Sehemu ya 50.
Tulifika Dar saa tisa alasiri. Tulifikia nyumbani moja kwa moja bila kwenda kazini na wala sikuwa na mpango wa kwenda kazini siku hiyo.
Asubuhi na mapema niliamka na kumpa maagizo kadha wa kadha mdogo wangu ingawa na yeye alitaka tuongozane kwenda wote kazini kwangu. Nilimwambia angeanza kesho yake ili kwa siku hiyo akae akiyazoea mazingira ya pale nyumbani.
Nilipofika kazini kwangu tu, kitu cha kwanza kabla sijafungua banda na kuanza kufanya kazi, nilikwenda kumsalimia mama jirani kwani isingekuwa heshima anikute niko kazini tayari wakati na yeye alinipa ushauri wa kwenda nyumbani kulingana na matatizo yangu.
Aliponiona alinichangamkia kwa maana kwamba alikuwa amenikosa kwa siku mbili ambazo sikuwepo kazini kwangu. Aliacha tabasamu akanisalimia.
"Hawajambo wazee lakini?"
"Hawajambo mama, wanakusalimia sana."
"Asante sana, mambo yote yalikwenda salama lakini?" aliniuliza.
"Yote yalikwenda salama mama," nilimjibu.
Mara yule mama aliangalia kule upande wa kibanda changu kama ameona kitu. Na mimi niligeuka kuangalia.
"Fundi sijui yuko karibu?" mtu mmoja aliuliza akiwa amesimama na wengine wengi, wakiwemo wanawake.
Nilikwenda haraka sana huku nikimuaga yule mama kwamba tutaonana baadaye kidogo.
"Sawa baba, tutaongea," aliniambia mama na yeye akiingia ndani kwake.
Wale watu walikuwa ni wafiwa na walikuwa wanahitaji kutengenezewa jeneza la mwanamke mtu mzima.
Walisema maiti wao alikuwa chumba cha maiti Muhimbili, lakini walikuwa wanakwenda kuzika Iringa. Niliwahakikishia kuwa jeneza lao wanaweza kulipata saa tisa na nusu alasiri.
Kwa upande fulani nakiri kuwa, kweli haya mambo yalikuwa yamejaa maajabu kwani spidi niliyokuwa naipata kwenye kutengeneza jeneza si ya kawaida.
Naapa kuwa, kwa wakati ule ningeweza kutengeneza jeneza moja hata kwa saa tatu kama ningeamua. Naamini leo hii kuwa, nilikuwa na nguvu ya ziada, lakini mwenyewe nilikuwa sijui tu.
Walipotoka tu, nilianza kazi. Kama nilivyokwisha kusema, mbao zilikuwepo tayari tena zikiwa zimechongwa na kurandwa. Kazi kubwa kwangu ilikuwa ni kuzipasua tu.
Saa tisa na dakika kama kumi na saba, nilimaliza kazi ya jeneza. Nikaliweka pale pale nje nikiwasubiria wenyewe kuja kulichukua.
Je nini kitaendelea?