Simulizi: Kiu ya talaka

Simulizi: Kiu ya talaka

Shunie

JF-Expert Member
Joined
Aug 14, 2016
Posts
157,400
Reaction score
465,165
Sehemu ya 01

Mtunzi:
Ally Katalambula

Ndoa ni kama jumba au ngome yenye siri kubwa, waliopo ndani wanataka kutoka nje na walioko nje wanatamani kuingia ndani. Waliotoka kwa makosa ya kujitakia wanatamani kurudi tena ndani na waliopo nje waliokutana na dhahama hawataki tena kuingia ndani. Mimi ni mmoja wa watu waliokutana na dhahama ambayo ilinifanya niichukie na kutoitamani tena.

Kwanza kabisa kabla ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kunipa pumzi na akili timamu za kuweza kuyatoa yaliyonisibu na kuamini nyoka mwenye sumu kali ana afadhali kuliko mwanadamu unayecheka naye mchana lakini usiku anakugeuka. Kupitia mlolongo wangu wa maisha naamini Mungu ni muweza wa yote na malipo ya kila kitu yapo hapahapa duniani, ahera huwa ni hesabu.

Mwanadamu anaweza kukufanya ukaichukia dunia wakati bado unaipenda, lakini nashukuru moyo wa kutokata tamaa na subira ndivyo vilivyonifikisha hapa na kupata ujasiri wa kuutoa ushuhuda huu mbele yenu.

Nina imani mlio ndani ya ndoa mtakubaliana nami haya nitakayoyaeleza inawezekana si yote yakafanana lakini kwa asilimia kubwa yamekukuta. Ndoa nyingi zimevunjika kutokana na kero za wakwe na mawifi. Cha kushangaza kabla hujaolewa unakuwa wa kwanza kuichokonoa ndoa ya kaka yako lakini ukiolewa na wewe yanakukuta na unaishia kulalamika na kusahau kwamba muosha huoshwa.

Najua umebaki na maswali juu ya kauli yangu, kwa nini siitaki tena ndoa na kwa nini siwezi kuwasamehe wala kuwasahau wabaya wangu japo tumefundishwa kuwasamehe watu saba mara sabini! Pia tumeelezwa tusamehe kwanza ndipo tusamehewe lakini kwa hili Mungu atanisamehe.

Naitwa Eliza Elias, umri wangu ni miaka 40 kwa sasa, elimu yangu kidato cha nne, nilikatisha masomo kwa ajili ya ndoa si kwa kulazimishwa bali kwa hiyari yangu mwenyewe. Nilibahatika kuolewa na mwanaume ambaye niliamini ndiye wa maisha yangu.

Alinipenda nami nilimpenda sana tena sana, mpaka tunakubaliana kuwa mke na mume kuna vitu vilinishawishi kuanzia yeye mwenyewe, familia yake akiwemo baba ambaye muda huu ni marehemu na mama pamoja na mawifi.
20191203_124348.jpg
 
Sehemu ya 02

Kwa jinsi walivyonipokea niliamini kabisa ndoa yangu ni moja ya ndoa bora zilizochaguliwa na Mungu. Naweza kusema kuna kitu kilichonivuta kuipenda ndoa na kutotaka kuendelea na masomo kilitokana na ndoa ya dada yangu.

Uwezo wa darasani ulikuwa mzuri japo si sana ambao niliamni kabisa ningeweza kuendelea na kidato cha sita mpaka chuo kikuu. Lakini kuifikia sana ndoa naamini kabisa ilipunguza uwezo wangu darasani . Niliipenda na kuitamani kupitia kwa dada yangu ambaye ndiye aliyenilea baada ya mama yetu mzazi kufariki nikiwa darasa la tano na yeye kuchukua jukumu la kunisomesha.

Pamoja ya kuwa ni dada yangu lakini mimi nilipenda kumwita mama kwa vile amenilea na kunifundisha adabu na hekima. Nakumbuka siku moja nilisikia mchungaji akisema wakati huo nilikuwa kidato cha kwanza kuwa ndoa njema yenye upendo ni pepo ya duniani. Nilikubaliana na kauli ile kutokana na maisha aliyokuwa akiishi dada na shemeji.

Kwa muda wote niliokaa kwa dada sikuwahi kuwaona wanagombana au kubishana zaidi ya kuelekezana pia kila mmoja kujishusha pale panapotokea kitu ambacho kilikwenda ndivyo sivyo. Dada na shemeji japokuwa hawakuwa watani lakini walitaniana muda wote kitu kilichonifanya nami nitamani kuolewa.

Pamoja na kuitamani ndoa lakini moyo ulijaa hofu kutokana aza zilizokuwemo kwenye ndoa kiasi cha watu kusema hawataolewa tena. Kama nilivyoeleza mwanzo nikiwa bado nipo shuleni nilipata rafiki wa kiume ambaye alikuwa akifanya kazi serikali akiwa na cheo kikubwa.

Mwanzo zikutaka kumsikiliza kwa vile niliamini niweza kuchanganya mapenzi na masomo na siku zote mapenzi huwa na nguvu na kumfanya mtu akatishe masomo na kuvuruga ndoto zake za maisha.
 
Sehemu ya 03

Siku za mwanzo sikutaka hata kumsikiliza lakini kila alipotoka shuleni alinifuata na gari lake. Siku moja niliamua kusimama kumsikiliza, alichonieleza kilinifanya nianze kumpenda baada ya kuonesha hakuwa kama wanaume wengine waliotanguliza ngono na kuharibu malengo ya wanafunzi wengi.

Alinieleza amenipenda hataki kuniharibia maisha yangu na yupo tayari kunisubiri hata kama nitafika chuo kikuu bila kuujua mwili wangu hasi tuingie kwenye ndoa. Si kwamba nilikuwa sijawahi kukutana kimwili na mwanaume la hasha lakini sikuwa muumini wa tendo hilo, kwangu ilitokea kama bahati mbaya na baada ya kujua thamani ya usichana kwa mtoto wa kike roho iliniuma sana.

Lakini sikuwa na sababu ya kuendelea kuumia zaidi ya kutorudia kosa ili nitimize malengo yangu. Nilikubaliana na yule mwanaume ambaye baada ya muda alikuja nyumbani kujitambulisha kwa dada na kueleza nia yake kwangu. Dada alimuelewa na kumpa masharti yake yakiwa kutonivuruga kimasomo.

