Simulizi: Kazi ya Kutengeneza Majeneza

Simulizi: Kazi ya Kutengeneza Majeneza

Sehemu ya 72.

Nilimwangalia kwa hamu kubwa yule mama kwani niliamini ujuaji wake ulikuwa na manufaa kwa yale mawazo yangu yenye utata kuhusu kauli ya yule kijana aliyedai anaishi nyumbani kwa yule mama.

"Leo umechelewa kufunga mwanangu! Wateja walikuwa wengi sana nini?" alisema yule mama jirani akiwa anafika kibandani kwangu na kusimama karibu na mimi huku akiwa anajifunga vizuri kitenge alichovaa.
"Si sana ndiyo tunajiandaa andaa sasa kufunga lakini namalizia kwanza kupaka vanishi hiki kitanda cha mteja," nilimjibu.

"Kumbe wateja wapo mpaka wa vitanda. Hongera sana," aliniambia kwa kushangaa.
"Kwani mama ukiwa na watoto si lazima utahitaji vitanda mara kwa mara," nilimwambia ili kumchokonoa kwa yale mawazo yangu.

"Sijui hao wenye watoto wanaohitaji vitanda, mimi nilimaliza siku nyingi sana," alinijibu.
"Kufanya nini?" nilimuuliza.

"Si kuzaa. Mimi nilishazaa mambo ya vitanda nilishamaliza navyo siku nyingi kama kuna wanaochonga kwa ajili ya watoto ni wale wanaozaa siku hizi."

Kauli hiyo nayo ilinishangaza pia, kwani ilipingana moja kwa moja na kauli ya yule kijana aliyeondoka.
"Kwani mama huna watoto wadogo, kama vijana hivi?" nilimuuliza huku nikimwangalia kimachalemachale.

"Aa, wapi! Wanangu wote wakubwa wanajitegemea tena wameoa na kuolewa wako makwao," alinijibu huku akitabasamu.
"Ina maana unaishi peke yako siku zote hizi?" nilimuuliza swali ambalo hata yeye mwenyewe kabla ya kunijibu, alicheka kwanza.

Najua kwanini alicheka, kwa sababu hata siku moja sijawahi kumwona mtu mwingine ndani ya nyumba yake sasa iweje nimuulize?
"Unanichekesha sana mwanangu. Kuna siku umekuja nyumbani ukamuona mtu mwingine zaidi ya mimi mama yako?" aliniuliza akiendelea kucheka lakini huku akigeukageuka kuangalia huku na kule.

Ni kweli sijawahi kumwona mtu ndani ya nyumba yake zaidi ya yeye. Hata mgenu sijawahi kumwona.

Na kama ilivyosema awali kuwa, kawaida ya yule mama ilikuwa kwamba hata akienda sokoni au popote pengine lakini mbali na nyumbani kwake, lazima funguo azilete kwangu mpaka atakaporudi. Ingawa sifahamu kwanini alikuwa akiziacha wakati anaishi peke yake. Sasa yule kijana alitokea wapi?

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 73.

Kingine ambacho ni cha ajabu, licha ya maneno yake ya kukanusha kuishi na mtu mwingine nyumbani kwake, mbona yule kijana nilimuona akiingia ndani ya nyumba yake na baadaye ndiyo yeye akatoka? Hapo pana maswali mengi ya kujiuliza.

Lakini sijui ni kwa nini mdogo wangu ulikuwa mzito kumwambia yule mama kuhusu tukio lililotokea muda mfupi tu kabla yeye hajaja la kijana aliyedai anaishi kwake.

Nahisi hapo pia palikuwa si kwa matakwa yangu bali kuna nguvu fulani iliyokuwa ikinisukuma kufanya hivyo. Yaani hiyo nguvu ilikuwa ikinikamata akili, sauti, kinywa na chochote kile ambacho kilionekana kuleta balaa.

