Sehemu ya 92.
"Mimi naona nirudi nyumbani Tanga," mdogo wangu aliniambia kisha akaniangalia usoni kwa kunichunguza nimepokeaje ombi lake hilo.
Badala ya kumjibu nilibaki namwangalia tu usoni, kwani sikujua kwanini aliniomba kurudi nyumbani.
"Je, ni kwa sababu ya haya maajabu anayoyashuhudia kwa mbali au?" nilijiuliza mwenyewe bila kutoa sauti.
"Au amekumbuka nyumbani, maana hata mimi siku za kwanza nilipokuja Dar nilikuwa nakumbuka sana nyumbani," niliendelea kujisemea moyoni mwenyewe.
Nilimkazia macho zaidi huku nikitafuta kumsoma usoni ambako kulionekana kabisa kwamba alichokuwa akikiongea kilikuwa cha dhati na cha kutoka moyoni mwake.
"Kuna nini?" ndiyo swali la kwanza kumuuliza baada ya kutoa ombi lake.
"Wapi?" naye aliniuliza. Ilionekana muda ulivyopita baada ya yeye kusema akawa amepoteza muungano wa ombi lake na swali langu.
"Si huko nyumbani," nilimjibu.
"Nataka kwenda tu," naye alinijibu.
"Kwenda tu! Kwenda tu," nilijikuta mimi nayarudia maneno hayo.
"Ndiyo kwenda, kuna matatizo au umeona nini wewe kuwepo hapa Dar? Si tulishakubaliana toka tunakuja, tukiwa kule nyumbani kwamba utakaa huku ujifunze kazi kama yangu halafu utafute maisha yako?" nilimuuliza kwa kumsuta na kumbana.
Niliamua kumbana kwa kujua kwamba kwa vyovyote vile lazima atasema kwanini anataka kurudi nyumbani.
"Ni kweli kaka, lakini naomba sana niende tu."
Aliponijibu hivyo nilijua kwamba hakuna njia nyingine itakayomfanya asiendelee kuniambia kwamba anataka kurudi nyumbani.
Nilimuuliza alitaka kuondoka lini, akajibu hata kesho yake. Nilimpa pesa ili aondoke hiyo kesho yake. Na mimi kutotaka kumwona tena nyumbani kwangu.
***
Usiku nikiwa nimelala, nilijikuta nikishikwa mguu wa kulia na kuvutwa. Kwa mbali sana nilianza kufumbua macho ili kuangalia nini kilikuwa kikifanyika mle chumbani mwangu.
Sikuyafumbua macho kabisa kama inavyokuwa, bali nilikuwa kama nusu nimelala, nusu niko macho.
Mwanamke yule yule aliyekuwa amenitokea siku moja nyuma akiwa amejifunika ushungi, alikuwa amesimama mbele yangu huku akiniangalia kwa umakini na akiendelea kunishika mguu kunivuta taratibu sana.
Je nini kitaendelea?