RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 36
Mtunzi:Kelvin Mponda
...akishuka kwenye ile lifti atoke kisha nikaingia mle ndani na kubonyeza kitufe ukutani nikiiamuru ile lifti inifikishe ghorofa ya tano ya lile jengo. Mlango ulipojifunga ile lifti ikaanza kupanda juu na wakati ule mawazo mengi yakawa yakipita kichwani mwangu.
Nilianza kwa kukumbuka mambo yote yaliyojili tangu siku ile ya kwanza nilipoondoka jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kuja pale Bujumbura nchini Burundi. Kisha nikamkumbuka yule msichana mrembo wa ajabu aitwaye Amanda niliyesafiri naye kutoka jijini Kigali nchini Rwanda namna alivyonisaliti kwa wale wanajeshi na kugeuka mwiba mchungu katika safari yangu. Nikiwa katikati ya mawazo yale nikamkumbuka Hidaya kabla ya mawazo yangu kuhamia tena kwa yule mtu aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Jean-Baptiste Nibizi muda mfupi kabla ya kuuwawa kwa risasi kwenye ukingo wa ule mto mkubwa kando ya daraja la barabara ielekeayo mbali na jiji la Bujumbura.
Hatimaye mawazo yangu yakahamia nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa muda mfupi uliopita nikikumbuka namna nilivyopambana na lile jitu hatari na hatimaye kuchomoka na ushindi mwembamba katika pambano la kukata na shoka. Mwishowe mawazo yangu yakahamia kwa yule kijana mfanyakazi wa nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Sundi. Kitendo cha kumkumbuka Sundi kikayapelekea mawazo yangu yaweke nanga kwenye mjadala mzito juu ya Padri Aloysius Kanyameza.
Kitendo cha ile lifti kugota haraka kikayarudisha mawazo yangu mle ndani na hapo nikashtukia kuwa tayari nilikuwa nimefika kwenye ghorofa ya tano ya lile jengo la New Parador Residence. Mlango wa kile chumba cha lifti ulipofunguka nikalitengeneza vizuri koti langu na kutoka nje.
Sasa nilikuwa nimetokezea kwenye korido pana iliyomezwa na utulivu wa aina yake. Korido ile ilikuwa ikipakana na milango mingi ya vyumba kwa upande wa kushoto na kulia. Nikasimama kidogo nikiichunguza korido ile kwa utulivu. Katikati ya ile korido kulikuwa na kitufe kikubwa chekundu cha kengele ya hatari pembeni ya mtungi mkubwa wa gesi ya kuzimia moto wa dharura. Kwenye dari ya korido ile kulikuwa na taa ndefu za tubelight za mtindo wa kupendeza zilizokuwa zikiangaza mwanga wa wastani katikati ya korido ile na hivyo kuyafanya mandhari yale tulivu yapendeze. Lile jengo lilikuwa kubwa hivyo na ile korido nayo ilikuwa ndefu kiasi kwamba sikuweza kuona mwisho wake vizuri.
Hatimaye nikaanza kutembea taratibu nikiichunguza kwa makini milango yote iliyokuwa ikitazamana na ile korido. Juu ya ile milango kulikuwa na vibao vidogo vya rangi ya kijivu vilivyokuwa na utambulisho wa namba ya chumba husika. Nikaendelea kutembea taratibu kwa utulivu huku nikiyatembeza macho yangu huku na kule kutazama zile namba milangoni. Haikuwa hadi pale nilipofika katikati ya korido ile upande wa kulia ndiyo nikauona mlango wenye kibao kilichochongwa vizuri namba 302.
Kwa sekunde kadhaa nikasimama nikiutazama mlango ule kwa makini. Jambo moja lilinishangaza kidogo huku nikijiuliza kama kweli ule mlango ulikuwa ni wa kuelekea ofisini kwa meneja wa ile hoteli kwa nini hapakuwa na utambulisho wowote pale mlangoni unaoelezea kuwa ile ni ofisi ya meneja wa ile hoteli?. Huku nikiendelea kujiuliza kwa nini ofisi ya meneja wa hoteli kubwa kama ile iwekwe ghorofa ya tano ya lile jengo badala ya kuwekwa ghorofa ya chini ambapo ndiyo ingelikuwa rahisi zaidi kufikiwa na wateja wanaohitaji huduma. Nikaendelea kujiuliza pasipo kupata majibu hata hivyo muda haukuwa rafiki kwangu hivyo hatimaye nikausogelea ule mlango na kubofya kitufe kidogo cha kingele kilichokuwa kando yake.
Ulipita muda mrefu pasipo mwitikio wowote wa kutoka ndani ya kile chumba na hali ile ikanisukuma nisogee tena pale mlangoni na kubofya kile kitufe cha kengele. Mara moja tu kengele ile ilipoanza kuita tena mara nikauona ule mlango ukifunguliwa taratibu na mbele yangu akasimama mwanaume mmoja mfupi mwenye sura ya umbo duara, macho makubwa, pua ya kibantu na mdomo wenye kingo pana uliozungukwa na ndevu zilizokatiwa vizuri. Mwanaume mfupi na mnene mwenye kitambi cha ukwasi huku amevaa suti ya kodrai ya rangi ya udongo, shati la rangi ya kijivu na tai nyeusi shingoni. Nilipomchunguza vizuri mtu yule nikaridhika kuwa alifaa kuitwa meneja wa hoteli ile kwa namna ya haiba yake. Tabasamu hafifu la kirafiki likaanza kuumbika usoni na hapo yule mtu akavunja ukimya akinikaribisha na nilipomtazama nikagundua kuwa umri wake haukwenda mbali zaidi ya miaka arobaini.
“Bien venu Monsieur et tu as de la chance, parceque je me préparer a quitté le bureau”. Karibu sana ndugu, tena una bahati sana maana ndiyo nilikuwa najiandaa kufunga ofisi. Yule mtu akanikaribisha kiungwana na wakati nikiingia mle ndani akanipa mkono na tabia yake ile ya ukarimu ikawa imenivutia sana. Ule mlango nyuma yangu ukafungwa.
“Merci beaucoup”. Ahsante sana. Nikaitikia kwa furaha huku nikipiga hatua zinazopwaya ndani ya ofisi ile ngeni kabisa machoni mwangu huku taratibu nikiyatembeza macho yangu kutazama mandhari ya ile ofisi.
Ilikuwa ofisi kubwa yenye mandhari tulivu ya kuvutia. Upande wa kulia kulikuwa na kiti kikubwa cha sofa nyuma ya meza kubwa ya ofisini yenye majalada mengi yaliyopangwa moja juu ya lingine, bendera ndogo ya mezani ya taifa la Burundi, kidau cha wino, mhuri, kompyuta moja ya mezani na simu ya mezani pembeni yake. Kando ya ile meza kulikuwa na kabati kubwa la mbao lenye nyaraka za kiofisi kando ya sefu moja ya chuma.
Nikaendelea kuyatembeza macho yangu taratibu mle ndani na kwa kufanya vile upande wa pili wa ile ofisi nikaliona dirisha kubwa ukutani likiwa limefunikwa kwa mapazia mawili marefu. Upande wa kushoto wa ile ofisi kulikuwa na seti moja ya makochi mazuri ya sofa nyuma ya meza fupi ya kioo yenye ua zuri juu yake na pembeni ya makochi yale ukutani kulitundikwa runinga pana flat screen iliyofungwa sistimu ya nzuri mziki. Nilipotazama kwenye kona moja iliyokuwa upande wa kushoto wa ile ofisi nikauona mlango na hapo nikahisi kuwa ule ulikuwa ni mlango wa kuelekea sehemu ya maliwato ya ile ofisi ingawa sikuwa na hakika ya moja kwa moja hata hivyo ule mlango ulikuwa umefungwa. Ofisi ilikuwa nzuri na yenye mandhari ya kisasa yaliyonogeshwa na hewa nzuri ya kiyoyozi kilichokuwa mle ndani. Sakafuni kulikuwa na zulia zuri la rangi ya chanikiwiti lenye manyoya laini ya kupendeza. Nilipochunguza vizuri kando ya dirisha kubwa la mle ndani nikakiona kipoza maji.
“Sʾil vous plais, assaiez-vous”. Tafadhali karibu uketi. Yule meneja wa hoteli akanikaribisha niketi kwenye kochi moja la mle ndani baada ya kuniona nikisitasita huku yeye akizunguka na kwenda kuketi kwenye kile kiti cha ofisini kilichokuwa nyuma ya ile meza yake ya utukufu.
“Merci”. Ahsante. Nikashukuru na kwenda kuketi kwenye kochi moja la sofa la mle ndani lililokuwa karibu na ile meza ya ofisini. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku nikiutumia muda wangu kuyazoea vizuri mandhari yale na hali ile ya ukimya ilipokuwa mbioni kushika hatamu nikavunja ukimya baada ya kukohoa kidogo kusafisha koo langu.
“Jʾai besoin de voir le directeur de cet hôtel, sans doute cʾest toi”. Nahitaji kuonana na meneja wa hii hoteli, bila shaka ndiyo wewe. Nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama yule mtu mfupi mbele ya kile kiti cha ofisi.
“Cʾest moi”. Ndiyo mimi. Yule mtu akaitikia kwa utulivu pasina mashaka yoyote kisha akakohoa kidogo kusafisha koo lake kabla ya kuendelea.
“Je mʾappelle Monsieur Vital Desire Habonimana, le directeur de cet hôtel. Quel est votre nom?. Naitwa ndugu Vital Desire Habonimana, meneja wa hoteli hii. Jina lako nani?. Yule mtu mfupi akamaliza kujitambulisha huku akinikodolea macho nami nikakohoa kidogo kabla ya kuvunja ukimya.
“Je mʾappelle James Lusungu Iʾofficié de Iʾembassade de Tanzanie ici à Bujumbura. Je vous savoir si le jour avant hier notre ambassadeur a arrivé ici à Iʾhôtel partucipé à la reunion”. Naitwa James Lusungu, afisa wa ubalozi wa Tanzania hapa Bujumbura. Nataka kufahamu kama juzi balozi wetu alifika hapa hotelini kwako kuhudhuria mkutano”. Nikadanganya kwa kujiamini huku nikimtazama yule mtu kwa makini. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku yule mtu mfupi akinitazama kwa utulivu kama anayefikiria jambo fulani pasipo kuonesha tashwishwi yoyote usoni mwake halafu baada ya kuitazama saa yake ya mkononi akavunja tena ukimya.
“Pourquoi ne pas rentre au bureau et demande cette question aupès de votre ambassadeur?”. Kwa nini usirudi ofisini na kumuuliza Balozi wako swali hilo?. Maelezo ya yule mtu yakanishangaza na haraka nikagundua kuwa kulikuwa na namna fulani ya jeuri katika maelezo yake tofauti kabisa na wakati ule alipokuwa akinikaribisha mle ndani muda mfupi uliopita. Hata hivyo kwa kuwa tayari nilikuwa ndani ya ofisi yake tena nikiwa na haja yangu binafsi nikaamua kujipa uvumilivu huku nikilazimisha tabasamu la kirafiki usoni mwangu.
“Notre ambassadeur maintenant il est en voyage vers Dar es Salaam Tanzania”. Balozi wetu sasa hivi yuko safarini anaelekea Dar es Salaam Tanzania. Nikaongea kwa kujiamini huku nikidanganya na hapo yule mtu mfupi akaangua kicheko cha ghafla kilichonishangaza na kuniacha kwenye mduwao wa aina yake. Kicheko kile kilipofika ukomo yule mtu akaongea kwa utulivu kama mtu aliyefyatukwa na akili kichwani.
“Un homme adulte comme toi, tu nʾas pas honte de tromper?”. Mtu mzima kama wewe hivi huoni aibu kudanganya?.
Maelezo ya yule mtu mfupi meneja wa hoteli ile yakanipelekea nihisi kuwa huwenda nilikuwa nikifahamika vizuri na mtu yule kuliko vile nilivyokuwa nikidhani. Hata hivyo nikapiga moyo konde na kumeza funda kubwa la mate kuitowesha hofu moyoni mwangu huku dalili zikiashiria kuwa mambo hayakuwa shwari tena mle ndani.
“Donc toi, tu connais là où est Iʾembassadeur Adam Mwambapa?’’. Kwa hiyo wewe unafahamu mahali alipo Balozi Adam Mwambapa?. Nikamuuliza yule mtu kwa jazba kidogo. Yule mtu akacheka tena huku akijishika kidevu chake kifahari kabla ya kuniuliza.
“Tu veus savoir là où est votre embassadeur ou tu veus savoir si le jour avant hier il a partucipé à la reunion ici à Iʾhôtel?”. Unataka kufahamu mahali alipo balozi wako au unataka kufahamu kama juzi alihudhuria mkutano hapa hotelini?.
“Les tout” Vyote. Nikamjibu kwa jazba.
“Ne te trompes pas camarade en pensant quʾ on est te connait pas qui tu es”. Usijidanganye komredi ukidhani kuwa hatukufahamu vizuri kuwa wewe ni nani”. Yule mtu mfupi akaniambia huku akiangua kicheko hafifu cha dhihaka.
“Je ne comprends pas, tu parles quoi?”. Mbona sikuelewi unaongea nini?. Nikamuuliza yule mtu kwa hasira za kudhihakiwa.
“Bien venu camarade jʾai pensé que tu sera encore malin et echaper à cet obstacle”. Karibu sana komredi nilidhani kuwa mara hii ungekuwa mwerevu kuruka kiunzi hiki. Sauti kavu ya kiume kutoka nyuma yangu ikazungumza kwa utulivu hali iliyonishtua na kunipelekea nigeuke haraka kutazama nyuma yangu na kwa kufanya vile nikajikuta nikitazamana na mdomo wa bastola yenye uchu aina ya Type 64 Silenced iliyofungwa kiwambo maalum cha kuzuia sauti. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu kisha kijasho chepesi kikaanza kunitoka sehemu mbalimbali mwili wangu.
Sasa nilikuwa na hakika kuwa nilikuwa nimejiingiza kwenye himaya ya adui pasipo kujua na pale ndiyo nikafahamu kwanini yule mtu mfupi mbele yangu aliyejinadi kuwa ni meneja wa ile hoteli alikuwa akiongea kwa kujiamini sana ule muda mfupi uliopita. Jambo la kushangaza zaidi ni kuwa ile bastola nyuma yangu ilikuwa imeshikwa na yule kijana wa mapokezi ya ile hoteli aliyekuwa akifuta glasi kwa kile kitaulo kidogo wakati ule nilipokuwa nikiingia kwenye ile hoteli kati ya wale vijana wawili wahudumu wa ile hoteli waliokuwa ile sehemu ya mapokezi kule chini. Yule kijana aliyenishikia bastola nyuma yangu bado alikuwa katika sare zake za kazi huku usoni akitengeneza tabasamu jepesi la ushindi wenye dhihaka na kejeli.
Kwa kweli sikuwa nimetarajia kabisa kuwa vijana wale niliowakuta kule sehemu ya mapokezi ya ile hoteli kuwa walikuwa ni mamluki waliopandikizwa eneo lile kwa ajili ya kufanikisha mpango wa kuninasa. Mara moja nikakumbuka namna vijana wale walivyokuwa wakitazamana wakati nilipokuwa nikizungumza nao kule chini sehemu ya mapokezi ya ile hoteli na hapo nikagundua kuwa kumbe kulikuwa na jambo lililokuwa likiendelea baina yao dhidi yangu.
Hata hivyo sikuweza kuelewa ni kwa namna gani yule kijana aliyenishikia bastola nyuma yangu alikuwa amefanikiwa kuingia mle ndani pasipo kufanya kelele yoyote ya kunishtua. Hisia zangu zikanitanabaisha kuwa nilikuwa nimekutana na watu hatari na professional katika harakati za kijasusi. Nikapiga moyo konde na kumeza funda kubwa la mate kuupoteza mshtuko mkubwa usoni mwangu kisha nikageuka na kumtazama yule mtu mfupi mbele yangu aliyejinadi kwangu kuwa ndiye meneja wa ile hoteli kisha nikavunja ukimya.
“Quelle obstacle?”. Kiunzi gani?. Nikauliza kwa kujiamini ingawa haraka niligundua kuwa sauti yangu ilikuwa imeanza kupwaya. Swali langu likaibua kicheko kingine cha ghafla kwa wale watu ingawa sikuweza kufahamu hasa ni kitu gani kikubwa katika swali lile kilichowapelekea wale watu waangue kicheko cha ghafla vile kama makahaba waliohongwa bia kaunta. Kicheko kile kilipokoma yule mtu mfupi mbele yangu akavunja ukimya na kuanza kuongea huku akinitazama kwa makini na nilipoyachunguza macho yake nikagundua kuwa hayakuwa na huruma hata kidogo.
“Premier jʾaimerais tʾappelle Tibba Ganza, et non tes noms de massonge les quels tu utilises pour depasser les frontierres de nos pays”. Kwanza ningependa kukutambua kama Tibba Ganza na siyo hayo majina yako ya uongo unayoyatumia kwa ujanja kuvuka mipaka ya nchi zetu. Yule mtu mbele yangu akaongea kwa hakika huku akionekana kuwa na taarifa nyingi juu ya nyendo zangu hali iliyonipelekea nihisi kuwa wale watu walikuwa na ushirika mmoja na Amanda. Hivyo sikuwa tena na shaka kuwa hata taarifa zangu walikuwa wamezipata kutoka kwake...ITAENDELEA