."
Akakaa kimya kidogo kisha akaendelea kunena:
"Itachukua siku nne mpaka mwezi upevuke kuwa kamili. Kwa siku zote hizo hatafanya jambo, lakini mwezi utakapowaka, atawafufua watu wake wote aliowaua na kuwageuza popo. Wote watakuwa jeshi lake na atakuwa ana uwezo wa kuimeza himaya yoyote ile mbele yake."
"Sasa wewe utakuja muda gani?" Akauliza mzee Harid.
"Pale nitakapoona ni muda huo," Akajibu Venim. "Sitabisha hodi, wala hamtajua saa, mtanikuta ndani ya himaya yenu. Mkampe taarifa hizo mfalme wenu.
Nitamsaidia, lakini namtaka Rhoda."
**