SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

*MKUFU WA MALKIA II -- 64*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Huko wakawaona vijakazi wengine wawili wa Jayit. Kabla vijakazi hao hawajafungua lango, wakamtazana mama Tattiana kisha wakaongea katika lugha yao ya pekee.

Mama Tattiana akapata hofu nzito. Sasa akajua zamu yake imewadia!!

ENDELEA

Lango likafunguliwa akachomolewa na kubebwa asijue aendako. Alipiga yowe la kilio lakini hakuna aliyemsikiza wa kumjali.

Waliomjali hawakuwa na uwezo wa kumwokoa kwani walikuwa ndani ya jela wakibanwa na malango ya vyuma.

Mama akatolewa mpaka nje, huko akastaajabu kuona bado akipelekwa tu asipopafahamu. Baada ya punde akatambua ni njia ya kwenda kwenye kasri ya mfalme.

Hapo akapatwa na maswali. Ni nini anapelekewa huko?? Je aenda kuuawa ama nini??

Akili yake yote ikawaza pengine anaenda kuuawa aliwe nyama na mfalne yani Jayit. Akafika kasrini na kabla hajazama ndani akapata fursa ya kumwona Phares.

Hapo akakurupuka na kuanza kuita akidhani Phares anaweza kumsaidia. Hakujua Phares hakuwa mkwewe tena. Hakufahamu kuwa Phares amebadilishwa na sada si binadamu!

Akatupwa kitini na kuamriwa aketi hapo pasipo kuhangaika kama kweli anapenda uhai wake. Naye kwa uoga angelifanya nini zaidi ya kutii??

Akitazama huko na huko wanajeshi walikuwa wamejaa. Watu wa ajabu. Watu wa kutisha. Moyoni akaapa kama angelitoka huru mule kasrini basi ataenda kutoa sadaka kwa mungu wake. Sadaka ya mnyama mnono kabisa katika fungu zima.

Ila sadaka hiyo ataitolea wapi na ilhali Jayit kakusanya kila kitu?? Na huo atautoa wapi wakati yu chini ya ulinzi gerezani??

Hakuwaza hayo. Macho yake yalikomea kwenye pumzi yake tu.

Muda si mrefu, akasikia sauti za viatu zikigonga sakafu. Haraka akatazama sauti hiyo inapotokea. Mara akamwona Jayit akiwa anaongozana na Kainus pembeni yake.

Mama akastaajabu. Mwanae alikuwa hai!! Tena mzima wa afya!! Hakuamini macho yake.

Lakini ngoja ...

Mbona macho yake yana umbijani?? Mbona rangi ya ngozi si nyevu tena?? Hakujali! Mwanae alikuwa hai, hilo ndilo la maana haswa.

"Tattiana mwanangu!" Akapayuka akisimama. Alimtazama mwanae machoni na kila jambo kwake akaona kheri.

Ila Kainus hakuwa anamjua mtu huyu! Alistaajabu kumwona hapo na akamtazama Jayit akimuuliza:

"Ni nani huyu??"

"Mimi ni mama yako!!" Mama akapaza sauti. "Tattiana mimi ni mamayo!"

"Mimi si Tattiana!" Kainus akafoka. "Naitwa Kainus ... sawa?"

Mama akaduwaa. Kainus?? Akamtazama Jayit na kumuuliza:

"Nini umemfanyia binti yangu??"

Akafoka kwa hasira. "Umemtendea nini??" Akanyanyuka akamuadhibu Jayit ila akadakwa na kuketishwa kitini kwa nguvu.

"Tulia hapo ama uuawe!" Mlinzi alifoka. Macho yake yalikuwa yanamaanisha anachokisema. Hakuwa na tembe za masikhara hata punje!!

Jayit akamtazama Kainus na kumpa ishara. Kainus akaendea njia ya kushoto na kumpatia faragha Jayit na mama yake Tattiana.

"Nimeambiwa wewe ni mkwe wangu," Jayit akasema akiketi kwenye kiti chake cha kifalme kilichokuwa kimekaa kwa mbali kidogo na mbele ya kile alichokalia mama yake Tattiana.

Akatabasamu.

"Nimefurahi kuonana na wewe."

Ila mama alikuwa anamtazama kwa jicho la hasidi. Hasira zilijionyesha kwenye paji lake la uso.

"Ni nini umemfanyia mwanangu ewe dhalimu??" Akafoka.

"Nimemsaidia," Jayit akasema akipandisha mabega. "Hauna shukrani nimemrudisha kwenye uhai na fahamu zake?"

"Fahamu gani??" Mama akadaka kamba. "Mbona hamtambui mama yake?"

"Ni kwasababu yupo ulimwengu mwingine. Mbali na huu. Huko ambapo hasikii shida wala mateso kama aliyokuwa anayapata awali."

"Nini unataka kwangu?"

"Safi sana!" Jayit akatikisa kichwa. "Hapo ndipo nilikuwa nataka ufike. Nimekuleta hapa kwa lengo moja tu, ukae na mwanao kumwondolea upweke. Wewe ni mtu ambaye naweza nikakuamini kwenye hilo ..

Bado hajazoeana na watu na hana marafiki. Hata waliopo hawataweza kumhudumia kama nitakavyo ufanye wewe."

"Nitakaaje na mtu asiyenitambua??" Mama akauliza.

"Usijali," Jayit akamwondoa shaka. "Hilo niachie mimi, najua cha kufanya. Alimradi tu umtunze vema kwenye hali yake."

"Hali gani hiyo??"

"Mwanao ana ujauzito," Jayit akasema kwa furaha. Lakini kwa mama hii kauli ilikuwa ni kama kisu kikali kilichochoma kifua chake.

Kwa muda kidogo alikosa cha kunena. Alidhani hakusikia, ama pengine alisikia lakini hakikuwa kinamhusu.

"Unasema??" Akauliza apate uhakika.

"Mwanao ana mimba. Kwahiyo anahitaji uangalizi wako."

Swala hili lilikuwa la kustaajabisha. Hata kwa mama halikumuingia akilini. Ni siku mbili tu tangu Jayit aje hapo na kuweka makazi, siku hizo zatosha mtu kuwa na mimba??

"Ana mimba ya nani?" Mama akauliza akitoa jicho. Akawaza pengine itakuwa ya Phares.

"Ana mimba yangu," Jayit akajibu akionyeshea kucha kifuani mwake. "Amebeba mtoto wangu tumboni. Nataka apate kila aina ya matunzo kabla hajajifungua hivi karibuni!"

Hivi ni nini huyu anaongea?? Akajisemea mama kifuani. Hakuwa anamweleza Jayit hata kidogo. Aliwaza pengine atakuwa amerukwa na akili!

Lakini kuna kitu alikuwa amesahau. Jayit hakuwa binadamu wa kawaida kama yeye, wala hakuwa anafanania na kiumbe chochote kile aina ya mamalia, hivyo hilo lingeweza kuwezekana!

Akamjuza mama. Mimba yake itadumu mwezi mmoja tu ndani ya tumbo la Kainus. Kisha atamzalia mtoto wa kiume atakayekaimu nafasi yake.

Kwa muda wote huo wa mwezi, Kainus anatakiwa kula chakula anachokitaka na kwa muda wowote ule anaoutaka.

Kwa ufupi, asiwe na shida yoyote ile. Hata pale atakapohitaji kulishwa basi ifanyike hivyo pasipo maulizo.

Lakini Jayit akatahadhari. Kwa muda wote ambao Mama atakuwa anakaa na mkewe hapo kasrini, atamrejesha mwanamke huyo kwenye hali yake ya ubinadamu. Na usiku au muda wowote akiwa anahitaji kuwa naye basi atarejea kuwa Kainus!

Asifikirie kutoroka hata kidogo kwani hawataweza kufanikiwa hata robo. Haitamchukua pumzi tatu atakuwa keshampata na adhabu yake ikiwa ni kuuawa, kisha kugeuzwa kuwa jini la ardhini!

Maisha yake yawe kama fuku ama fumbatu wa mchangani!

Mama akaogopa mno. Na kwa kumdhihirishia kuwa ana uwezo, Jayit akamteka mama huyo mkono na kuongozana naye mpaka chumbani alalapo na Kainus.

Akaufungua mlango na kumtaka mama aingie ndani. Alipofanya hivyo na kutazama kitandani akastaajabu kumwona Tattiana! Alikuwa mzima wa afya.

Alikuwa ni yule Tattiana anayemjua yeye. Wakafuatana na kukumbatiana kwanguvu na mwanaye. Jayit akaondoka zake akiwaacha peke yao.

Mama akapapasa tumbo la mwanae. Lilikuwa gumu kuonyesha ndaniye muna kitu. Akatahamaki. Kumbe aliyoeleza Jayit yalikuwa yana kweli ndani yake!!

Tattiana akalia sana. Akamwomba mama yake amkomboe lakini hakuwa na uwezo huo. Watakimbilia wapi na wakati Jayit amefumba himaya nzima kwa walinzi wake??

Na wataenda wapi ilhali ana kiumbe cha mlozi huyo tumboni??

**

"Bella!" Lucy aliita baada ya kufungua mlango kwanguvu. Alikuwa ametoka kukimbia kwa kasi kufika hapo.

Akatazama huku na kule, hakumwona mtu chumbani. Akalaani. Akatoka na kwenda huko nje kutafuta. Baada ya muda mfupi akamwona Bella akiwa amesimama kwenye bustani ya maua.

Akatabasamu.

Akaendea huko akikimbia.

"Bella! Bella!" Akaita akihangaika kuvuta pumzi. Bella akatahamaki na kumtazama.

"Ni nini??"

Lucy akacheka kwa taabu kwa kukosa pumzi.

"Tattiana amerudishwa kwenye umbo la binadamu!!"

"Umejuaje??" Bella akamtazama rafiki yake kwa mashaka. Alihisi pengine amechanganyikiwa.

"Nimejuaje?" Akashangaa Lucy. "Nimesikia kwa masikio yangu haya!"

Akacheka tena.

"Sasa ni wakati wa kummaliza. Siwezi nikachezea nafasi hii tena nikaja chelewa."

"Lu--"

"Ah! Ah! Usianze kuniambia mambo yako. Niambie kitu kimoja tu, utanisadia ama lah??"

Kabla Bella hajasema kitu, Lucy akamwambia:

"Tayari nina mpango."


***
 
*MKUFU WA MALKIA II -- 65*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

"Ah! Ah! Usianze kuniambia mambo yako. Niambie kitu kimoja tu, utanisadia ama lah??"

Kabla Bella hajasema kitu, Lucy akamwambia:

"Tayari nina mpango."

ENDELEA

"Upi huo?" Bella akawahi kuuliza.

Lucy asiwe na haraka akamtaka waketi na kumweleza mpango wake huo alioufuma kwa ustadi. Basi wakaketi kama Lucy alivyokuwa anataka.

Wakiwa wana maua mikononi mwao wakawa wanaongea taratibu. Walikuwa peke yao hivyo hawakuwa na haja ya kuogopa. Upepo ulikuwa unapuliza vema, kwa ujumla hali ya hewa ilikuwa shwari.

"Unajua mama yake Tattiana ameletwa kasrini," Lucy akafungua mjadala wake. Bella alikuwa anamsikiliza kwa umakini. "Ameletwa hapo ili amtunze mwanae ambaye ni mjamzito. Lakini kufanikisha hilo, kwakuwa Tattiana hamtambui mama yake akiwa Kainus, basi mwanamke huyo amerejeshwa kwenye hali yake ya binadamu."

Lucy akaweka komo hapo avute pumzi. Akalinyongorota ua alilolishika mkononi alafu akamtazama Bella akisema;

"Pengine mfalme anaweza kudhani nina chuki na Tattiana, hivyo kikitokea kifo chakw cha ghafla akanishuku. Sasa mimi nataka kumtumia mama yake Tattiana kukamlisha hili."

Bella akaguna. Hakungoja hata mwenzake amalizie habari. Akauliza:

"Unadhani mama anaweza kumuua mwanaye??"

Lucy akatikisa kichwa.

"Tatizo lako wewe mdomo wako umeshinda kasi miguu. Tulia nikueleze."

Bella akabinua mdomo wake asiseme jambo. Akaendelea kutega sikio kwa umakini japo alikuwa akitazama maua yaliyopo mkononi mwake.

"Ndio nataka kumuua Tattiana. Lakini nitafanya hivyo nikiacha mikono yangu ibakie safi. Hakuna mtu atakayejua kama nimemuua mimi. Na nitafanya hivyo kwa kumtumia mama yake mwenyewe, baada ya kumpumbaza na chami ya Quidus."

Bella akamtazama Lucy kwa macho ya uhaba wa imani. Na Lucy akilitambua hilo, akamwonyeshea kiganja chake kama ishara ya kutomtaka aongee.

"Ngoja nimalize ... najua utakuwa unajiuliza ni wapi nitatoa chami hiyo ya Quidus. Ila jua nitaipata! Nitatumia kila tone ya akili yangu kuhakikisha nanyofoa karatasi hizo kwenye kitabu kikuu."

Mara Bella akasimama. Alikuwa na uso wa kuparamiwa. Alishikilia gauni lake akamwambia Lucy:

"Sipo tayari!"

Lucy naye akasimama.

"Ni nini shida yako ewe mwanamke??"

"Lucy," Bella akaita. "Hizo nyayo zako za hatari siwezi kuzifuata. Nilikuwa radhi kufanya jitihada zozote alimradi nikusaidie ila si katika kimo hicho!"

Akashika kiuno chake akauliza:

"Unajua ni nini kinampata yoyote yule anayekaribia kitabu kikuu cha ANGA JEUSI LA KALE??"

"Najua kila kitu. Mimi si mjinga!" Lucy akajitetea.

"La!" Bella akatikisa kichwa. "Wewe ni mjinga. Na nishaona njia zako zinanielekeza kombo. Mimi si mjinga kama wewe. Mapenzi yamekupofusha, huoni, yamekuzibua masikio, husikii!"

Alah! Aliposema hayo akaokota maua yake na kwenda zake. Lucy akabaki akimtazama mwenzake huyo akiyoyoma. Hakusema kitu ila moyoni mwake alikuwa anaungua.

Alisaga meno. Macho yalijaa machozi. Uso wake ukawa mwekundu. Ni nani atakayemuelewa??

Akaketi chini akiwaza. Sasa mpango wake haukuwa siri kwani Bella alikuwa amehofia kushiriki. Je kama akiutekeleza, Bella atabaki akifunga kinywa chake?

Ulikuwa ni mpango hatari haswa.

**

Ni nini kitabu hiki kikuu?? Ni kitu gani hiki ambacho kimetetemesha moyo wa Bella na kumtibua kichwa??

Hichi kitabu ni kama bibilia kwa waumini wa kikristo. Ama kurani kwa wale waislamu. Kilikuwa ni kitabu kikuu. Kikuu haswa ndani ya falme ya Devonship!!

Kilikuwa ni kitabu kinachokaliwa na Jayit pekee. Kitabu kikuu cha ulozi ambacho kilipewa jina la ANGA JEUSI LA KALE kwasababu ulozi wake uliotunzwa humo ndani ndiyo ambao unafanya anga lao lawa jeusi miaka nenda rudi!

Kila siku kuna kunakuwa giza. Ambamo ndani ya giza hilo ndipo kuna nguvu ya Jayit na falme yake.

Kitabu hiki ni SIRI. Ni kharamu kwa mtu mwingine kukitia mkononi isipokuwa Jayit peke yake!

Ndani ya hicho kitabu, kuna ulozi wa kila aina. Wa kila namna aitumiayo mfalme huyo. Ni MOYO wake. Yoyote yule atakayekiuka na kukitia mkononi, basi atakutana na adhma itakayomtenda vibaya asisahau maisha yake yote!

Tangu uwapo wake, hakuna hata aliyewaza kukishika ndani ya falme hii.

Isipokuwa sasa huyu mwanamke ... Lucy! Yote kisa mapenzi. Anataka kuchezea moto.

**

Mpaka anaanza kusinzia, hakumwona Lucy yupo wapi. Bella huyu akajiuliza. Akawaza na kuogopa labda ndiyo Lucy ameendea kile kitabu.

Akajikuta moyo wake unamdunda sana. Alistaajabu kwanini Lucy amekuwa mkaidi kiasi hiko.

Alijigeuza kitandani huku na kule akiwaza. Mpaka anapata usingizi hakuwa amepata jibu wala kumwelewa Lucy. Aliona aihifadhi mikono yake badala ya kuitia ndani ya boksi hatari la bahati nasibu.

Akalowea usingizini.

Ikapita muda kidogo, mlango ukafunguliwa taratibu akazama Lucy. Haikujulikana ametokea wapi lakini hakuwa amekosea kufika hapo muda huo. Alikuwa ana mpango kabambe.

Akaketi kitandani na kumtazama Bella. Alikuwa anahema kwanguvu kuonyesha amezama usingizini. Lucy akatoa kifuko kidogo cha ngozi kwenye pindo lake la nguo, kisha akakifungua kwa kuvuta kamba.

Akazamisha vidole vyake ndani ya kifuko akatoka na unga kiasi. Akamtazama tena Bella kwa sekunde kadhaa. Kisha akasema:

"Kwaheri, rafiki."

Akaurushia unga huo usoni mwa Bella mara moja tu. Na mara Bella alipovuta hewa, akaamka na kuanza kukohoa kwanguvu mno akikaba koo lake.

KOH!! - KOH!! - KOH!!

Lucy akamtazama pasipo kujishughulisha. Bella akamtazama Lucy kwa macho ya hasidi ila hakuweza kufanya chochote kile.

Alikuwa anakohoa sana na mwishowe akakakamaa kuwa gogo! Akiwa amenyooshea mkono wake kwa Lucy.

Alikufa akiwa anajua nani aliyemuua.

**

Aliposhusha mzigo wake akatazama kombo na kombo. Hali ilikuwa shwari. Haraka akaanza kufukua ardhi kwa nguvu zake zote.

Huku nyuma ya kasri hakukuwa mahali panapotembelewa mara kwa mara, isipokuwa kwa sababu maalum au kama kuna haja kubwa.

Palikuwa ni mahali mahususi palipotengwa kama sehemu ya kupumzikia mfalme na mkewe, malkia.

Lucy alishaganya utafiti mdogo akaona hiyo ni mahali patakapokuwa salama kwake kuzika mwili wa Bella kisha akaseme mwanamke huyo hakuonekana pindi atakapoulizwa.

Akachimba shimo la wastani. Hakuchukua muda mrefu sana. Akautumbukiza humo mwili wa Bella kisha akaufunika kwa mchanga.

Akakung'uta mikono na kushusha pumzi ndefu. Kazi ilikuwa nzito. Alijipongeza kwa kuimaliza. Akatazama tena kushoto na kulia, hali bado ilikuwa shwari.

Akachomoka hapo kurudi chumbani kwake. Aliwaza leo atakuwa mpweke sana kwa kuwa peke yake ndani ya chumba kikubwa. Ila ni bora akawa hivyo ... ni lazima atekeleze mpango wake.

Bella alishageuka kuwa adui.

Akiwa ameacha kaburi hilo nyuma kwa hatua kadhaa, hata ajasonga sana mbali, mara akasikia sauti ya kiume ikimwamuru asimame!!

Akahisi mwili umepigwa na ganzi! Alisikia mtetemo mkubwa tokea kichwani mpaka miguuni. Moyo ulikita na kuanza kukimbia kwa kasi sana.

"Ni nini umefukia pale??" Sauti ikauliza. Lucy akakosa cha kujibu. Alikosa hata cha kudanganya.

Mara huyo mwanaume aliyemsimamisha akamtaka ageuke na warejee pale alipofukia jambo akaone. Lucy akageuka akiwa na uso wa hofu. Na kumbe mwanaume huyo alikuwa mlinzi wa kasri.

Akamwomba kwa utashi wake wote amwachie huru. Atampatia zawadi kubwa ambayo hataisahau maishani yake yote.

"Hapana!" Akajibu mlinzi. "Twende huko nikaone ulichokifukia."

Sasa Lucy akawaza, afanye nini kumtoka mwanaume huyo? Hakuwa radhi kushindwa mapema yote hiyo.

Aliamini anaweza kummudu mwanaume huyo mlinzi.

Lakini kabla hajafanta jambo, mara akaongezeka mlinzi mwingine hapo wakawa wawili!! Hakujua mlinzi huyu ametokea wapi. Alifika hapo haraka akiwa anataka kujua kinachoendelea na mwenzake akamjuza.

Wote sasa wakamsihi Lucy afukue alichokifukua. Wakamsimamia mpaka mwanamke huyo alipofanya kama alivyoagizwa. Walipoupekua mwili ule wakagundua ni wa Bella.

"Umemuua mwenzako!!" Mlinzi mmoja akafoka. Kisha akatazamana na mwenzake na kuambiana:

"Tumpeleke kwa mfalme!"

Lucy akahisi ameishiwa nguvu.
 
Shunie Malkia Sandarus na jeshi lake mbona wanakawia kufika? Mwambie harakishe bhana kuwahi Goshen mambo kule yameharibika!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom