Simulizi: Kazi ya Kutengeneza Majeneza

Shunie

JF-Expert Member
Aug 14, 2016
152,901
453,430
Mtunzi Juma hiza

Sehemu ya 01.

Naitwa Abdul Mensah, ni mzaliwa wa Mabawa, Tanga mjini. Nilipomaliza shule ya msingi mwaka 1992 sikubahatika kuendelea na masomo ya sekondari hivyo nilikuja jijini Dar kwa lengo la kutafuta kazi ya kufanya. Kikubwa kilichonileta Dar ni kutokana na familia yetu kuwa fukara.

Hapa Dar nilifikia Manzese kwa kaka wa rafiki yangu niliyekuwa nimesoma naye shule ya msingi.

Kibaraua changu cha kwanza kukipata kilikuwa cha kuwa msaidizi wa fundi wa kujenga nyumba, kule Ubungo Kibangu. Nilifanya kazi hii kwa muda wa miezi miwili nikaona hainilipi, hivyo nikaacha na kuanza kuuza karanga. Pia nikaja acha mwezi mmoja mbele. Nikajitosa kwenye kujifunza kazi ya ufundi seremala.

Aliyenipa wazo hili ni kaka wa rafiki yangu ambaye alisema afadhali nijifunze useremala kwani nikihitimu nitaweza kufanya kazi kwa uhakika na nitakuwa na ujuzi kichwani kuliko kuuza karanga ama kuhangaika kubeba zege.

Niliona ni wazo zuri sana, akanitafutia fundi mmoja maeneo ya Midizini.
Nilikuwa na kichwa chepesi cha kujifunza na kuelewa kwa haraka lakini nilichelewa kuondoka kwa yule fundi.

Kilichofanyika akaniondoa kwenye kundi la wanafunzi na kuwa fundi kama yeye, kwamba sasa niliweza kupata senti kidogo kwa ajili ya mahitaji yangu ya kimaisha.

Lakini baada ya mwaka mmoja niliamua kuachana na yule fundi na kwenda kufanya kazi zangu binafsi sehemu nyingine.
Pia, nilihama nyumbani kwa yule kaka wa rafiki yangu na kwenda kupanga chumba kimoja Magomeni.

Hapo ndipo nilipoanza kuandaa sehemu yangu ya kufanyia kazi mwenyewe.
Nikiwa na zana chache lakini nikajua muda si mrefu nitajikamilisha kila kitu.

Kazi nilizokuwa napokea zilikuwa ni za aina zote tu. Kutengeneza vitanda, makabati, meza, mpaka majeneza kwa wale waliokuwa wanahitaji.

Miezi mitano mbele bahati ilifunguka kwani niliweza kupata zana zote za kazi. Pia wateja walikuwa wanakuja kwa wingi wakitaka kutengenezewa vitu mbalimbali.
Lakini siku moja nikiwa sehemu yangu ya kazi, alinijia mzee mmoja wa jirani na sehemu hiyo na kuniambia;


Je, nini kitaendelea?
20210608_194456.jpg
 
Sehemu ya 02.

"Unajua kijana wangu mimi nakushangaa sana."
Nilimuuliza unanishangaa nini mzee wangu? Akanijibu;

"Wenzako wengi sana maseremala wametajirika kwa kutengeneza majeneza. Wewe sioni kama unaitilia mkazo shughuli hiyo."

Nilibaki nikitafakari kwa muda nikaona mzee ameongea kitu cha busara sana tena ananitakiwa mema katika maisha yangu ya mafanikio.

Nilimjibu sawa mzee wangu nitafanya hivyo. Lakini katika hali ya kunishangaza sana mimi, yule mzee sijui kama aliwahi kuwa fundi seremala au vipi, kwani aliniambia kwamba naweza kuanza kuchonga jeneza la futi sita kwa mbili kisha nione kama sitapata wateja.

Nilitaka kumuuliza yeye alijuaje vipimo hivyo na kwanini asinipe vipimo vingine akanipa hivyo, lakini midomo yangu ilikuwa mizito kumuuliza swali hilo. Nikaacha.

Hapo nilipokuwa na kibanda cha useremala na nyumba niliyopanga ni mbali. Kwa hiyo sikuwa nimezoeana na mtu zaidi ya huyu mzee ambaye naye mara zote alikuwa akija kibandani kwangu.

Lakini naye nyumba kamili aliyokuwa akiingia siijui ila nilikuwa najua ni mzee wa jirani kwani baadhi ya watu walikuwa wakipita njia ya jirani na kibanda changu walikuwa wakimsalimia kwa kujuana.

Basi siku mbili mbele nilichukua mbao na kutengeneza jeneza la kwanza kabisa ambalo halina mtu. Niliwahi kutengeneza siku za nyuma la mtoto lakini lilikuwa limeodwa na watu.

Nilitumia vipimo alivyoniambia yule mzee, kisha nikalipamba sana, huku nikiwa naomba Mungu linunuliwe kwani nilitumia pesa ya akiba nyumbani kununulia mbao na vitu vingine kama polish.

Kazi yote iliisha jioni ya saa kumi na mbili. Na saa kumi kamili yule mzee aliyekuwa amekaa sehemu mbali kidogo na kibanda changu aliondoka. Kwa hiyo mpaka namaliza hakuwepo.

Niliingia ndani ya chumba ninacholaza mbao ili kuona kama kulikuwa kuna nafasi ya kulilaza jeneza ndani humo.

Nafasi ilikuwepo lakini ni ile ya kupangapanga vitu ili kupata nafasi nzuri.
Nikiwa huko ndani watu waliniita. Nikatoka hataka. Walionekana wakiwa na nyuso za huzuni sana. Nikahisi wanataka jeneza. Mmoja tu ndiye aliyenisalimia. Wenzake walikuwa kimya.


Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 03.

Niliwauliza shida yao wakasema jeneza bwana.

"La saizi gani?" niliwauliza.
Mmoja akawa anatumbukiza mkono mfukoni kutoa kitu. Nikajua anataka kutoa kamba kwani hata wenzake walimwangalia yeye. Inaonekana yeye ndiye aliyekuwa na vipimo vya marehemu.

Akiwa anaendelea kutoa, niliwaonyesha lile ambalo tayari nilikuwa nimelitengeneza. Lakini hawakuonekana kulichangamkia zaidi ya kusubiri kamba itolewe.

Nilichukua ile kamba na kuitia mfukoni mwangu kisha nikawaomba wanisaidie kutoa jeneza nje. Walinisaidia wawili wao. Baada ya kuliweka chini nilichukua kamba ili kulipima. Mmoja akasema kuwa, endapo kamba italingana na jeneza lile itakuwa vizuri sana.

Mungu akabariki ikawa hivyo. Vipimo vya urefu katika kamba vilikuwa sawa sawa na jeneza. Vipimo vya upana pia. Yaani kama niliwapimia wao. Hata wao wenyewe walishangaa sana.

Wakasema Mungu amewasaidia.
Baada ya kumalizana kwenye malipo wakabeba jeneza lao, maana walikuja na Pick- Up. Nikaamua kwenda nyumbani kwa yule mzee ili nimpe japo pesa kidogo ya kununulia kahawa, kwani ushauri wake ulizaa matunda haraka sana hata siku haijapita.
Nilimuuliza mama mmoja kama anajua anapoishi yule mzee. Akanijibu;

"Sisi kila siku tunajua unakuja naye na kuondoka naye, maana ukija na yeye tunamuona amekaa pale, ukiondoka jioni na yeye hatumuoni. Hivi tulijua ni babu yako."
Nilishangaa sana kusikia hivyo kwani sikuwa nafikiria kama majirani wanajua hivyo kwamba yule mzee ananihusu mimi.

"Kwani si babu yako wala humjui?"
"Simjui mama. Hata mimi siku zote nilikuwa najua anaishi hapa kwako. Mara nyingi anapokaa hapo nje najua anaota jua baadaye anaingia ndani."

"Sisi tunachojua unapokuja wewe asubuhi tu na yeye anakuwepo. Tukajua unakuja naye, mwenyewe nilitaka nikushauri kwanini usiwe unamuacha nyumbani mzee wa watu?"
Nilifikiria sana maneno ya mama huyo.

Kwani kumbe ilivyokuwa ni tofauti kabisa na hali halisi. Niliaga haraka haraka ili niondoke. Lakini bado yule mama akawa anazidi kuniuliza maswali.

"Ni kweli humjui kabisa?"
Nilimjibu ni kweli simjui kabisa na wala sijawahi kumuona anavyoondoka jioni.



Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 04.

Lakini katika hali ya kushangaza zaidi yule mama akasema kuwa, wao majirani walianza kumwona yule babu mara baada ya mimi kuanza shughuli zangu za useremala.

"Siku ya kwanza unaanza kuchonga kama utakumbuka siku ile kulikuwa kuna manyunyu, ndipo na yeye alianza kuonekana akikaa hapa nje kwangu," yule mama aliniambia.

Niliondoka kurudi kwenye banda langu la kazi ili nifunge vizuri zaidi geti kisha niondoke. Lakini moyoni bado nilikuwa sikubaliani na kauli za yule mama. Niliamini kuwa kuna ukweli alikuwa akinificha. Labda pengine hakujua kwanini nilikuwa namtafuta yule mzee.

Nilipoingia ndani ya banda langu nilisikia mlio fulani ukipita masikioni, kama vile kulikuwa kuna ishara ya kitu cha hatari kinataka kutokea. Nilisimama na kuangalia juu, chini, kote kote, lakini kulikuwa salama.
Niliweka vitu sawa kisha nikawa natoka.

Lakini wazo moja lilinijia kabla sijatoka nje kabisa kuwa zile pesa ambazo nilipanga kumpa yule mzee niziache mulemule ndani nisije nikazitumia halafu nikashindwa kumpa.

Nilizibagua kama kiasi cha shilingi elfu tano, nikaziweka ndani ya kopo moja kisha lile kopo nikaliweka juu ya mbao. Nikaondoka zangu mpaka nyumbani.

Siku hiyo sikutoka kama ilivyokuwa kawaida yangu, nilijikuta nimekuwa mzito sana.
Usiku nikiwa nimelala niliota ndoto niko porini peke yangu natembea kuelekea nisipopajua, lakini ghafla! mbele yangu akatokea mnyama mkubwa sana ambaye simfahamu mpaka leo hii.

Tembo si Tembo, Kifaru si Kifaru, wala huwezi kusema ni Twiga am Simba. Niliposita kutembea na kusimama yule mnyama alinisogelea mpaka jirani yangu kisha akapotea mbele ya macho yangu.

Lakini kabla ya kufutika machoni mwangu alitabasamu kama vile alikuwa akinionyesha ni mnyama mkubwa lakini hakuwa na tatizo na mimi kama binadamu. Niliposhtuka kutoka usingizini, nilikuwa natiririka jasho kiasi cha kusababisha shuka lote kulowa. Niliamka na kukaa juu ya kitanda huku nikihema kwa nguvu.

Nilifikiria ile ndoto maana yake ni nini hasa lakini sikupata jibu la moja kwa moja. Ingawa mawazo mengi yaliingia akilini mwangu kwamba huenda hivi, huenda ni vile.

Je nini kitatokea?
 
Sehemu ya 05.

Lakini nilipojaribu kumfanya yule mnyama kuwa ndiye yule babu, niliona kama inakuja sawa. Kwamba mnyama mkubwa kutokea mbele yangu, ni yule babu alipoanza kukaa karibu na kibanda changu cha useremala.

Halafu kitendo cha yule mnyama kunisogelea lakini akapotea ghafla! machoni mwangu huku akitabasamu, kwamba ndiyo yule babu kunifuata mpaka kibandani na kunipa ushauri wa kazi ya kuchonga majeneza.

Halafu pia nikafikiria kwamba lile tabasamu la yule mnyama ilimaanisha ile tabia ya yule mzee ya kuongea vizuri sana na mimi siku zote. Kule kupotea machoni mwangu nilichukulia kama vile ninavyomfuata nyumbani kwa yule mama kisha naye akasema hakai pale wala hapajui anapokaa na kwamba alikuwa akijua ni babu yangu.

Usingizi ulinijia nikalala tena, lakini namshukuru Mungu safari hii sikuota ndoto yoyote mpaka nilipokuja kushtuka asubuhi yake.

Niliamka nikaenda kuoga, nikavaa na kuondoka. Nilifika kazini kwangu majira ya saa tatu kasoro hivi. Kwa mbali nilitegemea kumkuta yule babu akiwa amekaa mahali pale pale, kwani mara tatu nne hivi nilimkuta amekaa, lakini kama mara moja mbili hivi yeye ndiye aliyenikuta nimeshafika. Na mara mbili tatu yeye ndiye aliyekuwa akinishtukiza kwa kunisalimia muda huo tayari alikuwa amekaa kitako.

Mpaka nafungua kazi kwa kutoa zana za kazi yule mzee alikuwa hajafika pale. Hilo halikunifanya niwe na wasiwasi naye kwani zipo siku zilikuwa hivyo.

Siku hiyo nilikuwa na mpango wa kutengeneza jeneza jingine dogo dogo kama kujulisha wafiwa kwamba ninashughulika na hilo pia. Nikasema nitoe mbao mbili ambazo zingeweza kunisaidia, lakini wakati huo huo nikakumbuka kuwa, juu ya mbao ninazotaka kuzitoa nje jana yake niliacha kopo lenye pesa za kumpa yule babu siku hiyo na toka nifike hapo sikufikiria kuliangalia lile kopo.

Niliingia bandani, nikachukua na kuliweka pembeni kisha nikatoa mbao mbili ndefu. Nilisimama kwa muda kidogo nje kisha nikafikiria kuzichukua zile mbao kwenda kuziranda.
Nikakumbuka kwamba sikuwa nimechukua pesa ya kutosha nyumbani kwa ajili ya kuranda mbao.

Uzuri ni kwamba nilikumbuka kuna mama mmoja alitaka nimtengenezee kimeza cha kuwekea sahani ya kuuzia samaki na alisema angeleta siku hiyo.

Je nini kitatokea?
 
Sehemu ya 06.

Kwa hiyo niliamua kuzichukua zile pesa za yule babu elfu tano halafu baadaye nimrudishie baada ya yule mama kunipa.
Niliingia ndani na kuchukua kopo kisha nikalifungua. Cha kushangaza sikukuta hata senti moja ndani yake.

Nilishangaa sana tena sana. Nikatoka nje na kopo. Lengo ni kwenda kuangalia vizuri zaidi kwani ndani kulikuwa kuna hali kama ya giza giza fulani. Hakukuwa na pesa yoyote ile.
Hata senti tano. Niligeuza kopo chini juu, juu chini nikidhani labda lilitoboka, lakini wapi, hakukuwa na tundu wala upenyo.

Hapo sasa ndipo nilipoanza kuingiwa na wasiwasi juu ya yule babu. Kwa mara ya kwanza nilimfikiria kwamba huenda alikuwa na mazingaombwe yeye. Huenda alikuwa amezichukua zile pesa yeye maana zilikuwa za kwake kwa kunuia kumpa.

Nani afungue geti halafu afungue kwa ajili ya kuingia ndani kufuata shilingi elfu tano tu!
Pia si rahisi mimi mwenyewe ningejua kama geti lilifunguliwa.

Ina maana kulikuwa kuna mtu mwenye funguo kama zangu?
Haya yote ni maswali ambayo nilijiuliza wakati wa mshangao huo wa kuibiwa pesa kwenye kopo.

Niliishiwa nguvu kabisa. Mwili mzima ulinyong'onyea.Nilikosa na amani pia.
Nilisimama nje hapo nikiwa na kopo langu huku nikiangalia huku na kule kama vile nilikuwa natafuta mtu ambaye angenisaidia mchango wa mawazo ya nini cha kufanya baada ya tatizo lililonitokea.

Nilipoangalia saa, ilikuwa saa tano kasoro robo, muda ambao sijawahi kumuona yule mzee akiwa hafika pale nje ya nyumba ya yule mama.

Nililitupa lile kopo chini kisha nikatoka mpaka nyumbani kwa yule mama wa jirani na kibanda changu.

Kabla sijapiga hodi na yeye alikuwa akitoka nje huku akiwa ameshika kikapu.
"Hujambo mwanangu?" alinisalimia.
Nilimwitikia kisha nikamuuliza kama yule babu hajafika.

Yule mama alicheka kwanza kisha akanijibu;
"Mwanangu toka ile jana jioni tulipoongea hakuna kilichoendelea," alinijibu huku akifunga mlango.

Wakati anazishuka ngazi za nyumba yake nilitamani kumsimulia mkasa wangu lakini nilimwona kama ana haraka sana.
"Vipi kijana kwani kuna tatizo kati yako na yeye?" aliniuliza, akaonekana kukunja sura yake akinishangaa.


Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 07.

"Ni kweli mama lakini naona kama una....." kabla sijamaliza kusema alinishika mkono na kunivuta pembeni ya nyumba yake.
"Nini?" aliniuliza.

"Mama ni hatari sana," nilimjibu kwa woga.
Alikaa macho kuniangalia lakini sikumwambia kitu zaidi na mimi kumwangalia tu.

Tukawa tunaangaliana.
Lakini alinishika bega moja na kuniambia kwamba anakwenda mjini akirudi ataniita kwake ili tuongee vizuri.

Nilimkubalia.
Nilirudi kibandani kwangu na kuendelea na kazi ndogo ndogo ikiwemo ile ya kimeza cha yule mama wa kuuza samaki.

Kwenye saa saba hivi mchana alikuja yule mama wa kimeza akanikipa. Lakini ile anatoka tu, walitokea wazee watatu wakisema wanaomba niwatengenezee jeneza la mtoto wao.

Wakanipa vipimo kwa kamba ya katani, kisha wakanilipa pesa zote kisha wakasema wanakwenda kufanya mpango wa usafiri ili watakapokuja kuchukua jeneza waje na gari kabisa. Kwani maiti anasafirishwa kwenda Kilosa, Morogoro.

Nilichangamka kuifanya kazi hiyo huku nikisema moyoni kwamba, kama kweli yule mzee ndiye aliyeniibia zile pesa kwenye kopo lakini lazima na yeye pia alikuwa anahusika kunipa wateja kama wale.

Kwani sehemu yenyewe siyo ya kusema watu wanaweza kuja kutoa oda ya kazi ya kutengeneza majeneza wakati kuna sehemu kibao ambazo ni maalum kwa ajili ya shughuli hiyo.

Jioni ya saa kumi yule mama aliniita akiwa amesharudi kutoa mjini alikokwenda. Akasema amerudi haraka haraka kwa sababu yangu lakini safari yake ilikuwa ni ya kurudi usiku wa siku hiyo.

Niliingia sebuleni na kukaa kwenye kochi dogo. Wakati huo yule mama alikuwa chumbani. Nilikuwa namsubiria hapo.

Sehemu niliyokaa niliweza kuona nje moja kwa moja. Hata kama mtu angepita na yeye angeweza kuniona nilipokaa mimi. Ghafla! Nilimuona yule mzee akipita kutoka upande wa kulia kwenda upande wa kushoto wa nyumba hiyo.


Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 08.

Jioni ya saa kumi yule mama aliniita akiwa amesharudi kutoa mjini alikokwenda. Akasema amerudi haraka haraka kwa sababu yangu lakini safari yake ilikuwa ni ya kurudi usiku wa siku hiyo.

Niliingia sebuleni na kukaa kwenye kochi dogo. Wakati huo yule mama alikuwa chumbani. Nilikuwa namsubiria hapo.

Sehemu niliyokaa niliweza kuona nje moja kwa moja. Hata kama mtu angepita na yeye angeweza kuniona nilipokaa mimi. Ghafla! Nilimuona yule mzee akipita kutoka upande wa kulia kwenda upande wa kushoto wa nyumba hiyo.

Nilitoka mbio ili kumuita lakini nilipojitokeza sikumuona mtu zaidi ta watoto wawili waliokuwa wakicheza nje ya nyumba hiyo. Niliwauliza kama wamemuona mzee mmoja akipita hapo wakasema hakuna, ila kuna mwanamke mmoja ndiye aliyepita ameenda zake.

Nilirudi ndani na kukaa nikimsubiria yule mama mwenye nyumba ile. Alipokuja alikaa kochi la mbali kidogo na mimi na alianza kwa kuniuliza.

"Enhe, mwanangu ulikuwa unasemaje kwani?"

Niliamua kumsimulia kisa chote toka kuanza kumuona yule babu pale, kuzoeana naye mpaka kunishauri niwe natengeneza majeneza.

Pia nikamsimulia mpaka kuweka pesa kwenye kopo na kukuta hazipo.
Yule mama alishangaa sana. Wakati wote wa mazungumzo alikuwa akibadilisha mapozi tofauti tofauti.

Mara alijishika kidevuni, mara alijishika miguuni, mara aliegemea mto. Yote hiyo niligundua ilikuwa ni katika kushangaa maelezo yangu.

Funga kazi ni pale nilipomsimulia kuhusu kupita mzer huyo nje ya nyumba yake muda ule. Na kwamba nilitoka na kumwangalia lakini sikumkuta zaidi ya kuona watoto wawili wakicheza.

Aliniuliza kama nilipotoka niliwauliza wale watoto walisemaje, nikamwambia kwamba walisema hakuna mzee aliyepita zaidi ya mwanamke mmoja ambaye alikwenda na safari zake.

Lakini kitendo kingine kilishangaza palepale, kwani yule mwanamke alipotoka kutaka kuwauliza wale watoto hawakuwepo.
Akarudi ndani na kuniambia.

"Mimi mwanangu naongea kama mama yako, kama mzazi wako. Kuna kitu kwa huyu mzee. Siku moja jirani yangu aliniuliza kama ni mgeni wangu, nikamjibu simfahamu, lakini nikamwambia kwamba ni mzee anayekufuata wewe. Lakini kwa maneno yako naamini kitu fulani sasa.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 09.

Iko siku nilimsalimia, akaitika kwa sauti ya kike, lakini baadaye nilimsikia akiongea na wewe kwa sauti ya kiume. Huyu mzee ni tatizo."
Alipomaliza kusema hivyo nilisimama na kuaga kwani nilikuwa na kazi za watu na pia nilianza kuhisi uoga zaidi.

Mimi ni mwoga sana wa mambo ya ajabu. Hata usiku nikitembea siogopi majambazi wala vibaka. Hata watu wakisema njia ile ina majambazi au wanyama siogopi, hata simba lakini nikisikia njia ile ina maajabu, mauzauza naogopa sana.

Nilipofika na kuanza kumalizia kazi za watu, ya yule mama mwenye kimeza cha kuuza samaki na wale wa jeneza walitokea vijana wa makamo, wawili nao wakasema wanataka jeneza lakini la mti wa saispraisi. Ina maana kwamba uwezo wao wa kipesa haukuwa mkubwa ndiyo maana wakataka jeneza la msaispraisi.

Walinipa vipimo vyao vya kamba ya katani kisha wakaniuliza na bei. Niliwatajia, wakanilipa pesa, nikaanza kazi.

Kwenye saa kumi na mbili na nusu jioni nilikuwa nimemaliza kazi zote. Majeneza yote mawili na kimeza cha yule mama. Pia kuna mtu alikuja na kuulizia bei ya kitanda cha futi sita kwa nne.

Kifupi nilihisi nimepata sehemu nzuri kwa ajili ya kazi ya useremala.
Jeneza moja lilichukuliwa na wenyewe, meza pia ilichukuliwa. Likabaki jeneza moja ambalo niliweka nje nikitegemea wenyewe kuja kulitwaa wakati wowote ule..

"Hujambo bwana Abdul?" mzee mmoja alinisabahi akiwa amesimama nyuma yangu.
Nilipogeuka nilionana naye ana kwa ana. Alikuwa amevaa kikoi cha rangi ya bluu, lakini kikiwa kimechakaa kiasi. Juu alivaa singlendi nyeupe lakini iliyofubaa kwa maji ya kufulia ama matunzo hafifu.
Juu kichwani alivaa kofia maarufu kwa jina la balaghashia.

Chini kabisa akavaa sendozi nyeusi.
Huyu mzee sikuwahi kumuona hata siku moja. Sasa jina langu alilijulia wapi?
Hilo lilinisumbua kichwa kwa muda. Kumuuliza yeye ni nani nilisikia aibu. Niliamini pengine alikuwa akinifahamu sana ila mimi ndiye nilikuwa nimemsahau.

"Vipi unaendeleaje na biashara zako?" aliniambia huku akiwa ameifumbata mikono kwa nyuma.

"Mungu anasaidia," nilimjibu kwa mkato hata yeye alijua hilo.

Kwa jinsi alivyo hakuwa akifanana kwa namna yoyote ile na yule mzee niliyekuwa namshuku kwa mazingaombwe yaliyokuwa yakinitokea.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 10.

Pia niliamini hawana uhusiano wowote kwani hata yule hakuwa akilijua jina langu.
Licha ya kwamba aliona namshangaa lakini sikuona akichukua jukumu la kujitambulisha, akaaga na kuondoka zake huku akiwa bado ameiweka mikono yake kwa nyuma.

Hili lilinisumbua sana. Nikamwazia vibaya. Wakati anakwenda nilimtupia macho mpaka anaanza kwenye uchochoro wa nyumba fulani.

Nilichoshukuru ni kuwa, wakati wote anafika na kusimama pale kibandani kwangu, yule mama alikuwa amekaa nje ya nyumba yake. Kwa hiyo niliamini kwamba alimuona yule mzee na pia aliniona mimi nilivyokuwa nashangaa.

Nilimsogelea ili kumwambia tukio hilo ambalo nalo sikuwa nimelielewa.
"Mama umemuona huyu mzee aliyepita hapa kwako akitokea kwangu sasa hivi?"
"Hapana sijaona mtu," yule mama alinikatalia katakata.

Hilo nalo lilinishangaza sana kwa sasa ilionekana dhahiri kuwa kulikuwa na kitu kikubwa kuliko kawaida. Nilirudi kibandani kwangu na kuendelea na kazi. Yule mama, nadhani alishikwa na dukuduku akaja na kuniuliza kwa nini nilimuuliza yeye vile, nilikuwa nimemuona nani.

Nilimsimulia ilivyokuwa akastaajabu sana. Kwa mara ya kwanza aliniambia kitu ambacho sikuwa nimekiwaza.
"Kijana uliaga wazee wako kwenu wakati unakuja huku?"

"Waliostahili kuagwa wote niliwaaga, labda wasiostahili. Haikuwa na lazima sana!" nilimjibu kwa uhakika. Kwani ni kweli wale waliostahili kuagwa nilifanya hivyo na walinipa baraka zote.

"Unaabudu mambo ya kishirikina?"
"Hapana mama sikulelewa hivyo," nilimjibu.
"Hata mimi sina maana nataka ufanye hivyo, ila maana yangu ni kwamba, kama unashiriki mambo ya kishirikina huenda yanayokupata yanatokana na imani hiyo."

"Hapana mama siko katika mambo hayo," nilimjibu.

"Kiasili kwenu wapi?" aliniuliza.
Wakati najiandaa kumjibu, yeye akatanguliza majibu.

"Sumbawanga au Tanga?"
Sikujua kwanini alitaja miji hiyo ikiwemo ule ambao kweli mimi nilizaliwa, wa Tanga.
"Tanga," nilimjibu nikimkazia macho kutaka kujua atasema nini mara hii ya pili.

Kabla hajaanza kusema kitu, yule mzee ambaye alianza kumuogopa kwamba huenda alianza kunichezea michezo yote ile alitokea kwenye uchochoro mmoja akiwa amevaa kanzu.


Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 11.

Yule mama ndiye aliyeanza kumuona yule mzee, kwani alinigusa bega na kunielekezea kidole alikokuwa akitokea yule mzee.
"Kijana wangu hatujaonana tangu juzi kama sikosei," yule mzee alianza kusema akiwa amenikaribia. Alipofika akanipa mkono mimi huku akiniuliza kuhusu hali yangu. Nami nikamsalimia, kisha akampa mkono yule mama naye akamsalimia.

"Vipi mzee wangu kumbe hukai hapa. Mi nilifikiri unakaa kwa huyu mama," nilitoa dukuduku langu palepale. Alitabasamu na kunijibu.

"Kumbe sikukwambia nakaa hapo mtaa wa pili. Hapa nafuata kibaraza tu."
"Mbona jana sijakuona juzi uliondoka ghafla?" nilimuuliza.

"Juzi hali yangu haikuwa sawa, jana ikazidi kidogo. Lakini leo Mola kaniamsha salama na kunishindisha salama, namshukuru," aliniambia.

Nilianza kuhisi kuwa mawazo yangu yalikuwa mabaya kwake lakini kumbe sivyo alivyo mtu mwenyewe.

Nilimkaribisha kisha yule mama akaaga kuondoka huku akinikaribisha nyumbani kwake.

Nilikuwa nimebaki na yule babu, akawa ananiuliza habari ya kazi, kwamba inakwendaje.

Nilimjibu Mungu anasaidia kwani mambo si mabaya sana.
Wakati namjibu hivyo, nilikuwa naendelea kufanya kazi. Na yeye akawa anaingiza mkono mfukoni ili kutoa kitu huku akimuita mtoto aliyekuwa akipita njiani.

"Mjukuu wangu kaninunulie sigara bwana," alisema akimwambia yule mtoto huku akiitoa noti ya shilingi elfu mbili kamili. Hii noti sasa, cha kushangaza ilikuwa na rangi nyekundu katika upande mmoja kwa juu.

Na hata zile pesa zilizopotea kwenye kopo, kuna shilingi elfu mbili moja ilikuwa na rangi nyekundu kiasi kwamba hata wakati naiweka nilijiuliza kama nikimpa yule mzee kesho yake dukani watamkubalia?

Nilitaka kumuuliza babu umeitoa wapi pesa hiyo lakini nikaona kuwa huenda akajisikia vibaya kwa swali hilo.

"Mjukuu wangu mmoja kibaka jana alinipa pesa hii," alisema yule babu akimpa pesa yule mtoto akamnunulie sigara.

Kauli yake hii nayo ilinichanganya kidogo, niliamini kama mjukuu wake ndiye aliyempa ile noti ya shilingi elfu mbili ambayo mimi niliitambua kuwa ni moja kati ya zile nilizozihifadhi kwenye kopo basi inamaana huyo mjukuu wake ambaye anasema ni kibaka alifungua kibanda changu na kuiba pesa kwenyw kopo kisha akalifunga vilevile.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 12.

Lakini wazo hilo lilikuwa haliniingii akilini.
Siku hiyo alivuta stuli moja na kukaa jirani yangu.

Baada ya muda mtoto alirudi akiwa amebeba pakiti ya sigara mkononi. Alimpa na kuondoka zake.
Nilimuuliza yule babu nyumba anayoishi ni maarufu kwa mzee nani.

Alinijibu.
"Kwa mzee Saidi Mwinyi, humohumo ndani. Vyumba vya uani , naishi na mwanangu mkubwa anaitwa Ismail Jumaa. Jumaa ni mimi mwenyewe. Ana mke na ana watoto ambao ni wajukuu wangu, mmoja hasikii sana."

Nilimuuliza hasikii masikio au utundu. Akanijibu.

"Mimi namwita cha utundu, mwizi, mtukanaji. Hana adabu hata kidogo."
Kitu kingine babu aliniuliza kama nimepata wanunuzi wa majeneza aliyonishauri niwe nayatengeneza.

Nilimjibu nimepata tena katika hali ambayo sikuitegemea. Akashukuru Mungu yeye.
"Lakini juzi ulipoondoka nilikuletea pesa kwa yule mama ukanywe hata kahawa hukupatikana. Mi nilifikiria unakaa kwa yule mama," nilimwambia, akacheka kidogo kisha akajibu.

"We ungeniletea kwa mzee Saidi Mwinyi, unauliza mzee Jumaa, ndiye mimi mwenyewe," naye alinijibu.

Alipofika hapo niliomba samahani ya moyoni. Kumbe nilimfikiria bure kwamba ni mzee wa ajabu wakati ni mtu anayejulikana na amediriki kunifahamisha anapokaa.

Tena katoa sababu kwamba pale anafuata kibaraza tu. Na ni kweli, kibaraza chenyewe kimekaa vizuri sana kwa kupumzika.
"Basi leo tena utapata watu wawili wanaotaka majeneza," alisema yule babu, akaongezea.

"Lakini chonga kwa vipimo mbalimbali, kama mawili matatu yanakaa. Wakija wateja tu unawauzia. Hivi utapata shida, uchonge mpaka kuwa tayari ni muda wakati wengine wanataka haraka."

Nilimkubalia lakini nilijitetea kuwa, nilichokifanya ni kuranda mbao na kukaa tayari kwa kupigilia misumari ili ikamilike kwa matumizi.

Nilipomaliza kusema akaja mzee mmoja akisema anataka jeneza kwa kesho yake. Akanipa vipimo kwa kamba. Wengi ndivyo wanavyofanya.

Tulikubaliana bei kisha akanilipa kabisa na kuondoka zake.
Mara wakatokea wazee watano wakiwa na mkeka. Nao wakasema wanataka jeneza kwa kesho yake saa nne asubuhi liwe tayari siku hiyohiyo hata kama litaisha saa saba usiku.

Nao wakanipa vipimo na kunilipa pesa kabisa. Nilimuomba babu aningojee ili nikanunue misumari na vanishi ili kuanza kazi.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 13.

Nilikwenda madukani na kununua vitu hivyo. Nikiwa njiani niliwaza kuwa, kwa siku ile babu nimpe kama shilingi elfu kumi kwani ndiye baraka yangu. Lakini pia nilimshangaa kwa mdomo wenye matokeo ya kweli kama Nabii.

Kufika sikumuona babu wala mtu mwingine yeyote yule. Lakini hasa babu kwa sababu ndiye niliyemwacha pale. Nilisimama kwanza nje nikishangaa kisha nikasogea na kufungua geti. Ilionekana aliondoka kabisa kwani stuli ilirudishwa ndani, baadhi ya mbao zilizokuwa nje nazo ziliingizwa ndani na geti lilifungwa.

"Huyu babu vipi? Au kaenda kujisaidia akaona afanye hivi?" nilijiuliza moyoni.
Lakini kitu kimoja cha ajabu ni kwamba, kwa zile mbao nilizoziacha nje, na umri wa yule babu naona kama asingeweza kuziingiza ndani.

Ninaposema ni babu ni babu kweli kweli.
Basi nilitoa mbao nje ili kuanza kazi lakini nikatarajia kuwa wakati wowote babu angetoa na kunikuta nimesharudi. Lakini hakuja mpaka saa kumi na mbili wakati nafunga funga kazi. Majeneza nilishamaliza kutengeneza yote.

Kwa sababu alishanielekeza nyumbani kwa mwanae niliona ni vyema kama ningekwenda pale kumuuliza nimpe pesa yake kisha nirudi nyumbani kupumzika. Siku hiyo nilihisi kufanya kazi kupita kiasi kwa hiyo nilichoka sana.

Nilipomaliza kubamiza geti, yule mama alitokea kwake na kuniuliza kama babu alinielekeza vizuri anakoishi.
"Ameniambia hapo nyuma kwa mzee Saidi Mwinyi," nilijibu.

"Saidi Mwinyi anaishi na nani pale?" aliniuliza.

"Kasema yupo kwa mwanae, vyumba vya uani. Nikifika niulizie Ismail Jumaa na Jumaa ndiye yeye."

"Labda hivyo maana nyumba yenyewe ni nzuri nisingeamini kama angekuwa anaishi peke yake. Halafu hata hivyo si mwenyeji huyu babu, maana wakaaji mule ndani karibia wote nawafahamu kwa sura, ingawa si kwa majina."

Nilimwambia yule mama kwamba nakwenda kumuona kwa sababu nina mzigo wake nataka kumpa, akasema sawa.

Nilikata mtaa wa kwanza, nikapita uchochoro na kutokea mtaa wa pili ambako ndiko alikosema yule mzee, kwamba anaishi mtaa huo kwa mzee Saidi Mwinyi.

Nilimuuliza kijana mmoja aliyekuwa akisukuma toroli lenye maji kwenye madumu kama anapafahamu kwa mzee Saidi Mwinyi.
"Nyumba ile yenye geti jeusi," alinielekeza kwa kidole.

Je nini kitaendelea??
 
Sehemu ya 14.

Ni nyumba nzuri inayovutia hata kwa mbali tu. Ni kweli kwa mtu kama yule babu isingekuwa rahisi kupanga yeye kama mpangaji. Nilimkuta mzee mmoja nje, mnene, mweusi ana kitambi kikubwa. Nilimsalimia na kumuuliza.

"Hapa ndiyo kwa mzee Saidi Mwinyi?"
"Ndiyo mimi nikusaidie nini?" aliniuliza kwa sauti ya kujiamini.

"Nina shida na mzee Jumaa anayeishi kwa mwanae Ismail," nilijieleza.
"Mzee Jumaa anayeishi kwa mwanae Ismail?" yule mzee aliniuliza huku akionekana nimemuuliza kitu asichokijua.
"Ndiyo," nilimjibu.

Katika mazingira ya ajabu sana huyu mzee aliyekiri kuwa ndiye Saidi Mwinyi alionekana kutomfahamu mpangaji aliyeitwa Ismail Jumaa ambaye nilimwambia anaishi kwenyw nyumba yake.

Hili nililigundua kwa jinsi alivyoshangaa wakati namuuliza.
"Huyo Ismail ndiyw aliyekwambia anakaa hapa?" aliniuliza huku akinikazia macho.

"Hapana ila huyo mzee Jumaa ndiye aliyeniambia anakaa kwa mwanae ambaye anaitwa Ismail. Aliniambia ni nyumba ya mzee Saidi Mwinyi."

"Sawa sawa kabisa, mimi ndiye mzee Saidi Mwinyi mwenyewe lakinu humu ndani mwangu hakuna mtu anayeitwa Ismail wala Sadiki. Huko uani kuna vyumba vitatu tu, cha Mjolie, Musa na Mihayo. Halafu wote rika moja na kila mmoja anaishi peke yake," yule mzee Mwinyi aliniambia, akaendelea.

"Halafu nyumba kubwa ya mbele kuna mpangaji mmoja tu anaitwa Mama Sarah. Hana mume wala hawara anayefika hapa kumfuata. Ana watoto wawili wote wanawake."

Nilichoka mwenyewe. Nilijiinamia kwa muda nikimfikiria yule babu kwa tabia anayokwenda nayo, nikapata picha kwamba huenda alitaka kuniingiza katika matatizo makubwa.

"Haya mzee wangu nakwenda mimi," nilimuaga yule mzee Mwinyi huku nikigeuka na kuondoka zangu.

Najua nyuma alinikazia macho kuniangalia, sasa sijui alikuwa akiwaza nini.
Moja kwa moja nilikwenda nyumbani huku nikiendelea kumfikiria yule mzee.

Usiku wakati nataka kulala nilifanya kitu kimoja kwanza. Kwanza kabisa nilichukua pesa zote za siku hiyo nikaziweka juu ya kabati halafu nikazibagua. Shilingi elfu kumi na moja ya noti niliirudisha ndani ya mfuko wa suruali niliyokuwa nimeivaa siku hiyo.
Zilizobaki nikazificha sehemu. Lengo la kuiweka shilingi elfu kumi nilidhani huenda kesho yake ningemuona yule babu na kumpa.

Je nini kitaendelea??
 
Sehemu ya 15.

Usiku nikiwa nimelala nikaota ndoto, Eti yule babu amenifuata na kunilaumu, akisema.
"Yaani wewe mtu mzima na akili zako umeshinda kupatambua kwa mzee Saidi Mwinyi?"

"Mbona nimefika babu. Lakini mzee Saidi Mwinyi mwenyewe amekataa wewe hukai mule ndani mwake wala hakuna mpangaji anayeitwa Ismail Jumaa," nilimjibu babu katika ndoto.

"Mbona tupo. Au ulipotea njia?"
Aliniuliza huku akitabasamu.
Mara nilishtuka kutoka usingizini.


Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 16.

Kwa hofu na wasiwasi niliokuwa nao niliamka kabisa na kutafutatafuta kila mahali mle chumbani kwangu. Nilihisi kumuona yule babu katika picha katika picha ile ile aliyonijia nayo ndotoni. Nilikosa usingizi kwa muda mrefu mpaka kunakaribia kucha ndipo ukanijia nikalala.

Kwenye saa moja kasoro robo hivi niliamka siku hiyo. Kwa kuwa nilichelewa kuoga, niliswaki tu halafu nikaondoka ili kuwahi kazini kwa ajili ya majeneza ya watu. Lakini kabla sijaondoka nilichukua shilingi mia tano ya nauli nikaichanganya kwenye mfuko ule ambao jana yake usiku nilitumbukiza shilingi elfu kumi ya kumpa babu.

Nikiwa ndani ya daladala, konda alipotaka nauli yake nilitumbukiza mkono mfukoni lakini nikatoa shilingi mia tano tu, ile elfu kumi haikuwepo.

Nilishtuka kwanza, halafu nilianza kujikagua kila mahali ndani ya mifuko hakukuwa na pesa.

Hata baada ya kushuka kutoka garini niliendelea kuitafuta ile shilingi elfu kumi kwenye kila mfuko nikitegemea ningeiona, lakini sikuiona.

Mawazo yalinijia yale yale kuwa huenda yule babu aliichukua usiku kama alivyofanya kwenye zile pesa za mwanzo na nilianza kukubali kuwa, haikuwa kibaka mjukuu wake wala mwizi mwingine yeyote.

Nilipofika kazini kwangu mara baada ya kufungua geti, nilibeba jeneza moja mpaka nje lengo lilikuwa ni kulipaka vanishi kwa sababu lilimalizika toka jana yake. Nilipofika nje, nikalifungua mfuniko wa juu.

Macho yangu yalikutana na shilingi elfu kumi.
Lakini sasa nilishindwa kutambua kama shilingi elfu kumi hii ndiyo ile niliyokuwa naitafuta au nyingine?
Lakini kwa jinsi ilivyoonekana uchakavu wake na ilivyokunjika ni ile ile bila ubishi.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 17.

Niliogopa sana, nikaliacha kwanza hili jeneza na pesa yake ndani. Nikalitoa lile jeneza la pili. Lilikuwa zito sana lakini sikushangaa kwani mbao nilizozitumia kutengenezea zilikuwa ni nzito tofauti na mbao za lile jeneza ambalo nilikuta shilingi elfu kumi ndani yake. Wakati wote huo mapigo ya moyo wangu yalikuwa yakinienda mbio kwa wasiwasi na hofu.

Nilipolifikisha nje nililiweka sambamba na lile jingine halafu nikabeba mfuniko na kwenda kuuweka pembeni na jeneza hili lililokuwa linatakiwa kupakwa vanishi kama lile jingine.

Wakati narudi huku nikiliangalia ndani nikakuta paka amekaa akinitumbulia macho. Niliruka na kwenda kusimama pembeni ili nione vizuri kwamba macho yangu kweli yanaona au mawazo tu.

Ni kweli alikuwa paka mweusi ambapo aliendelea kunikazia macho halafu alipanua kinywa. Sasa sielewi alikuwa akiongea, akicheka au akipiga mwayo.
Niligeuka kuangalia nyumbani kwa yule mama jirani, nilimuona akitoka kwake huku akisema.

"Leo sijakuona mwanangu, hatujasalimiana wala."
Niliporudisha macho kwenye yale majeneza yote, sikuona paka na nilipoliangalia lile jingine sikuona shilingi elfu kumi.
"Mama," nilimwita huku nikiwa nimeacha kinywa wazi kwa mshangao.

"Unasemaje kijana wangu?" yule mama aliniuliza huku na yeye akionekana kunishangaa. Alikuja mpaka nilipokuwa nimesimama pale nje ya kibanda changu huku akiendelea kuniuliza nasemaje?

"Mama," nilisema hivyo tu nikashindwa kuhadithia. Akili yangu ilikuwa ni kama imesimama vile. Akili iliniambia kuwa siku zangu za kuishi duniani zilikuwa zimefikia ukingoni na zilikuwa zinahesabika.

Je nini kitaendelea??
 
Sehemu ya 18.

"Kuna tatizo tena?" yule mama aliniuliza alipofika. Alisimama mbali na mimi kama vile ananiogopa.

"Mama ni makubwa yanayonikuta mama, hayasemeki, nahisi nikisema nitakufa," nilimwambia yule mama.

"Kama yapi?" aliniuliza huku akionekana kupenda kujua matatizo yangu.
Ukweli ni kwamba sikuthubutu kumsimulia chochote nikamuomba aniache kwanza nimalize kazi za watu ambazo nilijua wangetokea muda wowote.

Na kweli alipoondoka tu wale wateja waliotaka majeneza kwa mara ya kwanza walitokea lakini walinikuta namalizia kupaka vanishi.

Kitu kimoja kilichojitokeza kwa watu hawa ni kwamba katika kuitana ni kuwa mmoja alikuwa akiitwa Ismail mwingine Jumaa. Katika kumbukumbu zangu nilikumbuka kwamba Jumaa ni yule babu niliyemfikiria kwamba alinifanyia mauzauza.

Halafu Ismail jina la mtu ambaye alisema ni mtoto wake anayeishi kwa mzee Saidi Mwinyi.

Katika maongezi yao niliwagundua kwamba wao ni watu wa Tanga lakini wilalayani Pangani. Na barabara inayokwenda Pangani inaoita kitongoji cha mabawa ambacho ndicho mimi natoka.

Nilitamani kuwauliza lakini nilijikuta tu moyo unasita kufanya hivyo. Walipoondoka na jeneza lao tu, walikuja wanajeshi nao walitaka kutengenezewa jeneza la mtoto wao mwenye miaka kumi na mbili.

Walisema mwanajeshi mwenzao amefiwa na wanatarajia maiti kuisafirisha Musoma, Mara kwa mapumziko ya milele. Walinipa vipimo na kiasi cha pesa kisha wakaniuliza wanaweza kurudi saa ngapi kulichukua jeneza lao?

"Saa hizi saa tano njooni saa kumi na moja jioni."
Mmoja wao akasema.
"Hapana tutakuja saa kumi na mbili si utakuwa bado upo?"

Niliwakubalia kwa sababu nilijua ilikuwa ni lazima waondoke na jeneza lao. Walisema maiti ilikuwa hospitali ya Lugalo. Walipoondoka hawa tu, niliingia ndani ya banda nikakaa kwenye mbao na kuwaza.

"Hivi kinachowafanya wateja wakimbilie kwangu ni nini? Na huku uchochoroni wanajuaje kama kuna mtu anatengeneza majeneza? Halafu mbona wote wanalipa pesa keshi. Hawabishi na hawalalamiki kulipa?"

"Hodi wenyewe," sauti iliniita, nikashtuka na kutoka huku mapigo ya moyo yakinienda mbio kwa wasiwasi na hofu.
"Shikamoo," nilimsalimia mzee mmoja ambaye ndiye aliyeniita.

Je nini kitaendelea??
 
Sehemu ya 19.

Nikamkazia macho na kumshangaa kwani alionekana wazi hakuwa mteja wa jeneza.
"Marahaba mwanangu, hivi umeonana na mzee Jumaa siku mbili hizi?" aliniuliza huku akiwa ameinamisha uso chini. Kama vile alikuwa anaona aibu.

Nilitaka kumuuliza mzee Jumaa ndiyo nani lakini niliamini kwamba kusema hivyo kungeweza kusababisha matatizo ambayo yalishaanza kunichosha kiakili.

"Hapana sijamuona. Kwani yupo?" ndivyo nilivyomjibu.

"Aende wapi?" alinijibu na yeye.
Lakini mimi sikumjibu kitu zaidi ya kushika hiki na kile kwa ajili ya lile jeneza la wanajeshi.

"Hata jana hajafika?" yule mzee aliniuliza lakini sasa alianza kukasirika na kubaki na maswali kibao kichwani. Kwa upande wa hasira zilinijia kwa sababu yule mzee anayeniuliza kuhusu mzee Jumaa ndiye mzee Jumaa mwenyewe.

Halafu kingine alikuwa mgeni machoni pangu kiasi kwamba isingekuwa rahisi yeye kuniuliza habari za mzee Jumaa. Ni lini amewahi kuja na mzee Jumaa kibandani kwangu hata siku moja? Hakika niliamini yule mzee ndiye mzee Jumaa mwenyewe.

"Kwani we mzee uliwahi kuonana na mimi wapi?" nilimuuliza, aliachia tabasamu pana huku akiangalia mazingira ya kibandani kwangu. Ilionekana kama alikuwa akitafuta kiti cha kukalia. Ndani ya kibanda kulikuwa na stuli lakini sikutaka kumpatia.
Cha kushangaza hakunijibu swali langu, aliniuliza swali lingine.

Je nini kitaendelea??
 

Similar Discussions

7 Reactions
Reply
Back
Top Bottom