Simulizi: Kiu ya talaka

Simulizi: Kiu ya talaka

Daaah yaani hujatoa nafasi ya waheshimiwa kutoa maoni,au mawazo??

Wewe noma sana.
Hamkataliwi kutoa maoni au mawazo naona watu wanasoma kimyakimya tu au sijui haina wafatiliaji
 
Hamkataliwi kutoa maoni au mawazo naona watu wanasoma kimyakimya tu au sijui haina wafatiliaji
Wakati naona simulizi nikashuka chini kwanza nione mtunzi kafika ep ya ngapi ajabu Hadi nagonga namba 79 sikuona maoni ya mtu hata mmoja.

Japo sijasoma ila nimesubscribe nikitulia nasoma yoteee.
 
Hamkataliwi kutoa maoni au mawazo naona watu wanasoma kimyakimya tu au sijui haina wafatiliaji
Umezishusha mfululizo so mimi ni miongoni mwa wanao subiri ikamilike nishuke nayo jumla jumla.
 
Madame shunie endelea hatimae nimefika ilipoishia.

Ila mapenzi yana maajabu ukiyatumia vizuri unafurahi ila ukifanya kinyume unaumia.
 
Wanawake wachache wenye moyo huo . Mgonjwa sometimes pona yake ni faraja tu. Inanikumbusha wastara na marehemu mume wake sajuki
 
SEHEMU YA 72

“Nimekuelewa mke wangu, naomba leo niache nirudie nina imani sitalizungumza tena.”
“Mmh! Haya zungumza,” nilimruhusu.
“Mke wangu lazima nikiri nilichokifanya si ubinaadamu na ulichokionesha siamini kama kuna binadamu wa kawaida anaweza kukifanya. Nataka kukueleza baada ya kukataa kurudi kwako nilichanganyikiwa na kuiona dunia si sehemu yangu sahihi ya kuendelea kuishi.
“Mama yangu na wadogo zangu ni viumbe ambao sitawasahau katika maisha yangu kwa kuweza kuugeuza moyo wangu na kuyafanya niliyoyafanya.

Naamini haikuwa akili yangu ya kawaida kuitelekeza familia yangu eti kwa ajili ya mtoto wa kiume. Kwa waliyonifanyia naapa sitawasamehe na kama leo nitakufa naomba mke wangu unizike sitaki hata waguse maiti yangu.

“Wale ni zaidi ya mashetani, walichonifanyia ndicho kilichonifanya leo niwe katika hali hii. Siamini lazima walitumnia nguvu za giza kunighilibu na kusababisha kuigeuka familia yangu...Mimiii? Hapana..hapana.. lazima kuna mkono wa mtu... yaani niione famila yangu kama kinyesi. Namuomba mwenyezi Mungu anikuhumu kama nilichokifanya zilikuwa akili zangu timamu.

“Najua kiasi gani nilivyokuumiza mke wangu, kama ungekuwa na roho nyepesi ningeweza kuchukua maamuzi mabaya... Naomba maji.”

Mume wangu aliomba maji, baada ya kunywa aliendelea kuzungumza huku machozi yakiweka michirizi kwenye mashavu. Alitulia kama anawaza kitu kisha aliniuliza.
“Muda huu ni saa ngapi?” Niliangalia saa ya mkononi iliyonionesha ni saa kumi na moja na nusu jioni.

“Saa kumi na moja.”
Aligeuka na kufunua mtu ambako kulikuwa na bahasha, alitoa kikaratasi kidogo na kunipa.
“Piga namba hii.”
Niliandika kwenye simu yangu na kupiga.
“Akipokea nipe nizungumze naye.”
“Sawa.”

Baada ya simu kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili na sauti nzito ya kiume, sikupokea nilimpa mume wangu. Aliipokea na kuanza kuzungumza
“Haloo... Swedi mbona unaniangusha?...eeh...sawa.. basi nakusubiri.”

Baada ya kuzungumza maneno yale machache alinirudishia simu yangu.
“Asante, naomba umwite baba na wanangu wote waje ndani.”
Bila kujibu nilitoka nje ya wadi na kuwafuata baba mkwe na wajukuu zake ambao nilirudi nao ndani.
 
SEHEMU YA 73

“Vipi kuna nini?” baba mkwe aliuliza.
“Kawaida tu baba,” mume wangu alijibu.
Mara aliingia bwana mmoja mtanashati aliyekuwa amevaa suti, nilimkumbuka bwana yule alikuwa ni mwana sheria na rafiki ya mume wangu.

“Karibu bwana Swedi.”
“Asante, naona leo matumaini yapo.”
“Siku azilingani.”
“Shikamoo baba, shemeji za siku?”
“Marahaba.”
“Nzuri.”
Baada ya kusalimiana, mume wangu alisema:

“Bwana Swedi nafikiri hatuna muda wa kupoteza tufanye zoezi lile ili uwahi majukumu yako.”
Nilijiuliza zoezi gani linalotakiwa kufanyika muda ule, nilitulia nione mwisho wake.
“Vitu vyote si viko tayari?” Swedi aliuliza.

“Ndiyo,” mume wangu alijibu huku akigeuka na kuchukua bahasha lililokuwa chini ya mto na kumpa.
Baada ya kupitia karatasi zilizokuwa, alimgeukia mume wangu na kusema:
“Nafikiri zoezi lifanyike.”
“Mke wangu, baba,” mume alituita.
Tuliitikia kwa pamoja na kumsikiliza anataka kusema nini.

“Najua hamjui kipi kinatakiwa kufanyika, baada ya kupata nafuu naamini ilikuwa nafasi aliyonipa Mungu ili kuhakikisha mali zangu nazigawa kwa wahusika. Nina imani kila kitu nimeandika kwa akili zangu timamu, unaweza kumpa mke wangu na baba wasome.”

Swedi alitupatia karatasi zilizokuwa zina maelezo ya mume wangu kugawa mali zake, nyumba mbili aliniandikisha mimi na wanaye moja alimuandikisha baba yake. Pia kiwanja kimoja aliniandikisha mimi. Magari matatu aliagiza yauzwe kwa ajili ya kuwasomesha watoto wake na moja ambalo alikuwa amemuazima rafiki yake alimpa baba mkwe.

Baada ya kusoma nilikuwa wa kwanza kuuliza.
“Kwa nini umefanya hivi?”
“Nina sababu yangu, majibu yake utayapata siku chache zijazo.”

“Kwa nini usiniambie leo?”
“Kuwa na subira mke wangu, baba naomba upokee nilichokupa, naheshimu mchango wako katika maisha yangu. Nina imani sasa sitakuwa tena na nguvu za kuweza kutafuta wanangu, nilivyo vigawa ndiyo wanaotakiwa kutazamwa na msimamizi mkubwa ni mama yao.”
“Kwa nini mali zingine hukuacha kwako?” nilimuuliza.

“Naomba swali hili niulize baada ya siku mbili.”
“Mmh! Sawa,” sikuwa na jinsi nilimkubalia.
 
SEHEMU YA 74


Baada ya wote kupitia wosia ule, kila mmoja aliweka sahihi yake pamoja na mume wangu na mwana sheria naye aliweka sahihi yake na kupiga muhuri kisha kila mtu alipewa karatasi yake.

Baada ya zoezi lile mwana sheria aliondoka na kutuacha, tulikaa mpaka jioni huku mume wangu muda mwingi akicheza na wanaye. Kila dakika alimweleza mwanaye mkubwa Jackline.
“Jacky soma mama.”

“Nitasoma baba.”
“Wapende wadogo zako.”
“Nitawapenda baba.”
“Usimtupe mama yako!”
“Ndiyo baba.”

“Mama Jacky sitakusahau katika maisha yangu,” aliniambia kwa sauti ya upole.
“Hata mimi mume wangu,” nilimjibu kwa sauti ya upole.
“Baba nashukuru kwa kunizaa,” mume wangu alisema huku akiushika mkono wa baba yake.

“Nashukuru kulitambua hilo,” baba mkwe naye ajibu huku akiupapasa mkono wa mwanaye.
“Jamani naombeni usichoke kuniombe kwa sababu nina makosa makubwa kwenu na kwa muumba wangu.”

“Tutaendelea kufanya hivyo, nawe unajukumu la kujiombea kwa vile sasa umeweza hata kushika Biblia. Mkumbuke muumba wako na kurudisha shukrani kwake kwa kila alilokufanyia kupigania maisha yako,” baba mkwe alisema.
“Nitafanya hivyo baba,” mume wangu alikubali.

Jioni kabla ya kuondoka mume wangu aliomba tufanye maombi ya pamoja ambayo yaliongozwa na baba mkwe. Baada ya maombi yale tuliagana na mume wangu ambaye alimwita tena mwanaye mkubwa kabla ya kuondoka.
“Abee baba.”

“Naomba usome!”
“Sawa baba.”
Kabla ya kuondoka aliwakumbatia wanaye kisha aliwaachia, nilishtuka kumuona mume wangu akiangua kilio. Nilijua bado ana maumivu ya kuwatenga, lakini tulikuwa tumeyamaliza japokuwa sikuweza kuuzuia uchungu ulio moyoni kwa mtu.

Siku zote tulielezwa kutoa machozi ni sawa na kukamua uchungu moyoni, nilimwacha aukamue.
“Mke wangu Mungu atakulipia,” alisema kwa sauti ya upole.

“Asante.”
“Nendeni kwa salama na Mungu awatangulie.”
“Asante, pia nawe mungu akupe usingizi mzuri na aendeleaa kuonesha uweza wake ili kesho tukija tukute maendeleo makubwa.”

“Amina na dua lenu lipokelewe.”
Kabla ya kuondoka mume wangu aliniita, nilimsogelea na kukumbatiana kwa muda huku kila mtu akiyasikia mapigo ya moyo wa mwenzake.
 
SEHEMU YA 75

Baada ya muda mume wangu alirudia neno la awali.
“Mke wangu Mungu atakulipa amini hilo, kwa ulichonifanyia hata niijaze dunia fedha haitalingana na thamani ya wema wako.”

“Asante mume wangu.”
“Haya, unaweza kwenda, jioni njema Mungu akutangulie,” alisema huku akiniachia na kunishika mabegani, macho ya mume wangu yalikuwa yamejaa machozi na kunifanya na mimi kutokwa machozi.

“Na kwako pia nakupenda sana mume wangu.”
“Hilo lipo wazi, asante kwa upendo wako.” Nilimuachia mume wangu na kutoka huku moyo ukiniuma, nilijitahidi kujizua kulia lakini nilishindwa. Nilitoka huku nimeshika kifuani na kulia kilio cha kwikwi kilichomshtua baba mkwe.

“Vipi mama?”
“Hamha kitu baba.”
“Mbona unalia?”
“Nashindwa kuvumilia, maneno ya mume wangu yataka moyo wa chuma kuyahimili, lakini ipo siku nitafurahi na mume wangu.”

“Mungu atakuongoza kwa hilo.”
Tulikodi gari na kurudi nyumbani. kwa kumpitisha baba mkwe kwake na sisi kurudi kwetu.

Kama kawaida usiku baada ya mambo yote kabla ya kulala niliwakusanya wanangu kumuombea mume wangu. Nilitangulia kwa kumshukuru Mungu kwa muujiza aliokuwa akinifanyia kwa kujibu maombi yangu haraka ambayo aliyadhirisha kwa matendo si kwa maneno.

“Baba Mungu, natanguliza shukrani zangu kwa uweza wako wa ajabu aliouonesha mbele ya macho yangu. Naamini wewe ni kila kitu na kila alichotuahidi wanadamu ndicho ulichotupatia.

“Baba Mungu sitachoka kukuomba endelea kuonesha uweza wako katika ugonjwa wa mume wangu. Asante baba.. Asante Mungu.. Asante kwa kusikiliza maombi yangu.”

Baada ya maombi niliwarudisha watoto chumbani kwao na mimi kurudi kulala. ***
Usiku niliota ndoto kama niliyoota siku za nyuma lakini ya safari ile ilikuwa nusu tofauti ya awali niliyoanzia kituo cha basi ile ilianzia nikiwa na wanangu kwenye kiza kizito, ghafla ulitokea mwanga ambao alirudisha furaha ambayo haikudumu kiza kizidi zaidi ya mwanzo kilitanda tena na kututia hofu mimi na wanangu.

Nilishtuka kitandani na kukaa kitako huku jasho likinitoka, aliwasha feni kunipepea koo nalo lilikuwa limekauka kama mtu alikuwa akinikaba kabali.
 
SEHEMU YA 76

Nilinyanyuka hadi chumba cha wanangu na kuwakuta wote wamelala. Niliwasogelea na kuwatikisa mmojammoja huku nikiwaita kwa majina yao.

Kila mmoja aliitikia lakini bado alikuwa na usingizi mzito kichwani, niliwaacha na kurudi chumbani kwangu. Nilipiga magoti na kumuomba Mungu aniepushe na njozi ambayo niliamini haikuwa nzuri kwa vile iliashiria kunitia hofu.

Baada ya maombi niliingia bafuni kuoga kisha nilirudi kitandani kulala. Nililala vizuri mpaka siku ya pili.

Niliamka alfajiri kama kawaida huku nikishagaa mwili kuwa wa uchungu. Nilikuwa kama nilifanya kazi nzito jinsi nilivyokuwa najisikia kuchoka.

Niliandaa chakula cha mgonjwa, kisha nilitoka kuelekea hospitali. Nililikuwa wa kwanza baba mkwe siku ile nilimuwahi. Niliingia wadini na kumkuta mume wangu bado amelala.

Kwa vile alitakiwa kuamshwa kwa ajili ya usafi na kumpatia uji, nilimuamsha. Alionekana usingizi umemshika sana na kuniomba nimuache alale kidogo.
Nilimbembeleza aamke nimpe uji kwa ajili ya kujiandaa na dozi ya asubuhi.

“Amka mume wangu.”
“Niache nimechoka sana.”
“Hapana mume wangu kunywa hata kikombe kimoja ili upate dawa kisha upumzike.”

“Mmh! Sijui,” mume wangu alisema huku akitaka kukaa kitako lakini alishindwa kunyanyuka na kurudi kitandani.
“Leo una nini mume wangu?” hali ile ilinishtua.

“Hata sijielewi,” alijibu kama mtu anayesikia maumivu makali.
“Hujielewi kivipi mume wangu?”
“Usiku wa leo ulikuwa mgumu sana kwangu, sikuamini kama ningefika asubuhi salama.

Nina imani nimechoka kupigania uhai wangu.”
“Kupigania uhai wako?” mume wangu alinishtuka na kauli ile.

“Ndiyo.”
“Nani alitaka kuchukua uhai wako.”
“Mtoa roho, adhana ya asubuhi ndiyo iliyoniokoa akaniacha na kuondoka.”
Maneno ya mume wangu yalinishtua na kumuona kama amechanganyikiwa kutokana na maneno yake

“Mume wangu itakuwa ni njozi tu hiyo.”
“Wewe utasema hivyo, lakini nashukuru umewahi kuja, baba yupo wapi?”
“Hajafika.”

“Wanangu hawajambo?”
“Wazima wanakusalimu.”
“Kwa nini hukuja nao.”
“Mume wangu ni asubuhi sana pia wanatakiwa kwenda shule.”
“Mmh! Sijui kama watanikuta.
 
SEHEMU YA 77

“Wanangu hawajambo?”
“Wazima wanakusalimu.”
“Kwa nini hukuja nao.”
“Mume wangu ni asubuhi sana pia wanatakiwa kwenda shule.”

“Mmh! Sijui kama watanikuta.”
“Unakwenda wapi?”
“Mmh! Basi nipe huo uji haraka naona moyo unanitetemeka,” mume wangu alizungumza huku akijinyoosha kama mtu aliyechoka sana.

Nilimuandalia uji harakaharaka kwa vile nilikuwa nimeisha upoza niliuweka kwenye kikombe na kuuweka kwenye meza ya pembeni ya kitanda.
Nilichukua beseni la maji nilimuosha uso na kumpigisha mswaki, japokuwa siku ya jana yake alikuwa ameanza kufanya vitu vingi bila msaada.

Baada ya kumsafisha nilimrudisha kitandani ili nikamwage maji nje. Bahati nzuri baba mkwe alikuwa amefika. Alichukua beseni na kwenda kumwaga maji, niliuchukua uji na kukilaza mume wangu kichwa juu ya mapaja yangu na kuanza kumnyesha taratibu.

Mdomo ulikuwa haufunguki vizuri nilichukua kijiko na kuanza kumnywesha. Alikunywa vijiko viwili cha tatu nilishangaa kuona uji ukirudi. Niliufuta uliomwagika na kumnywesha mwingine.

Lakini nao aliulirudisha kitu kilichionifanya nimbembeleze mume wangu.
“Mume wangu kunywa basi upate nguvu.”
“Hebu mama,” baba mke alisema huku akisogea kitandani.

“Nashangaa leo baba Jacky sijui amekuwaje?” Nilisema huku nikimfuta uji pembeni ya mdomo na shingoni, alionekana kama mtu mwenye usingizi mzito sana.
Nilimlaza kitandani na kumpisha baba mkwe, aliyenituma nimfuate daktari haraka.

“Mama mfuate daktari.”
“Sawa baba, kwani kuna nini?”
“Kamwite kwanza daktari.”
Nilikwenda haraka kumfuata daktari ofisini bila kujua nitamwambia tunamuitia nini.
“Vipi mama Kijoki?” Daktari aliniuliza.
“Yaani leo mume wangu hayupo vizuri.”
“Labda usingizi.”

“Hapana twende ukamuone.”
Niliongozana na daktari hadi wadini, aliingia na kwenda moja kwa moja kitandani nami nilikuwa nyuma yake. Baba mkwe alikuwa amesimama pembeni ya kitandani akimuangalia mume wangu aliyeonekana amelala.

Alimpima kwa mkono kisha aliniomba mimi nitoke nje peke yangu.
“Kuna nini?” niliuliza tena.
“Hakuna kitu, toka tu nichukue vipimo.”
 
SEHEMU YA 78

Nilitaka kugoma kwani moyo wangu ulikuwa mzito na kuhisi mwili kama hauna nguvu. Nilitoka hadi nje na kukaa kwa muda lakini roho haikunipa nilirudi ndani na kukuta mume wangu akifunikwa shuka gubigubi.

Nilishtuka na kwenda kwa kasi hadi kitandani na kuwauliza kwa sauti ya juu iliyochanganyikana na mkwaruzo.
“Noo, Mume wangu kafanya nini?” nilifika na kumfunua shuka aliyokuwa amefunikwa na baba mkwe.

Alionekana amelala, niligeuka kuwaangalia wote usoni baba mkwe na daktari. Niligundua kitu usoni kwa baba mkwe alikuwa analia macho yalikuwa yamegeuka rangi na mishipa ya kichwa kumsimama.
“Baba, mume wangu amefanya nini?” nilipiga kelele kali kama nagombana na mtu.

“A..a..,” baba mkwe aliingia kigugumizi.
Nilimgeukia daktari na kumshika koti na kuanza kumtikisa huku nikimuuliza kwa sauti kali na machozi yakinitoka.
“Daktari mume wangu amefanya nini? Amefariki?”

“Tumejitahidi lakini Mungu ndiye mwenye uamuzi wa mwisho.”
“Aah! Mungu umefanya nini, mbona leo hukunifuta machozi kwanini umeniongezea maumivu, umenionjesha furaha yenye maumivu ya muda mrefu.

“Mume wangu...kumbe jana alikuwa ukiwaagana wanao na kumtaka Jacky asome kumbe ulikuwa na siri moyoni.
“Nimekusamehe mume wangu kwa nini umekufa? Eeh! Mungu umefanya nini..aah!” Nilimshika mume wangu kama mtu aliyekuwa hai na kumuuliza maswali.

“Mume wangu kwani ulinificha jana, haya aamka uniambie si uliniahidi kunipa siri baada siku mbili? Kiko wapi kwa nini umenificha, nimekukosea nini?” Kuchanganyikiwa kubaya, niliulalia mwili wa mume wangu na kujikuta nikipoteza fahamu. ***

Niliposhtuka nilijikuta nimelazwa kitandani nikiongezwa maji, nilipokumbuka kifo cha mume wangu nilianza kilio upya. Hakuna aliyeweza kuninyamazisha mpaka alipokuja dada ambaye alinikemea.
“Wee, Eliza kufuru gani unayoifanya?”
“Dada kwa nini Mungu kwa hili amekataa maombi yangu?”

“Kwani Kuumbaji na mauti yameisha?”
“Hapana dada, inauma jana nilifurahi na mume wangu wa watoto wetu, kumbe Mungu alikuwa na siri nzito. Wanangu wameupata uyatima bila kutegemea, Mungu yupo atanilipia kwa wote waliosababisha wanangu wawe yatima.”
 
SEHEMU YA 79

Dada alinikanya kwa maneno yangu makali juu ya kufiri ninayotaka Mungu anifafanyie kwa matakwa yangu.
“Dada, wameniulia mume wangu,” niliendelea kulia kwa uchungu niliwa nimeishiwa nguvu.

“Kazi ya Mungu, tunatakiwa kushukuru tunapopewa vilevile tunapochukuliwa vinavyo vipenda.”

“Dadaa! Mama mkwe na wifi zangu sitawasamehe kamwe. Wametumia ushirikina kiisambalatisha ndoa yangu. Wamefanikiwa... Wamefanikiwa.”
Presha ilipanda tena na kusababisha nidungwe sindano ya usingizi.

Nilishtuka siku ya pili na kutolewa hospitali dada alifanya kazi ya ziada kunituliza kwani kila nilipomkumbuka mume wangu niliangua kilio. Japokuwa kifo ni haki ya kila kiumbe kwangu niliamini mume wangu muda wake ulikuwa bado bali amewahishwa na mama mkwe na wifi zangu.

Namshukuru Mungu kwa kunijaza moyo wa uvumivu kwa kuweza kumzika mume wangu. Huwezi kuamini siku za mwisho wa maisha mume wangu mapenzi yangu yalikuwa yamezidi maradufu hasa baada ya kugundua kosa lake na kuwajua wabaya wangu.

Nilimzika mume wangu katika wakati mgumu wakati wa kuuaga mwili wake nilizimia mara mbili. Lakini bado Mungu alinipa nguvu na kuweza kumzika mume wangu baba Jacky katika nyumba ya milele.

Niliamini kwa matukioa niliyopitia mpaka mauti ya mume wangu angechukua muda kutoka katika akili yangu.
Huwezi kuamini mama mkwe na wifi zangu hawakuhudhulia msiba wa mume wangu ambayo baba mkwe alinipa nimzike mwenyewe.

Kwangu lilikuwa kovu lisilofutika katika maisha yangu yaliyobaki duniani. Inawezekana ukajiuliza kwa nini nimlilie na kuumia kiasi kile kutokana na aliyonitendea pia kwa vile maisha yangu niliweza kuyaendesha mwenyewe kwa kipindi kirefu nilipokuwa mbali na mume wangu.

Siri niliijua mwenyewe kutokana na kukijua kilichofuta ndoto yangu ya kuishi maisha kama ya dada yangu ambaye anazeeka na mume wake.

Mwanzo ya ndoa yangu nilimpenda sana mume wangu na kumuona yeye ni kila kitu kwangu. Hata baada ya kugeuka bado sikukata tamaa japokuwa niliumia sana kwa kuamini Mungu ni muweza angemrudisha kundini.
 
SEHEMU YA 80:


Katika ugonjwa wa mume wangu mapenzi yangu yaliongezeka mara dufu lakini kumbe Mungu naye alikuwa na siri yake.
Nitaendelea kumshukuru Mungu siku zote za maisha yangu kwa kuweza kumuuguza mume wangu na kufia mikononi mwangu kuonesha jinsi gani ndoa yetu aliifunga yeye ila ilipita mikono ya wanadamu.

Wanangu walibaki yatima kwa kumpoteza kipenzi baba yao ambao hawakupata mapenzi yake hasa mwanangu Jeska ambaye niliondoka naye mdogo na baba yake amefariki akiwa hana akili ya kujua kinachoendelea tofauti na wenzake.

Sikuchoka kumshukuru Mungu kunipa nguvu kama aliyonipa wakati wa matatizo na kuweza kuwalea wanangu. Niliamini mwanzo ulikuwa ugomvi ambao niliamini ipo siku utaisha lakini kifo hakina rufaa zaidi ya kumuombea apate mapokezi mema.

Baba Mkwe alisimamia vizuri mirathi na kugawa kama alivyoelekeza marehemu mume wangu. Sehemu ya fedha nilizouza magari nilimjengea kaburi mume wangu.
Kipindi cha mwanzo baada ya kumzika mume wangu ndoto za mara kwa mara za kumkumbuka zilinipa shida, lakini namshukuru Mungu alinitia nguvu na kuweza kumkumbuka mume wangu bila mapigo ya moyo kwenda mbio au kumwaga machozi.

Nilijipanga kuwasomesha wanangu huku nikiimalisha biashara zangu kwa kuamini sikuwa na kimbilio jingine la wanangu bali mimi mwenyewe.

Walitokea watu waliotaka kunioa, sikuwa tayari kwa vile nilihitaji muda zaidi wa kupumzisha akili yangu. Siku zote kila lenye mwanzo lina mwisho, baada ya kukaa kwa miaka mitatu nikiwa peke yangu. Nilikubali kuolewa na bwana mmoja mtu mzima ambaye alikuwa tayari kuilea familia yangu kwa vile naye wakati huo hakuwa na mke aliyefariki miaka mitano iliyopita.

Niliolewa na Bwana Ezekiel Lukuba na kuwa mke wake wa ndoa. Narudia kusema hili si kujipendekeza kwa Mungu bali ukweli wa moyo wangu. Namshukuru Mungu kwani amekuwa msimamizi na kiongozi mwema wa njia pale nilipokosa macho ya kuona na kuwa mfariji wa msukosuko wa moyo wangu.

Kilio changu kilipata jibu alinipatia bwana bora mwenye mapenzi ya dhati nami na kuwapenda watoto wangu kama wake.
 
sehemu ya 81

Nilimkuta na watoto wakubwa wawili wa kike.
Japokuwa nilikuwa sijawazidi sana, lakini waliniheshimu kama mama yao mzazi. Kwa tabia ile wa watoto wake niliamini mume niliyempata ni baba mwema.

Maisha yalikuwa mazuri japokuwa nilipenda maisha yale ningekuwa nikiishi na marehemu mume wangu. Mume wangu alinipa uhuru wa kufanya shughuli zangu bila mipaka.

Nilijikuta nikipata ujauzito ambayo uliongeza mapenzi kwa mume wangu. Niliamini naye alikuwa na hamu ya mtoto wa kiume. Japokuwa sikutakiwa kumpangia Mungu, lakini alituelekeza tumuombe yeye shida zetu, nilimuomba anipatie mtoto wa kiume. Muda ulipofika nilijifungua salama mtoto mwingine wa kike.

Pamoja na furaha ya kupata mtoto lakini moyo wangu uliingia unyonge kukosa mtoto wa kiume japokuwa mtoto ni mtoto lakini wa kike tayari alikuwa amenipa hata mume wangu niliamini alikuwa na hamu ya mtoto wa kiume.

Lakini maisha yaliendelea huku mapenzi ya mume wangu kwa wanangu yakiwa makubwa sana. Kila nilipomuangalia mume wangu akicheza na wanangu, badala ya kufurahi nilitokwa na machozi kwa kumkumbuka mume wangu hasa siku ya mwisho alipokuwa akicheza na wanawe hospitali.

Lakini kwa upande mwingine Mungu alisikiliza kilio changu na kunipatia mume mwema ambaye alikuwa mtu mzima mwenye kujua thamani ya mke ni nini. Mwanangu ambaye nilijua ndio wa mwisho nilimpa jila la Marylinda, naye alikuwa vizuri na kuendelea kufurahia maisha.
 
SEHEMU YA MWISHO:

Ndugu zanguni baada ya kupoteza muda wenu kufuatilia simulizi yangu ambayo nina imani kuna kitu mmepata. Mazuri yachukueni udhaifu wako uacheni kwa vile tunajifunza kutokana na makosa ya wenzetu.

Basi hapa ndipa ndiyo namalizia mkasa wangu Mungu awalipe kwa kupoteza muda wenu kusoma mkasa huu. Namalizia kwa kuowaomba wazazi wote hasa wa kike na watoto wao wa kike wajiepushe kuingilia ndoa za watoto wao au kaka zao.

Kila mtu ana haki ya kuiongoza nyumba yake mzazi au wifi ni mshauri na si mwenye mamlaka bali wana ndoa wenyewe. Tujiepeshe kuwa chanzo cha migogoro ya familia za wenzetu.

Mwisho kabisa nataka niseme, mtoto ni zawadi toka kwa Mungu, kwa vile mtoto ni mtoto awe wa kiume au wa kike. Mtoto yeyote anaweza kuwa mrithi wa mali za wazazi kwa vile wapo viongozi wa kike mwenye madaraka makubwa dunia na wameongoza vyema.

Kumbagua mtoto wa kike ni sawa na kuingilia kazi ya Mungu na kuona alimuumba mwanamke kimakosa. Napenda kusema nawapenda wote, namuomba mwenyezi Mungu awatangulie kwa kila jambo pia msichoke kumuomba yeye kwa vile ni kila kitu kwetu, asanteni sana.

Ni mimi, Eliza Elias.
Mwisho.
 
Ahsante Shunie japo mwisho nmetoa machozi
 
Kuna somo hapa nimejiongezea maarifa asante shunie
 
Aaaiseeee. Natamani kujua upande wa pili pale mtu anapokuwa amefariki roho inapotengana na mwili huwa anajisikiaje anafanya Nini au anaenda wapi plus kuona na kusikia nini,. Je wanaomlilia anawaona? Wanaomzika anawaona, au roho inazikwa na mwili?

Mnisaidie kumtag mchawi wa jf mshana Jr tafadhari.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom