Simulizi: Kiu ya talaka

Simulizi: Kiu ya talaka

SEHEMU YA 55

Wakati najiandaa kutoka baada ya kumuachia maagizo msichana wangu, moyo ulishtuka kumuona shoga yangu ambaye mara nyingi huja na habari za kushtusha.

Pamoja na kuwa tayari nimeachana na mume wangu kidunia japokuwa kwa Mungu ndoa yetu bado ilikuwa ikitambulika. Lakini sikupenda kusikia habari mbaya za mzazi mwenzangu.
Nilipomuona nilimkaribisha.

“Karibu shoga.”
“Asante.”
“Za siku? Umepotea!”
“Mambo mengi, nilikuwa nalima kijijini, si unajua maisha ya mjini bila mihangaiko unaweza kuwa malaya bure.”

“Lakini kijijini kumekupendeza, umekuja lini?”
“Wiki sasa.”
“Mmhu, una jipya gani? Maana kila nikikuona moyo unapaa.”

“Ni kweli, kuna vitu unaweza kuvikalia kimya lakini vingine huwezi, wacha niitwe mbeya lakini ukweli utabaki palepale.”
Mmh! Kauli ile ilinitisha na kujiuliza kuna kitu gani tena ambacho kimemfanya afunge safari kuja kwangu.

“Kuna nini tena shoga yangu?” moyo uliingia woga.
“Shoga inasikitisha na kuuma, sijui ni laana yako na wanao au ya baba yake?”
“Kwa nini unasema hivyo kwani kuna kitu gani tena kimemtokea mume wangu?”
“Yote iliyopita ilikuwa trela sasa ndiyo picha kamili.”

“He! Nini tena?” nilijikuta nikishtuka na mapigo ya moyo kunienda mbio na kujikuta nimeshindwa kusimama na kukaa kwenye kiti kirefu.

“Una muda gani hujaonana na mzazi mwenzio?”
“Kitambo kidogo!”
“Kama nilivyo kueleza nilikuwa sipo, nimerudi wiki jana, siku ya pili toka nirudi nilimuona mzazi mwenzio baba Jacky, kama una moyo mdogo lazima ulie.”

“Mungu wangu kafanya nini tena?”
“Inasemekana mumeo kaukwaa.”
“Mungu wangu nisaidie mja wako! Una maanisha nini?” nilishika kifua kwa hofu.
“Inasemeka yule mwanamke aliyekutoa ndani alikuwa mwingi wa habari.

Baada ya kuachana na mzazi mwenzio zilipatikana taarifa kuwa ni muathirika, taarifa zile ziliifikia familia ya mumeo.
“Walimweleza kaka yao ambaye wakati huo alikuwa amechanganyikiwa baada ya wewe kumtolea nje.

Alikuwa hajijali alivaa nguo bila kufua wala kuoga, “Mama na wifi zako aliwaona maadui wakubwa walioharibu nyumba yake na maisha yake. Hakutaka kuwaona wala kuzungumza nao kabisa hata kwenye mazishi yake aliwapiga marufuku wasifike.”
 
SEHEMU YA 56

“Mmh!” niliguna huku nikihisi moyo kutetemeka kama unataka kutoka sehemu yake lakini nilijikaza.
“Mzazi mwenzio baada ya kupewa taarifa zile alikwenda kupima na majibu yalionesha naye ameathirika.”
“Mtume roho yangu!” nilitoa sauti ya mshtuko.

“Inasemekana tokea siku hiyo mzazi mwenzio yeye na pombe, pombe na yeye. Mwezi uliopita kwa mujibu ya watu wanaofahamu ishu nzima alianza kukohoa kutokana na kutumia pombe bila kula.

“Sasa hivi amekwisha anasema anasubiri mauti yake, ila aliye kwenda leo nyumbani kwake kamkuta amelala chini akiwa amepoteza fahamu pembeni yake imekutwa damu nyingi sana.”

“Mungu wangu! Mume wangu baba Jacky,” nilijisahau kama nipo dukani na kuanza kulia.
“Dada kuna nini?” msichana wangu aliniuliza.

“Baba Jacky,” nilimjibu kwa mkato.
“Amefanya nini? Amekufa?”
“Hapana, anaumwa,” alijibu shoga yangu.
“Dada usilie muombee kwa Mungu,” alinipa ushauri.

“Sasa yupo wapi?”nilimuuliza shoga yangu kwa sauti ya kilio huku nikifuta machozi kwa kitambaa.

“Nimeacha anakimbizwa hospitali.”
“Na familia yake?”
Aliyetoka ni baba yake tu, lakini mama yake na dada zake hakuna aliyenyanyua mguu kwa vile anajua ndiyo adui zake namba moja.”

“Kapelekwa hospital gani?”
“Ya Mkoa.”
Nilifungua droo na kuchukua fedha bila kujua ni kiasi gani na kuziweka kwenye mkoba kisha nilimweleza shoga yangu tuongozane wote. Tulitoka hadi barabarani na kukodi gari mpaka hospitali.

Nilipofika niliingia ndani ya hospitali kwa mwendo wa kukimbia. Japokuwa haukuwa muda wa kutazama wagonjwa, lakini sikuliangalia hilo. Mbele yangu nilikutana na muuguzi na kumuuliza.

“Eti dada mgonjwa wangu yupo wodi gani?” nilimuuliza kama anamjua mgonjwa wangu.
“Mgonjwa wako nani?”
“Kijoki.”

“Ameletwa lini?”
“Leo.”
“Mmh! Kwa kweli sijui kaulize ofisini.”
Nilichepua mwendo hadi ofisini na kuuliza, waliangalia kwenye kitabu na kuniuliza.

“Ameletwa saa ngapi?”
“Eti ameletwa saa ngapi?” nilimgeukia shoga yangu kumuuliza.

“Muda wa asubuhi,” shoga alijibu.
“Alikuwa na tatizo gani?” “Amekutwa amepoteza fahamu huku akiwa ametokwa na damu nyingi mdomoni.”