Tokea hapo yule bwana akawa ananihudumia kwa kila kitu kama mkewe, dada alinionya nisikubali kufanya mapenzi kabla ya wakati. Nilimuhakikisha kufanya tulichokubaliana. Siku zilikatika huku ndoa ya dada nikiendelea kunivutia na kutamani nami siku moja kuwa na mume wangu.

Nilijikuta nikiamua kuishia kidato cha nne ili tu nami niolewe, baada ya matokeo ya kidato cha nne kutoka nilipata four ya 27 ambayo haikuniwezesha kujingana na kidato cha tano shule za serikali. Dada na mchumba wangu walitaka niendelee shule za kulipia lakini nilikataa na kusema nataka niolewe.
 
Sehemu ya 04

ILIPOSHIA

Nilijikuta nikiamua kuishia kidato cha nne ili tu nami niolewe, baada ya matokeo ya kidato cha nne kutoka nilipata four ya 27 ambayo haikuniwezesha kujingana na kidato cha tano shule za serikali. Dada na mchumba wangu walitaka niendelee shule za kulipia lakini nilikataa na kusema nataka niolewe.

SASA ENDELEA... Kutokana na umbile langu kubwa japokuwa nilikuwa ndiyo nafikisha miaka kumi na tisa hakukuwa na maswali labda mi ni mtoto mdogo.

Kabla ya ndoa nilipata nafasi ya kutembelea familia ya mume wangu mtarajiwa. Kwa kweli kila mmoja aliyeniona alinifurahia, kupokewa vyema kwenye familia ya mume wangu mtarajiwa ilinipa faraja ya kujua sehemu niliyoangukia ni salama na ile pepo ya dunia nilianza kuiona kabla sijaingia kwenye ndoa.

Baada mipango kwenda vizuri niliolewa na kuwa mke wa bwana Richard.
Baada ya kuolewa ndoa yangu iliyoacha simulizi midomoni mwa watu, Eliza mimi niliyaanza maisha kama mke wa mtu niliamini nami nitaishi maisha kama ya dada yangu na shemeji walikuwa kama kulwa na doto..

Niliishi ndani ya jumba la kifahari kulala kitanda cha kifahari kutembelea gari la kifahari nilikula chakula nikitakacho na kujipamba kwa vito vyote vya gharama. Weupe nilio nao nilikuwa kama malaika.

Ni kweli niliamini ndoa ni pepo ya duniani kwa maisha niliyoishi na mume wangu kwa kuonyesha mapenzi ya kweli na upendo ulioonekana dhahiri shairi. Mapenzi hayakuwa kwa mume wangu tu familia yake yote ilinipenda sana kila mmoja aliniona kama yai, nilipendeza machoni mwa watu.

Fedha ya matumizi niliyoachiwa na mume wangu ilikuwa haina mahesabu ilipokwisha hakuuliza zaidi ya unipatia nyingine.

Kutokana na fedha kukosa mahesabu nilijikuta nikipata wazo la kutunza fedha kwa siri bila mume wangu kujua. Fedha zote nilimpa dada aniwekee, kwa muda wa miezi sita ndani ya ndoa dada aliweza kuninunulia kiwanja bila mume wangu kujua.
 
Sehemu ya 05

Ndoa yangu kwa kweli niifurahia haikuwa tofauti na ya dada kutokana na waume zetu kutokuwa wakali walikuwa waelewa pale unapotokea kutoelewana. Siku nazo zilikatika mtoto wa kike bila kushika ujauzito. Mwanzo sikushtuka niliona jambo la kawaida kwa kuamini muda bado.

Kwa vile nyumba niliyokuwa nakaa ilikuwa kubwa mume wangu aliniomba nikae na wifi zangu ili kunichangamsha. Kutokana na mapenzi na ukaribu wetu sikuwa na kipingamizi. Wifi zangu wawili wadogo wa mume wangu walihamia kwangu. Mwanzo ulikuwa mzuri kutokana na wifi zangu kunidekeza hata kazi zote za nyumbani walifanya wao.

Baada ya mwaka kukatika bila kushika ujauzito hali ilianza kubadilika kwa mawifi zangu kuanzisha nyimbo za mafumbo na kuvaliwa kanga zenye maneno KAZI IMEKUSHINDA WAACHIE WENZAKO.

Mwanzo sikuelewa lakini nilikuja kuelewa baadaye kumbe yote yale yalikuwa kwa ajili yangu. Lakini nilishindwa niwaulizie wapi kwa vile hawakunitaja jina.

Ile hali kidogo ilinitia unyonge lakini nilishindwa nianzie wapi, nami nilianza kujishtukia kwa kukaa mwaka mzima bila kushika hata ujauzito wa bahati mbaya. Nilishindwa nikamueleze dada kutokana na kunikataza kusikiliza watu wa pembeni alinieleza ni sumu kwenye ndoa.

Niliamua kukaa kimya lakini moyo uliniuma na kujifikiria nifanye nini ili kuikimbia aibu ile. Siku moja tukiwa kitandani tumelala mume wangu aliniamsha saa nane za usiku.

“Eliza...Eliza,” aliniamsha usingizini.
“Abee mume wangu,” niliitika huku nikifumbua macho.

“Kuna jambo nataka tuzungumze.”
“Mmh! Kwani muda huu ni saa ngapi?” nilimuuliza huku nikikaa kitako.
“Saa nane.”
“Saa nane?”
“Ndiyo.”
“Mbona umeniamsha muda huu?” nilimshangaa mume wangu.

“Kuna jambo nataka tulizungumze.”
“Mmh! Sawa, lakini mbona usiku sana,” nilimuuliza huku nikipiga miayo ya usingizi.
 
Sehemu ya 06

Nilikaa kitandani huku nikipekecha macho Kwa mume wangu, nilijua kuna jambo zito lililomtatiza mume wangu.
“Unasemaje mume wangu?” nilimuuliza huku nikiyalazimisha macho kutazama.
“Hivi ndoa yetu unaionaje?”
“Ipo vizuri, kwani vipi?”

“Hakuna kitu kilichopungua katika ndoa yetu?”
“Kitu! Kitu gani hicho?” nilituliza mawazo sikuona kitu chochote kwani kila kitu kilikuwemo ndani, kwa kweli baada ya kufikiri kwa muda nilimjibu.

