SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

*MKUFU WA MALKIA II -- 67*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Venim akiwa amekabwa na kifo, hakupata kunena neno. Akabaki ameachama. Anatoa macho. Anakufa!! Venis akambusu paji lake la uso na kumwambia kwa sauti ya chini, "ahsante kwa kila kitu."

Kisha akautia moyo wa Venim mdomoni na kuutafuna.

ENDELEA

Venim akawa historia. Akalala kitandani akiwa ameachiwa tundu kubwa kifuani mwake. Macho yake yamekodoa kwa kutokuamini. Mpaka anakata roho alikuwa anamtazama Venis. Mpenzi wake wa moyo aliyegeuka kuwa muuaji wake!

Basi Venis akatabasamu na kucheka kwa nguvu. Kifuani mwake alikuwa mweupe kwa kujawa na amani. Sasa kazi imebakia moja tu, nayo ni kupambana na Goshen, kisha kuitawala!

Usiku ukawa mrefu sana kwake maana alibanwa na kufikiria namna ya kuikamata himaya ile. Hakutaka kuwaza namna atakavyokuwa na furaha pindi atakapokaa katika kiti kile cha kifalme kwa kuwa haitakuwa na kifani!

Palipokucha, akaitisha jeshi lote uwanjani na kisha akawatangazia mabadiliko. Kuanzia sasa, ni yeye ndiye atakuwa kiongozi mkuu wa falme hiyo, kwa hivyo wamsikize na kumtii.

Jambo hilo likazua zogo kidogo miongoni mwa askari. Ni kivipi linatokea hivyo kwa wepesi? Yu kwapi Venim - jemedari wao?

"Amekufa!" Venis akasema kwa kujiamini. Akatazama jeshi lake lote la mamia ya melfu, alafu akaongezea. "Nimemuua kwa mkono wangu mwenyewe na kisha moyo wake nikautafuna! ... na hivyo ndivyo ndivyo n'tafanya kwa wale wote watakaokaidi!"

Lakini nani atasadiki hayo? Wote walikuwa wanaamini Venim ni bwana wa vita. Simba wa mapambano. Ni kwa namna gani amalizwe kiurahisi hivyo? Tena na mwanamke!!

Basi Venis akacheka sana. Nyuso za watumishi wake zilikuwa zimejawa na mashaka kwa hivyo alitaka kuwaonyesha umwamba wake hadharani. Namna gani alivyokuwa si mtu wa kutiliwa shaka hata doa!

Akasema, "tazama kule!" Akinyooshea mkono wake magharibi ya mbali. Askari wote wakageuza nyuso zao kuangaza. Kwa mbali jua lililokuwa linachipuka lilikuwa linawaziba kutokuona vema, lakini waliona mwili wa binadamu huko.

Na mwili huo ulikuwa unaning'inia kitanzini. Basi Venis akasema, "na yule ndiye shababi wenu mliyekuwa mnamsujudia! Yupo pale nimeshamuua! Je bado hamsadiki na uwezo wangu?"

Bado hawakuamini kama ni Venim yule, mtu mmoja akatumwa akatazame. Upesi akakimbia kwenda huko. Baada ya muda mfupi, akarejea akiwa na uso wa huzuni na mshangao. Akasema, "ndiyo, malkia. Ni bwana wetu yule!"

Askari wakajazwa na hofu. Miongoni mwao kuna ambao hawakutaka kuwa chini ya Venis, basi wakadondosha ngao zao na mmoja akapaza sauti kwa niaba yao.

"Sisi hatuwezi kumtumikia bwana mwingine zaidi ya Venim!" Wakataka kuondoka zao, walikuwa kama kumi kwa idadi. Venis akapaza sauti yake kuu kuwaita. Na mara kwa haraka, akatokea akiwa karibu na wale askari. Akamkaba yule kiongozi wao na kumnyanyua juu kama karatasi!

Basi wale askari wengine tisa, wakataka kumwokoa mwenzao. Wakamtupia Venis mikuki! Ikamtoboa na kutokea upande wa pili, lakini ajabu Venis hakutetereka. Akaendelea kumkaba yule kiongozi wao na punde akakauka kuwa kama gofu!

Venis akamtupia chini kisha wakageukia wale wengine tisa. Walikuwa wamesimama kwa hofu kuu. Wanatetemeka miguu yao yagongana. Mmoja wao akajikaza nafsi na kujitoa mhanga. Haraka akakimbia kumfuata Venis, ila kufumba na kufumbua akajikuta amenyofolewa koo kwa kucha kali, amelala chini akivuja damu lukuki!

Wale wengine nane wakaogopa sana. Hata wakapiga magoti na kusujudu wakisema, "tusamehe ewe malkia. Nasi hatukujua haya. Tumeshasadiki kuwa bwana wetu yupo ndani yako!"

Na basi jeshi zima likapiga magoti na kusujudu mbele ya Venis kuwa kiongozi wao mpya. Wakaapa kumtumikia kwa nguvu na akili zao.

Venis akatabasamu. Akacheka tena na kusema, "inukeni kwani ninyi mmeshakuwa wangu hata sasa!"

Jeshi likainuka na basi Venis akawaambia kuwa kuna kazi ya kufanya mbele yao. Kazi kuu na watakapoikamilisha hiyo atawapatia zawadi ambayo hawatakaa waisahau maishani mwao!

Akaapa kuwafanya bora zaidi. Maisha yao yatakuwa na kheri kuliko ilivyo sasa maana watakula watakacho na kunywa wanachopenda. Maisha yao yatakuwa paradiso tofauti na walivyokuwa watumwa chini ya Venim.

Basi askari wakajawa na shauku kuskiza. Venis akawahabarisha juu ya kazi hiyo, akasema, "Tutakuwa safarini tangu leo kuelekea falme ya binadamu, huko tutakamata kila kilicho chao na kukifanya chetu. Tutakusanya dhahabu na fedha zao zikawe za kwetu. Na pia tutakunywa damu zao asubuhi, mchana na jioni!"

Habari hizo zikawafurahisha askari. Ni muda sasa hawakufanya matukio kama hayo tokea walipokuwa chini ya Venet. Kwao ikawa sherehe, maana walipata uhakika wa kunywa damu za watu kwa wingi wautakao. Kubaka wapendavyo na hata kukejeli binadamu kwa uwezo wao hafifu.

Basi Venis akawataka wakafungashe haraka kila kinachohitajika, na safari ianze. Askari wakatokomea kwenda kwenye makazi yao. Baada ya lisaa limoja wote wakawa tayari wamekusanyika mbele ya kasri ya malkia Venis kumngoja.

Venis akawatazama askari hao na hakika moyoni akapata faraja. Walikuwa wengi vya kutosha. Na walikuwa wana ari. Aliona machoni mwake hakuna askari binadamu atakayeweza kuzuia vikosi vyake. Kwa hivyo himaya inaenda kuwa mikononi mwake!

Akapandisha mkono wake wa kuume juu ukiwa umebebelea jambia. Nao askari wote wakafanya hivyo wakipiga nduru. Wakaimba Malkia! Malkia! Malkia!

Venis akashuka chini na kumkwea farasi wake. Alikuwa wa rangi nyeupe, mwenye uso wa ajabu. Kwenye paji lake la uso alikuwa amechomoza pembe moja ndefu iliyochongoka.

Basi na safari ikaanza. Safari ya kuelekea Goshen.

**

Mama Tattiana aliingia chumbani alimo mwanae, akasema, "Mwanangu, mambo si mepesi hata kidogo!"

Akaketi kitandani alipokuwa amelala mwanaye. Alafu akamtazama akiwa na uso uliopungukiwa subra. Akasema, "nimetazama kila njia na kila kona na kila chochoro, hakuna palipo salama. Hakuna pa kupita mwanangu!"

Macho ya mama yalikuwa mekundu. Alikuwa amepungukiwa na imani ndani yake. Tattiana akamshika mamaye bega na kumwambia, "usijali, mama. Kama hukuona njia leo huko ulipoenda si mwisho wa tumaini letu."

Mama akakunja sura, akasema, "sasa tutapita wapi? Angani? Sisi sio ndege!"

Tattiana akashusha pumzi na akasema, "Hapana. Hivyo ulivyoona haiwezi kuwa hivyo hivyo muda wote. Kuna wakati walinzi hao watakuwa wanapumzika toka kwenye majukumu yao. Inabidi ujue ratiba zao."

Mama akastaajabu. Aliona kazi inakuwa kubwa kuliko alivyowaza lakini mwanae akamtia moyo. Lazima wafanye hivyo, la sivyo watafia hapo.

"Mama," Tattiana akaita. "Kesho lazima uwe mwisho wetu kuwa hapa maana nahisi kabisa keshokutwa naweza nikajifungua. Huku chini pametanuka na hata viungo vyangu sasa havipo kama hapo awali."

Mama akamshika mkono, na kumtazama machoni. Akasema, "nitajitahidi mwanangu ... basi kula kwanza na upumzike, baadae nitaenda tena kutazama."

Mama akamlisha na kuhakikisha mwanaye ameshiba na yupo katika hali nzuri. Yakapita masaa kadhaa, Tattiana akabebwa na usingizi. Alipokuja kufumbua macho, hakumkuta mama yake. Alikuwa tayari keshajiendea.


**

"Simama hapo hapo!" Sauti kali ilitokea nyuma yake. Haraka akasimama akitetemeka miguu. Moyo wake ukaanza kwenda mbio akichanganyikiwa hana la kufanya.

Basi akasikia vishindo vya miguu vinajongea karibu yake, na alipovisikia karibu zaidi vikakoma, na mara sauti nzito ikauliza, "ni nini unafanya hapa mara ya pili sasa nakuona? Je watazama njia ya kutoroka?"

"Ha - hapana!" Mama akanena akikunja uso wake kwa hofu kuu. Aka akasikia ubaridi wa upanga begani mwake alafu akaulizwa:

"Bali?"


**
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom