Simulizi: Kiu ya talaka

Simulizi: Kiu ya talaka

SEHEMU YA 21:

Najua nimekuhamisha kwenye mkasa wangu baada ya kuingia habari nyingine ambayo niliamini ni lazima nanyi muijue kwani sehemu ya simulizi hii ni kuelezea makosa ya kibinadamu ili ujifunze kupitia makosa yetu.

Waswahili wana usemi kuwa hasidi hana sababu. Mwaka tangu nijifungue kumbe kulikuwa na moto unawaka taratibu, sina habari. Kitendo changu cha kuzaa watoto wa kike kiiuudhi familia ya mume wangu pamoja na mume wangu.

Taratibu wifi zangu wakaanza chokochoko zao kwa kunitolea maneno ya kejeri kuwa nitawazalia watoto wa kike mpaka lini nani atakuwa mrithi wa mali za mume wangu.

Taarifa zilizonifikia kutoka katika chanzo changu makini zilisema, kama nitaendelea kumjazia mitoto ya kike basi si muda mrefu nyumba nitaiona chungu.
Kama kawaida taarifa rasmi ilinifikia kwa kunieleza. Nakumbuka vizuri siku hiyo nilikuwa namuosha mtoto baada ya kumlisha uji.

"Shoga una mpya?" Shositi wangu alianza kuniuliza swali ambalo lilifanya mapigo ya moyo yalipuke kwa kujua kwa ujio ule kuna jambo zito.

"Ipi tena hiyo mpenzi?"
" Mambo yameanza upya."
"Mambo gani?"
"Wanadamu kweli hawana shukrani yaani kila nikiwaangalia wifi zako siwamalizi."
"Kivipi mpenzi?" "Yaani wameanzisha kampeni mpya ya kukutoa tena ndani."

"Ipi hiyo mbona kila kukicha hila za wanadamu zinaongezeka Yarabi." Mapigo ya moyo ulipiga dhahili "Ni hivi baada ya kufeli mpango wao wa kukutoa ndani baada ya kupata mtoto. Sasa wamekuja na mpya eti umewajazia malaya nani atakuwa mrithi wa mali za mumeo.

“Imeanzishwa kampeni nyingine ya kutafuta mtoto wa kiume nje ya ndoa ili kukung'oa ndani."
Habari zile zilinishtua na kuninyima raha. Nilijiuliza kosa langu nini mpaka wanifuatilie maisha yangu.

"Basi ndiyo mpango wao na mumeo siku hizi kila akitoka kazini anaanzia kwa bi mdogo mwingine ndipo arudi kwako. Yamerudi ya wakati ule ulipochelewa kupata mtoto."

Nilijikuta moyo ukiniuma na kuona kila moyo ukitulia wanaanzisha mapya. Nilipanga baada ya kuondoka shoga yangu niende kwa dada kumueleza habari zile. Sikuamini wanangu kuonekana machangudoa, kosa langu nini kuzaaa watoto wa kike?
 
Sehemu ya 22:

ILIPOISHIA…

Nilipanga baada ya kuondoka shoga yangu niende kwa dada kumueleza habari zile ambazo zilikosesha raha. Sikuamini wanangu kuonekana machangudoa, kosa langu nini kuzaaa watoto wa kike.

SASA ENDELEA....

"Basi shoga mpango uliopagwa ndio huo kazi kwako kuupangua kama ulivyo wanyamazisha mwanzo nakuombea Mungu leo kesho ubebe mimba uzae mtoto wa kiume. "

"Mimi sina uwezo mwenye uwezo huo ni Mungu pekee hakuna mwanadamu anayejipangia."

"Lakini Mungu yupo pamoja nawe nakuhakikishia na hili utawaziba mdomo."
"Hata nisipo pata mtoto wa kiume bado Mungu yupo nami."

"Basi shoga ni hayo nami nakuombea Mungu upate mtoto wa kiume."
"Mmh! Shoga hata mwaka ujaisha nibebe tena mimba wacha nipumzike, liwalo na liwe."

Baada ya shoga yangu kuondoka sikukaa kusubiri chochote nilimfua maji mwanangu, mimi kiguu na njia mpaka kwa dada ambaye alishangaa kuniona.
"Vipi mbona hivyo nikikuona upo hivyo najua mambo sio mazuri."
"Dada wee! Unamjuaje mtu akiwa kwenye mabadiliko maana mimi nilipokuja nilikuwa nimeyaficha moyoni."

"Mkubwa yeyote unapokuja jicho lake la kwanza usoni kwa mtu kujua umekuja na heri au shari. Nilipokuangalia tu nimegundua hakuna heri."
“Ni kweli kabisa dada.”
"Mhu! Tatizo nini?”

Sikuwa na kumficha nilimueleza ukweli, baada ya kunisikiliza asema:
"Mdogo wangu jiepushe na maneno ya pembeni siku zote sio mazuri hata kama ni ya kweli yeye yanamuhusu nini.

Hebu fikiria mwenzio baada ya kukueleza yale yupo tuli, lakini wewe presha juu."
"Hapana pamoja yananiumiza lakini yana ukweli asilimia mia moja," nilimtetea mpasha habari wangu.

"Ndio maana nasema yakatae maneno ya pembeni. Hata kama ni ya kweli, yanamuhusu nini, kwani mwenendo wa mume wako unauonaje?"
"Japokuwa anarudi kama kawaida lakini nimesikia kumbe huwa anawahi kurudi na kupitia kwa mwanamke wake."

"Mdogo wangu nakuomba hata kama ni jambo la kweli ambalo hulijui mkomeshe tena akome huyo mletea habari wako. Hata sisi waume zetu walikuwa na makosa yao lakini tuliziba masikio mpaka leo tupo nao.
 
Sehemu ya 23:

“Tungekuwa na akili za kusikiliza kila neno leo hii nisingekuwa na shemeji yako. Najua unatuoana kila siku tunacheka lakini hujui yapo mazito tuliyotumia busara kuyamaliza. "

"Sasa dada huoni kama mtu anaye kueleza ukweli ni mtu mzuri?"
"Mdogo wangu huyo ni nyoka tena mwenye sumu kali, unafikiri ukiachika atakusaidia nini?"
"Sasa dada unanishauri nini?" maneno ya dada yalinichanganya.

"Mpende mumeo kama ilivyo ada usikubali ya kuambiwa siku zote neno la kuambiwa linauma sana. Na siku zote mleta taarifa huongeza chumvi ili zionekane zina ukweli tena amezithibitisha kwa macho yake.

“Jiepushe naye uwe naye kama rafiki lakini maisha yako aachane nayo, kwa vile mzigo wa matatizo baada ya kuachwa utaubeba mwenyewe yeye ataruka futi mia."

"Sasa akija nimwambieje?" Nilitaka ushauri wa dada.
"Akianza tu habari zake mwambie mbona shoga hizo habari ninazo kitambo. Hapo utakuwa umemkata maini na kuona hila zake zimegonga mwamba." Baada ya maelezo ya busala ya dada niligeuza na kurudi nyumbani.

Njia nzima kichwa kilinichemka na kuona dada kama ananilizimisha kuupindisha ukweli.
Niliona pamoja na dada kunieleza yale, hakunisaidia lolote. Nilijua atanieleza cha maana kumbe kumuona shoga muongo.

Nilijiuliza mbona ya mwanzo yote yalikuwa kweli ubaya upo wapi?
Nilirudi nyumbani na kutulia tuli bila kuonesha dalili zozote za mabadiliko. Siku hiyo mume wangu alichelewa kurudi, moyo uliniuma kwa kujua lazima alikuwa kwa mwanamke wake.

Maumivu yalizidi kuongezeka, baada ya mume wangu kurudi alikataa chakula nilichomuandalia kwa kusingizia ameshiba. Nilijikuta nalia peke yangu na kujikuta nakosa raha na kuoina ndoa kwangu jahanamu.

Lakini maneno ya dada kwa upande mwingine niliyaona yana maana kubwa. Nilijiuliza bila shoga yangu kunieleza japamoyo lile nisingejua lolote na moyo wangu ungekuwa kwenye amani.

Siku zote kabla ya kuelezwa yale nilimuamini mume wangu kwa kila alichokifanya na kuniambia. Lakini toka nilipopata siri ya nyuma ya pazia ya mume wangu nilikuwa mtu wa maumivu ya moyo kila dakika moyo haukiisha kunilipuka.
 
SEHEMU YA 24

Nilijiuliza maumivu ya moyo ninayoyapata ni kwa ajili ya maneno ya shoga yangu japokuwa niliyaamini kwa asilimia mia na yalikuwa na ukweli mtupu.

Kwa kweli siku ile sikupata usingizi nilijigeuza kitandani kama nimelalia miba. Nilijiuliza nimpelekee nani mambo yangu ikiwa dada yangu hataki kunisikiliza.

Niliamini hata kama ningerudi na kumueleza tabia za mume wangu zinazojionesha bado angenieleza niendelee kuvumilia wakati maumivu moyoni mwangu ni makubwa.

Alfajiri iliingia naiona, niliamka mapema na kwenda zangu nje kufanya usafi wa nyumba, kwa vile mawazo yalinifanya nikione kitanda kama kina moto.

Kutokana na kutigwa na mawazo mengi hata kumuandalia mume wangu maji ya moto ya kuoga nilisahau. Alinifuata nje kunishtua mtoto ameamka, kutokana na donge kukikaba kooni hata kumsalimia nilishindwa.

Mume wangu baada ya kuoga maji ya baridi aliniachia fedha ya matumizi juu ya meza na kunifuata nje kuniaga nilipokuwa nafanya usafi na mtoto mgongoni.

“Mi’ natoka.”
Nilimuitikia kwa kunyanyua kichwa, kutokana na maumivu makali moyoni nilishindwa kuzungumza. Alipoondoka niliacha kufanya usafi na kuingia chumbani kwangu na kuanza kulia huku nikiapa siri zangu sitamwambia mtu yeyote nitakufa kizungu na tai shingoni.

Siku zilikatika mabadiliko ndani yalikuwa makubwa, mume wangu alinieleza kuwa nisiache chakula cha usiku nilipohoji aliniambia kila jioni ofisini kwao wana semina ambayo huisha usiku na kupata chakula kabisa.

Nilishindwa kumkatalia kwa vile sikuwa na tabia ya kubishana na mume wangu. Tangu niolewe sikuwahi kumchunguza mume wangu. Baada zoezi la kuacha kula usiku kufanikiwa alianza tabia mpya ya safari za kikazi nazo zilikuwa haziishi.
Kama kawaida shoga yangu hakuacha kuja kunipasuka moyo. Siku za kawaida nilikuwa simuoni lakini pakitokea jambo alitokea kama mtoa roho.

Nilipo muona moyo ulinilipuka na kutaka kujua kuna jambo jipya la mume wangu. Nilikaa mkao wa kutaka kujua kuna nini.
Alipofika baada ya salamu akaanza kumwaga mchele kwenye kuku mmoja.
“Shoga za siku?”
 
SEHEMU YA 25

ILIPOISHIA

Nilipo muona moyo ulinilipuka na kutaka kujua kuna jambo jipya la mume wangu. Nilikaa mkao wa kutaka kujua kuna nini.
Alipofika baada ya salamu akaanza kumwaga mchele kwenye kuku mmoja.
“Shoga za siku?”
“Shoga za siku?”

SASA ENDELEA...

“Nzuri, mbona umenitupa?” nilimuuliza huku nikilazimsha tabasamu.
“Nilitoka kidogo nilikwenda shamba nimerudi juzi usiku.”

“Mmh! Karibu, najua una mapya maana nikikuona moyo wangu hautulii.” "Shoga yangu wee! Mambo kila kukicha yanazidi kuwa mabaya.”

Kauli ile ilifanya moyo wangu unywee na kufanya nisikie kama umepasuka na kumwaga damu ya baridi iliyofanya nisikie baridi ya ghafla.

Niliyakumbuka maneno ya dada ya kumkanusha lakini nilishindwa. Pamoja na kuelezwa nisimsikilize lakini hamu ya kumsikiliza ilinipata na kutaka kujua anataka kuniambia nini.

Nilipiga moyo konde na kumuuliza:
"Mambo gani tena Yailahi mbona mwaka huu nitakufa kwa kihoro?"
"Yaani shoga nimeamini wanaume watu wabaya sana."

"Kwa nini?"
"Kwanza shemeji yupo wapi?" aliuliza kwa sauti ya chini yenye mashaka.
"Yupo kazini."

"Kazini ofisini au kasafiri?" aliniuliza swali kama ameona ninamdanganya.
"Mbona unanitisha kulikoni?" alinishtua.
"Ndio maana nikasema wanaume ni wauaji tena wana sumu kali kama ya nyoka."

"Mbona sikuelewi?" nilishindwa kumuelewa ana maana gani.
"Basi unajua juzi nilipokuja ukanieleza mumeo amesafiri, nilikubali lakini mtandao ulimkamata kumbe sasa hivi amehamia kwa bi mdogo tena ana tumbo la leo la kesho."

"Mmh! Utani huo!"
"Basi muda wote yupo na huyo mwanamke ambaye amempangia nyumba nzima. Na sasa safari zitazidi kila kukicha."

"Mungu wangu! Mbona nanyanyaswa hivi mtoto wake?" niliuliza huku nikinyanyuka mkono kiunoni.

"Sikiliza Eliza nawe umezidi upole kama upo tayari nitakupeleka mpaka alipo mumeo.Tena nitakusaidia kumfundisha adabu huyu mwanamke. Ndiyo tabia yake kuwachukua waume za wenzie."

"Yaani we niache tu, hata nguvu zenyewe zimeyeyuka zote," nilisema huku nikirudi kitini na kujilaza.
"Sasa nikusaidieje?" shoga yangu aliuliza.

Baada ya kukaa na kutafakari maneno ya dada na kuamini kabisa niliyekuwa naumizwa na hali ile ni mimi mwenyewe. Nilijua nikimpiga marufuku nitakuwa na amani ya moyo.
 
SEHEMU YA 26

Japokuwa moyo ulikuwa na aibu nilijikaza na kumueleza:
"Ni hivi shoga, nakuomba kuanzia leo hii, lolote linalo muhusu mume wangu kama unalijua liishie huko huko. Naomba leo iwe mwanzo na mwisho kuniletea habari za kizushi."
"Ha! Ishakuwa hivyo?" shoga yangu alishtuka.

"Wewe si rafiki bali adui yangu, huwezi kila siku kuniumiza roho, wewe unatoka moyo wako tuli. Naomba leo iwe mwisho na kwangu nisikuone," nilimweleza makavu bila aibu.

"Basi nisamehe shoga, nia yangu haikuwa kukuumiza moyo bali kukueleza ubaya wa wifi zako na jinsi wanavyokuzunguka," aliniomba msamaha.

"Nimekusamehe ila ushoga basi."
“Naomba ushoga ubakie ile kila nitaloliona litabakia siri yangu.”
“Sasa ndiyo itakuwa nini ndiyo kuja kuning’onga?”

“Hapana shoga.”
“Naomba tu uondoke kwa vile sitakuelewa kwa lolote, umekuwa chanzo cha mateso ya moyo wangu.”

Pamoja na kuniomba msamaha sikumkubalia zaidi ya kuuvunja ushoga rasmi japokuwa moyo ulinisuta.
Pamoja na kuuvunja ushoga lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote. Tabia za kuchelewa kurudi ziliendelea kukomaa. Mwanzo mume wangu alikuwa akiniomba msamaha, lakini ilipotea taratibu na kukaa kimya.

Alipochelewa kurudi ilionekana hali ya kawaida, nilishindwa kumuuliza kwa vile ile haikuwa tabia yangu niliyokuwa nayo na mafunzo niliyopewa na dada.
Hakuishia katika kuchelewa kurudi tu akanzisha tabia nyingine ambayo ilinifanya kila usiku ukiingia nilie peke yangu.

Mume wangu bila huruma kwa mateso aliyonipatia akaanza kulala nje na akirudi kwake aliona jambo la kawaida tu.
Niliumia mtoto wa kike na kupoteza uzito mwilini kwa mawazo. Kila nilipopata wazo la kwenda kumueleza dada tabia za mume wangu moyo uliingia kiza kwa kujua lazima nitapigwa siasa tu.

Nilijiuliza kama wote wanapata misukosuko katika ndoa zao kama mimi, Nilikuwa na maswali mengi kichwani mwangu kwa kujiuliza dada naye alivumilia matatizo kama yale.
Niliamini kama aliweza kuvumilia mateso yale ambayo hayakuwa tofauti na mtu kupasuliwa moyo bila ganzi kwa kisu butu. Basi lazima alikuwa na moyo wa chuma si wa nyama kama wangu.

Nilijiuliza ina maana hivyo ndiyo wanaume wote wanavyokuwa kwa wake zao na wanawake nao
 
SEHEMU YA 27:

kuvumilia mateso yale na nyumba yao kujaa furaha siku zote.
Pamoja na kufunga milango ya kupokea umbea juu ya mume wangu, nilikuwa najua ana mwanamke na ni mjamzito. Siku zote sikio halilali njaa.

Nilipata taarifa kuwa hawara wa mume wangu amejifungua mtoto wa kiume. Kutokana na maneno aliyonieleza shoga yangu niliyempiga marufuku, nilijua kama nilivyo ahidiwa basi safari yangu ilikuwa imeiva.

Baada ya taarifa ile ilipita miezi mitatu bila kuonekana kitu chochote lakini tabia za mume wangu hazikubadirika kula nyumbani alisahau kulala ndani ilikuwa mara mbili kwa wiki. Niliendelea kuyavumilia kwa vile nilijua yana mwisho.

Siku moja majira ya asubuhi nikiwa na wanangu tukipata kifungua kinywa. Ghafla waliingia wifi zangu bila hodi.

Sikutaka kuwauliza chochote niliwakaribisha chai. Lakini hawakuonesha kunijali zaidi ya kusema kwa majigambo: "Hukumu imetimia." Nilijiuliza hukumu ipi hiyo, bila hata ya kunisalimia nilishangaa kuwaona wakiingia chumbani kwangu.

Sikutaka kubishana nao siku zote nilielezwa kuwa ukiona kimbunga kipishe usipambane nacho kinaweza kukuzoa na kunitupa mbali. Nilitulia nione wanataka kufanya nini.

Baada ya muda nilishangaa kuona vitu vyangu vikitolewa na kuhamishiwa chumba cha watoto. Hatua ile ilinifanya nishindwe kuvumilia nilinyanyuka na kuwauliza:

"Hei! Jamani mbona hivyo?"
"Utawala wako umekwisha uliruka ile na hii ruka tena." Wifi yangu alijibu kwa majigambo huku akielekea chumba cha watoto wakiwa amebeba kapu la nguo za watoto.

"Mbona siwaeleweni?" niliuliza nikiwa nimesimama bila kuwagusa.
"Utatuelewa tu, we si kenge husikii mpaka utoke damu masikioni sasa utasikia." Wifi yangu mdogo alinijibu maneno ya shombo. Pamoja na kuwa wifi yake lakini hata kiumri alikuwa hanipati. Maneno yale yalinipandisha hasira baada ya kuona dharau ya waziwazi.

"Naomba mtoke chumbani kwangu," nilisema huku niliwafuata chumbani.
"Hiki si chumba chako tena, sasa utalala na watoto." Nilijikuta napandwa na hasira na kutaka kukamatana na wifi zangu, lakini niliogopa wangeniumiza kwa sababu walikuwa wengi. Nilijikuta nikikubali yaishe na kusubili nione mwisho wao nini.
 
SEHEMU YA 28

Nilisubiri nione nini kinaendelea, baada ya kuondoa vitu vyangu vyote walifanya usafi wa chumba kizima. Baada ya saa moja na nusu nilisikia sauti ya gari nje, nilitulia sebuleni na wanangu ambao walikuwa bado hawajaelewa kitu.

