*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II -- 45*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Akatazama kule kwenye mlango wa ua ya ghorofa kisha taratibu akaanza kujongea kwenda kule. Alitaka kujua leo Lucy alikuwa anaongea na nani usiku mzito kama huo.
Akapiga hatua kama tano, akabakiza mbili tu kutimiza lengo. Lakini ghafla! Mlango ukafunguliwa kabla hajaugusa. Na mara Tattiana akakutana uso kwa uso na Bella, kijakazi mwingine wa kasri mbali na Lucy, akitokea huko nje!
ENDELEA
Bella akashtuka na kushika kifua chake kwa mshangao. Akashusha pumzi ndefu na kuuliza;
"Kipenzi cha mfalme, hujalala hata sasa?"
Tattiana alirusha macho yake nyuma ya Bella. Akaangaza lakini hakuona mtu huko. Alijawa na shaka, akamuuliza Bella.
"Ulikuwa unaongea na nani, Bella?"
Bella kabla hajajibu akageuza uso wake kutazama nyuma alipotokea kisha akapandisha mabega.
"Hapana, sikuwa naongea na mtu!"
"Una uhakika?" Tattiana akamkazia macho.
"Ndio, nina uhakika!"
Tattiana akasonga kwenda kutazama kule nje. Akaangaza asione mtu yeyote. Akamrudia Bella na kumuuliza:
"Lucy yupo wapi?"
"Amelala," Bella akamjibu.
"Mbona wewe hujalala mpaka saa hii?" Tattiana akauliza.
"Sina usingizi," Bella akajibu. "Nikaona nitembee tembee tu!"
Kwa muda kidogo Tattiana akanyamaza akimtazama Bella machoni. Bella akatazama chini.
"Nisamehe, kipenzi cha mfalme. Sitarudia tena kutembea nyakati za usiku kama nimekuogopesha."
Tattiana hakusema kitu.
"Kweli sikuwa naongea na mtu!" Bella akaendelea kusisitizia. "Nilikuwa mwenyewe napunga upepo!"
Sura yake ilikuwa inatia huruma. Kwa ishara ya kichwa Tattiana akamruhusu aende zake kisha yeye akasonga kwenda kutazama huko nje.
Akafunga mlango na kukaa huko kwa muda. Upepo ulikuwa mkali. Na kulikuwa kimya haswa. Hakuona wala kuhisi kitu zaidi ya baridi, akatoka na kwenda zake chumbani kwake akalale.
Lakini Bella, akiwa amejibanza ngazini, akamtazama mwanamke huyo akiyoyoma. Akahesabu dakika kadhaa kisha akarejea kule alipokuwa mwanzo, nyuma ya mlango wa uani.
Akaufunga kabisa mlango huo kwa komeo huko kwa nje kuepusha usumbufu.
Ndani ya muda mfupi, sauti ya kunong'ona ikaanza tena. Ikadumu kwa kama robo saa, kisha Bella akatoka na kuelekea zake kwenye chumba walalacho vijakazi. Chumba hicho alikuwa anaishi yeye na wenzake watatu, akiwamo Lucy.
Chumba kilikuwa kipana mno na kila mmoja alilala kwenye kitanda chake.
Vitanda vyote vilikuwa na umbo la duara vikivutia machoni kwa mtindo wake.
Vijakazi wote walikuwa wamelala, isipokuwa huyu Bella aliyeingia hivi punde.
"Lucy!" Bella akaita kwa kunong'oneza. "Lucy, amka!"
Lucy alikuwa ameshabebwa na usingizi. Ilikuwa ngumu kumwamsha, lakini kwa usumbufu wa Bella akaamka akiwa amejawa na mang'amung'amu.
"Ni nini lakini?" Akauliza kilevi.
"Yule kipenzi cha mfalme ameniona!"
Hapo usingizi wote ukamkatika Lucy. Akamtazama mwenzake kwa macho ya kukodoa.
"Unasemaje?"
"Ameniona kule!" Bella akapayuka kwa sauti ya chini.
"We!" Lucy akabweka. Haraka Bella akawahi kumfunga mdomo.
"Ongea taratibu! Watu watasikia..."
Lucy akameza mate.
"Alivyokuona akafanyaje?" Akauliza akiwa mjawa wa hamu. Bella akamwambia ilitokea kama ilivyokuwa kwake, kabla hajaufungua mlango akamuwahi na kujifanya amegutuka.
"Una uhakika hajakusikia?" Lucy akauliza.
"Sidhani," Bella akajibu. "Lakini sasa lazima atakuwa na hofu nasi. Huoni inabidi tufanye jambo kabla mambo hayajaharibika?"
Lucy akajivuta na kuketi kitako.
"Unadhani jambo gani linastahili tufanye?"
"Tuhamishe madhabahu!" Akashauri Bella. "Pale atakuwa ameshapakariri, huenda akawa anapita mara kwa mara. Hata tukikutana naye tena pale, ni nini tutasema?"
Lucy akaridhia jambo hilo, wabadilishe madhabahu. Basi akamsihi mwenzake kesho yake aende kutafuta kila linalohitajika wakamilishe adhma yao hiyo.
Wakalala.
**
Hata sasa na ni usiku mzito, Ottoman na Oragon walikuwa nje kama mayatima ama mafukara. Upepo wa baridi ulikuwa unawapuliza kwa kasi na hawakuwa na nguo za kujikinga wala kujisitiri zaidi ya walizonazo mwilini.
Walikuwa wamejilaza chini ya mti mkubwa wa mkuyu wakiwa wamejikunyata kana kwamba watoto wachanga, vifurushi vyao wakivitumia kama mto.
Hata usingizi huu ulikuwa ni wa mashaka, kama ule wa sungura, kwa kulaza jicho moja huku jingine likiwa kazini. Utapataje amani na unatafutwa na wanajeshi huku na huko himaya nzima? Tena kwa kesi kubwa ya cedar!
Kulikuwa kimya lakini haukudumu. Ndani ya muda mfupi tu, Oragon akakurupuka, akamwamsha Ottoman kwa fujo.
"Wanakuja, amka!"
Ottoman akasimama upesi kumkuta kaka yake. Wakatazama mbali upande wa mashariki, huko wakaona kikosi cha wanajeshi walio juu ya farasi wakifanya msako. Mikononi wameshikilia maginga ya moto.
Basi upesi wakaanza kukimbia kuokoa nafsi zao. Wakazama zaidi msituni, ndani ndani. Wakatembea kwa kama lisaa, na basi wakaja jikuta wamekaribia mpakani. Hapo mpakani walikuwa wamesimama wanajeshi wanne wakiwa wanarandaranda, mikononi wamebebelea mikuki.
Hakukuwa na njia ya kupita zaidi ya hapo. Hapo kwenye geti lichungwalo na wanajeshi. La sivyo warudi ndani ya Goshen ambapo palikuwa ni hatari zaidi.
"Sasa tunafanyaje?" Akauliza Ottoman.
Hakukuwa na mwenye jibu. Lakini walipoendelea kukaa hapo wakasikilizia, mara kwa mbali, ndani ya msitu wakaona mwanga wa maginga ya moto!
Wale wanajeshi walikuwa wanakuja!
Hapa sasa wakachanganyikiwa. Sasa ilibidi wachague moja kati ya haya, waende kukutana na wanajeshi wa mpakani ama wale wa msituni.
Oragon akafanya maamuzi. Akajitokeza akinyoosha mikono juu akielekea langoni mwa mpaka. Hata Ottoman akabaki anashangaa.
"Wewe ni nani na unaenda wapi?" Akafoka mwanajeshi akimwonyeshea mkuki. Akaamriwa asimame pale pale alipo, akithubutu kupiga hatua ya ziada, ataukosa uhai wake!
"Naitwa Oragon, nipo na kaka yangu Ottoman. Tunataka kuvuka mpaka," Oragon akajieleza kwa kujiamini. Wanajeshi wale wakatahamaki. Majina hayo hayakuwa mapya masikioni mwao.
"Oragon, hujui mipaka imefungwa mpaka pale taarifa itakapotolewa?" Akauliza mwanajeshi. Punde akamwona na Ottoman akijongea karibu kwa uoga.
"Najua," Oragon akajibu. "Lakini ninaomba msaada!"
Mwanajeshi akamtazama kisha akamuuliza:
"Hata kibali cha kuvuka mpaka unacho?"
"Hapana, sina!" Oragon akajibu. "Lakini nina kingine cha ziada."
Akatoa fedha nyingi kwenye kifurushi chake na kumwonyeshea mwanajeshi. Mwanajeshi akasogea karibu. Akazichukua fedha hizo, na kisha akaamuru geti lifunguliwe vijana hao wapite baada ya kuwapooza wenzake kwa fedha kichele.
Oragon na Ottoman wakatoka Goshen! Wakapotelea huko kwenye himaya ya kigeni. Himaya wasioijua hata kwa chembe!
Tangu wazaliwe hawakuwahi kuuvuka mpaka wa Goshen mpaka wamefikia umri huo. Leo ikawa mara yao ya kwanza.
Alitakalo mwana ndilo hulipata. Waswahili hawakunyima maneno.
Wakatembea kwa lisaa limoja wakikata pori. Wakaona nyumba kadhaa, na kwakuwa walikuwa wamechoka, sasa wanahitaji mapumziko, wakazijongelea nyumba hizo waombe msaada wa kulaza mbavu zao.
Wakabisha hodi lakini hawakufunguliwa. Ulikuwa ni usiku sana. Ni ngumu kuamini mtu akugongeaye nyakati hizo. Hivyo juhudi zao zikashindwa kuzaa matunda.
Sasa wafanye nini? Wakaamua kujongea tena mbele pengine wanaweza wakapata msaada. Lakini wakatembea kwa umbali mrefu, wakachoka. Wakaamua kujilaza kandokando kidogo mwa barabara pakikucha wajue wa pa kuenenda.
Wakang'ang'ania vifurushi vyao wakijipa matumaini watakuwa salama.
Lisaa limoja likapita, hata usingizi wakazama. Ila asubuhi pasikuche, wakakurupushwa na wanaume watatu waliobebelea maginga ya moto.
Wakahofu sana wakijiminya kwa karibu. Wanaume wale, ambao hawakuwa na taswira ya kuvutia, wakawauliza wao ni wakina nani na kwanini wapo pale muda huo?
Basi wakajieleza. Wale wanaume wakawaambia.
"Tufuateni, tutawasaidia."
Wakaongozana nao wakielekea kusini, kwa mwendo wa dakika chache, wakafika kwenye nyumba moja ndogo mithili ya ghofu.
"Hapa ndiyo kwetu!" Mwanaume mmoja akatamba. Wakawakaribisha kwa ukarimu.
Nyumba hii ilikuwa ni kuukuu haswa. Haikuwa na samani za maana, imejawa na tando za buibui na uchafu.
Lakini ilikuwa kheri, kuliko kulala nje, akawaza Oragon akiipekua nyumba hii kwa macho.
Wakashtuliwa,
"Mbona mwalala haraka na hatujawakarimu vema?" Alisema mwanaume mmoja mfupi kuliko wote. Uso wake ulikuwa umejawa na ndevu lukuki macho tu yakionekana.
Basi wakapewa bilauri za pombe wanywe. Wakanywa na kisha wakalala kama wafu. Walipoamka asubuhi, wakajikuta hawana kitu! Vifurushi walivyokuwa wamevibebelea vilikuwa vimeenda. Na hata nguo walivuliwa wakibakizwa uchi wa mnyama!
Wakachanganyikiwa. Wakatazama ndani huku na kule, hakuna mtu. Walipotazama nje, wakaona wanajeshi kama kumi kwa idadi ya haraka. Mbele ya wanajeshi hao alikuwa amesimama mzee mnene mwenye ndevu nyeupe, kiremba kichwani na joho la rangi ya maziwa.
Mzee huyo alikuwa anaikagua nyumba waliyomo kwa macho akishika kidevu chake. Alifanya zoezi hilo kwa muda mfupi, kisha akawatazama wanajeshi na kuwaagiza:
"Ichomeni tu!"
Ginga la moto likawashwa.
***