Simulizi: Kazi ya Kutengeneza Majeneza

Sehemu ya 55.

Nilitamani sana kumsimulia kila kitu mdogo wangu kuhusu mambo yaliyotokea siku hiyo japokuwa alikuwa anajua kuna mambo ya ajabu yalinitokea kwa kusimulia nilipofika nyumbani Tanga, lakini kila nilipofikiria jinsi ya kuanza ile sauti ya kunionya ilisikika akilini mwangu.

Usiku wa saa sita hivi, nikiwa bado nimelala nilishtuka ghafla lakini bila kujua ni kitu gani kilinishtua. Nilitupa macho moja kwa moja mlangoni na kukutana na maajabu mengine.
Jeneza nililolichonga kazini ambalo lilitakiwa kuchukuliwa kesho yake lilikuwa mlangoni likiwa halina mfuniko.

Nilishtuka sana na kukurupuka kutoka kitandani hadi kwenye kona ya chumba. Lakini kabla sijapiga kelele, sanduku lilitoweka machoni mwangu. Nilitupa macho kumwangalia mdogo wangu pale kitandani kama naye ameshtukia tukio lile. Ghafla nikaliona sanduku kitandani lilikuwa limelala palepale sehemu nilipokuwa nimelala mimi. Hilo nalo liliniogopesha sana.

"Hee! Hee!" nilipiga kelele bila kutarajia. Zilikuwa kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani. Pia kwa mdogo wangu ambaye naye licha ya kelele zangu hakuonesha hata dalili za kugeuka pale kitandani.

Ghafla niliacha kupiga kelele na kulikodolea macho jeneza. Safari hii lilikuwa na mfuniko wake juu.

Pembeni yake kulikuwa na kitu kama kamba nyeusi imelizunguka. Halafu pale pale nikaendelea kusikia ile sauti ikinionya vile vile kwamba, ili kuokoa maisha yangu sikuwa natakiwa kusema kwa mtu yeyote yule kuhusu yale mambo yaliyokuwa yakinitokea.

Nilipata wazo la kumfuata mdogo wangu pale pale kitandani ili nimwamshe na kumjulisha mambo yalivyo. Pia alione mwenyewe lile jeneza. Lakini je, ningemfikiaje wakati jeneza lilikuwa bado lipo kitandani?

Akili za haraka haraka ziliniambia nitoke nje na kwenda kumgongea jirani yangu ili aje aokoe jahazi. Nikiwa nimesimama mlangoni, sijaufungua, ile sauti, safari hii si kwamba ilinijia kwa kuhisi, bali ilisikika wazi wazi mle chumbani.

Nikasita kutoka. Nilibaki nimesimama nikiliangalia jeneza. Kwa jinsi nilivyoona mimi ilikuwa kama tunaangaliana na mtu ana kwa ana.



Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 56.

Ghafla niliona jeneza likitoka kitandani kwa kuseleleka mpaka pembeni ya kitanda. Upande uliotangulia ukateremka chini. Lakini pale chini likawa linapotea taratibu na nusu nusu mpaka likapotea lote.

Lakini licha ya jeneza kupotea nilishindwa kurudi kitandani kulala. Kwanza niliogopa mahali palipotoka jeneza kulala mimi ingawa jeneza lenyewe ni lile ambalo nililichonga mimi. Pili ile sehemu iliyolaliwa jeneza ilikuwa na alama ya jeneza na pia ilinyooka kama shuka lilipigwa pasi.

Hivyo niliogopa mwenyewe kurudi. Ghafla pale pale mahali palianza kufuka moshi.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 57.

Lakini wakati moshi unafuka, ndipo mdogo wangu akashtuka. Lakini hakushituka kuamka bali alijigeuza na kuangalia ubavu mwingine. Sasa aliangalia ukutani wakati mwanzo alikuwa kama analiangalia jeneza.
Nilijikuta nikishuka na ukuta na kukaa chini sakafuni. Machozi yalianza kunichuruzika bila kupenda huku nikiwa na moyo wa wasiwasi.

Nilijifikiria sana. Je, hali ile ni mpaka lini? Na nini itakuwa hatma yangu?
Nikiwa katika kufikiria hivyo, wazo jingine lilinijia, kwamba ni kweli kwa kutengeneza majeneza nilikuwa napata pesa nyingi sana. Lakini mara nyingi sana kila nilipokuwa nimetengeneza jeneza mchana, basi usiku wake nikilala lazima niote ndoto nalawitiwa na mwanaume mwenzangu.

Hili nililikumbuka baada ya kufikiria sana usiku huo. Nikagundua matukio yote hayo yalinitokea baada ya mchana wake kutengeneza jeneza.

Sijui ni nini kilitokea kwani wakati nawaza hayo, ghafla usingizi ulinijia na kulala kabisa. Nililala usingizi mzito. Nilikuja kushituka na mdogo wangu ambaye alisimama mbele yangu akinishangaa baada ya kunitingisha niamke.

"Vipi kaka mbona umelala huku umekaa?" aliniuliza. Nilikuwa kama naweweseka vile kwa jinsi nilivyomjibu.

"He! He! Liko wapi? Limekwenda?" nilisema.
Mdogo wangu aliniogopa hata mimi.
Kwani wakati namjibu hivyo alisogea na kusimama mbali kidogo. Lakini akiwa ananikodolea macho ya mshangao.
"Kaka ni nini?" aliniuliza.

Akili zilinirudia, nikasimama, yeye akakimbilia upande mwingine wa kitanda.
Nilimwambia niko sawa kabisa ila kuna wakati nilijikuta nimechoka kulala kitandani ndiyo maana niliamua kulala pale ukutani.

Kidogo alinielewa na kurudi katika hali ya kawaida.
Nilimuuliza ni saa ngapi, akajibu taarifa ya habari ya Redio One imegonga saa nyingi sana.

"Kwa hiyo si ajabu kuwa ni saa mbili au kasoro," aliniambia huku akitenga vikombe vya chai mezani. Kumbe aliamka mapema sana mpaka kufikia hatua ya kukoka moto na kupika chai.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 58.

Lakini hakuwa amefungua dirisha ndiyo maana mle ndani kulikuwa na giza.
Nilipotoka nje jua kali lilikuwa limepanda sana juu. Redio ya jirani ambayo ndiyo mdogo wangu aliisikia ishara ya taarifa ya habari ya redio One ilikuwa ikimalizia muziki, kwani ulipungua sauti mpaka mtangazaji alipoingilia kati.

"Sasa ni saa tatu kasoro dakika tatu, tatu kamili itakuwa mwisho wa kipindi hiki," alisema mtangazaji.

Niliwakumbuka wale wateja walioweka jeneza lao, nikanawa na kutoka mbio nikimwambia mdogo wangu ningemfuata baadaye. Wale wateja waliahidi sasa nne, hivyo toka nyumbani hadi kazini na kwa usafiri wa daladala ilikuwa lazima nichemke sana ili kuwahi.

Nikiwa ndani ya daladala niliwaza kama kweli ningelikuta lile jeneza! Kwani ndilo lililokuwa nyumbani usiku. Nikiwa nakaribia kazini kwangu, niliwaona wale wateja wakiwa wamesimama nje wakionekana kuongea kwa kulalamika. Pengine kwa kuwa kibanda kilikuwa hakijafunguliwa. Mmoja aliponiona akaangalia saa yake ya mkononi.
Nahisi alitaka kujua kama niliwahi au nilichelewa.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 59.

"Samahani sana jamani, kuna mambo yaliingiliana ndiyo maana nimechelewa kidogo," niliwaomba samahani.
Lakini wao wakasema kuwa, wamekuja si kuchukua jeneza lao bali kuomba tena likae hadi saa kumi jioni kwani kuna ndugu wa marehemu ambaye alitarajiwa kuingia asubuhi kutoka Kenya, lakini amekosa ndege, hivyo angefika mchana.

Niliwakubalia kisha wakaondoka wakiwa na gari lao walilokuja nalo siku hiyo. Na mimi nikaanza kufunga geti ili kwanza nilione hilo jeneza lao kama lipo. Ingawa mmoja wao aliniuliza kama nililitengeneza vizuri, nikamhakikishia kuwa mimi ndiye kiboko wa kutengeneza majeneza maeneo ya pale.
Geti lilifunguka, nikatupia macho moja kwa moja sehemu iliyokuwa na jeneza.

Halikuwepo wala dalili ya kuwepo. Lakini pembeni ulikuwepo ule mfuko wa rambo wenye maua ambao alikuja nao mmoja kati ya wale wateja wangu.

"Mungu wee! Ni kweli?" nilijikuta nikijisemea moyoni mwenyewe. Lakini kwa mbali nilijijibu mwenyewe kuwa, ni kweli nilichokuwa nakiona mbele yangu.

"Sasa itakuwaje?" nilijiuliza.
"Hakuna jinsi, ndiyo hivyo!" nilijijibu."Ina maana nianze kutengeneza jingine chapchap?" niliendelea kujiuliza mwenyewe.
"Kama unaweza anza kutengeneza," nilijijibu mwenyewe tena.

"Hapana sitengenezi. Inaweza kuwa vile vile," nilijiambia tena mwenyewe.
Nilizungusha macho kila sehemu huku nikiwa nimesimama katikati ya chumba hicho kilichokuwa na mbao mbao na zana za kazi.

Kila nilipoangalia mahali nilipoliacha jeneza jana yake jioni, palikuwa kama hapajawahi kuwekwa kitu chochote kile. Niliishia kutingisha kichwa huku nikijilaumu kitu, lakini nikiwa sijui ni kitu gani nilichokuwa najilaumu nacho.

Ukweli ni kwamba jeneza halikuwepo na sijui lilikwenda wapi! Ingawa usiku lilinitokea nyumbani, ina maana halikurudi lilikotoka.
"Huyu mama jirani yako ndiye anayekuchezea kwa mambo yote haya," kama niliisikia sauti ikisema hayo kichwani mwangu. Lakini najua ilikuwa mawazo yangu.

Kisha nikafikiria sana kuhusu uamuzi wa kuanza kazi upya ili hapo saa kumi jioni watakapokuja wale watu wakute jeneza lao au la! Nilipowaza sana nikagundua kuwa, itakuwa ujinga sana kama sitalitengeneza jeneza jingine. Sasa watamchukuaje maiti wao kama sitalichonga jipya.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 60.

Kwa sababu halitalala kwangu tena niliamua kulichonga jeneza jingine.
Mpaka inafika saa kumi na nusu jioni, wale wateja walikuwa hawajatokea. Na mbaya pia, sikuwa nimemaliza jeneza lao. Lilibaki sehemu ndogo sana, hata kama wangekuja isingekuwa tabu kumalizia wakiwa pale pale.

Saa kumi na dakika kama thelathini na tano hivi, yaani dakika tano baada ya saa kumi na nusu nilisikia mlio wa gari lile walilokuja nalo asubuhi, kwani ulikuwa kama unamisi halafu kama 'eksosi' ilipasuka mahali, kwa hiyo lilikuwa linatoa mlio mzito.
"Hao wanakuja," nilisema moyoni mwenyewe.
Lakini cha kushangaza ni kwamba mlio huo ulikuwa unakaribia mpaka kwenye kibanda changu kwa upande wa kaskazini ambapo kuna njia kuu ya magari. Lakini hilo lao lilikuwa halifiki kabisa.

Niliingia kwenye uchochoro fulani na kutokea upande wa pili ili kuangalia kama wana matatizo gani, lakini sikukuta licha ya gari lao, hata lolote jingine.
Sasa mlio huo wa gari ukahamia kule kibandani kwangu nilikotoka.

Nilirudi mbio ingawa ukweli ni kwamba, hakukuwa na njia ambayo gari linapita mpaka kule.
Nilipofika, mlio ule ule wa gari lile ukarudi kule kule barabarani nilikotoka.
Nikabaki nimesimama huku nikishangaa sana.

Je nini kitaendelelea?
 
Sehemu ya 61.

Mpaka inafika saa kumi na mbili jioni, walikuwa hawajafika na kila wakati mlio wa gari lao ulikuwa ukiendelea kusikika.
Ilipofika saa moja, wasiwasi uliniingia kuwa, wale watu watakuwa wamekwamia wapi sasa. Na mimi nitakaa hapo mpaka saa ngapi nikiwasubiri wao?

Nilipata wazo la kuliacha jeneza nje kisha mimi kwenda nyumbani kwa yule mama jirani kumwachia maagizo kwamba niliacha jeneza nje, wakija watu wanalitaka awaruhusu kwani ni wenye nalo.

"Sawa liko wapi?" yule mama aliniuliza huku akinifuata kwa nyuma kwenda kumuonesha.
Tulipofika nikasikia tena mlio wa lile gari kwa barabarani. Safari hii ulikuwa juu zaidi na breki zikafungwa, nikamwambia mama basi kwani watu wenyewe ndiyo hao ambao gari lao linasikika mlio huko barabarani.

