Sehemu ya 44.
"Sijakuelewa bibi, au unataka kusema matatizo yanayonipata yalitokea nyumbani Tanga?"
"Kijana nasema hivi yale uliyosimulia siku ile kwamba yalikutokea huko kazini kwako, yaendee Tanga vipi mpaka nikufafanulie?" alisema bibi.
Hapo tena akawa amebadili mtazamo wangu kuhusu yeye. Wakati mimi nilijua yeye kababaika, kumbe sivyo, amefurahi sana na ushauri wake ni huo.
"Mh," niliguna.
"Unaguna nini sasa?"
"Sijajua nini kinaendelea bibi," nilimjibu.
"Hujajua nini bwana. Kila kitu kiko wazi kabisa. Wewe safiri, kawaambie wazazi wako kila kitu kuhusu matatizo yako. Wao watajua wakufanyie nini, vinginenvyo hapa mjini kijana wangu utakufa siku si zako," alisema bibi.
Niliingia ndani bila kumuaga bibi nilipokuja kutoka, nilikuwa nimeshika begi langu dogo mkononi nikimwambia bibi.
"Bibi labda keshokutwa au mtondogoo ndiyo nitarudi."
"Haya bwana wahakikishie kwamba hawa watu unaokaa wanajua matatizo yako," alisema bibi wakati natoka.
Njiani wakati nakwenda kituoni niliingiwa na mawazo kuwa, bado pengine yule bibi ndiye aliyekuwa mbaya wangu. Na pengine alikuwa akisubiri nifike nyumbani kwetu ili aanze kunifanyia mauzauza.
Nilifika kituo cha mabasi na kupata basi saa nne kamili asubuhi tayari kwa safari ya kwenda Tanga.
Nilifika nyumbani saa nane mchana, baadhi ya ndugu walikuwepo, lakini wengine walikuwa katika mihangaiko yao.
Waliokuwepo nyumbani walinipokea kwa mshangao kwani walisema kuwa, nimebadilika sana.
Nimenenepa sana na kunawiri tofauti na nilivyoondoka kwenda Daresalaam.
Jioni yake mama aliniuliza mambo yangu yanakwendaje Dar? Nikamjibu kuwa nilikuwa niko pale nyumbani kwa makusudi maalum.
"Lakini yaliyonileta siwezi kukwambia mpaka awepo baba," nilimwambia mama.
"Ina maana kuna matatizo, mi nilijua umekuja kusalimia," alisema mama.
"Hapana mama, kuna matatizo tena makubwa sana."
Kwa kauli yangu hiyo, ilibidi mama afanye kazi ya kumtafuta baba kwa kuwatuma watoto sehemu mbalimbali ambazo anapenda kufika, hasa kwenye maeneo wanayocheza bao.
Mara baba alifika haraka sana akisema kuwa, aliweza kuhisi kuna mgeni nyumbani lakini kila alipokuwa akitaka kusimama kurudi nyumbani alikuwa akisikia uvivu.
Je nini kitaendelea?