Nilimkumbuka shoga yangu pamoja na kumuona mbea bado alikuwa na umuhimu kwangu. Kama ningekuwa naye karibu ningeweza kunipasha mpango ule ambao ningekabiliana nao kabla ya kudhalilishwa vile.

Wifi zangu walitoka nje na kurudi na mizigo waliyoiingiza chumbani kwangu kikiwemo kitanda cha mtoto mchanga. Mara nilisikia: "Karibu malkia wetu," alisema wifi yangu huku akifungua mlango.

Mara aliingia mume wangu akiwa amempakata mtoto mchanga akiwa ameongozana na mwanamke mmoja aliyekuwa amevalia vazi la kitenge kuanzia chini mpaka kiremba.

Sikusema kitu japokuwa niliwaona wifi zangu walikuwa wamejiandaa kwa shari. Sikunyanyua mdomo wangu niliwaangalia wafanye watakavyo.

Baada ya mwanamke wa mume wangu kuingia ndani. Wifi zangu waliingia jikoni na kuanza kumuandalia chakula cha mchana. Walikuwa wamekuja na vyakula vyao kabisa kazi ilikuwa kuingia jikoni na kupika tu.

Niliwachukua wanangu na kujifungia ndani na kuanza kulia huku nikisaidiwa na wanangu. Kilio cha wanangu kilinifanya ninyamaze na kuanza kuwabembeleza kwa vile hawakujua mama yao nalilia nini.

Roho iliniuma na kuona la muhimu ni kuondoka kurudi nyumbani kwa kuwa sikuwa na mapungufu kwenye maisha yangu. Niliamini hata dada asingeweza kuvumilia hali ile. Nikiwa bado nimekumbatiana na wanangu nilishtushwa na mlango uliokuwa ukigongwa.

Sikunyanyuka mpaka niliposikia sauti ya mume wangu.
Nilinyanyuka huku nikifuta machozi na kwenda kufungua mlango. Nilipofungua mlango nilikutana na mume wangu ambaye aliyaona machozi yangu na kuniuliza: "Sasa unalia nini?"

"Yaani umeamua kunifanyia hivyo mume wangu?" nilijikuta nikilia upya.
"Kipi cha ajabu?"
"Hakuna cha ajabu?" nilimuuliza mume wangu macho yamenitoka pima.
"Sasa kinacho kuliza?"
 
SEHEMU YA 29:

Mume wangu aliniuliza bila huruma, hakuwa ninayemfahamu, mpole na mwenye huruma, aliyejali machozi yangu. Lakini aliyekuwa amesimama mbele yangu, alikuwa mwingine aliyenigeuka kwa ajili ya kuifurahisha familia yake na kusahau tulipotoka mimi na yeye.

"Mume wangu unadiliki kumtoa chumbani mke wako wa ndoa na kumuingiza malaya ndani?"

Nilisema kwa uchungu huku nikiendelea kulia, kwa kweli moyo uliniuma kama umepasuliwa.
"Basi huyo unaye muona malaya ndiye mwenye thamani kwenye familia yangu," mume wangu alisema kama amelewa pombe.

"Thamani gani kuliko mke wako wa ndoa, nimekuzaliwa watoto wangapi mume wangu, leo hii umewaona si kitu?"
"Hivi wewe mwanamke ni nani aliyekuambia hapa nataka kufungua baa au grosary?"

"Una maana gani kusema hivyo mume wangu?"
"Nani amekwambie nina shida ya mitoto ya kike ndio mwanzo wa kugeuza kituo cha kulea watoto wasio na baba wala hakuna mrithi wa mali zangu."

"Mume wangu nani aliyekwambia mtoto wa kike arithi mali za wazazi wake?"
"Mrithi siku zote ni mtoto wa kiume na ndiye aliyeniumiza kichwa na sasa amepatikana, mama aliyemletea ndiye mwenye thamani kwangu."

"Mume wangu hata dini inakataza kutoka nje ya ndoa, umemkosea Mungu wako umenikosea mkeo, umewakosea wanao bado unamleta ndani. Kibaya zaidi unanitoa chumbani kwangu, kweli mume wangu?" nilimuuliza kwa sauti ya kilio.
"Hiyo unajua wewe, ni nani aliyekuambia yaliyoandikwa kwenye vitabu yanatoka kwa Mungu?"
 
SEHEMU YA 30

Nilishtuka kuona mume wangu amechanganyikiwa kufikia hatua ya kukikana kitabu kitakatifu kwa ajili ya kuharalisha dhambi zake.

"Leo hii usaliti wako umekufanya umsaliti Mungu wako, lakini kumbuka ghadhabu ya Mungu huwezi kuizuia mume wangu. Chezea vyote si muumba wako," nilimtaadhalisha mume wangu ambaye nilijua amepotea.

"Sasa tuachane na hayo, sikufuata kuhubiliwa injili hapa. Kilichonileta ni kukujulisha kuwa kuanzia leo mgeni ndiye atakaye kuwa na madaraka kwenye nyumba hii wewe utakuwa chini yake."

“Hivi mume wangu unazungumza kutoka mdomoni mwako au kuna mtu anakusemea?” “Nimekueleza sikuja kusikiliza mahubiri na kujibu maswali kila kitu nimemaliza, kinachotakiwa utekelezaji tu.”

Yalikuwa maneno makali kama kumeza moto au kuuchokonoa moyo wangu kwa mdenge. Nilipandisha pumzi na kujibu kwa sauti ya kilio.

"Sa..sa.aa.awa, Mungu kama ni huyuhuyu malipo ni hapahapa duniani."
"Hayo unajua wewe na huo ndio uamuzi kuanzia sasa na mambo yote utamfuata yeye na kukupangia."

Unajua mambo mengine unaweza kuona kama maigizo kama hayajakukuta unaweza kusema uongo. Lakini likikukuta utaamini, sipendi yakukute yaliyonikuta. Ila muombe Mungu akupe mume wenye kuijua thamani ya mke.

"Sawa hakuna tatizo mume wangu." Nilijibu huku nikifuta machozi kwa kuamini hata kama ningelia machozi ya damu isingebadilika. Baada ya kuondoka nilirudi kitandani na kukianza kilio upya.
Safari ile sikusikiliza kilio cha watoto, nililia mpaka uso na macho yakanivimba. Ndani palikuwa kama kuna msiba mpaka mume wangu alipokuja na kunieleza niache uchimvi, mwanaye akifa nitamla nyama.

