Kamati Kuu ya Chadema kujadili uamuzi wa Dk Slaa
Exuper Kachenje na Fidelis Butahe
KAMATI ya Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), inatarajiwa kukutana kati ya Novemba 27 na 28 mwaka huu, kujadili pamoja na mambo mengine, pepo baya la kisiasa lililoanza kukikumba chama hicho cha upinzani.
Pepo hilo, linafuatia uamuzi wa Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa, kuwafuta kazi maafisa wawili wa Chadema kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi.
Kufutwa kazi kwa maafisa hao David Kafulila aliyekuwa Ofisa habari wa chama hicho na Danda Juju, aliyekuwa akishughulikia mambo ya Bunge katika chama hicho, kulitangazwa juzi na Dk Slaa.
"Tena andika mwandishi wala usiogope ni kwamba leo, (juzi) kulikuwa na kikao, nimekiongoza mwenyewe na maamuzi nimeyatoa mwenyewe, tumetengua uteuzi wao. Sasa ni wanachama wa kawaida," alinukuliwa Dk Slaa katika mahojiano na gazeti hili juzi.
Hatua hiyo imeibua majeraha ya kisiasa yaliyotokana na uchaguzi wa viongozi ndani ya chama hicho, uliofanyika Septemba mwaka huu.
Tayari Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amepinga vikali hatua ya kufukuzwa kwa watendaji hao, wanaotajwa kuwa ni washirika wake wakubwa kisiasa, tangu mbio za uchaguzi uliomtikisa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Jana Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema, Bob Makani alisema, "suala hilo tutalijadili katika kikao cha Kamati Kuu ambayo itakutana kabla ya mwisho wa mwezi huu. Bahati mbaya sijawasiliana na uongozi siwezi kujua ni tarehe gani."
Hata hivyo alielezea matumaini yake kuwa haki itakuwa imetendeka kwa wanachama hao ambao walikuwa waajiriwa wa Chadema na kwamba ndiyo maana walipewa nafasi ya kujitetea.
Makani alifafanua kwamba, kimsingi, mwajiriwa anapaswa kufuata sheria na kanuni za mwajiri wake na kwamba, kama Kafulila na Juju hawakuzingatia hayo na kuendekeza majungu ndani ya chama na kuvunja katiba, hawawezi kuvumiliwa.
"Hao ni waajiriwa, katika ajira kuna maadili, sheria na kanuni, kama ni kweli wameleta majungu ndani ya chama hawawezi kuvumiliwa," alisema Makani.
Hata hivyo vyanzo huru vya habari, vilidokeza kuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika kati ya Novemba 27 na 28 mwaka huu.
Habari hizo zimekuja huku kukiwa na habari nyingine kuwa Mwenyekiti wa chama hicho (Mbowe), Dk Slaa na maafisa wao kadhaa walitarajiwa kukutana jana katika kikao cha siri, kujadili upepo ulivyo ndani ya Chadema.
Habari zaidi zilisema baadhi ya wanachama wa Chadema mikoani wakiwemo wenyeviti wao, wamekerwa na kitendo cha
Dk Slaa, kumlinganisha Kafulila na mdudu sisimizi.
Kwa mujibu wa habari hizo, wanachama hao wamekuwa wakihoji kama ndani ya Chadema kuna sisimizi na tembo na kwamba kama yapo basi chama kina matabaka ya watu, jambo ambalo si la haki.
Akizungumzia kuwepo kwa mpasuko ndani ya Chadema , Makani alisema haoni kama uamuzi huo unaweza kuathiri chama wala kuzidisha ufa.
Alisema mpasuko unaweza kujitokeza zaidi kama tuhuma dhidi ya maafisa hao zitathibitika kuwa ni za kweli na wakaachwa ndani ya chama.
Katika uamuzi wake Dk Slaa alisema ametengua ajira za wanachama hao wawili kwa maslahi ya chama, hatua iliyotangazwa siku kadhaa tangu kuvuja kwa siri za kikao kati ya Mbowe na baadhi ya viongozi wa Chadema.
Habari za awali zilisema kikao hicho kilichofanyika mjini Dodoma, kilijadili pamoja na mambo mengine, nidhamu ya wanachama hao pamoja na mama mzazi wa Zitto, Shida Salum.
Habari tulizopata wakati tunakwenda mitamboni zilisema baadhi ya wazee wa Kigoma, wamemtaka Kafulila kuwa jasiri na kutokata tamaa ili hatimaye awanie ubunge katika Jimbo la Kigoma Kusini.
Vyanzo vya habari za kuaminika, vilifafanua kwamba wazee hao walikutana na Kafulila juzi usiku baada ya kuvuliwa wadhifa aliokuwa nao.
Habari hizo zilieleza kwamba, wazee wakiwemo viongozi wa dini wameelezea kuchukizwa na uamuzi wa Dk Slaa, kumvua Kafulila wadhifa wake.
Kafulila alipoulizwa kuhusu mkutano huo na wazee, alijibu: "Hapana kaka hakuna kitu kama hicho, mimi bado naombea Chadema kiwe chama kimoja."
Hata hivyo, habari hizo za ndani zilikariri wazee hao wakitaka Kafulila na mwenzake Juju warejeshwe kwenye nafasi zao mara moja ili kuleta amani na utengamano katika chama.
Wakati mzee Makani akiweka matumani ya uhai wa Chadema, hali ya kisiasa ndani ya chama hicho ni tete kufuatia kuwepo kwa kambi zinazopingana.
Hali hiyo tete kisiasa inatokana na baadhi ya wanachama kuona, uamuzi huo wa Dk Slaa, kuwa umefanywa kwa chuki zilizotokana na majeraha ya uchaguzi wa viongozi ndani ya chama.
Katika uchaguzi huo wa Septemba, Zitto alimtikisa Mbowe, baada ya kuingia kwenye kinyang'anyiro cha uenyekiti. Mpasuko mkubwa ambao ulijitokeza katika kipindi hicho unaonekana kuisumbua Chadema