"Lakini maneno yako yanaonesha kama kuna kitu zaidi ni kipi nikusaidie?" mama aliniuliza, sura yake ikionekana kuwa makini kunisikiliza.

"Hakuna kitu mama," nilimjibu kwa kusitasita.
Hakukaa sana akaaga na kurudi nyumbani kwake huku akisema kama tutaondoka bila kuonana tena basi tutaonana kesho yake na jioni njema.

Tukiwa njiani tunarudi nyumbani mdogo wangu aliniambia kitu kipya ambacho kilinishangaza pia. Alisema kuwa, wakati nilipoondoka kwenda Jangwani yule mama alimfuata na kumuuliza mimi niko wapi?
Mdogo wangu alipomjibu nimetoka yule mama akamuuliza au amekwenda kwenye huo mkutano Jangwani nini?

Mdogo wangu aliendelea kuniambia kuwa, aliamua kunieleza kwa sababu yule mama alionekana kama alikuwa na shida sana na mimi, lakini alishangaa niliporudi na tulipoonana hakusema kama aliniulizia wala hakusema shida yake.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 74.

Nilimjibu mdogo wangu kwamba yule mama ndivyo alivyo, asimshangae kabisa. Niliamua kumwambia hivyo kwa sababu sikutaka amtilie shaka mapema kwani kuna vitu nilikuwa navichunguza mwenyewe kuhusu yule mama.

Lakini kuanzia hapo nilikosa amani moyoni kuhusu kauli ya yule mama ya kumuuliza mdogo wangu kuwa au nimekwenda Jangwani kwenye mkutano nini!
Kwanza sikutaka mdogo wangu ajue kama nilikwenda kwenye mkutano Jangwani. Hata wakati namuaga nilimwambia tu nitatoka kidogo baadaye ya saa tisa.

Sikumwambia nakwenda wapi wala kufanya nini. Na hata yeye hakuniuliza nakwenda wapi. Pili, yule mama alijuaje kwamba nakwenda kwenye mkutano Jangwani? Waliosema kuna mkutano ni watu wa mtaa wa pili wala mama hakuwepo.

Moja kwa moja nilianza kumwelewa vibaya yule mama kwamba ndiye anayeniumiza siku zote na kwa tabu zote zilizokuwa zikinipata.

Hakuna ubishi wowote ule mambo mengi yaliyonitokea kwa pamoja ilionekana alihusika kwa namna zote. Nilijikuta nikimuogopa sana moyoni.

Tulipofika nyumbani ile kabla ya kuingia ndani nilipata salamu. Mke wa mpangaji mwenzangu mmoja aliniambia kwamba mumewe alinihitaji nikirudi tuonane.

Alimwambia nikiwa narudi anipe taarifa hizo.
Kwa hiyo sikuona haja ya kuingia kwangu, kwani nilikuwa nimechoka sana, nikaona afadhali nimsikilize huyo mpangaji mwenzangu nikiingia ndani kwangu iwe moja kwa moja.

Niliingia ndani kwa huyo mpangaji nikiongozwa na mkewe aliyenipa salamu. Nilimkuta akiangalia Tv.

Alinikaribisha kwa furaha huku akisimama na kunipa mkono wa salamu.
Baada ya kukaa, akamwambia mkewe atoke nje ili sisi tuongee ya kiume. Moyo ulinishtuka sana!

Nikajiuliza kuna nini tena?
Mkewe alipotoka tu, yeye mume akasimama na kuufunga mlango kisha akarudi kukaa alipokuwa amekaa.

"Ee bwana nataka tuongee mambo fulani hivi ambapo naamini bila kuongea na wewe naweza kupata dhambi hapo baadaye kwamba kwanini sikukwambia," alianza kwa kusema hivyo huku akiniangalia.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 75.

Nilimuinulia macho kumwangalia huku nikisikia mapigo ya moyo yakienda mbio kuliko kawaida yake.

"Enhe ni mambo gani hayo?" nilimuuliza kwa mkato huku nikiendelea kumwangalia.
"Usihofu sana.

Ilivyo ni kwamba huyu bibi yetu hapa nyumbani ana tabia fulani za vituko vituko. Alipo hapa anaweza kukuzukia hata chumbani akageuka nyoka na kuanza kukusumbua," aliniambia yule mpangaji mwenzangu. Akaendelea.
"Kuna wakati niliwahi kusumbuliwa sana na popo," alisema.

"Popo! Polo ndege au?" nilimuuliza.
"Popo huyu huyu, alikuwa akiingia chumbani kila inapofika saa sita usiku. Anaongea, anaimba kama binadamu."
Nilihema kwa nguvu kisha nikamtazama vizuri huku nikisikia uoga.

Kiufupi alinisimulia vitu vingi sana kuhusu yule bibi mpaka mwisho alipomaliza kwa kuniambia yale yale niliyoambiwa na yule mpangaji mwingine kuwa yule bibi aliwahi kufa akafufuka kwa hiyo watu wengi wamekuwa wakisema kwamba huenda katika kufa ndiko alikopatia maajabu yake yote.

Sikumjibu kitu yule mpangaji. Wala sikumwambia nilichowahi kusikia kabla ya yeye. Unajua kwanini?

Nilikuwa najaribu kuangalia kati ya yule bibi na yule mama jirani kule kazini kwangu nani chanzo cha matatizo yangu?

Kifupi yule mama jirani aliingia moja kwa moja kwenye mawazo yangu kuliko huyu bibi mwenye nyumba.

Kwanza vituko kwa kule kazini kwangu ni vingi kuliko nyumbani. Halafu vina ushahidi wa kutosha sana kuliko kwa huyu bibi.
"Sasa tumfanyaje?" ndilo swali nililomuuliza yule mpangaji mwenzangu.

"Kuna watu wameniambia hata wewe umekumbwa na matatizo sana. Kwa hiyo tumeongea kwamba, tumwite, tumweke kikao na kumuuliza. Ikibidi tumuonye."
"Itawezekana?" Nilimkatisha.

"Itawezekana, unajua wahenga walisema mchawi mpe mwanao akulelee."
Nilifikiria kwa muda kisha nikamjibu.

"Sasa lakini mimi binafsi naomba nisiwepo katika hicho kikao cha kumuonya kwa sababu sijakubali kama yeye ana hayo maajabu mnayoyasema."
Yule mpangaji alisimama kwa kunishangaa kisha akaniambia.

"Basi hayajakupata! Ingekuwa yamekupata kama yaliyotupata wenzako usingesema hivyo."

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 76.

Alipomaliza kusema akakaa.
Na mimi nilisimama na kuaga, nikaenda kwangu huku nikiwaza yale mazungumzo. Kwa kweli sikuwa na ushahidi wowote wa kutosha kwamba yule bibi alikuwa na matukio ya ajabu anayowafanyia wapangaji wake au raia wengine wa mtaani.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 77.

Usiku nikiwa nimelala, niliota ndoto. Niliota niko kazini kwangu natengeneza boksi la nguo la mbao ambalo liliagizwa na mteja mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mama Khadija wa Magomeni Mapipa.

Nikiwa naendelea kulitengeneza boksi hilo, mara alitokea yule mama jirani yangu akasimama mbele yangu na kuniambia.

"Yaani unaacha kutengeneza majeneza yanayokupatia pesa nzuri, unababaika na hilo boksi la mbao la mama Khadija wa magomeni Mapipa. Nani asiyemjua kuwa ni mwanga mkubwa."

Nikiwa bado ndotoni, moyoni nilihisi kuwa, ni wivu wa mama yule juu ya mwenzake. Kwani wakati anaongea, mama Khadija alisimama karibu na geti kubwa la kuingilia ndani.
"Acha kabisa bwana, mimi sipendi," alisema yule mama jirani.

Niliirusha mbali ile nyundo niliyokuwa natengenezea lile boksi, kisha nikasimama wima. Yule mama jirani akanishika mkono huku akisema niachane na mama Khadija.
Nilimfuata hadi sehemu moja ambayo ina bomba la maji la nje.
"Haya lala hapo," yule mama jirani aliniambia.

Bila kuuliza wala kuhoji sana, nilianza kulala chini ya bomba lile. Kisha yeye akafungulia maji kwa kasi.

Ili kukwepa maji yake yasiniloweshe nguo, niliamka haraka. Na nikashtuka kutoka ndotoni!

"Haa!" nilijikuta nikisema huku nikijishika kifua kwa sababu nilikuwa nahema sana.
Ajabu macho yangu yalikwenda kusimama mlango wa kutokea nje ya chumbani kwangu. Nikaona sehemu ya miguu ya mwanamke aliyejifunga kaniki ikiishia.
Nilikaza macho ili kuona sawa sawa, ingawa nilikuwa siamini nilichokuwa nakiona pale mlangoni.

Huyo mwanamke alisimama mlangoni kisha akageuka kuniangalia. Tukakutana macho, lakini sikuweza kumtambua vizuri kwani sehemu kubwa ya uso wake alikuwa ameificha kwa kujizingira na ushungi mweusi pia.

"Wewe ni nani?" nilimuuliza kwa sauti, nikashtuka kwamba huenda mdogo wangu angeamka na kuhoji nilikuwa naongea na nani?

"Umenisahau mara moja hii jamaniii," alinijibu yule mwanamke huku akijifunua ule ushungi.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 78.

"Wewe ni nani?" nilimuuliza kwa sauti, nikashtuka kwamba huenda mdogo wangu angeamka na kuhoji nilikuwa naongea na nani?

"Umenisahau mara moja hii jamaniii," alinijibu yule mwanamke huku akijifunua ule ushungi.
Kabla sijamjibu kumkatalia nilimwangalia kwanza mdogo wangu kama anaamka kwani alianza kujitingisha.

"Kaka," alisema mdogo wangu alikuwa ameamka.
"Vipi mbona umeamka?" nilimuuliza nikijabalaguza.

Pale mlangoni yule mwanamke alikuwa bado amesimama huku akiniangalia. Lakini kama nilivyokwishasema alikuwa amejitanda ushungi kuuzunguka uso, kwa hiyo sikuweza kumtambua kirahisi.

"Kama nimekusikia ukiongea kaka," mdogo wangu aliniambia huku akiinuka na kukaa kitandani.

"Ooh nimeota vibaya sana kuhusu yule mama kule kazini kwako," aliniambia mdogo wangu.

Nilitupa tena macho mlangoni na kumuona yule mwanamke bado amesimama. Safari hii akipanua kinywa kwa kuachia tabasamu.
"Umemuotaje?" nilimuuliza mdogo wangu.
Lakini si kwamba katika mazingira hayo nilikuwa niko katika hali ya kawaida.

Nilikuwa nikitetemeka sana tena sana. Mwili ni kama uliishiwa nguvu kwa tukio lile.
"Eti...!" alianza kusema mdogo wangu, lakini kabla hajaendelea yule mwanamke pale mlangoni alimkimbilia na kumwekea mkono mdomoni na kumfanya ashindwe kusema.

"Aa, bado nina usingizi," alisema mdogo wangu kabla hajamaliza kusema kisha akajitupa kitandani kulala moja kwa moja.
Yule mwanamke alirudi tena mlangoni akasimama vile vile kama alivyosimama mara ya kwanza.

"Sasa umenikumbuka?" aliniuliza.
"Sikujui kabisa," nilimjibu kwa mkato.
"Jamani wewe," aliniambia kwa sauti kama ya mahaba sasa. Nilishangaa sana.
"Kama unaingia ndani kwangu ingia, kama unatoka toka," nilimwambia kwa ukali kidogo.

"Kwani si nilikuwa ndani mwako na sasa naondoka zangu," alinijibu yulr mwanamke huku akizidi kujitanda sawa sawa ule ushungi.

Niligundua kuwa, moja kati ya malengo yake yalikuwa ni kuhakikisha simtambui kwa sura. Kwani hata sauti yenyewe ilionekana kwamba alikuwa anajitahidi sana kuibana ili isitoke ile yenyewe.

Kwahiyo picha ya moja kwa moja hapo ni kwamba alikuwa akijua mimi namtambua sawa sawa.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 79.

Ndipo nilipoanza kumfikiria mdogo wangu na ile ndoto yake baada tu ya kuamka kutoka usingizini. Kwamba alimuota vibaya yule mama jirani kule kazini. Nilizidi kuamini kuwa, yeye ndiye msumbufu wa tabu zangu zote.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 80.

"Kama sio yeye kwanini wakati mdogo wangu anasema vile yeye alimkimbilia akamziba mdomo asiseme na sijui akamfanya nini hadi mdogo wangu akalala usingizi ghafla!" ni maswali niliyojiuliza mwenyewe nikitumia vigezo vyangu ninavyovijua mimi.

Nilipoangalia tena mlangoni, yule mwanamke alinipungua mkono kama vile alikuwa akisubiri nimwangalie ili afanye hivyo, kisha akatoweka ghafla.

Kumbe na mimi nilikuwa katikati ya mawazo ya kutekwa kwani kutoweka kwake kulinirejeshea akili zangu timamu na kuanza kuona ukubwa wa tukio lile. Nilijikuta nikihema kwa nguvu zangu zote huku nikiogopa zaidi ya ilivyokuwa awali.

Nilitoka kitandani na kusimama katikati ya chumba huku miguu ikicheza kwa kutetemeka kwa woga. Kila wakati niliangalia mlangoni huku nikiiona sura ya yule mwanamke imesimama kama vile mwanzo.

Pia ile sauti ya maneno ilikuwa ikijirudiarudia kila sekunde huku ikiacha mwang'wi chumbani wakati chumba kilikuwa na vitu ambavyo isingekuwa rahisi kuwepo kwa mwang'wi.

Nilikwenda hadi mlangoni na kufungua kitasa kwa funguo lakini sijui mawazo gani yalinijia nikajikuta nikiacha kuufungua na kuufunga tena kwa funguo.
Nilirudi kitandani kulala.

***
Asubuhi ya saa moja na nusu kesho yake, mimi na mdogo wangu tulikuwa ndani ya daladala tukielekea kazini kwangu.
Kila nilipomwangalia mdogo wangu nilitamani sana kumuuliza kuhusu ndoto aliyoota jana yake usiku ili inipe mwanga wa yale yote yaliyokuwa yakinitokea.

Lakini kila nilipomwangalia na kutaka kumwambia, kuna kitu kilijitokeza na kunifanya niache.

Mfano, kuna wakati niliishia kwa kuanza kusema, " hivi...." kabla sijamaliza konda akauliza kama kuna abiria mwenye chenji ya shilingi elfu tano.

Nikajikuta nimeacha kumuuliza mdogo wangu na kumgeukia konda kwa sababu mimi nilikuwa na chenji ya pesa hiyo..
Lengo langu lilikuwa ni kumuuliza, "hivi usiku ulisema uliota ndoto mbaya kumuhusu yule mama pale kazini, kwani ulimuotaje?"

Halafu mfano mwingine. Kuna wakati nikaanza kwa kutaka kumuuliza, "usiku uli..." lakini mama mmoja aliyekuwa amekaa jirani yangu mtoto wake alipiga kelele za ghafla! Huku akinyoosha kidole nje ya gari kwa kutumia dirishani.
Lengo langu lilikuwa kumuuliza "usiku ulisema uliota nini vile?"

