Kiimani zaidi
ZABURI 137
Maombolezo juu ya maangamizi ya Yerusalemu
1 Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi,
Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.
2Katika miti iliyo katikati yake
Tulivitundika vinubi vyetu.
3Maana huko waliotuchukua mateka
Walitaka tuwaimbie;
Na waliotuonea walitaka tuwatumbuize;
Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.
4Twawezaje kuimba wimbo wa BWANA
Katika nchi ya ugeni?
5Nikikusahau, Ee Yerusalemu,
Mkono wangu wa kulia na upooze.
6 Ulimi wangu na ugandamane
Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.
Nisipoikuza Yerusalemu
Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu.
7 Ee BWANA, uwakumbuke wana wa Edomu,
Siku ile Yerusalemu ilipotekwa.
Kwa namna walivyosema, Bomoeni!
Bomoeni hata misingini!
8 Ee binti Babeli, uliye karibu na kuangamia,
Heri atakayekupatiliza, ulivyotupatiliza sisi.
9Heri yeye atakayewakamata wadogo wako,
Na kuwaseta wao juu ya mwamba.