Nchimbi apata mpinzani uenyekiti Vijana CCM
Mwandishi Wetu
Daily News; Monday,May 19, 2008
MBIO za kuwania uenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeanza kupamba moto baada ya Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Mkoa wa Tabora, Hussein Bashe, kutangaza azma yake ya kuwania nafasi hiyo inayoshikiliwa kwa sasa na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Emmanuel Nchimbi.
Bashe alitangaza azma hiyo Dar es Salaam jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, huku akiahidi mabadiliko makubwa ya UVCCM Taifa endapo atafanikiwa kumrithi Dk. Nchimbi.
Kijana huyo aliyezaliwa Agosti 26, 1978 wilayani Nzega ambaye kwa sasa ni Meneja Mauzo na Usambazaji wa New Habari 2006 Limited, amesema kutokana na dhima kuu ya UVCCM ya kuandaa vijana kuwa raia wema, lakini pia kuwa tanuri la kupika viongozi wa Taifa, "hali ya mabadiliko katika umoja huu kwa sasa ni jambo lisiloepukika."
"Kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa ndani ya umoja wetu," alisema Bashe, ingawa anakiri kuwa historia ya jumuiya hiyo imejengewa misingi na viongozi waliopita na waliopo na msingi hiyo ni kama umoja na kujiamini, vitu ambavyo alisema ni vya msingi kwa jumuiya yenye dhima kama UVCCM.
"Hivyo basi leo natangaza msimamo na azma yangu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa UVCCM Taifa nikiwa na lengo la kufanya mapinduzi hayo na kuurejesha umoja huo kwenye chati yake kama ilivyokuwa enzi za TANU, kuwa chombo kinachobeba sura ya vijana wa taifa hili," aliongeza.
Katika baadhi ya mambo anayokusudia kuyafanya akichaguliwa ni kuifanya jumuiya hiyo kuwa jukwaa la vijana wote; kubadili muundo wa utawala/oganaizesheni; kubadili kalenda ya vikao vya jumuiya; kuipatia uhai Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji; kuifanya jumuiya kujitegemea kiuchumi; kudhibiti uhamisho usio wa lazima na kuboresha maslahi ya watendaji.
"Ili kusaidia vijana wafikie maisha bora kwa kila Mtanzania, nitafungua milango ya mijadala kwa wana CCM na wasiokuwa wana CCM ikiwa wote tutakutana kwa njia ya kutafuta majibu ya matatizo ya vijana wa Tanzania, pia nitasimamia kuwapa Wazanzibari nafasi katika kuongoza idara za jumuiya yetu," alisema Bashe ambaye anasema nafasi hizo zimetawaliwa na watu wa Bara na hilo kwake ni upungufu.
Kwa sasa, jumuiya za Chama Cha Mapinduzi zinaendelea na mchakato wa kuchagua viongozi wa ngazi mbalimbali, na kwa UVCCM wamefikia katika matawi na sasa wanaingia katika kata.
Mbali ya kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM Mkoa wa Tabora, Bashe ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa; Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Tabora; Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa; Mjumbe wa Mkutano Mkuu Wilaya ya Nzega; Mjumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya ya Nzega na Katibu wa Uchumi na Fedha Kata ya Nzega Mjini.
HabariLeo