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 81.

Ilifika mahali niliamua kuacha kabisa nia yangu ya kutaka kumuuliza mdogo wangu kuhusu ndoto yake.
Lakini pia niligundua kuwa, hata yeye hakumbuki kama aliota chochote kile kwani angekumbuka si angeniambia.

Tulipofika kazini, mdogo wangu alifungua geti, mimi nikiwa nimesimama nasubiria. Mara walitokea watu watano, wawili wao wakiwa wamevalia kanzu nyeupe sana. Huenda ikawa zilikuwa mpya zile.

"Habari yako bwana fundi?" mmoja kati ya wale waliovalia kanzu nyeupe alinisalimia lakini wenzake walibaki kimya wakiniangalia.
Kwa haraka haraka niligundua kuwa, walitaka kuchongewa jeneza.

"Salama tu, shikamooni," niliwasalimia kwani wote walikuwa wakubwa kwangu. Walikuws rika la baba yangu.

"Marahaba bwana fundi," aliyeitikia shikamoo yangu ni mwingine, lakini pia alivaa kanzu. Wengine pamoja na yule aliyeanza kunisalimia hawakuniitikia shikamoo yangu.

"Bwana tunataka jeneza leo leo muda huu huu, inawezekana?" yilr aliyeanza kunisalimia aliniuliza.

"Inawezekana," niliwajibu.
"Lakini hatutoki, tutakuwa hapa hapa mpaka utakapomaliza,"alisema yule mwenys kanzu wa pili.

Haraka sana nikagundua kwa kutokuwa na uhakika kuwa huenda wale wenye kanzu ndiyo wenye pesa au ndiyo wafiwa halisi.
"Sawa tu," niliwajibu.

Mmoja kati ya wale watatu wasiovaa kanzu, aliingiza mkono mfukoni na kutoa kipimo cha kamba akanikabidhi huku akijipangusa mikono kama vile alishika vumbi.

Kama nilivyootea, mmoja kati ya wale walio na kanzu aliingiza mkono kwenye mfuko wa kanzu na kutoa burungutu la noti nyekundu tupu tena mpya.

Tulikubaliana bei kisha wakalipa huku wengine wakitoka kwenda kusimama pembeni kidogo ambako kuna gogo la mti ulioanguka siku nyingi.

Zile pesa kwa kweli licha ya kwamba zilikuwa mpya sana, lakini pia zilikuwa zinatisha kwani wekundu wake ulitofautiana kabisa na wekundu wa noti nyingine za shilingi elfu kumi.

Pia, wakati naziangalia nilijikuta nikiziogopa tu, nikampa mdogo wangu aziweke.
Dakika tano mbele walikuja wote na kuniuliza kama kuna sehemu wanauza soda, nikawaelekeza duka moja la jirani.

Lakini ili ufike kwenye duka hilo lazima upite nje ya nyumba ya yule mama jirani yangu.
Wakaanza kuelekea huko. Niliwakazia macho ili niwaone mpaka wanapopotea.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 82.

"Kaka nitoe mbao za kuanzia kuchonga jeneza?" mdogo wangu aliniuliza kwa ghafla kiasi kwamba nilishtuka na kujikuta nikiachana na wale watu na kumjibu yeye.
Nilipokumbuka na kurudisha macho kwao, nilibahatika kuona kama mguu wenye kanzu ukifutika ndani ya ile nyumba ya yule nama jirani yangu.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 82.

"Kaka nitoe mbao za kuanzia kuchonga jeneza?" mdogo wangu aliniuliza kwa ghafla kiasi kwamba nilishtuka na kujikuta nikiachana na wale watu na kumjibu yeye.
Nilipokumbuka na kurudisha macho kwao, nilibahatika kuona kama mguu wenye kanzu ukifutika ndani ya ile nyumba ya yule nama jirani yangu.

Je nini kitaendelea?
nipo nawe unyayo kwa unyayo
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom