SEHEMU YA 50
“Kumbe ilikuwa wazi mimi sitakiwi katika familia ya mume wangu, likatafuta la kutafuta na kufanikiwa kunitoa ndani."
"Hapana mwanangu bado hujatolewa ndani," nilimshangaa baba mkwe kukataa kuwa sijatolewa ndani.
“Baba imepita miaka mingapi leo ndiyo uje uhoji, kama kweli ulikuwa hujui kilichoendelea, uliwahi kuja kuhoji kilichoendelea?” nilimuuliza huku nikimkazia macho.
“Pamoja na hayo, bado mama ulitakiwa kurudi kwangu kama kuna kitu kimekwenda tofauti na maagizo yangu.”
"Kwa wewe mzazi wangu utasema hivyo, hebu fikiria toka siku ile ulipomuamuru mume wangu amtoe ndani yule mwanamke wake mpaka leo hii sijamtia machoni. Kweli mimi ni mke wake wa ndoa au anakuheshimu wewe mzazi wake?
“Baba, mama mkwe wifi zangu na mume wangu hawanipendi hivyo siwezi kuishi kwa shinikizo lako. Je, ukifa nani atakuwa mtetezi wangu, baba akumulikae mchana usiku atakuchoma."
"Ni kweli mwanangu, lakini mumeo amelipata funzo sidhani atarudia upuuzi wake."
"Baba siwezi kuwa Punda wa Dobi kamwe."
"Mwanangu ile ni hadithi tu," majibu ya baba ilionesha aliijua hadithi ya zamani kisa cha punda wa dobi.
"Lakini iliyotolewa makususi kwetu wanadamu, wamenikosa mara mbili ya tatu ni mauti yangu siwezi kuyakimbilia mauti nayaona mbele ya macho yangu."
"Hapana mwanangu huu mguu ni wa mumeo anaomba umsamehe na kuyasahau yote ili muwalee wenenu."
"Baba nakuapia maisha ya ndoa mimi tena basi, kurudi kwa mume wangu au kwenye familia yako siwezi labda maiti yangu. Lakini nikiwa mzima navuta pumzi katu abadani." nilisimamia msimamo wangu.
"Hapana mama mrudie bwana Mungu wako, msamehe mumeo amefanya makosa kama mwanadamu wala si malaika."
"Ni kweli, lakini sitarudi kwa mume wangu siwezi kuwa Punda wa Dobi mwambie amfaute mwanamke mwingine amuoe. Mwisho kabisa baba sipendi kuongea sana kwa vile nachubua madonda yaliyoanza kupona.
“Nakuheshimu sana mzazi wangu naomba tuishie hapa naogopa kuropoka maneno mazito ambayo lazima nitakuvunjia heshima.
“Sitaki mzazi wangu nikuvunjie heshima, katika watu duniani ninao waheshimu na sitawasahau na kuwaona ni kiumbe wa kipekee waliojaliwa na Mungu, wewe ni mmoja wao.