Nov 12, 2009
ALIYEKUWA Ofisa Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), David Kafulila amesema licha ya kuvuliwa wadhifa wake, hana mpango wa kuhamia chama kingine.
Kafulila amesema, Chadema ni chama mbadala, hivyo kwa sasa kinahitaji kuwa imara zaidi na yeye kuondoka katika chama ambacho alidai Watanzania wana matumaini nacho, itakuwa si kuwatendea haki.
Amesema, hata alivyokutana na wazee wa Kigoma ambao wanakwenda Hijja Saudi Arabia, walimtia moyo na aliwahakikishia kuwa hawezi kuondoka Chadema, kwani wenye tatizo ndani ya chama hicho ni mtu mmoja mmoja na si chama.
Sifikirii kuondoka Chadema, kwangu mimi nimeipenda tangu niko shule ya msingi, hilo la kuondoka haliwezekani kamwe, alisema. Kiongozi mwingine aliyevuliwa wadhifa wake ni Danda Juju, ambaye alikuwa anahusika na mambo ya Bunge.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu madai ya mgogoro ndani ya chama hicho, alisema masuala ya watendaji kuvuliwa nyadhifa, yako chini ya Katibu Mkuu wa Chama.
Mimi sipendi kuzungumzia suala hilo kwani si la kisiasa, masuala ya kiutendaji tumemwachia Katibu Mkuu ndiye msimamizi wa watendaji wote wa makao mkuu, alisema Mbowe.
Wakati Mbowe anatoa msimamo huo, Kafulila alisisitiza kuwa licha ya kuwa Katiba inampa mamlaka Katibu Mkuu kuwavua nyadhifa zao watendaji, lakini anaamini Dk Wilbroad Slaa, hakumtendea haki.
Aliongeza kuwa licha ya kuwa haungi mkono kuondolewa kwenye nafasi ya uofisa habari, lakini anaamini kuwa hizo ni changamoto za kisiasa na siku moja Chadema itatengemaa.
Alipotakiwa kueleza undani wa yeye kuvuliwa wadhifa, Kafulila alisema sitaki kuzungumzia mambo ya ndani ya chama chetu, kufanya hivyo nitakuwa naibomoa Chadema, chama ambacho ni matumaini ya Watanzania.
Kuhusu kama hatua hiyo inaweza kumdhoofisha kisiasa, alisema haamini kuwa hatua hiyo imemdhoofisha badala yake aliwataka wafuasi wa chama chake Kigoma watulie, kwani hicho ni chama chao wote.
Kafulila pia aligoma kusema alichojadiliana na wazee wa Kigoma; bali akasema tu kwamba walikutana wakajadili mambo mengi yanayohusu siasa.
Wale wazee si wanasiasa, wale ni viongozi wa dini, siwezi kusema tulichojadiliana nao, ila ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba wazee walinipa ujasiri wa kuendelea mbele katika harakati zangu za siasa, alisema mwanasiasa huyo chipukizi.
Alisema wazee wale wanafahamu harakati zake za kupigania haki tangu akiwa Kigoma na ndiyo maana waliposikia kuhusu matatizo yake kuwa amevulia wadhifa kwa chuki, waliona vema watete naye kabla ya kwenda Hijja.
Juzi baadhi ya vyombo vya habari vilimkariri Dk Slaa akisema kuwa ametengua ajira za watu hao wawili kwa maslahi ya chama na kuongeza kuwa hatua hiyo ina lengo la kukisafisha chama kwani wakiacha hali hiyo iendelee wanaweza kuingia Ikulu na mambo ya ajabu.
Lakini uamuzi huo ulipingwa na Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, ambaye alisema unaweza kukidhoofisha chama kwani Kafulila anaandaliwa kugombea ubunge Kigoma Kusini ambako CCM ilifanya vibaya kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Source: Habari Leo