SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

Mkuu Shunie naona umejitosa kwenye riwaya. Angalia tu usije acha watu arosto kama banker !
 
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 003*

*Simulizi za series*



“Nyie binadamu mnafanya nini Tanashe?” Malkia akatahamaki zaidi kwani lilikuwa ni swali lilelile aliloulizwa akiwa ndotoni. Na sasa hapo ndipo akajua ya kwamba yale aliyoyaona ndotoni yalikuwa ni yale yatakayotukia mbele yake.

Sasa afanyaje?

Hakuwa na muda wa kumueleza Zura juu ya yale aliyopata kuyashuhudia ndotoni. Waliongozana na bibi wale kama ilivyokuwa kwa mujibu wa ndoto mpaka pale walipofika kwenye nyumba kubwa nyeusi ambamo waliingia na mjadala kuhusu mkufu ukazuka baada ya muda mfupi, bibi wale wakiwa wanataka kuuona na kuugusa.

Hii ndiyo nafasi! Akaamini Malkia Sandarus. Kama kweli alikuwa anataka kuokoka dhidi ya wale vigagula basi ilimbidi atumie mwanya huu vema. Aliuvua mkufu wake akiwa anajua fika ya kwamba utawaunguza wale viumbe.

Alipomkabidhi bibi mmojawao, ulimuunguza akaudondodha chini. Malkia akauwahi mkufu wake na kuwanyooshea kana kwamba silaha.

“Kaa mbali!” Alifoka. Bibi wale walisogea mbali na walihofia. Walikumbatiana kwa woga na ni wazi nyuso zao za kizee zilizojikunja zilionyesha hofu. Malkia alimtazama Zura akamtaka anyanyuke kitini waondoke upesi. Zura akatii.

Walisogelea mlango, bado Malkia akinyooshea mkufu wake kwa wale bibi, wakaondoka kumfuata farasi waliyemkwea na kumuamrisha aondoke haraka! Farasi alikimbia upesi na ndani ya muda mfupi alikuwa amemezwa na giza asionekane hata mahali alipoelekea.

“Umeruhusuje akaondoka?” Alilalama bibi mmoja kana kwamba hakuwepo wakati tukio linatokea.

“Ila hawezi akafika mbali,” Mwingine naye akasema.

“Ndio, hawezi akafika mbali. Ila tumeshakosa ule mkufu. Vipi kama wakiupata wachawi wengine?” Aliuliza mmoja kwa jazba. Ilikuwa ni ngumu kweli kuwatofautisha tangu kila mmoja alikuwa na jicho moja tu.

“Endapo wakiupata wachawi wengine basi itakuwa mbaya sana kwetu.” Aliendelea kuongea.

“Sasa tutafanyaje?” Akauliza mwingine.

“Inabidi tuwafuatilie mpaka pale tutakapoupata mkufu huo. Hatuwezi tukaipoteza hii nafasi!” Alilonga mmoja kwa shari. Haraka bibi hao watatu waliungana wakatengeneza mtu mmoja mkubwa mno mwenye macho matatu.

Mikono yake ilikuwa imejaza kimraba na miguu yake ilikuwa mipana kama shina la gogo. Kabla hajaondoka kwenda kuwafuatilia Malkia na Zura, alinguruma kama simba. Kunguru wote waliokuwa wanazunguka hilo eneo wakakimbia wakitawanyikia kila pande.

Mtu huyo mkubwa, ama tunaweza kumuita jitu, alikimbia upesi akitupa miguu yake chini na kusababisha kishindo kikubwa, kishindo ambacho hata kama ungelikua maili moja mbali basi ungelipata kukisikia.

Kichwa chake kilichokuwa juu kilimuwezesha kutazama kila pande na basi akawa anabashiri wapi anaowatafuta wameelekea. Kila alipopita miti ilitikisika na viumbe wakakimbia kuokoa maisha yao.

Baada ya kukimbia kwa muda wa dakika nne tu, sauti yake ya kishindo ikawafikia Malkia na Zura ambao bado walikuwa juu ya mgongo wa farasi.

“Malkia, wanakuja!” Zura alisema kwa hofu. Malkia hakutia neno, zaidi alimwamrisha farasi wake aongeze mwendo.

Haikujalisha ni kwa namna gani farasi alivyokimbia, jitu lilizidi kuwakaribia zaidi na zaidi. Hata kwa mtoto angeliweza kubashiri ndani ya muda finyu Malkia na Zura watakamatwa.

“Malkia, anazidi kutukaribia!”

Malkia aligeuza uso wake kutazama. Hapo farasi akajikwaa. Alidondoka akawamwagia Malkia na Zura mbali! Malkia alibiringita mara tatu wakati Zura akibiringita mara tano kabla hajatulia tuli.

Malkia alinyanyua uso wake akamtazama Zura, hakuonekana kama ana fahamu. Alimtazama na farasi wake akamuona anagugumia kwa maumivu.

Kwa muda kidogo hakujali kama anakimbizwa bali kutazama usalama wa wenziwe. Alipokuja kutazama anayewakimbiza, alishangaa kumuona tayari amemfikia mguuni! Alijaribu kunyanyuka, akakandikwa kofi zito akazirai.


Jitu lilimbeba Zura na Malkia likaondoka nao. .
.
.
.
.
*** HAKUNA ZAIDI … ZAIDI YA MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***
.
.
.
.
.
Jitu lilifika nyumbani kwake akawatua mateka wake. Punde akaparanganyika na kuwa wale bibi watatu.

“Tunawaua?” Mmoja aliuliza.

“Hapana!” Mwingine akajibu. “Tunamuhitaji zaidi akiwa hai.”

“Kwanini?”

“Huyu ni Malkia!” Alifoka. “Tukimtumia huyu Goshen itakuwa chini yetu.”

“Tukimtumiaje?”

“Tukimtumiaje! – Kwani hujui? Mbona akili yako imelala sana wewe?”

Kukawa kimya kidogo.

“Tukikamata kichwa cha Malkia, tutapata yale yote tunayoyataka toka Goshen!” Alisema mmojawao. Walifurahi wakionyesha vinywa vyao vyenye uhaba wa meno.

Ulikuwa ni wasaa mzuri sasa kurudi kwenye ardhi ya Goshen baada ya kufukuzwa huko kwa muda mrefu tangu pale walipogundulikana ni wachawi.

Ilikuwa ni desturi. Tanashe ni tawala ya wachawi ambao wamerundikwa hapo toka kwenye tawala mbalimbali baada ya kuvumbuliwa toka kwenye jamii zao ya kwamba ni wachawi.

Kwa mtu yeyote pale anapogundulikana kuwa na sifa zozote za kilozi, basi adhabu yake huwa ni kumtupia kwenye ardhi hiyo ya Tanashe – ardhi iliyolaaniwa.

Ardhi isiyo na maji wala chakula. Na kama mtu ni kweli alikuwa mlozi, akishaingizwa Tanashe huo unakuwa mwisho wake kwani hawezi toka tena humo kurudi tawala aliyotokea.

Mipaka yake imetiwa dawa madhubuti ambayo hakuna mchawi yeyote anayeweza kuvuka na kwenda kwenye tawala yoyote za karibu. Huko ndani ya Tanashe atajua anakula ama kunywa nini. Atajua anaishije muda uzidi kusonga.

Wachawi wengi walipoteza familia zao. Hawakuweza tena kuona aidha watoto, wake ama waume zao baada ya kupelekwa Tanashe.

Si tu kwamba kwasababu hawakuweza kutoka humo, bali pia binadamu wa kawaida wasio wachawi hawakusogelea tawala hiyo. Watu kadhaa ambao walijaribu kuingia humo waliishia kuwa vitoweo na isijulikane hata walipoelekea.

Sifa kubwa ya tawala hiyo ya Tanashe ilikuwa ni kutokuwa na alama yoyote ya binadamu pale jua linapochomoza. Kama ungelikuwa karibu na mpaka ukatazama ndani ya tawala hiyo muda wa mchana, usingeona chochote bali mithili ya jangwa.

Lakini ifikapo usiku, mji unakua na unaweza ukawaona watu wanakatiza katiza. Na kama basi upo karibu, si ajabu kuona mtu anakutazama huku akikulaghai kwa kukuita.

“Usisogelee karibu na Tanashe!” Lilikuwa ni mojawapo ya onyo maarufu walilokuwa wanapewa watoto na aidha wazazi wao ama watu wazima.

Hakuna mtoto aliyepotea kwa kuingia humo alafu akapatikana. Inasemekana wakiingia humo nao wanawakuwa walozi.

Kuelekea upande wa kaskazini wa tawala ya Tanashe ndipo kulipokuwa kunapatikana tawala ya Devonship chini ya katili Jayit. Tofauti ndogo zilizokuwepo kati ya tawala hizi ni swala la uongozi na pia mawio na machweo ya jua.

Tanashe haikuwa na kiongozi, bali tu kila eneo lina mchawi anayelitawala. Lakini pia vilevile jua lilikuwa linachomoza na kuzama kwenye tawala hiyo. Kinyume na Devonship, mtawala alikuwa mmoja tu tawala nzima: Jayit, na ndani ya tawala hiyo jua halikuwahi kamwe kuonekana!

Mkufu wa Malkia uliviringishwa ndani ya kikaratasi cheusi na mmoja wa wale bibi. Alipomaliza kuufungasha vema mkufu huo, aliwatazama wenzake wakaanza kujadili ni namna gani ya kuufanya mkufu huo.

Ila wakiwa wanajadili wakagundua kuna umuhimu wa kujua ni wapi mkufu huo ulipotokea kwa minajili kwamba ndipo itakuwa rahisi kwao kuuongoza lakini hata kuuamrisha kutokana na matakwa yao.

“Tunaweza kutawala Tanashe na mkufu huu!”

“Sio tu Tanashe. Tunaweza tukarejea Goshen kwenye familia zetu na kutawala huko!”

Walienda uwani mwa nyumba yao kubwa, huko waliteka kioo cha saizi ya kati na fuvu mbili za vichwa vya binadamu. Waliviweka pamoja juu ya meza.

Meza hiyo pia ilikuwa imeshikiliwa na mifupa ya miguu ya binadamu. Walifungua kile kikaratasi kilichofichama mkufu kwa malengo kwamba wautoe mkufu huo na kuutazamisha kwenye kioo ili wapate kuona kwa kupitia kioo chao, wapi haswa chimbuko la mkufu huo.

Mmojawao akiwa ameushikilia huo mkufu kwa kile kikaratasi ili asipate kuungua, aliutupia huo mkufu juu ya kioo, na kisha kwa pamoja wakasema maneno yasiyoeleweka.

Punde macho ya fuvu zile mbili za binadamu yakaanza kufuka moshi wa kijani. Moshi huo ulitanda karibia eneo lote. Bibi wale walitabasamu wakijua sasa pale moshi utakapokoma wataweza kuona yale wanayoyataka ndani ya kioo chao cha ajabu.

Moshi ukakoma.

Walitazama kwenye kioo upesi wakiwa na nyuso za hamu. Ajabu hawakuona chochote!

“Unaona kitu?” Mmoja aliuliza.

“Hapana, sioni. Najiona mwenyewe na nyie.”

Punde kioo kikaanza kupiga ufa kana kwamba ukuta. Kklaakk! Kakkaakakakk! Kakaaakkak! Kufumba kufumbua kikapasuka kwanguvu. Vipande vyake viliruka juu na vikawaingia machoni mwa wale bibi wakaishia kulalama kwa maumivu wakishikilia nyuso zao.

Haikupita punde, wakasikia sauti za fisi mbele ya nyumba yao. Kila mmoja alinyofoa jicho lake akalipangusa dhidi ya vioo na kuyarudisha tena usoni.

“Nani huyo?” Mmoja aliuliza.
“Si mwingine bali ni Faki!” Mwingine akajibu.
“Atakuwa anataka nini?”

Swali hilo lilikosa majibu. Waliuchukua mkufu kwa kutumia kile kitambaa mmojawao akauficha sehemu za siri na kisha wakaenenda huko nje waliposikia sauti ya fisi akibweka.

Walikuta fisi wakubwa karibia mia moja na hakukuwa na alama yoyote ya binadamu.

“Unahitaji nini Faki?” Bibi mmoja aliuliza. Wote walikuwa wamekunja mikono yao wakiiweka kifuani.

Fisi walikaa kitako, kutoka nyuma yao akasogea fisi mkubwa kuliko wote. Alipojongea mbele aligeuka na kuwa binadamu mrefu mwenye misuli ya kutosha.

Alikuwa mweusi mwenye ndevu nyingi. Uso wake ulifanana na fisi kabisa. Hakuwa amevalia kitu chochote, hivyo alikuwa uchi mnyama. Alisogea karibu na bibi wale watatu akapandisha nyusi moja juu.

“Nahitaji mlichokichukua kwangu,” Alisema Faki kwa kujiamini.

“Kipi tumechukua kwako?” Bibi mmoja aliuliza. Faki akatabasamu kwa kejeli.

“Hamjaingia kwenye himaya yangu leo hii?” Aliuliza. Bibi wakatazamana na kisha mmoja akajibu:
“Tumeingia lakini tulikuwa tunafuata kitu chetu.”

Faki akatabasamu.

“Hamuwezi mkafuata kitu chenu kwangu. Kitu kikiwa kwenye himaya yangu, ni changu. Naomba mnipatie sasa hivi!”

“Faki, hatuwezi tukakupa kisicho chako,” alisema bibi mmoja.

“Ila mliweza kuingia kwenye eneo langu, si ndio?” Akauliza Faki. Kukawa na kaukimya kafupi.

“Sina muda wa kupoteza hapa na nyie vikongwe. Naombeni kilicho changu niende.”

“Unakijua hata hicho unachodai ni chako?” Aliuliza bibi.

“Najua ndio,” akajibu Faki. “Ni binadamu – wawili!”

“Tutakupa mmoja.”
“Nataka wote!”
“Tutakupa mmoja tukagawane.”
“Nimesema nataka wote!”
“Basi hautopata kitu!” Alisema bibi mmoja kwa kujiamini akimtazama Faki machoni.

Faki alirudi nyuma kuungana na fisi wenzake. Ndani ya muda mfupi aligeuka mwili akawa fisi mkubwa kama alivyokuwa hapo awali. Pasipo kupoteza muda, bibi nao wakajikusanya na kuwa mtu mkubwa mno mwenye macho matatu.

Alinguruma kama simba akielekeza mdomo wake angani. Faki alibweka naye kwanguvu kisha akaamrisha fisi mia moja aliokuja nao wamshambulie yule mtu mkubwa – jitu!

Kufumba na kufumbua ikawa vita!


Fisi wakamrukia yule jitu wakamrarua na kumng’ata. Lakini naye jitu asiwe nyuma alikuwa anawakamata na mkono wake mkubwa akawavunja vunja ama kuwatupia mbali.

Makelele ya fisi na ya jitu yalitapakaa. Malkia Sandarus na Zura waligutuka toka kwenye usingizi mzito wa kutokuwa fahamuni. Walikuwa wamefungiwa kwenye kichumba kidogo cheusi chenye dirisha dogo juu.

Kwa mujibu wa dirisha hilo, anga lilikuwa linaanza kung’aa kuelekea asubuhi ya mapema zaidi.

“Zura, mkufu upo wapi?” Aliuliza Malkia. Alikuwa anaogopa, kama ungelimuona tu uso wake basi ungeling’amua hilo.

“Sijui Malkia wangu,” Zura alijibu. Malkia alipapasapapasa shingo yake lakini hakuona kitu, mkufu haukuwepo! Aliendea mlango wa chumba hicho akajaribu kuufungua, akashindwa.

Zura alimtengea Malkia wake mkono kama ngazi, Malkia akaupanda na kuchungulia nje kwa kupitia ka mwanya ka dirisha. Huko nje akaona pambano kubwa kati ya fisi na lile jitu kubwa. Aliperuzi huku na kule kutafuta lakini hakuona mkufu wake.

Ndani ya muda mfupi wakasikia mlango unafunguliwa. Haraka walifuata mlango huo, wakamkuta farasi wa Malkia! Ilikuwa ni ajabu. Kwa kutumia mdomo wake, farasi huyo alipindua kitasa akijua fika ndaniye mulikuwa na dereva wake, malkia wake: Sandarus.

Ilikuwa ni bahati kwa farasi huyo kuachwa peke yake pale Zura na Malkia walipotwaliwa. Yule jitu, ama wale bibi, hawakuona umuhimu wa kumchukua farasi huyo. Walimuacha wakitumai hatodumu muda mrefu kabla hajaliwa na viumbe vingine ndani ya Tanashe.

Hawakufahamu kwanini farasi huyo alikuwa ni wa Malkia. Hawakujua kwamba kiumbe huyo ana uwezo wa kumtafuta Malkia wake popote pale ndani ya maili tano. Mnyama pekee ndani ya Goshen anayemjua bwana wake na hayupo radhi kumtumikia mtu mwingine yeyote zaidi ya huyo.

“Roob!” Aliita Malkia akimkumbatia farasi wake. Alimkwea yeye pamoja na Zura akamuamuru kuzunguka ndani ya nyumba ile kubwa wakitafuta mkufu wake.

Walizunguka kote lakini hawakuuona. Walizunguka uani wakawa wanachungulia mpambano ambao bado ulikuwa unaendelea – kati ya fisi na jitu. Lengo lao lilikuwa ni kutafuta mkufu wa Malkia. Jitu alikuwa amejeruhiwa vibaya mno akivuja damu, na hata fisi nao hawakuwa wengi – kama arobaini tu ndio bado walikuwa hai.

Kitendo cha Malkia kuchungulia, mkufu ulianza kuhangaika ndani ya sehemu za siri za jitu.

Ulijinyongorota ukaenda huku na kule kwa nguvu ukitaka kuchoropoka. Ulimsumbua jitu huyo kiasi kwamba akapoteza kabisa atensheni kwenye mpambano. Fisi walimshambulia vibaya mno. Walimdondosha chini na kuendelea kumng’ata. Mkufu ulitoka ndani ya vazi lake ukaenda upesi kwenye mkono wa Malkia. Haraka Malkia akamruhusu farasi wake akimbie!

Sauti ya farasi akikimbia ikakamata masikio ya fisi. Faki – fisi mkubwa kiongozi – akaamuru fisi wote kumkimbiza farasi yule aliyebebelea binadamu. Fisi wote walio hai wakaanza kumfukuza farasi huyo kwa kasi. .

.
.
.*** HAKUNA ZAIDI … ZAIDI YA MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! *** .
.
.
.
.
Farasi wa Malkia alikimbia upesi. Mbio zake hazikuweza kumithilika na zile za fisi wanaomkimbiza. Japokuwa fisi walikuwa wanakimbia taratibu ukilinganisha na farasi wa Malkia, hawakuonekana kuchoka ama dalili za kukata tamaa!

Kama ingelikuwa muda ulikuwa upande wao basi wangelihakikisha wanawapata binadamu wale juu ya mgongo wa farasi, ila jua la asubuhi lililokuwa linachomoza likawakatisha hamu, tena wakiwa wamekaribia kumkamata farasi huyo aliyetupa miguu yake kuvuka mpaka na kuingia ardhi ya Goshen.

Fisi hao waligeuka na kuanza kukimbia kurejea kwenye makazi yao. Kadiri walivyokuwa wanakimbia, na jua lilivyokuwa linachomoza, walikuwa wanageuka kuwa binadamu.
.
.
.
.
MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN!
.
.
.
Lako jicho!
 
Katika karne za enzi zile, zile zamani kabisa, kitu cha thamani kilikuwa ni aidha dhahabu ama silva. Kila himaya ilijivuna kwa wingi wa dhahabu zao, utawala imara na shibe za watu.

Si zaidi ya hapo.

Lakini je, nini kinatokea pale kinapojiri kitu cha thamani zaidi? Ndio. Yani cha thamani kushinda hizo dhahabu, hizo silva, shibe na tawala imara zikiunganishwa zote kwa pamoja?

Kitu cha kuwatoa watu mate. Cha kuwanyima usingizi. Cha kufanya vita baina ya himaya na himaya?

Na ubaya basi kitu hicho kiwe kinamilikiwa na mtu mmoja tu! Na endapo kikikanyaga kwenye kiganja cha mtu mwingine kikamwongoza kunyonya damu za watu, kuwa kubuhu wa ulozi?

Sijamaliza, na hicho kitu kiwepesi akapewa mwanamke kama zawadi. Hajui kuendana nalo. Hajui yaliyomo. Na hata hajui hao waliompatia kama zawadi wamekitoa wapi!

Na kwa wakati huo, akiwa ameshapewa majukumu ya kuongoza himaya kubwa huko Uajemi iitwayo Goshen. Himaya iliyopo kwenye uadui mkubwa na himaya ya Devonship, iongozwayo na dhalimu na mlozi makbuhu aitwaye Jayit mwenye kisasi cha damu na Goshen!

Jayit aliyefukuzwa na kwenda kuiinua himaya yake binafsi isiyokuchwa jua. Jayit mwenye haja ya kuiweka Goshen chini ya miguu yake, hayo akiyatekeleza endapo akirudi Goshen kuteka mifupa ya marehemu babu na bibi yake kaburini!

Nisikuchoshe, niazime muda wako ambao hautauujutia, nikupeleke zama hizo za kutumia jua kama majira na panga kama silaha.

Ni hapa ... hapa... mpaka mwishowe.
Tantaw steve Mollel husna muba Money Talk Gentries Tumosa dumejeuri mTz mweusi @koncho 77 carbamazepine Evarist Massawe kisukari na wengineo mambo ni motoooo [emoji91] [emoji91]
d7f4532f84dccba1d04f30411ecf8c0e.jpg
Nipo mpenzi asante[emoji120][emoji120][emoji120]
 
Bibie kitu hiki kimesimamia kucha nimeona unajua kuvaa viatu vya Baba vizuri na majirani wasijue kuwa Baba hayupo Big up sana mkuu [HASHTAG]#Steve[/HASHTAG] kwa kulea Bibie [HASHTAG]#shunie[/HASHTAG]
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom