SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

Sasa hivi uko chobingo naitwa shemeji
[emoji23][emoji23][emoji23][emoji23][emoji23] nimecheka kwa sauti yaan sakayo wangu hao mashemeji hewa wa jf sijui anao wangapi
 
Shunie Leo vipi shusha basi ninaUgwadu kinyama!
 
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II -- 37*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Tattiana akahisi moyo wake umekuwa mzito ghafla. Hata akastaajabu ni kwa namna gani mfalme aliweza kukenua kwa kicheko muda mfupi hapo nyuma.

"Sasa tutaepukaje kikombe hiki?" Akauliza akijawa na woga.

"Kwa njia moja tu," akajibu mfalme. "Nayo ni kumpata mtu aliyepanda, kuchuma na kusafirisha Cedar kwenda huko."

"Hakuna mbadala mwingine!" Akamalizia.

ENDELEA

Haki Tattiana akavuja jasho. Hili lilimtetemesha kwa woga haswa. Mfalme alinyanyuka akaenda zake akimwambia aenda kupumzika kwani baadae ana kazi kubwa ya kufanya.

Basi Tattiana akaachwa mpweke mezani. Hakudumu hapo muda mrefu wakaja wale vijakazi ambao walikuwa wameshamzoea mwanamke huyo kwa wepesi. Wakastaajabu kumkuta tofauti.
Lile tabasamu walilomuona nalo hapo awali halikuwapo tena.

"Nini shida ewe kipenzi cha mfame?" Wakamdadisi. Tattiana asiseme ukweli, akalaghai tumbo lamsumbua. Lakini vijakazi hao walikuwa watu wazima, wakautambua huo uongo.

"Pole, kipenzi cha mfalme. Twaweza saidia?" Akauliza mmoja wao.

"Hapana, msijali," Tattiana akawatoa hofu.

"Au pengine tayari ushambebea mfalme mtoto?" Kijakazi mwengine akatania. Wakacheka.

"Atafurahi sana, mfalme. Bila shaka furaha yake itauneemesha hata na sisi."

"Hapana, sina ujauzito," Tattiana akasema kwa tabasamu la bati. "Ni tumbo la kawaida tu."

Wale vijakazi wakamshauri abebe mimba ya mfame haraka iwezekanavyo. Asikawie kwani hiyo ndiyo njia madhubuti ya kumtia mfalme mkononi.

"Mfalme hawezi akamwacha mwanamke aliyemtia mimba. Hata kama akikuacha, basi utahudumiwa kifalme maisha yako yote."

Tattiana akashukuru kwa ushauri ila akaanza kukereka na uwepo wa vijakazi karibu naye. Si kwamba hakuwa anawapenda, la hasha! Walikuwa ni wanawake wacheshi wenye upendo lakini kichwani mwake hakuwa sawa.

Akaona kheri aondoke akakutane na mfalme chumbani.

"Unamwonaje?' Kijakazi mmoja akauliza. Aitwa Lucy.

"Yu safi sana, nampenda," mwingine akadakia, anaitwa Bella, alafu wakacheka na kugongesha viganja vyao.

"Ila naamini sasa penye miti panakosa wajenzi," Lucy akasema akishika kiuno.

"Kwanini?" Wenzake wakawahi kumuuliza.

"Laiti ningekuwa ndimi mimi nimechaguliwa na mfalme," akaweka kituo akatikisa kichwa.

"Nisingepata hata muda wa kukaa na nyinyi vijakazi maana kila saa ningekuwa nampatia vitu vitamu mfalme. Akigeuka nipo hapa, akikohoa naitika. Akicheua mimi nabeua. Akipika mimi napakua."

Wenzake wakaangua kicheko. "Na ndiyo maana hujawahi chaguliwa!" Akasema Bella.

"Unadhani kwanini? Kwani mimi ni mbaya?" Lucy akauliza akijitazama.

"Wala si mbaya, sema una mdomo. Uliumbwa mdomo kabla ya vingine vyote mwilini!"
Lucy akasonya kisha akaenda zake.
"Wivu tu wawasumbua!"



**


"Mfalme anaingiaaa!" Sauti kubwa ya mwanajeshi ilipiga yowe kutaarifu maafisa wa gerezani na wafungwa wote juu ya ujio huo mkubwa.
Yowe hilo likafuatiwa na mlio wa pembe mara moja kwa sauti kuu.

Mfalme, akiwa ameongozana na walinzi, pamoja pia na viongozi kadhaa wa juu, akiwemo Alphan, wakazama ndani ya gereza na kukatiza koridoni mwa vyumba walimojazwa wafungwa.

Wakiwa wanapita, baadhi ya wafungwa wakawa wanapaza sauti kumuomba mfalme awasamehe wapate kutoka kwani wamekaa muda mrefu mno.
Zilikuwa ni kelele sasa, mfalme asijue zipi za kusikiliza ama kuacha. Nao maafisa magereza wakawa wanajitahidi kuwanyamazisha wafungwa hao wasimsumbue mkuu.

Lakini kabla mfalme hajakatiza bewa hili la wafungwa wanaume, akamwona kikongwe mmoja ndani ya chumba cha lupango. Akajikuta anamwonea huruma.

Akamsogelea na kumtazama.

Kikongwe huyu alikuwa yu hoi, amevalia nguo za kusitiri sehemu zake za siri tu. Nywele zake zilikuwa zimenyonyoka, mwembamba mno na mwenye macho madogo yaliyozama ndani.

Alitamani naye amuite mfalme amuokoe lakini hakuwa na uwezo huo. Hiyo nguvu hana. Ila ajabu mfalme akasikia kunong'ona kwake.

"Unaitwa nani?" Mfalme akamuuliza.

"Nebukadeza," akajibu yule kikongwe kwa shida. Sauti yake ilikuwa chini mno.

"Umefanya kosa gani kuwekwa humu?" Mfalme akauliza. Kabla kikongwe yule hajajibu, akadakia afisa magereza.

"Alikuwa muuzaji wa matunda haramu!"

"Cedar?" Mfalme akauliza.

"Ndio, mfalme!" Afisa magereza akawahi kujibu.
Nebukadeza akatazama chini. Matumaini yake ya kutoka ndani ya chumba cha gereza yakafifia kama siyo kufa kabisa.

"Ni kweli?" Mfalme akamuuliza. Kwa sauti yake ya chini inayokwaruza, Nebukadeza akasema:

"Ndio, ni kweli mfalme. Naomba unisamehe. Niruhusu nikafie nyumbani kwangu, watoto wangu wanizike," Akalia. "Nakuomba, mfalme!"

Mfalme akamtazama afisa magereza na kumuagiza amwachie huru Nebukadeza mara moja. Afisa akashangaa.

"Mfalme, alikuwa muuz--"

"Nimeshasikia," mfalme akamkatiza. "Muweke safi, usiku huu nitakuwa na maongezi naye kwenye meza moja.'

Afisa akapokea amri hiyo na kufanya kama alivyoagizwa. Mfalme akaendelea na safari yake ndani ya gereza mpaka alipofika bewa ya wanawake kukutana na Rhoda.

Huko akamkuta mwanamke huyo akiwa ameketi amegeukia ukutani.

"Amekuwa akiketi hivyo tokea tulipomleta. Na muda mwingine amekuwa akiongea maneno yasiyoeleweka," akaeleza Afisa magereza. Mfalme akamwamuru amfungulie mlango akaongee naye yeye mwenyewe.

"Ni hatari, mfalme!" Afisa akapaza sauti. "Anaweza kukudhuru, si wa kumsogelea karibu!"

Mfalme asiseme jambo akamtazama Afisa yule kwa uso wa kukunja ndita. Haraka Afisa akafungua mlango asiseme kitu tena.

Mfalme akamjongea Rhoda na kuketi naye karibu.
"Rhoda, kipi kimekukumba?" Akauliza kwa sauti ya chini. Rhoda hakujibu. Mfalme akarudia tena swali.

"Naomba uniambie, nakusikiliza."

Wakati huo wanajeshi wakiwa wamekaa tenge kwa lolote litakalotokea. Walikuwa wameshikilia silaha zao vema wapate kuhudumu endapo mfalme atahitaji msaada muda wowote ule.

Bado Rhoda akawa kimya. Mfalme naye akanyamaza. Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, Rhoda akageuza shingo yake kama roboti, akamtazama mfalme na kutabasamu.

"Kumbe wewe ndiwe mfalme?" Akauliza kwa sauti ya kiume! Mfalme akaogopa. Rhoda akaendelea kukunja shingo yake mpaka nyuma ya mgongo, akamtazama Alphan kwa jicho jeusi!

Ilikuwa ni maajabu namna alivyokuwa anatengua shingo yake ikienda popote anapotaka. Hakuna binadamu wa kawaida angeweza kufanya hivyo kabisa.

Alimtazama Alphan pasipo kusema kitu. Upesi mfalme akatoka zake ndani ya chumba hicho, kikafungwa mara moja!

"Nitakuja kukusalimu siku moja," Rhoda akasema. Mfalme akamwambia hatopata siku hiyo kwani kesho atanyongwa mbele ya hadhira.

Rhoda akacheka sana. Akacheka sana, kisha akanyanyuka na kusogelea mlango.

"Ngoja tuone nani ataning'inia kwenye hicho kitanzi kwanza," akasema kwa kujiamini. Mfalme akaenda zake asimjibishe. Sasa akiwa ameamini kwa asilimia zote, Rhoda ni mlozi.

Hakuongea na yoyote yule mpaka anafika kasrini. Kichwani alikuwa anawaza ni kivipi Rhoda amefikia hali ile? Nini kimemsibu?

Akajikuta anamwonea huruma sana mwanamke huyo. Hakuwa na budi sasa bali kuidhinisha zoezi la unyongaji.

"Mfalme .. mfalme ... mfalme!" Tattiana aliita, mfalme akakurupuka toka kwenye dimbwi la mawazo.

"Chakula tayari," Tattiana akamwambia kwa sauti nyororo. "Na mgeni wako pia ameshafika."

"Mgeni?" Mfalme akatahamaki. "Mgeni gani huyo?"

Tattiana alipomweleza akakumbuka ni yule kikongwe, Nebukadeza. Akatikisa kichwa chake na kunyanyuka aende huko.

**

- NINI NEBUKADEZA ATAMWAMBIA MFALME JUU YA BIASHARA YA CEDAR?

- RHODA ALIMAANISHA NINI KWENYE YALE MANENO ALIYOMWAMBIA MFALME GEREZANI?
 
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II -- 38*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

"Chakula tayari," Tattiana akamwambia kwa sauti nyororo. "Na mgeni wako pia ameshafika."

"Mgeni?" Mfalme akatahamaki. "Mgeni gani huyo?"

Tattiana alipomweleza akakumbuka ni yule kikongwe, Nebukadeza. Akatikisa kichwa chake na kunyanyuka aende huko.

ENDELEA

"Upo sawa?" Tattiana akamuuliza.

"Ndio!" Mfalme akajibu akijinyoosha. "Nipo sawa tu."

Tattiana hakumuuliza tena lakini alijua mfalme hayupo sawa. Mawazo yalikuwa yanamsumbua. Alitamani kumsaidia lakini hakuwa na namna.

Akaongozana naye mpaka mezani kisha wakaketi wote pamoja na yule mgeni Nebukadeza ambaye alifika kuitikia wito wa Mfalme.

Nebukadeza, kwa heshima zote, alimsalimu mfalme na kumshukuru sana kwa kumsaidia. Hana cha kumlipa, nk Mungu pekee ndiye atamrudishia fadhila.

"Sina mali yoyote, zote zilitaifishwa, bali familia yangu tu. Nisamehe, mfalme, kwani sina cha thamani cha kukulipa. Naomba upokee mzigo huu kama shukrani yangu kwako."

Nebukadeza akanyanyua kifurushi cha rangi ya maziwa na kukiweka mezani kumsogezea mfalme.

"Natumai itakupendeza, mfalme wangu," akasema kwa sauti yake kavu. "Ni cha kitambo sana lakini kina thamani kukitunza."

Mfame akashukuru pasipo kutazama kilichomo ndani. Akamuita kijakazi na kumuagiza apeleke chumbani kwake, akiweke mezani.

"Beba kwa uangalifu," Nebukadeza akamsisitiza kijakazi kisha akamtazama akiondoka na kifurushi hicho kuelekea alipoelekezwa.

"Nebukadeza," mfalme akaita. "Nina shida kubwa sana na natumai utanisaidia," akasema kwa msisitizo.

"Ewe mfalme," Nebukadeza akaita. "Ulinipa mkono nilipokuwa mpweke. Dhoofu lihali, ukanikomboa dhidi ya kifo cha aibu na ukanipatia nafasi tena kwa macho yangu ya kizee kuona familia yangu. Nitaanzia kwenye kona gani ulimwenguni kutokukusaidia? Hata kama itanigharimu maisha yangu, ni tayari!"

Mfalme akamshukuru na kumsihi aendelee kula wakiongea.

"Nimefurahi sana kusikia hivyo. Sina mengi sana toka kwako ila kutambua kuhusu biashara uliyokuwa unafanya."

"Biashara ile haramu?" Akauliza Nebukadeza.

"Ndio," mfalme akamjibu. "Nataka kujua kila chembe ya biashara hiyo. Kila nukta kila tembe. Usinifiche jambo kwani mimi ni mhitaji."

Nebukadeza akaapia kutoficha chochote. Akamwambia mfalme namna biashara hiyo ilivyokuwa na pesa na jinsi inavyoenenda kwa siri kubwa mno kuanzia kwa wafanyabiashara, wanunuzi na hata wasafirishaji.

"Hapa kunakuwa na ubunifu mkubwa sana. Kila mtu hutafuta namba ambayo ataweza kutoa mtunda hayo nje ya mipaka. Kwa upande wangu, nilikuwa nikitumia mbegu kubwa ya mapapai. Napasua mapapai hayo na kuyajaza matunda kwa ndani kisha nikiyaunga tena.

Lakini baadae nikaja ona njia hiyo ni hatarishi kwani ukaguza ulizidi mpaka kufikia pahala pa tunda moja moja kukaguliwa tofauti na hapo awali yalipokuwa yanakaguliwa yale ya juu tu. Hapa ikanibidi nibalishe namna.

Sasa nikaanza kufuma matoroli ya farasi yaliyokuwa na nafasi uvunguni ambamo humo nikajaza matunda haya pasipo shida yoyote, nikiyafunika na vipande vya mbao thabiti vilivyobanwa na misumari mirefu."

Mfalme akashangazwa na janja hiyo.

"Ikawaje ukakamtwa?" Akauliza.

"Ilikuwa ni siku moja nikiwa mpakani nakaguliwa. Siku hiyo nilipakia mzigo wangu kama ilivyo ada. Lakini sijui nini kilitokea, labda uvungu wa kitoroli haukuwa umefungwa vema, tunda moja likadondoka. Huo ukawa mwisho wangu."

Mfalme akamtaka amweleze ni wapi wanapotoa hayo matunda. Wanawauzia wakina nani huko nje ya mipaka ya Goshen, yaani wafanyabiashara. Na kama yupo tayari kumsaidia kuwang'amua watu hao, nje na ndani, kwa kutumia ufahamu na uzoefu wake wa muda mrefu.

Nebukadeza pasi hiyana akaeleza kinagaubaga. Pia akamuahidi mfalme kumsaidia katika kila hali atakapouhitaji msaada wake.

Wakakomea maongezi yao hapo sasa wakaendelea kula tu. Walipomaliza Nebukadeza akaaga na kwenda zake. Mfalme akarejea chumbani pamoja na Tattiana.

Wakaongea kidogo tu, mfalme akapitiwa na usingizi. Alikuwa amechoka. Tattiana akamwacha mwanaume huyo apumzike wakati yeye akiendelea kufikiria yale yaliyokuwa yanaongelewa pale mezani.

Hakujua kwanini lakini maongezi yale yalimpatia shaka. Namna Nebukadeza alivyoeleza kwa undani kulianza kumpa hofu juu ya mienendo ya familia yake na kile kitu cha siri.

Vipi kama mzee wa baraza akawa anatumia wadhifa wa baba yake kutimiza haja yake kama fadhila kwa mzee huyo kwa 'kumuuza' kwa mfalme?

Mawazo haya yalimfanya Tattiana aone kuna haja ya kwenda nyumbani.

- JE, ATAFANIKIWA KWENDA? AKIENDA HUKO ATAELEZA NINI?

- NEBUKADEZA ATAFANIKISHA KUKAMATWA KWA MZEE WA BARAZA NA MELKIZEDEK?

**

Giza la usiku lilikuwa limeshatawala.

Kwenye nyumba ya Alphan familia ilikuwa imeketi mezani kupata chakula cha usiku. Alphan akiwa pamoja na watoto wake wawili wa kike walionekana kujazwa na furaha.

Vicheko na matabasamu vilitawala meza. Kila mtu angetamani familia hii. Usiku huu ulikuwa bora kwao kwani baba alileta habari njema. Habari ya kujivunia.

Habari ya kumkamata mlozi.

Kama vile babu ama bibi wafanyavyo kwa wajukuu zao, Alphan aliwahadithia watoto zake kila hatua aliyopitia mpaka kufanikisha zoezi hilo. Habari hizi zilikuwa za kusisimua na kuvutia. Na kwa namna Alphan alivyozieleza, zilikuwa ni kana kwamba tamthilia ya majigambo jukwaani.

Watoto wake wakajivunia kuwa na baba mwerevu, shujaa na mzalendo.

"Inabidi mfalme akuzingatie," akasema mmoja.

"Hakika atafanya hivyo," Alphan akajivuna. "Ni kazi kubwa hii!"

Wakacheka.

"Lakini nimefanya kwa moyo wa kuipenda ardhi yangu," Alphan akasisitizia.

Wakala na kumaliza. Wakaagana wakapate kupumzika. Alphan akiwa wa kwanza kwenda chumbani mwake, akakoga kwanza kisha akatazama baadhi ya nyaraka kadhaa kabla hajaulaza mwili wake kitandani.

Hakuchukua muda, akamezwa na usingizi.

Usiku ukaendelea kuyoyoma.

Katikati yake, kwa majira ya sasa mishale ya saa nane ama tisa, popo akatua dirishani mwa Alphan. Kama ilivyo kawaida ya kiumbe huyu, alikuwa amebinuka, miguu juu kichwa chini.

Akamtazama Alphan aliyekuwa hajielewi usingizini kwa sekunde kadhaa kisha akapaa kutokomea!

Lakini mara huko nje, mlangoni mwa chumba cha Alphan ukasikika mzigo mkubwa ukidondoka chini. Tih!

Nini hicho? Hakuna kitu kingine kinachokaa mlangoni mwa Alphan zaidi ya mlinzi wake. Punde mlango ukafunguka, na kundi kubwa la popo likaingia! Chumba kikawa giza.

Asubuhi palipokucha, Alphan hakuwa kitandani! Walinzi wakamtafuta nyumba nzima pasipo mafanikio. Waliambulia maiti ya mwenzao tu.

Watoto wa Alphan wakasaga meno wakiia kwa hofu. Ni jana tu walikuwa wanacheka na kufurahi.

Baadae kidogo, taarifa zikaja. Alphan ameonekana. Lakini hakuwa hai, mwili wake umeshapoa kuwa baridi wa mauti!

Amekutwa uwanjani akiwa ananing'inia kitanzini. Hana alama wala ishara ya jeraha lolote.

**
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom