SEHEMU YA SABINI NA TISA
Samson aliwaza mbali sana alitulia sebuleni akiwa anaitazama runinga iliyokuwa mbele yake, lakini pengine ungemuuliza nini kinaendelea sidhani kama angejibu.
Sasa haya ni maisha gani, mambo gani yasiyoisha, Ina maana Kila mgeni atakayekuja ataambiwa stori zangu huku nikitishwa na kusimangwa? siwezi kulazimisha maisha ya shule tena, huenda familia yetu iliandikiwa umasikini, si ajabu nikawa napoteza muda tu kama mama anavyosema.Samson aliwaza asipate majibu.
Mzee Mgaya alirudi ndani huku akiwasalimia wale wasichana pale nje kwa bashasha na upendo kabisa Kisha akaingia zake ndani chumbani, lakini baada ya dakika kadhaa alitoka huku akimtaka Samson amfuate.
Wakaingia kwenye gari huku wakienda mahali ambapo Sam hakupajua, njia nzima Mzee Mgaya alionekana kama akicheka, huku akitikisa kichwa, lakini Samson hakuuliza wala hawakuongea chochote. Walishuka sehemu fulani ambapo ni makutano ya barabara huku watu wakiwa wengi eneo lile ambapo biashara ndogondogo zilifanyika, walipiga hatua kuelekea kwenye kimgahawa fulani local, wakakaribishwa vizuri sana.
Hivi Samson ulivyotoka shule ulikula kweli au ndiyo mama yako kazidisha gubu tu hadi usiku huu unaingia hakuna lililoendelea, aliuliza mzee Mgaya.
Samson akajibu kuwa hajakula. Msosi wa maana na wa haja uliletwa Samson akaanza kula huku Mzee Mgaya akiwa katulia tu anaongea na kutaniana na Binti fulani pale ndani.
Mzee Mgayaaaaa babaaa ! Na wewe unakujaga humu, acha ubahili Mzee wangu, wewe hapa hata siyo hadhi yako Yaani, pesa uliyokuwa nayo wewe ulitakiwa kwenda kuspend pesa kwenye mahoteli makubwa huko, kizuri zaidi umri wako ni sahihi tofauti na sisi ambao hatujatoboa, mtu una miradi kibao , una mzunguko mzuri wa pesa , usafiri ndiyo ule umepaki pale una shida gani babaaa.
alikuwa ni kijana muuza nyama , ni butcher iliyokaribu na mtaa wa mzee Mgaya hivyo alimfahamu vyema, juu ya kuropoka kote lakini Mzee Mgaya hakujibu aliishia kucheka tu.
Huku mama mwenye mgahawa wake akionesha kachukia kidogo kwa maneno ya yule kijana.
Sasa Mzee juzi wakati yule binti yenu alikuja kuchukua nyama pale, Sasa nimeona kama ana mabadiliko fulani eeeh, hata uso wake haupo sawa kabisa , vipi imekuwaje dah ila wahuni, wahuni siyo watu pamoja na mikwara yako Mzee lakini wamepenya sijui walikuwa wanaruka geti , sijui walifunguliwa, daah mapenzi achana nayo, huwezi kuingilia mapenzi wala kuzuia wanaopendana . aliendelea kuropoka yule kijana lakini hakujibiwa na yeyote japo Samson alipata hofu kidogo kwa kuona jamaa anaweza amsha hasira za Mzee Mgaya. Walimaliza kula Kisha wakatoka na kwenda mbele kidogo huku Mzee Mgaya akiagiza pombe na Samson akipewa soda.
Sidhani kama ni mazingira mazuri sana wewe kuwa hapa haswa ukizingatia wewe ni mwanafunzi, ila siyo kesi ndiyo maana nimekuleta huku siyo mitaa ya nyumbani.
Mwanangu kwanza pole sana kwa yote yanayoendelea kwako, nadhani unatakiwa ujute kwa dhati kabisa kwani yote haya ulishaonywa,
Samson unatakiwa uyapambanie maisha mazuri, yatakupa unavyostahili , utapewa heshima , utakuwa kioo kwenye jamii mzima, mfano pale tulipotoka kula yule muuza nyama amesema kuwa Mimi sistahili kula pale, kwanini aseme vile.
Ni kwasababu anahisi nina pesa.
Na hajadanganya, ninaishi maisha anayotakiwa kuishi binadamu yeyote wala si utajiri bali yoyote .
Namshukuru MUNGU ninaweza kula vizuri, naweza kwenda popote hata kama ni mbali kwa kutumia usafiri wangu, naweza kwenda nchi yoyote ile kwani nazimudu gharama zote,huwa naenda Nje ya nchi mara nyingi kufuata mizigo mbalimbali, kwani si nina uwezo wa kuagiza? Lakini sababu ni nini yote ile huwa ni kuenjoy maisha tu. Naweza kukaa hadi miezi miwili sina cha maana nafanya bali natumia pesa.
Kubwa zaidi nashukuru nimepata heshima kwenye jamii inayonizunguka, Samson mwanangu heshima haiji kwa mtu masikini hata siku moja, Ukiwa mkimya na mwenye hekima na busara lakini ni masikini unaonekana kama mwezi mchanga watu wanajua kuna mahali haupo vizuri, lakini Ukiwa na pesa, utaonekana ni mtu makini na utaitwa una misimamo au huna mambo mengi. Utaitwa kwenye vikao na mikutano hata kama hujui kuongea wala kujieleza.
Lakini pia juu ya uharaka na kuongea kwako hata kama upo vizuri utaishia kuitwa mjuaji tu, hata uanzishe jambo lako hutaitwa mbunifu utaonekana umeiga na kukopi mahali, huku ukibezwa hadharani, ulikutana na waswahili zaidi watakuita chizi tu, Sasa sijajua Samson umechagua maisha yapi.
Hivi uliwahi hata kutamani maisha yangu, kwamba siku moja niwe na vitu kama baba mkubwa, au wewe unaishi tu huku ukivizia Mzee Mgaya na mkewe watalala saa ngapi Ili Mimi ninyate niingie kwa Rahma.
Halafu upate faida gani?
Yale masimango umejisikiaje au ndiyo sikio la kufa mwanangu, Nina watoto watano, mtoto wa tatu shule ilimshinda licha ya kufanya juu chini lakini aliishia kuolewa tu, yupo kijitonyama hapo siyo mbali,
Wasomi wangu ni wawili tu Jose, na yule dada yako uliyemuona, wale hata haya maisha yangu hawayapendi na Mimi siyo mfano kwao kwani wanawaza mbali zaidi , wawe na maisha zaidi ya ninayoishi Mimi baba yao, sasa wewe sijui unawaza nini nwanangu.
Kuhusu mapacha wale bado wapo vizuri wanaangaliwa siwezi kuwatabiri japo maendeleo yao si mabaya kwani wangekuwa na shida tungepokea malalamiko yao siku nyingi. Lakini huwezi kusikia , je wewe una matatizo gani Samson, unajua kuwa jina lako liliuzwa kwa watu Mimi nikapambana kwa hali na Mali huku nikipoteza muda mrefu sana kwaajili ya jambo lako, nikaenda hadi kwa mkuu wa wilaya tukaongea kirafiki kwanza , kabla hajachukua maamuzi yake kama mkuu wa na Rais wa wilaya ile, unadhani ni mtu gani local angesikilizwa na yule bwana? unapaswa ujue kuwa Elimu ni bahari, Elimu ina upana wake , Elimu ni ufunguo wa milango mingi, hata kama huna uhakika wa ajira wewe kuwa nayo tu Elimu,
Naizungumzia Elimu inayohamasishwa hata kwenye vitabu vya Dini.
Samson mwanangu usijidanganye , sisemi kwamba Kila mwenye mafanikio amesoma hapana, ila sisi wengine tusiyojua milango ya mafanikio inafunguliwa na nini, kwanza tunaikimbilia Elimu.
Mzee Mgaya aliongea sana huku pombe ikionesha nayo inachukua nafasi yake. Walilipa bili zao na kupanda kwenye gari huku akiongea mambo mengi na Samson njiani.
Walishuka Kisha Mzee Mgaya akiliacha gari nje kabisa akaingia ndani akawakuta familia nzima wote watatu wapo pale huku kukiwa angalau Kuna amani maana huenda Glory alifanya jambo, si mama Kulwa si Rahma , hakuna aliyekuwa amenuna wote walipiga stori na kufurahi, akawaaga kuwa kwa siku hiyo hayupo pale akaondoka Samson akifunga geti baada ya mzee Mgaya kutokomea .
Samson alirudi kwa wasiwasi huku akiwa anawasoma mmoja mmoja usoni,
Eenhee baba mtu mtarajiwa vipi, naona mlituacha mlienda wapi tena, na mzee wenu anaonekana kalewa, afadhali alivyoondoka, maana huwa nakerwa sana na harufu ya pombe ingawa na Mimi nakunywa.mbona unashangaa kuitwa baba mtu, kwani uongo, hapa tunahesabu miezi tu, naona umefundishwa kinadharia huko ukaamua kufanya practical kabisa. alitania mama Kulwa na kuwafanya watu wote wacheke hata Rahma mwenyewe.
Samson alishangaa furaha ile imetoka wapi, maana mama Kulwa alivuruga watu wote mchana
Samson tafadhali usisahau kunipa mitihani yako, naingia nayo chumbani nataka nijiridhishe vitu fulani huenda ukawa kwenye mipango yangu. Nataka nimsaidie mama yangu maana umemsumbua vya kutosha Sasa utakuwa mikononi mwangu, ila ni baada ya kutambua uwezo wako, kaniletee maana sikai hapa naenda nayo chumbani kwangu, nitalala na wifi yangu Rahma. alitania Glory , Samson akaangalia chini kwa aibu.
Itaendelea...............