- 18 -
Riwaya: Msako
Mtunzi: Japhet Nyang’oro
Baada ya kutoka nyumbani kwa Afande Lucas, mpelelezi Jacob Matata alikanyaga mafuta hadi posta Mpya. Aliangalia saa yake ilikuwa saa sita na dakika hamsini na tatu asubuhi. Alipomaliza kuegesha gari lake maeneo fulani, aliingia Benki akachukua kiasi cha hela za kutosha. Safari hii hakutaka kutumia gari alilokuwa amekuja nalo, hivyo akachukua taxi hadi Tazara, Uchumi Super Market (USM) ndani ya Quality Plaza (QP). Hapo aliingia akanunua vitu vingi vya kula, lakini pia, akanunua kitabu cha riwaya Patashika, hakuwa amechukua kitabu hicho wakati anatoka safe house.
* * *
Saa nane kasoro dakika ishirini na tano mchana wa jua kali katika jiji la Dar es salaam, mpelelezi Jacob Matata anatembea kutoka jengo la Quality Plaza akiwa amebeba mfuko wenye vitu alivyonunua. Wakati yeye akitembea kutoka, kuna watu watatu walikuwa wanabishana ndani ya gari hatua chache toka pale alipokuwa.
“Wewe hebu mmalize bana tukafanye mambo mengine.” Mmoja alisema.
“Hapana, tumeambiwa kummaliza lakini natamani tummalize kwa namna ambayo itatupa sifa na majina makubwa baadaye. Unadhani kumuua mpelelezi hodari kama huyu ni nafasi ya kuchezea?’’ Mwingine alisema.
“Lakini kweli maana kesho unaweza jikuta umeingia kwenye orodha ya wauaji mashuhuri duniani.” Mwingine alisema kabla ya kuongeza, “Ila unadhani ni busara kupambana na Jacob Matata? Maana nasikia ni moto wa kuotea mbali!’’
“Sikiliza si unaona pale anatafuta taxi, twende halafu tumzoe kama mzoga na kuondoka naye. Napenda tuache majina yetu kwenye mwili wake ili watu wajue siye ndio tumemuua. Hiyo itatupa heshima sana!’’ Huyu alisema.
“Wazo zuri, haya naona anaelekea kwenye kile kijinjia pale. Akifika kwenye kile kibanda ndio tunaweza kumbana vema na kumzoa. Iwe kasi sana.” Mwingine alisema. Wakakubaliana.
* * *
Wakati hawa wanakubaliana, Poka Kingu yeye alikuwa akimwangalia Jacob Matata kwa husuda. Alikuwa ameshapewa maelekezo toka kwa Ngongoseke kuwa amwache kwanza kwa sasa. Hivyo japo alikuwa kwenye nafasi ya kummaliza Jacob Matata lakini aliheshimu uamuzi wa Ngogoseke. Alimwona Jacob Matata akiwa anakaribia kwenye kibanda fulani cha kuuzia vocha za simu.
* * *
Jacob aliendelea kutembea kueleke upande ambao kulikuwa na taxi za kukodisha. Wakati amekaribia kibanda cha simu mara akasikia gari likija kwa kasi nyuma yake.
Hakutaka kugeuka kuangalia ilikuwa nini, alijirusha na kuparamia mlango wa kile kibanda. Halafu akamwona mtu anamjia kwa kasi pale alipokuwa. Kwa kasi sana alijigeuza na kuachia teke kali ambalo lilimpata yule mtu kiunoni. Jamaa alijikakamua akanyanyuka kwa haraka wakati huo Jacob alikuwa ameshatoa bastola yake baada ya kuona gari lilikuwa limesimama. Hakuchelewa kujua nia ya wale watu kuwa ilikuwa ni kumteka nyara. Aliachia risasi mbili haraka zote zikampata yule Jamaa kifuani. Kuona hivyo Jamaa aliyekuwa kwenye gari aliliondoa gari kwa kasi kuelekea barabarani. Jacob Matata aliachia risasi kulenga taili za gari lile. Gari likaingia Kilwa road kwa fujo na kusababisha ajali mbaya. Liligongwa na magari mengine yaliyokuwa kwenye kasi kubwa, yalilisomba na kuliburuza ubavu ubavu. Wakati watu bado wako kwenye taharuki kubwa, Jacob Matata aliokota vitu vyake alivyokuwa ameviagusha wakati wa purukushani halafu akafanikiwa alijipenyeza katikati ya watu, kabla haijawa shida kubwa.
————————————————————
RIWAYA HII SI YA KUKOSA KITABU CHAKE. KITABU KINATOKA WIKI IJAYO KWA WALIOWEKA ODA NA KULIPIA.
————————————————————
Poka Kingu alitabasamu, ‘ndio maana ushujaa mwingine miye huwa siupendi’, alijiwazia. ‘Kilichowafanya watake kumchukua mzima-mzima ni nini? Shenzi zao wamepata walichostahili’. Hata hivyo Poka Kingu hakufanikiwa kumwona Jacob Matata alivyotoweka. Poka alijilaumu kwa kukubali kuambukizwa uzembe na wale wazembe waliokuwa wakitaka kuonekana mashujaa mbele ya mtu anayewazidi uwezo. Alijitahidi kadiri alivyoweza lakini hakufanikiwa kumwona tena. Hii ilimaanisha apange mbinu mpya za kuweza kupata mwenendo wa Jacob Matata.
* * *
Njia za vichochoroni zilimfikisha vichochoro vya Buguruni. Safari yake iliishia kwenye moja ya nyumba ambayo ilionekana kuwa wenye nyumba walikuwa wamesafiri muda mrefu. Jacob Matata ndiye alikuwa mpangaji wa nyumba hii, hakuwa akiitumia, ila alikuwa mwaminifu kwa mwenye nyumba wake, ambaye alikuwa akimpa kodi nono. Alikuwa ameweka mtu ambaye alikuwa akimsafishia mara moja kwa mwezi na kisha humlipa kwa kazi hiyo tu.
Aliingia ndani na kuangalia vitu vyake harakaharaka. Kisha akachukua daftari lake na zile nakala za kitabu alizokuwa amefanya toka nyumba ya hazina. Hapo kazi ya kusoma ikaanza upya. Alikisoma kitabu Patashika kuona jinsi mwandishi Japhet Nyang'oro alivyokuwa ameelezea matukio kwa kina.
Baada ya kusoma kwa kina na kuunganisha matukio kadhaa, hatimaye aliafikiana na muhtasari aliokuwa ameuandika wakati akiwa safe house.
Sasa aliona lazima aanzie Upanga NHC nyumba namba 41A. Alihis kuwa Afande Mwenda Lucas, alikuwa amegundua kitu hadi akaitaja nyumba hiyo kwenye ripoti yake aliyokuwa anaikusanya. Baada ya hapo angemtafuta mtu anayeitwa Luteni Frank Misanya, maana huyu alikuwa kwenye ripoti na hata Nana mke wa Afande Lucas alisema kuwa mumewe alimtaja. Japo aliona ingekuwa rahisi kwake kuweza kufuatilia watu au mtu aliyeweka kinasa sauti kwa Nana lakini alijikumbusha kuwa uzoefu unamwambia kuwa ukiwa kwenye upelelezi mgumu kama huo si vema kufuata njia rahisi maana hakuna adui aliye fundi wa mambo angependa kuacha nyayo zake kirahisi kama si mtego. Hivyo aliamua kumwacha Nana na mazingira yake kama kiporo.
* * *
Saa tisa na robo alasiri, wakati Jacob Matata anakata shauri kuanzia Upanga NHC nyumba namba 41A, Poka Kingu na yeye alikuwa kwenye hesabu zake.
“Wapelelezi ni kama Inzi tu, wanapoona kinyesi hawaachi kuzungukia hapo. Nina hakika atarudi tena kwa Nana, hivyo watatu mtakwenda nyumbani kwa marehemu Lucas Mwenda kumngoja Jacob Matata. Nina hakika baada ya kuona kile kifaa tulichomwachia Nanalungu kwa vyovyote atataka kwenda ili asubiri yeyote atakeyekwenda akabiliane nae na kuweza kutufikia. Hakuna anayeweza kukabiliana na Jacob Matata hapa kati yenu, hivyo mtakachofanya mkimuona tu ni kumfuatilia kila anapokwenda na kunipa taarifa. Nataka kujua ameweka kambi wapi. Maana sasa anatafutwa sana na vyombo vya usalama hivyo najua kuna sehemu amejizika ili isijulikane alipo.” Poka Kingu alisema kwa vijana wake ambao alikuwa amewakusanya wamsaidie kufanya kazi ya kukusanya taarifa na kufuatilia watu huku yeye akiwa amejiwekea kazi ya kung’oa visiki.