Nilinyamaza na kutoka hadi sebuleni na kukuta hali ya sebuleni imebadilishwa na kupangwa tofauti na nilivyo panga mimi. Tena wifi zangu walikuwa kama wasichana wa kazi, tena walifanya kazi kwa furaha huku wakisimamiwa na mwanamke wa kaka yao.
 
SEHMU YA 31

Nilipopita nimeongozana na wanangu yule mwanamke alinibinulia mdomo na kutema chini. Sikujali niliwachukua wanangu hadi nje na kumuomba dereva anipeleke kwa dada.

Lakini dereva alisema kuwa amekatazwa kusikiliza amri ya mtu yeyote zaidi ya mwanamke mgeni. "Mama wacha nikamuombe ruksa ya kukupeleka mjini," dereva alisema huku akiwa na aibu.

"Hapana Salumu wacha tu tutapanda daladala." Nilimwambia vile kwa kujua thamani yangu haipo tena, hivyo naweza kujibiwa majibu yatakayoongeza maumivu moyoni mwangu. "Hapana mama wacha nikachukue ruhusa nikupeleke kwa nini upande daladala wakati magari yapo?"

"Salumu we acha tu."
"Kwani mama imetokea nini?" Salumu alitaka kunidadisi.
"Hakuna lolote," sikutaka kumwambia kitu nilijua atayajua baada ya mimi kuondoka.

"Sawa mama, au nikupeleke tu kwani hata nikikupeleka atanifanya nini?" dereva alitaka kujitoa muhanga.

"Salumu nashukuru kwa msaada wako, najua unani thamini." Niliagana na dereva wetu ambaye alikuwa kwenye maswali mazito yasiyo na majibu. Nilikwenda hadi kituo cha teksi na kukodi gari hadi kwa dada.

Aliponiona alishtuka sana na kuniuliza kulikoni maana kila kukicha yanazuka mapya yaliyomfanya naye moyo wake kukosa amani. "Mmhu! Lete taarifa au shoga yako kayaleta mapya? Maana leo nakuona na watoto?" dada aliniuliza mkono kiunoni bila hata ya kunipokea mizigo.

Nilimueleza yote yaliyonisibu na kumfanya dada abakie kinywa wazi baada ya kutulia kwa muda alisema: "Yote ilikuwa lele sasa ndiyo ngoma kamili, yaani mumeo amefikia hatua hiyo? Kwa hiyo amekufukuza?"
"Hapana."

"Ila?"
"Kwa hali ile sio lazima ufukuzwe."
"Sasa sikiliza mdogo wangu suala hili ni zito, kabla ya kukupokea nakushauri kwanza kabisa muda huu bila kupoteza wakati nenda kwao na mumeo uwasikilize wanasemaje, ndipo nasi tutakuwa na la kusema."
 
SEHEMU YA 32

ILIPOISHIA... "Sasa sikiliza mdogo wangu suala hili ni zito, kabla ya kukupokea nakushauri kwanza kabisa muda huu bila kupoteza wakati nenda kwao na mumeo uwasikilize wanasemaje, ndipo nasi tutakuwa na la kusema."

ENDELEA...
“Dada nikafanye nini, ikiwa mpango mzima inaonekana wazi umefanywa na familia ya mume wangu?”

“Sikiliza mdogo wangu siku zote usimuhukumu mtu bila kujitetea. Tatizo la mumeo lipeleke kwao wakishindwa lilete kwetu.”

"Sawa dada nimekuelewa." Maneno ya dada siku zote yalijaa busara japokuwa wakati mwingine yalinizuia kujua mambo mengi. Baada ya kukubaliana na dada nilikodi gari mpaka kwa wazazi wa mume wangu.

Bahati nzuri niliwakuta wazazi wake wote. Waliponiona walinikalibisha na kunishangaa na hali niliyokuwa nayo. Bila kupoteza wakati niliwaeleza yote yaliyonisibu. Cha kushangaza wote walionyesha kushangazwa na habari zile na kuniambia nipumzike ili wafanye utaratibu wa kumwita mume wangu.

Nilitulia uwani kwenye mkeka chini ya mti kumsubiri mume wangu. Nilijiuliza mume wangu atajibu nini kwa wazazi wake kama wataamua yule mwanamke aondoke.

Moyoni nilijiapiza kama nitarudi kwangu basi wifi zangu sitawasaheme pia ningewapiga marufuku kuwaona kwangu wala kuzungumza nao kwa vile niliamini wao ndiyo wanaompapu mume wangu na kuiharibu nyumba yake.

Nikiwa nimekaa na wanangu huku mdogo akiwa amejilaza miguuni kwangu, mume wangu aliwasiri. Alinipita bila kunisalimia na kuingia ndani, kitendo kile kilizidisha machungu moyoni mwangu.

Mume wangu kuniona kama mtu baki si mkewe wa ndoa. Nikiwa katikati ya mawazo niliitwa ndani, nilinyanyuka na watoto wangu. Kwa vile mdogo alikuwa amepitiwa usingizi alichukuliwa na bibi yake kwenda kulazwa ndani na mimi kwenda sebuleni.

Sebuleni alikuwa mume wangu na wazazi wake. Baada ya kuketi kwenye kochi la mbali na mume wangu baba mkwe aliniita.
“Mama,” jina ambalo alipenda kuniita baada ya mtoto wangu wa kwanza kumwita jina la mama yake.

“Abee baba.”
“Hebu elezea kilichotokea na kukufanya ondoke kwako na watoto?”
Nilielezea yote bila kuacha moja kwani ilionekana mengi yaliyotokea wakwe zangu walikuwa hawajui japokuwa niliamini mama mkwe alikuwa akijua kila kitu.
 
sehemu ya 33:

Kwa vile baba mkwe alitaka kujua nilianzia mbali kuelezea kutokea sijapata ujauzito na tabia za wifi zangu pamoja na mume wangu kwa kuninyanyapaa kutokana na kuchelewa kupata mtoto.

Niliendelea kueleza baada ya Mungu kusikia kilio changu na kuweza kupata watoto hali ilivyogeuka tena na tukio la siku ile la kuondolewa chumbani kwangu na kuingizwa hawala.

“Mmh!” baba mkwe alishtuka kama anatoka usingizini na kumtazama mwanaye na kumuuliza.

“Anayosema mkeo ni kweli?” alimuuliza akiwa amemkazia macho. "Wazazi wangu najua mnajua vizuri jinsi nilivyo umia na mrithi wa mali zangu. Kila kukicha mke wangu ananijazia mitoto ya kike anafikiri mimi nataka kufungua baa, grosary au danguro..." Nilijikuta namkata kauli mume wangu baada ya maneno yake kunichoma:

"Mume wangu ni maneno gani hayo, yaani leo hii wanangu umewabashilia kuwa mabaa medi au machangudoa kwa lipi hasa. Ina maana hawatasoma na kuwa na nyadhifa serikalini?"
"Labda serikali yako ya mabaa medi au machangudoa," mume wangu alijibu bila kuogopa anazungumza mbele ya wazazi wake.