“Aah! Yule kapelekwa hospitali ya rufaa.”
“Ina maana hali yake ni mbaya sana?” niliuiliza.
 
SEHEMU YA 57

“Ni kweli, lakini Mungu atamsaidia atapona,” muuguzi mmoja alinipa moyo.
Niliondoka na shoga yangu hadi nje ya hospitali na kukodi teksi iliyokuwa imemleta mtu. Tulikwenda hadi hospitali ya rufaa na kuingia ndani.

Bahati nzuri ulikuwa muda wa kuona wagonjwa.
Kwa vile tulikuwa hatujui kapelekwa wadi gani, niliteremka hadi mapokezi na kuulizia jina la mume wangu. Baada ya kuangalia kwenye daftari la wagonjwa alinieleza.

“Wadi namba saba.”
Nilikwenda kwa kasi hadi wadi namba sana, nikiwa naelekea ofisini kuulizia, kwa mbali nilimuona baba mkwe akiwa ameshika mikono nyuma huku ameinamisha kichwa na kutembea hatua kwenda mbele baada ya hatua tano aligeuka na kurudi alipotoka.

Hali ile ilinionesha mambo ni mabaya kutokana na baba mkwe kuonekana amechanganyikiwa. Mpaka nafika mbele yake hakuwa na habari.
“Baba,” nilimwita.
“Na..naam.”
“Vipi baba?” nilimuuliza huku nikizizuia pimzi zangu zilizojaa kifuani.
“Mmh! Bado.”

Baba mkwe aliachana na mimi na kumfuata daktari aliyetoka ndani ya wadi. Nami nilimfuata nyuma ili kutaka kujua anamuuliza nini.
“Baba vipi mgonjwa wangu?”
“Mzee endelea kumuomba Mungu.”

“Anaendeleaje?”
“Ni mapema kusema chochote, lakini tunajitahidi kadiri ya uwezo wetu.”
“Eti kaka mume wangu anaumwa nini?”
“Dada mbona unachekesha mpaka mumeo anafika katika hali hii hujui anaumwa nini?” daktari alinishangaa.

“Hatupo pamoja muda mrefu.”
“Fanyeni subira kila kitu kitajulikana ila zidisheni maombi.”

“Tunaweza kumuona?” niliuliza.
“Nitawajulisha, naomba niendelee na majukumu mengine,” daktari alituomba aondoke.
“Sawa baba.”
Baada ya kuondoka nilimgeukia baba mkwe.

“Baba vipi hali ya mume wangu?”
“Bado mbaya, mmh! Sijui.”
“Hujui nini baba?” kauli yake ilinishtua.
“Tumuachie Mungu,” baba mkwe alisema huku akifuta machozi.

Machozi ya baba mkwe yalikuwa kama kisu butu moyoni kwangu kilichoupasua bila ganzi. Niliamini mpaka mzee mzima amedondosha chozi hali ya mume wangu ilikuwa mbaya sana.

Bila kujielewa machozi yalinitoka. Chumba alichotoka daktari kilikuwa kimeandikwa Chumba wa wagonjwa mahututi ‘ICU’. Nilisogea pembeni na kukaa chini baada ya miguu kupoteza uwezo wa kuendelea kusimama.
 
SEHEMU YA 58

Kila alivyomfikiria mume wangu na yote tuliyopitia na kilichomkuta moyo uliniuma sana. Niliyahamishia mawazo kwa wanangu na kuwaona wakiishi bila ya baba ambaye hakuiona thamani yake japokuwa mwishoni alitaka kujirudi baada ya pigo mujarabu la kuumbuka mchana kweupe.

Japokuwa niliamini huenda ni malipo ya kile alichokifanya, lakini sikutaka Mungu amchukue kwa vile niliamini wanangu bado wanahitaji malezi ya baba yao.

Niliuona uyatima ukiwanyemelea wanangu, kufika hapo nilijikuta nikiangua kilio cha kwikwi huku moyo ukielendelea kuniuma baada ya kuona mume wangu amechuma janga ambalo si kwao hata nami lilinigusa.

Shoga yangu alinifuata na kunibembeleza.
“Mama Jacky huu si muda wa kulia bali kuelekeza maombi yetu kwa Mungu ampe nafuu mgonjwa.”
“Najitahidi lakini moyo unaniuma, maskini wanangu ndo wanabakia yatima,” nililia kwa uchungu.

“Hapana mama Jacky usiseme hivyo, baba Jacky hajafa bali unaumwa.”
“Nitajitahidi lakini roho inaniua sana, kama mume wangu atakufa, mama mkwe na wifi zangu Mungu atawalaani.”
Baada ya muda daktari alitoka wadini na kusogea kwa baba mkwe. Nami nilijitahidi na kunyanyuka hadi pale, nilimsikia akisema:

“Jamani mnaweza kuingia mmojammoja kumuona mgonjwa lakini hali yake bado.”
Kwa vile chumba cha wagonjwa mahututi alitakiwakuingia mtu mmoja mmoja. Alitangulia baba mkwe kumtazama mume wangu. Alikaa kwa dakika kumi kisha alitoka akiwa anafuta machozi.

Japokuwa hali yangu haikuwa nzuri baada ya kuhisi presha ipo juu, nilisogea mlangoni na kuvua viatu kisha nilivaa ndala zilizokuwa mlangoni kwa ajili ya watu wanaokwenda kuangalia wagonjwa.

Niliingia hadi ndani cha chumba ambacho kilikuwa kikitisha asilimia kubwa ya wagonjwa walikuwa akitumia mashine ya kupumulia. Mume wangu alikuwa amelala kitandani akiwa ametulia huku macho yake yakionesha kutulia.

Hakuwa tofauti na maiti, nilijikuta nikiingiwa na wasiwasi huenda amekwisha kufa. Mashine iliyokuwa pembeni yake ilikuwa ikiendelea kufanya kazi.

Mwili wa mume wangu ulikuwa umepukutika, alibakia mifupa na ngozi. Nilijiuliza kilichomfanya awe vile ni hayo maambukizi au pombe na kuacha kula.
Nilipiga magoti pembeni ya kitanda na kusali kwa sauti ya chini.
 
SEHEMU YA 59

“Baba Mungu wewe ndiye muweza wa yote hakuna kinachoshindikana kwako. Lililokosa ufumbuzi kwa wanadamu wewe kwako ni jepesi, basi baba Mungu ‘zihirisha’ uweza wako kwa mume wangu.
Kama ni kipigo kinatosha, yaweza kuwa ni sehemu ya kilio changu ndicho kilichochangia hali hii.

“Baba umetufundisha kusamehe japokuwa hujisahau kwa kiburi cha kibinadamu kwa kushindwa kuzuia hasira zetu. Baba Mungu namsamehe mume wangu kwa niaba yangu na wanangu.

“Naufungua moyo wangu ili iwe sehemu yako baba Mungu kumshika kwenye ugonjwa na maumivu ili ajue muweza wa yote ni wewe peke yako muumba mbingu na ardhi.

“Ametufundisha tuhamishie vilio vyetu kwako kwa vile wewe ni mfariji kwa wenye mateso mazito.

Kwa vile wewe ni msikivu na mtendaji naimani utakisikia kilio changu na kutenda muujiza mwingine kama ulioitenda wakati wa kutafuta mtoto. Sikutumia hirizi wala miti shamba bali ulijidhihilisha kwa wanadamu kuwa unaweza kutenda.

“Baba Mungu mponye mume wangu maradhi, rudisha furaha ya wanangu ambao wameegemea nguzo mbovu ya uyatima ambayo inaweza kuanguka wakati wowote.

Lakini kwa uweza wako mume wangu atanyanyuka kitandani na kurudi kama zamani.
Asante Mungu, asante Yesu uliyehai unayetenda na kuendelea kutenda miujiza.”

Nilimaliza maombi yangu huku macho yakiwa hayaoni kutokana na kufunikwa na machozi. Nilichukua mtandio na kufuta machozi na kunyanyuka nilipokuwa nimepiga magoti.

“Pole sana,” daktari aliyekuwa pembeni yangu aliniambia ambaye alionekana alisimama pembeni yangu muda mrefu.
“Bado sijapoa kwa nini nimekuwa nikiumizwa nikiwa ndani na nje ya ndoa? Kwa nini kila siku niwe mimi tu jamani?”

“Yote mipango ya Mungu asichoke kumuomba kwani yeye ni Alfa na Omega.”
“Nina imani atasikia maombi yangu.”
“Nina imani kabisa, bwana Mungu si muongo pale alipotuleza niombeni nitawasiliza, pia ametueleza tukimuamini yeye hakuna kinachoshindikana duniani na mbinguni.”

“Ameni.”
Kwa vile nilikuwa nimetumia muda mrefu wodini, nilitoka na kwenda kukaa chini. Shoga yangu alifuata kuniuliza.

“Vipi mgonjwa?”
“Bado,” nilisema huku nikitikisa kichwa na kufuta machozi yaliyokuwa wamekosa kizuizi.
“Shoga mbona unalia tu.”
 
SEHEMU YA 60

“Hali ya baba Jacky siyo nzuri.” Nilimjibu nikiwa nimeinama mkono kwenye paji la uso huku machozi yakiendelea kunitoka bila kumuangalia. Nilijishangaa jinsi nilivyoumizwa na ugonjwa wa mume wangu.

“Tuendelee kumuombea,” shoga yangu alinieleza kwa sauti ya upole.
“Mmh!” niliguna huku nikitosa kitambaa na kupenga kamasi zilizoanza kunichuruzika, pamoja akili yangu haikuwa kurudi kwa mume wangu.

Lakini bado nilimtambua kama mzazi mwenzangu ambaye alikuwa muhimili wa wanaye, pamoja na yote aliyoyafanya haikubadilisha wanangu kuwa siyo wanaye.

Siku ile tulikaa mpaka saa moja usiku bila kula tukiwa nje ya chumba cha wagonjwa mahututi mpaka alipokuja daktari mwingine tofauti na yule wa kwanza na kutueleza kwa pamoja.

“Jamani, kwa vile hali ya mgonjwa si ya kubadilika mara moja, mngekwenda kupumzika nyumbani ili kesho mje kumuona.”

Baada ya kusema vile mimi na baba mkwe tulitazamana kutafuta jibu la pamoja.
“Mama, nina imani daktari tumemsikia, tukapumzike ili kesho tuje tena,” bamkwe alisema.

“Sawa baba.”
Tulikubaliana kurudi nyumbani, tukiwa tunatoka baba mkwe ambaye alikuwa mnyonge alisema kwa sauti ya kukwaruza.

“Nimeamini mshahara wa dhambi mauti. Kama angekuwa na wewe haya yangemfika, sijui nitamfanya nini mke wangu na wanawe kama mwanangu atakufa?” baba mkwe alisema kwa uchungu kitu kilichozidi kuumiza moyo wangu. “Baba usiseme hivyo, hatutakiwi kumkatia tamaa bali tuendelee kumuombea.”

“Ni kweli, ILA haya ni malipo aliyoyafanya japo sehemu kubwa imechangiwa na mama yake na wadogo zake kuingilia ndoa yenu.”
“Baba yameishapita, tuangalie tutamsaidia vipi ndipo tujue waliosababisha wanafanywa nini.”

“Yaani wee acha tu, kila ni..niki..ku..ku,” baba mkwe hakuimaliza alianza kulia.
Pamoja na kuwa kwenye wakati mgumu, lakini nilijitahidi kumtuliza baba mkwe ambaye niliamini alikata tamaa kwa hali ya mwanaye.

“Baba inauma lakini tusimkatie tamaa, bado baba Jacky ana nafasi ya kuendelea kuishi.” “Ni kweli mama, kukuacha wewe alipoteza mwanamke wa kweli na kukikimbilia kifo.”
“Baba kuugua siyo kifo,” niliendelea kumpoza baba mkwe.
 
SEHEMU YA 61:

Tulipofika nje ya hospitali tulikodi teksi, kwa vile mimi nilikuwa karibu kuliko wenzangu. Niliwahi kupelekwa kwangu kisha nilimweleza dereva ampeleke kila mmoja kwake na kumlipa nauli kwa safari ya watu wote.

Baada ya kurudi kuingia ndani, nilikwenda moja kwa moja chumbani na kujitupa kitandani na nguo zangu. Nilikuwa na maswali mengi juu ya hali ya mume wangu.

Sikuamini mtu aliyeathirika kuwa katika hali ile ya kutapika damu kisha kupoteza uwezo wake wa kawaida wa kupumua mpaka asaidiwe na mashine. Kutokana na kuona mgonjwa wa upungufu wa kinga mwilini mtu akiwahi huduma na kufuata masharti alikuwa akirudi katika hali ya kawaida.

Moyoni alipanga kupigania hali ya mume wangu na akipona nitamchukua mwenyewe na kukaa naye kwangu. Moyo wangu ulijaa ujasiri kuliko kulia kwa vile niliwafahamu watu wengi walioathirika wanaoishi maisha mazuri ambao ni vigumu kuwajua mpaka uambiwe na mtu au kujisema wenyewe.

Kingine kilichonipa moyo ni hali ya watu kujitangaza tofauti na zamani pia hali ya unyanyapaa kupungua katika jamii. Niliamini yote hutokea ili Mungu kuangalia imani zetu kwa wenzetu.
Nilikumbuka kulipa jema kwenye baya ni vizuri ili baya likose nafasi.

Baada ya kuelezwa kulipa kisasi ni vita isiyo na mwisho na haina mshindi zaidi ya majuto na kusema kama ningejua nisingefanya.
Baada ya kuoga na kula kabla ya kulala niliwakusanya wanangu na kufanya maombi ya pamoja kumuombea dua baba yao Mungu amponye kwenye kikombe kile kizito.

“Baba Mungu bado sijachoka kukuomba, mponye mume wangu na maradhi mazito ambayo kwako si chochote. Mimi na wanangu tunapiga magoti kwako kumuombea ili umponye na ugonjwa uliomlaza kitandani na kutishia uhai wake.

“Baba wewe ndiye aliyetueleza tukiwa na matatizo tukimbilie kwako, nami na wanangu tunakimbilia kwako ili utufute machozi.

“Baba zuia roho ya magonjwa, zuia roho za mauti, zuia roho za kuzimu, zuia roho ya uyatima, kwa uweza wako baba yote yanawawezekana.
 
SEHEMU YA 62

Nilimaliza kuomba na kuwakusanya wanangu ambao hawakujua kilichokuwa, wakati wa kunyanyuka mwanangu Jackline ambaye naye aliguswa na nilichokuwa nikikisema kwa uchungu kikiambatana na machozi aliniuliza:
“Mama baba amefanya nini?”

Nilipomuangalia niligundua naye machozi yalikuwa yakimtoka, wanangu wengine walikuwa kama wamepigwa na butwaa.
“Anaumwa.”
“Anataka kufa?” Jacky aliendelea kunidodosa.

“Hapana ila anaumwa.”
“Mama nipeleke kwa baba,” mwanangu wa mwisho alisema.

“Nitawapeleka.”
“Na mimi?” na wengine walisema.
“Mama mbona unalia?” Jacky aliyeonekana yupo makini aliniuliza.

“Basi tu mwanangu.”
Baada ya dua niliwarudisha chumbani kwao na mimi kurudi chumbani kwangu na kujitupa kitandani.

Niliwaza mengi juu hali ya mume wangu, nilijiuliza kama atakufa nini hatima ya maisha ya wanangu, japokuwa mwanzo niliamini naweza kuwatunza bila ya baba.
Lakini nilijikuta nikiingiwa na hofu ya kuelemewa na malezi ya upande mmoja.

Kabla ya kulala nilimweleza dada hali ya baba Jacky alinieleza tutakutana alfajiri hospitali. Usingizi ulivyonipitia sikujijua na kujikuta nikiota ndoto ambayo iliniachia maswali mengi niliposhtuka usingizini.

Niliota nikiwa peke yangu kituoni nikisafiri, baada ya basi kufika nilipanda, kila mmoja alikuwa na furaha ndani ya basi. Baada ya muda safari ikiwa na misukosuko kitu kilichonifanya niingiwe hofu ya kufika salama lakini wenzangu walikuwa wakishangalia hali ile kitu kilichonishangaza.

Ghafla gari liliharibika na kunifanya mimi niteremke peke yangu na kutembea kwa miguu japokuwa pori lilikuwa linatisha.

Baada ya muda gari lilelile lilinikuta njiani na kusimama pembeni yangu nilipanda tena. Baada ya safari yenye furaha huku nikishangaa kujikuta ndani ya basi nipo na wanangu.

Gari liliharibika tena na kunifanya niteremke tena na wanangu na kutembea kwa miguu japokuwa ilikuwa shida sana.

Baada ya mwendo mrefu gari lilelile lilikuja lakini niligoma kupanda na kuliacha liondoke. Liliondoka na nikiacha nikitembea na wanangu japokuwa moyo ulinituma kupanda.
 
SEHEMU YA 63

Tukiwa njiani tulisikia kishindo, ghafla kilitanda kiza kizito cha kutisha.
Niliwakusanya wanangu kwa hofu bila kujua kiza kile kina maana gani, taratibu kiza kilianza kuondoka.

Nilijikuta nikipata matumaini ya kuendelea na safari.
Kabla hatujafika mbali ghafla tena kiza kilirudi tena kikiwa kizito kuliko cha awali na sauti za vilio zilitoka sehemu yenye kishindo.

Nilishtuka usingizini huku moyo ukinienda mbio,koo lilikuwa limenikauka kama mtu niliyekuwa nabuya unga. Nilikaa kitandani nikiwa na hofu,nilikwenda kwenye meza ya chakula na kunywa nusu jagi kutokana na ukali wa kiu.

Nikaelekea kwenye chumba cha wanangu kuwaangalia, niliwakuta wamelala katika hali nzuri. Niliwaacha na kurudi chumbani kwangu nilikaa kitandani na kujiinamia nikiwa na maswali ndoto ile ilikuwa na maana gani.

Kuhusu safari kilikuwa kitu kilichokuwa wazi kwa kuamini ile ilikuwa ni safari yamgu kabla ya ndoa na misukosuko ya ndoa yangu mpaka nilipofikia. Lakini kuhusu kiza kile kilichotoa mwanga wa muda mchache kisha kikaja kiza kizito kilikuwa kikimaanisha nini?

Nilijikuta nikikosa jibu la moja kwa moja.
Alipoangalia saa ilinionesha ni saa kumi na moja kasoro alfajiri. nilikwenda kuoga ili kujiandaa kwenda hospitali.

Nilikwenda kuoga na kunywa maziwa ya moto, kabla ya kuondoka nilimuamsha msichana wa kazi na kumuachia maagizo. Sikuingia tena chumbani kwa wanangu, sikutaka kuwasumbua. Nilipoangalia saa ilinionesha ni saa kumi na mbili kasoro.

Nilitoka hadi barabarani na kukodi gari mpaka hospitali kumuangalia mume wangu. Nilishangaa kumuona dada naye amefika hospitali. Baada ya kusalimiana wakati tunajiandaa kusogea kwenye mlango wodi,baba mkwe alifika, tukawa watatu.

Tuliungana wote nakusogea kwenye chumba alicholazwa mume wangu, kwa vile ilikuwa hairuhusiwi mtu kuingia ndani kwa muda ule kwa vile madaktari walikuwa wanamshughulikia mgonjwa aliyekuwa kwenye hali mbaya.

Tulisubiri nje, alipokuja muhudumu akatueza tunaweza kuingia mmojammoja.
Alitangulia baba mkwe ambaye alikaa zaidi ya dakika kumi akatoka huku akinizama usoni.
Uso wake ulionesha kukata tamaa.
 
SEHEMU YA 64

Uso wake hakuonesha matumaini yoyote ulionesha kukata tamaa, niliponosogelea nilimuuliza.
“Vipi baba?”
“Bado.”

Dada alifuata kuingia kumtazama mume wangu wakati huo baba mkwe alikuwa amegeukia ukutani mkono kashika ukutani kitu kilichozidi kunitia mashaka moyoni mwangu. Kumuuliza nilitaka lakini mdomo ulikuwa mzito kwa kujua nami nilikuwa naingia ndani ningekwenda kumuona.

Baada ya muda dada alitoka vilevile nilimtazama usoni, naye niligundua hali aliyoikuta ndani haikumpa matumaini. Dada alikuwa ameweka kitambaa pembeni ya macho kuonesha alikuwa akifuta machozi.

Alisogea pembeni na kuegemea ukuta sikutaka kumuuliza chochote.
Niliingia ndani na kupokelewa na sauti za mashine za kusaidia kupumua. Nilipoangalia kitanda kimoja niliwaona madaktari wakiwa wanahangaika kuokoa maisha ya mgonjwa mtu mzima kidogo.

Nilimsogelea mume wangu na kumkuta yupo kama nilivyomwacha jana yake hakukuwa na mabadiliko yoyote.
Nilijaribu kumuita kwa sauti ya chini huku nikimtikisa taratibu labda atashtuka, lakini nilikuwa kama natikisa gogo.

Nilimuangalia mume wangu nilijikuta nikipatwa na uchungu mkubwa moyoni kwa hali ile na machozi yalinitoka bila kupenda. Sikucha kumuombe kwa Mungu kwa kupiga magoti kabla ya kutoka.
Baada ya maombi nilitoka nje huku nami nilitumia kitambaa kuzuia machozi yaliyokosa kuzuizi.

Niliwakuta baba mkwe na dada wakizungumza, niliwasaogelea karibu waliponiona waliacha kuzungumza na kunitazama kama walikuwa wakinisubiri kunisikia nitazungumza nini.
“Baba kipi kinaendelea?” nilimuuliza baba mkwe.

“Mama si tumefika wote pamoja, sijajua kipi kinaendelea.”
“Ni vizuri kumuuliza daktari kipi kinaendelea,” dada alitoa ushauri.
Tulimsibiri daktari aliyetoka wadini na kumfuata kumuuliza kuhusu hatima ya mgonjwa wetu.

“Siwezi kuzungumzia chochote, majibu ya vipimo naweza kuyapata asubuhi hii.”
Tulikubaliana kuendelea kusubiri mpaka muda wa majibu, dada aliwahi kuondoka na kuniacha na baba mkwe tukisubiri majibu ya vipimo vya mume wangu japokuwa kitu kimoja kilikuwa wazi cha upungufu wa kinga mwilini.

Sikuamini mwenye tatizo kama lile kufikia hatua ya kupumua kwa mashine.
 
SEHEMU YA 65

Tukiwa tunasubiri majibu kilitoka kitanda kilichokuwa na mgonjwa aliyefunikwa shuka, moyo ulishtuka. Ba mkwe kwa sauti ya chini alisema. “Tayari Mungu kafanya kazi yake.”

“Kwani nini baba?” nilishindwa kuelewa japokuwa niliona.
“Mgonjwa mmoja amefariki.”
“Mungu wangu!” nilishika mikono kifuani kwa woga.

Nilijikuta nikichanganyikiwa na kuhisi kama tumbo la kihara likinishika. Nilikumbuka kauli za watu wengi kuhusu wagonjwa wanaoingizwa chumba cha ICU wanaotoka ni wachache sana. Kauli ile ilinitisha sana na kujikuta nikimuuliza baba mkwe.

“Eti baba kutoka ICU huwa ni bahati?”
“Ni kweli, mgonjwa wako akiingia ni kumuomba Mungu kwani toka jana wameisha kufa watu wawili.”
“Mungu wangu!”

“Ndiyo maana tunatakiwa kuzidisha maombi ili Mungu amuepushe mgonjwa wetu na kikombe hiki.”
Saa nne kasoro tuliitwa ofisini kupewa majibu, baada ya kukaa daktari alitueleza:

“Mgonjwa baada ya kumfanyia vipimo, majibu ya vipimo yanaonesha kwenye ini kuna tatizo na mapafu yamejaa maji pia figo moja imeharibika. Inaoneka mgonjwa alikuwa akitumia kilevi kikali bila kula na kusababisha matatizo hayo.”

Maneno ya daktari yalifanya nihisi kama moyo umepasuka na kumwagika damu ya baridi, nilihisi ubaridi ukitembea mwili mzima.

“Utatusaidia vipi?” baba mkwe aliuliza.
“Ndiyo tupo katika kupigania maisha yake.”
“Nini kinatakiwa?” niliuliza.
“Kwanza hebu tuachieni kazi hii tuangalie tutafika wapi.”

Baada ya kupata maelezo ya daktari tulitoka ofisini, tulikubaliana tuondoke. Tulikodi gari na kuondoka mimi nilipitia dukani na yeye kurudi nyumbani. Siyo siri nilikuwa dukani kimwili lakini mawazo yalikuwa mbali kutokana na hali ya mume wangu.

Nilipofikiria matatizo yaliyokuwa yamemuandama kila moja lilikuwa zito.
Tatizo la ini nilijua ni kubwa kuliko yote, figo niliamini moja lingeweza kumvuta hata kama zingekuwa zote ningekuwa radhi kutoa yangu moja kwa kuamini nisingekuwa na matatizo kutokana na kutotumia vitu vikali.

Mapafu niliamini yangetolewa maji na kuendelea kupumua kama kawaida.
Lingine kubwa ni kukosa kinga mwilini japokuwa kwangu hilo halikunitisha sana bali ugonjwa wa ini.
 
SEHEMU YA 66


Nilijiuliza nini hatima ya maisha yake, pamoja na kujipa moyo lakini malaika mtoa roho nilimuona kamsimamia mbele akiiomba roho yake. ***

Hali ya mume wangu iliendelea vilevile kwa zaidi ya wiki moja na nusu bila kuonesha mabadiliko yoyote japokuwa madaktari walitueleza ana mabadiliko makubwa ambayo hatukuyaona na kutueleza kama hali ile itaendelea kwa siku mbili basi wangemtolea mashine ya kupumulia baada ya mapafu yake kuanza kufanya kazi vizuri.

Japokuwa niliona kauli ile kama kutupa moyo kwa vile sikuona mabadiliko yoyote. Lakini siku zote uongo wa mganga nafuu ya muuguzaji.

Bado sikuchoka kumuombe mume wangu huku nikitaka aliyosema daktari yawe kweli.

Nakumbuka siku ya pili tuliyoelezwa kuwa mgonjwa atatolewa mashine ya kupumulia nilikwenda hospitali peke yangu mchana, kwa vile asubuhi sikwenda kutokana na kuwashughulikia watoto.
Nilipofika nje ya wadi kilitoka kitanda kikiwa na mtu kafunikwa shuka gubigubi kuonesha kiumbe kilicholala pale hakina uhai.

Nilijikuta mapigo ya moyo wakienda mbio na mwili kuniisha nguvu. Nilijiuliza yule ni nani? Nilitamani nimfuate kumfunia ili nimjue, lakini nilikosa ujasiri huo nilibakia nimesimama huku nguvu za mwili zikinipungua.

Nilisogea pembeni na kukaa kwenye benchi kupumzika huku kijasho chembamba hofu kikinitoka kwa mbali.
Lakini kwa upande mwingine niliona ujinga kujirusha roho bila kuingia ndani. Nilijinyanyua nilipokuwa nimekaa na kusogea mlangoni, nilivaa kikoti na viatu na kuingia wodini.

Moyo ulikufa ganzi na nguvu kuniishia baada ya kukuta kitanda alicholazwa mume wangu kitupu, nilijua yametimia. Nilihisi kizunguzungu na kiza kinene kilichoendelea sikujua.

Nilipozinduka nilijikuta nimelazwa kitandani, nilijishangaa pale nimefikaje pale. Taratibu nilikumbuka hali niliyokutana nayo asubuhi. Nilijikuta mapigo ya moyo yakianza kunienda mbio na jasho kunitoka.

ITENDELEA KESHO
 
SEHEMU YA 67

Bahati nzuri alikuwa akiingia daktari aliyesogea kitandani. Alinishangaa kunikuta nikihema kwa shida.

“Mbona hivyo, tatizo nini?”
“Hata sijielewi,” nilijibu kwa shida.
“Hebu punguza presha.”
“Mume wangu yupo wapi?”
“Yupo wadini.”

“Muongo, ameisha fariki.” “Nani kakwambia amefariki?”
“Si nimekutana na maiti yake ikipelekwa mochwali.”

“Maiti uliyoiona uliifunia?”
“Hapana.”
“Basi mumeo yupo wadini wala hajafa.”
“Si kweli unanipa moyo.”
“Tunaweza kwenda mguu kwa mguu kukuonesha.”

Nilijikuta nikinyanyuka kitandani na kuongozana na daktari mpaka wadini ambako nilishtuka kumkuta mume wangu akiwa amelala kitandani bila kutumia mashine ila alikuwa na mipira ya kumlishia chakula.

Moyo kidogo ulipumua na kumshukuru Mungu kwa hatua kubwa ya hali ya mume wangu kwa kuweza kutolewa mashine ya kupumulia japokuwa alikuwa akilishwa kwa mipira hilo niliamini ni moja katika njia za kupata nafuu.

Nilisogea pembeni ya kitanda na kumtazama, alikuwa amefumba macho kuonesha amelala, lakini nilipomuangalia vizuri niliona kama ahemi kitu kilichonishtua na kumuuliza daktari. “Daktari mbona naona kama ahemi?”
“Anahema kwa taratibu sana, mgonjwa anaendelea vizuri.”

“Lini ataongea?”
“Sijajua kutokana na magonjwa yake kumshambulia sana, lakini taratibu atalikava.”

Sikukaa sana kwa vile sikuweza kuzungumza naye. Kutokana na hali yangu kutokuwa nzuri nilirudi nyumbani kulala.

