*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 027*
*Simulizi za series*
"Dada, hatuna muda, Sultan atatukuta hapa!" Alisema Karim akitoa macho kumtazama Sultana. Joto lilikuwa kubwa. Akili ya Sultana ilivurugika, alishindwa kufanya maamuzi akabaki tu ameduwaa.
.
.
.
Karim alinena maneno kadhaa kisha akapangusa viganja vyake kwanguvu, na kumpakaa Sultana usoni, kufumba na kufumbua Sultana akapotea! Alijitahidi kubadili mazingira yasilete walakini, akafanikiwa kwa kiasi kidogo sana kwani vitu vilikuwa vingi. Maandalizi yalichukua muda hivyo huwezi yatengua ndani ya sekunde chache tu.
.
.
.
Alijikuta anakutwa na Sultan akiwa anahangaika. Aliigiza kama mtu asiyejua ujio huo, akashangazwa na kumuona kiongozi mkubwa mbele ya macho yake.
.
.
.
Alitabasamu akikutanisha viganja.
.
.
.
"Sultan!" Aliita. Aliinamisha kichwa chake kisha akaendeleza soga. "Mbona ghafla kiongozi wangu, utokako kwema?"
.
.
.
Sultan alitazama mazingira kwa muda wa dakika tatu pasipo kusema jambo. Aligeuka akawatazama walinzi wake wawili na kuwatikisia kichwa, walinzi wakaanza fanya upekuzi wakienenda na kutazama huku na huko.
.
.
.
"Sultan, kuna shida gani kiongozi wangu?" Aliuliza Karim. Bado Sultan hakutaka kuongea, bali kutazama mazingira.
"Naomba unishirikishe, pengine naweza nikasaidia," alishauri Karim. Sultan akamtazama mwanaume huyo kwa macho ya ghafira.
.
.
"Ulishindwa kwenye mkufu, utaweza nisaidia na nini kingine?" Aliuliza. Karim akapata haya.
"Sijashindwa, Sultan. Ni kitendo cha muda tu."
"Karim, unadhani tunaishi duniani milele?"
"Hapana, kiongozi. Jambo hili limekuwa zito sana. Si jepesi hata kidogo. Kila kona ya ulimwengu huu inataka mkufu huo. Hakika ngoma hii si lelemama."
.
.
.
Ghafla walisikia sauti ya mwanaume inalia kwanguvu. Walishtuka wakakimbilia huko sauti ilipotokea. Walimkuta mlinzi akiwa amelala chini amefichama uso wake. Pembeni kulikuwa kuna chungu, kile Karim alikuwa anatumia kupikia madawa.
.
.
.
"Nini hiki?" Aliuliza Sultan.
"Ndio maana nikakuomba unishirikishe, Sultan, tuepushe mambo haya," Karim alisema na kuongezea: "Hii ni dawa niliyokuwa naitengeneza, ni kali na ya moto sana"
"Embu nione," Sultan akaagiza. Karim alifungua chungu, Sultan akatazama yaliyomo ndani akiwa amesimama mbali kupisha mvuke wa moto wenye harufu kali.
"Hizo ni nini, si nywele?" Sultan aliuliza akinyooshea kidole.
"Ndio, ni nywele, Sultan," akajibu Karim.
"Nywele za nani? Mbona ni ndefu, ni za mwanamke?"
"Ndio, Sultan. Nimezitoa huko kaskazini ya mbali, kwa mwanamke mmoja wa hadhi ya chini."
.
.
.
Karim alifunga chungu wakaongozana na Sultan kuelekea ndani.
.
.
.
"Karim, nimekuja kwako kwa madhumuni makubwa mawili, na sikuona kama nina haja ya kukutaarifu juu ya ujio wangu, ulipangwa uwe hivi hivi."
"Unanipa hofu, Sultan. Ingekuwa vema ukaniweka wazi," Karim alipendekeza. Walifika sebuleni wakaketi.
"Dhumuni langu la kwanza ni mke wangu, najua yupo hapa, japokuwa sifahamu haswa mahali gani. Nashindwa kuelewa mambo kadhaa kumhusu huyu mwanamke, na ningependa unipatie majibu ya mantiki."
Moyo wa Karim ukatikisika. Alimtazama na kumsikiza vema Sultan, alikuwa anaongea akiwa na uhakika kana kwamba aliambiwa na mtu anayemuamini kuwa Sultana yu pale. Alijikuta anaanza kuandaa na kupangilia majibu kichwani.
.
.
.
"Nimesema hivyo kwasababu kwanza, wewe ni ndugu yake. Pili, wewe ni mganga, hivyo basi kwa hili nina uhakika waweza fua dafu. Sijamkuta mwanamke huyu nyumbani, na nimepewa taarifa hakuwepo pia kwa siku kadhaa. Kasri lilikuwa pweke akipuyanga. Nataka kujua kwanini."
.
.
.
Karim alishusha pumzi ndefu. Kwa kutazama mboni ya macho yake ungalifahamu namna gani alivyozama fikirani. Alichagua na kubagua maneno ya kujibu.
.
.
.
"Sultan, nimeshangazwa sana na habari zako," alisema Karim. "Sina taarifa yoyote kuhusu dada yangu, na wewe ndiwe umekuwa wa kwanza kunambia. Sijui alipo, lakini naweza kukusaidia kumtafuta."
"Alishawahi kuja hapa?" Sultan aliuliza. Karim alisita kujibu upesi swali hilo, ila kutokana na jibu lake la mwanzoni alikuwa tayari ameshajifunga. Hakuwa na budi kujibu:
"Hajawahi kuja."
"Tangu lini?"
"Ni muda mrefu sasa."
.
.
.
Sultan akatabasamu. Tabasamu hili halikuwa la kheri, hata Karim alilijua hilo.
.
.
.
"Vipi hao farasi na watumishi wangu niliowakuta kwenye ukumbi wa jengo lako? Ni wa nani?"
.
.
.
Hili swali likammaliza Karim. Sasa hakuwa na ujanja. Alijiona mjinga kwa kutojua hilo jambo na kulichukulia hatua mapema. Alijikuta anakosa jibu la maana, ila hakutakiwa pia kunyamaza. Akajitutumua kujibu:
"Watumishi na farasi hao niliwaagiza toka kasrini kwako. Nilituma ujumbe kwa Sultana kwamba nahitaji ulinzi zaidi, bila shaka akaamua kumsaidia kakaye."
"Ulituma ujumbe huo lini?"
"Siku kenda sasa zapita."
.
.
.
Sultan akasimama akiita:
"Karim!" .
.
.
Uso wake alikuwa ameukunja. Macho yake yakiwaka hasira.
.
.
.
"Unaiudhi sana kwa majibu yako. Hakika umenifanya nijihisi mtoto na mjinga mbele zako. Nimepoteza imani na wewe, na hata ile iliyobakia, ndogo mithili ya mbegu ya haradali, nayo umeisaga kwa ulimi wako.
Hautakiwi kuwa huru, wala hai."
.
.
.
Sultan alipiga makofi matatu, mara wanaume watano wakaingia ndani. Aliwaamuru wamkamate Karim haraka na kisha wakague nyumba nzima kumtafuta Sultana. Walinzi wakatii.
.
.
.
Walitafuta kila kona, hawakupata kitu. Walimfunga Karim mikono na miguu, wakamtia kwenye keji ngumu ya mbao waliyokuja nayo, wakaondoka naye.
Sultan hakupata wasaa wa kumalizia dhamira yake ya pili iliyomleta eneo hilo. Alipungukiwa subira.
.
.
.
.
.
***
.
.
.
.
Aliwasili mbele ya nyumba ya bibi yake ikiwa ni jioni nzito. Mwanamke huyu, Sultana mdogo, alikuwa ameongozana na wanaume wawili waliobebelea jambia ndefu na nguo za mapambano. Wanaume hao walikuwa warefu na wenye miili ya wana usalama. Nyuso zao zilikuwa ngumu,macho yao yalikuwa mepesi kurandaranda huku na kule.
.
.
.
Sultana alishuka upesi farasini, mlinzi mmoja akawakusanya farasi na kuwafungia, mwingine akaongozana na Sultana kuufuata mlango wa makazi, hapo Sultana akagonga si chini ya mara tatu pasi na mafanikio.
.
.
.
Aliita lakini bado ilikuwa bure. Alizunguka nyuma ya nyumba akaangaza, hakuona mtu. Alikasirika akavimbisha mdomo. Aliona muda unaenda kama vile risasi. Alienenda kwa majirani kuuliza, mmoja akamwambia bibiye ametoka tangu asubuhi, hakuaga anaenda wapi.
Sultana aliishiwa nguvu. Alirudi kwenye makazi ya bibi yake akaketi kibarazani akiweka tama. Alikuwa amechoka kweli, ila dhamira yake ya moyoni ilikuwa kubwa. Alisubiria kama lisaa limoja, akapitiwa na usingizi.
.
.
.
Hakujua alilala kwa muda gani, alikuja kushtuliwa na mlinzi aliyekuwa amesimama kandokando yake akimtaka aamke maana mwenyeji wake amekuja. Sultana akaamka upesi, akamkimbilia bibi yake na kumkumbatia. Bibi alikuwa amebebelea furushi kubwa alilolining'iniza kwenye mti uliolala begani.
.
.
.
Waliingia ndani, na pasipo kupoteza muda Sultana akamwambia Bibi kilichomleta.
.
.
.
"Kwahiyo hivyo tu?" Aliuliza Bibi.
"Ndio hivyo, bibi," akajibu Sultana, akiongezea: "Sijaelewa lengo lake lilikuwa ni nini, japokuwa najua si zuri. Haiwezekani aje usiku ghafla, nipoteze fahamu, nizinduke asubuhi, tayari ameshaondoka! Inaingia akilini kweli?"
.
.
.
Ungeweza kuona hofu juu ya uso wa Sultana.
.
.
.
"Usijali, mjukuu wangu. Ni jambo dogo sana hilo. Ilimradi umeshafika hapa, tena salama, basi kila jambo litaenda vema," alisema Bibi akimtazama mjukuu wake kwa macho ya matumaini. Alinyanyuka akaenda zake chumbani na kifurushi chake alichokuja nacho, baada ya muda kidogo akarejea akiwa amebebelea kachupa kadogo kanene chenye mfuniko mwekundu.
.
.
.
Ndani ya kachupa hako kulikuwa kuna vitu vidogo vidogo vya bluu vinavyowaka waka kama taa. Vitu hivi vilikuwa vinapaa vikienda huku na huku. Vilikuwa vingi kiasi. Mbali na vitu hivyo, chupa ilikuwa giza usimuone mtu wa upande wa pili.
.
"Vua nguo, ulale chini," Bibi aliagiza, Sultana akatii. "Fumba macho, hema kwa kina: vuta hewa ndefu ndani, toa hewa ndefu nje," Bibi alitoa maagizo mengine, Sultan akatii.
.
.
.
Akiwa ameshikilia kichupa kwa mkono wake wa kushoto, Bibi akaweka kiganja cha mkono wake wa kuume kwenye paji la uso la Sultana. Akafumba macho na kunena maneno kadhaa, alafu akaanza kuuzungusha mkono wake wa kushoto kila pande. Akanena tena maneno kadhaa yasiyoeleweka.
.
.
.
Bado akiwa amefumba macho, akaweka kichupa kile tumboni kwa Sultana, akasikilizia jambo hapo kwa sekunde tatu. Baada ya hapo aliweka kichupa kwenye paji la uso la Sultana, akasikilizia napo kwa sekunde tatu. Mara kichupa kikaanza kutikisika.
.
.
.
Bibi alifungua macho yake akatazama kichupa. Vile vitu vya bluu vilikuwa vinazunguka kwa kasi, na mara vikatengeneza taswira ya nywele, nywele alizokatwa Sultana.
.
.
.
"Alichukua hiki toka kwako," alisema Bibi akimuonyeshea Sultana kichupa. Sultana alifungua macho akatazama.
"Nywele!" Alistaajabu.
"Ndio, nywele," Bibi akajibu alafu akainamisha kichwa cha Sultana na kukipekua. Baada ya sekunde kadhaa, alisema:
"Amechukua nywele za utosi!" .
.
.
Macho ya bibi yalionyesha hofu. Nywele za utosi ni malighafi kubwa mno kwa walozi. Ni tofauti na nywele zingine, za upande mwingine. Nywele hizi zina mamlaka, na zina uwezo mkubwa wa kumfinyanga mwenye nazo kadiri mlozi anavyotaka. Utosi ni chanzo, lakini pia ni ufunuo.
.
.
.
"Sasa Bibi atakuwa amenifanyia nini?"
"Usijali mjukuu wangu, poa mama. Poa." .
Bibi alirudi chumbani, punde akatoka akiwa amevalia kitambaa cha rangi ya dhambarau kichwani na chupa ndefu yenye unga mweupe. Kitambaa hicho kilikuwa kimeandikwa lugha ngeni tusiyoitambua.
.
.
.
Bibi aliketi chini akifungasha miguu yake kana kwamba yu ndani ya dojo. Aifungua chupa akaweka unga kiganjani na kuanza kuurushia kwa Sultana aliyekuwa bado amelala chini. Baada ya hapo alifunga macho yake na kusafirisha mwili wake kilozi.
.
.
.
Akiwa fikirani humo, alipata kuona kila jambo alilolifanya Sultana mkubwa, na mpaka mwisho wake. Alirejea fahamuni akamwamsha Sultana, mjukuu wake, akiwa anatabasamu.
.
.
.
"Vipi Bibi?"
"Kila jambo lipo shwari," alijibu Bibi akionyeshea dole gumba. Alimwelezea mjukuu wake alichokiona huko ulimwengu mwingine. Sultana akachomoza tabasamu.
"Kwahiyo amekuwa upepo?" Aliuliza Sultana.
"Ndio, amegeuka upepo kumkimbia Sultan. Na Karim mgangawe amekamatwa, hamna wa kumrudisha kwenye umbo lake!"
.
.
.
Sultan alifurahi. Aliamka upesi akajivesha nguo.
.
.
.
"Vipi tena?" Bibi akauliza.
"Inabidi niwahi nyumbani, Sultan anaweza akaja," Sultana alijibu.
"Usiku huu?"
"Hapana, anaweza akaja asubuhi. Endapo nikitoka huku asubuhi, dhahiri ntachelewa. Unajua huku na makazi yangu kuna umbali mkubwa mno. Ila tokea kasri ya Sultan ni karibu usitoe jasho kabisa kufika."
"Vipi lakini usalama wako mjukuu wangu? Huoni hatari usiku mzito kuwapo njiani?"
"Ndio maana nimekuja na walinzi bibi!"
Sultana aliaga akatoka ndani, akakwea farasi na kutimka pamoja na walinzi wake.
.
.
.
***
.
.
.
."Kundi la kwanza litapita huku!" Alisema Fluffy akielekeza uelekeo wa kushoto. "La pili litapita huku." Akaelekezea kulia. "La tatu tutatumia njia hii." Akaelekeza kaskazini. "Tumeelewana?" Akaliza.
"Ndio!" Wanaume wakajibu kwa sauti kuu.
.
.
.
Mwanamke huyo alikuwa amevalia nguo za mapambano, ngumu na zenye uzibe mgumu kifuani. Miguu yake ilikuwa imefunikwa na viatu virefu mpaka magotini. Mkono wake wa kuume ulikuwa umeshikilia panga refu jembamba, na wa kushoto ulikuwa umebebelea ngao kubwa ya duara.
.
.
.
Alibana nywele zake vema. Mikono yake kwenye viwiko ilikuwa imefunikwa na kava gumu la ngozi. Alijiandaa kwa mapambano.
.
.
.
Alioongozana na wanaume mia tatu kwa idadi ya macho ya haraka. Wanaume hao nao walikuwa wamebebelea silaha mbalimbali, kama vile jambia, visu, shoka, miti yenye misumari na kadhalika. .
.
.
Malkia hakuwapo, alibakia nyuma pamoja na Zura wakiwa na idadi ya wanaume waliobakia.
.
.
.
Fluffy akiongozana na wanaume kadhaa, wakati wengine wakielekea pande zingine, walizama ndani ya himaya ya Kuhani wa pili mwanamke akiongoza msafara. Walitembea kwa takribani robo saa, wakaanza kuona makazi ya watu. Makazi haya yalikuwa dhoofu, useme yanaanguka upepo ukipuliza. Ndani ya makazi hayo kulikuwa kuna wanaume waliojilalia humo.
Tarumbeta kubwa lilipigwa na mwanaume aliyekuwa nyuma ya Fluffy. Tarumbeta lililia kwa sauti kuu na ikavuma ndani ya himaya nzima. Kila mtu mwenye uwezo wa kusikia akasikia, na kutazama itokeapo sauti hiyo. Kuhani alipanda chumba cha juu akaangaza, kwa mbali akaona kikosi cha watu wachache wakiongozwa na mwanamke.
.
.
.
Alijiuliza maswali kadhaa. Alishuka chini upesi akasimama mlangoni pa jengo lake kuu. Hapo alikuwa na wanaume takribani ishirini wakimlinda.
.
.
.
Kutokana na Fluffy kuongozana na wanaume ambao hawakuwa wageni ndani ya himaya ile, hakupata bughdha, bali alisindikizwa mpaka mbele ya nyumba kuu ya Kuhani mkuu, hapo akasimama.
.
.
.
"Wewe ni nani?" Kuhani mkuu aliuliza.
"Mimi ni Fluffy, kamanda mkuu wa himaya ya Sawaridi."
"Kamanda mkuu?" Kuhani mkuu aliuliza kisha akaangua kicheko. Wafuasi wake nao wakafuatia kwa cheko la haja.
"Kamanda mkuu? Sawaridi ndiyo nini? Na nyie ..." Kuhani mkuu aliwanyooshea kidole wanaume walioongozana na Fluffy.
.
.
.
"Huyu kikaragosi hapa ni nani?"
.
.
.
Kufumba na kufumbua, mkono wa Kuhani mkuu ulidondoka chini. Haikujulikana nini kilitokea, ila panga la Fluffy lilikuwa linachuruza damu.
.
.
.
***
***
Lako jicho!