Nikakimbia hadi barabarani ambako nilisikia mlio. Lakini cha ajabu nilipofika sikukuta gari lolote, achilia mbali lile ambalo niliamini ndilo.
Niliguna kwanza kisha nikaachia tabasamu kama vile nilikuwa nimegundua nimefanya ujinga fulani vile.

Niligeuza kurudi mwenyewe kibandani kwangu huku nikiwa nimekosa amani ya moyo kutokana na tukio lililojitokeza.
Nilimkuta yule mama jirani akinisunbiri kwa hamu huku akinitania kwa kuniambia kwamba wateja wasiozingatia saa watanifanya nilale nje ya nyumbani kwangu kwa siku hiyo.

Na mimi nilicheka lakini nikiwa sina la kumjibu wazi wazi kuhusu tuhuma zake hizo. Yeye alionekana kupenda kuendelea ucheka na kuuendeleza utani ule kwa muda mrefu zaidi ya nilivyofikiria mimi.

Nilikatisha kwa kumwambia yale yale niliyomwambia wakati ule, kwamba naliacha jeneza nje ya kibanda changu cha kazi, wakija watu na kujitambulisha kuwa waliacha toka jana yake wakaahidi wangelifuata kesho yake basi awape, kwani kwa vyovyote vile watakuwa ndiyo wenyewe.

"Sawa mimi nipo," mama jirani alinijibu huku akijikunyata kwa baridi ya jioni.
Lakini kwa upande mwingine mimi kuna sauti kama ilikuwa ikiniuliza swali fulani. Nalo ni hili.

"Wewe unamuamini vipi huyo mama jirani yako mpaka unamwachia kitu kikubwa kama hicho yeye? Je, kama yeye ndiye mbaya wako?" hiyo ni sauti ilikuwa ikisema nami kwa namna ya kusikika akilini. Lakini nikaipuuzia moja kwa moja.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 62.

Niliondoka mpaka nyumbani na kupumzika baada ya kuoga maji jioni hiyo. Mdogo wangu aliponiuliza kwanini sikumfuata kumchukua kama nilivyomuahidi wakati naondoka asubuhi, nilimwambia aniache kila kitu nakisimamia mimi mwenyewe, siku ikifika tutakwenda. Akakaa kimya.

Usiku nikiwa nasoma gazeti moja hivi, kabla sijalala, yule bibi mwenye nyumba alimtuma mjukuu wake aje kuniita.

Nilipokutana naye aliniuliza kwanini sijampa maendeleo ya safari yangu wakati na yeye alinishauri kwenda nyumbani kujiangalizia matatizo yangu?

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 63.

Nilimuomba msamaha kwamba toka nimerudi mambo yangu yamekuwa mengi sana ndiyo maana tulishindwa kuonana na kumsimulia habari za safari.

Hata hivyo kwa mara nyingine tena nikasikia sauti ya mwang'wi ikinionya kutomwambia habari yoyote yule mzee kwa kuwa huenda ni yeye ndiye mbaya wangu.

"We huoni siku zile baada ya kugundua una safari alikuwa hachoki kukuuliza na kujifanya anakusisitizia usafiri. Pale alikuwa anataka kujua kama utasafiri kweli au vipi ili na yeye ajiimarishe anavyojua mwenyewe. Na si ajabu yeye ndiye alimfanya baba yako awe vile siku ile ya kufanya tambiko," sauti iliniambia.

Lakini pia nilikuwa na uzoefu na sauti. Kuna sauti ambazo zikikujia kwenye masikio na kupenyeza mpaka akilini unaweza kuamini kwamba unachokisikia ndicho, wakati hata sicho.

Nilimwambia bibi kwamba matatizo yangu yote mzee wangu aliyasikia na kunifanyia mambo ya kinyumbani kwetu. Wakati namwambia hivyo alikuwa akikaza macho kuniangalia kama vile alikuwa anategea kusikia nitakachomalizia kusema.

"...Lakini mwisho baba aliniambia kuwa huyo mtu anayenifanyia mchezo huo zake zimekwisha endapo atarudia tena," nilimaliza kwa kumwambia yule bibi mwenye nyumba.
Nilimuona akijiweka sawa kitini kisha akataka kama kusimama huku akiwa ameiegemesha mikono wake kwenye bakora anayopenda kuitumia akitembea.

"Kwa hiyo toka umerudi hujatokewa na maajabu yoyote?" aliniuliza. Swali hilo kwangu nililiona kama lina mtego kwani kama ni yeye mbaya wangu, nikisema sijatokewa ataona nimemdanganya kwani anajua jinsi alivyoendelea kunitesa hata baada ya kurudi toka Tanga.

Lakini pia niliona kuwa lolote lile kwake ni sawa.
Nikimdanganya kuwa sijatokewa atajua, nikimkubalia pia atajua. Kwani kama ni yeye ndiye mbaya sasa ni kitu gani ambacho atakuwa hakijui?

Ilibidi nimdanganye kwa kumwambia kuwa sijatokewa na maajabu yoyote yale kwa sababu kama ningekubali kumwambia ukweli matokeo yake yangekuwa ni yaleyale.
***

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 64.

Asubuhi ya saa moja mimi na mdogo wangu tulikuwa ndani ya daladala tukienda wote kazini kwangu. Yeye mdogo wangu alikuwa anakwenda kwa mara ya kwanza.

Tukiwa tumeshafika lakini kwa mbali huku nikiwa napaona kazini kwangu, nilimuona yule mama jirani akiwa amesimama nje ya banda langu akiwa peke yake lakini kama anashangaa shangaa. Mapogo ya moyo yalilipuka kwa kasi ya ajabu. Nikahisi kupungukiwa nguvu kwa haraka. Alikuwa hajatuona.

Nilipoangalia vizuri sikuona lile jeneza. Nikajua kwwa vyovyote vile wale wateja walishafika kulichukua jeneza lao. Lakini je, mama alikuwa anatafuta nini asubuhi ile?
"Shikamoo mama," nilimsalimia baada ya kufika. Alishtuka sana kusikia sauti ya salamu. Akageuka.
"Aa, marahaba. Afadhali umekuja," alisema.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 65.

"Vipi kuna matatizo mama?" nilimuuliza licha ya kwamba sikuwa nimeliona jeneza. Akilini mwangu nilijua wenyewe walikuja kulibeba usiku nilipoondoka.

"Kama unavyoona mwanangu jeneza lako mpaka naingia ndani kulala saa nne usiku walikiwa hawajaja kulichukua lakini naangalia asubuhi sijaliona. Inawezekana walikuja wakalichukua wenyewe kweli?" mama alisema.

Nilitingisha kichwa kwa maana haiwezekani. Halafu jeneza gani linafuatwa usiku? Nilijihoji mwenyewe bila kutamka.

"Basi kuna matatizo kijana! Tena kuna matatizo hasa, angalia sana," mama alisema.
"Au limeibiwa, si nasikia Daresalaam kuna vibaka sana," mdogo wangu alisema akichangia tukio lile.

"Kuna wezi kweli lakini si wa kuiba jeneza mwanangu. Mtu aibe jeneza akalifanyie kazi gani? Kama lingekuwa la dhahabu tungesema kweli," alisema mama akiwa amejishika kiunoni.

"Sasa jamani sijui nifanyaje? Lakini hata hivyo sidhani kama na wao bado wana shida na jeneza, hata kama kweli limeibiwa na wezi," nilisema huku moyoni nikijua ni mchezo ule ule unaendelea kwangu.
Nilimuomba mama aendelee na mambo yake huku nikimpa pole. Kwanza kwa kumsababishia kuchelewa kulala usiku, pili kwa hofu iliyompata baada ya kuamka asubuhi na kugundua jeneza halipo.

Alipoondoka tu, nilifungua geti kubwa ili kutoa vifaa vya kazi kisha nikamjulisha mdogo wangu kuwa ile ndiyo sehemu yangu ya kazi lakini sikumfafanulia matukio yaliyokuwa yakiendelea kutokea pale zaidi ya vile alivyosikia nikisimulia kule nyumbani Tanga.

"Kaka huyu mama mbona simwelewi elewi, mzima kweli?" ghafla mdogo wangu aliniuliza.
Kabla sijamjibu, nilikumbuka kuwa sikuwa nimemtambulishamdogo wangu kwa mama wala mama kwa mdogo wangu. Sijui ni kwanini.

"Mzima vipi kwani?" nilimjibu, nikamuuliza.
"Namuona kama ana macho ya woga woga hivi. Utafikiri yeye ndiye aliyeliiba hilo jeneza," aliendelea kusema mdogo wangu. Nikacheka na kuyaacha hayo.

Nilimwingiza ndani ya banda, nikamuomba anitolee baadhi ya mbao ambazo nilimwelekeza. Lakini mwenyewe mdogo wangu akasema atatoa mbao zote asafishe kwanza ndani kote, kisha za kubaki nje zitabaki na kurudi zitarudi.


Je, nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 66.

Alitoa mbao zote, huku nikimwamboa kuwa akichoka apumzike kwanza. Mara alitokea mama akiwa ameshika kikapu.
"Nakwenda mjini mara moja, akija mgeni wangu anaweza kuingia ndani anisubiri," alisema mama huku akinipa funguo.
Dakika kumi na tano baada ya mama kuondoka tu, nilisikia mlio wa gari upande wa barabarani nikahisi ni wale wateja.

Nilikaza macho ili kuona ni kweli. Ni kweli mara walitokea wao na wengine watatu. Wao wawili walikuwa wamevaa vile vile kama walivyovaa siku ya kwanza kuonana nao. Hilo ni kawaida kwa wafiwa.

Moyo ulinilipuka sana, nikajisikia kutetemeka. Walinikazia macho huku wakitabasamu. Wakati mdogo wangu alikuwa anapanga mbao nje kwenye kona ya banda.

"Samahani sana bwana kuvurugika kwa utaratibu wa usafiri wa ndugu wa karibu wa marehemu wetu ndiyo uliotufanya hata jana tusije," mmoja wao alisema akinipa mkono wa salamu.

"Poleni sana," nilijibu hivyo tu huku nikiangalia huku na kule kwa kutunga kitu cha kuwaambia.

"Sasa acha tulichukue ili tuwahi," alisema mmoja akiingia ndani na wenzake wakimfuata. Na mimi nilimfuata haraka ili kumwambia kitu cha kumdanganya. Na pia nilipanga kuwa, watakaponiuliza itakuwaje sasa kuwa kulikosa jeneza lao, ningewapeleka sehemu wanayotengeneza majeneza na kuwanunulia hapo.

Ajabu, jeneza lilikuwepo pale pale na juu yake kulikuwa na ule mfuko wa rambo.
"Ha!" nilijikuta nikihamaki hivyo lakini nikajikausha kama si mimi niliyehamaki.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 67.

"Tunashukuru sana kwa hifadhi yako bwana fundi. Mungu akubariki sana," alisema mmoja huku wenzake wakiinama kulibeba jeneza na mimi nikiwasaidia mpaka walikuwa wamepaki gari walilokuja nalo.
Niliporudi, nilimkuta mdogo wangu amesimama wima huku akihema kwa nguvu sana.

"Kaka unajua sielewielewi," aliniambia.
"Nini?" nilimuuliza.
"Kwani wewe hujui kaka?" aliniuliza akionekana anaogopa usoni.
"Hili jeneza si ndiyo tulikuwa tunalita..." hakumaliza kusema akanyamaza.

Kisha akawa anaangalia kila upande kama vile alikuwa akisikia sauti fulani sasa anatafuta anayeongea yuko wapi.."Vipi mbona na mimi sikuelewielewi," nilimuuliza mdogo wangu kufuatia hali aliyokuwa nayo.

"Hata salama tu," alisema akiendelea na kazi zake. Mimi moyoni nilipanga kumwambia hata mimi sijui imekuwaje!
Lakini nikasikia tena ile ile sauti ikinionya juu ya uamuzi wangu wowote wa kumwambia mtu kuhusu matukio yanayotokea.

Ilibidi nibaki kimya na mpole ili kuokoa uhai wangu. Kwani sikuwa nimejitolea kupoteza maisha kwa kukiuka masharti hayo ya mtu nisiyemfahamu.

Hata yule mama aliporudi nilijiuliza kumwambia habari za lile jeneza kupatikana na wenyewe kulichukua. Lakini cha ajabu sasa, yeye akasema:

"Kama nimewaona wale watu wako wamekuja kuchukua jeneza lao, walilipata?"
Nilimjibu ndiyo, akaniuliza lilikuwa wapi, nikamjibu ndani, lakini hakushangaa wala hakuuliza zaidi ya hapo. Akaingia ndani kwake.

Aliniacha na mawazo mengi sana kwani sikujua yeye alikuwa wapi mpaka awaone wale wamekuja kulichukua jeneza wakati aliaga anakwenda mjini.

Pia muda waliokuja wale kuchukua jeneza lao na muda alioondoka yeye vilipishana sana. Hata njia aliyorudia yeye ni tofauti na ile waliojia wale waliokuja kuchukua jeneza lao. Nilijikuta nikijilaumu kwanini sikumuuliza maswali hayo yote na pia sikuwa tayari kumuuliza baadaye.
***

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 68.

Ilikuwa ni siku ya jumamosi moja, niliposikia watu wakisema kuwa kuna mkutano mkubwa sana wa kikristo kwenye viwanja vya Jangwani. Sijui ni kwanini kwani nilijikuta nikitamani kwenda kusikiliza hayo yanayoongelewa kwenye mkutano huo wa kikristo.

"Nitakwenda unaanza saa ngapi?" niliwauliza wale watu.

"Kuanzia saa kumi jioni kwa siku saba. Na ulianza jana," mmoja wao alinijibu.
Halafu mwingine akaniambia kuwa, ni mahali pazuri kufika kwani hata kama una matatizo makubwa yanaombewa na kutoka.

Niliwauliza kama mtu unatokewa na mambo ya ajabu, wakasema kila tatizo litakwisha. Nilishikwa na hamu sana ya kufika huko Jangwani kusikia mwenyewe kinachoongelewana ikibidi niombewe nipone kwa matatizo yangu.

Nilimwambia mdogo wangu kuwa ikifika saa tisa na nusu siku hiyo aniambie kuna sehemu nakwenda.

Niliendelea na kazi zangu mbalimbali huku kila wakati nikiangalia muda kama umekaribia. Lakini ilipofika saa tisa na dakika ishirini na tano, mdogo wangu alinikumbusha kuhusu agizo langu.

Niliingiza baadhi ya zana za kazi ndani kisha nikamwambia ikifika saa kumi na mbili afunge kwani mimi sirudi. Nikampa maagizo ya baadhi ya watu ambao wangefika kuchukua kazi zao.

Nilipanda daladala la Kariakoo ili nishuke Jangwani. Lakini cha ajabu ni kwamba, nilishtuliwa kutoka usingizini na mama mmoja aliyekaa kiti kimoja na mimi akisema tumefika safari. Niliangalia huku na kule na kugundua kuwa, kufika kwenyewe si Jangwani bali ni Kariakoo kabisa.
Nilishangaa sana!

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 69.

"Ilikuwa niteremke jangwani kwenye mkutano," nilimwambia yule mama. Naye akashangaa sana huku akinipa pole nyingi sana.

"Itabidi ugeuze nalo hili hili," alinishauri sasa.
Lakini nilishuka na kuvuka upande wa pili wa kituo ambako kuna daladala zilikuwa tayari kwa kuondoka.

Nilikaa siti ya mbele dirishani. Na daladala lilianza safari dakika mbili mbele baada ya mimi kuingia.

Lakini sijui ni nini, kwani nililala na wakati nashtuka, daladala lilikuwa linapanda kilima cha kukaribia mapipa pale maeneo ya Kwamacheni. Nilishuka hivyo hivyo na kurudi nyuma mpaka Jangwani kwa miguu.

Kufika tu kwenye kona ya kukata kuingia Jangwani na kukutana na barabara kuu, nilikuta watu wengi sana wamesimama mbele yangu. Weusi tii wote wakiniangalia.
"Unakwenda wapi huku?" mmoja ambaye alikuwa nyuma ya wenzake aliwapita wote na kuja mbele yao na kuniuliza.

Badala ya kumjibu niligeuka nyuma yangu ili kuona kama kulikuwa na wenzangu wengine ambao nao walikuwa wakielekea mkutanoni hapo.

Ni wengi walikuwa wakivuka barabara kwenda kwenye mkutano huo huku wengine wakiwa wawili wawili, wengine zaidi na wapo ambao ilikuwa ni mtu mmoja mmoja lakini katika msululu au foleni ya kwenda huko.
"Nakuuliza wewe?" yule mtu akaniuliza tena huku macho yake akiyaelekezea kwangu.

Kwa kuwa katika maisha yangu sikuwahi kuhudhuria hata mkutano mmoja wa kikristo hivyo sikujua wale watu walikuwa ndiyo walinzi wa mkutano ule na sasa walijua mimi siyo mkristo ama vipi.

Ajabu ni kwamba watu wengine walipokuwa wakipita wale watu wa kutisha walitawanyika pembeni ya barabara inayokwenda mkutanoni wakapita salama.
"Rudi," waliniambia wale watu.

Sikuwa tayari kugeuka kurudi mapema. Niliendelea kusimama lakini kwa tahadhari kubwa sana kwa lolote lile litakalotokea.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 70.

Hata baadhi ya magari yalipokata kona kuingia barabara ya kwenda viwanjani wale watu waliyapisha pembeni mpaka yalipopita lakini wakarudi tena ili kunidhibiti mimi.
Kiufupi walinitisha sana, sikuwahi kuona watu weusi kama wale na siamini kama nitakuja kuona tena hapo siku za mbele. Walitisha!

Ghafla! Kibasi kimoja chenye watu waliokuwa wakiimba nyimbo za kikristo kwa furaha kilikata kona kuingia barabara ile. Cha ajabu wale watu wakatoweka ghafla bila kujua walikopotelea.

Niliona ile ndiyo ilikuwa nafasi yangu ya pekee kufika uwanjani. Nililifuata lile basi kwa kulikimbilia nyuma ingawa nilikuwa nikioga vumbi kupita kawaida.

"Ina maana umetupuuza siyo?" yule mtu aliniuliza akiwa amesimama mbele ya wenzake palepale kwenye kona kama mwanzo.

Ina maana kukimbia kwangu ilikuwa ni bure. Nilisimama ghafla na kurudi palepale pembeni nilipokuwa nimesimama mwanzoni.

"Vipi mbona unasita? Twende?" mwanaume mmoja aliyekuwa na mkewe na watoto aliniambia akiwa ameshika Biblia ndogo mkononi. Walikuwa wakielekea mkutanoni.
Sikufanya ajizi, niliamua kugeuka kurudi kazini kwangu huku nikiamini kwamba bado wabaya wangu walipania kuniangamiza kwa kunizuia kwenda hata kwenye eneo ambalo ningeweza kupata ukombozi kama siyo msaada.

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 71.

Nilipofika kibandani kwangu nje nilimkuta yule kijana aliyetoa oda ya kutengenezewa kitanda siku za nyuma.

Pia nilimkuta mdogo wangu bado hajafunga na alikuwa akiongea na yule kijana.
"Afadhali umekuja fundi," alisema yule kijana akinipa mkono wa salamu.

Nikimuuliza kama alifuata kitanda chake au alikuja kunisalimia tu.
"Kwani siku ya ahadi si ilikuwa jana fundi?" alisema akimaanisha alichofuata ndicho hicho.

Nilikuwa bado kupaka vanishi kwa hiyo nilimuomba arudi kesho yake kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda sana siku hiyo. Alikubali akaondoka kwa shingo upande. Niliona kabisa namna alivyo kasirika.
Wakati anaondoka nilikumbuka kumuuliza kuhusu siku ile aliyotoa oda kisha akaondoka.

Je, alielekea usawa gani?
Nilimrudisha ili kumweka sawa kwa ajili ya swali hilo naye akajibu bila wasiwasi kwamba anaishi kwa mama Sajuki.
"Mama Sajuki ni nani?" nilimuuliza kwanza alicheka kama vile kunishangaa.

"Siku zote hizo humjui mama Sajuki!"
"Simjui kabisa," nilimjibu, akazidi kucheka.
"Kwani mama mwenye nyumba ile anaitwa nani?" aliniuliza huku akielekeza kidole kwenye nyumba ya yule mama jirani.

Nilimkatalia kwa sababu nijuavyo mimi yule mama anaishi peke yake kwanza. Pili sikuwahi kusikia kwamba anaitwa mama Sajuki. Mimi ninajua anajulikana kwa jina la mama Livingstone. Tena kwamba Livingstone ni jina la marehemu mume wake.

Hizi taarifa mimi nilisikia kwa yule mzee Jumaa aliyepotea kimiujiza na ndiyo maana nilikuwa nikimfikiria kwamba alikuwa akiishi nyumbani kwa mama jirani.

"Mimi najua anaitwa mama Livingstone," nilimjibu akaachia tabasamu huku akiondoka bila kutoa jibu wala ufafanuzi.
Safari hii nilimkazia macho ili nijue mwelekeo wake na uchochoro atakaopotelea.

Kweli alikwenda kwenye nyumba ya mama Livingstone au mama Sajuki kama anavyodai yeye, akaingia.
"Hivi inawezekana muda wote huu tangu nianze kazi hapa nisijue kama ndani kwa yule mama kuna kijana anaishi?" nilijiuliza mwenyewe.

"Halafu mbona yule mama kila akiondoka nyumbani kwake funguo anaacha kwangu, kijana wake anakuwa wapi?" niliendelea kujiuliza.
Mara yule mama alitokea akawa anakuja kwangu.

Je nini kitaendelea?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom