Sakata la Mahujaji: Utendaji ATCL na Yaliyojiri Hadi Leo Hii

Naona dhana ya uwajibikaji bado ni ngeni kwetu! Kazi ipo!

Rais ameishasema kwamba sakata la mahujaji lilitokana na sababu ndogo ndogo kwa kuwa ATCL bado haijawa na ndege za kwake na hivyo yaliyotokea yangeweza kutokea. Kama hawakuwa na ndege za kwao au kwa maneno mengine kama hawakuwa na uwezo wa kuwasafirisha mahujaji kwanini walijiingiza kwenye hiyo shughuli? Hiyo hasara ya milioni 160 italipwa na nani kama si kutoka kwenye kodi za walalahoi? Nyang'anyi akisikia kauli hiyo hata kama alikuwa na nia ya kujiuzulu unatarajia ajiuzulu? Maana mtu aliyemteua tayari kaishasema kwamba tatizo lilikuwa ni dogo na kwamba serikali inafanya jitihada za kuhakikisha wanarudi mara baada ya hijja. Kwa mwendo huu sidhani kama kuna watu watakuja kuwajibika chini ya utawala wa JK labda kama jamaa akiboronga sana kiasi cha kushindwa kumbeba! Tusitarajie chochote si Nyang'anyi ama Mattaka atakayejiuzulu ... Mkuu wa Kaya ameishawatetea, na hivyo Chenge nadhani anatwanga maji kwenye kinu tu!
 
Rais ameishasema kwamba sakata la mahujaji lilitokana na sababu ndogo ndogo kwa kuwa ATCL bado haijawa na ndege za kwake na hivyo yaliyotokea yangeweza kutokea... Nyang'anyi akisikia kauli hiyo hata kama alikuwa na nia ya kujiuzulu unatarajia ajiuzulu? .... Mkuu wa Kaya ameishawatetea, na hivyo Chenge nadhani anatwanga maji kwenye kinu tu!

Point! ATCL kutokuwa na ndege ni suala jingine na Nyanganyi Mahujaji Inc. ni suala jingine. Mhe. Raisi alipaswa kutofautisha masuala haya mawili.
Kwa maelezo ya Mhe. Raisi ni kuwa it was OK for Nyanganyi Mahujaji Inc kuitia Serikali hasara.CASE CLOSED!
 
Sakata la mahujaji hatarini kujirudia

* Hawajaambiwa siku ya kurudi nchini

* Ni wale waliokwama Uwanja wa Ndege Dar

* Waliopelekwa na Bwakata kurejea Januari Mosi

* Mwenyekiti ATC arushia mpira Serikali


Na Muhibu Said

WASIWASI umetanda miongoni mwa mahujaji 1,077 wa Tanzania waliokwenda Makka, Saudia kwa kwenye ibada ya Hijja, wakihofu kutorejea nchini katika wakati muafaka kutokana na kutokuwa na uhakika wa ndege ya kuwasafirisha.

Habari kutoka Madina, Saudia, ambako mahujaji walielekea jana kwa ajili ya ibada na kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria, zinaeleza kuwa mahujaji hao wamekumbwa na wasiwasi huo baada ya siku waliyotarajia kuanza kurejea nchini, kutoonekana katika kumbukumbu za mamlaka ya nchi hiyo.

Baadhi ya mahujaji, akiwamo kiongozi wa mahujaji kutoka taasisi ya Tanzania Muslim Hajj Trust ya jijini Dar es Salaam, Alhaj Juma Nchia waliozungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa simu kutoka Saudia jana, walithibitisha kuwa na wasiwasi huo.

Ibada ya Hijja kwa mwaka huu, ilikamilika Desemba 22 baada ya mahujaji kutekeleza ibada ya kumpiga mawe shetani katika eneo la Jamarati, lililoko Mina, mjini Makka.

Baada ya kukamilika kwa ibada hiyo, kundi la kwanza la mahujaji hao ambao wiki chache zilizopita walikwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya siku kumi na moja kutokana na kukosa ndege ya kuwasafirisha katika muda muafaka, lilitarajiwa kuanza kurejea Desemba 29, wakati kundi la pili lilitarajiwa kurejea nchini siku inayofuatia.

Wote walitarajiwa kurejea nchini na ndege ya kukodiwa na serikali baada ya kuingilia kati safari yao ya kwenda na kurudi Saudi Arabia baada ya mahujaji hao kukwama kuondoka nchini kwa zaidi ya siku kumi na moja.

Hata hivyo, wakati mahujaji hao ambao safri yao ilioratibiwa na baadhi ya taasisi za Kiislamu za Tanzania Bara na Zanzibar wakishikwa na wasiwasi huo, mahujaji 164 walioratibiwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), wameondolewa wasiwasi, baada ya uongozi wa baraza hilo kuwahakikishia safari yao ya kurejea itakuwa Desemba 31, mwaka huu.

Akizungumza kwa simu kutoka Saudi Arabia jana, Nchia alisema mamlaka ya Saudia inayohusika na usafirishaji, iliwazuia kuondoka nchini humo, baada ya tarehe walizoombewa nafasi ya kusafiri kutokana na kutoonekana katika kumbukumbu za kompyuta za mamlaka hiyo.

Nchia alisema wamekumbana na mkasa huo baada ya kuondoka Makka na kwenda Madina kufuatilia nafasi za safari walizoombewa bila mafanikio.

Alidai kutokana na hali hiyo, walijitahidi kuwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini humo kuomba msaada, lakini hadi kufikia jana jioni walikuwa hawajapewa ushirikiano wowote.

"Kila tunapojaribu kufuatilia Balozi wetu hapoa anatukwepa hivyo hatujui tutaondoka lini. Tunalazimika kupata huduma zote kwa mashirika yaliyoratibu safari yetu," alidai Alhaj Sheikh Asbatt ambaye ni mmoja wa mahujaji walioko nchini humo.

Alipoulizwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), Balozi Mustafa Nyang'anyi, alisema hawezi kuzungumzia suala lolote linalohusika na mahujaji na kumtaka mwandishi awasiliane na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu, Omar Chambo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Serikali ya Kushughulikia Safari ya Mahujaji.

Chambo alipoulizwa, alisema haoni sababu kwa mahujaji hao kuwa na wasiwasi kwani ndege ya kuwarejesha nchini ipo.

Alisema wanachosubiri ni mahujaji hao kupanga siku ya kurejea nchini na kuongeza kuwa siku tatu zilizopita, walituma ujumbe wa watu watatu kwenda Saudi Arabia kushughulikia suala hilo.

"Kule Saudi Arabia tuna Balozi wetu, tumepeleka watu watatu na wamekutana na Balozi. Tutawapelekea ndege. Kazi yetu ni kuhakikisha mahujaji wanarudi nchini," alisema Chambo.

Wakati hayo yakijiri, Katibu wa Idara ya Hijja na Umra ya Bakwata, Alhaj Swed Twaibu aliliambia gazeti hili juzi kwa simu kutoka Saudia kuwa mahujaji wote walioratibiwa safari hiyo na baraza hilo, wako salama na kwamba wanatarajia kurejea nchini Desemba 31, mwaka huu majira ya saa 4:00 usiku na ndege ya Shirika la Ndege la Yemen (Yamenair).

Alhaj Swed alisema kuanzia juzi walikuwa Madina wakiendelea na ibada.

"Mahujaji wote wako salama, hivi sasa tuko Madina tunaendelea na ibada. Tutarejea tarehe 31 Desemba saa 4:00 usiku na Yemenair...," alisema Alhaj Swed.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Taifa, Sheikh Khamis Mataka, ambaye ni mmoja wa viongozi wakuu wa baraza hilo wanaowaongoza mahujaji hao, alimwambia mwandishi wa Mwananchi kwa simu kutoka Saudia jana kuwa wanatarajia kurejea nchini Januari Mosi, mwakani.

"Mahujaji wote wako salama. Hali ya hewa ambayo ni ya baridi na msongamano wa watu, inasababisha mafua, kifua na homa kwa baadhi ya mahujaji," alisema Sheikh Mataka.

Alisema jambo jana walienda Madina ambako watazulu kaburi la Mtume Muhammad (S.A.W.) na kuswali katika msikiti wake (Mtume Muhammad S.A.W.

"Sala moja katika msikiti huo ni sawa na sala elfu moja zinazosaliwa katika misikiti mingine ukiondoa msikiti mkuu wa Makka," alisema Sheikh Mataka.

Alisema mbali na kuzuru kaburi hilo, mahujaji pia watatembelea sehemu mbalimbali za kihistoria, likiwemo eneo la makaburi ya Baqii, walikozikwa maswahaba wengi wa Mtume Muhammad (S.A.W.).

"Hakuna muda maalum wa kuwapo Madina kwa kuwa kuwapo Madina ni nje ya ibada ya Hijja ambayo imeshatimia. Wengi hupenda kukaa siku nane angalau wapate jumla ya sala 40 katika msikiti wa Mtume.

Source: Mwananchi
 
JK akiongea na Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusu miaka yake miwili, mwezi huu wa December alisema:
Naquote: Akijibu swali kuhusu huduma duni zinazotolewa na Shirika la Ndege Tanzania (ATC) ambazo katika siku za karibuni, zilisababisha usumbufu mkubwa kwa mahujaji waliokuwa wakienda kuhudhuria Ibada ya Hija, Rais Kikwete alilitetea na kubainisha kwamba kwa sasa lina ndege moja tu, kilichotokea, lilikubali kuchukua dhamana ya kuwatafuatia usafiri mahujaji hao.

"Tunachofanya ni kuhakikisha tatizo walilopata wakati wa kwenda halitokei wakati wa kurudi. Awali tulianza na ndege tisa, tukabaki na ndege mbili. Sasa ndio tumeanza programu ya umiliki, tumeanza na mwanzo mzuri," alisema
Source: Majira 21/12/07

Jamaa ndio hawajui lini watarudi, sasa nasubiri kuona which is which!
 
Alisema wanachosubiri ni mahujaji hao kupanga siku ya kurejea nchini na kuongeza kuwa siku tatu zilizopita, walituma ujumbe wa watu watatu kwenda Saudi Arabia kushughulikia suala hilo.
"Kule Saudi Arabia tuna Balozi wetu, tumepeleka watu watatu na wamekutana na Balozi. Tutawapelekea ndege. Kazi yetu ni kuhakikisha mahujaji wanarudi nchini," alisema Chambo.

Jamani kuna haja kweli kutuma ujumbe Saudia kushughulikia swala hili? Ubalozi, simu, mtandao n.k. vinafanya nini? Sitoshangaa nikisikia kuwa gharama ya kushughulikia suala hili ikifikia ya kununua ndege mpya!
 
Fundi Mchundo,
Unataka wakale wapi? Hapo tayari wizara nayo imepata dili la nguvu sana. Kufa kufaana ndugu yangu! Hapo ndiyo ujue jinsi hela ya walipa kodi inavyoliwa kwa makosa ya kifisadi. Yaani fisadi kasababisha ufisadi mkubwa zaidi!
 
Mahujaji wako salama na watarudi tarehe 31.12.07 Inshallah.Nimeongea na baadhi yao jana na wako salama na hawana wasiwasi.Mmojawao ni mama yangu mzazi naamini mambo yatakuwa salama.
 
Danadana za mahujaji zahamia Makka

na Nasra Abdallah na Ratifa Baranyikwa
Tanzania Daima

MAHUJAJI waliokwenda kwenye ibada ya Hija, jana walikwama kuondoka katika mji wa Makka, kutokana na kukosa vielelezo kuhusu ratiba ya safari yao ya kurejea nchini kwenye kompyuta, Tanzania Daima imeelezwa.
Mahujaji wote walitakiwa kuondoa Makka jana na kuelekea Madina au Jeddah kwa ajili ya safari za kurudi, lakini wanaweza kuondoka katika mji huo mtakatifu baada ya uthibitisho wa ratiba za safari zao.

Mmoja wa viongiozi wa Taasisi ya Kiislamu aliliambia gazeti hili jana kwa njia ya simu kuwa mahujaji wa Tanzania walishindwa kuondoka Makka kwa sababu hakukuwa na taarifa zozote kuonyesha ratiba ya kurudi.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, mahujaji hao, ambao wangetakiwa kuondoka juzi kutoka Makka kuelekea Madina au Jeddha, ambako ndiko mahujaji wa nchi zote hupandia ndege kurejea makwao, wameshindwa kwenda kwenye miji hiyo kwa sababu ya kutokuwa na vielelezo vyovyote kwenye kompyuta vinavyoonyesha kwamba wamefanya taratibu za usafiri (booking).

Chanzo hicho kilieleza kuwa taratibu hizo ndizo zingewawezesha mahujaji hao kufika nchini Desemba 29 au 30.

"Unajua kule Makka utaratibu wa kusafiri kwa mahujaji ni lazima kwenda kupandia ndege Madina au Jeddah na ili uweze kwenda huko mnatakiwa muwe mmeshakamilisha taratibu za usafiri, ikiwemo kujulikana ni ndege gani mnapanda, ambapo kazi hiyo huakikishwa na Mamlaka ya Usafiri ya Makka.

"Lakini mpaka jana mahujaji wetu walipofika katika ofisi za Mamlaka hiyo na kutafuta kwenye kompyuta kuangalia ni ndege gani wanayosafiria na ni siku gani, hakukuwa na taarifa zozote zilizoonyesha hilo," alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo, ofisa wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), aliiambia Tanzania Daima kuwa jukumu la kuwasafirisha mahujaji hao kwa safari ya kurudi nchini si la shirika hilo, bali ni la serikali na kwamba wao hawaelewi chochote kuhusu safari hiyo.

Kwa upande wake, serikali imesema kuwa ina mpango wa kuwarudisha mahujaji hao pindi watakapomaliza ibada ya Hijja.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Omari Chambo, ambaye yupo kwenye kamati ya kufuatilia suala hilo, alisema kuwa ndege ya kuwarudisha ipo.

Hata hivyo, alipotakiwa kutaja shirika la ndege ambalo litabeba jukumu la kuwarudisha mahujaji hao, Chambo alisema: "We vipi bwana, ndege ziko nyingi sana hewani, tutawarudisha, wao wakimaliza sisi tuko tayari."
 
Jamani kuna haja kweli kutuma ujumbe Saudia kushughulikia swala hili? Ubalozi, simu, mtandao n.k. vinafanya nini? Sitoshangaa nikisikia kuwa gharama ya kushughulikia suala hili ikifikia ya kununua ndege mpya!

FM, sasa mafisadi wakale wapi kama hawataongeza gharama hizo mara mia zaidi? Kamwe gharama za sakata hili hazitatangazwa hadharani lakini kwenye vitabu vya siri kali itaonekana walitumia shilingi milioni 800 kama siyo zaidi. Wanapopata upenyo tu wa kujitajirisha basi huwa hawalazi damu. Hapa JF tutaliuliza swali hilo, je sakata la mahujaji limeigharimu siri kali kiasi gani? I hope we'll be able to get a straight answer.
 
Mahujaji, ATCL: Nyang’anyi atoswa

Mwandishi Wetu Desemba 26, 2007
Raia Mwema

BODI ya Shirika la Ndege nchini (ATCL), imependekeza Mwenyekiti wake, Balozi Mustafa Nyang’anyi, awajibike kwa kuboronga safari ya Mahujaji ya mwaka huu.

Pamoja na kutaka Balozi Nyang’anyi awajibishwe, Bodi hiyo, iliyokaa chini ya Balozi Ami Mpungwe mwishoni mwa wiki iliyopita, imependekeza pia Mtendaji Mkuu wa ATCL, David Mattaka, apewe karipio kwa kuachia Mwenyekiti kuingilia shughuli za Menejimenti na kutoifahamisha Bodi kuhusu suala hilo la safari za Saudia.

“Kutokana na sakata hili la ATCL na Mahujaji, maneno mengi ya kejeli na kashfa dhidi ya Uongozi wa ATCL yamekuwa yakitolewa na baadhi ya Viongozi wa Mahujaji ambayo yanatia dosari kwa Shirika hii,” inasema sehemu ya taarifa ya Bodi hiyo katika waraka ambao Raia Mwema limefanikiwa kuuona na ambao umechapishwa katika ukurasa wa 3 wa toleo hili.

Unaongeza waraka huo: “Wajumbe pamoja na kukubaliana na Mwenyekiti kukubali kuwajibika kwa kushawishi Menejimenti kuidhinisha kuingia Mkataba wa ukodishaji wa ndege; Wajumbe waliona kuwa ilikuwa ni kosa kwa kuwaingiza watendaji katika mikataba mizito kama hii, bila Bodi kuhusishwa.

“Pamoja na nia nzuri ya Mwenyekiti kutaka kufanikisha safari hii, lakini wasiwasi wa kuwatumia mawakala wa ndege za kukodi bila kutumia taratibu zetu za nchi na Sheria za manunuzi, zinatia dosari utendaji wa Bodi katika kusimamia taratibu hizi.

“Ni kutokana na hilo Bodi inaona kuwa Mwenyekiti anastahili kuwajibika na kutoa maelezo hayo kwa chombo cha uteuzi wake ili kuisafisha Bodi na Wajumbe wake ambao hawakuhusika kabisa katika sakata zima la ukiukaji wa taratibu zote za maandalizi ya safari za Hijja”.

Kuhusu ushiriki wa Mattaka katika sakata hiyo, Bodi imesema: “Pamoja na maelezo ya kina yaliyojitokeza kama ilivyoainishwa kwenye taarifa yake, kama Mtendaji Mkuu wa Shirika na Mshauri Mkuu wa Bodi, angeweza kukataa ushauri wa Mwenyekiti na kuleta suala hili kwenye Bodi kwa maamuzi.

“Inaonekana hakufanya hilo na badala yake alikubaliana waendelee na utekelezaji wa ushauri huo kinyume cha sheria, kanuni na maelekezo ya Bodi.

“Tatizo hili lilichukua sura mbaya baada ya ATCL kuendelea kuvurugwa na ratiba za ndege za kukodi hata bila Bodi kuwa na taarifa. Maji yalikuwa yamefika shingoni, hakukuwa na nafasi ya kukwepa mzigo huu.

“Mkurugenzi Mtendaji kwa hili, pamoja na barua ya awali ya kutaka kupinga ATCL isijihusishe katika ukodishaji wa ndege za Mahujaji, hawezi kukataa kuwajibika kwa kuwa alikuwa na kila sababu ya kuwajulisha Wajumbe wa Bodi kuhusu mapatano hayo ambayo kiutaratibu yalitakiwa yapate kibali cha Bodi.

“Pamoja na uwezo wake mzuri wa kikazi lakini kwa hili anastahili kukiri kosa kwa tabia kama hii ”.

Baada ya kukwama kwa siku 12 uwanjani, hatimaye Mahujaji hao waliweza kusafirishwa, lakini baada ya Serikali kuingilia kati.

Tayari kipindi cha kuhiji huko Makka na Madina kimekwisha na sasa Mahujaji hao wanatarajiwa kurejea nchini wakati wowote.
 
waache wamtose huwezi kula hela za waumini wanoomba mungu kila siku na kufikiri mungu atakuacha,,leo nimeshangazwa na hii habari kwenye raia mwema,,BADO TUNAULIZA MASWALI YAFUATAYO

1)MAHUJAJI WAMEDAI WAMETOA DOLA 2400 KWENDA NA KURUDI JAMANI,,HUYU MWENYEKITI ANADAI ATCL IMEPEWA DOLA 870,,WAKAONGEZEA DOLA500 KUSRIFISHA MAHUJAJI,NANI MKWELI,,NA HII HELA ILIOZIDI IMEKWENDA WAPI MUSTAFA

2)KAMA NDEGE WALIOKODI KUPELMAHUJAJI WAMELIPA DOLA 1400 HII YA ZIADA NANI AMETOA NA KAMA WAMETOA ATC NANI ATAILIPA KWANINI WANANCHI WAUMIE MAANA HII PESA WANATOA SERIKALI KULIPA ATCL KILA MWEZI IENDELEE KUWEPO MUNGU TUONYESHE UKWELI WAJA WAKO
 
Hapo naona kuna mawili"
1. Kulikuwa na ubishi kati ya mkurugenzi na mwenyekiti wa bodi, labda mwenyekiti kaleta siasa na mkurugenzi kaleta utaalamu vikagongana, na hivyo mwenyekiti akaamua kulichukua mikononi mwake, kuagiza kukodi ndege nk.
2. Mkurugenzi akafanya "nidhamu ya woga" na kuanza kutekeleza maagizo yasiyotekelezeka ya mwenyekiti, ili hata mwishoni akikwama aseme "si unaona? Nilisema mimi!" (Ndio maana aliandika barua awali kupinga ATCL kujihusisha na hizo safari za mahujaji, alijua uwezo wa shirika lake ni duni)

Lakini hili halimpi kinga ya kutowajibika. Alipaswa "kuazima ukurasa" kutoka kwa mwenzie wa TANESCO ambaye "alimkomalia" mwenyekiti wake hadi mwisho. Kwa kushindwa kusimamia taratibu za shirika lake, naye pia ni guilty by association, na anapaswa kuadhibiwa.
 
nimeona gazeti la raia mwema wameitoa kwenye toleo lao la 26/12/2007. its worth reading japo ni ndefu kidogo hiyo ripoti, naona mkurugenzi na mwenyekiti wake wako kwenye kikaango

hapo ilitakiwa wawe wameshajiuzulu au kwa vile hatuna utamaduni huo?
http://www.raiamwema.co.tz/07/12/26/5.php


Bodi ya ATCL yamkandamiza Balozi Nyang’anyi

Mwandishi Wetu Desemba 26, 2007



Kwa siku 12 Mahujaji wa Tanzania na baadhi ya wengine kutoka nchi jirani, walikwama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, baada ya taratibu za kuwasafirisha hadi Saudia kukwama. Hatimaye, walisafiri lakini baada ya Serikali kuingilia kati. Sasa jitihada zinafanyika waweze kurejea bila matatizo makubwa. Baada ya sakata hiyo, Serikali iliagiza ipewe taarifa ya hali ya mambo. Raia Mwema imefanikiwa kupata nakala ya taarifa hiyo ya Bodi ya ATCL na inaichapisha kwa faida ya wasomaji.

1.0 UTANGULIZI

Kuanzia Desemba 10 , 2007 hadi Desemba 14, 2007 Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) lilikuwa katika msukosuko mkubwa. Hiyo ilitokana na matatizo ya kukwama kwa Mahujaji kwenda Hijja Saudi Arabia. Tatizo hilo lilianza kama tukio la kawaida la kiutendaji, lakini taratibu lilianza kuchukua sura mpya kiasi cha kuihusisha Serikali wakiwamo viongozi wa juu kabisa wa nchi.

Tatizo hilo kwa kiasi kikubwa limeleta usumbufu usio kifani kwa Mahujaji ikiwamo aibu na fedheha kwa shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Taifa kwa ujumla, Serikali na viongozi wake wakuu.

Kutokana na hayo, Mheshimiwa Andrew Chenge (Mb), Waziri wa Miundombinu, aliiagiza Bodi kwa kupitia barua yake Kumb. Na. MC 62/2270/01 ya Desemba 17, 2007, kwamba iundwe kamati ya Bodi ya ATCL kufanya uchunguzi juu ya suala la kukwama kwa Mahujaji, na kutoa taarifa yake siku ya Ijumaa, 21 Desemba, 2007.

1.1 UAANDAAJI WA TAARIFA

Kamati ya Bodi katika maandalizi ya taarifa yake ilizingatia yafuatayo:-

Maelezo ya mdomo ya wahusika wakuu wakiwamo wafuatao:-
- Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL
- Mkurugenzi Mkuu, ATCL na
- Manager Flight Operations

maelezo yaliyotolewa katika kikao cha dharura cha 14 cha Bodi ya Wakurugenzi cha Desemba 17, 2007

Maelezo ya maandishi ya wahusika muhimu katika suala hili yaliwahusu wafuatao:-
Mwenyekiti wa Bodi – ATCL (Balozi M. Nyang’anyi)
Mkurugenzi Mtendaji - ATCL (D. Mattaka)
Manager, Flight Operations – (M. Manji)
Kaimu Mkurugenzi wa Operations (Capt. S. Muze)
Afisa Masoko - (J. Kagirwa)
Katibu Muhtasi – (M. El-Hady)
Mwanasheria wa Kampuni – (A. Mziray)
Maoni ya Wajumbe wa Bodi ya ATCL
2.0 MAELEZO YA AWALI (BACK GROUND)

Kufuatana na maelezo ya Menejimenti ya ATCL, mnamo mwezi Julai, 2007, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, aliwaomba viongozi mbalimbali wa Jumuiya za Kiislamu zinazoshughulika na safari za Mahujaji kulipatia shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) biashara ya kusafirisha Mahujaji kwenda Makka na Madina, Saudi Arabia (Lakini Mwenyekiti anasema ni viongozi wa Mahujaji ndio waliomfuata na kumuomba).

Mnamo Julai 19, 2007 Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL alimwita ofisini kwake Mkurugenzi wa Uendeshaji, Capt. Sadiki Muze, na kumtambulisha kwa viongozi mbalimbali wa Taasisi za Kiislamu, na kumueleza kwamba mwaka huu ATCL itaandaa safari za Mahujaji. Mkurugenzi huyo alitoa taarifa hiyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa ATCL kuhusu maongezi yake na Mwenyekiti wa Bodi. Baada ya majadiliano marefu na wataalamu wahusika kwenye Shirika ilionekana kuwa shirika halina uwezo (ndege) wa kuandaa safari hizo.

2.1 HATUA ZILIZOFUATIA

Mkurugenzi Mkuu aliandika barua kwa Mwenyekiti wa HAJJ Trust, ya Julai 26, 2007, ikimuelezea kuwa ATCL haina uwezo wa kuandaa safari za Hijja. Hata hivyo barua hiyo haikupelekwa kwa walengwa, kwani wakati Katibu Muhtasi anatafuta ofisi za Hajj Trust ili barua iwasilishwe huko, Mwenyekiti wa Bodi aliagiza kuwa barua hiyo isipelekwe mpaka afanye mawasiliano na Menejimenti. Katibu Muhtasi aliwajulisha Mkurugenzi Mtendaji na Mkurugenzi wa Uendeshaji (Capt. Muze) kuwa barua haikupelekwa kutokana na maagizo ya Mwenyekiti wa Bodi.

Mwenyekiti wa Bodi aliwasiliana na Mkurugenzi wa Uendeshaji na kumhakikishia kwamba ATCL ingeliweza kufanya safari hizo, kwani ndege zingeweza kupatikana, hususan kutoka katika kampuni ya RAK Leasing ya Dubai. Pia Mwenyekiti alimpatia Mkurugenzi wa Uendeshaji jina na namba ya simu za mhusika ili awasiliane naye kuhusu upatikanaji wa ndege.

Captain Muze aliwasiliana na kampuni ya RAK Leasing ambao walimwambia kuwa wanayo ndege aina ya Boeing 747-200 yenye uwezo wa kubeba abiria 489, ambayo kwa wakati huo ilikuwa katika matengenezo ya Check “C” na kwamba ingekuwa tayari mwezi wa Septemba, 2007. Capt. Muze aliwaomba wamletee “Documents” za ndege hiyo ili aweze kufanya maandalizi ya kupata vibali muhimu, zikiwemo “slots”. Pia aliwasiliana na kampuni ya Al-Wassam ambao ni “Ground Handling Agent” wa Makka na Madina (ambao hapo zamani walikuwa wana “handle flights” za Hijja za Air Tanzania Corporation) ili wafanye matayarisho muhimu, ikiwamo utafutaji wa “slots”.

Hata hivyo, “documents” za ndege zilichelewa kufika na ilibainika kuwa zilikuwa zinaisha muda wake Novemba 30, 2007, na hivyo zisingefaa kutumika kuombea vibali pamoja na “slots”. Kampuni ya RAK Leasing iliahidi kuwa ingepata “documents” zingine na kuahidi kuitafutia ATCL kampuni nyingine za “ku-handle” ATCL. Pamoja na ahadi hizo kampuni hiyo haikufanya hivyo.

Wakati huo huo Capt. Muze alisafiri kikazi kwa muda mrefu na kumuachia shughuli hii Afisa Masoko, Josephat Kagirwa.

Kadiri muda ulivyopita, na safari za Mahujaji kukaribia ilidhihirika kuwa ndege isingepatikana kutoka kampuni ya RAK Leasing. Hii ilithibitika baada ya wafanyakazi wa ATCL, akiwamo mwanasheria wa ATCL Mziray kwenda Dubai, na kurudi mikono mitupu bila mikataba na au “documents” za ndege ya RAK Leasing na hiyo ilikuwa mwishoni mwa mwezi Novemba, 2007, zikiwa zimebakia siku chache mno kabla ya safari za Mahujaji kuanza.

Baada ya hapo Mwenyekiti wa Bodi na Capt. Muze walianza kufanya mipango mipya ya kutafuta ndege nyingine. Walifanikiwa kupata ndege kupitia msaada wa Al-Wassam, wa Jeddah. Ndege hiyo ni aina ya DC 10 inayomilikiwa na Global Aviation ya Afrika Kusini. Hata hivyo, ndege hiyo ilipatikana kupitia kwa wakala mwingine ambaye ni SAMEK Aviation Services wa Jeddah, (Ground Handling Agent).

Katika mikataba ATCL iliyoingia na SAMEK AVIATION ilijumuisha pia kuipatia ATCL “slots” za ndege hiyo. Mkataba huo ilibidi usainiwe Saudi Arabia na Balozi Hamis Msumi kwa niaba ya ATCL, kutokana na ucheleweshaji wa maandalizi na ufupi wa muda. Wakati haya yanakamilika ilikuwa 6/12/07 na tayari Mahujaji kutoka sehemu mbali mbali walikwisha kuwasili ikizingatiwa kuwa ratiba ya awali ya Mahujaji ingelikuwa 4/12/07.

SAMEK Aviation Services, waliahidi kuwa safari za Hijja zingeanza 8/12/07, na ahadi hii ilithibitishwa kwa Balozi wetu nchini Saudi Arabia, kwamba ndege husika ilikuwa inakuja. Kwa bahati mbaya haikufika kama ilivyoahidiwa, pamoja na ATCL kutimiza masharti yote, ikiwamo kulipa malipo ya awali ya Dola za Kimarekani 550,000.

Kufuatia kutowasili ndege hiyo kama ilivyokuwa imetarajiwa, na Mahujaji kuzidi kusongamana uwanja wa ndege wakati wanasubiri ndege ambayo haikuwa na uhakika, ndipo hali ya wasiwasi na mtafaruku kwa Mahujaji ilitanda na kuanza kuongelewa na vyombo mbalimbali vya habari, hadi Serikali kufahamu kuwa kulikuwa na tatizo.

Kuanzia 9/12/07 Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mtendaji, ilibidi wahamie uwanja wa ndege ili kuwafariji Mahujaji na kutafuta ufumbuzi kadri hali ilivyokuwa ikijitokeza. Hata hivyo, ndege haikufika kati ya tarehe 9 na 10/12/07 kama ilivyo ahidiwa na SAMEK Aviation Services kwa visingizio mbalimbali. Baadaye iligundulika kuwa sababu za ucheleweshaji wa ndege hii ni kwamba:-

Ndege hiyo ilikuwa inaendelea kufanya kazi nyingine za kusafirisha Mahujaji kutoka Baghdad kwenda Saudi Arabia.
Mawakala waliokodisha ndege hiyo walishindwa kupata “Slots”.
Hatimaye ndege hiyo ilifika nchini 11/12/2007 bila kuwa na “slots” kama ilivyotarajiwa.

3.0 UUZAJI WA TIKETI KWA MAHUJAJI

Mnamo 20/08/07 Capt. Muze kwa niaba ya Menejimenti aliwasiliana na Taasisi ya Waislam, Tanzania, akiwafahamisha upatikanani wa ndege aina ya Boeing 747-200 na nauli ya kiasi cha dola za Marekani 950 ambayo kila abiria angetakiwa kulipa.

Baada ya majadiliano baina ya ATCL na viongozi wa Taasisi ya Waislam Tanzania, mambo yafuatayo yaliendelea kufanyika:-

Alichaguliwa Afisa Masoko ili ku-“coordinate” uuzaji wa tiketi kwa Mahujaji
Viongozi wa Mahujaji walimchagua Wakala FAST TRACK kuwa wakala wao wa usafiri, hivyo fedha zote kwa mauzo ya Dar es Salaam zilipitia FAST TRACK.
Afisa Masoko alipata kibali toka kwa Mkurugenzi wa Masoko, Ajay, kuingiza ratiba ya safari za Mahujaji kwenye mtandao (Reservation System).
Afisa Masoko alipata kibali kingine kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Eliasaph, cha kuuza tiketi kwa Mahujaji.
Nauli halisi iliyopokelewa na ATCL ilikuwa ni Dola za kimarekani 870 kwa kila Hujaji na pesa taslimu kwa Mahujaji wote ni Dola za Kimarekani 1,248,013 kiasi ambacho ni baada ya makato yote (commission).
Kuweka ratiba ya Hajj Charters kwenye mtandao (Reservation System) ni kuwezesha safari hizi kuuzwa mahali popote ndani na nje ya nchi, hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Comoro, Malawi na kadhalika.
3.1 MAPUNGUFU YA NAULI

Baada ya kukosekana kwa ndege toka kampuni ya RAK Leasing, ndege ya DC10 ambayo ilisafirisha Mahujaji imegharimu dola za kimarekani, 1,450 kwa kila Hujaji, wakati nauli iliyotozwa na ATCL ilikuwa ni dola za Kimarekani 870 kwa kila Hujaji. Kwa sababu hiyo, ulitokea upungufu wa dola za Kimarekani 580 kwa kila Hujaji. Baada ya majadiliano kati ya Mwenyekiti wa Bodi na Viongozi wa Mahujaji walikubaliana kwamba Mahujaji walipie dola za Marekani 230 kila mmoja na zilizobaki zitafidiwa na ATCL. Hata hivyo, Mahujaji waliahidi kwamba fedha hizo watazilipa watakaporudi kutoka kwenye Hijja.
Imedhihirika kwamba upo utata katika mkataba kati ya SAMEK AVIATION SERVICES na ATCL kuhusu gharama za nauli. Upande wa ATCL imeeleweka kuwa gharama za nauli ni za kwenda na kurudi, japo katika mkataba suala hilo halijawekwa wazi. ATCL kwa ushirikiano na ubalozi wetu nchini Saudi Arabia wanawasiliana ili kuhakikisha swala hili linaeleweka vizuri kabla ya safari za kurudi kuanza.
4.0 SERIKALI KUINGILIA KATI

Baada ya ndege kuwasili 11/12/07, Manager Flight Operations, Mark Manji aliwasiliana na mwakilishi wa SAMEK AVIATION SERVICES kuhusu suala la “Slots” na alihakikishiwa kuwa “slots” zipo. Wakati wanatayarisha utaratibu wa ndege kuondoka Mark Manji vile vile aliwasiliana na kapteni wa ndege ambaye alimjulisha kuwa kila kitu kilikuwa tayari.

Mark Manji aliwajulisha viongozi wenzake wa ATCL kuwa ndege ilikuwa tayari na abiria waruhusiwe kupanda kwa ajili ya safari. Kabla ya hapo muwakilishi wa SAMEK AVIATION SERVICES, alidai na kukabidhiwa fedha kiasi cha dola za Marekani 160,000 kama malipo ya ziada ya safari ya kwanza.

Abiria walipopanda kwenye ndege uongozi wa ATCL uligundua kwamba ndege hiyo haikuwa na kibali “slots” cha kutua Saudi Arabia. Suala hili lilipojitokeza ungozi wa ATCL haukuwa na namna nyingine yeyote ila kuwashusha abiria waliokuwa wamepanda kwenye ndege. Itakumbukwa kwamba tukio hili lilitokea baada ya Rais na Waziri Mkuu pamoja na viongozi wengine wa Serikali kuwaaga Mahujaji ambao tayari walikwisha hakikishiwa kuwa safari ingekuwapo.

Kadri muda ulivyopita ilidhihirika kuwa SAMEK AVIATION SERVICES walikuwa na mikakati ya ubabaishaji kuhusu upatikanaji wa “slots” na hivyo Serikali iliamua kuingilia kati suala hili. Hatimaye “slots” zilipatikana na ndege ya kwanza iliondoka na kundi la kwanza la Mahujai 11/12/2007.

Bahati mbaya kundi la pili halikuweza kuondoka kwa muda uliopangwa kutokana na ndege kuharibika ilipotokea Madina. Hata hivyo, kundi hilo liliondoka 12/12/2007 saa 11.30 jioni badala ya saa 1.30 asubuhi. Kundi la tatu lilisafiri 14/12/2007 mnamo saa 3.30 asubuhi.

5.0 USHIRIKI WA BODI

Bodi ya Wakurugenzi ya ATCL ilipanga kuwa na kikao chake cha 16 cha kawaida kuanzia 9/12/07 huko Bagamoyo. Tarehe 10/12/07 asubuhi baadhi ya wajumbe walipokutana iligundulika kwamba Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji hawakuwapo. Wajumbe walifahamishwa kwamba kulikuwa na tatizo kubwa lililohusu kukwama kwa Mahujaji uwanja wa ndege, hivyo Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Menejimenti walikuwa uwanja wa ndege wa Mwl. Nyerere wakishughulikia suala hilo. Wajumbe walifanya kikao cha dharura chini ya uenyekiti wa Balozi (Ami) Mpungwe na kuamua yafuatayo:-

Kuahirishwa kikao cha kawaida cha 16 kutokana na dharura hiyo na hivyo kurudi Dar es Salaam.
Kuagiza Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mtendaji waitishe kikao cha dharura, siku iliyofuata yaani 11/12/2007 ili Bodi ipewe maelezo juu ya suala hilo, ambalo wajumbe wa Bodi walikuwa hawana taarifa yeyote; na
Wajumbe walikubaliana kwa kuwa suala hili walikuwa hawalijui, wasiliongelee popote, hasa kwenye vyombo vya habari.
Kikao hicho cha dharura hakikuweza kuitishwa kutokana na hali halisi ilivyokuwa, hadi ilipofika 17/12/2007.

6.0 ATHARI ZA KIUTENDAJI KWA ATCL

Kutokana na sakata hili la ATCL na Mahujaji, maneno mengi ya kejeli na kashfa dhidi ya Uongozi wa ATCL yamekuwa yakitolewa na baadhi ya Viongozi wa Mahujaji ambayo yanatia dosari kwa Shirika hili.
Kuanzia 10/12/2007 vyombo vya habari vimekuwa vikitoa maoni na maneno yasemwayo na Mahujaji. Mifano michache ni pamoja na:-
- Katibu wa kundi la Mahujaji la AL-BIZ Abdallah Mohamed alikaririwa akisema “Safari hii imeandaliwa na kundi la kisanii – kisanii …. Tutadai haki na fidia kwa ATC”

- Kiongozi wa Taasisi ya MUSLIM Hajj Trust Juma Nchia alisema “watu waliotenda kosa kubwa wanapaswa kukatwa kichwa kwa mujibu wa Dini yao ……….. tutajadili hukumu yake baada ya safari hii kushidikana kabisa”.

- Katibu wa Taasisi ya Alh-Bir Abdallah Harith Mohamed alisema kuwa “waliingia mkataba na ATC baada ya Nyang’anyi ambaye ni Muislamu mwenzetu na mtu aliyewahi kuwa Balozi wa Saudia Arabia, ambaye aliwaomba Waislam wasafiri na ndege yao….”

Aliendelea kusema “sisi tulikuwa tumeachana na Shirika hili kwa miaka 10 … Taasisi zote ziliambiwa kuwa ATC ina ndege ya kukodi Boeing 747-200 yenye uwezo wa kubeba abiria 480”.
Akalalamika kuwa ATC imewatia hasara kubwa na lazima walipe gharama zote hizi pamoja na fidia ya usumbufu.

- Uzembe huu wa ATC ulitaka kuwasha moto wa hasira ya maandamano kwenye RUN WAY ya ndege ili kuzuia ndege zozote zisiondoke wala kutua uwanjani hapo.

Yote haya yanaashiria kuwa bado Mahujaji kupitia viongozi wao wanatarajia kufanya mamabo yafuatayo:-
Kudai fidia na gharama ya usumbufu.
` (ii) Kuishitaki ATCL kwa kukiuka mkataba.

Kuitaka Serikali kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na kuvuruga safari yao ya Hijja.
Serikali kuwaomba radhi Hadharani kwa usumbufu wowote ule uliotokea.
Kuitaka ATCL kupitia Serikali kuwahakikishia kuwa kosa hili halitarudiwa tena wakati wa kuwarejesha nyumbani Mahujaji.
7.0 HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA BODI

Katika kikao cha dharura kilichofanyika 10/12/2007 huko Bagamoyo na baadaye kuhitimishwa kwa pamoja 17/12/2007 katika Ofisi za ATCL Dar es Salaam, Wajumbe wa Bodi walimtaka Mwenyekiti na Menejimenti ya ATC itoe maelezo ya kina kuhusiana na sakata lote hili kuanzia mwanzo lilipojitokeza hadi tarehe ya kikao hicho. Pia Bodi ilitakiwa kutoa majibu ya masuala yaliyojitokeza kama barua ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu ilivyokuwa imeelekeza Menejimenti na Bodi kufuatilia kwa undani nini kiliathiri mpango mzima wa safari za Hijja.

7.1 MAELEZO YA MWENYEKITI WA BODI

Bodi ilipata maelezo ya kina toka kwa Mwenyekiti wa Bodi Balozi Mustafa Nyang’anyi na baadaye akayaweka kwenye maandishi.

7.2 MAONI YA BODI

Wajumbe pamoja na kukubaliana na Mwenyekiti kukubali kuwajibika kwa kushawishi Menejimenti kuidhinisha kuingia Mkataba wa ukodishaji wa ndege; Wajumbe waliona kuwa ilikuwa ni kosa kwa kuwaingiza watendaji katika mikataba mizito kama hii, bila Bodi kuhusishwa.

Pamoja na nia nzuri ya Mwenyekiti kutaka kufanikisha safari hii, lakini wasiwasi wa kuwatumia mawakala wa ndege za kukodi bila kutumia taratibu zetu za nchi na Sheria za manunuzi n.k. zinatia dosari utendaji wa Bodi katika kusimamia taratibu hizi.

Ni kutokana na hilo Bodi inaona kuwa Mwenyekiti anastahili kuwajibika na kutoa maelezo hayo kwa chombo cha uteuzi wake ili kusisafisha Bodi na Wajumbe wake ambao hawakuhusika kabisa katika sakata zima la ukiukaji wa taratibu zote za maandalizi ya safari za Hijja.

7.3 MAELEZO YA MKURUGENZI MTENDAJI

Pamoja na maelezo ya kina yaliyojitokeza kama ilivyoainishwa kwenye taarifa yake, kama Mtendaji Mkuu wa Shirika na Mshauri Mkuu wa Bodi, angeweza kukataa ushauri wa Mwenyekiti na kuleta suala hili kwenye Bodi kwa maamuzi. Inaonekana hakufanya hilo na badala yake alikubaliana waendelee na utekelezaji wa ushauri huo kinyume cha sheria, kanuni na maelekezo ya Bodi.

Tatizo hili lilichukua sura mbaya baada ya ATCL kuendelea kuvurugwa na ratiba za ndege hizo za kukodi hata bila Bodi kuwa na taarifa.. Maji yalikuwa yamefika shingoni, hakukuwa na nafasi ya kukwepa mzigo huu.
Mkurugenzi Mtendaji kwa hili, pamoja na barua ya awali ya kutaka kupinga ATCL isijihusishe katika ukodishaji wa ndege za Mahujaji, hawezi kukataa kuwajibika kwa kuwa alikuwa na kila sababu ya kuwajulisha Wajumbe wa Bodi kuhusu mapatano hayo ambayo kiutaratibu yalitakiwa yapate kibali cha Bodi.
Pamoja na uwezo wake mzuri wa kikazi lakini kwa hili anastahili kukiri kosa kwa tabia kama hii.

8.0 MAJUKUMU YA BODI

Kwa mujibu wa majukumu ya Bodi kama yalivyoainishwa kwenye Waraka wenye Kumb. Na. SHC/B.40/6/21 imedhihirika kuwa Menejimenti imesahau na pengine haikufuatilia maelekezo kwenye waraka huo ambao ulifafanua yafuatayo:-

Majukumu ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
Majukumu ya Wakurugenzi wa Bodi
Majukumu ya Watendaji Wakuu


Imedhihirika kuwa, wajumbe wamesahau na pengine hawakuyafuatilia maelekezo yaliyomo katika waraka huo. Matukio ya hivi karibuni ya SAKATA la ATCL na Mahujaji, yamedhihirisha udhaifu huo kwa kutozingatia maelekezo na utendaji wa kazi za kila siku.

Bado hatujachelewa, hili ni fundisho kubwa kwa Shirika letu la ATCL katika kusimamia maelekezo yale yote yaliyomo kwenye waraka huo.

9.0 MAJUMUISHO

Katika sakata hili, Bodi imebaini kuwa:-

Utaratibu mzima wa kushughulikia suala hili ulikosewa baada ya Mwenyekiti kuanza kujiingiza kwenye utendaji.
Mkurugenzi Mtendaji hakuwajibika ipasavyo baada ya kuandika barua ya kutoridhia maombi ya Mahujaji na kushindwa kuhakikisha kwamba maamuzi yake ya awali ya kukataa yanatekelezwa.
Uongozi wa ATCL haukuwajibika ipasavyo kwa kuliacha suala hili liwe “one man show” badala ya kushughulikiwa na kamati maalum ya Hijja, yaani “Hijja Committee” ambayo ingehusisha idara ya Masoko, Uendeshaji, (Operations) Fedha na Mwanasheria wa Shirika. Kamati hii ingesaidia sana kugundua mapema kasoro za upatikanaji wa ndege “slots” na vibali vingine na kutafuta mipango mbadala ya kuokoa hali hiyo.
Makabidhiano yaliyofanyika kati ya Mkurugenzi wa Uendeshaji na Afisa Masoko hayakuzingatia taratibu za kiutawala. Kazi hii muhimu ilipaswa ikabidhiwe kwa Mkurugenzi Masoko, ambaye angeweza yeye kwa wadhifa wake kutumia maafisa wengine waliochini yao.
Mwenyekiti wa Bodi alikosea kukutana na Mahujaji na kuwaahidi kuwa ATCL itabeba mzigo wa kutoa ruzuku bila kibali cha Bodi ya Wakurugenzi. Jambo hili lina athari ya kifedha na Bodi ndiyo yenye maamuzi ya mwisho juu ya masuala ya fedha na haswa ambayo hayamo kwenye Bajeti ya Shirika.
10.0 MAPENDEKEZO

Bodi inasisitiza kuwa mamlaka yake ya kiutendaji yasiingilie kamwe shughuli za uendeshaji wa Shirika kama ilivyoainishwa katika Waraka wenye Kumb. Na. SHC/B.40/6/21 wa tarehe 28/3/1994.
Vile vile na Menejimenti isijichukulie mamlaka ya kufanya maamuzi kwa niaba ya Bodi.

Kwa vile kuna uwezekano mkubwa wa Shirika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria (kushitakiwa) na Mahujaji ni vyema ifanywe mikakati ya kukutana na uongozi wa Mahujaji walioko nchini ili kutafuta muafaka mapema kabla Mahujaji hawajarudi nchini.
Shirika lisijihusishe tena na usafirishaji wa Mahujaji hadi hapo litakapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo baada ya kupata idhini ya Bodi ya ATCL na Serikali.
Kutokana na uzito wa suala lenyewe lilivyojitokeza kwa umma wa Tanzania na ulimwengu kwa ujumla Bodi inapendekeza kuwa Mwenyekiti alitolee maelezo bayana kwa umma kwa jinsi alivyohusika.
Kutokana na kutosimamia kikamilifu suala hili Bodi inapendekeza kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL apewe karipio ili iwe fundisho kwake.
Bodi itachukua hatua itakazoona zinafaa kwa kuwawajibisha waliohusika katika Menejimenti.
11.0 MWISHO

Bodi ya ATCL inaishukuru Serikali ambayo ndiye mwenye hisa zote za Shirika hili kwa jinsi walivyoingilia kati.

Shukurani ziende kwa Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Edward Lowassa, Waziri wa Miundombinu Andrew Chenge, Katibu Mkuu wa Kamati rasmi ya Komandi ya kuokoa ATCL, Dr. Enos Bukuku kwa kazi nzuri sana waliyoifanya kupunguza aibu ambayo ingetupata.

Tunawapongeza na kuwashukuru Viongozi wa dini ya Kiislamu na Mahujaji wote kwa utulivu na uelewa waliouonyesha wakati wote huu wa usumbufu wa safari yao ya Hijja. Tunaiomba Serikali kwa wakati huu ambao Bodi inajaribu kusawazisha athari hizi mbele ya watumishi na mbele ya Umma wote wa Tanzania, iendelee na Kamati yake (Command Post) hadi Mahujaji watakaporejea.

Ni ukweli usiopingika kuwa Bodi nzima imechafuliwa mbele ya uso wa Watanzania; ni kweli pia Mwenyekiti wa Bodi aliwatenga wajumbe wa Bodi kutowahusisha katika maamuzi makubwa kama haya. Ni kweli pia Mkurugenzi Mtendaji alishindwa kumkatalia Mwenyekiti wa Bodi juu ya ATCL kutokuwa na uwezo wa kuingia katika mikataba ya ukodishaji wa ndege kwa ajili ya Mahujaji.

Lakini ni kweli pia katika hali hii wajumbe wamesononeshwa na kitendo hiki cha Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji kwa kutokutoa taarifa yeyote hata sakata lilipoanza hadi lilipotolewa na vyombo vya habari. Ni matarajio yetu kuwa Serikali italifafanua suala hili vizuri ili UKUNGU uliotanda mbele ya uso wa ATCL uondolewe.
 
Kiungwana Nyang'anyi angeandika barua resignation- ormay be anasubiri hadi hawa mahujaji warudi ndo aandike!

Pia ATC imechemsha- na Mataka naye afunge virago- hii ni hasara kwa shirika na hatimaye sisi walipa kodi!

Haya ndo mambo ya kisanii tunayoyaongelea Tanzania kila siku!
 
Si afadhari tuliwe $400 kwa sababu mtu anakwenda kuhiji kuliko tukiliwa fedha, eti kimada wa mtu anapelekwa shopping London?
 
Kiongozi wa Taasisi ya MUSLIM Hajj Trust Juma Nchia alisema "watu waliotenda kosa kubwa wanapaswa kukatwa kichwa kwa mujibu wa Dini yao ……….. tutajadili hukumu yake baada ya safari hii kushidikana kabisa".

Hivi inaruhusiwa kutishia hivi? Hivi kweli hii ni hukumu ambayo imeainishwa na dini yeyote? Ni hukumu gani wanayoweza kuitoa nje ya mahakama?
 
Mwenyekiti wa Bodi huteuliwa na Rais, suppose JK akiamua kutoifanyia kazi repoti hii, Mh. Chenge aliyeagiza uchunguzi na apewe report, atafanya nini??? Hapa ndipo huwa ninasema kwamba madaraka ya Rais kwenye uteuzi ni makubwa sana kiasi kwamba hana mtu wa kum-question kwenye maamuzi yake!

Kitendo cha report hii kuwekwa kwenye gazeti ni move nyingine ya kumkaba koo JK iwapo ataamua kufumbia macho mapungufu ya Nyang'anyi kama mwenyekiti wa bodi. Nina uhakika wajumbe wa Bodi walijua kwamba report ikienda kimya kimya inawezekana JK akamezea na kuamua kumwacha Nyang'anyi abakie wakati tayari ameishaonekana ni mzigo kwa shirika.

Kauli ya JK ya kusema kilichotokea kwenye sakata la mahujaji ni swala dogo, ilikuwa ni dalili kwamba aidha hana mpango wa kumbebesha mzigo mtu ama haoni kama hiyo ni kubwa sana. Je, JK atakubali kumtosa Nyang'anyi?????
 
Back
Top Bottom