*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 30*
*Simulizi za series*
Aliposema hayo, taswira ile ndani ya kioo ikatabasamu. Meno yalikuwa ya kahawia na yaliyochongoka. Badala ya tabasamu kumtengeneza uso, ikamharibu na kumfanya atishe zaidi. "Venin?" Taswira ikaita, na kuongezea: "Vita baina yangu nawe itakoma punde tu mpango huo utakapofanikiwa!"
"Pasi na shaka, kaka, mpango huu utatimia. Niamini mimi na kuwa na subra," akasema Venin kwa kujiamini.
Akaweka kiganja chake cha kushoto kwenye kioo akiitazama taswira machoni. Taswira nayo ikaweka kiganja chake vikagusana.
Mara taswira ile ikayoyoma kama vile sukari inavyozama kwenye uji. Kufumba na kufumbua haikuwepo.
Venin akabakia mwenyewe akiwa bado amepachika kiganja chake kiooni. Uso wake u na bumbuwazi, lakini pia huzuni.
Alikaa hapo kwa kama dakika tatu baada ya taswira kupotea, ndipo naye akatoka na kuendelea na shughuli zingine.
.
.
.
Akabadili nguo na kushuka chini alipomkuta Rhoda na Bonas wakiwa wamesimama wanateta jambo. Macho ya Venin yakamwona vizuri Rhoda na kushuhudia uzuri wake.
.
.
.
"Vipi, tayari?" Aliuliza.
"Ndio, Venin," Rhoda akajibu upesi. Swala hili likamshtua kidogo Venin.
"Mmetoa wapi haraka hivi?"
"Tumeona tuteke damu ya mlinzi wetu mmoja. Hatuwezi kurudi Goshen kwa huu muda na kurejea tena hapa," alijibu Rhoda. Venin akatabasamu. Haki alipendezwa na hilo jibu.
.
.
.
"Ama kweli wewe ni mwanamke jasiri," akasema akizidi kujongea.
"Nashukuru. Tunaweza sasa tukaendelea na mengine?"
"Bila tatizo lolote," akajibu Venin. "Lakini hamna haja ya kuwa na haraka, Rhoda."
.
.
.
Mwanaume huyo alizimaliza ngazi akasimama pembezoni mwa mwanamke huyo kiubavu, akimtazama kwa umakini. .
.
.
Akanyanyua kidole chake kionyeshi na kuteka unywele wa Rhoda kwa kucha. Akawa anauchezea kwa kuuviringita.
.
.
.
"Utakuwa na mimi kwa siku tatu hapa. Kaa, tule, tuongee, tupange."
.
.
.
Rhoda akageuza uso wake na kumtazama Venin. Kwa kugeuka huko akawa amempoka Venin nywele zake.
.
.
.
"Nashukuru sana, Venin," akasema kwa uso mkakamavu. Akajitoa karibu na mwanaume huyo na kuelekea kwa Bonas.
.
.
.
"Natumai siku zangu tatu hapa, zitakuwa za kheri na za kazi."
.
.
.
Venin akatabasamu kipembeni. Akapandisha mabega yake juu akibinua mdomo.
.
.
.
"Nitahakikisha hilo, Rhoda."
.
.
.
Baada ya muda mfupi karamu ikawa imeandaliwa kwa ajili ya wageni. Wanawake wazuri wasiojulikana wametokea wapi, wakaandaa chakula kitamu na kinono.
.
.
.
Vinywaji vikajazwa mezani na hata ala za muziki zikapamba.
.
.
.
Venin akamkarimu Rhoda, pamoja na wote aliokuja nao waje wale wafurahi. Rhoda na walinzi wake wakajumuika kula na kunywa.
.
.
.
"Mam, hii si kawaida," Bonas akamnong'oneza Rhoda. "Venin hajawahi kukaa na vijakazi meza moja. Sijawahi kuona mara zote nilizowahi tia miguu hapa."
.
.
.
Rhoda akazipokea taarifa hizo kwa tabasamu. Ila halikudumu sana usoni baada ya Bonas kumwambia:
"Kuna jambo atakuwa amelipanga, kuna jambo anataka kulifanya."
Taarifa hiyo ikampa tafakuri Rhoda.
Akamtazama Venin aliyekaa upande wake wa pili, Venin akatabasamu na kumuonyeshea kikombe cha mvinyo.
.
.
.
"Kuna taabu, Rhoda?" Akauliza.
.
.
.
Rhoda akatikisa kichwa pasipo kusema jambo.
.
.
.
Macho ya Venin yakamtazama Rhoda anavyokula na hata anavyomeza. Yalikuwa yanawaka tamaa na hamu. Alijikuta anapenda kumtazama mwanamke huyo kila nyendo aliyokuwa anafanya.
.
.
.
Ilikuwa ni ombwe sasa, nini ataenda kulifanya muda wa usoni.
.
.
.
Jambo hili likamfikirisha pia Rhoda, na kwa kiasi fulani likamnyima raha. Ila alikuwa mtaka cha uvunguni, ilibidi ajiandae kuupinda mgongo.
.
.
.
. ***
***
.
.
.
.
.
.
Jua lasimama na kumkuta Sultana mdogo akiwa yu macho na mwenye nguvu. Alikuwa amevalia sketi ndefu rangi ya zambarau iliyokaba kiuno chake na kukomea chini ya magoti.
.
.
.
Kifuache kilifunikwa na blauzi nyeusi nyepesi iliyokaba shingo na kuacha huko kwingine. Mikono yake, kama kawaida, haikukosa bangili zilizometameta na kuvutia. .
.
.
Kichwa chake alikifunga kiremba cheusi kilichokatizwa na kamba kamba kadhaa mithili ya mikufu yenye vidani vya kung'aa.
.
.
.
Hapo alikuwa amevaa kawaida. Yaani siku yake ilikuwa ya kazi, la sivyo angejikwatua ipasavyo. Lakini mbali na yote bado akapendeza mwanamwali huyu. .
.
.
Hakuwa na haja ya kujieleza kwamba yeye ni mke wa Sultan. Macho yako yangetosha kukupatia majibu, tena ya haja. Ni kama vile nguo ziliumbiwa mwili wake.
.
.
.
Hata akijezeka magunia, la haula anapendeza!
.
.
.
Asubuhi nzima hii alikuwa anaambatana na vijakazi wake kufanya usafi wa nyumba. Kila kona ya dari akaigusa na fyagio na sakafu ikang'azwa zaidi.
Japokuwa ni hulka yake kutenda hivi kila mwisho wa juma, yaani kufanya usafi wa jumla, ila wa siku hii ulikuwa kabambe.
.
.
.
Aliusindikiza yeye mwenyewe, alielekeza na kupendekeza baadhi ya mabadiliko. Nyumba ikang'aa na kunawiri. Mwishowe akaifukiza marashi kwa kumalizia.
.
.
.
Akajipata bafuni, akasuguliwa mwili na kijakaziwe. Kisha akajikwatua yeye mwenyewe, hapa hakumwamini kijakazi zaidi tu ya kioo na mkono wake.
.
.
.
Akajifukiza marashi na kuketi sebuleni akijipatia sharubati ya matufaha matamu toka Uajemi.
.
.
.
Mwili wake ulituama vema ndani ya gauni maridadi la kahawia, jembamba na refu, likiacha mgongo wake mwekundu wazi. Huku nywele zake ndefu, nyeusi ti, zikiwaka mafuta na kusongwasongwa vizuri ndani ya banio jeusi la ishara ya mapenzi.
.
.
.
Loh! Mwanamke alinoga. Harufu yake ilitamba sebule nzima. Kama ni bustani, basi hili halikuwa jingine bali uwaridi. .
.
.
Alikuwa mbichi zaidi. Kama vile msichana wa miaka kumi na misaba. Ama yule ambaye hata ungo haujui sembuse kuuvunja.
.
.
.
Hapa kama mume huaja kwa msongo wa kazi, akifika hapa lazima akunjue sura. Na hilo ndilo lilikuwa lengo la mwanamama huyu.
.
.
.
Alijua fika Sultan atakuja nyumbani kwake, hakujua muda, ila alijua lazima atakuja. Na mwanaume huyu atakapokuja, hatakuwa na furaha.
.
.
.
Ana mawazo juu ya mkewe mkubwa. Ana mawazo juu ya mkufu. Haya matatizo, kwa namna ya lazima, yatamfanya aghafirike.
.
.
.
Na hapa ndiyo mkono wa mwanamke utaonekana. Mkono wa Bi mdogo. Kumpokea, kumbembeleza na kumtuliza mume.
Kwa Sultana huyu, haya matatizo yalikuwa mtaji na fursa kwake. Alitaka kucheza nayo aushinde moyo wa Sultan ambayo nusura aupoteze kwa blanda ya dawa ya bibiye aliyoipoteza njiani.
.
.
.
Sasa anataka ajitahidi acheze karata kuu. Karata ya kutengeneza kasri ya Sultan katika mji wake.
.
.
.
Alifungua pazia la dirisha akatazama nje, bado muda ulikuwa mchanga. Akaagiza glasi nyingine ya sharubati hii aipendayo na kuendelea kujipatia mafundo ya kusogezea muda.
.
.
.
Akanywa nusu ya glasi, na mara kijakazi wake akaja upesi kumkuta.
.
.
.
"Sultana, pasipo shaka Sultan anakuja. Msafara wake unaoneka kwa mbali unakuja."
.
.
.
Sultana akatabasamu. Akapandisha kichwa chake kumpa ishara kijakazi wake aliyetimka kwenda nje.
.
.
.
"Karibu Sultan kwenye mikono yangu," akajikuta anasema kabla hajamalizia sharubati yake na kwenda nje ya geti kumlaki mgeni.
.
.
.
Alimjaza Sultan kifuani mwake, akamteka mkono mpaka sebuleni alipomkalisha na kuketi pembeni yake.
.
.
.
Mkono wake wa kuume ulichezea ndevu za Sultan, mguu wake wa kulia akiuweka juu ya paja la mwanaume huyo.
.
.
.
Macho alilegeza na sauti yake ilikuwa kavu lakini nyororo. kichwa chake akilikilaza kifuani mwa Sultan akisikiliza mapigo ya moyo.
.
.
.
"Ungependa nikuandalie nini, Sultan wangu?" Sultana akauliza.
"Nashukuru sana, sina hamu ya kula kitu," akajibu Sultan akitikisa kichwa.
"Hapana, Sultan. Huwezi kuja kwa mpenzi wako, tena ambaye hujamuona muda mrefu, ukakataa kula," akasema Sultana kwa sauti shinikizi.
"Si kwamba nakataa, bali sina hamu."
"Sultan, angalau sunna. Sitajisikia vema hakika. Najua haujala hata jana."
"Umejuaje?"
"Mie si mgeni kwako. Natambua yote hayo nikikutazama usoni, laaziz."
.
.
.
Sultan akavuta na kushusha pumzi ndefu. Kweli hakuwa amekula. Ila pia mwili wake haukuwa na hitaji la kula. Mawazo yalijaza mpaka tumbo.
.
.
.
Sultana alinyanyuka akamtazama mumewe.
.
.
."Najua una mawazo, mengi yanakutatiza. Sipendi ukinyong'onyea na ukiwa mhaba wa furaha. Acha nkufanyie jambo."
.
.
.
Akaenda jikoni yeye mwenyewe. Akawatoa vijakazi wake wote ndani. Akahudumu sharubati ya ukwaju mzito kwa ajili ya kupalilia hamu ya chakula kwa Sultan.
.
.
.
Akavua nguoze na kubakiza fupi iliyoacha maungo yake tamanishi wazi. Sultan akanywa sharubati kisha mwanamke akamtaka waende kupata maji pamoja.
.
.
.
Sultana akamkogesha mume na kumpeleka chumbani alipomlaza kifudifudi na kummiminia mafuta ya mzeituni kumkanda mwili mzima kumuondolea uchovu.
Pasipo kuomba ruhusa, Sultana akalala usingizi mzito. Akakoroma akiachama kabisa mdomo wazi.
.
.
.
Mpaka hapo Sultana akawa ameshinda pambano moja; kumpa pumziko mume. Pumziko ambalo hakupata kwa takribani siku mbili.
.
.
.
Akijua wazi mumewe akiamka atahitaji chakula, akajivesha nguo na kuwapa kazi hiyo vijakazi, kisha yeye akaenda kujilaza kando na Sultan.
.
.
.
Baadae yakiwa majira ya jua kupooza wakawa wapo mezani, yeye na mumewe, wakipata biriani, viazi, ndizi na nyama ya ngamia. Nyama aipendayo Sultan. Akishushia pia na sharubati yake pendwa, dhabibu.
Hapo sasa Sultan akaanza kutoa yaliyobana kifua. Akaeleza juu ya mkewe na ya Karim. Mbali na mkufu ambao tayari ameshaanza kuukatia tamaa.
.
.
.
Sultana akamsikiliza mumewe mpaka mwisho. Akashusha pumzi yake ndefu kabla hajaanza kuuliza maswali utadhani hajui kinachoendelea.
.
.
.
"Ina mana mpaka leo hujapata kumuona?"
"Sijamuona na sijui wapi alipo!"
"Umeenda na kuulizia kwa nduguze?"
"Kote huko. Hakuna anayejua!"
"Pole sana, Sultan. Ila usijali, mkeo ni mtu mzima. Anajua anachokifanya. Cha muhimu ni kumuombea salama tu."
"Lakini ..." Sultan akachombeza. "Nina mashaka sana na Karim. Na usiri wake unanipa mashaka zaidi. Nilikuta farasi wa mke wangu kwake. Pamoja na vijakazi wake hapo. Najua alikuwapo pale, lakini sikumuona abadani!
Nahisi kuchanyikiwa."
.
.
.
Kweli ilikuwa inakanganya. Na Sultan alichanganyikiwa kwasababu hakufikirisha akili yake zaidi ya ubinadamu. .
.
.
Alisahau Karim ni nani, na ana uwezo gani. Alimuweka Karim kwenye kategoria moja na binadamu wengine hivyo basi akaishia kustaajabishwa.
.
.
.
Wakaendelea kula mpaka walipomaliza kabla hawajajipumzisha Sultan asionekane mwenye dalili ya kuondoka leo, kesho ama mtondogoo.
.
.
.
Wakati huku ikiwa hivi, watu wakifanya jitihada za kutafuta furaha na amani, huko upande mwingine wa dunia, kwenye kasri ya Sultan ndani ya lupango palikuwa kisima cha huzuni na majuto kwa Karim.
.
.
.
Alikuwa amejilaza juu ya sakafu akiwa amejikunyata kwa baridi. Akihangaika mara kwa mara kupambana na wadudu waliokuwa wanamtambalia.
Alikuwa amevalia bukta tu, tena fupi. Mwili wake uliojaa nywele ukibakia wazi kukaribishwa wadudu kadhaa kusaka kitoweo.
.
.
.
Yalikuwa tayari ni majira ya usiku. Mataa yakawashwa kasrini na walinzi kuanza kuzunguka huku na kule.
.
.
.
Mlinzi mmoja akasogelea selo ya Karim akiwa kabebelea sahani ya chakula baridi. Akafungua mlango na kuiweka sahani chini. Akaisukumia kwa Karim kwa mguu kisha akatoka ndani na kufunga.
.
.
.
Akaenda zake. Punde Karim akaamka na kula. Alikula matonge mawili tu, akaacha. Chakula kilikuwa kibovu. Alikula tu apate jikomboa dhidi ya kifo.
.
.
.
Akajikunyata na kujilaza. Akatazama dari la chumba kwa muda kabla kope zake hazijafunga kwa usingizi.
.
.
.
Akiwa usingizini, mara akasikia sauti ya dada yake yamuita. Yamlilia.
.
.
.
"Kaka, nirudishe duniani!"
.
.
.
Akashtuka kweli. Akatazama kushoto na kulia asione mtu. Akafikicha macho yake mara tatu akihema kwanguvu.
.
.
.
Hakukaa punde, sauti ikarudia tena. Mara hii akiwa macho hajalala. Aliisikia kwenye sikio lake la kushoto.
.
.
.
Sauti yamlilia.
.
.
.
"Kaka, kaka, nirudishe duniani!"
.
.
.
.
.
.
***
*** LAKO JICHO! .