"Kweli mume wangu umenichoka, asante sana." Baada ya kusema yale nilinyanyuka ili niondoke lakini baba mkwe alinirudisha na kusema:
“Hebu rudi kwanza mama,” alinyanyuka na kunishika mkono.

Lakini niliukwepesha mkono wangu huku nikisema kwa sauti ya kilio.
“Hapana baba niache niondoke nina imani kauli ya mume wangu ni ushahidi tosha kwa yote niliyowaambia.

Wacha nikatengeneze serikali ya mabaa medi na machangudoa.”
“Hapana mama, punguza munkari, umeleta mashtaka hujasikia sisi wazazi tunasemaje?”
“Baba kama mume wangu kasema hivyo kuna nyumba tena?” niliuliza huku nalia.
 
SEHEMU YA 34:

“Hapana hebu kaa kwanza,” baba mkwe alinirudisha na kunikarisha kitini.
Kutokana na kumuheshimu yule mzee nilirudi na kukaa huku nikilia kilio cha chinichini. Nilimsikia baba mkwe akimwita mwanaye.

“Kijoki.”
“Naam baba,” mume wangu aliitikia. "Mwanangu katika siku umetukosea adabu wazazi wako toka utoke tumboni kwa mama yako ni leo au kwa sababu ya vijipesa zako.

Yaani umefikia hatua ya kuwaita wajukuu wangu mabaa medi na machangudoa? “Siamini kitendo chako kinatuweka wapi mbele ya familia ya mkeo? Watatujua sisi wote ni wahuni na familia yangu wote wahuni," baba mkwe alisema kwa uchungu mpaka povu la mdomo lilimtoka.

"Lakini baba wewe unasema hivyo, suala hili hata mama anajua." Kauli ile ilifanya moyo upige pa! Na kushika mikono kifuani kwa mshtuko baada ya kupata ukweli wa lile nililoliwaza mwanzo juu ya uratibu ya mambo yale kufanywa na familia ya mume wangu.

"Ndiye aliye kwambia uwaite wajukuu zangu mabaa medi na machangudoa...Eti mama Kijoki?" baba mkwe niliamini alikuwa hajui kitu kwani alizungumza huku jasho likimtoka na povu mdomoni. Alimgeukia mkewe na kumuliza.

"Mmh! Ha..a.a..pana, we mtoto usinigombanishe na baba yako!" mama mkwe aliruka futi mia.
"Baba hili siyo jambo la siri tulikubaliana kutafuta mtoto wa kiume ili awe mrithi wangu," mume wangu alianza kumwaga mchele kwenye kuku.

"Yaani kweli ninyi ni wapumbavu wa hali ya juu, nani alikwambia mrithi wa mali ni mtoto wa kiume tu? Kama hukuzaa mwanaume mali yako inakwenda wapi?" Kauli ya baba mkwe japo sikujua hatma ya kikao lakini moyo ulipata farijiko.

"Baba Kijoki usimlaumu mtoto ameisha kosa la muhimu ni kumkosoa ili asirudie makosa," mama mkwe alimtetea mwanaye.

"Asirudie nini? Kama kuzaa nje ya ndoa halifutiki, kitendo kile ni dhambi kubwa. kibaya zaidi ..Mwanangu unadiliki kumfukuza mkewe wa ndoa kwenye chumba chake kwa ajili ya hawala wako?

“Haya ni matusi makubwa kwa familia yangu pia umeidhalilisha wa haki ya mwanamke tena kuwadharau wote walipoteza muda wao kuja kwenye harusi yako, mchungaji aliyefungisha ndoa.
 
SEHEMU YA 35

“Mwanangu umemdhalilisha mkeo kiasi gani? Umewakosea kiasi kikubwa sana wanao, sijui wakikuwa utawaeleza nini na kauli yako chafu kama choo kisicho na uangalizi, watu wanajisaidia ovyo bila mpangilio?" baba mkwe alisema mpaka mishipa ya kichwa ilimsimama.

"Baba Kijoki ni maneno gani hayo? Mwanao amekosa hata ukisema nini maji yameisha mwagika hayazoleki. Kinachotakiwa ni kumuelekeza ili asirudie makosa yake," mama mkwe aliendelea kumtetea mwanaye.

"Mmh! Sasa nimeelewa kumbe mbaya wa ndoa ya mwanangu si mwanangu bali wewe mke wangu. Sasa ni hivi ngoja nimalize haya nina kazi na wewe, yako yanakushinda unaingilia maisha ya mwanao? Mwanamke mbaya wewe!"

Baba mkwe alisema kwa uchungu mkubwa.
Nilitamani kwenda kummbeba juu kwa furaha alipokuwa amesimama akilanda kwa hasira kama nyati aliyejeruhiwa.
"Baba Kijoki yamekuwa hayo?" mama mkwe alitahayali.

"Kwanza funga kopo lako chafu, na ukizidi nitakugeukia na kukutandika mbele ya watoto.

Mwanamke mbaya wewe usiye na haya. Kumbe wewe ndiye chanzo cha yote." Kwa kweli nilijikuta najilaumu kwa kutofikisha matatizo yangu kwa baba baada ya kuona mama mkwe na wifi zangu wakinigeuka. Ilionesha jinsi gani baba mkwe alivyo na msimamo thabiti juu ya ndoa. Mama mkwe aliufyata kama sio yeye. “Nauliza huyo mwanamke yupo nyumbani kwako?”

“Ndiyo baba.” "Nasema hivi, ukitoka hapa ukauondoe uchafu wako sitaki kuuona na hao dada zako wamekosa adabu kiasi gani kufikia hatua ya kuingia chumba cha wifi yao bila idhini yake.

“ Kijoki mwanangu niliyekutegemea kuiongoza familia yangu baada ya kufa, lakini kabla sijafa umeonesha udhaifu mkubwa. Unashikwa maskio na mama yako?

“Hivi ndivyo nilivyokufundisha uishi kwa mtindo huo wa kukosa adabu wa kutoheshimu ndoa hata kutoithamini damu yako na kuamini watakuwa mabaa medi na machanguduo?

“Nasema hivi hao wadogo zako waliokosa haya watarudi watanikuta, leo watatafuta pa kwenda naona wamenisahau. Kati yao hakuna hata mwenye mtoto wacha wa kike hata wa kusingiziwa.

“Huyo mume tu kwao kitendawili waolewe na nani kwa tabia zao mbaya kama hizo, yao yamewashinda wanaingilia ndoa ya wenzao. Kijoki umenielewa?”
 
SEHEMU YA 36:

“Nimekuelewa,” mume wangu alikuwa mpole kama kanyeshewa mvua.
“Na sitaki kusikia ujinga huu tena!”
“Sawa baba,” mume wangu alijibu ameinama kama kondoo.

Baada ya kusema yale alinigeukia mimi niliyekuwa nimewapakata wanangu. “Samahani sana mama kwa yote yaliyotokea, kwa nini ulikaa nayo haya muda mrefu kwa nini hukuja mapema mwanangu? "

“Baba nilichanganyikiwa.” "Pole sana mama, lakini nimeisha mjua mchawi wa ndoa yako. Niliyasikia nakayadharau kumbe yalikuwa na maana yake. Leo ndio nimesadiki mvunja nchi ni mwananchi... Mwanangu rudi kwako nakuhakikishia nitakuwa na wewe muda wote," baba mkwe alikata mzizi wa fitina.

"Asante baba kwa kuliona hilo, ni mengi sikujua kumbe yote ningeyaleta kwako."
"Mwanangu yote nayajua niliwaonya, kumbe walifanya mambo yao kwa siri, sasa nasema kwanza sipendi kuongea mengi...Mama niache niongee na hawa washenzi wa tabia kapumzike nje na wanao."

Nilitoka nje na kuwaacha mume wangu na wazazi wake kwenye kikao cha dharura. Baada ya nusu saa mume wangu aliondoka bila kuniaga. Baada ya muda niliitwa na baba mkwe na kunieleza:

"Mama nimemtuma akarudishe vitu vyako ndani na kisha auondoe ule uchafu ili urudi chumbani kwako, pole sana mwanangu. Lakini kwa nini hukuja kunieleza mapema?" baba mkwe alirudia swali lake la awali.

"Kutokujua baba." Nilishinda ukweni mpaka jioni na kufuatwa na dereva wetu Salumu, aliyenichukua na kunirudisha nyumbani kwangu. Njiani Salumu aliniuliza maswali:
“Mama mbona mpaka sasa sijui, kwani kuna nini?”

“Kwani vipi Salu?”
“Asubuhi aliondoka na kuonesha kuna tatizo baada ya kuingia yule mwanamke. Huwezi kuamini muda mfupi aliishaanza kuwa kero. Mchana aliporudi baba na nilishangaa kuona vitu vya yule mwanamke vilivyoingizwa asubuhi vikitolewa ndani na kupandishwa kwenye gari na wote kuondoka.

“Baada ya muda walirudi wifi zako na kupanga vitu ndani kisha nao wakaondoka ndipo nilipoambiwa nikufuate kwani kuna nini?”

“Utajua tu Salumu, usiwe na haraka.”
Salumu aliliponifikisha nyumbani, niiingia hadi chumbani na kukuta vitu vyangu vimerudishwa bila kupangwa. Niliingia kazi ya kuvipanga na kugundua vitu vyangu vingi vimechukuliwa, lakini sikujali sana.
 
SEHEMU YA 37:

Baada ya kupanga vizuri chumba changu niliingia jikoni kuandaa chakula cha wanangu ambao muda wote hawakupata chakula cha haja.

Usiku wa siku ile nililala peke yangu mume wangu hakurudi, hiyo haikunishtua nilijua ni kawaida yake. Kwa vile ilikuwa mapema niliona aibu kwenda kumueleza baba mkwe.
Siku mbili zilipita bila mumeo wangu kuonesha sura yake.

Ilionyesha kiasi gani mume wangu asivyo nipenda bali amelazimishwa na baba mkwe. Vilevile ilionesha jinsi nisivyopendwa na familia ya mume wangu zaidi ya baba mkwe. ******* Siku ya tatu nilirudi hadi nyumbani kwa dada na kumueleza nilipofikia, dada alisema:

"Unaona vitu vingine sisi kama sisi hatuwezi kuviamua kwa kuwa ni waolewaji, hatuna uamuzi.Imeonyesha jinsi gani mkweo wa kiume alivyo na msimamo na jinsi gani mama mkwe wako alivyo adui yako namba moja."
"Dada unafikiri kwa hali hiyo kuna ndoa hapo?"

"Inaweza kuwepo na isiwepo kwa kuwa umezungukwa na wabaya wako. Lakini kwenye haki ushindi huwa juu, Mungu atakusaidia utawashinda."

"Asante dada na dua letu lipokelewe."
"Amina." Baada ya maongezi na dada nilirudi kwangu, nilimuuliza mlinzi wa nyumba kama mume wangu amerudi.
“Vipi Samwel baba Anna alikuja?”
“Sijamuona.”

“Samweli au ulitoka alikuja hakukuta?”
“Mama sijatoka tangu niingie nipo hapa.”
“Mmh! Sawa.”

“Kwani vipi mama?”
“Basi achana nayo.”
Niliingia ndani mwangu na kuendelea kukaa na wanangu ambao muda huo ndiyo wafariji wangu. Siku ile nayo ilipita bila kumuona mtu yeyote si mume wangu wala ndugu wa mume. Sikujali sana japo roho iliniuma, nilichoshukuru hakutunyima fedha za matumizi.

Siku zote alimpa dereva wetu aliniletea. Nilipata wazo la kwenda kumueleza baba mkwe,lakini wazo hilo sikutaka kulipa nafasi. Nilijiuliza kuna ajenda gani ya mume wangu na hatma ya maisha yangu kwake.
 
SEHEMU YA 38:

Nilikuwa nina imani kwa kauli nzito ya baba mkwe basi angekuwa na uoga moyoni mwake.

Ilionesha wazi alikuwa amedhamilia kufanya vile, ilionesha wazi sitakiwi na mume wangu kwa kuwa nimemjazia machanguzoa na mabaa medi.
Nilijikuta nakosa amani moyoni mwangu, kama uvumilivu nimeonesha wa hali ya juu kila mmoja atakili hilo.

Nilijiuliza nitaendelea kulia mpaka lini? Nitaendelea kukosa amani ya moyo mpaka lini? Nani wa kunifuta machozi yaliyokosa thamani? Nani wa kuupoza moyo wangu?

Ilionesha lazimisha penzi au ndoa wakati sitakiwi na familia ya mume wangu. Niliyangalia maisha yangu si mabaya ni ya kawaida tu nilikuwa na nyumba moja aliyonijengea mume wangu enzi ya mapenzi motomoto na nyingine niliyojenga kwa fedha niliyodunduliza kwa kupewa na mume wangu za matumizi.

Kwa kweli akili yangu iligota na kuamini muda ule nilitakiwa nitoe maamuzi yangu mwenyewe bila kumshirikisha mtu kwa vile kila ushauri niliufuata mwisho wake niliishia kuumia tu.

Niliijiwa na wazo baya la kuondoka pale kwangu na kurudi kwetu na huo ndio uwe mwanzo na mwisho wa ndoa yetu. Lakini maamuzi yalikuwa mazito, nililiangalia jumba lote nililoachiwa na watoto tu, nilijiuliza nikipatwa tatizo nani atanisaidia.

Nilijiuliza swali jingine kung'ang'ania pale nimeolewa au nimejioa au sina pa kwenda ni wazi mume wangu anajua sina pa kwenda ndio maana kaamua kuniachia jumba lile.

Baada ya mashauri ya peke yangu ya siku mbili mfululizo nikiwaza mambo mengi niliyojiuliza na kujijibu mwenyewe. Hatimaye nilipata jibu ambalo ndilo litakalo kuwa la mwisho bila kusikiliza ushauri wa mtu yoyote.

Siku zote ushauri mwingi huwa kama maji yanayo upoza moyo wa mtu pale unapotendewa kosa, lakini sio kosa la makusudi. Nilifundishwa kusamehe saba mara sabini lakini kwangu ilikuwa too much niliona inatosha.

Mpaka hatua ile nilisema Mungu atanisamehe.
Niliweza kuvumilia ndoa yangu kwa miaka saba na kukubali kuyasahau yote yaliyotangulia.

Japokuwa unaweza kuona miaka saba kati ndoa lakini maumivu ya moyo niliyajua mwenyewe.
Ndoa yangu naweza kusema furaha ilikuwa ndogo kuliko maudhi.
 
SEHEMU YA 39:

Kuna vitu ambavyo sikutaka kuvisema kwa watu juu ya ndoa yangu kwani ni kujivua nguo. Lakini yaliyodhahili hata wewe msomaji umeyashuhudia kwa vile nimejitahidi kulisema kila lililotokea ndani ya ndoa yangu.

Kuna usemi unaosema ndoa ni safari ndefu yenye mapito mengi kikubwa katika safari hiyo ni uvumilivu.

Lakini kwa hili langu niliona inatosha kwa vile maisha ya ndoa si uhai wa mtu na kama ingekuwa uhai basi ningekuwa tayari kufa kwa vile mateso juu ya ndoa yangu yalikuwa hayasemeki kila kukicha. Kuna kipindi niliumia mpaka nikaona kama roho inapaa.

Sikuona umuhimu wa kurudi kushtaki kwa baba mkwe kwa vile mume wangu ameonesha dharau dhahili.
Niliamini kama nitapeleka tena malalamiko kuna uwezekano wa mume wangu kupewa radhi au ndoa ya mama mkwe kuvunjika.

Niliamini kuna muda nilitakiwa nichukue uamuzi mimi kama mimi ili mwingine asikie matokeo.

Niliamini naweza kusimama mwenyewe hata bila ya mume na maisha yangu yakaendelea. Ilikuwa inawezekana kabisa uamuzi wangu wa kuondoka na kugoma kurudi tena kwa mume wangu ingemfanya mume wangu kuishi kwa uhuru mkubwa na kuweza kumleta mwanamke wake ndani.

Japokuwa mume wangu aliujeruhi moyo wangu lakini sikutaka mimi niwe chanzo cha kulaaniwa na baba yake.

Nilijua kuna njia nyingi za kuepusha mataizo ya kukubali yaishe ili kumuachia mwenzangu mwenye mayai ya kiume sio mimi mwenye mayai ya machangudoa na mabaa medi.
Nilijikuta kwenye kipindi kigumu katika kupitisha uamuzi wangu. Kuondoka na kuiacha nyumba yangu ulikuwa uamuzi mzito kama kumeza mfupa.

Moyo uliniuma sana nililia usiku mzima, lakini nilimuomba Mungu anisamehe kwa maamuzi wangu mazito ambayo niliamini hautakuwa na suruhu baada ya kufika mwisho wa uvumilivu.

Nilijua baada ya kuondoka kwangu ningetapata shida siku za kwanza kwa vile nilizoea kuishi maisha ya kuwa chini ya mtu. Nilijiuliza wajane waliofiwa na waume zao mbona wanafurahia maisha sembuse mimi?
 
SEHEMU YA 40

Nami nilihitaji uhuru wa moyo wangu na furaha ya maisha. Nilijua kama nimeikosa kwenye ndoa sidhani nje ya hapo itakosekana.

Japokuwa moyo uliniuma kwa kushindwa kutimiza ndoto yangu ya tangu utotoni kuishi na mume wangu na kutenganishwa na kifo au kila mmoja atembelee mkongojo.

Kufika hapo nililia sana na kumuuliza Mungu nilikuwa nimekosea sehemu gani mpaka ndoa yangu kugeuka jehanamu ya duniani. Baada ya kulia sana nilijiuliza nitalia mpaka lini wakati uamuzi ninao mwenyewe.

Nilinyanyuka na kwenda kukusanya nguo zangu na za wanangu na kuacha kila kitu. Vingi nilivyobeba vilikuwa vya wanangu. Lakini mimi nilibeba nguo chache kwa kujua suala la nguo kwangu sio tatizo.

Nilifanya vile kumuonesha mume wangu sikufuata alivyo vifikiria kwa kufikiri labda nyumba yake na magari yake pamoja na utajiri wake ndiyo unaonifanya ning'ang'anie kwake.

Nilipanda gari hadi nyumbani kwa dada, kama kawaida dada alishtuka na kutaka kujua kulikoni maana ndoa yangu ilikuwa ikimweka roho juu kila siku.

"He! Mdogo wangu kulikoni maana kila nikikuona roho hunipaa. Mara ya mwisho ulikuja na watoto leo umeongeza na mizigo juu?"
"Dada haya ni maamuzi yangu baada ya kufikiria kwa muda mrefu. Nafikiri umefika muda ukiniona roho yako inatua sio kupaa tena."

"Una maana gani kusema hivyo?"
“Dada haraka ya nini, hebu kwanza niache nipumzike, kwa vile sasa nimefika sitoki tena.”

Baada ya kupumzika nilipata muda wa kumueleza yote na uamuzi nilioamua kuuchukua. Dada aliniangalia kwa jicho la huruma na kusema kwa sauti ya upole:
"Kwanza lazima nikusifu wewe ni mmoja wa wanawake wa shoka, lakini bado sijakubaliana na uamuzi wako."
"Kwa nini dada?" kauli ya dada ilianza kunivunja nguvu.

"Umerudi kwa mkweo kumsikia naye anasemaje?"
"Dada ndoa yangu imekuwa si ndoa bali ndoana."

"Najua, lakini kwa msaada wa baba mkwe ulikuwa na nafasi kubwa ya kuiokoa ndoa yako kwa vile tayari kuna mkono wa mtu umeisha ingia."
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom