SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

*MKUFU WA MALKIA II -- MWISHO*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Mapambano makubwa yakazuka! Ila askari wale wa Venis wangewezaje kupambana na watu wasioonekana?? Ndani ya nusu saa, wakajikuta wote wakiwa wameshauawa! Hakuna hata mmoja aliyebaki anahema.

Napo ndipo Jayit akakoma kucheka. Akakaza uso wake na kumsogelea Venis. Akamuuliza, "ulikuwa unasema??"

ENDELEA

Basi Venis akatazama nyuma yake, hakukuwa kumebakiwa na mtu hata mmoja, lakini hakujita, akajikaza na kumsogelea Jayit, akamwambia anataka kuichukua na kuiweka Goshen mikononi mwake.

Jayit akatabasamu. Akamwambia mwanamke huyo kuwa hana huo uwezo, na kamwe hawezi kumtikisa kwani yeye bado yu mchanga.

"Mimi ni Jayit! Jabali la kwenye miamba. Siwezi kutikiswa na yeyote yule juu ya uso wa dunia. Hata wewe naweza kukumaliza kwa kutumia mkono wangu mmoja tu!"

Venis akang'ata meno kwa hasira! Na mara akaanza kupambana na Jayit, hakuna askari aliyethubutu kuwasogelea maana walipigana katika ulimwengu wao wa tofauti kabisa!

Walipigana kwa ustadi wa ulozi, walipigania hewani pasipo kugusa ardhi. Na wakiwa kwenye pambano hilo, upepo mkali ukazuka, wale askari wote wakalazwa chini, wasione kinachoendelea. Katikati ya Jayit na Venis kulikuwa na kitu kama mduara wenye mwale mkali uliokuwa unawaumiza macho kila walipojaribu kuangaza.

Ila mara, wakamwona Jayit akiwa ametupwa nje ya mwale huo unaong'aa. Akadondoka chini kama mzigo wa kuni, kisha akalalama kwa maumivu na kukohoa mara mbili.

Akatazama mwale wa mwanga angani, mara ukanyauka na Venis akaonekana akiwa amesimama anaelea. Mkononi mwake alikuwa amebebelea moto uunguzao ila yeye usimguse!

Kabla Jayit hajafanya jambo, mara Venis akatupa mikono yake kwenda kwa jeshi la Jayit! Askari mamia wakashikwa na moto kana kwamba wamemiminiwa petroli.

Wakawaka haswa. Wakapiga kelele kali za maumivu wakikimbia huku na huko!

Venis akacheka akielekezea kichwa chake angani. Mikono yake inayowaka moto alikuwa ameitanua kana kwamba ndege anayetaka kupaa.

Alikuwa ana haja ya kucheka. Alimjulia adui yake. Alifanikiwa kujua siri ya kumsumbua Jayit, jabali la mwamba, ya kwamba alikuwa ni mdhaifu awapo mwangani. Jayit ni mtu wa giza, mtu wa kiza. Hawezi kuwa na nguvu zake akiwa mwangani!

Na basi kulitambua hilo, Venis akajizingira na mwanga mkali. Kisha akamshambulia Jayit kwa upanga wake wa kilozi.

Askari wa Jayit wakamezwa na hofu. Waliona sasa wanakwisha. Venis akawatazama tena kisha akawamwagia moto pasipo huruma. Wakaungua mamia kwa mamia. Wakakimbia huku na huko wakilia!

Venis aliporudisha uso wake kumtazama Jayit, akastaajabu hayupo! Akatazama kila pande, Jayit hakuonekana. Basi kwa hofu akaanza kurusha moto kila upande, kushoto na kulia, juu na chini!!

Akaangaza akikunja shingo huku na kule akitoa macho yake yanayotisha!

Sasa akawa amepatikana. Hatimaye akarudi kwenye kiwanja cha kujidai cha Jayit maana mwanaume huyo mlozi alikuwa amefichama akiwa anamtazama, akimvizia kumpa shambulio kali litakalomwacha hoi hajiwezi.

Basi kufumba na kufumbua, mara akahisi mtu nyuma ya mgongo wake. Kabla hajashtuka, akadidimiziwa kisu mgongoni kikatokea tumboni!

Akaachama mdomo na kutoa macho ya kifo. Jayit akamfunika kinywa na kiganja chake kipana kisha akampulizia upepo masikioni kisha akachomoa kisu chake na kumwacha Venis adondoke chini.

Ila bado hakuwa amekufa.

**

"Mke wa mfalme ametoroka!" Askari mmoja alifoka. Lucy akafungua mlango na kuchungulia kwa jicho moja. Koridoni akawaona askari watatu waliobebelea mikuki, walikuwa wanapashana habari za kutoroka kwa Tattiana na mama yake.

"Lazima tuwatafute," askari mmoja akasema akiwa na uso wa woga. "Mfalme hatotuelewa. Atatuua. Hima twende!"

Mara wote watatu wakatokomea wakikimbia upesi. Basi Lucy akafungua mlango zaidi na kutoka. Mkononi mwake alikuwa amebebelea kitabu kile KIKUU. Alikuwa ametoka kukiiba!

Haraka akashika njia kukimbilia chumba chake. Alipokamata kona ya kwanza akakutana na askari. Akasimama haraka, wakatazamana. Askari akatazama mkononi, akaona kitabu kile KIKUU mkononi mwa Lucy.

Kabla hajafanya kitu, Lucy akamuwahi kwa kumpiga ma kitabu kichwani. Askari akadondoka chini kwa kuzirai! Lucy akaendelea kukimbia na mwisho wa siku akaingia chumbani na kujifungia.

Haikuwa ngumu sana kwani askari hawakuwapo wengi kasrini. Waliosaliani kama kumi tu kwa idadi.

Basi haraka, Lucy akafungua kitabu kile KIKUU na kuanza kupekua. Kilikuwa ni kikubwa mno. Hakuna kitabu kikubwa cha kilozi kama hiki. Kutafuta kitu unachokitaka, ilihitaji utulivu mkubwa na muda haswa.

Ila Lucy alikuwa tayari alimradi lengo tu litimie! Lengo la kupata chami ya kumfanya Mfalme ampende. Asisikie wala kuona yeyote zaidi yake tu!


**

"Kazana!" Mama alisema akitazama mbele. Tattiana alikuwa amechoka kukimbia. Miguu inamuuma. Anahisi mwili wake umekuwa mzito kupitiliza!

Walikuwa ndani ya msitu wakikimbia kutafuta himaya nyingine wanusuru nafsi zao. Walikuwa wanafahamu fika kama wakishindwa kutoroka siku hii basi hawatakuja kufanikiwa milele. Hii ndiyo ilikuwa siku pekee. Vita iliyozuka, iliwapa mwanya wa kujivinjari na kutimiza mpango wao kwa wepesi.

Tattiana akasimama akihema kama mbwa. Akashika kiuno chake akipambana kupata hewa.

"Nimechoka!" Akanena kwa tabu. "Nimechoka, mama!"

Mama naye akadaka kiuno chake, alikuwa amechoka mno. Ila hakuwa na budi kuendelea kukimbia. Akamsisitizia mwanae aamke waendelee kukimbia kwani la sivyo, watakutwa hapo na kukamatwa.

Tattiana akashindwa kabisa kuendelea. Aliomba aheme kwanza. Wakangoja kwa sekunde kama ishirini hivi, na mara wakasikia sauti ya kishindo cha watu wakija! Wakashtuka. Walikuwa ni askari wa Jayit. Wale wanaume watatu.

Basi Tattiana na mama yake wakaanza kujikongoja kukimbia. Mwendo wao ulikuwa hafifu maana walichoka sana. Na hawakuwa wanaona vema mule msituni kutokana na kiza.

Kwa hivyo ndani ya muda mfupi tu, wale askari watatu wakawaona.

"Wale kule!"

Wakakimbia kwa kasi na kuwanyaka.

"Mlidhani mnaweza kutoroka kirahisi hivyo?" Askari mmoja akawauliza kwa kebehi. Wakaangua kicheko. Tattiana na mama yake wakalia wakiwaomba wawaachilie, ila askari hawakujali. Wakawaswaga waende mbele!

Wakasonga hatua kumi tu, mara askari mmoja akapigwa na jiwe kubwa la kichwa. Akadondoka chini maiti! Wenzake wakatahamaki na kuangaza.

Huku na huko, huku na huko, mara wakatokea Oragon na Ottoman! Mikononi mwao walikuwa wamebebelea magongo makubwa. Wakawafokea wale askari wa Jayit wawaachilie wanawake hao mateka haraka iwezekanavyo!

Wale askari wakacheka. Mikononi mwao walikuwa wamebebelea jambia ndefu zinazong'aa. Alafu wakina Oragon wamebebelea magongo na kuwatishia. Lilichekesha hili!

"Mtatufanya nini tusipotii amri yenu?" Akauliza askari mmoja.

"Tutawamaliza!" Akajibu Oragon akijikaza.

Basi wale askari wakawavamia wakina Oragon na kuanza kupambana nao. Vijana hao hawakuwa na ujuzi wowote wa sanaa ya mapambano. Pili, hawakuwa na silaha ya kivita, kwa hivyo, Walikuwa wanapigana kwa nasibu. Kwa wazi wasingeweza kufua dafu kwa wale majabali!

Basi baada ya muda mfupi, Oragon akawa amesimikwa jambia ya tumbo. Akapiga kelele kali ya maumivu. Ottoman akawehuka kwa hasira lakini hakuwa na cha kufanya.

Aliambulia kumtwanga askari mmoja gongo la kichwa na kumdondosha chini, ila naye akawahiwa kusimikwa jambia ya kifua. Akadondoka chini akimimina damu pomoni.

Askari pekee aliyebakia, ambaye ndiye alimsimika jambia, akamsogelea na kumtazama kwa kebehi. Akatabasamu.

Ila mara ghafla, akakitwa na jiwe kubwa kichwani. Lile lililomkita mwenzake wa awali. Akadondoka chini na kufa papo!

Alikuwa ni mama Tattiana ndiye aliyemsulubu. Haraka akiongozana na mwanae, wakamfuata Ottoman kumjulia hali.

"Ottoman!" Mama Tattiana akaita. Ottoman akatabasamu. Kaka yake Oragon alikuwa tayari ameshakata kauli.

Ottoman akamtazama Tattiana kwa macho yake yanayofifia. Kisha akasema kwa kinywa chake kinachotema damu.

"Nisamehe, Tattiana."

Tattiana akavuja machozi. Akamshika Ottoman mkono. Ottoman akafariki.

Tattiana akiwa hapo anamtazama Ottoman, mara akabanwa na uchungu wa kujifungua. Akalia kwa maumivu makubwa. Mama yake akajaribu kumtuliza na kumsaidia.

Ndani ya muda mfupi akajifungua kiumbe cha ajabu. Binadamu si, mnyama si.

Akiwa mjawa wa hasira za kisasi, Tattiana akanyaka jambia ya wale askari, kisha akamchoma kifuani yule mwana aliyemzaa, mara mbili pasipo kujiuliza!!

**

Kule uwanja wa vita ...


Puuh!! Venis alidondoka chini kama mzigo, Jayit akanyoosha mikono yake juu, askari wake wakapiga kelele kuu ya ushindi.

Sasa Venis hakuweza kuamka tena. Alikuwa ameshindwa! Alikuwa amechakazwa vya kutosha. Hakuwa na ulozi wowote mwili mwake kumnusuru na kadhia hii.

Upepo ambao Jayit aliupuliza kwenye tundu lake la masikio ulimmaliza na kumgeuza kuwa mtu wa kawaida mbele ya jabali huyo.

Jayit akacheka sana. Akapiga kifua chake konde kwanguvu na kumtazama Venis aliye hoi hajiwezi. Akasema,

"Mimi ni jabali! Jabali wa kiza kikuu. Hakuna anayeweza kupambana nami akatoka na uhai! Kaskazini ya dunia. Kusini ya dunia. Si magharibi wala mashariki! ... hakuna!"

Mara akashtuhwa na sauti ya kike. "yupo wa kupambana nawe!"

Akageuka haraka na kuangaza. Upande wake wa magharibi akamwona Malkia Sandarus akiwa anakuja, anatembea kwa madaha. Pembeni yake walikuwapo Fluffy, Zura, Alk na Seth!

Kichwani Malkia alikuwa amevalia kofia ya Pharao, na kifuani mwake ana mkufu wake amali.

Jayit akatazama vema. Watu hao hawakuwa na jeshi. Na wala mikononi mwao hawakuwa na silaha! Zaidi Malkia alikuwa ameshikilia kamba kumvuta farasi wake.

Basi akacheka. Akauliza, "na wewe ni nani??"

Malkia hakujibu mpaka alipomsogelea karibu. Akamwambia, "Mimi ni Malkia Sandarus. Jinamizi ndotoni mwako. Mtawala wa haki wa Goshen. Nimerudi nyumbani."

"Malkia Sandarus?" Jayit akavuta kumbukumbu. Alah! Akamkumbuka. Akacheka zaidi na kumuuliza, "haujionei huruma kukaa mbele yangu? Jabali wa miamba?"

Malkia akatabasamu. Kisha akatikisa kichwa chake na kusema, "yakupasa wewe ndiye ujionee huruma. Umewachezea wanangu vya kutosha. Sasa mama yao yupo hapa. Kwa usalama wa uhai wako, kimbilia Tanashe kabla sijaruhusu mikono yangu ikutawanye!"

Jayit akaguna kwa dharau. Akatazama kando ya Malkia na kusema,

"Naona umejipanga haswa!"

Askari wake wakaangua kicheko.

Malkia akamwambia, "Basi na kwakuwa umekuwa mkaidi, acha nikufunze!"

Akatanua mikono yake, mara ardhi ikaanza kutikisika. Kufumba na kufumbua, watu wakaanza kutokea chini ya ardhi!

Mamia! ... mamia! ... mamia! ... maelfu! Maelfu!! Maelfu!!

Jayit akaachama kwa kushangaa. Akasema: "jeshi la wafu!!" Hakika akapaliwa na hofu.

Haraka akatekenya ulozi wake na kupotea eneoni mara moja, akaacha jeshi lake likiwa limezingirwa na maelfu ya askari waliokufa miaka nenda rudi huko nyuma!

Jeshi nalo likatwaliwa na woga. Hawakuwahi kuona mifupa ikiwa imesimama. Inaongea. Inatembea. Inabebelea silaha!!

Basi jemedari wao, bwana Phares, akajitutumua, na kuwaamuru washambulie. Loh!! Wakakutana na kitu wasichokitarajia. Kitu ambacho hawakuwahi kukutana nacho kwenye uwanja wowote wa vita!

Utapambanaje na watu wasiokufa?? Hata pale walipopotea kimazingara, askari wa jeshi la wafu nao wakazama ardhini na kutambua nyendo zao. Wakawamaliza!!

Ndani ya muda mfupi maiti zikazagaa na kufunika ardhi. Malkia akatanua mikono yake, na kufumba macho. Mara hao maiti wakaanza kunyanyuka na kujiunga jeshi la wafu!

Wote.


**


Akiwa na uso wenye hofu, alifungua makabati na kila droo. Hakuona kitabu!!

Akashika nywele zake akiwa amewehukwa. Alichanganyikiwa haswa. Kitabu kiko wapi?? Alikihitaji kupambana na jeshi la wafu!

Alikihitaji kupata chami ya kumudu jeshi lile la kutisha! Jeshi la watu wasiokufa!!

Akainamisha mgongo wake atazame uvunguni, hakukiona, alipoamka akakutana uso kwa uso na Malkia!

Pia uso kwa uso na ncha ya jambia iliyomtoboa kifua.

Akapiga kelele za kuugulia. Kama haitoshi, Malkia akachomoa jambia yake upesi kisha akamfyeka kichwa. Mwili wa Jayit ukadondoka chini, kichwa kikimbilia uvunguni!

Basi jua likarejea angani, kukawa kweupe. Mabaki yote ya Jayit yakaungua kwa kushindwa kustahimili mwanga wa jua, hakuna hata chembe ya Devonship iliyobaki! Wote waliungua na kugeuka majivu!

Watu wote wa Goshen wakafunguliwa toka vifungoni. Nao wakambeba Malkia juu wakamzungusha himaya nzima kwa furaha kubwa! Hata wakina Tattiana wakasikia kelele hizo, nao wakajikokota kushuhudia.

Malkia alikuwa amerudi!

Goshen ilikuwa imerudi, hatimaye.
 

Similar Discussions

46 Reactions
Reply
Back
Top Bottom