Wiki moja baadaye mume wangu alifumbua macho na kuweza kuzungumza kwa shida, siku nilipokwenda nilimkuta amelala.

Nilimkuta baba mkwe ambaye alitangulia na kunieleza kuba mabadiliko makubwa ya hali yake. Sikuondoka mpaka alipoamka na kushtuka kuniona.
“Ha! Mke wangu?” alisema kwa sauti ya chini.

“Abee, mume wangu.”
“Nisamehe m..m..ke wangu,” mume wangu alikutanisha mikono kuniomba radhi huku machozi yakimtoka.

“Nimekusamehe mume wangu,” nilimjibu huku nikimfuta machozi.
“Wanangu wapo wapi?”
“Wapo nyumbani.”
“Naomba walete nao niwaombe msamaha.”

“Nao wamekusamehe.”
“Hapana mke wangu naomba niwaone wanangu kabla sijafa najua lazima nitakufa tu.”

“Huwezi, kuugua si kufa,” nilimpa moyo.
“Ni kweli, lakini nilichowafanyia sisitahili kuendelea kuishi.”
 
SEHEMU YA 68

“Mume wangu kuna umuhimu gani wa kuniomba msamaha kama bado huoni faida ya msamaha wangu.”

“Nauuumwa mke wangu!” mume wangu alisema huku akikunja uso kutokana na maumivu aliyokuwa akisikia.

“Mungu atakusaidia, hali iliyoliyokuwa nayo mwanzo si uliyonayo sasa utapona na kurudi katika hali yako kwa vile kwa Mungu yote yanawezekana.”

“Halafu mama mwenzio hataki kula,” alisema baba mkwe.
“Mume wangu kwa nini hutaki kula?”
“Sijisikii.”

“Hapana.”
Nilichukua bakuli la chakula laini na kumpakata mume wangu aliyekuwa amebakia mifupa mitupu. Japokuwa moyo ulikuwa ukiniuma lakini nilijikaza kike ili niweze kumlisha.

Nilianza kumlisha, mume wangu alikula vijiko vitatu na kuanza kulia kilio cha kwikwi kitu kilichozidisha kuumiza moyo wangu.

“Mume wangu unalia nini?”
“Nakufa mke wangu bila kutimiza ahadi niliyokuahidi.”

“Ipi mume wangu?”
“Kuwa mume mwema na baba mwenye mapenzi na wanaye.”

“Mume wangu bado nafasi hiyo unayo kwa vile ukitoka hospitali utakuiwa na nafasi ya kusahihisha makosa yako, basi kula mume wangu.”

“Mke wangu siwezi, najua hujui ninachoumwa unawezekana wamekuficha, nimeathirika mimi ni maiti mtalajiwa,” alisema mume wangu huku machozi yake yakikosa kizuizi, niliamini magonjwa mengine alikuwa hayajui.

“Mume wangu nani alikuambia kuathirika ni kufa? Hizo ni imani potofu, ukifuata masharti utaishi maisha marefu.”
“Ataweza kukaa na mimi muathirika?”
“Wacha kukaa hata kushea mapenzi kwa kufuata taratibu.”

Kauli yangu ilimfanya mume wangu aangue kilio cha sauti kitu kilichotufanya tuingie katika kumnyamazisha.

Nilimbembeleza mume wangu kwa maneno yote mazuri huku nikimuhakikishia bado yupo moyoni mwangu kwa vile kiapo nilichokiapa mbele ya kasisi hakijatoka moyoni mwangu pamoja na hasira za kibinaadamu nilizopata nilikuwa bado nampenda.

“Mke wangu, nalia kwa majuto nalia kwa pigo mujarabu alilonipiga Mungu la kuiterekeza familia yangu na kwenda pasipo sahihi. Hiki ninachokipata ndiyo malipo ya usaliti.”

“Mungu alitueleza yeye ni mpole na msikivu mwenye kisamehe hivyo una nafasi ya kuzaliwa tena kiumbe mpya.”
 
SEHEMU YA 69

“Asante mke wangu, asante kwa mapenzi uliyooneka kipindi chote cha ugonjwa wangu Mungu atakulipia.”

“Asante.”
Nilimalizia kumlisha kitu kilichomshangaza baba mkwe ulaji ule.
“Mama unatakiwa kila siku uje mlishe mume wako.”
“Hakuna tatizo na chakula chake chote nitakitayalisha mimi.”

“Nitashukuru, huwezi kuamini kazi yote niliifanya mimi mama yenu na wanaye wamesusa baada ya kufukuzwa kama mbwa na mumeo toka alipokutafuta na kumkatalia kurudi.”

Siku ile nilishinda hospitali na mume wangu mpaka jioni, muda wote nilimpa moyo kutokana na kujikatia tamaa. Tulielezwa tumpe chakula kingi kabla ya kuanza dozi kali ya ini na figo. Siku hiyo niliondoka saa tatu siku na kurudi nyumbani nikimuacha akipitiwa usingizi.

Nilipofika nyumbani nilipiga magoti kumshukuru Mungu wa maajabu aliyonionesha kwa kuweza kumfanya mume wangu kufumbua macho kuongea na kula. Kwa kweli siku ile nililala usingizi mzuri mpaka asubuhi bila njozi mbaya. *** Hali ya mume wangu iliendelea vizuri na kuweza kutolewa chumba cha wagonjwa mahututi na kuhamishiwa cha wagonjwa wanaoendelea vizuri.

Hali ile ilinifurahisha, niliwapeleka watoto kumuona baba yao. Kwa kweli nilivyoangalia jinsi watoto walivyofurahi kuwa na baba yao roho ilinuma sana.
Nilikumbuka maisha ya awali kabla hakujatokea matatizo nilijikuta nikikosa amani moyoni.

Watoto walionesha jinsi gani walikuwa wamekosa mapenzi ya baba yako. Kila mmoja alikuwa kama kinda kwa mzazi wake jinsi alivyo mchezea huku wakimuuliza maswali mengi ambayo yalimfanya mume wangu atokwe machozi.

Lakini niliamini wanadamu tuna nafasi nyingi katika maisha baada ya kujikwaa, ugonjwa wa mume wangu moyoni mwangu haukuwa tatizo bali kufikiria kuitengeneza upya familia yangu iliyo sambaratika. Watoto wangu waliongeza chachu ya kumchukua mume wangu baada ya kutoka hospitali kwa jinsi walivyonionesha baada ya kumuona baba yao.

Niliamini kabisa pamoja na ugonjwa wake mume wangu angekuwa karibu na familia yake pia kupata faraja moyoni mwake angejisikia furaha.
 
SEHEMU YA 70


Akili yangu iliniambia huenda tatizo hilo lingeweza kumpata hata kama ningekuwa naye hivyo sikutakiwa kumtenga. Bado nilikiangalia kiapo cha ndoa mara mbili kuhusu kutenganishwa na kifo.

Nami niliuapia moyo wangu kipindi kile sitamuacha mume wangu kama kufa basi afe mikononi mwangu japokuwa sikuomba jambo lile litokee kwa vile nilijikuta nikimuhitaji sana kipindi kile kulicho wakati wowote uliopita.

Hakuacha kunishukuru kutokana na kumjali sana kipindi ambacho aliamini angekufa kibudu. Nilimweleza asahau yote kwa vile kama kujifunza amejifunza, nilimuakikishia sitalipiza kwa lolote zaidi ya kuijenga familia iliyo bora mbele ya macho ya watu.

Hali yake ilizidi kuimalika siku hadi siku ikionekana kuna kila dalili za mume wangu kutoka hospitali ili akajiuguzie nyumbani. Daktari alinieleza kuhusiana na hali ya mume wangu kuwa kumekuwa na maendeleo ya ajabu ambayo hawakutegemea. Hivyo alikuwa katika uangalizi wa muda ili atolewe hospitali ili auguziwe nyumbani.

Hali ya mume wangu ilirudisha furaha ndani ya familia yangu huku nikijiona kama nataka kuzaliwa upya katika maisha ya ndoa, nilisubiri kwa hamu siku ya mume wangu kutoka hospitali nilikubaliana na baba mkwe kumchukua mume wangu na kumuuguza.

Siku zote baba mkwe hakuacha kunishukuru mimi na familia yangu kutokana na kujitolea muda wote kumuhudumia mume wangu. Nilimweleza nisingeweza kumtenga kwa kufanya vile ningekuwa sawa na kuwatenga wanangu ambao hawakuwa na hatia.

Pia nilimweleza sababu ya mume wangu kuwa vile ilikuwa shinikizo la mama yake ambalo lilimtaka kulitekeleza bila hivyo angemuachia radhi. Kipindi chote kile mama mkwe na wanawe hawakugusa hospitali. Nilijua waliona aibu kuja kwa vile matatizo yote wao ndiyo walio sababisha na pia kufukuzwa na mume wangu baada ya kuugundua ubaya wao.

Nakumbuka siku moja ya jumapili nilikwenda hospitali na wanangu kumuangalia baba yao, baada ya wiki nzima kuwa shule. Ilikuwa siku niliyojawa na furaha mume wangu alikuwa amechangamka huku afya yake ikijengeka vizuri hata vinyama kwa mbali vilianza kurudi.
 
SEHEMU YA 71

Daktari aliyemuona siku ile alisema wakati wowote mume wangu ataruhusiwa kutoka hospitali. Maneno yale yalinifurahisha sana, niliendelea kumuombea kwa Mungu ili atoke hospitali salama. Siku ile ilikuwa kama tupo nyumbani kutokana na uhuru tuliopewa pale hospitali.

Siku ile alikula mpaka nikafurahi, hata waliokuja kumtazama waliyaona mabadiliko makubwa na kuyashangaa. Mume wangu aliomba tuzungumze kitu, alisema ilikuwa ni lazima aniambie siku ile hakutaka ipite bila kunieleza. Ba mkwe alitoka nje na wajukuu zake na kuniacha na mume wangu.

“Mume wangu una kipi kilicho moyoni mwako?” nilianza kumuuliza baada ya ukimya.

Mume wangu alitulia kwa muda akiwa kama anafikiria jambo kisha aliniita jina langu.
“Eliza.”
“Abee.”

“Kwanza nashukuru kwa kila alilolifanya kwangu, nimeamini mwanamke bora hatafutwi na mtu bali huchaguliwa na Mungu. Wewe ni chaguo nililochaguliwa na Mungu, lakini nimekuwa kipofu na kushindwa kukuona na kuangalia kwingine ndipo nilipokutana na mazito ambayo sidhani kama nitakuwa na maisha marefu.”
“Kwa nini?” nilimuuliza huku nikimtazama usoni.
“Hali yangu pamoja na kuimalika lakini tayari ubovu umeisha ingia sawa na kukalia kuti kavu kuanguka si ajabu.”

“Hapana mume wangu tuendelee kumuomba Mungu kila kitu kwake ni chepesi, Kijoki si yule niliyokuja kukuta chumba cha ICU siku ya kwanza na wa leo. Lazima umshukuru Mungu kwa uweza wake kwako na kuweza kunifanya leo nicheke kwani toka siku ya kwanza kuletwa hospitali nilikuwa mtu wa kulia lakini leo nacheka lazima ashukuliwe kwa hilo,” nilimtia moyo mume wangu.

“Ni kweli mke wangu, napenda kuchukua nafasi hii kukuomba msamaha tena, najua nimewakosea kiasi gani, sikuwa mtu wa kusameh...”

“Mume wangu tuliisha lizungumza tukalimaliza, sipendi kulisikia tena kwa vile sitaki kukumbuka yaliyopita,” nilimkata kauli mume wangu.
“Nimekuelewa mke wangu, naomba leo niache nirudie nina imani sitalizungumza tena.”
“Mmh! Haya zungumza,” nilimruhusu.

ITAENDELEA JIONI.
 
Daaah yaani hujatoa nafasi ya waheshimiwa kutoa maoni,au mawazo??

Wewe noma sana.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom