*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II-- 40*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Mzee mmoja akapendekeza wafunge safari kumwendea Venim!
"Huyo naye si mlozi?" Akauliza mzee mwingine.
"Baniani mbaya kiatu chake dawa!" Akasema mtoa wazo.
ENDELEA
Kwa pamoja wakaonekana kuliunga mkono hili shauri. Waende kwa Venim. Japo yupo mbali, ndiye mtu wa pekee aliye karibu kwao kwa jambo la utaalam.
Basi pasipo kupoteza muda, ikabidi wateuliwe watu wa kwenda huko kusimamia hilo jambo. Wakateuliwa wazee wawili na kupewa kikosi cha wanajeshi kuwalinda safarini.
Mmoja wa wazee walioteuliwa alikuwa ni baba yao Oragon na Ottoman. Ebu tutumie jina iwe rahisi kumrejelea, mzee Harid.
Wakapewa muda mchache wa kujiandaa kabla ya kuanza safari hiyo mara moja.
"Wanangu," Harid akaita akiwatazama watoto wake wa kiume. "Nimetumwa na mfalme kwenda mbali sana na nisingeweza kukataa. Kwa muda wote huo nitakaokuwa huko, hakikisheni kila jambo laenda sawa hapa, mmeshakua. Mnatambua kila njia. Sawa?"
Lakini mzee kabla hajaondoka akawapa angalizo muhimu.
"Kuweni waangalifu mno, na mkalitende lile nililowaambia kwa ustadi mkubwa. Endapo pumzi ile ikiendelea kudumu, hakuna tena biashara!"
Alipomaliza kusema hayo akaenda zake kutimiza agizo la mfalme. Walikusanyika mbele ya kasri wakapatiwa kila hitaji, pamoja na walinzi, farasi wakaanza kuvuta matairi.
"Sasa na sisi tunaoachwa tunafanyeje?" akauliza Tattiana wakiwatazama wazee na kikosi chao cha wanajeshi wakiyoyoma.
Mfalme akashusha pumzi ndefu, alafu akamwita mmoja wa majemedari na kumuagiza ahakikishe wanamtazama vema Rhoda kule gerezani.
Kila muda awepo ndani ya chumba chake, akiwa anachungwa na macho na silaha. Agizo likaenda kutekelezwa.
Wakaongezwa wanajeshi wawili kutimia watano mbele ya lango la chumba cha gereza cha Rhoda. Wanajeshi hawa wote wakiwa wamebebelea mikuki ama mapanga. Au vyote.
Rhoda akawatazama kisha akatabasamu. Akawaambia:
"Acha niwahadithie simulizi moja ya kunguru." Aliposema hayo akasimama na kuanza kusogea kwenye lango la chuma.
"Hakuna ndege yoyote aliyekuwa anamchukia kunguru. Alikuwa anavutia kwa rangi yake, sauti ya kinanda na mwonekano wake wa kifalme. Kila alipokatiza ndege wote wakatua na kumtazama. Haki walimpenda! Japo baadhi walimuonea wivu.
Lakini unajua nini kilitokea kunguru akawa mweusi mpaka mdomo na miguu? Akapoteza rangi zake za thamani, sauti yake tamu na madaraka mbele ya wengine? Unajua?"
Mwanajeshi mmoja akatikisa kichwa kwa ishara. Mara akadondoka chini na kufa papo hapo. Rhoda akacheka kweli.
"Mnaona?" Akauliza. "Hakuna anayeweza kunilinda. Ninaweza kuwamaliza wote hapa pasipo kuweka kidole changu kwenye miili yenu."
Akakamata chuma za lango kwanguvu. Wanajeshi wakahofu.
"Muda wangu utakapofika, wote mtasujudia miguuni mwangu. Mtaniita mfalme mkiimba nyimbo za kunisifu. Kwa atakayekaidi, atageuka kuwa vumbi la majivu!"
Akanyamaza kidogo akiwatazama wanajeshi ambao walionyesha uso wa hofu.
"Pale jua litakapozama, gereza hili litakuwa mali yangu. Kila nafsi iliyokuwemo humu itakuwa yangu. Wekeni hili kichwani." Akarudia tena. "Pale jua likizama ... pale jua liki ZAMA... tunzeni hilo kichwani."
Akacheka tena kwanguvu akirejea pale alipokuwa ameketi awali. Akakaa kimya asiseme tena jambo lolote.
**
"Waheed!" Malkia akaita akigonga mlango wa chumba. "Waheed! Waheed!" Kimya.
Akaenda kukutana na wenzake waliokuwa wameketi sebuleni, akawaambia hamna matokeo.
"Jamani!" Akashangaa Zura. "Tokea asubuhi atakuwa amelala tu mpaka saa hii?"
"Labda anaumwa!" Akasema Fluffy. "Vipi kama tukafungua mlango kumtazama?"
"Kama yuko uchi je?" Malkia akauliza, na kuongezea: "Sidhani kama itakuwa ustaarabu."
Kukawa kimya kidogo. Walikuwa kwenye bumbuwazi. Iweje mwenyeji wao huyo asiitikie hodi zilizobishwa kwa muda wote huo tangu asubuhi?
Yupo ndani kweli? Na kama yupo, atakuwa mzima? Wakatafakari cha kufanya. Walikuwa wanataka kwenda safari lakini haikuwa kheri kwenda pasipo kuaga japokuwa walishamtanabaisha mwenyeji wao juu ya hilo.
"Ebu kajaribu tena," akashauri Seth. "Mara hii piga hodi kwanguvu zako zote!"
Malkia akaenda tena, akafanya kama alivyoagizwa. Bado hakufanikiwa. Sasa wakajawa na shaka kubwa. Hamna nyingine zaidi ya kuvunja mlango.
Alk, jitu la Azeth, likabeba jukumu hilo. Kwa mkono wake wa kuume likausukuma mlango ukajidondokea.
Kutazama kitandani, Waheed hakuwamo!
"Unaona? Hata hayupo!" Akasema Fluffy.
"Sasa tunafanyaje?" Zura akauliza. "Tutaenda hivyo hivyo?"
Seth akaguna. "Litawezekanaje hilo na huku hatumjui hata huyo mwanaume tunayeenda kumtafuta huko? Kitu pekee tunachofahamu anaishi karibu na bahari ya Mediterania, hakuna zaidi!"
Kweli. Walikuwa wanamtegemea Waheed peke yake kufanikisha hilo zoezi. Sasa ikawabidi tu waketi kumngoja.
Wakakaa mpaka majira ya jioni. Jua limelegea kwa kuishiwa nguvu. Bado Waheed hakuja. Wakakata tamaa ya safari yao. Isingewezekana tena kwenda huko kwa siku hiyo.
Lakini kabla jua halijapotea kabisa, wakamwona mtu kwa mbali akiwa juu ya farasi mweupe. Kwa mbali tu wkaamtambua mtu huyu alikuwa ni Waheed! Nywele na ndevu zake za kumwaga.
Wakasimama kumngoja, isipokuwa majeruhi Seth.
"Lakini sikumwona akitoka nyumbani leo!" Seth alistaajabu. "Tokea asubuhi ya mapema sana nilikuwapo macho. Nikasikia mtu chumbani kwake."
Ilikuwa ni ajabu. Aliondoka muda gani? Mbona hakuaga? Mbona aliondoka na alikuwa anajua taarifa za wageni wake kufunga safari kwenda kumtafuta mzee yule wa kando ya bahari?
Waheed alikuwa anayatambua maswali haya yatakuwa yanawatatiza vichwani mwao. Alipomfungia farasi wake, akawataka waende ndani kuteta kidogo. Akawaomba radhi kwani alipata dharura. Na hakuwa na namna zaidi ya kwenda kuikabili.
Hakuwaeleza dharura hiyo ni nini, lakini alisisitizia ilikuwa ni muhimu isiyoepukika.
"Mniwie radhi sana. Nimewaangusha."
Malkia akamuuliza sasa ni lini wataenda huko walipokubaliana kwani muda waenda. Hawaweza kukaa hapo milele.
Waheed akatabasamu kwanza,
"Siku yoyote ile, hata kesho ni sawa!" Akajibu kwa kujiamini kisha akanyanyuka na kuwaaga, aelekea chumbani kupumzika kwani amechoka.
Akiwa anaelekea huko, Malkia akagundua pindo la nguo ya Waheed lilikuwa na damu. Na hata kandokando ya kiganja chake cha mkono wa kulia, kulikuwa na masalia ya damu!
Akapata wasiwasi. Ni wapi alipotoka Waheed? Akajiuliza nafsini, lakini hakuwashirikisha wenzake, akalimezea.
Aliamini kuna jambo lipo mgongoni mwa Waheed.
**
Hatimaye Jua likazama. Giza likashika amri ya uso wa dunia.
Kulikuwa ni kimya na giza. Giza na kimya kwenye ardhi ya Goshen. Kimya isipokuwa gerezani ambako kulikuwa kuna zogo na maneno ya hapa na pale, kama ujuavyo mahali ambapo watu wamekusanyika kwa pamoja.
Lakini tofauti na kwengine, kwenye chumba cha Rhoda, alipokuwa mwenyewe, kulikuwa kimya. Kimya haswa Rhoda akiwa ameketi anatazama ukuta.
Lakini kimya hiki hakikudumu kwa muda mrefu, Rhoda akasimama na kunyoosha viungo vyake kisha akawatazama walinzi.
"Muda wangu umefika!" Akasema kwa tabasamu.
Ila muda wake huu ulikuwa ni upi? Mbona mwezi ulikuwa umefichama angani na si mzima kama yeye atakavyo kila atakapo kufanya jambo, haswa kubwa!
Walinzi wakiwa wanashangaa, mara Rhoda akageuka kuwa kundi kubwa la popo likatawala gerezani na kufanya kuwa kiza totoro!
Baada ya hapo milio ya watu wakipiga yowe za kifo zikatawala. Pale popo wote walipojikusanya na kuwa mwili wa Venet, hakuna hata mtu mmoja, mwanaume kwa mwanamke aliyekuwa hai ndani ya gereza.
Wote walikuwa maiti wamelala chini!
"Naomba uende kwenu, hapa si salama kwako usiku huu!" Mfalme Phares alimwambia Tattiana. Alimsihi binti huyu tangu jioni lakini akawa mkaidi.
"Sitaenda popote, mfalme, nitakuwa mtu wa aina gani kumkimbia mwenzangu wakati wa shida?" Tattiana akajibu.
Wasiendelee kuongea, hodi ikabishwa akaingia jemedari. Alikuwa mwenye sura ya hofu. Alikuwa anahema kwanguvu na kutota jasho.
Akamwambia mfalme,
"Watu wote wameuawa gerezani, na haijulikani wapi Rhoda ameenda!"
Mfalme akashtuka kusikia habari hizo. Haraka akasogelea dirisha na kuangaza nje. Kulikuwa kimya.
Akatazama kila upande lakini hakuona kitu. Wanajeshi walitapakaa kasrini wakiwa wamebebelea silaha wamejiandaa kwa vita!
Hali ya tahadhari ikatangazwa himaya nzima, watu wakihusiwa kukaa ndani mpaka pale taarifa itakapotolewa.
Muda ukasonga. Bado hakukuwa na kitu.
Kulikuwa kimya mno kiasi cha kudhani aidha umekuwa kiziwi.
***