“Kila kitu kipo mume wangu sioni mapungufu labda mwenzangu umeona kitu.”
“Siyo vitu vya matumizi ya ndani.”

“Vitu gani?”
“Watu wanapooana mnategemea nini?”
“Kuishi maisha mazuri na kuelewana.”
“Mkiisha elewewana basi?”
“Mjenge familia bora kama Mungu atajalia kupata mtoto.”

“Huoni kuchelewa kwetu kupata mtoto nyumba imepwaya?”
“Ni kweli mume wangu,” maneno ya mume wangu yaliushtua moyo wangu.

“Sasa tutafanyaje?”
“Mume wangu swali gani hilo, kupata au kutopata ipo nje ya uwezo wangu.”
“Hii hali unaipenda?”
“Siipendi moyo minaniuma nami natakani kuwa na watoto kama wenzangu,” nilisema kwa uchungu mpaka machozi yakanitoka.

“Basi mke wangu usilie.”
“Hapana mume wangu sisemi tu lakini moyo unaniuma sana.”

“Basi nisamehe mke wangu kwa kukuumiza.”
“Siyo hivyo mume wangu una haki ya kuuliza japokuwa jambo lenyewe lipo nje ya uwezo wangu.”

“Nimekuelewa mke wangu.”
Japokuwa tulimaliza lakini sikupata usingizi nilijiuliza mengi juu ya swali la mume wangu juu ya mtoto na mafumbo ya wifi zangu. Siku ya pili baada ya mume wangu kwenda kazini wifi zangu waliendelea na mafumbo yao. Nilijikuta naingia unyonge na kuanza kuona adha ya ndoa.

Yote ilikuwa ni kutokana kuchelewa kupata mtoto na kuonekana mgumba. Jioni mume wangu aliporudi nilimueleza tabia za wifi zangu. Baada ya kumueleza nilimuona akishtuka na kuniuliza.
 
SEHEMU YA 07

Jioni mume wangu aliporudi nilimueleza tabia za wifi zangu. Baada ya kumueleza nilimuona akishtuka na kuniuliza.
“Ina maana wamefikia hatua hiyo?”
“Ndiyo.”

“Basi niachie kazi hiyo mimi tena wataondoka usiku huu.”
“Usiwafukuze ila waeleze waache tabia zao mbona mwanzo hawakuwa na tabia hizo.”

“Hapana mke wangu mwenye wasiwasi wa mtoto ni mimi sio wao.”
“Wana haki ya kusema lakini si kunihukumu mbona dada yangu amepata mtoto baada ya miaka miwili ya ndoa yake na baadaye alipata watoto wengi, mi mwaka tu maneno.”

“Mke wangu mwenye haki ya kuhoji ni mimi wala si mtu yoyote hata wazazi wangu hawana haki hiyo.”
“Basi naomba uwaeleze waache siyo kuwafukuza.”

“Nimekuelewa.”
Mume wangu alipoa na kutoka kwenda kuzunguza na wadogo zake. Baada ya muda alirudi na kumuuliza.
“Vipi wamekuelewa?”
“Wanielewe wasinielewa nimewaeleza waondoke.”

“He! Mbona umekwenda kinyume na makubaliano yetu?”
“Wanataka kunipanda kichwani, hujui jinsi gani walivyokosa adabu kwangu.”
“Jamani, wazazi wako watanielewa kweli?”
“Watakuelewa tu kwani niliyeamua si mimi.”

Mmh! Nilianza kuona kuchelewa kupata kwangu mimba kumeleta utafaruku kwenye familia ya mume wangu.

Usiku huo wifi zangu walikuja kuniomba radhi kutokana na yote yaliyotokea. Pamoja na kufanya hivyo mume wangu hakuwa tayari kuwasamehe. Lakini niliwakingia kifua awasamehe, naye alikubali kwa vile mimi mwenyewe nilikuwa nimeridhia.
 
SEHEMU YA 08

Baada ya kuzimwa chokochoko zile nilimshukuru Mungu kwa kuweza kuirudisha nyumba yetu kwenye hali ya kawaida. Hakukuwa tena na maneno wala kuvaa khanga za mafumbo. Wifi zangu hawakuacha kuniomba msamaha kwa yote yaliyojitokeza huku wakisema mafumbo yale hayakuwa yangu.

Siku zote waswahili wanasema funika kombe mwana haramu apite, japokuwa nilijua madongo yote yalikuwa yakinielenga mimi lakini nilikubaliana nao ili kurudisha hali ya amani ndani ya nyumba yetu.

Siku zilikatika huku moyo ukinifukuta juu ya kuchelewa kupata mtoto. Wasiwasi wa ugumba ilinitawala sana akilini mwangu kutokana na kauli nilizozisikia kwa wifi zangu japokuwa dada yangu alichelewa sana kupata mtoto. Lakini yeye hakunyanyapaliwa na mama mkwe na mawifi zake.

Nilipata wazo la kumuomba mume wangu twende hospitali tukapime japokuwa dada alinieleza nisiwe na wasiwasi nitapata mtoto kwa vile hata marehemu bibi kizaa mama alipata mtoto katika miaka miwili ya ndoa yake.

Siku moja saa saba usiku nami nilimuamsha mume, siku ile kutokana na mawazo kuwa mengi nilishindwa kulala nilipata wakati mgumu kumueleza mume wangu.

Nilipomuamsha alishtuka kumuamsha usiku wa manane.
“Vipi mke wangu mbona usiku sana?”
“Kuna jambo linanila sana akili sana mume wangu.”

“Jambo gani tena mke wangu?” aliniuliza huku akikaa kitako na kufikicha macho.
“Kuhusu kuchelewa kupata mtoto.”
“Mke wangu hebu achana nalo tuliisha liongelea likaisha, vipi wifi zako wameanza tena?”
“Walaa.”
“Sasa nini?”
“Nilikuwa na wazo la kucheki afya zetu.”
“Kuhusu nini?”

“Kuchelewa kwangu kupata mtoto huenda ni matatizo ya kiafya.”
“Mpenzi si ulisema familia yenu mnachelewa kupata watoto?”
“Ndiyo, lakini wapo waliowahi kupata watoto sio wote.”

“Kwangu nina imani nipo sawa.”
“Kwa nini?”
“Niishawahi kufanya uchunguzi wa afya yangu.”
“Ha! Kwa nini hukuniambia?” Nilishtuka kusikia vile.
 
SEHEMU YA 09

ILIPOISHIA “Ndiyo, lakini wapo waliowahi kupata watoto sio wote.”
“Kwangu nina imani nipo sawa.”
“Kwa nini?”
“Niishawahi kufanya uchunguzi wa afya yangu.”
“Ha! Kwa nini hukuniambia?” Nilishtuka kusikia vile.

SASA ENDELEA...

“Nisingeweza kukuambia haraka mpaka kwanza nijichunguze mwenyewe.”
“Baada ya kujua afya yako kwa nini hukuniambia nami nikapime?”
“Mi sina wasiwasi na wewe.”
“Mmh! Sawa, basi kesho naomba na mimi nikaangalie afya yangu.”
“Hakuna tatizo.”

Kwa vile usiku ulikuwa mkubwa tulilala kuitafuta siku inayofuata. Kesho yake nilikwenda Hospitali ya Agha khan kufanya uchunguzi wa afya yangu na kukuta nina uwezo wa kupata mtoto.

Jioni mume wangu aliporudi alimjulisha taarifa ya hospitali. Aliendelea kunipa moyo wa kupata mtoto siku yoyote Mungu akipenda. Hata dada nilipokwenda kumwambia kuhusu hali yetu alinishangaa.

“Eliza nikuambie mara ngapi mtoto ni zawadi tupewayo na Mungu hatuwezi kumpangia muda wa kutupa hiyo ni siri yake.”

“Sawa dada, japo sikuhizi hawasemi lakini najua kuna maneno yanasemwa juu yangu japokuwa siyasikii.”
“Mumeo anasemaje?”
“Hana maneno amesema tuendelee kusubiri.”

“Basi acha kujitia presha, hata mimi nilikuwa kama wewe lakini mama alinituliza wala sikwenda kupima hospitali. Alinikataza kwenda kupima unaweza kupewa majibu ya uongo ukafa kwa kihoro.”

“Sawa dada nimekuelewa.”
Niliendelea kuwa na subira ya mtoto japokuwa roho iliniuma kila nilipomuona mwanamke mwenye mtoto mdogo au mjamzito na kujiuliza nimemkosa nini Mungu.

Kuna siku niliona mwanamke mmoja akitoa ushuhuda ametafuta mtoto wa miaka ishirini na kumpata akiwa na miaka arobaini kupitia maombi ya kanisa moja na kilokole.

Habari zile zilinivuta sana na kumshauri mume wangu niende kwenye maombi. Alinikatalia kwa kusema wengi wanaotoa ushuhuda huwa waongo ni watu waliopagwa.

Nilitamani kutoka kwa siri ili niende kwenye maombi, lakini niliogopa kuonekana kwenye tivii na kusababisha matatizo kwenye ndoa yangu. Mara nyingi wakati wa maombi kwa njia ya tivii kila mmoja alipoambiwa ashike sehemu inayomsumbua mimi nilishika tumbo.
 
SEHEMU YA 10

Nilifanya vile kwa siri kwa kuamini nami nitafanikiwa kwa vile wapo waliotoa ushuhuda kuwa waliponywa kwa njia ya kuangalia tivii tu. Kipindi cha maombi kilipofika kama kuna watu nilikosa raha na kuacha kipite kwani sikutaka mtu ajue nafanya nini.

Siku nazo zilikatika bila dalili zozote za kushika ujauzito. Nami sikukata tamaa niliendelea kusubiri mtoto kwa hamu kubwa huku kila siku nikifanya maombi ya nguvu.

Waswahili wanausemi wao mtu anaweza kukunyima chakula siyo neno. Kuna msichana mmoja ambaye alikuwa mtu wa karibu sana ya wifi zangu ambaye naye nilikuwa nimezoeana naye sana aliniuma sikio.

Nakumbuka siku hiyo wifi zangu waliondoka na kuniacha peke yangu. Alipofika kwanza aliwaulizia wifi zangu na kumueleza wamekwenda kwao. Baada ya mazungumzo mafupi aliniambia:
“Samahani shoga kuna jambo nataka kukueleza lakini naogopa naweza kuonekana mbeya.”

Nilishtuka kusikia vile.
“Hapana niambie shoga yangu,” nilimtoa wasiwasi japo moyo ulinipiga.
“Shoga una kifua?”
“Ninacho,” mlimjibu.

“Nitakalo kueleza utalimeza kama lilivyo hutalitapika mbele za watu?”
“Mmh! Mbona unanitisha?” nilishtuka kidogo.

“Aah! Kama huwezi niliache.”
“Hapana naweza niambie tu.”
“Ni hivi, kuna jambo linafanyika kwa kwa siri kwa kweli halinifurahishi hata kidogo.”

“Jambo! Jambo gani?”
“Kuhusu wewe.”
“Mimi! Nimefanya nini?” niliuliza huku nikijishika kifuani.
“Kuna mpango unaendelea chinichini wa kukutoa ndani bila wewe kujua.”
“Kwa sababu gani?” niliuliza macho yamenitoka pima.

“Eti wee mgumba.”
“Mtume!” kauli ile iliushtua moyo wangu kidogo nipoteze fahamu kwa mshtuko.
“Basi shoga kaa ukijua sasa hivi kuna kampeni ya chinichini ya kukutoa ndani ya nyumba. Hivi ninavyokueleza mumeo kutafutiwa mwanamke wa nje ambaye akizaa wewe ndoa huna!”

“Mmh! Kweli?”
“Kwani siku hizi mumeo anarudi kama zamani?”
“Hapana”
“Unmajua kwa nini?”
“Kazi zimemzidi.”

“Basi mwenzangu unaliwa shere mwenzio siku hizi anapitia kwenye kidumu kisha anakuja kwako, nina wasiwasi hata haki yako ya ndoa imekuwa ya mashaka.”

Kauli ile ilikuwa kama ya mganga wa kienyeji aliyepiga ramli na kuyaona mambo yangu ya ndani.
 
SEHEMU YA 11

“Mmh! Wewe umejuaje?” japo yalikuwa na ukweli lakini sikutaka kuamini moja kwa moja.

“Nayajua muda mrefu, nilitaka kukaa kimya lakini nimeshindwa kuvumilia moyo unaniuma kwa kujua wewe huna hatia.”
“Mmh! Makubw,a asante shoga,” nilijibu huku nikishusha pumzi ndefu.

“Basi shoga chondechonde usinitaje ili niendelee kuwapeleleza. Hata ukitaka nikupeleke anapokwenda mumeo baada ya kutoka kazini nipo tayari.”
“Nashukuru sana, kwa sasa hebu subiri kidogo.”

Baada ya kupata habari zilizoupasua moyo wangu kwa kisu butu bila ganzi. Mtoto wa kike nilichanganyiki lakini bado sikutaka kuamini moja kwa moja kutokana na maelezo niliyopewa na dada kuwa nyumba yangu haendeshi na mtu wa pembeni.

Usiku wa siku ile wifi zangu walirudi saa nne wakiwa na mume wangu. Nilijikuta nikiona kama yule msichana muongo. Sikutana kuonesha mabadiliko yoyote.

Usiku nilipomtaka kimapenzi mume wangu alinipa kama kawaida. Nilijikuta nikiyakumbuka maneno ya dada kuwa nyumba yangu niiendeshe mwenyewe na mumewe wangu na si kusikiliza maneno ya watu wa pembeni.

Lakini sikutaka kuyapuuza moja kwa moja kutokana na tabia za mume wangu. Siku zilikatika bila kuwepo mabadiliko yoyote. Hali ilikuwa ileile ya siku mojamoja mume wangu kuchelewa kurudi.

Kama kawaida siku moja nikiwa nyumbani peke yangu na wifi zangu wakiwa wamekwenda kwao alikuja yule mdada aliyenipa habari za awali kuhusu mume wangu kutafutiwa mwanamke wa pembeni.

Siku hiyo alikuja na mapya kuwa yule mwanamke aliyetafutiwa mume wangu na familia yake amembebesha ujauzito na kuandaliwa mpango kabembe kuwa siku akijifungua na mtoto kufikisha arobaini basi ndiyo siku yangu ya kuondoka ndani mwangu.
 
SEHEMU YA 12

ILIPOISHIA... Siku hiyo alikuja na mapya kuwa yule mwanamke aliyetafutiwa mume wangu na familia yake amembebesha ujauzito na kuandaliwa mpango kabembe kuwa siku akijifungua na mtoto kufikisha arobaini basi ndiyo siku yangu ya kuondoka ndani mwangu.

SASA ENDELEA...
Nilimkubalia kwa vile sikutana kumbishia kwani siku zote lisemwalo lipo kama halipo linakuja.

Nilishindwa kufanya uchunguzi kuhofia kujiingiza kwenye matatizo ya kujitakia. Japokuwa lilinifukuta moyoni sikutaka kumshirikisha dada na kuamua kufa kizungu na tai shingoni.

Lakini kuna mabadiliko niliyaona ambayo kidogo yalinitia wasiwasi. Dharau za mbali kati ya mume wangu na wadogo zake zilianza kujionesha kitu kilichonifanya nianze kuamini maneno ya yule mdada.

Hali ile vilevile sikutaka kumweleza dada nilikaa kimya nione mwisho wake. Dharau za wifi zangu zikarudi upya na mume wangu aliangalia tu, japokuwa mwanzo aliwakataza na kuwaonya.

Taarifa za kidaku ziliendelea kunipasha kuwa uliandaliwa mpango kabambe siku ya kujifungua ndiyo siku ya mimi kutolewa ndani kwani yule mwanamke akitoka hospitali breki ya kwanza ndani katika chumba changu mimi mgumba.

Kanga za mafumbo zilirudi kwa kasi na kuimbiwa nyimbo nyingi zenye kutia kichefuchefu. Yote nilijitahidi kuyavumilia manyanyaso yalipozidi nilimueleza dada ambaye alinipa moyo na kuniambia nivumilie hayo huwa ya mpito.

Alinieleza maisha ya ndoa yana misukosuko ambayo yanahitaji ujasiri wa hali ya juu na kuwa na moyo wa chuma hasa kuzingatia hali yangu ya kuchelewa kupata mtoto watu huichukulia kama dhambi.

Alinieleza kuwa nimsikilize mume wangu ndiye aliyeniweka ndani na ndiye mwenye maamuzi yote.

Siku moja nililetewa habari ambazo zingeweza kusimamisha mapigo ya moyo wangu mpasha habari wangu aliponiijia na kunieleza. "Shoga una habari mpya?"
"Hata sina."

"Kuna kitu nilikuwa nakichunguza jana nimeupata ukweli.”
“Kitu gani?” niliuliza huku mapigo ya moyo yakiwa juu.

“Basi shoga kumbe yule msichana ujauzito wake una miezi saba na nusu, kuna mpango umeandaliwa siku akiingia nawe utatoka.”

"Usiniambie!" nilihisi kuishiwa nguvu na mwili kunitetemeka hali iliyomtisha shoga yangu na kutaka kuacha kunisimulia.
 
SEHEMU YA 13:

"Basi shoga naona leo mambo sio mazuri moyo wako umekuwa mwepesi."

"Sio mwepesi hata wewe ungeshtuka malizia tu shoga," japokuwa hali yangu ilikuwa mbaya nilijitahidi.
"Basi mpango uliopangwa ni kuwa akijifungua tu na wewe out tena sio siri nashangaa we ndio hujui, kila mmoja anakuonea huruma kwa kitendo cha kinyama wanachotaka kukutendea."

"Mungu wangu! yaani wameisha kuwa miungu wa duniani wananihukumu. Sawa Mungu ndiye anayejua yote namuachia yeye." Huwezi kuamini muda wote wa misukosuko nilikuwa nimebakia mfupa na ngozi.

Hata haki yangu ya ndoa nilipewa pale alipopenda. Kweli nilikuwa nimechokwa na mume wangu kwa kuniambia bila aibu kuwa nimepoteza mvuto.

Pamoja na kupewa haki yangu kwa kupenda lakini nilijikuta nikitokewa na mabadiliko ya hali yangu yaliyonifanya niingiwe na wasiwasi kwa kupita muda bila kuziona siku zangu kwa mwezi wa pili. Wakati huo kutokana na maelezo ya mpasha habari wangu kuwa mwanamke wa pembeni alikuwa amebakiza mwezi mmoja ajifungue.

Hali yangu ilinifanya niende hospitali kufanya uchunguzi wa afya yangu. Majibu ya uchunguzi wa afya yangu yalionesha kuwa nimenasa yaani mjamzito.

Sikuamini kusikia habari zile ambazo kwangu niliziona sawa na ngamia kupita katika tundu la sindano. Nilijua Mungu ameyakomboa maisha yangu kwa kulifanya lile ambalo kwa mwanadamu haliwezekani.

Taarifa nilimfikishia Mume wangu,kwa kweli alishtuka na kusema:
"Muongo mkubwa."
"Ha! Yaani mume wangu badala ya kufurahi Mungu kusikiliza kilio chetu wewe unasema uongo?" nilimshangaa mume wangu.

"Hiyo sio dawa safari ipo palepale."
“Safari! Safari gani?” Sikumuelewa.
“Itaijua muda si mrefu,” Maneno ya mume wangu niliyalinganisha na mpasha habari na kugundua safari niliyoelezwa ndiyo ile.
"Mume wangu ulikuwa na lingine au hilihili?"

"Baada ya kunifanya nikose amani kwa familia yangu sasa unataka kunigombanisha kabisa."
"Mume wangu kukugombanisha kivipi?" nilizidi kuyashangaa maneno ya mume wangu.

"Kwa kuwaeleza uongo."
"Mume wangu ina maana vyeti hivi vinasema uongo?"
"Nitaamini vipi labda umemuhonga daktari ili kukuokoa?"
 
SEHEMU YA 14:

"Mume wangu sikulazimishi kukaa na mimi hata kama utaniacha leo basi uelewe umeniacha na ujauzito wako," nilisema kwa uchungu. "Siamini twende wote hospitali."

Niliongozana na mume wangu hadi hospitali na kuchukuliwa vipimo mbele yake na majibu yalimfanya mume wangu ahudhunike. Lakini hakuomba msamaha nilijua ni kiburi na ubabe. Bila kutarajia nilimwambia neno ambalo lilinitoka mdomoni. "Mume wangu sasa nenda ukawaambie wamlete huyo walio kuandalia."

"Wamlete nani na kina nani?"
"Unawajua na vikao vyenu vya kichawi."
"Naona umenikosea adabu."
"Na nitakukosea sana ninyi si miungu watu?" Maneno yalimuingia mume wangu na hakutaka kusema neno. Tulipofika nyumbani aliondoka bila kuaga. Roho iliniuma na kujikuta nalia peke yangu na kujiona sina thamani tena.

Jioni akili ilinituma nirudi nyumbani kwa dada,nilibeba kila kilicho changu na kupakiza kwenye gari na kurudi nyumbani. Dada aliponiona alishangaa na kunihoji kulikoni:

"Dada nimechoka mimi na shemejio basi."
“Tatizo nini tena?” dada alishtuka kuniona katika hali ile.
“Dada inatosha, nimevumilia lakini sasa to much,” nilisema huku nikilia.
“Kuna tatizo gani hebu kaa kwanza unieleze.”

Dada alinipa glasi ya maji kunywa ili nipunguze munkali, baada ya kutulia kwa muda nilimuelezea yote yaliyotokea baada ya kujingundua nina mimba na maneno aliyosema mume wangu baada ya kumuelezea hali yangu.

Baada ya kumueleza yaliyojili, kabla ya kujibu alishusha pumzi na kusema:
"Hapana mdogo wangu maisha hayaendi hivyo utamfanya Mungu mjinga kwa kukupa kile ulichokiomba kwake kwa machozi ya damu."

“Unayosema ni sawa, lakini thamani yangu ipo wapi? Wacha nife na umaskini wangu, Mungu atanisaidia nitajifungua salama mtoto asiye na baba,” nilisema huku nikiendelea kulia kwa uchungu. “Hukutakiwa kuchukua uamuzi wa kuondoka ulitakiwa uzungumze na mumeo umsikie atasemaje.”

“Hapana dada wacha nipumzike yanayonikuta nimefanya siri vya kutosha lakini sasa nimechoka.” "Mdogo wangu nikikurudisha muda huu nitakuwa sikutendei haki pumzika kwanza.

Ni kweli ndoa ni makubaliano ya mke na mume lakini matatizo yakizidi unatakiwa kupumzisha akili na kutafakari upya."
 
SEHEMU YA 15:

"Dada sina haja ya kutafakari lolote kwa upande wangu ndoa basi...dada nimenyanyapaliwa sana kuchelewa kwangu kupata mtoto.

Nilifananisha na nguruwe kazi yangu kunenepeana bila faida...dada nashukuru nimerudi kwenye hali yangu ya mwili mdogo tena nikiwa mjamzito... “Mungu akijalia nikijifungua salama watamfuata mtoto wao na kulelewa na mama yake mpya."
"Mwanangu una ukweli gani na hayo unayosema?"

"Dada ni mimi tu nilikuwa sijui lakini kila mmoja anaelewa ninavyo nyanyapaliwa..huoni nilivyokwisha kwa ajili ya mateso ya ndoa?" nilisimama kumuonesha dada nilivyokuwa.
"Ni kweli, lakini mpango wao Mungu kaupangua na ukijifungua salama midomo itawashuka."

"Si leo wacha nipumzike kwanza niepukane na karaha za wanadamu huenda wakasababisha kuharibu mimba yangu kwa hasira."

"Pumzika mdogo wangu," dada alikubaliana na mimi. Siku ile nilipumzika kwa dada hata siku ya pili vile vile nilikaa kwa dada. Shemeji yeye alisema nipumzike pale mpaka mume wangu atakaponifuata kama hata kuja basi nitaaendelea kuwepo pale mpaka nitakapojifungua.
 
SEHEMU YA 16

Siku ya tatu mume wangu alikuja na kuniomba msamaha kwa yote yaliyotokea ili nirudi nyumbani kwangu. Nilimkatalia na kumwambia:

"Bado mwezi mmoja mkeo aingie ndani, wa nini mimi mgumba tena tasa ninaye kujazia choo bila faida," maneno makali yalinitoka mdomoni.

"Mke wangu maneno ya watu yatavunja ndoa yetu wewe ni mke wangu tuliyeapa mbele ya Mungu kuwa kifo ndicho kitakacho tutenganisha. Haya unayoyasema niliyasikia mdomoni kwangu?"

“Sijasikia lakini ukweli utabaki palepale.” Siku zote dada alikuwa na maneno ya busara na mumewe,walinisihi nirudi kwangu na kumueleza mume wangu maisha ya ndoa yanavyotakiwa kuwa.
Japokuwa sikuwa radhi kurudi nilikubali kurudi kwa mume wangu kwa shingo upande kutokana na kuwaheshimu dada na shemeji.

Nilirudi kwangu na kuyaanza maisha ya awamu nyingine wakati huo wifi zangu sikuwa na uelewano nao kwa kuwaona wao ndio wabaya wangu.

Kwa vile dawa ya ubaya ni ubaya niliwafurusha wifi zangu kwangu. Mume wangu alipotaka kuwatetea nilimuomba achague kukaa na ndugu zake au akae na mimi.

Mume wangu alikubali kwa shingo upande kuwaondoa dada zake. Hapo awali kabla ya matatizo wifi zangu walikuwa marafiki zangu wakubwa kwa kuwapa chochote wakitakacho hata walichonyimwa na kaka yao.

Lakini waswahili wanasema mfadhili mbuzi utaambulia hata mchuzi, lakini mwanadamu utapata maudhi. Niliapa sitawapa kitu chochote wataula wa chuya kwa uvivu wa kuchangu, hata walipokuja nyumbani walijichekeleza. Sikuwa na mchangamfu nao walipolingudua hilo waliondoka bila kwaheri.

Mwezi mmoja baadaye hawara ya mume wangu alijifungua mtoto wa kike. Taarifa nilizipata kupitia kwa shoga yangu ambaye aliifanya kazi usiku na mchana kama nimemtuma.

Mume wangu aliporudi nilimuuliza kuhusu kuletwa ndani mke mwenzangu na mimi kujiandaa kutoka. Uso ulimshuka hakuwa na jibu, sikutaka kumuudhi sana niliachana na yale na kuendelea na mambo yangu.

Siku zilikatika nami siku za kujifungua nazo zilipokaribia. Nilikwenda kwa dada kwa vile sikuwa na muangalizi kutokana kukosana na mawifi zangu.
 
SEHEMU YA 17:

Nilipofika kwa dada nilikaa siku moja tu, kesho yake majira ya jioni nilishikwa na uchungu na kukimbizwa hospitali ya Sekou Toure.

Mungu alinisaidia nilijifungua salama salimini mtoto wa kike. Mume wangu alifurahi sana na kuniomba msamaha kwa yote yaliyotokea.

Sikuwa na budi kumsamehe pamoja na wifi zangu ambao walikuja kuniangukia. *** Niliyaanza maisha upya na mume wangu na mwanangu mpenzi niliyempa jina la dada yangu Minza. Mwanangu Minza alikuwa vizuri kwenye afya njema. Hali yangu ya mwili ilirudi kama kawaida na kunawili na kunenepa kama mwanzo.

Uhusiano na familia ya mume wangu ulirudi kama mwanzo lakini sikuwaamini kwa asilimia mia kwa vile walikwisha nimulika mchana usiku nilikuwa na taadhali nao.

Baada ya miaka mitatu ambayo naweza kusema ilikuwa mizuri ambayo ilinifanya niifurahie ndoa yangu na kumsifu dada kwa yote aliyochangia kuiokoa ndoa yangu.

Niliamini bila yeye ningekuwa labda nimeolewa na mwanaume mwingine. Mwaka wa tatu nilishika ujauzito mwingine ambao uliongeza mapenzi kwa mume wangu.

Wakati wote wa kulea mimba yangu wifi zangu alinilea kama malkia. Kwa mara ya kwanza nilifurahia ujauzito wangu nikiwa chini ya wifi zangu na kunifanya niyasahau yote yaliyopita.
Muda ulipotimu nilijifungua watoto mapacha wote wa kike.

Ilikuwa furaha kwa familia yote iliyozidi kuongeza mapenzi kwa ndugu na jamaa wa mume wangu ambao mwanzo walijua mimi ni mgumba. Wanangu walikuwa vizuri na afya nje na wenye miili mikubwa. Na mimi hali yangu ya maisha ilikuwa kwa kumpelekea dada pesa ambazo ndizo alizo zilianzisha ujenzi wa siri ambao ulisimamiwa na dada.

Kutokana na uwezo wa mume wangu hasa baada ya kufanya makosa ilikuwa kila nilichokitaka alinipa. Fedha zote alizonipa hakuniuliza hata siku moja nafanyia kazi gani.

Baadaye dada alinishauri nifungue mradi kwa ajili ya kujipanga kwa maisha yangu kama kutatokea matatizo katika ndoa yangu japokuwa sikupoenda yatokee kwa vile mume wangu nilikuwa nampenda sana.
 
SEJHEMU YA 18:

Nilimkubalia dada na kumwambia anifungulie mradi wowote na kumtafuta mtu wa kuusimamia. Alinitafutia miradi kwa kunitafutia fremu za maduka na kunifungulia maduka.

Nami niliendelea kuonesha mapenzi mazito kwa mume wangu japokuwa niliamini kabisa mwanamke wa nje ambaye alizaa naye na mtoto kupewa jina kama la mwanangu.

Mwanzoni aliposikia nilitaka kuchachamaa na kutaka kulibadili lakini dada alisema niachane na kufuatilia mambo ya pembeni.

Niliamua kukaa kimya huku nikiongeza mapenzi kwa mume wangu kwa kujua nina ushindani toka nje kwa mwanamke aliyezaa na mume wangu. Niliamini alikuwa na nafasi kubwa katika familia ya mume wangu kutokana na kukubalika. Lakini dada alinieleza siku zote mwanamke anatakiwa kuyafanya yote muhumu kwa mumewe na wanawe.

Nami niliyafanya yote na kuweza kumdhibiti mume wangu japokuwa kulikuwa na maneno ya chini kwamba nimemuendea kwa mganga kutokana kuwa karibu nami na kunipa kila nilichokitaka.

Niliweza kujitanua kimiradi ambayo ilisimamiwa na mtoto wa kiume wa dada yangu. Mungu alizidi kumuonyesha mume wangu anapoamua hana mpinzani.

Aliniongezea ujauzito mwingine baada ya miaka miwili baadaye kitu kilichofanya mume wangu kuongeza mapenzi mazito na kuninunulia gari la kutembelea la kifahari.

Muda ulipokaribia wa kujifungua mume wangu hakuwepo alikuwa ametoka kikazi na kuniacha katika matayarisho yote muhimu ya kujifungua kwangu.

Siku ilipotimu wifi zangu walisimama kidete na kunipeleka hospitali. Muda ulipotimu nilijifungua salama mtoto wa kike mwenye afya njema. Nikiwa nyumbani baada ya kuruhusiwa kurudi nyumbani, mume wangu alipiga simu na kutaka kujua hali yangu.

“Haloo.”
"Haloo my sweet." Mume wangu alipokea kwa furaha.
"Haloo my Honey."
"Vipi?" aliuliza.
"Safi."

"Umejifungua salama?"
"Salimini mume wangu," nilijibu kwa furaha huku nikikinika vizuri kichanga changu.
"Mtoto gani?"
"Wa kike"
"Duh! Mkosi gani?"
 
SEHEMU YA 19

ILIPOISHIA...
"Umejifungua salama?"
"Salimini mume wangu," nilijibu kwa furaha huku nikikinika vizuri kichanga changu.
"Mtoto gani?"
"Wa kike"
"Duh! Mkosi gani?"

SASA ENDELEA...

"Mkosi wa nini?" sikumuelewa mume wangu alikuwa na maana gani kusema vile.

"Aaa..aa, mke wangu unajua sikupenda kila mara ujifunguapo ninakuwa mbali nawe."

"Mmh! Mume wangu yaani kuwa mbali nami wakati wa kujifungua ni mkosi?"
"Aaa..aa unajua ni ulimi nilitaka kusema nina bahati mbaya," mume wangu alinyoosha kishwahili.

"Pole mume wangu najua ni kuchanganyikiwa na furaha, Mungu kaamua kukufungulia bomba la maji."

"Wanne wanatosha."
"Mimi sina neno ni wewe tu uliyekuwa na haraka ya watoto."
"Basi mke wangu nakuombea afya njema wewe na watoto wetu hasa huyo mgeni wetu."

"Amina mume wangu Mungu atazipokea dua zako." Mume wangu alirudi baada ya siku tatu na kuja kujumuika na familia yake. Ilikuwa nifuraha isiyokifani ya kuungana na familia yake tena, Kwa kweli nilimshukuru Mungu kwa maajabu aliyonifanyia ya kunipatia watoto mfurulizo na kuwafunga midomo walioona labda mtoto wa kwanza nilikuwa nimebabatisha.

Nashukuru maisha yalikuwa mazuri na mimi mambo yangu yalizidi kuninyookea, miradi yangu iliendelea vizuri huku mtoto wa dada yangu akiisimamia vizuri sana.
Naye kwa vile alikuwa akihitaji mahitaji muhimu katika maisha yake.

Muda wa kuoa ulipotimu nilimsimamia kila kitu ikiwa pamoja na kumwacha akae kwenye nyumba niliyomaliza kujenga. Baada ya ndoa ya mwanangu niligundua maisha ya ndoa ni kama msumeno yanakata nyuma na mbele.

Mwanzo nilijua wenye matatizo ni wanaume tu, kumbe hata sisi wanawake tuna matatizo makubwa tena ya kutisha.
Ndoa ya mwanangu ilipotimiza mwaka mmoja ilikuwa na mambo mazito ambayo mengine hayaandikiki gazetini.

Mwanzo aliona aibu kunieleza yaliyoisibu ndoa yake, mengi aliyonieleza yalikuwa ya juujuu. Ajabu matatizo yake yote aliniletea mimi badala ya mama yake ambaye alimuogopa kumwambia.

Nami nilichukua nafasi ya dada, nilimweleza avumilie kwani ndoa inatakiwa uvumilivu wa hali ya juu kwa vile nilijua hata kama atamwacha bado anaweza kupata mwenye tabia mbaya kuliko ya aliyemwacha.
 
SEHEMU YA 20

Baada ya kuona ninambana, ndipo aliponieleza vitu ambavyo niliamini kabisa kama ataendelea kuwa na yule mwanamke basi atakuwa anakitafuta kifo cha lazima.

Yule mwanamke japokuwa alikuwa mwanamke mwenzangu alikuwa malaya mbwa kwa kuchanganya wanaume huku taarifa zenye uhakika zikisema ametoa mimba nyingi za wanaume wa nje iliyopelekea kuharibika mfuko wa uzazi.
Ilionesha tabia hizo alikuwa nazo kabla ya kuolewa.

Mwanzo aliponieleza sikumkubalia kwa kuona kama anamsingizia isingewezekana kufanya uchafu wote ule. Alinihakikisha kuwa kila alichoniambia kilikuwa na ukweli kwani aliisha mfumania na wanaume zaidi ya wanne na mara ya mwisho alimfumania ndani kwa mtu baada ya kukamata ujumbe wa mapenzi ndani ya simu yake bila yeye kujua.

Ili kukubaliana naye nilimchukua mkwe wangu na kwenda kumpima kuhusu kutoa ufuko wa uzazi kwa ajili ya kutoa sana mimba. Ilionekana ni kweli na kukiri kufanya hivyo mbele yangu, lakini aliomba msamaha.

Kwa kweli nilikuwa na wakati mgumu kuivunja ndoa ile lakini niliamini kabisa mwanangu yupo kwenye wakati mgumu. Mpaka kufikia hatua ya kujivua nguo mbele yangu kutoa siri nzito za ndani kuhusu uchafu wa yule msichana, sikuwa na jinsi kumruhusu kuivunja ndoa ile.

Japokuwa ni dhambi kuivunja ndoa ya mtu lakini kwa hali ile ilikuwa haina jinsi kama kumkata kiungo mgonjwa wa kansa. Japo unampunguza kiungo lakini ndiyo pona yake.

Nilisimamia ndoa ile na kuivunja kwa mkono wangu japokuwa dada alijaribu kuiokoa bila mafanikio. Mambo aliyofanyiwa mtoto wa dada yalikuwa hayafai kufanyiwa mwanadamu hasa ndani ya ndoa.

Nilikuwa na wasiwasi na kukutana kwao mpaka kuoana. Niliamini alimuokota changudoa akijiuuza na kuamua kumuoa kwa kuangalia uzuri bila kuijua tabia yake.

Kweli dini inatuzuia kuachana lakini kwa mtindo ule huwezi kukubali kuona nyumba yako inateketea na kuiacha. Lazima utamwaga maji na kuizima, ukikosa maji utatumia hata mchanga.

Kitendo alichotendewa mwanangu kilifanya awachukie wanawake wote na kuapa kuchukua muda mrefu kuoa mwanamke mwingine.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom