Riwaya: Ufukwe wa Madagascar

RIWAYA; UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 12
Mtunzi:Kelvin Mponda

....Kwa kweli niliumudu vyema usukani wa gari na mwendo wangu ulikuwa siyo wa kubabaisha nikipanda milima na kushuka mabonde kama upepo huku akili yangu ikijikita katika kuwaza hali ya mambo itakavyokuwa baada ya kufika jijini Bujumbura nchini Burundi. Nikiwa katika mawazo yale mara Amanda akaniuliza tena.
“Il ya une chose que je doute avec”. Kuna kitu bado nina wasiwasi nacho. Amanda akaongea kwa utulivu na hapo nikageuka na kumtazama kwa shauku huku nikishtushwa na maongezi yale.
“La quelle?. Kitu gani?. Nikamuuliza Amanda huku nikimkata jicho hata hivyo Amanda aliendelea kutabasamu kisha akaniuliza.
“Un beau homme comme toi, tu nʼas pas une femme ni une fiancée?”. Mwanaume mzuri kama wewe kusema kuwa hujaoa na huna mchumba?. Swali la Amanda likanipelekea nitabasamu kidogo na kuongea.
“Crois moi, mais aussi cʼest le temps de chercher mon partenaire”. Niamini, lakini hata hivyo nadhani muda wa kutafuta mwenza wangu pia umefika. Niliangua kicheko hafifu huku nikiendelea kukanyaga mafuta na kutokomea kwenye barabara ile na kwa kweli akili yangu haikuwepo kabisa katika masuala ya mapenzi kama Amanda alivyokuwa akidhani. Badala yake akili yangu ilikuwa imejikita katika kuwaza namna ya kuanza harakati zangu mara baada ya kufika jijini Bujumbura.
_____
Tulikuwa tumetembea umbali usiopungua kilometa hamsini na ushei katika barabara ile iliyopakana na misitu mizito, tukivuka madaraja, kupanda milima na kushuka mabonde katikati ya giza nene na mvua kubwa ya masika isiyokuwa na kikomo pale Amanda alipoamua kuvunja ukimya ulioanza kuota mizizi mle ndani ya gari.
“Diminuer la vitesse!”. Punguza mwendo!. Ghafla Amanda akaniambia huku akionesha hakika kuwa nilikuwa sijakiona kile alichokuwa amekiona katika barabara ile mbele yetu.
“Quʼ est-ce quʼil ya?. Kuna nini?. Nikamuuliza Amanda huku nikipangua gia za gari lile kwa fujo kama niliyeshikwa na wazimu. Kitendo ambacho hata mimi mwenyewe sikupenda.
“Au côté gaushe là devant, il y a une voiture en panne”. Pale mbele kuna gari limeharibika. Amanda akaniambia kwa taharuki huku akinionesha kwa kidole chake mbele ya ile barabara upande wa kushoto. Nikaendelea kupangua gia na kupunguza mwendo kwa pupa huku macho yangu yakijitahidi kufuata uelekeo wa kile kidole cha Amanda. Nilipoyatuliza vizuri macho yangu nikaliona gari jeupe aina ya Landcruiser hardtop likiwa limeegeshwa barabarani huku nyuma yake kukiwa na matawi kadhaa ya miti yaliyokatwa na kulazwa barabarani kama alama ya kutambulisha kuwa gari lile lilikuwa limeharibika.
Niliendelea kupangua gia na kupunguza mwendo huku macho yangu yakilitazama lile gari kwa udadisi. Gurudumu moja la nyuma la lile gari lilikuwa limefunguliwa na kulazwa chini huku sehemu yake ikiwa imenyanyuliwa na kuwekwa juu ya kipande cha gogo. Chini kwenye uvungu wa lile gari niliiona miguu ya mtu fulani aliyelala ikiwa nusu imetokeza nje na kunipelekea niamini kuwa gari lile lilikuwa likifanyiwa matengenezo. Nikaendelea kupunguza mwendo huku nikiendelea kulitazama lile gari na nilipotazama juu yake kwenye carrier nikagundua kuwa lile gari lilikuwa limebeba shehena kubwa ya mzigo uliokuwa umefunikwa vizuri kwa turubai.
Nilipoendelea kupunguza mwendo na kuzidi kulikaribia lile gari nikagundua kuwa ndani ya lile gari kulikuwa na watu ingawa jinsia na idadi yao ilikuwa ni vigumu kuifahamu haraka kutokana na giza lililokuwa mle ndani. Haraka nikayapeleka macho yangu pembeni kumtazama Amanda na hapo nikagundua kuwa alikuwa amesogea karibu zaidi na kioo cha mbele cha ile gari kutazama kule mbele. Amanda hakusema neno lolote ingawa nilikuwa na kila hakika kuwa alikuwa akifahamu kuwa nilikuwa nikimtazama. Haraka nikawaona wanaume wawili wakija nyuma ya ile gari na kutupungia mikono katika namna ya kututaka tusimame ili watuombe msaada.
“Arrête toi, je pense quʼil ont besoin dʼaide”. Simama, nahisi wanahitaji msaada. Amanda akaniambia kwa msisitizo katika namna ya kunihimiza nisimame. Wale watu wakaendelea kutupungia mkono kwa bidii huku mmoja akitumia shati lake alilolivua haraka baada ya kuhisi huwenda hatukuwaona.
“Arrête toi!”. Simama!. Amanda akaendelea kunisihi. Kwa kweli nilijikuta katika wakati mgumu wa kuamua nisimame au niendelee na safari kwani kumbukumbu ya lile tukio la utekaji lililokuwa limetokea masaa machache yaliyopita kule nyuma yetu tulipotoka ilikuwa bado haijatoweka katika fikra zangu.
Hatimaye nafsi yangu ikaingiwa na hali ya utu hivyo nikazidi kuminya breki na kupunguza mwendo zaidi nikitafuta sehemu ya maegesho hatua chache baada ya kulipita lile gari bovu. Lakini wakati nikiwa katika harakati zile mara ghafla nikawaona wanaume wengine wawili mbali na wale wa awali waliokuwa wakitusimamisha wakichomoza gizani kutoka upande wa kushoto wa lile gari na kuanza kukimbia taratibu wakija pale tuliposimama. Tukio lile likaupelekea moyo wangu ushtuke na kupoteza utulivu kabisa huku nafsi yangu ikianza kunisimanga katika namna ya kunilaumu kuwa huwenda nilikuwa nikifanya maamuzi yasiyokuwa sahihi kwa kusimama eneo lile.
Wale watu waliokuwa wakikimbia kutufuata walikuwa wamesaliwa na hatua chache kutufikia pale tulipoegesha gari wakati nafsi yangu iliposukumwa kufanya maamuzi magumu. Sikuruhusu aina yoyote ya mjadala mwingine kuzitongoza fikra zangu hivyo haraka nikaingiza gia na kukanyaga mafuta nikiliingiza lile gari barabarani. Mshangao uliomvaa Amanda haukutofautiana sana na ule uliowapata wale watu nyuma yetu wakati nilipowatazama kupitia kioo cha ubavuni cha lile gari Land Rover 110. Wale watu kuona vile wakasimama ghafla na kuweka mikono yao vichwani katika namna ya kukata tamaa kama wachezaji wa mpira wa miguu waliokosa penati ya mwisho katika mchezo fainali. Amanda akageuka na kunikata jicho la mshangao lenye hasira iliyotokana na kupuuzwa kwa hoja yake.
“On ne peut pas sʼarrêter, ce milien ne pas bon”. Hatuwezi kusimama kwani hii sehemu siyo salama. Nikaongea kwa msisitizo huku nikionekana kupuuza waziwazi ombi lile kwani hisia zangu zilikuwa zimenitanabaisha waziwazi kuwa kusimama pale ilikuwa ni sawa na kuhatarisha usalama wetu.
Amanda akaendelea kunitazama kwa hasira kana kwamba nilikuwa nimefanya dhambi kubwa iliyomshangaza hata shetani mwenyewe. Hata hivyo sikutaka kabisa kukubaliana na hisia zake na vilevile sikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiamini mawazo ya mtu mwingine hususani katika mazingira hatarishi kama yale.
Kupitia vioo vya ubavuni vya lile gari Land Rover 110 niliendelea kuwatazama wale watu nyuma yetu huku wakiwa wamesimama katikati ya barabara na kuendelea kulitazama gari letu namna lilivyokuwa likitokomea mbele yao bila matumaini ya kusimama. Hatimaye Amanda alipoona kuwa simsemeshi akaamua kuegemea vizuri siti yake huku akigeuka na kutazama dirishani dhahiri akionekana kununa na hali ile ikawa afadhali kubwa kwangu.
Mvua ilikuwa ikiendelea kunyesha na sauti pekee iliyokuwa ikisikika katika misitu ile ilikuwa ni ile sauti ya muungurumo wa injini ya lile gari letu wakati tukipanda milima na kushuka mabonde.
_____
“Il y a la voiture qui vient derière nous”. Kuna gari linakuja nyuma yetu. Sauti hafifu ya Amanda ikazirudisha fikra zangu mle ndani ya gari baada ya kitambo kirefu cha ukimya na hapo nikageuka haraka na kumtazama Amanda kama ambaye sikuwa nimemsikia vizuri maelezo yake.
“Quʼest quʼil y a?”. Kuna nini?. Nikamuuliza Amanda kwa shauku huku nikigeuka kidogo na kumtazama kabla ya kuyarudisha macho yangu kutazama tena mbele ya gari.
“Régarder les paraprises de côtés”. Tazama kwenye vioo vya gari ubavuni. Amanda akaniambia kwa hamaki na hapo haraka nikayapeleka macho yangu kutazama kwenye vioo vya ubavuni vya lile gari. Macho yangu yalipotulia vizuri mara nikauona mwanga mkali wa taa za mbele za gari lililokuwa likija kwa kasi nyuma yetu.
“La voiture…?”. Gari…?. Nikajiuliza kwa mshangao wakati jibu ninalo.
“Cʼest la voiture quʼon a passé qui été en panne”. Ni lile gari lililoharibika tulilolipita kule njiani. Amanda akaniambia huku akiendelea kutazama kwenye kioo cha ubavuni cha gari kilichokuwa upande wake.
“Cette fois-ci cette voiture est dépannée?”. Mara hii tu lile gari litakuwa limepona?. Nikamuuliza Amanda kwa wasiwasi huku nikiendelea kutazama kwenye kioo cha ubavuni cha lile gari letu.
“Même moi aussi je suis étoné, et elle vient très rapide”. Hata mimi nashangaa na linakuja kwa kasi sana. Amanda akaniambia huku dhahiri akionekana kuanza kuingiwa na hofu.
Niliendelea kulitazama lile gari namna lilivyokuwa likija kwa kasi na kutukaribia nyuma yetu huku akili yangu ikianza kutafakari juu ya tukio lile lisiloeleweka akilini mwangu. Baada ya muda mfupi lile gari hatimaye likawa limetufikia na nilipolichunguza vizuri nikapata hakika kuwa lilikuwa ni lile gari tulilolipita kule nyuma njiani. Ingawa sikuwa nimefahamu tatizo la lile gari lakini hata hivyo haikuniingia akilini kuwa ndani ya muda mfupi tu kiasi kile lile gari lingekuwa tayari limepona na kuendelea na safari yake. Hivyo tukio lile lilinipa wasiwasi mwingi.
Nikiwa naendelea kutafakari mara lile gari likaanza kutupita kwa kasi ya ajabu. Tukio lile likanipelekea nipunguze mwendo wa gari letu nikilipisha lile gari litupite kwa uhuru na kuendelea na safari yake. Hata hivyo hilo halikutokea kwani mara baada ya lile gari kutupita ghafla nikaliona likipunguza mwendo na kwenda kutuzuia kwa mbele. Kwa kweli nilishikwa na hofu na taharuki isiyoelezeka nikijitahidi kwa kila namna kulikwepa lile gari lakini ufundi wangu katika udereva iligonga mwamba. Kwani bila ya kupenda nilijikuta nikiligonga lile gari kwa nyuma na hapo sauti ya kishindo kikubwa ikasikika huku vioo na taa za nyuma za lile gari mbele yetu vikipasuliwa vibaya na ngao ngumu ya lile gari letu Land Rover 110 .Ilikuwa ajali mbaya lakini ya makusudi.
Amanda akapiga yowe la hofu hata hivyo ule haukuwa muda wa kushauriana baada ya kuhisi nini ambacho kingefuatia baada ya pale. Hivyo haraka nikajisogeza karibu na ule mlango wa kando ya Amanda kisha nikavuta kabali ya ule mlango kwa juu na kuufungua kwa teke moja la nguvu. Ule mlango ulipofunguka nikamfanyia Amanda ishara ya kichwa kuwa ashuke haraka na akimbie akajifiche kwenye msitu mkubwa uliokuwa kando ya ile barabara. Amanda akashikwa na hofu na nilipomuona hanielewi nikamwambia.
“Va te casher à la foret et toute chase qui va arriver nʼoser pas de sometrer”. Nenda kajifiche msituni na chochote kitakachotokea usithubutu kujitokeza. Nilimwambia Amanda huku nikimsisitiza hata hivyo sikumuona akionesha dalili zozote za kukubaliana na hoja yangu.
“Je nʼy vais pas moi même sans toi”. Siendi peke yangu bila wewe. Hatimaye Amanda aliniambia huku akitikisa kichwa chake kuonesha kukataa.
“Nʼaye pas peure mon amour, je serai bien”. Wala usihofu mpenzi nitakuwa salama. Nikamsisitiza Amanda huku nikihisi kuwa sikuwa na muda mrefu wa kuendelea na majadiliano yale. Haraka nikayapeleka macho yangu kutazama kule mbele kwenye lile gari na hapo nikauona mlango wa dereva ukifunguliwa taratibu kisha akashuka mwanaume mmoja aliyevaa suruali ya jeans na fulana mchinjo ya rangi nyeupe huku kichwani akiwa amevaa kofia ya pama na mkononi alikuwa ameshika bunduki aina ya Smg.
Sasa nilikuwa na hakika kuwa mambo hayakuwa shwari tena. Nilitamani sana nishuke kwenye lile gari pamoja na Amanda kisha tuanze kukimbia tukipotelea kwenye ule msitu mkubwa uliokuwa kando ya ile barabara. Hata hivyo haraka nikajikuta nikipingana na wazo lile pale nilipohisi kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kukamatwa endapo ningeamua kukimbia huku nikiwa nimeongozana na Amanda. Kwani nilikuwa nimemchukulia Amanda kama walivyokuwa wasichana wengine wa kawaida wasiokuwa na mazoezi yoyote ya mwili. Vilevile kutokana na mazingira yale sikuwa na silaha yoyote ya kujihami. Kwa kifupi nilipoteza kabisa matumaini ya kutoroka salama eneo lile. Hatimaye nikageuka haraka na kumshawishi Amanda kwa mara ya mwisho nikimnong’oneza na kumsihi.
“Sʼil vous plaît allez ma cherie”. Tafadhali nenda mpenzi. Sauti yangu ilikuwa ni yenye kusihi na kushawishi sana hali iliyompelekea Amanda anitazame kwa makini kama mtu aliyesikia habari mpya kabisa masikioni mwake. Kisha pasipo upinzani wowote nikamuona akiyachukua yale mabegi yetu mawili halafu haraka akausukuma ule mlango wa gari na kushuka chini akianza kukimbia kuelekea kwenye ule msitu uliokuwa kando ya ile barabara. Niliendelea kumtazama Amanda namna alivyokuwa akipotelea kwenye ule msitu hadi alipotoweka kabisa machoni mwangu. Nilipoyarudisha macho yangu kutazama nje ya gari nikagundua kuwa lile gari letu Land Rover 110 tayari lilikuwa limezingirwa na wanaume sita walioshika bunduki zao vyema mikononi.
Kuona vile ghafla moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu, koo likanikauka huku jasho jepesi la hofu likianza kunitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu. Kwa sekunde kadhaa nikajikuta nimeganda nyuma ya usukani wa gari kama sanamu huku akili yangu ikikataa kabisa kufanya kazi. Hatimaye nikayainua macho yangu na kuanza kuyatembeza taratibu nikitazama nje kupitia vioo vya madirishani.
Miongoni mwa wale watu sita, wanne haraka niliwakumbuka. Wawili kati yao walikuwa ni wale waliokuwa wamesimama nyuma ya lile gari wakitusimamisha wakati tulipokuwa tukiwapita kule msituni. Wale watu wengine wawili nikawakumbuka vizuri kuwa walikuwa ni wale waliotukimbilia baada ya kulisimamisha gari letu kule msituni. Wawili waliosalia sura zao zilikuwa ngeni kabisa kwangu ingawa sasa nilikuwa na hakika kuwa huwenda walikuwa wamejificha wakati wenzao walipokuwa wakijitahidi kutusimamisha kule msituni.
“Descendez vous tous!”. Wote shukeni chini!. Mara nikamsikia mmoja wao akifoka kwa sauti huku akilipigapiga lile bodi la gari kwa kitako cha bunduki yake mkononi. Sikuwa na namna ya kukaidi amri ile hivyo taratibu nikafungua mlango wa gari kwa unyonge na kushuka chini. Hata hivyo sikupiga hatua yoyote ya mjongeo mbali na eneo lile. Kitendo kile kikawapelekea wale watu wanne wanaume wanisogelee na kunizunguka. Kisha mmoja wao akawasha kurunzi yenye mwanga mkali na kunimulika usoni. Tukio lile likanitia hasira hata hivyo nilijionya kutofanya purukushani za aina yoyote eneo lile badala yake nikaipa akili yangu utulivu huku nikihisi hatari ilikuwa ikininyemelea kwa kasi ya risasi.
“Est-ce quʼil y a un problème?”. Kuna tatizo gani?. Nikawauliza wale watu huku kwa hila nikianza kuzikagua vizuri nyendo zao. Hata hivyo nilijikuta nikikabiliana na maumivu makali ya ngumi mbili kavu za mgongoni kutoka kwa mtu aliyekuwa nyuma yangu na kunifanya niheme juu juu kama niliyeamshwa na njozi mbaya kutoka usingizini. Wakati nikiugulia maumivu yale nikajikuta tena nikichapwa makofi mawili ya nguvu usoni yalionipelekea nione maluweluwe mbele yangu...ITEANDELEA
 
RIWAYA; UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU : 14
Mtunzi:Kelvin Mponda

“Ta femme est très belle”. Mke wako ni mrembo sana. Yule mtu akaongea kwa utulivu huku akitabasamu kisha akageuka na kumtazama Amanda usoni huku akipiga hatua taratibu kumsogelea pale aliposimama halafu nikamsikia akimuuliza Amanda.
“Où est de Iʼargent?”. Pesa ziko wapi?. Lile swali likampelekea Amanda ageuke kidogo na kunitazama hata hivyo sikuona tashwishwi yoyote usoni mwake. Kisha akamtazama tena yule mtu hatari kiongozi wa wale watekaji na kumwambia.
“Je les est caché à la brousse”. Nimezificha kule msituni. Amanda akaongea kwa utulivu huku akionekana kujawa na hofu.
“Tu es sure?”. Una uhakika?. Yule mtu akafoka huku akimtazama Amanda kwa makini usoni.
“Oui”. Ndiyo. Amanda akaitikia kwa woga kisha nikamuona yule mtu mtu akageuka na kuwatazama wale wapambe wake wawili.
“Toi et toi, allez avec lui pour prendre cet argent, et quʼil nʼose pas faire la rusé”. Wewe na wewe, nendeni naye mkachukue hizo pesa na asithubutu kufanya hila. Mara baada ya yule mtu kutoa amri wale wapambe wake wawili wakaanza kuongozana na Amanda wakielekea kule msituni na wakati wakiondoka Amanda akageuka tena na kunitazama na namna ya utazamaji wake nikahisi kuwa kulikuwa jambo fulani ambalo mimi sikulifahamu. Hata hivyo nikajipa subira huku sote tukiwatazama Amanda na wale watu namna walivyokuwa wakitokomea kwenye ule msitu wa jirani na ile barabara.
Wakati lile tukio likiendelea na kuonekana kuwachukua sana wale watekaji waliosalia pamoja na kiongozi wao. Mimi akili yangu ilikwishaanza kuchangamka huku nikiiona kuwa ile ndiyo ingekuwa nafasi pekee ya kujiokoa. Haraka nikayatembeza macho yangu kuwapeleleza vizuri wale watekaji. Mmoja alikuwa kiasi umbali wa hatua zisizopungua nne kutoka pale chini nilipokuwa nimekaa na mwenzake alikuwa mbali zaidi akiwa amesimama nyuma ya lile gari huku akivuta bangi. Yule kiongozi wao alikuwa hatua moja zaidi mbele yangu huku akiwa amejikita katika kutazama kule msituni walikopotelea Amanda na wale wapambe wake.
Sikuona kama kungekuwa na nafasi nyingine nzuri ya kucheza na akili za wale binadamu kama ile. Mikono yangu ikiwa imefungwa na kukazwa kikamilifu kwa nyuma kama mbawa za kuku, nikafanya tukio moja la kushangaza lakini hatari na makini. Nilikusanya nguvu za kutosha kisha kufumba na kufumbua nikajibetua na kuuzungusha chini mguu wangu wa kulia nikimchota mtama maridadi wenye ufundi wa hali ya juu yule kiongozi wa wale watekaji mbele yangu. Ambapo alishikwa na taharuki ya aina yake wakati alipokuwa akitupwa hewani na kuweweseka kama aliyepagawa na jinamizi baya ndotoni. Yule mtu alipotua chini akajikuta tayari ameenea vizuri kwenye kabari matata ya miguu yangu iliyomnyima nafasi ya kuhema vizuri huku macho yakiwa yamemtoka kwa mshangao. Tukio lile lilikuwa limepelekea ile bastola yake mkononi imponyoke na kuangukia kando yangu.
Mahesabu yangu yalikuwa yameenda vizuri kwani haraka nikaiokota ile bastola huku yule bwege akiendelea kufurukuta bila ya mafanikio. Wale wenzake kuona vile wakataharuki wakizielekezea bunduki zao kwangu. Risasi moja iliyofyatuliwa na mmoja wa wale watekaji nikawahi kufanya hila haraka nikijipindua na yule mateka wangu na kupelekea ile risasi ipekenye na kuvunja mfupa wa paja la yule kiongozi wao na hapo nikamsikia yule mtu akipiga yowe kali la maumivu na kulaani kitendo kile kwa matusi mzito mazito ya kila sampuli.
Nikafurahi na kuangua kicheko cha dhihaka nikimpongeza yule mtu kwa tabasamu. Tukio lile likampelekea yule aliyefyatua ile risasi ashikwe na kihoro kwa kumtindua risasi kiongozi wake kwa kutokuwa makini. Yule kiongozi wao ambaye sasa nilikuwa nimemtuliza vizuri kwa kabari yangu matata akaendelea kutukana matusi ya aina zote duniani huku akilalamika kwa maumivu makali ya jeraha la risasi na kulaumu kwa kitendo kile. Ilikuwa kama mchezo wa kuigiza jukwaani lakini chochote kilichokuwa kikifanyika pale lilikuwa ni tukio la kweli.
“Déposez vos armes, si non je vais mourir avec votre mari”. Tupeni silaha chini vinginevyo nitakufa na huyu mume wenu. Nikafoka kwa hasira nikiwaambia wale watekaji wawili na bunduki zao mkononi. Hata hivyo nikawaona ni kama wanaotaka kunipuuza hivyo kwa kuwahakikishia kuwa nilikuwa sifanyi mzaha nikajipinda mgongo ili kuiruhusu mikono yangu iliyoshika ile bastola ya yule bwege iweze kupata mhimili mzuri wa shabaha. kisha nikavuta kilimi cha ile bastola.
Lilikuwa shambulio makini kwani ile risasi ilipenya kwenye goti la yule kiongozi wao niliyemtuliza vizuri kwa kabari yangu na hapo akapiga yowe kali la maumivu huku akijitahidi kufurukuta bila mafanikio. Kwani bado nilikuwa nimemdhibiti vizuri kwa ile kabari yangu miguuni. Yule mateka wangu kuona vile akaanza kulalamika kwa kulia huku akifoka kuwaambia wale wapambe wake.
“Ecoutez vous les idiots, déposer vos armes au bien vous voulez que je meure?”. Msikilizeni nyinyi wapumbavu, tupeni silaha zenu chini au mnataka mimi nife?. Yule kiongozi wao akafoka kwa hasira akiwaambia wale wapambe wake huku akiwa bado nimemtuliza vizuri kwenye kabari yangu matata ya miguuni. Wale watekaji wengine kuona vile hawakuwa na pingamizi tena badala yake wakaweka bunduki zao chini huku wameshikwa na mshangao wasijue la kufanya. Kwa kweli nilifurahishwa sana na kitendo chao kile cha nidhamu na utii kwa kiongozi wao. Nilipohakikisha kuwa tayari walikuwa wameweka silaha zao chini nikawaambia.
“Bien!, alors rentez cing pas en arrière”. Vizuri!, haya rudini nyuma hatua tano. Wale watekaji kusikia vile wakasita kidogo wakitazamana lakini waliponiona nikijipinda tena na kuielekezea ile bastola mikononi mwangu kwa yule kiongozi wao wakaingiwa na hofu na kuanza kurudi nyuma kama nilivyowaamuru.
Wale watekaji waliporudi nyuma katika umbali wa kuridhisha nikageuka na kumwambia bosi wao kuwa anifungue zile kamba zilizokuwa zimefungwa na kukazwa mikononi mwangu kwa nyuma huku bado nikiwa nimemtundika kabari kwa miguu yangu. Yule mtu akasita kidogo lakini alipoona nikizidi kuibana miguu yangu na kuzidi kumpa wakati mgumu wa kuhema ikabidi aipitishe mikono yake nyuma yangu na kuanza kuifungua ile kamba taratibu huku macho yangu yakiwa makini kuwatazama wale wapambe wake pale waliposimama.
Zoezi la kuzifungua zile kamba likafanyika kwa muda mfupi sana huku nikihofia kukutwa na wale watu walioongozana na Amanda kwenda kule msituni ule muda mfupi uliopita Yule mtu alipomaliza kunifungua, mikono yangu ikarudiwa tena na uhai huku mishipa yake ikianza kuruhusu mjongeo mzuri wa damu kupita na kuitowesha ganzi mikononi mwangu. Hatimaye nikaifungua ile kabari na kusimama huku nikiinyooshanyoosha mikono yangu. Kitendo cha kuifungua ile kabari yangu ya miguuni kikampelekea yule kiongozi wao aanze kukohoa na kuhema ovyo huku akilishika koo lake kwa viganja vyake na macho yametoka pima.
Wale wapambe wake wakiwa bado wamesimama wasijue la kufanya nikaamua kuwashangaza. Kufumba na kufumbua nikageuka na kuwachapa risasi za kutosha. Wale watu wakapiga mayowe ya maumivu wakianguka chini na kutapatapa ovyo kabla ya kutulia huku kifo kikiwa tayari kimewachukua. Sasa nikageuka na kumtazama yule mtu aliyeonekana kuwa ndiye kiongozi wao ambaye sasa alikuwa akijitahidi kuinuka pale chini bila mafanikio kwani miguu yake yote miwili ilikuwa na majeraha ya zile risasi zangu.
Yule kiongozi wao kuona vile akaanza kusota taratibu akiondoka eneo lile huku akinitazama kwa woga. Hata hivyo tukio lile lilikuwa ni sawa na kutapatapa tu kwani yule mtu hakufika popote badala yake mimi nilikuwa nyuma yake nikimfuata taratibu pasipo kutia neno lolote. Jamaa akaendelea kusota na alipoona kuwa jitihada zile zisingemfikisha popote hatimaye ilifika sehemu akaamua kukaa huku damu nyingi ikiendelea kumtoka kwenye yale majeraha yake ya risasi. Kisha akaanza kuniomba msamaha akinisihi kuwa tusameheane na nisimdhuru. Sikusema neno lolote kwani hoja ile haikuwa katika mipango yangu.
Nilianza kwa kumchapa risasi moja ya goti lake la mguu wa kushoto kisha nikaendelea na goti la mguu wake wa kulia huku yule mtu akiendelea kupiga mayowe ya maumivu makali. Yule mtu akaendelea kulalamika sana akiniomba msamaha na kunisihi nimuache lakini ilikuwa kazi bure kwani niliunyoosha tena mkono wangu na kuielekeza tena ile bastola kwenye bega lake la kushoto kisha nikavuta kilimi cha ile bastola na kuuchangua vibaya mfupa wa bega lake. Yule mtu akapiga yowe na kubweka kama mbwa wakati maumivu yale makali ya risasi yalipokuwa yakisambaa haraka mwilini mwake.
Nilimkumbuka vizuri yule mtu namna alivyonitemea mate usoni kwa dharau na kunichapa makofi kadha wa kadha wakati nilipokuwa nimefungwa kamba mikononi ule muda mfupi uliopita. Kwa kweli sikuona sababu ya kumuacha mtu yule aendelee kuishi. Nilitaka afe kifo cha aibu na chenye maumivu makali ya risasi nilizokuwa nimepanga kumuadhibu nazo taratibu katika maeneo tofauti ya mwili wake ambayo yangekichelewesha kifo chake ili iwe kama fundisho kwa vitendo vile vya kiharamia vya utekaji wa magari vilivyokuwa vukiwanyima raha wasafiri wa barabara ile nyakati za usiku na mchana.
Nilikuwa katika harakati za kujiandaa kumchapa risasi nyingine ya bega la kulia yule kiongozi wa watekaji wakati niliposhtushwa na mlio wa risasi kutoka kwenye ule msitu wa jirani na barabara alipokuwa Amanda na wale watekaji wawili. Tukio lile la mfyatuko wa risasi likanishtua sana na kuniletea hisia mbaya zisizoelezeka. Hivyo nikajikuta nikiganda kama nyamafu huku shughuli za mwili wangu zikisimama kwa sekunde kadhaa. Masikio yangu yakasumbuliwa na ugeni wa kelele za mbawa za ndege ambao walikuwa wakijitahidi kuyakimbia matawi ya miti mirefu ya msitu ule baada ya ndege wale kushtushwa vibaya na ile sauti mbaya ya ule mlio wa risasi.
Nikiwa bado nimeyatega masikio yangu mara nikashtushwa tena na mlio mwingine wa risasi kutoka kwenye msitu ule na hapo hofu juu ya usalama wa Amanda ikazidi kuzimeza hisia zangu taratibu kama sindano ya sumu kali isambaavyo mwilini. Moyo wangu ukashikwa na mfadhaiko huku ukianza kwenda mbio isivyo kawaida. Miguu yangu nayo ikawa mizito kupiga hatua huku jasho jepesi likianza kunitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu. Hata hivyo hali ile haikuendelea zaidi kwani muda uleule mara nikahisi nikipigwa pigo moja la nguvu na kitu kizito nyuma ya kichwa change. Nikajitahidi kujitetea bila mafanikio badala yake nikajikuta nikikabiliana na maumivu makali yaliyoanza kusambaa taratibu mwilini yakitokea sehemu ya nyuma ya kichwa changu.
Nikaanza kuhisi kuwa hali yangu ilikuwa ikizidi kuwa mbaya kadiri sekunde zilivyokuwa zikiyoyoma. Kichwa changu nacho kikawa kizito mno kama niliyebebeshwa mzigo mzito kichwani nisioweza kuumudu. Nilitamani kufungua mdomo ili nipige yowe la kuomba msaada lakini nikajikuta nikiishilia kufumbua mdomo tu huku ile sauti ikigoma kabisa kutoka na hivyo kuishilia akilini mwangu tu. Macho yangu nayo yakaanza taratibu kupoteza nguvu ya kuona. Hatimaye shughuli mbalimbali za mwili wangu nazo nikazihisi kuwa zilikuwa mbioni kusitisha utendaji wake. Nikajiuliza ni kitu gani kilichokuwa kikinitokea lakini kabla sijapata jibu nikaanza kuhisi taratibu nilikuwa nikiishiwa nguvu mwilini na hatimaye kuanguka chini. Nilitamani sana kufumbua macho na kuona nini kilichokuwa kikinitokea eneo lile lakini hilo halikuwezekana kwani macho yangu yalikuwa yakizidi kuwa mazito sana na hatimaye nikaanguka chini kabisa kama bondia aliyetupiwa konde zito la kichwani na mpinzani wake.
Nikiwa pale chini sijielewi vizuri mara kwa mbali nikasikia mlio mwingine wa risasi hata hivyo safari hii nilihisi kuwa risasi ile ilikuwa imefyatuliwa umbali mfupi kutoka pale chini nilipokuwa nimeanguka. Nilijitahidi kusimama lakini sikuweza kwani taratibu fahamu zangu zilikuwa zikinitoka na kunifanya nijihisi mzembe sana kwa kusumbuliwa na maradhi nisiyoyafahamu. Hatimaye nikalala chini kabisa nikiwa sina uwezo wa kufanya chochote. Nikiwa nimelala pale chini huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha mara nikaanza teja kuhisi kuwa nilikuwa nikinyanyuliwa taratibu na kitu nisichokijua na ingawa nilijitahidi kuleta pingamizi la kila namna hata hivyo sikufanikiwa. Muda mfupi baada ya pale sikuweza tena kufahamu kilichoendelea.
_____
Niliyatega masikio yangu kwa makini huku nikijaribu kutafakari kuwa pale nilikuwa wapi. Sikusikia sauti ya kitu chochote na utulivu wa eneo lile ulikuwa ni wa hali ya juu kiasi kwamba nafsi yangu ilianza tena kuingiwa na hofu.
Nilikuwa nimerudiwa na fahamu, hisia zangu zilinitanabaisha hivyo huku nikikumbuka vizuri masaibu yote yaliyonitokea kule barabarani msituni wakati nilipopambana kikamilifu na wale watekaji. Sikuweza kufahamu nini kilichokuwa kimenitokea wakati macho yangu yalipokuwa yamejikita kutazama upande ule wa msitu alipokuwa Amanda na wale watekaji wawili baada ya milio ya risasi kusikika na kisha fahamu zangu kuchukuliwa na pigo zito la nyuma ya kichwa changu na baada ya pale sikufahamu kilichofuata. Hata hivyo nikapiga moyo konde na kumshukuru Mungu kwa kuniweka hai hadi wakati ule kwani niliamini kuwa mambo mengine ningekuja kuyafahamu baadaye.
Nilikuwa kitandani nimelala kwenye foronya laini na mto wa kuegemeza kichwa. Sikusikia upepo mkali, baridi wala yale manyunyu makubwa ya mvua zile za masika za kule msituni. Hivyo nilikuwa na kila hakika kuwa nilikuwa ndani ya nyumba. Nyumba ile ilikuwa ya nani na nilifikaje fikaje pale?. Nikajiuliza bila kupata majibu hali iliyonipelekea niyafumbue macho yangu taratibu na kuanza kuyatembeza huku na kule katika kutathmini vizuri mandhari yale.
Nilikuwa kwenye chumba kikubwa chenye kitanda kikubwa cha samadari, cha futi sita kwa sita, cha mbao ngumu ya mnin’ga, chenye droo mbili upande wa kushoto. Mbele ya kitanda kile kulikuwa na runinga pana ya inchi arobaini na mbili. Sistimu ya kisasa ya muziki aina ya Jvc, deki ndogo ya runinga yenye kutumia cd na flash disc, vyote vikiwa katika meza nzuri nyeusi ya kioo.
Upande wa kushoto wa kile chumba kulikuwa na kabati kubwa la kisasa la nguo hata hivyo kabati lile lilikuwa limefungwa. Pembeni ya kabati lile kulikuwa na kochi moja la sofa huku kando yake kukiwa na meza fupi ya mbao yenye simu ya mezani na kitabu kidogo chenye orodha ya majina ya watu na kampuni zilizokuwa zikitumia huduma ile ya simu ya mezani ama landline. Kwenye kona ya chumba kile upande wa kushoto kulikuwa na mlango. Nilipouchunguza mlango ule nikagundua kuwa ulikuwa ni wa kuelekea kwenye chumba kidogo cha maliwato na bafu.
Niliendelea kuyatembeza macho yangu taratibu nikitazama ukutani na hapo nikaona picha mbili kubwa nzuri za kuchorwa zikiwa zimetundikwa sehemu mbili tofauti. Moja ilikuwa ni ya mama wa kiafrika akiwa amembeba mtoto wake kwa mbeleko mgongoni na picha nyingine ilikuwa ya ua zuri la rangi nyekundu lililochorwa kwa ustadi wa hali ya juu. Picha zote mbili zilikuwa ndani ya fremu nzuri za kioo na kuzifanya zionekane vizuri katika zile kuta nyeupe na...ITAENDELEA
 
RIWAYA; UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU; 16
Mtunzi:Kelvin Mponda

... na Burundi. Mbali na kadi zile pia kulikuwa na ramani ndogo ya kukunja ya kijasusi niliyokuwa nimepewa na mratibu wangu wa safari za kijasusi Brigedia Jenerali Ibrahim Gambari. Muda mfupi kabla ya kuanza safari yangu jijini Dar es Salaam, Tanzania. Kwa kweli nilijikuta nikiishiwa nguvu pale nilipohisi kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa nyaraka zile muhimu za kijasusi kuwa tayari zingekuwa zimeonwa pale ambapo Amanda angeamua kufanya upekuzi kwenye begi langu wakati fahamu zikiwa zimenitoka.
Hata hivyo sikuwa na namna ya kufanya kwani chochote ambacho kingetokea nilipaswa kujipanga kukabiliana nacho ingawa uzima wa afya yangu kilikuwa ni kipaumbele cha kwanza. Hatimaye nikameza funda kubwa la mate nikijitahidi kuyatowesha mawazo yale kichwani mwangu huku zile dawa za kutuliza maumivu zikiendelea kufanya kazi mwilini.
_____
Sikuweza kufahamu ni wakati gani lepe hafifu la usingizi lilikuwa limefanikiwa kuziteka fikra zangu pale kitandani wakati nilipokuwa nikiendelea kuwaza hili na lile juu ya safari yangu ile ya kijasusi, pale niliposhtuka kutoka usingizini baada ya kitasa cha mlango wa kile chumba kusikika kikizungushwa taratibu na ule mlango kufunguliwa ukisukumwa kwa ndani.
Hisia zangu zikanitanabaisha kuwa yule alikuwa Amanda na alikuwa akija mle ndani kuniletea chakula. Hivyo nikageuka taratibu nikitabasamu na kuyapeleka macho yangu kuutazama ule mlango wa kile chumba huku nikitarajia kumuona Amanda akiwa na sinia kubwa lenye maakuli. Hata hivyo hilo halikutokea na badala yake mbele yangu nikajikuta nikikabiliana na mshtuko usioelezeka.
Ule mlango ulipofunguliwa Amanda akaingia mle ndani huku akiwa ameongozana na wanaume watatu, warefu na weusi wenye miili iliyojengeka imara. Huku wote wakiwa wamevaa sare za jeshi la wananchi wa Burundi na kofia za bereti vichwani mwao. Jamaa walikuwa wamepanda hewani kisawasawa na namna ya mikono ya gwanda zao ilivyokuwa imekunjwa niliweza kuiona misuli yao imara ya mikononi namna ilivyotuna kikamilifu kwa mazoezi ya nguvu yasiyokuwa na kikomo. Haraka nilipowachunguza nikagundua kuwa walikuwa ni makomandoo waliofuzu vizuri katika medani za masuala ya kijeshi na hapo koo langu likanikauka ghafla kwa hofu. Mapigo ya moyo wangu yakaanza kunienda mbio huku baridi nyepesi ikisafiri katika maungo yangu. Hali ile ikanipelekea nijihisi kuwa nimepona kabisa yale maradhi yangu na kuanza kujilaumu kuwa nilikuwa nikipoteza muda wangu pale kitandani.
Sasa nilikuwa na hakika kuwa Amanda alikuwa ameniuza tena kwa bei ya rejareja isiyokuwa na majuto yoyote katika nafsi yake na kwa kweli sikutaka haraka kuamini vile. Wale wanajeshi huku wakiwa wameongozana na Amanda wakazitupa hatua zao kwa tahadhari huku wakitembea kikakamavu katika namna iliyonipelekea niweze kuzisikia vizuri buti zao ngumu miguuni namna zilivyofanikiwa kwa kiasi kikubwa kuitetemesha sakafu ya kile chumba. Nilitamani nilitupe kando lile blanketi nililojifunika kisha nikurupuke na kuanza kutimua mbio. Lakini hilo halikuwezekana kwa kuwa muda haukuniruhusu kufanya vile na wale watu walikuwa ni kama tayari wameshanifikia pale kitandani nilipolala. Mbali na vile pale kitandani sikuwa na nguo hata moja ya kunisitiri, hali iliyonipelekea sasa niamini kuwa Amanda alikuwa amenifanyia hila kwa kunivua nguo ili hata zikitokea purukushani zozote nisiweze kukimbia loh!.
Wale wanajeshi walipofika pale kitandani nilipolala wakajigawa katika mtindo wa kukizunguka kile kitanda. Mmoja akaja na kusimama nyuma yangu, mwingine upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia. Amanda yeye akasimama mbele ya kile kitanda huku akinitazama kwa tabasamu la kinafiki lenye tafsiri ya ushindi. Nikiwa nimeshikwa na mshtuko wa hali ya juu, nikayatembeza macho yangu taratibu nikizikagua vizuri sura za wale watu kisha nikaweka kituo nikimtazama Amanda huku nikijitahidi kuumeza mshtuko niliokuwa nao moyoni. Amanda akanitazama na baada ya kitambo kifupi akavunja ukimya akiniambia.
“Jean ne tʼenfait pas cʼest sont mes amis, ils vont tˊaider”. Jean, hawa ni marafiki zangu, watakusaidia. Maelezo ya Amanda yenye kila namna ya chuki na usaliti yakanipelekea nitabasamu kidogo kujifariji na kuitowesha hasira iliyokuwa imeanza kuchemka moyoni mwangu na hapo nikamuona yule mwanajeshi wa upande wa kulia akisogea kidogo pale kitandani huku tabasamu la kifidhuli likijitokeza taratibu usoni mwake na mikono yake ameishikamanisha mbele yake. Kwa heshima akajitambulisha.
“Je mʼappelle Major Pascal Karibwami, je suis contant de te voir ici”. Naitwa Meja Pascal Karibwami, nafurahi sana kukuona hapa. Yule mwanajeshi akaongea kwa kujiamini huku akinipa heshima zote utasema mimi nilikuwa mkuu wake wa kazi. Alikuwa mwanaume mrefu na mweusi kama mjaruo. Hali iliyonipelekea niyaone vizuri macho na meno yake meupe wakati alipokuwa akitabasamu. Alipomaliza kujitambulisha mwenzake naye akasogea na kujitambulisha kwa nidhamu zote hali iliyonipelekea nishikwe na mduwao.
“Staff Surgent Anatole Nkunda”
Wakati yule mwanajeshi mwingine akijitambulisha nikageuka na kumtazama na sura yake ikanitia mashaka. Macho yake yalikuwa makubwa yenye uchovu lakini yanayoonya. Uso wake mrefu ulikuwa umetulia kama maji ya kisima na ijapokuwa alikuwa amevaa kofia ya bereti lakini kofia ile ya kiafande ilikuwa imetuama vizuri kwenye upara wake unaowaka na usiokuwa na unywele hata mmoja. Isipokuwa mishipa ya damu iliyotuna na kusambaa kichwani kama mizizi ya mmea wa mhindi. Yule afande akakaza sura akinitazama utasema alikuwa akivishwa medani ya heshima na amiri jeshi mkuu. Alipomaliza kijitambulisha yule askari mwenzake aliyekuwa nyuma yangu nikamsikia naye akijitambulisha. Hata hivyo sikuweza kumuona kutokana na namna nilivyokuwa nimelala pale kitandani isipokuwa sauti yake ilikuwa nzito mno.
“Corporal Adolphe Sahinguvu”
“Je ne, veux pas lʼaide de qui que ça sole”. Sihitaji msaada wa mtu yeyote. Nikaongea kwa jazba hata hivyo wale maafande wakaishia kuangua kicheko cha dharau ambacho kilinishangaza sana na kunitia hasira. Kicheko kile kilipokoma nikamsikia yule mwanajeshi mkubwa kwa cheo aliyejitambulisha kwangu kama Major Pascal Karibwami akiniuliza kwa utulivu.
“Comment ça va camarade?”. Vipi komredi unajisikiaje?.
“Je ne me sens pas bien, et je suis trés enfamé”. Sijisikii vizuri na nasikia njaa sana. Nikaongea kwa utulivu huku nikianza kuhisi usalama wangu ulikuwa ukielekea kudorora mbele ya uwepo wa watu wale. Ingawa taratibu za kijasusi zilikuwa zikinionya kutomuamini mtu yeyote katika mazingira yoyote lakini kwa kweli sikuwa nimetarajia kabisa kuwa Amanda angekuja kunisaliti tena katika mazingira kama yale. Hata hivyo nilijionya kuwa ukorofi wowote ambao ningeamua kuuleta katika mazingira yale usingenisaidia kitu kwani afya yangu bado ilikuwa dhaifu. Hivyo nikaishia kumeza funda kubwa la mate kuipoza hasira yangu kifuani.
“On ne tʼa pas encore donner à manger?”. Hujapewa chakula?. Major Pascal Karibwami akaniuliza kwa utulivu huku akitabasamu. Ingawa nilikuwa na hakika kuwa alikuwa akinidhihaki hata hivyo ilinibidi nimjibu.
“Oui”. Ndiyo.
“Ne tʼenfaite pas, nous allons te donner à manger”. Usijali sisi tutakupa chakula kingi na utashiba vizuri. Meja Pascal Karibwami akaniambia huku akiendelea kutabasamu na nilipomtazama usoni nikashtushwa na tabasamu lake la kinyama. Hali iliyonipelekea nizidi kushikwa na mashaka juu ya hatima yangu.
“Qui etes des qui?”. Nyinyi ni akina nani?. Nikawauliza wale watu huku nikifoka kwa kitendo kile cha kuchezewa akili yangu kama mtoto mdogo.
“Ne te derange pas, dans peu de temps tu vas nous connaître”. Ondoa shaka, muda siyo mrefu utatufahamu vizuri sisi ni akina nani. Meja Pascal Karibwami akaniambia huku akikenua meno yake na kunitazama kwa furaha. Alipoyatoa macho yake kwangu akayatembeza taratibu akimtazama Amanda pamoja na wale askari wenzake kisha akayarudisha tena pale kitandani nilipolala na kuniambia kwa sauti tulivu lakini yenye kumaanisha.
“Nous venons te prendre camarade”. Tumekuja kukuchukua komredi. Maelezo ya Meja Pascal Karibwami yakanipelekea nishikwe na mshangao huku nikishindwa kuelewa kuwa alikuwa amenuia nini. Hatimaye nikamuuliza huku nikiwa nimeanza kushikwa na wasiwasi juu ya kauli ile.
“Vous mʼamainer où?”. Mnanipeleka wapi?. Swali langu likawapelekea wale maafande wote mle ndani waangue kicheko kana kwamba nilikuwa nimeongea kitu cha kipuuzi na cha kuchekesha sana. Wakati wale watu wakiendelea kucheka nikiwa pale kitandani nikamtazama Amanda na kitendo cha kumuona akiungana na wale watu kunicheka kikanitia gadhabu. Kile kicheko chao kilipofika kikomo Meja Pascal Karibwami akaniambia kwa hadhari huku akinitazama.
“Nous tʼamainons à lʼhospitale parceque votre santé ne pas bonne”. Tunakupeleka hospitali kwani afya yako siyo nzuri.
“Qui vous a dit que je veux lʼaide dʼaller à lʼhospitale?”. Nani aliyewaambia kuwa nahitaji msaada wa kupelekwa hospitali?. Nikamuuliza kwa jazba yule mtu huku nimeshikwa na hasira kwa kudhihakiwa.
“Si tu es bien, pourquoi maintenant tu dors ice de dans comme une femme aceinte?”. Sasa kama wewe ni mzima kwanini unalala lala humu ndani kama mama mjamzito?. Meja Pascal Karibwami akaniuliza na kuwapelekea wale watu wote mle ndani waangue kicheko.
Kwa kweli nilishikwa na hasira hasa nilipokumbuka namna nilivyomuokoa Amanda kutoka katika ile mikono ya wale watekaji kule njiani msituni.
“Je ne veux pas lʼaide de qui que ça sole”. Sihitaji msaada wa mtu yoyote. Nikaongea kwa msisitizo na hapo nikamsikia yule mwanajeshi aliyekuwa nyuma yangu akiniambia kwa kufoka.
“Arreter de sʼopposer toi singe!”. Acha ubishi wewe tumbili!. Hali ile ikanipelekea nimuulize Amanda kwa hasira.
“Amanda, quʼest-ce quʼevolue ici de dans, je nʼarrive pas à te comprendre?”. Amanda, nini kinachoendelea humu ndani, mbona sikuelewi?.
“Sans doute tu es troublé Jean, qui est Amanda?”. Bila shaka umechanganyikiwa Jean, Amanda ndiyo nani?. Amanda akanimbia huku akiangua kicheko cha dhihaka.
“Cʼest toi!”. Si ni wewe!. Nikamwambia Amanda kwa mshangao huku nikijihisi kuchanganyikiwa kwa kutumbukia katika mkasa ule wa hatari. Meja Pascal Karibwami akaangua kicheko hafifu kabla ya kuniambia.
“Cʼest pour quoi je te dis que nous venons tʼamainer à lʼhopital, votre inteligence nʼest pas bonne, tu vois tu es entré de baptiser les gents le noms qui ne sont pas les leur!”. Ndiyo maana nikamwambia kuwa tumekuja kukuchukua tukupeleke hospitali. Akili yako siyo nzuri, huoni unavyowabatiza watu majina yasiyo yao?.
“Je ne vous comprend pas?”. Mbona siwaelewi?. Nikawauliza wale watu kwa hasira hata hivyo swali langu likawapelekea wale watu waangue tena kicheko wakinidhihaki. Kisha Meja Pascal Karibwami akaniambia kwa utulivu huku akitabasamu.
“Ne tʼenfait pas camarade, nous allons te faire comprendre”. Usihofu komredi, tutakuelewesha. Kisha nikamuona Meja Pascal Karibwami akiwafanyia ishara fulani ya kichwa wale askari wake hali iliyonipelekea nihisi jambo baya lilikuwa likielekeza kutekelezwa juu yangu.
Muda uleule lile blanketi nililokuwa nimefunikwa pale kitandani likaondoshwa kwa kasi na yule mwanajeshi aliyekuwa amesimama kushoto kwangu. Nilijitahidi kulizuia lakini kutokana na udhaifu wa mwili wangu sikufanikiwa. Hivyo nikajikuta nimebaki uchi kama nilivyozaliwa pale kitandani. Muda siyo mrefu mara nikamuona yule mwanajeshi mwenye cheo cha Koplo ambaye hapo awali alikuwa amejitambulisha kwangu kama Koplo Adolphe Sahinguvu, akizunguka kwenye kile kitanda na kunishika miguu. Kisha akanivuta chini kwa nguvu zake zote hali iliyonipelekea nitue pale chini sakafuni kwa matako na hivyo kupelekea maumivu makali yanisambae mwili mzima. Nilijitahidi kujitetea lakini ilikuwa kazi bure kwani mapigo ya mateke mgongoni na mabegani mwangu yakazidi kunipelekea niishiwe na nguvu kizunguzungu kikanishika na kunipelekea nijihisi kutaka kutapika.
Wale watu waliporidhika kuwa kile kipigo kilikuwa kimenilegeza kiasi cha kutosha, wakaamua kuniacha huku nikihema ovyo. Damu sasa ilikuwa ikinitoka puani, sehemu ya juu ya jicho langu la kulia ilikuwa imevimba na kuchanika huku ikivuja damu taratibu. Mdomo wangu nao ulikuwa umechanika sehemu yake ya chini na hivyo kunipelekea nihisi ladha nyepesi ya chumvi ya damu iliyokuwa ikivuja kwenye jeraha lile. Ikafikia hatua nikawa siwezi kuona vizuri mbele yangu. Nikiwa pale chini sijielewi vizuri baada ya kuleweshwa na ule mkong’oto wa nguvu kutoka kwa wale watu mara kwa shida nikamuona yule askari mwenye cheo cha chini kabisa kuliko wenzake akanisogelea pale nilipokuwa na kuanza kunifunga kamba mikononi na miguuni. Sikuweza kuleta upinzani wowote kutokana na hali yangu ya kiafya kuzidi kuzorota. Yule askari alipomaliza kunifunga zile kamba akaambiwa neno fulani la kirundi na yule Meja Pascal Karibwami ambalo muda mfupi baadaye nilifahamu vizuri maana ya neno lile kupitia vitendo. Kwani muda uleule yule mwanajeshi aliyenifunga zile kamba akanizoa pale chini sakafuni mzegamzega na kujitwisha begani huku nikiwa uchi wa mnyama bila nguo yoyote ya kujisitiri mwilini.
Huku nikiwa ninaning’inia begani kwa yule askari muda uleule safari ya kutoka mle ndani ikaanza huku yule askari aliyenibeba akitangulia mbele. Nyuma akafuatia Amanda na wale wanajeshi wengine. Hali yangu kiafya ilikuwa mbaya sana hata hivyo nilijitahidi kuituliza akili yangu na kuyachunguza vizuri mazingira yale.
Mara tu tulipotoka kwenye kile chumba tukajikuta kwenye korido pana kiasi iliyokuwa ikitazamana na milango mitatu upande wa kushoto ambayo kwa wakati ule yote ilikuwa imefungwa. Upande wa kulia wa ile korido kulikuwa na dirisha kubwa la kioo lililofunikwa kwa pazia refu na mwisho wa dirisha lile kulikuwa na mlango uliofungwa...ITAENDELEA
 
RIWAYA; UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU; 17
Mtunzi:Kelvin Mponda

...Tulipoipita ile korido tukaingia upande wa kushoto ambapo tuliifuata korido nyingine fupi na mwisho wa korido ile nikauona mlango mwingine ukiwa umefungwa. Hata hivyo hatukuufikia mlango ule na badala yake mbele kidogo tukachepuka na kuingia upande wa kulia sehemu kulipokuwa na mlango mwingine. Mara tulipoufikia ule mlango yule mwanajeshi aliyenibeba akaufungua na hapo tukajikuta tukitazamana na ngazi za mbao za kushukia sehemu ya chini zilizotengenezwa kwa ustadi. Wale watu wakiwa nyuma yetu mara tukaanza kuzishuka zile ngazi kwa makini tukielekea sehemu ya chini ya lile jengo na wakati tukishuka zile ngazi nikayatega masikio yangu vizuri na kushangazwa na ukimya wa eneo lile. Kwani kwa namna nyingine ni kama ni sisi tu peke yetu ndiyo tuliokuwa mle ndani ya lile jengo kutokana na utulivu wa kushangaza uliokuwa mle ndani.
Tukaendelea kushuka zile ngazi na ndani ya muda mfupi tukawa tumefika sehemu ya chini mwisho wa zile ngazi katika ukumbi mpana ulioonekana kutumika kama sebule kubwa ya kisasa yenye samani za kila aina. Kama seti mbili za makochi makubwa ya sofa, meza moja kubwa ya kulia chakula, rafu kubwa ya vitabu, kabati la vyombo ukutani na sistimu kubwa ya muziki. Nilipenda kuendelea kuipeleleza vizuri sebule ile kwa macho yangu hata hivyo sikupata nafasi kwani yule mwanajeshi aliyenibeba hakuonekana kujali kitu chochote na mwendo wake ulikuwa wa kijeshi huku nikining’inia begani mwake kama gunia la viazi.
Hatimaye tukakatisha katikati ya sebule ile na wakati tukifanya vile nikabahatika kuiona picha moja kubwa iliyokuwa imetundikwa ukutani katika kuta moja ya ile sebule. Ilikuwa ni picha ya kiongozi mmoja mkubwa wa jeshi la wananchi wa Burundi hata hivyo sikuweza kuliona jina la kiongozi yule kutokana na mwendo kasi wa yule bwege aliyenibeba. Ingawa nilifanikiwa kuinakili vizuri sura ya yule kiongozi wa kijeshi kwenye ile picha ukutani.
Mara tulipofika kwenye kona ya ile sebule nikagundua kuwa kulikuwa na mlango lakini haraka nikafahamu kuwa ule mlango ulikuwa haujafungwa kwani yule bwege aliyenibeba akakishika kitasa chake na kuufungua ule mlango pasipo pingamizi lolote. Ule mlango ulipofunguka tukawa tumetokeza kwenye korido nyingine lakini fupi na mwisho wa korido ile kulikuwa na dirisha refu na jembamba la kioo na upande wa kushoto kulikuwa na ngazi nyingine za kushuka chini zaidi ya lile jingo. Hali ile ikanipelekea nigundue kuwa ile nyumba ilikuwa ni jengo la ghorofa kutokana na zile ngazi ingawa sikuweza kufahamu lilikuwa ni jengo la ghorofa ngapi.
Tulipozifikia zile ngazi tukaanza kushuka chini tena na nilipochunguza eneo lile nikagundua kuwa zile zilikuwa ni ngazi za mwisho kabla ya kufika sehemu ya chini kabisa ya lile jengo.
Amanda na wale viongozi wawili wa kijeshi walikuwa hatua chache nyuma yetu na wote walikuwa makini kunichunguza. Baada ya muda mfupi hatimaye tukawa tumefika kwenye sehemu ya chini kabisa ya lile jengo tukitokezea kwenye korido pana kiasi lakini yenye kona nyingi za kuweza kufanikiwa kumchanganya mtu yoyote ambaye ingekuwa ni mara yake ya kwanza kufika eneo lile. Hata hivyo nilikuwa makini kuzihesabu kona za korido ile wakati tulipokuwa tukizipita moja baada ya nyingine. Zilikuwa kona nane zilizokuwa zikitazamana na milango ya vyumba vingi vilivyofungwa. Hatimaye korido ile ikatufikisha mbele ya mlango mkubwa wa mbao.
Tulipofika pale yule bwege aliyenibeba akaufungua ule mlango na baada ya ule mlango kufunguka nikaanza kuhisi nini kilichokuwa kikielekea kutokea. Wale watu walikuwa bila shaka wamepanga kunisafirisha mbali na eneo lile kwa sababu nisizozifahamu kwani hatua chache mbele ya mlango ule gari la kijeshi aina ya Tdi-Discover lilikuwa limeegeshwa huku milango yake ya nyuma ikiwa wazi.
Tulipofika nyuma ya lile gari yule mwanajeshi aliyenibeba akanibwaga nyuma ya lile gari kama gunia hali iliyonipelekea nitue vibaya na kulalamika kwa maumivu makali. Hata hivyo hakuna aliyeonekana kujali badala yake kule nyuma akapanda yule mwanajeshi aliyenibeba na yule mwenzake mwenye cheo cha Sajenti kisha wakafunga ile milango ya nyuma. Amanda na yule Meja Pascal Karibwami wao wakaingia sehemu ya mbele ya lile gari na muda mfupi uliofuata safari ikaanza.
Hisia zangu zikanitanabaisha kuwa nilikuwa nikipelekwa katika mazingira hatari zaidi yenye usiri wa hali ya juu na yasiyokuwa na haya na matendo yoyote ya kinyama. Hata hivyo sikuwa na namna yoyote ya kuweza kujitetea na vioo vya lile gari vilikuwa vimewekwa tinted nyeusi hivyo ilikuwa vigumu kwa mtu aliyekuwa ndani ya lile gari kuweza kuona nje vizuri. Lakini sikukata tamaa badala yake niligeuka taratibu wakati lile gari lilipokuwa likiondoka eneo lile na kwa kufanya vile nikafanikiwa kuiona kwa sehemu tu ile nyumba tuliyotoka.
Ilikuwa ni nyumba ya ghorofa nne iliyozungukwa kwa bustani nzuri ya maua na miti ya vivuli iliyopandwa katika utaratibu maalum lakini unaopendeza. Mbele ya lile jengo la ghorofa chini yake kulikuwa na gari moja bovu la kijeshi aina ya Tata pamoja na lile gari Land Rover 110 tulilosafiri nalo kutoka jijini Kigali nchini Rwanda. Nikaendelea kuyachunguza mandhari yale hata hivyo sikuweza kuona ziada nyingine na badala yake kadiri tulivyokuwa tukitokomea mbali na eneo lile ndivyo taswira ya lile jengo la ghorofa na mandhari yake ilivyokuwa ikitoweka machoni mwangu. Kutokana na miti mingi mikubwa na mirefu iliyokuwa imepakana na ile barabara hafifu ya magari iliyotawaliwa na mawe mengi madogomadogo na vichaka vya nyasi ndefu kando yake. Hatimaye ile taswira ya lile jengo la ghorofa na mandhari yake ikatoweka kabisa machoni mwangu.
Nikiwa bado nipo uchi huku nimefungwa mikono na miguu yangu mara baada ya taswira ya lile jengo la ghorofa na mandhari yake kutoweka machoni mwangu nikageuka kuwatazama wale wanajeshi niliokuwa nimekaa nao kule nyuma ya gari. Kwa kufanya vile nikakutana na macho yao makali yaliyonionya huku wakionekana kucheza vizuri na nyendo zangu. Sikuwasemesha neno lolote badala yake nikamtazama kila mmoja na kutabasamu kama mwendawazimu. Hata hivyo sikufanikiwa kuzilainisha nyuso zao kwani wale wanajeshi walionekana wapo kikazi zaidi huku sura zao wamezikaza kama ambao wapo kwenye gwaride la heshima. Sikuipenda hali ile ya ukimya kwa vile sikujua nini walichokuwa wakiniwazia vichwani mwao. Hivyo kwa kutaka kuilainisha mioyo yao nikawauliza.
“Où allons-nous?”. Tunaelekea wapi?. Nikawauliza wale wanajeshi huku nikiendelea kutabasamu hata hivyo hawakunijibu badala yake wakanitazama kama jiwe la barabarani. Sikuwasemesha tena badala yake nikageuka tena na kutazama nje kupitia dirishani.
Tulikuwa tukisafiri kwenye kipande cha barabara ya msituni yenye vichaka hafifu na miti mikubwa kando yake huku nikijaribu kuchunguza kama kungekuwa na nyumba yoyote ya jirani na eneo lile. Sikuona nyumba nyingine na lile eneo ni kama lilikuwa limejitenga. Hatimaye nikageuka na kutazama kule mbele ya gari na hapo nikamuona Amanda ndiye aliyekuwa akiendesha lile gari huku Meja Pascal Karibwami akiwa ameketi kwenye siti ya abiria kando yake. Hata hivyo hakuna aliyemsemesha mwenzake hali iliyopelekea mle ndani kutawaliwe na ukimya wa kushangaza utasema tulikuwa tukielekea kwenye msiba mkubwa uliotushtua sana.
Nikamchunguza Amanda na kugundua kuwa alikuwa dereva mzuri na makini sana kuliko vile nilivyokuwa nikimchukulia wakati ule tulipokuwa tukisafiri kutoka stendi ya mabasi ya Nyabugogo jijini Kigali nchini Rwanda.
Amanda alikuwa amenisaliti na kuniuza kwa bei nafuu kwa watu wale hatari bila kulifahamu kosa langu ingawa hadi kufikia pale nilianza kuamini kuwa Amanda naye alikuwa mwanajeshi wa jeshi la wananchi wa Burundi kwani vinginevyo sikuona mahusiano mengine kati ya wale watu hatari na Amanda. Mazingira ya mle ndani yakanieleza kuwa sikuwa sehemu salama tena na kwa vyovyote vile hisia za wale watu bila shaka zilikuwa zimejikita katika kuamini kuwa mimi ni jasusi kutokana na zile nyaraka muhimu zilizokuwa kwenye begi langu kwani niliamini kuwa Amanda angekuwa tayari amewaonesha wale watu. Hivyo kwa tafsiri ya haraka ni kuwa nilikuwa nikipelekwa sehemu fulani kufanyiwa mahojiano ya kulazimishwa nizungumze kuwa mimi ni nani na nilikuwa nimefika pale nchini Burundi kufanya nini. Kwa kweli niliingiwa na hofu, wasiwasi na mashaka pale nilipowaza kuwa nilikuwa nikielekea kukabiliana na kifo cha mateso makali. Hatimaye nikameza funda kubwa la mate kuikabili hofu ile.
Baada ya safari ndefu kidogo ile barabara ikachepuka upande kulia na kuanza kushuka mteremko mkali wenye barabara mbovu yenye mashimomashimo. Hata hivyo Amanda alijitahidi kwa kila hali kuumudu usukani wa lile gari na baada ya muda mfupi tukawa tumetokezea kwenye barabara ya lami. Tayari kulikuwa kumepambazuka na jua la asubuhi lilikuwa limeanza kuchomoza hali iliyonipelekea niweze kuona kwa unafuu zaidi nje ya lile gari.
Mara tu tulipoingia kwenye ile barabara ya lami tukashika uelekeo wa upande wa kushoto wa ile barabara tukisafiri katika mwendo wa kasi na wakati wote nilikuwa makini kuchunguza mandhari ya barabara ile. Kitu pekee kilichonishangaza ni kuwa wakati tukisafiri katika barabara ile njiani hatukupishana na gari hata moja. Baada ya mwendo mfupi wa safari yetu hatimaye tukaja kukutana na barabara nyingine ya lami ambayo ilikuwa kubwa zaidi ukifananisha na ile tuliyotoka. Mara tu tulipoingia kwenye barabara ile tukaanza kupishana na magari mengi kiasi lakini yakiwa katika mwendo kasi kana kwamba hapakuwa na kituo ama makazi ya watu karibu na eneo lile.
Upande wa kushoto wa barabara ile niliona mabango matatu makubwa ya matangazo. Bango la MTN, bango la benki ya wananchi wa Burundi na bango lingine la kampuni ya mawasiliano ya Airtel. Nikakumbuka kuwa kabla ya kufika pale Bujumbura nchini Burundi, Amanda alikuwa ameniambia kuwa angefikia mtaa wa Boulevard de 1er Novembre jijini Bujumbura. Hivyo nilijitahidi kwa kila namna kuchunguza kama kungekuwa na kiashiria chochote kuwa pale ni wapi. Hata hivyo lilikuwa jambo gumu kwani Amanda alikuwa akiendesha lile gari kwa kasi sana kiasi kwamba sikupata nafasi nzuri ya kufanya uchunguzi wangu kwa wepesi.
Njiani tulikutana na vijana wengi waliokuwa wakiimba nyimbo nyingi za kizalendo za nchi ya Burundi huku wakilisifu jeshi la wananchi wa Burundi kwa kufanya jaribio la mapinduzi ya kijeshi. Huku mikononi wakiwa wameshika matawi ya miti na kuyapunga hewani kwa furaha. Wale vijana walipokuwa wakiliona lile gari letu la kijeshi wakawa wakilishangilia kwa furaha huku wakilipisha bila upinzani wowote. Kupitia tukio lile nikajifunza kitu kuwa wananchi wa Burundi hususan vijana wengi walikuwa wameshachoshwa na utawala uliokuwa madarakani wa serikali ya nchi ile.
Baada ya muda mfupi wa safari yetu mara nikaanza kuhisi kuwa tulikuwa tukishika uelekeo wa katikati ya jiji la Bujumbura kwani kadiri tulivyokuwa tukiendelea na ile safari nikawa nikiyaona majengo marefu ya ghorofa na makazi ya watu yaliyopangwa vizuri kando ya barabara ile. Nilipochunguza vizuri kupitia dirishani nikawaona polisi wa Burundi wakiwa wametanda kila kona katika namna ya kukabiliana na maandamano yale huku wakitumia mabomu ya machozi, mbwa wakali wa polisi na magari yenye maji ya kuwasha. Hata hivyo wale polisi hawakutuwekea kizuizi cha namna yoyote badala yake wakawasalimia wale wanajeshi walioniteka na kuturuhusu tuendelee na safari yetu.
Zile dawa za kutuliza maumivu alizokuwa amenipa Amanda mapema alfajiri ile zilikuwa zimenisaidia kwa kiasi kikubwa. Kwani yale maumivu ya kichwa yalikuwa yamepungua sana na sasa nilianza kuhisi kuwa kichwa changu kilikuwa kimeanza kuwa chepesi ingawa njaa tumboni bado ilikuwa ikiniuma sana. Safari yetu bado iliendelea na kwa tathmini yangu dhidi ya mandhari ya barabara ile ni kuwa bado tulikuwa mbali na jiji la Bujumbura, kwani tulifika sehemu tukawa mbali kabisa na yale makazi ya watu. Ingawa bado niliweza kuyaona yale majengo marefu ya ghorofa yakiwa mbali kidogo na barabara ile.
Ile barabara kando yake ilikuwa imepakana na miti mizuri ya kivuli iliyopandwa katika utaratibu unaopendeza ingawa bado sikuweza kumuona mtu yeyote akitembea kwa miguu kando ya barabara ile. Ile barabara ilikuwa ngeni kabisa machoni mwangu. Labda ningeweza kuufahamu uelekeo ule endapo ningekuwa na ile ramani yangu ndogo ya kijasusi. Hivyo ilifika sehemu nikashindwa kabisa kuelewa kama tulikuwa tukielekea katikati ya jiji la Bujumbura au tulikuwa tukitokomea mbali na jiji lile.
Baada ya mwendo wa safari usiopungua muda wa nusu saa hatimaye tukaja kukutana na kizuizi cha mawe makubwa matano yaliyokuwa yamepangwa barabarani, katikati ya daraja kubwa la barabara ile ambapo mto mkubwa ulikuwa ukikatisha eneo lile. Haraka nikayapeleka macho yangu kutazama mawe yale makubwa mfano wa majabali huku nikikikumbuka kile kizuizi cha mawe cha kule msituni barabarani yalipotokea yale mauaji ya abiria wenzetu wakati tulipokuwa tukitoka jijini Kigali nchini Rwanda. Hata hivyo sikutarajia tukio kama lile kutokea katika mazingira kama yale.
Yale mawe yalikuwa yamepangwa katikati ya lile daraja hivyo tulipofika pale tukasimama na nilipochunguza upande wa kushoto wa ile barabara nikashtuka kuiona maiti moja ya mwanaume ikiwa imetelekezwa kando ya ile barabara. Huku maiti ile ikionekana kuwa na majeraha makubwa ya risasi kichwani. Hapakuwa na mtu yoyote eneo lile na kwa namna fulani uwepo wa ile maiti ya mtu eneo lile ulinitia mashaka. Niliendelea kulichunguza eneo lile kwa tahadhari na hapo nikaona magurudumu mengi ya magari yalikuwa yamewashwa moto na kutelekezwa ovyo eneo lile huku yakiendelea kuteketea taratibu na hivyo kufukiza wingu kubwa la moshi mweusi angani. Kulikuwa pia na vipande vya magogo makubwa ya miti pamoja na chupa nyingi zilizokuwa zimevunjwa eneo lile. Kwa tathmini ya haraka ni kuwa muda mfupi uliopita sehemu ile ilikuwa imeshuhudia rabsha za aina yake. Bila shaka mvua kubwa ilikuwa imenyesha usiku wa kuamkia siku ile kwani ule mto ulikuwa umejaa na maji yake yalikuwa yamevurugika kwa tope zito lililokokotwa kutoka sehemu mbalimbali za mto ule na hivyo kuyafanya maji yale yawe makendu na yanayosafari kwa kasi mno.
Amanda akawahi kusimamisha gari haraka umbali wa hatua chache kabla ya kile kizuizi cha yale mawe mbele yetu. Kisha yule mwanajeshi mwenye cheo cha Koplo ambaye hapo awali alikuwa amejitambulisha kwangu kwa jina la Koplo Adolphe Sahinguvu. Ambaye pia alikuwa miongoni mwa wale wanajeshi wawili waliokuwa nyuma ya lile gari wakinilinda. Haraka akafungua ule mlango wa nyuma wa lile gari na kushuka kisha akaanza kuelekea kule mbele kulipokuwa kumewekwa kizuizi cha yale mawe.
Hatua zake zilikuwa za hakika na nilipoendelea kumchunguza nikamuona akiingiza mkono nyuma ya kiuno chake na kuchomoa bastola ambapo aliikamata vyema mkononi. Koplo Adolphe Sahinguvu alipoyafikia yale mawe yaliyopangwa kule mbele kuzuia ile barabara akatazama tazama huku na kule kisha akaanza kuyaondoa yale mawe moja baada ya jingine akiyasogeza kando ya ile baabara na sote tuliokuwa ndani ya lile gari tukajikuta tukimtazama...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 18
Mtunzi:Kelvin Mponda

...Hata hivyo nikagundua kuwa yale mawe kutokana na ukubwa wake yalikuwa mazito mno. Hivyo kasi ya Koplo Adolphe Sahinguvu ya kuyatoa yale mawe pale barabarani ilikuwa ndogo mno huku akitumia nguvu nyingi. Ukimya ukaendelea kutawala mle ndani huku sote tukiendelea kumtazama Koplo Adolphe Sahinguvu namna alivyokuwa akikukurika na zoezi lile. Hata hivyo yule Koplo Adolphe Sahinguvu alipofanikiwa kuliondosha jiwe la pili nikamuona akihema ovyo huku akionekana kuanza kukata tama na zoezi lile. Muda mfupi baadaye nikamuona akisimama kwa uchovu huku amejishika kiunoni akihema ovyo. Baadaye taratibu nikamuona akigeuka na kutazama pale tulipoegesha lile gari na hapo nikamuona akinyoosha mkono na kuanza kuita kwa kiganja chake katika namna ya kuonesha kuwa alikuwa akiomba msaada kwa mwenzake.
Tukiwa mle ndani ya lile gari kila mtu akaoneka kuelewa vizuri maana ya wito ule. Tukio lile likampelekea yule mwanajeshi mwenye cheo cha Staff Surgent ambaye hapo awali alikuwa amejitambulisha kwangu kwa jina la Anatole Nkunda. Ambaye pia wakati ule ndiyo alikuwa amebakia peke yake kule nyuma akinilinda, ageuke haraka na kunitazama na hapo macho yake makubwa na mekundu yaliyohifadhi kumbukumbu ya kila unyama yakanionya. Muda uleule nikamuona Staff Surgent Anatole Nkunda akiichomoa bastola yake kutoka mafichoni katika gwanda lake la kijeshi kisha taratibu akauelekeza mdomo wa ile bastola yake katikati ya paji langu usoni huku ameikaza sura yake kama aliyepigwa ngumi ya mgongo. Halafu kwa sauti ya kunong’ona yenye chuki akaniambia.
“Ne pas déplacer, chaque étape a une seule balle”. Usithubutu kusogea, kila hatua yako moja ina risasi yake. Lilikuwa onyo la dhahiri lisilohitaji ufafanuzi. Staff Surgent Anatole Nkunda kweli alikuwa akimaanisha na kwa kutaka kunihakikishia juu ya onyo lake akanichapa kofi moja la usoni kisha ni nikamuona akiingiza tena mkono wake mfukoni na kuchukua mfuko mweusi wa nguo na kunivalisha kichwani. Nilijitahidi kwa kila namna kupingana na kitendo kile nikikiyumbisha yumbisha kichwa changu huku na kule katika namna ya kumpotezea malengo yule mtu. Lakini hata hivyo sikufanikiwa badala yake nikajikuta nikikabiliana na maumivu makali ya makofi mawili ya nguvu niliyozabwa shingoni na kunipelekea nihisi kutaka kutapika huku ule mfuko tayari ukiwa umevalishwa vizuri kichwani mwangu.
Mara baada ya yule askari kumaliza kunivisha ule mfuko muda uleule nikamsikia akishuka chini kule nyuma gari tulipokuwa na hapo nikajua kuwa alikuwa akienda kule mbele ya gari kumsaidia yule mwenzake kuyaondoa yale mawe yaliyowekwa barabarani. Tukio lile likaamsha hisia mpya kichwani mwangu na hapo wazo fulani likatumbukia katika fikra zangu na kunipa mzuka wa matumaini. Uzoefu katika harakati nyingi za kijasusi nilizowahi kushiriki au kuzishuhudia ni kuwa hukumu ya mtu yeyote anapokamatwa akifanya ujasusi katika nchi nyingine huwa ni kifo, tena kifo chenyewe huwa ni cha mateso makali na ya kinyama yenye kutaabisha mwili, nafsi na roho. Hivyo mara tu jasusi anapokamatwa tumaini lake pekee huwa ni katika kutoroka na hivyo kupelekea kila nafasi ya kutoroka inayojitokeza kuwa ni hatua ya muhimu kwake katika kuepukana na kifo cheye uchungu wa mateso makali.
Hivyo nilifahamu fika kuwa mwisho wa safari ile nilikuwa nikienda kukabiliana na kifo chenye uchungu na mateso makali baada ya mahojiano ya kina na kwa kweli sikupenda kwenda kufa kifo cha kondoo mpole huku nimeinamisha kichwa chini. Kwanza sikutaka kufa mapema huku kazi niliyotumwa nikiwa hata kuianza sijaianza kwani huo ndiyo ungekuwa upumbavu nambari moja. Suala la kifo kwangu haikuwa hoja ya kunishtua kwani ni dhahiri kuwa kila mtu atakufa hapa duniani apende au asipende. Lakini kufa huku nikiwa sijafanikiwa kutekeleza hata sehemu tu ya kile nilichokuwa nimetumwa kukitekeleza ilikuwa ni zaidi ya hoja kubwa katika maisha yangu. Kamwe sikuogopa kufa lakini kufa kifo cha mbinde au kufa kijerumani na tai shingoni kwangu ilikuwa ni heshima kubwa zaidi ya ile ya buti zangu za kijeshi na ile bendera kubwa ya taifa kulifunika jeneza langu wakati wa safari yangu ya mwisho kuelekea kaburini itakapofanyika hapa duniani.
Kwangu jambo muhimu lilikuwa ni kucheza na muda vizuri bila kuipuuza akili ya adui yangu. Hivyo wakati yule Staff Surgent Anatole Nkunda akishuka kwenye gari na kuniacha kule nyuma peke yangu sikutaka kupoteza muda. Kwa maana nyingine ni kuwa sikuona kama kungekuwa na nafasi nyingine nzuri kama ile katika kutimiza mpango wangu. Japokuwa nilikuwa nimefunikwa ule mfuko mweusi wa nguo lakini tayari taswira ya mandhari yale ilikuwa imenasa vizuri katika fikra zangu. Bila kupoteza muda nikaanza kuzifungua haraka zile kamba za mikononi mwangu kwa msaada wa meno. Lakini wakati nikiwa katikati ya harakati zile mara nikahisi kuwa miongoni mwa wale wanajeshi wawili walioenda kuyaondoa yale mawe barabarani kule mbele kwenye lile daraja mmoja wapo alikuwa akirudi ghafla kule nyuma ya gari nilipokuwa.
Huku hofu ikiwa imeanza kuniingia sikuona kama lingekuwa ni jambo la busara kuendelea kusubiri badala yake haraka nikajilaza chini pale nilipokuwa kwenye lile gari kisha taratibu nikaanza kujiviringisha nikiangukia nje chini ya lile gari. Bado nilikuwa na kumbukumbu nzuri juu ya mandhari yale niliyoipata kabla ya kuvalishwa ule mfuko mweusi. Hivyo nikatua chini ya lile gari pasipo kusababisha mshtuko wowote kisha kwa kasi ya gurudumu la gari haraka nikajiviringisha nikipotelea chini ya lile gari huku nikiwa uchi wa mnyama na mikono na miguu yangu bado ikiwa imefungwa kwa kamba na ule mfuko mweusi umevalisha kichwani mwangu. Nikiwa chini ya lile gari niliweza kuzikia vizuri hatua za yule mtu aliyekuwa akirudi kule nyuma ya lile gari.
Huku nikifahamu fika kuwa muda siyo mrefu siri yangu ya kutaka kutoroka ingefichuka baada ya yule mtu kufika kule nyuma ya gari na kunikosa sikutaka kupoteza muda. Kwa mujibu wa kumbukumbu kichwani mwangu ni kuwa ule mto uliokuwa ukikatisha chini ya lile daraja ulikuwa ukitokea upande wa mashariki ukisafiri kuelekea upande wa magharibi na kutoka pale nilipokuwa sikuwa mbali na kingo ya lile daraja la ule mto kwa upande ule wa magharibi. Hivyo sikuwa na muda wa kusibiri zaidi badala yake nikaanza tena kujiviringisha nikitokea chini ya lile gari kuelekea kwenye kingo moja ya lile daraja huku shughuli za mwili wangu bado zikiendeshwa kwa hisia kwani kichwani bado nilikuwa nimefunikwa na ule mfuko mweusi wa nguo.
Muda uleule mara nikasikia sauti mbaya ya risasi umbali mfupi kutoka pale nilipokuwa hata hivyo sikusita katika dhamira yangu badala yake nikaongeza kasi zaidi katika kujiviringisha na kuelekea kwenye kingo ya lile daraja. Risasi ya pili iliyofyatuliwa ikauparaza kidogo ule mfuko mweusi niliovalishwa kichwani kisha ikagonga chuma kimoja cha lile daraja na kusababisha ukulele mbaya masikioni mwangu. Risasi ya tatu huwenda ilikuwa na shabaha makini zaidi lakini mlengaji yule hakuwa makini kwani niliisikia ikichana anga bila matokeao yoyote nyuma yangu huku mimi nikiwa tayari nimeshaifikia kingo ya lile daraja na kujiachia kwenye yale maji mengi ya ule mto yaliyokuwa yakisafiri kwa papara za aina yake.
Kufumba na kufumbua nikawa nimemezwa na yale maji na kupotelea ndani ya ule mto. Nilikuwa nimefanya uamuzi wa ujasiri na wa hatari sana kwa kujitosa ndani ya ule mto hata hivyo sikuwa na namna kwani niliiona kuwa ile ndiyo ingekuwa namna pekee ya kujiokoa kutoka katika mikono hatari ya wale watu. Yale maji yakanisomba na kunizamisha chini kabisa ya ule mto sehemu ambayo japokuwa sikuwa na kipimo maalum lakini niliweza kuhisi kuwa nilikuwa kwenye kina cha zaidi ya futi kumi na tano kwenda chini. Yale maji yalikuwa na nguvu mno na kule chini ya ule mto kulikuwa na mawe hali ambayo ilikuwa hatari sana kwangu kwa vilevile mikono na miguu yangu bado ilikuwa imefungwa huku kichwa changu kimefunikwa kwa ule mfuko mweusi.
Nilijigonga begani kwenye jiwe moja huku yale maji yakinisomba na kunipigiza magongoni kwenye jiwe la pili na kufanikiwa kunichana upande wa kushoto wa mgongo wangu. Jiwe la tatu lenye ncha kali likanichana nyuma ya paja langu la mguu wa kushoto na kunisababishia jeraha lenye maumivu makali sana. Hata hivyo sikuwa na namna kwani yale maji yalikuwa yakinikokota ovyo katika namna yalivyotaka.
Huku nikiwa nimeanza kuingiwa na hofu ya kujeruhiwa vibaya na yale mawe hatari chini ya ule mto nilijitahidi kujitetea kwa kila namna lakini kitendo cha miguu na mikono yangu kuwa imefungwa kilininyima ushindi wa haraka. Hivyo nikawa nikiendelea kusombwa na yale maji huku mikono yangu nikiwa nimeitanguliza mbele katika namna ya kukipa ulinzi kichwa changu. Hata hivyo kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kusonga nikawa naanza kuhisi kuishiwa na pumzi ya kuzidi kutabaruku ndani ya yale maji mengi ya ule mto yenye kuzizima.
Woga wa kifo ukiwa umeanza kuniingia nikawa nikijitahidi kupapasa huku na kule kutafuta jiwe ambalo ningelishikilia kikamilifu ili yale maji ya ule mto yasiendelee kunisomba zaidi na kunipeleka kule mbele ya ule mto. Hata hivyo mahesabu yangu ni kama yalikuwa yamegonga mwamba kwani kule mbele kadiri ule mto ulivyokuwa ukizidi kutokomea ndiyo yale mawe yalivyokuwa yakizidi kuwa madogo zaidi kiasi kwamba hayakuwa na msaada wowote. Badala yake yale mawe yalikuwa yakizidi kumezwa na mchanga laini wa chini ya ule mto na hali ile ikanifanya nizidi kukata tamaa ya kutoka salama kwenye ule mto wenye maji mengi.
Nilikuwa nimesafirishwa umbali mrefu na yale maji ya ule mto huku pumzi ikiwa mbioni kuniishia pale nilipojikuta nimenasa kwenye kitu fulani nisichokijua. Nilipojaribu kupapasa vizuri nikagundua kuwa nilikuwa nimenasa kwenye gogo kubwa la mti lililokuwa likiteleza sana kutokana na kukaa kwa muda mrefu kwenye yale maji. Kwa kweli ilikuwa ni bahati ya kipekee ambayo kamwe haikuwa katika fikra zangu. Matawi yaliyopishana ya lile gogo yalikuwa yamekinasa kiwiliwili changu na hivyo kunizuia nisiendelee mbele. Hivyo nikaileta ile mikono yangu mdomoni na kuanza kuzifungua zile kamba mikononi mwangu na kwa kuwa zoezi lile nilikuwa nimelianza muda mfupi kabla ya kujitumbukiza katika ule mto zile kamba hazikunipa upinzani mkubwa.
Ndani ya muda mfupi nikawa nimemaliza kuzifungua zile kamba na kuiacha mikono yangu huru kisha haraka nikajivua ule mfuko mweusi wa nguo kichwani mwangu. Kitendo cha kujivua ule mfuko kikanifanya niweze kuhisi vizuri wingi wa yale maji ya ule mto. Yalikuwa maji mengi sana labda ningeweza kuufananisha ule mto na mito kama mto Kilombero wa mkoani Morogoro au mto Rufiji mkoani Pwani nchini Tanzania. Kwani kulikuwa na mito mingine midogomidogo iliyokuwa ikitiririsha maji yake katika mto ule.
Nikiwa bado nimenasa kwenye tawi la ule mti nikajipinda na kuanza kujifungua haraka zile kamba za miguuni na kwa kweli mapafu yangu yalikuwa yakihangaika ovyo kutafuta hewa. Nilikuwa nimetumia muda mwingi ndani ya yale maji na endapo ningeendelea kukaa zaidi mle ndani ya mto basi muda siyo mrefu ningeishiwa nguvu na hatimaye kupoteza maisha. Baada ya hangaika hangaika ya hapa na pale hatimaye nikafanikiwa kuzifungua zile kamba za miguuni na hivyo kujinasua kutoka kwenye lile tawi la mti. Yale maji ya mto yalikuwa na nguvu sana na kule mbele ule mto ulikuwa umezidi kutanuka na bila shaka kina chake cha maji pia kuongezeka.
Sikuwa na nguvu za kutosha za kuendelea kupambana zaidi na yale maji istoshe pumzi nayo ilikuwa mbioni kuniishia hivyo niliamua kulitumia lile gogo kama nyenzo muhimu ya kujiokoa. Nikayakamata vizuri matawi ya lile gogo nikiyatumia vizuri kujitafutia sehemu nzuri ya kulikumbatia lile gogo la ule mti. Muda mfupi uliofuata nikawa nimefanikiwa kupanda juu ya lile gogo na hapo nikalikumbatia vizuri na kuanza kusota nalo taratibu nikiitumia miguu na mikono yangu kujivuta. Ilikuwa ni kazi ngumu na ya hatari kwani lile gogo katika baadhi ya maeneo yake lilikuwa limekwishaanza kuoza na lilikuwa likiteleza sana. Lile gogo lilikuwa ni la mti mkubwa wa mvule uliokuwa kando ya ule mto. Mmomonyoko mkubwa wa udongo kando ya ule mto uliosababishwa na maji mengi ulikuwa umetia udhaifu mkubwa katika mizizi na shina la ule mti na hivyo kuupelekea ule mti kuangukia ndani ya ule mto huko siku za nyuma.
Niliendelea kusota na hatimaye nikatokezea kwenye sehemu ya lile gogo iliyokuwa juu ya yale maji ya ule mto. Kwa kweli nilishikwa na furaha isiyoelezeka huku nikiweka kituo kidogo sehemu ile, nikivuta hewa na kusambaza oksijeni ya kutosha kwenye mapafu yangu na kuhema ovyo kama shujaa aliyetoroka kifo. Hata hivyo sikutaka kujidanganya kuwa pale nilikuwa sehemu salama hasa nilipowakumbuka wale watu hatari niliyowatoroka kule darajani muda mfupi uliopita. Hivyo mara baada ya kuvuta hewa ya kutosha nikaendelea na safari yangu ya kuzidi kuukwea ule mti. Muda mfupi baadaye nikawa nimefanikiwa kutoka kabisa kwenye ule mto na kuifikia sehemu ya nchi kavu kando ya ule mto kwenye shina la ule mti. Kwa kweli nilijisikia furaha sana kwani japokuwa nilikuwa bado nikisikia maumivu makali kutokana na yale majeraha yaliyosababishwa na mawe hatari ya ule mto lakini sehemu kubwa ya maumivu yale ilikuwa imemezwa na kitendo kile cha kufanikiwa kuinusuru roho yangu.
Nikiwa pale juu ya shina la ule mti nikaanza kuyachunguza vizuri mandhari yale. Ule mto ulikuwa mkubwa na mpana na kwa sehemu ile ulikuwa umekatisha katikati ya msitu wenye miti mirefu na mikubwa. Ingawaje nilipochunguza vizuri kwa mbali niliweza kuyaona makazi ya watu hali iliyonitanabaisha kuwa eneo lile halikuwa mbali sana na mji mdogo. Nikageuka na kutazama kule nyuma ule mto ulipokuwa ukitokea huku nikitarajia kuliona lile daraja nilipowatorokea wale watu lakini sikuliona kwani matawi makubwa ya miti mirefu iliyokuwa kando ya ule mto iliukinga upeo wa macho yangu vilevile niligundua kuwa katika eneo fulani ule mto ulikuwa umekunja kona na kushika uelekeo wa pale nilipokuwa. Hivyo haraka nikagundua kuwa nilikuwa nimesafirishwa umbali mrefu na yale maji ya ule mto kutoka kwenye lile daraja ingawa sikuweza kufanya makadirio ya haraka ya umbali ule.
Baridi ilikuwa ikinipiga kwa vile sikuwa na nguo yoyote ya kunisitiri mwilini na yale majeraha ya mawe mgongoni na pajani yalikuwa yakiendelea kuvuja damu taratibu na kwa kweli hali ile sikuipenda lakini vilevile sikuwa na namna ya kukabiliana nayo. Niliitazama saa yangu ya kijasusi mkononi aina ya BBE-HD Spywatch isiyoweza kuingiza maji na yenye ujazo wa 8GB. Inayoweza kurekodi sauti na picha lakini vilevile yenye uwezo wa kunasa sauti ya tukio lolote lililopo umbali wa mita nane na pia inayotoa utambulisho wa hali joto ya mwili na mazingira na uelekeo wa pande za dunia. Dakika chache zilikuwa zimesalia kabla ya kutimia saa mbili asubuhi, majira ya saa ile yalionesha hivyo. Njaa ilikuwa ikinuuma ingawa nilijitahidi kwa kila hali kuipuuza. Jambo muhimu la kwanza nililokuwa nikilifikiria ni juu ya namna ya kupata nguo za kujisitiri mwilini na baada ya hapo mambo mengine yangefuatia.
Nikiwa pale juu ya shina la ule mti mawazo mengi yakawa yakipita kichwani mwangu na kabla sijaamua nifanye nini mara nikashtushwa na mtikisiko wa kichaka hafifu chenye nyasi ndefu kilichokuwa ng`ambo ya ule mto. Nikageuka na kukitazama kile kichaka kwa makini na hapo nikaona kiashiria cha mjengeo wa kiumbe hai. Sikutaka kusubiri...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU; 19
Mtunzi:Kelvin Mponda

...nikaona kiashiria cha mjengeo wa kiumbe hai. Sikutaka kusubiri zaidi hivyo haraka nikashuka kwenye shila la ule mti kisha kwa tahadhari nikanyata nikipotelea kwenye ule msitu uliopakana na ule mto kwa kasi ya mjusi pori. Huku nikifanya hivyo pasipo kutengeneza kiashiria chochote cha uwepo wangu eneo.
Mara baada ya kuingia kwenye ule msitu sikwenda mbali badala yake nikajibanza nyuma ya mti mmoja mkubwa uliokuwa kando ya ule mto ambao uliniwezesha kuona vizuri ng’ambo ya ule mto kwenye lile eneo ulipotokea ule mtikisiko wa kile kichaka. Muda mfupi uliofuata mara nikawaona watu wanne wakijitokeza kwenye kile kichaka kilichokuwa ng`ambo ya ule mto. Kuona vile nikasogea karibu ili niweze kuona vizuri watu wale ni akina nani. Taswira iliyonasa machoni mwangu ikapelekea moyo wangu upoteze utulivu kabisa.
Amanda alikuwa ameongozana na Meja Pascal Karibwami, Staff Surgent Anatole Nkunda na Koplo Adolphe Sahinguvu huku wote wakionekana katika nyuso zenye hasira na mikononi mwao wameshika bastola. Walipofika kando ya ule mto wakasimama huku wakionekana kushauriana jambo fulani. Nilipomtazama Meja Pascal Karibwani nikagundua kuwa uso wake ulikuwa umefura kwa hasira bila shaka kutokana na ule uzembe uliofanywa na askari wake kiasi cha kunipa mwanya mzuri wa kutoroka.
Wakiwa wamesimama ng’ambo ya ule mto mara nikawaona wakiyatazama yale maji ya ule mto kwa makini kama waliokuwa wakitarajia kuniona nikiibukia maeneo yale. Lakini maji ya ule mto yaliendelea kuwasuta huku yakisafiri taratibu kwa mzizimo wa aina yake hali iliyonipelekea nitabasamu kidogo. Kisha nikamuona Meja Pascal Karibwani akizungumza jambo fulani ambalo sikuweza kulisikia huku akinyoosha kidole chake kuwaelekeza wale askari wake katika lile gogo la ule mti uliotumbukia kwenye ule mto, ambalo dakika chache zilizopita nilikuwa nimekaa pale juu ya shina lake. Tukio lile likanipelekea nianze kushikwa na mashaka juu ya maamuzi ambayo yangefuatia baada ya pale.
Kulikuwa na majadiliano fulani ya kina kati ya Meja Pascal Karibwami na wale askari wake huku kila mmoja akionekana kutoa hoja yake kwa kina kwa kadiri alivyohisi kuwa huwenda ingekuwa na msaada mkubwa katika kunikamata tena. Nikiwa bado nimejibanza nyuma ya ule mti nikaendelea kuwatazama wale watu kwa utulivu huku nikisubiri hatima yao ingawa kwa namna moja au nyingine nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa mimi ndiye niliyekuwa ajenda yao kubwa katika maongezi yale. Baada ya muda mfupi mara nikahisi kuwa yale maongezi yao ni kama yalikuwa yamefika ukomo na sehemu iliyosalia ilikuwa ni ya utekelezaji wa mkakati.
Nikiwa bado nimejibanza nyuma ya ule mti kando ya ule mto mara ghafla nikawaona wale watu wakigeuka tena na kulitazama kwa makini gogo la ule mti mkubwa ulioangukia mle ndani ya ule mto. Huku Meja Pascal Karibwami akionekana kuwaelekeza wale askari wake juu ya jambo fulani ambalo liliwapelekea wote wageuke vizuri na kuutazama kwa makini ule msitu uliokuwa ng’ambo ya ule mto ambao mimi nilikuwa nimejibanza nyuma ya ule mti nikiwatazama kwa makini.
Haukupita muda mrefu mara nikamuona yule mwanajeshi kauzu matata aliyejitambulisha kwangu hapo awali kwa cheo cha Staff Surgent Anatole Nkunda akijirusha kujitosa kwenye ule mto na kuanza kuogelea taratibu akiuvuka ule mto kwa kulifuata lile gogo la ule mti uliotumbukia mtoni. Tukio lile haraka likanipelekea nianze kuhisi nini ambacho kilikuwa kinaelekea kutokea baada ya pale na kwa vile sikuwa muumini mzuri wa kitu kinachoitwa bahati sikutaka kuondelea kusubiri.
Taratibu nikauacha ule mti niliokuwa nimejibanza nyuma yake kisha kwa tahadhari ya hali ya juu nikaingia ndani zaidi ya ule msitu nikitokomea huku tayari nikiwa na wazo jipya kichwani mwangu. Wazo lililofufua tumaini na kunipa furaha isiyoelezeka kutoka katika sakafu imara ya moyo wangu. Nafsi yangu ikanitanabaisha kuwa ile ndiyo ingekuwa nafasi nzuri ya kujiokoa vizuri mbali na wale watu hatari katika mtindo nilioupa kauli mbiu ya perfect get away ya mshangao wa aina yake.
Mara nilipouacha ule mti na kutokomea kwenye ule msitu nikaanza kutimua mbio za kijeshi nikiupangua ule msitu kwa kasi ya ajabu kurudi kule kweye lile daraja nilipowatoroka wale watu kwa kujitosa mtoni huku nikiwa uchi wa mnyama kama nilivyozaliwa. Hata hivyo niligundua haraka kuwa ule msitu ulikuwa bado haujaathiriwa sana na shughuli za kibinadamu vinginevyo mtu yeyote ambaye ningekutana naye katika ule msitu nikiwa katika hali ile ya uchi asingesita kunipa mgongo na kutimua mbio huku akidhani kuwa mimi ni mwendawazimu kama siyo kiumbe kutoka sayari nyingine.
Ndani ya muda mfupi tu hatimaye nikawa nimelifikia tena lile daraja lililokuwa na kuzuizi cha yale mawe ambapo muda mfupi uliopita nilikuwa nimejitosa kwenye ule mto mkubwa uliokuwa ukitatisha chini yake wakati nilipokuwa nikiwatoroka wale watu hatari. Nilipolifikia lile daraja nikajibanza kwenye mti mmoja uliokuwa jirani na eneo lile huku nikichunguza kwa makini hali ya usalama ya eneo lile. Sikumuona mtu yeyote na lile gari la jeshi TDI-Discover lilikuwa bado limeegeshwa palepale kama nilivyokuwa nimeliacha wakati ule nilipotoroka. Kitu cha kushangaza zaidi ni kuwa hata yale mawe ya kizuizi yaliyokuwa kule mbele ya lile daraja bado yalikuwa hayajaondoshwa yote hali iliyonipelekea nifahamu kuwa lile tukio la kutoroka kwangu lilikuwa limewachanganya sana wale watu kiasi cha kutokushughulika tena na kile kizuizi cha yale mawe.
Nikiwa nimeridhishwa vizuri na usalama wa eneo lile taratibu nikayaacha yale maficho ya kwenye ule mti na kunyata kwa tahadhari nikienda kwenye lile gari. Muda mfupi uliofuata nikawa nimelifikia lile gari hivyo hali bado ilikuwa shwari. Nilipochungulia sehemu ya mbele ya lile gari nikaliona lile begi langu na kunifanya nijisikie furaha. Haraka nikafunga milango ya nyuma ya lile gari kisha nikaelekea kule mbele ambapo nilifungua mlango wa dereva na kuingia ndani. Nilipochunguza mle ndani haraka nikagundua kuwa funguo ya lile gari haikuwepo mahala pake. Hata hivyo hali ile haikunitatiza sana kwani haraka nikaibomoa ile swichi ya injini iliyokuwa chini ya usukani wa lile gari na kisha kutafuta nyaya mbili muhimu ambazo nilipozigusisha mara moja shoti ndogo ya umeme ikapiga na kuipelekea injini ya lile gari kuwaka. Sikutaka kupoteza muda hivyo haraka nikafanya jitihada za kuondoka eneo lile.
Bila kupoteza muda nikaligeuza lile gari kwa fujo na kushika uelekeo wa kurudi kule tulipotoka huku mwendo wangu ukiwa wa kasi isiyoelezeka. Macho yangu mara kwa mara yakawa yakitazama kwenye vioo vya ubavu wa lile gari hadi ile taswira ya madhari yale nyuma yangu ilipotokomea kabisa machoni mwangu. Baada ya mwendo mrefu wa safari yangu hatimaye nikajiridhisha kabisa kuwa hakukuwa na gari lolote lililokuwa likinifuatilia nyuma yangu. Hata hivyo sikutaka kujidanganya kuwa bado nilikuwa salama kwa kuendelea kulitumia lile gari la jeshi la wananchi wa Burundi. Hivyo wakati nikiendelea na safari yangu macho yangu yakawa makini kutazama huku na kule na kwa kufanya vile mara nikaiona barabara moja ya vumbi iliyokuwa ikichepukia upande wa kulia. Pasipo kujishauri nikapunguza mwendo na kuingia upande wa kulia nikiifuata barabara ile ya vumbi.
Ilikuwa ni barabara nyembamba ya gari iliyosongwa na nyasi hafifu na vichaka vya miti. Nilipochunguza vizuri nikagundua kuwa ile barabara ilikuwa ikielekea mashambani. Baada ya mwendo mfupi nikawa nimepata maegesho mazuri chini ya mti mkubwa wa mwembe uliozungukwa na vichaka hafifu vya miti na nyasi.
Yalikuwa ni mazingira tulivu na sehemu isiyokuwa na dalili zozote za uwepo wa watu. Nilipoegesha gari chini ya ule mwembe nikalichukua lile begi langu kutoka kwenye siti ya abiria upande wa kushoto ambapo alipokuwa ameketi Meja Pascal Karibwami pale awali. Ndani ya lile begi kulikuwa na nguo zangu chache hivyo haraka nikajifuta vizuri mwilini kwa kitambaa changu cha leso. Nilipomaliza nikachukua kisanduku kidogo cha huduma ya kwanza kilichokuwa ndani ya lile gari na nilipokifungua nikakuta vifaa vyote muhimu vya huduma ya kwanza kama; mikasi midogo, mabunda ya pamba safi, bandeji, vidonge vya kutuliza maumivu, spiriti, gv na vifaa vingine muhimu vya huduma ya kwanza.
Kupitia vifaa vile nikaanza kujitibu lile jeraha la kwenye paja langu la mguu wa kushoto lililotokana na yale mawe hatari ya kwenye ule mto niliyojitosa nikiwatoroka wale watu. Wakati nikijitibu nikawa ni kama niliyeamsha maumivu makali mwilini. Hata hivyo sikuwa na namna ya kuepukana na kadhia ile.
Hatimaye nikamaliza kujitibu lile jeraha vizuri na kujifunga bandeji imara iliyoukamata vyema msuli wangu wa paja. Nilipomaliza nikaanza kujitibu yale majeraha ya maongoni. Maumivu yalikuwa makali mno wakati nilipojimwagia dawa nyingi kwenye yale majeraha na kuyasafisha kwa pamba safi niliyoibana vyema kwa ncha ya makasi. Hatimaye nikamaliza zoezi lile na kuyafunga yale majeraha kwa bandeji. Kisha nikachukua vile vidongea vya kutuliza maumivu na kumeza tembe mbili. Kutoka katika lile begi langu nikachukuwa suruali ya jeans ya rangi ya samawati, fulana ya rangi ya kijivu na kofia nyeusi ambapo nilizivaa zile nguo. Zile buti zangu ngumu za ngozi zilikuwa kwenye mfuko mweusi wa nailoni uliokuwa pale mbele hivyo haraka nikazivaa zile buti miguuni.
Nilipojitazama kupitia kwenye kioo cha mbele kilichokuwa chini ya paa la lile gari nikaridhishwa vizuri na muonekana wangu. Nilipochunguza vizuri mle ndani ya lile bagi langu la mgongoni nikafurahi sana kukuta zile nyaraka zangu zote muhimu zikiwa salama pamoja na kile kiasi cha fedha nilichotokanacho jijini Kigali nchini Rwanda. Kwa kweli kichwa changu kilikuwa kimepata utulivu wa hali ya juu huku nikiwa bado siamini vizuri kama nilikuwa nimefanikiwa kukiponyoka kifo zile dakika chache zilizopita.
Hatimaye nikaanza kufanya upekuzi wa kina ndani ya lile gari katika namna ya kuchunguza kama ningebahatika kupata silaha yoyote ya kuanzia harakati zangu pale jijini Bujumbura nchini Burundi. Mungu mkubwa kwani baada ya upekuzi wa kina ndani ya lile gari kwenye droo moja iliyokuwa kwenye dashibodi ya lile gari nikaikuta bastola moja aina ya SP-21 Barak Silenced na magazini zake mbili zilizojaa risasi. Nikaichukua ile bastola na kuisunda kibindoni kisha nikaichukua ile ramani yangu ndogo ya kukunja ya kijasusi na kuitia mfukoni. Sasa nilikuwa tayari kuanza harakati na nilipojitazama tena kupitia kile kioo cha mle ndani cha chini ya paa la lile gari pale mbele nikagundua kuwa sura yangu ilikuwa imerejewa na uhai.
Sikuwa na sababu ya kuendelea kukaa zaidi eneo lile hivyo haraka nikawasha gari na kugeuza nikirudi kwenye ile barabara ya lami kwa kupitia tena kwenye ile barabara hafifu ya vumbi iliyosongwa na nyasi ndefu na vichaka vya hapa na pale. Baada ya muda mfupi tu nikawa nimeifikia tena ile barabara ya lami. Kabla ya kuingia kwenye ile barabara ya lami nikasimama kwanza nikichunguza hali ya usalama wa eneo lile. Sikumuona mtu yeyote eneo lile wala gari la doria hivyo mambo bado yalikuwa shwari. Hivyo bila kusubiri zaidi nikatia moto gari na kuingia kwenye ile barabara ya lami ambapo nilishika uelekeo wa upande wa kulia nikizidi kutokomea mbali na kule nilipotoka.
Nilipofika mbele kidogo nikaiacha ile barabara baada ya kuhisi kuwa mbele yake kulikuwa na dalili za uwezekano wa uwepo wa maandamano kama zilivyokuwa sehemu mbalimbali za jiji la Bujumbura. Hivyo nikaingia upande wa kushoto kuifuata barabara nyingine ya lami na nilipochunguza kupitia ile ramani yangu ndogo ya kijasusi nikagundua kuwa nilikuwa kwenye barabara iliyokuwa pembezoni mwa ufukwe wa Ziwa Tanganyika katika eneo lililofahamika kwa jina la Muha. Kwani wakati nikiendelea na safari yangu kwa mbali upande wa kushoto niliweza kuona mandhari nzuri ya Ziwa Tanganyika na hapo nikakumbuka kuwa hata ule mto niliyojitosa huwenda ulikuwa ukitapisha maji yake katika ziwa lile. Kwa kweli nikajikuta nikimshukuru tena Mungu kwa kuniepushia mbali na janga lile.
Nilichokuwa nimepanga kichwani mwangu kwa muda ule ilikuwa ni kufika katikati ya jiji la Bujumbura kwani nikiwa pale ningekuwa na nafasi nzuri ya kuanza harakati zangu. Ile barabara niliyoingia haikuwa na msongamano mkubwa kwani magari yalikuwa machache sana huku yakipita kwa ustaarabu. Kwa kweli niliomba nisikutane na kizuizi kingine chochote mbele yangu. Nikiwa naendelea na safari yangu katika baadhi ya maeneo nilikutana na vijana wengi waliojazana kwenye Toyota Pickup ambapo walinipungia mikono kwa furaha na hapo nikajua kuwa kitendo cha wale vijana kuliona lile gari la jeshi huwenda walikuwa wakidhani kuwa mimi ni mwanajeshi wa jeshi la Burundi. Kwa vile hadi wakati ule jaribio la mapinduzi ya kijeshi lilikuwa likiendelea nchini Burundi. Hata hivyo nikafanya hisani kwa kuwapungia mkono huku usoni nikiumba tabasamu jepesi hadi pale nilipopishana nao huku kila mmoja akiendelea na hamsini zake.
Sikupenda kuendelea na harakati zangu kwa kutumia lile gari la jeshi la wananchi wa Burundi kwa vile niliona kuwa lingekuwa ni jambo la hatari sana kwa usalama wangu. Hasa baada ya suala la amani nchini Burundi kuzidi kuwa tete. Hivyo wakati nikiendelea na safari yangu nikawa nikiyatembeza macho yangu huku na kule nikitafuta sehemu nzuri ambayo ningelitelekeza lile gari bila ya mtu yeyote nyuma yangu kufahamu kuwa ningekuwa nimeshika uelekeo upi baada ya pale. Niliipita hoteli ya kifahari ya La Bamba iliyokuwa upande wa kulia huku nikiendelea kuiona mandhari nzuri ya Ziwa Tanganyika kwa upande wa kushoto kwangu. Nikaendelea na safari yangu hadi pale nilipokutana na barabara ya Avenue du Cercle Nautique. Nilipoyafikia makutano yale nikapata wazo kuwa pale ndiyo ingekuwa sehemu nzuri ya kulitelekeza lile gari la jeshi kwa vile niliona kuwa ingekuwa vigumu kwa mtu yeyote kuweza kufahamu kuwa ningekuwa nimeshika uelekeo upi baada ya pale. Hivyo nilipofika pale nikaingia upande wa kuchoto wa ile barabara sehemu yenye kichaka hafifu cha kuelekea kwenye ufukwe wa Ziwa Tanganyika. Kisha nikaligueza lile gari na kulitelekeza eneo lile katika uelekeo wa lile gari kutazama kule nilipotoka. Nilipomaliza nikafunga vioo na milango ya lile gari na kushuka chini. Nilipolichunguza vizuri eneo lile sikumuona mtu yeyote na hali ile ikanipa faraja kubwa kuwa hila yangu ilikuwa bado haijashtukiwa.
Jua la asubuhi lilikuwa tayari limekwisha chomoza vizuri na miale hafifu ya jua lile iliponifikia mwilini ikazidi kuvipa uhai viungo vyangu. Begi langu dogo la shanta likiwa mgongoni nikaanza kutembea taratibu nikiliacha eneo lile na kuendelea na safari yangu nikiifuata ile barabara.
Kwa mujibu wa ile ramani yangu ndogo ya kukunja ya kijasusi ni kuwa kutoka pale kulikuwa na mwendo mrefu endapo ningeamua kutembea kwa miguu hadi kuifikia kona ya barabara ya Avenue du 13 Octobre. Iliyokuwa kando ya kituo cha mzungo wa maji wa Bujumbura ujulikanao kama Cercle Nautique de Bujumbura kwa upande wa kushoto katika ufukwe wa...ITAENDELEA
 
RIWAYA; UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU; 20
Mtunzi:Kelvin Mponda

...Ziwa Tanganyika. Ambapo mara baada ya kufika kwenye kona ya barabara ile kwangu ingelikuwa ni jambo rahisi kuweza kupata usafiri wa kunifikisha ninapotaka katikati ya jiji la Bujumbura.
Nikiwa naendelea kutembea kwa miguu kandokando ya barabara ile nikapishana na magari matatu. Magari mawili yakiwa ni madogo na ya kawaida na gari moja lilikuwa ni lori la jeshi la wananchi wa Burundi lililokuwa limewabeba wanajeshi wengi waliovaa sare zao na bunduki zao mikononi.
Hata hivyo kupitia kofia yangu ya kapero iliyonikinga vyema usoni nikajitahidi kwa kila hali kuuficha uso wangu wakati wale wanajeshi kwenye lile lori walipogeuka na kunitazama nilipokuwa nikipishana nao. Hata hivyo hawakusimama na hali ile ikawa salama kwangu. Hatimaye nikaifikia ile kona ya barabara ya Avenue du 13 Octobre huku nikiwa nimetembea kwa muda usiopungua nusu saa.
Nilipofika kwenye kona ya ile barabara nikajisikia faraja kidogo baada ya kukutana na pilika pilika hafifu za watu wa eneo lile. Kulikuwa na watu wengi kiasi watembea kwa miguu na hata idadi ya magari nayo ilikuwa imeongezeka barabarani. Hata hivyo hali ya utulivu katika barabara ile ilitosha kunitanabaisha kuwa hali ya usalama jijini Bujumbura nchini Bujumbura bado ilikuwa tete.
Mara nilipoingia kwenye ile kona barabara ya Avenue du 13 Octobre nikaiacha ile kona na kushika uelekeo wa mbele zaidi ambapo muda mfupi baadaye nilikuja kukutana na barabara ya Avenue de La Plage. Nikiwa naendelea kutembea kando ya barabara ile magari kadhaa yakawa yakinipita huku mara kwa mara nikijaribu kusimamisha teksi bila ya mafanikio. Jambo lile kwa kiasi fulani lilinishangaza sana kwani hali kama ile ilikuwa ni vigumu sana kuiona jijini Dar es Salaam ampao wasaka tonge hawalali usiku na mchana kutafuta mkate wa kila siku. Sehemu ambapo hata takataka za jiji tayari zimegeuka dili katika kujipatia kipato cha kujikimu kwa baadhi ya wakazi wake. Kwani zile teksi nilizojitahidi kuzisimamisha zilikuwa zikinipita bila kisimama ingawa ndani yake hazikuonekana kuwa na abiria.
Baada ya mwendo mrefu wa miguu hatimaye nikawa nimekifikia kituo kimoja kikubwa cha kujazia mafuta kilichokuwa upande wa kushoto wa ile barabara huku nyuma yake kikiwa kimepakana na ufukwe wa Ziwa Tanganyika. Nilipokifikia kile kituo cha kujazia mafuta nikawa nimeingiwa na tumaini baada ya kuziona teksi kadhaa zikiwa zimeegeshwa kando yake.
Mzee mmoja dereva wa teksi mwembamba mrefu na mwenye mvi nyingi kichwani akawahi kunisomea ramani mapema kabla ya wenzake wakati nilipokuwa nikikaribia maegesho yale ya taksi. Bila kupoteza muda mara tu nilipoifikia ile teksi ya yule mzee nikafungua mlango wa nyuma na kuingia ndani. Yule mzee dereva wa ile teksi kuona vile na yeye akafungua mlango wa dereva wa ile teksi yake na kuingia mle ndani huku akigeuka na kunitazama katika uso wa tabasamu la kibiashara. Nilipomchunguza yule mzee nikagundua kuwa umri wake ungekuwa ni kati ya miaka sitini na tano na sabini na mbili. Mtu ambaye asingeona umuhimu wowote wa kukimbia vita kwani kwa hesabu ya Mungu kwa umri wa miaka ya kuishi binadamu hapa duniani basi huwenda mzee yule alikuwa amebakiwa na miaka michache sana ya kuishi duaniani. Lakini bado alikuwa imara na mwenye siha njema na nilipomtazama usoni macho yake yakanitanabaisha kuwa yalikuwa yamehifadhi historia ndefu ya jiji la Bujumbura na vichochoro vyake.
“Ou vas-tu jeune homme?”. Unaelekea wapi kijana?. Yule mzee akaniuliza huku akinikata jicho la udadisi na hapo nikatabasamu tu mbele yake kabla ya kumwambia.
“Me prendre pour le centre-ville”. Nipeleke katikati ya jiji. Ombi langu likampelekea yule mzee anitazame kwa mshangao kidogo kisha kwa utulivu akaniambia.
“Il est pas très sûr dʾy aller maintenant”. Siyo salama sana kwenda katikati ya jiji kwa sasa.
“Je besoin dʾun endroit agréable pour le petit dejeuner”. Nahitaji sehemu nzuri kwa ajili ya kufungua kinywa. Nikamwambia yule mzee dereva wa teksi kwa utulivu hali iliyompelekea anitazame kwa utulivu kama mtu afikiriaye jambo fulani kisha akaniambia huku akitabasamu.
“Je vais vous prendre pour Havana Club. Il est un endroit agréable et sécuritaire”. Nitakupeleka Havana Club. Ni sehemu nzuri na yenye usalama.
“Oui!”. Sawa!. Nikamuitikia yule dereva wa teksi pasipo kufanya mapatano ya kiasi cha pesa ambacho angenitoza hadi sehemu ilipokuwa hiyo Havana Club.
Muda uleule ile teksi ikayaacha yale maegesho yake kando ya kile kituo cha kujazia mafuta na kuingia kwenye ile barabara ya Avenue de La Plage tukielekea mbele kuifuata Hotel Restaurant Tanganyika Lake View. Hata hivyo hatukuifikia hoteli ile kwani tulipofika mbele kidogo tukakunja kona upande wa kulia na kuanza kuifuata barabara ya Rue des Swahili. Ilikuwa ni barabara pana iliyoonekana kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara.
Mbele ya ile barabara kulikuwa na vijana wengi waliokuwa wakiandamana kuunga mkono jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililokuwa likiendelea nchini Burundi. Mapinduzi yenye lengo la kuingʾoa madarakani serikali ya rais Pierre Nkurunziza. Wale vijana walikuwa wakipambana kikamilifu na polisi wa kutuliza ghasia waliokuwa wakitumia mbwa, maji ya kuwasha na mabomu ya mzchozi kuwatawanya waandamanaji wale. Zoezi lile lilionekana kuwa gumu kwelikweli kwani wale vijana walikuwa wakijibu mashambuli kwa kurusha mawe na silaha nyinginezo za jadi.
Tuliendelea mbele kuifuata ile barabara na tulipoona kuwa zile vurugu kati ya wale vijana waandamanaji wa wale polisi wa kutuliza ghasia zikiongezeka yule dereva akaamua kuiacha ile barabara ya Rue des Swahili na kuingia upande wa kushoto akifuata barabaraya Rue Karuzi Halafu baada ya safari fupi hatimaye tukaja kuyafikia makutano ya barabara ya Avenue Ntahangwa na barabara ile ya Rue LʾLmbo. Tulipoyafikia yale makutano yule dereva wa teksi akaingia upande wa kulia akiifuata barabara ya Rue LʾLmbo. Hata hivyo hatukwenda mbali sana katika barabara ile kwani tulipofika mbele kidogo yule dereva akaiacha ile barabara na kuingia tena upande wa kushoto akiifuata barabara ya Rue du Tanganyika. Tulipoingia kwenye barabara ile nikakumbuka kugeuka nyuma na kutazama kama kungekuwa na gari lolote nyuma yetu likitufungia mkia. Sikuliona gari lolote hivyo hali ya usalama bado ilikuwa shwari.
Kama zilivyokuwa nchi nyingine nyingi masikini za dunia ya tatu za Afrika nchi ya Burundi nayo haikuwa tofauti kabisa wakati nilipoichunguza mitaa mingi ya jiji la Bujumbura na kuiona hali ya makazi yake. Sehemu kubwa ya jiji la Bujumbura ilikuwa na makazi duni ya watu wengi na machache ya daraja la kati.
Tulipofika kwenye pembe ya ile barabara ya Reu du Tanganyika tukaingia upande wa kulia tukiifuata barabara nyingine ya Reu des Pecheurs. Tulipoingia kwenye barabara ile haraka nikagundua kuwa tulikuwa tumeingia kwenye barabara iliyokuwa ikikatisha katikati ya makazi ya watu waliokuwa na afya ya kutosha kiuchumi kwani barabara ile ilikuwa imepakana na nyumba za kisasa zenye kuta na mageti makubwa ya uzio mbele yake na pia ilikuwa ni barabara yenye utulivu wa hali ya juu.
Baada ya safari ya kitambo kifupi hatimaye tukaja kukutana na barabara kubwa ya kisasa ya Boulevard du 1er Novembre kwa upande wa kushoto. Tulipoyafikia makutano yale ghafla akili yangu ikawa ni kama iliyopigwa shoti kali ya umeme hatari wenye nguvu nyingi na hivyo kuzipelekea shughuli za mwili wangu kusimama kwa ghafla kama niliyepigwa kumbo na ugonjwa hatari wa kiharusi.
Nilikuwa nimeyakumbuka vizuri maelezo ya Amanda wakati ule tulipokuwa tukisafiri wote kuja jijini Bujumbura wakati aliponiambia kuwa angefikia kwenye nyumba moja iliyokuwa kwenye mtaa wa Boulevard du 1er Novembre jijini Bujumbura. Kisha nikakumbuka kuwa mara tu niliporudiwa na fahamu kwenye ile nyumba ya ghorofa niliyotekwa na wale watu hatari wakishirikiana na Amanda kabla ya kuwatoroka. Nilikuwa nimemuuliza Amanda kuwa pale ni wapi na Amanda alikuwa amenieleza kuwa pale kwenye ile nyumba ya ghorofa tulikuwa kwenye mtaa wa Boulevard du 1er Novembre.
Kwa kweli nilijikuta nikiitazama barabara ya mtaa ule huku hisia zangu zikasafiri kilometa nyingi katika ufikirivu wangu kabla ya hisia zangu kuchotwa na jinamizi la matukio yote niliyoyashuhudia hadi kufikia pale. Hata hivyo kipo kitu kimoja cha ajabu kilichokuwa kimenishangaza. Mandhari ya barabara ile ya Boulevard du 1er Novembre hayakuelekea kufanana walau hata chembe na yale mazingira ya lile jumba la ghorofa lililojitenga kule msituni nilipotekwa na Amanda na wale watu wake hatari. Boulevard du 1er Novembre ilikuwa ni barabara pana ya kisasa yenye sifa zote sawa na zile barabara nyingine za kisasa za jiji la Bujumbura. Barabara ile ikipakana na makazi ya kisasa yenye nyumba nyingi za ghorofa na ofisi chache zenye nidhamu kiuchumi na nilipozidi kuichunguza sikuweza kuona dalili zozote za uwepo wa msitu au nyumba iliyojitenga kama ile niliyotekwa.
Nikiwa nimegeuka nyuma na kuendelea kushangaa mandhari yale dereva wa ile teksi akaingia upande wa kulia akiifuata ile barabara ya Boulevard du 1er Novembre huku upande wa kushoto tukiliacha jengo zuri la ghorofa la hoteli ya Old Presidential Palace na mbele kidogo mgahawa wa kisasa wa Snack La Fantasia. Tulipofika mbele kidogo ya ile barabara tukakutana na makutano mengine ya barabara Chaussée P.L.Rwagasore.
Tulipofika kwenye makutano yale tukauvuka ule mzunguko wa barabara na kuingia barabara ya Chaussée P.L.Rwagasore huku mwendo wetu wa gari ukizidi kuongezeka. Tulipishana na magari mengi katika barabara ile hata hivyo hatukufika mbali sana mara nikamuona yule dereva wa teksi akipunguza mwendo na mbele kidogo akaingia upande wa kushoto akiifuata barabara fupi ya Reu de la Victoire. Ilikuwa ni barabara pana lakini fupi iliyopakana na ofisi za kisasa na makazi yanayopendeza yenye utulivu.
Mwisho wa barabara ile tukaingia upande wa kulia kuifuata barabara kubwa ya Boulevard de IʾUprona. Ilikuwa ni barabara pana ya kisasa iliyopakana na migahawa ya kisasa na ofisi mbalimbali za mashirika yenye afya kiuchumi. Hatukusafiri kwenda mbali sana katika barabara ile mara nikamuona yule dereva wa teksi akipunguza mwendo na hatimaye kusimama mbele ya mgahawa mkubwa wa kisasa wenye kuta safi za vioo juu yake kukiwa na bango kubwa jeupe lenye maandishi ya rangi ya kahawa yakisomeka HAVANA CLUB. Chini ya bango lile kukiwa na maandishi madogo yanayosomeka More than just a venue.
Mara baada ya ile teksi kusimama mbele ya mgahawa ule kwa sekunde kadhaa nikayatembeza macho yangu kwa utulivu nikiutazama mgahawa ule na tukio lile likaipelekea akili yangu ishikwe na mduwao hafifu. HAVANA CLUB ulikuwa ni mgahawa wa kisasa wenye kila kionjo cha zama za leo. Nilifurahi sana kwani dereva wa ile teksi alikuwa amenifanyia uchaguzi mzuri kwa kunileta katika mgahawa ule.
Dereva wa ile teksi akayarudisha tena mawazo yangu mle ndani ya teksi pale alipovunja ukimya kwa kunidai pesa kwa ajili ya ile huduma ya usafiri. Alikuwa amenitoza pesa nyingi kwa kunipiga cha juu hata hivyo kwa kuwa nilikuwa na uzoefu mkubwa na madereva wa teksi wa mijini sikutaka kutia upinzani wowote badala yake nikafungua pochi yangu kutoka mfukoni na kutoa kiasi kile cha pesa na kumpa yule dereva huku nikitabasamu. Wakati yule dereva akizihesabu zile pesa mimi nikalichukua lile begi langu dogo la mgongoni kando yangu kisha nikafungua mlango wa nyuma wa ile teksi na kushuka.
Muda mfupi uliofuata ile teksi ikaondoka nyuma yangu ikitokomea mitaani na hivyo kunipa nafasi nzuri ya kuvaa begi langu dogo la shanta mgongoni huku nikipiga hatua zangu kwa utulivu kuelekea kwenye mlango wa mbele wa HAVANA CLUB. Hata hivyo wakati nikitembea kuelekea kwenye Club ile nikawa nikiyatembeza macho yangu kwa makini kupeleleza mandhari yale.
Kulikuwa na magari machache yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la maegesho ya magari la Club ile na nilipoyachunguza vizuri magari yale haraka nikagundua kuwa mengi yalikuwa ni magari ya watu wenye vipato vya kueleweka. Baadhi ya magari yale yalikuwa ni ya kubebea watilii mbugani na mengine yalikuwa ni ya maafisa wa umoja wa mataifa waliokuwa wakisimamia suala la amani nchini Burundi. Kupitia yale magari nikahisi kuwa huwenda watu wale walikuwa mle ndani ya mgahawa wakijipatia chakula, vinywaji au starehe yoyote iliyokuwa ikipatikana ndani ya Club ile.
Kulikuwa na watu wachache waliokuwa wamesimama nje ya Club ile wakiendelea na mazungumzo yao. Watu wale wakageuka kidogo kunitazama wakati nilipokuwa nikiufikia mlango wa mbele wa ile Club hata hivyo sikuwatilia maana badala yake nikaendelea na hamsini zangu.
Mara tu nilipoufikia ule mlango wa mbele wa HAVANA CLUB nikausukuma taratibu na kuingia ndani na hapo nikajikuta nikikabiliana na macho ya watu waliokuwa wameketi mle ndani wakiendelea na starehe zao. Watu wale haraka wakageuka kidogo na kunitazama na macho yao yaliponizoea wakageuka na kuendelea na hamsini zao kana kwamba mtu waliyekuwa wakimsubiri mle ndani hakuwa mimi na hali ile ikanifurahisha kwani sikupenda kuendelea kuzatamwa na kugeuka kivutio.
Hatimaye nikaurudisha ule mlango mkubwa nyumba yangu kisha taratibu nikaanza kupiga hatua zangu kwa utulivu nikikatisha katikati ya ukumbi mkubwa wa ile Club katika namna ya kutafuta sehemu nzuri ya kukaa na wakati nikitembea nikawa nikiyatembeza macho yangu taratibu kuwatazama watu waliokuwa mle ndani. Tathmini yangu ya haraka ikanieleza kuwa idadi kubwa ya watu waliokuwa mle ndani ya ile Club walikuwa ni wageni wa kutoka nje ya nchi ya Burundi na zaidi kabisa nje ya bara la Afrika. Kulikuwa na wazungu wengi huku wakiwa wameyaweka mabegi yao chini pembeni ya viti walimoketi. Wazungu wale walikuwa wakijipatia vinywaji na vyakula huku wakiendelea na maongezi yao na nilipowachunguza nikagundua kuwa wengi wao walikuwa ni watalii wa kutoka nchi za ulaya hususan Ufaransa na bara la Marekani kutokana na lugha walizokuwa wakizungumza. Waafrika wenzangu kama...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 21
Mtunzi:Kelvin Mponda

...Waafrika wenzangu kama mimi walikuwa wachache sana labda kutokana na gharama za juu za huduma zilizokuwa zikitolewa mle ndani.
HAVANA CLUB ilikuwa ni Club ya kisasa kabisa yenye kila kionjo cha daraja la kimataifa kama Snack-Bar Pizzeria, ukumbi mkubwa wenye meza nyingi za mchezo wa Pool table. Ukumbi mwingine mkubwa kwa ajili ya kujipatia vyakula vya kimataifa wenye meza ndefu za kisasa zilizozungukwa na viti vizuri vya sofa vyenye foronya laini pamoja na ukumbi mwingine mkubwa wenye jukwaa zuri linalotazamana na viti vingi vya kisasa kwa ajili ya kufanyia matamasha ya muziki na mikutano mbalimbali. Kila ukumbi ulikuwa imejitenga na hivyo kutengeneza mgawanyo mzuri wa starehe tofauti zenye utulivu zinaweza kufanyika kwa wakati mmoja.
Nilikuwa nimetokezea kwenye sehemu ya Bar ya ile Club na lile halikuwa lengo langu kwani njaa ilikuwa ikiniuma sana. Hivyo akili yangu yote ilikuwa imejikita kwenye kupata mlo wa nguvu na baada ya hapo mengine yote yangefuatia.
Mtu yeyote ambaye angekuwa akizifuatilia kwa karibu nyendo zangu mle ndani isingemuwia vigumu kunigundua kuwa nilikuwa mgeni wa mandhari yale na ile ndiyo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kabisa kufika pale kwa namna hatua zangu zilivyokuwa zikipwaya katika kufanya maamuzi ya haraka ya uelekeo wangu. Muziki laini ulikuwa ukisikika taratibu mle ndani na hivyo kuzikonga vizuri nyoyo za watu waliokuwa mle ndani.
Ule ukumbi ulikuwa mkubwa pengine wenye uwezo wa kumeza watu wasiopungua mia tano kwa wakati mmoja bila bugdha yoyote huku ukiwa na meza nyingi ndogo fupi na pana zilizozungukwa na makochi mazuri ya sofa laini. Katika baadhi ya meza zile watu walikuwa wameketi kwa utulivu huku wakijipatia vinywaji na japokuwa tayari ilikuwa imetimia saa nne asubuhi lakini taa nzuri zenye mwanga hafifu zilikuwa zikiendelea kuangaza mle ndani. Runinga pana zilizokuwa zimetundikwa ukutani mle ukumbini zilikuwa zimejikita katika kurusha taarifa mbalimbali za jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililofanyika jijini Bujumbura huku mara kwa mara picha za vijana waliokuwa barabarani wakiandamana kuunga mkono mapinduzi yale na kuishinikiza serikali iliyoko madarakani iachie ngazi zikirushwa.
Nilimaliza kukatisha katikati ya ukumbi ule na nilipokuwa mbioni kuifikia kaunta ya vinywaji upande wa kulia nikauona mlango mkubwa uliokuwa wazi lakini uliofunikwa kwa pazia zuri na jepesi. Juu ya mlango ule kulikuwa na kibao cheusi chenye maandishi meupe yakisomeka kwa lugha ya kifaransa Salle à manger yenye maana ya Dining Hall kwa lugha ya kiingereza ama ukumbi wa chakula kwa lugha ya kiswahili. Chini ya maandishi yale kulikuwa na maelezo mengine ya kifaransa yakisomeka Vous êtes les bienvenus yenye maana ya Wote mnakaribishwa sana.
Sikuona sababu ya kuuliza hivyo nikashika uelekeo wa upande wa kulia nikipotelea kwenye ule mlango. Mara tu niliposogeza pazia refu la ule mlango nikajikuta nikitazamana na ngazi chache za kuelekea sehemu ya chini ya lile jengo na hapo nikaanza kuzishuka zile ngazi taratibu. Nilipofika chini ya zile ngazi nikauona mshale mdogo mweupe uliochorwa ukutani ukielekeza upande wa kushoto. Nilipoufuata ule uelekeo mbele kidogo upande wa kulia nikaiona korido nyembamba inayotazamana na milango minne na upande wa kushoto kulikuwa na mlango mmoja uliokuwa wazi ukifanana na ule wa awali ukiwa umefunikwa kwa pazia jepesi. Juu ya mlango ule kulikuwa na kibao kingine cheusi chenye maandishi meupe kama yale ya awali na hapo nikajua kuwa ule mlango ndiyo uliokuwa wa kuelekea kwenye ukumbi wa chakula. Hivyo bila kupoteza muda nikashika uelekeo ule na kutokomea mle ndani.
Hatimaye nikajikuta nimetokezea kwenye ukumbi mkubwa wa kisasa wenye madirisha makubwa ya vioo yaliyofunikwa na mapazia safi marefu yaliyosogezwa kando kidogo kuruhusu mwanga wa jua kupenya kwa urahisi kutoka nje na kuangaza mle ndani. Utulivu wa mandhari yale ulikuwa wa hali ya juu uliomezwa na sauti ya muziki laini wa kubembeleza unaoweza kuacha kumbukumbu ya muda mrefu kwa mtu yoyote baada ya kuondoka eneo lile. Sauti ile tamu ya muziki ilikuwa ikirushwa kutoka katika spika zilizokuwa maeneo fulani kwenye kona za ukumbi ule.
Kulikuwa na wahudumu wa kike warembo waliokuwa wakihudumia wateja wachache waliokuwa mle ndani wameketi kwenye meza nzuri za mbao ya mti wa jacaranda na viti vifupi vyenye foronya laini. Nilipoyatembeza haraka macho yangu mle ndani nikagundua kuwa idadi ya watu wengi waliokuwa mle ndani walikuwa ni wazungu wapenzi na familia zao. Upande wa kulia wa ule ukumbi kulikuwa na mlango na dirisha dogo la jikoni na mle ndani nikawaona wapishi katika mavazi yao ya kazi.
Mara tu nilipoingia mle ndani watu wote wakageuka kunitazama kabla ya kuendelea na hamsini zao na hapo nikaanza kuzitupa hatua zangu kwa utulivu nikitafuta sehemu nzuri ya kuketi mle ndani. Kwa kufanya vile nikaiona meza moja iliyokuwa imejitenga kwenye kona ya ukumbi ule. Muda mfupi uliofuata nikawa nimeifikia meza ile ambapo nilivuta kiti na kuketi.
Nikiwa nimeketi kwenye ile meza nikasogeza pazia na kupitia ukati msafi wa kioo cha dirishani nikaweza kuyaona mandhari tulivu ya kuvutia nje ya ukumbi ule. Kulikuwa na nyasi nzuri za rangi ya kijani kibichi zilizopakana na maua ya rangi tofauti ya kuvutia na nyasi zile zilikuwa zimepandwa kuzunguka mabwawa matatu ya kuogelea kando yake kukiwa na viti vya kupumzikia kwa waogeleaji vyenye miavuli mizuri ya kujikinga na miale ya jua. Katika viti vile baadhi ya wazungu walikuwa wameketi na wengine wakiogelea huku wote wakiwa katika mavazi ya kuogelea na bikini nzuri zenye mvuto wa aina yake. Kando ya mabwawa yale kulikuwa na bustani nzuri ya miti yenye viti visivyohamishika katika mandhari tulivu.
Msichana mrembo mhudumu wa ukumbi ule wa chakula akayarudisha mawazo yangu mle ndani wakati alipokuja na kusimama mbele ya ile meza niliyoketi huku tabasamu la kibiashara likivinjari usoni pake. Nilipoyainua macho yangu kumtazama mhudumu yule kwa sekunde kadhaa macho yangu yakajikuta yakipumbazwa na uzuri wake.
Alikuwa msichana mzuri na mrembo sana ambaye kamwe sikuwahi kumuona msichana wa namna ile katika pitapita zangu. Japokuwa alikuwa amevaa sare za kazi lakini bado uzuri wake haukuchujuka hata chembe. Nywele zake nyeusi za kibantu alikuwa amezikata vizuri katika mtindo wa Lowcut na hivyo kumpelekea aonekane mzuri wa asili. Macho yake makubwa na meupe yaliyozungukwa na kope ndefu na nyeusi, pua yake ndefu ya kihabeshi, mdomo wake wa kike wenye kingo pana kiasi na vishimo vidogo mashavuni vinavyochomoza haraka kila anapotabasamu vikazidi kuzisulubu vibaya hisia zangu.
Kidani cha asili chenye herufi V kilikuwa kimenasa vyema kwenye shingo yake ndefu na kupotelea katikati ya kichochoro hafifu kilichofanyika katikati ya matiti yake makubwa kiasi yenye chuchu imara zilizotuna na kuisumbua kidogo blauzi yake. Mkono wake wa kushoto alikuwa amevaa saa nzuri ndogo ya kike iliyotengenezwa kwa namna ya kupendeza na hivyo kuongeza ziada nyingine katika uzuri wake. Sketi yake nyeusi fupi iliyoishia juu ya magoti ilikuwa imenasa vyema kwenye kiuno chake chembamba kilichoshikilia mzigo mkubwa wa makalio yake imara yaliyoimarisha vizuri minofu ya mapaja yake yaliyotuna kama chura na kumpelekea aonekane kama aliyeficha vipande vya mikate mfukoni. Niseme pia rangi yake ng’avu ya maji ya kunde ilikuwa ni kigezo kingine kilichotumika kumruhusu auteke moyo wangu bila pingamizi lolote na hivyo kunifanya nisahau hata kile kilichonifikisha mle ndani.
“Bien venu frère, je ne sais pas quʾest-ce que tu veux quʾon tʾapporte?”. Karibu kaka sijui ungependa kuagiza nini?. Yule mhudumu akaniuliza kwa sauti tulivu iliyotuama vyema kwenye sakafu ya mtima wangu na hivyo kunipelekea kwa sekunde kadhaa nikose neno la kuongea kutokana na kupumbazika na uzuri wake. Baada ya kitambo kifupi hatimaye nikavunja ukimya huku nikitabasamu.
“Je demande dʾabord la soupe de poisson à la rouille que je chauffe un peu la vendre, et après je vais comander un forte repas”. Naomba kwanza uniletee supu ya samaki nipashe tumbo joto halafu baadaye mlo wa nguvu. Nikamwambia yule mhudumu baada ya kusoma orodha ya vyakula iliyokuwa juu ya ile meza nikiipitia kwa utulivu.
“Il y a autre chose?”. Kuna kingine chochote?. Yule msichana mrembo mhudumu akaniuliza na baada ya kufikiri kidogo na kuitazama tena ile orodha ya vyakula pale mezani nikavunja ukimya.
“Amaine moi du vin de la Navette de Marseille”. Naomba uniletee na mvinyo mwepesi wa Navette de Marseille. Yule mhudumu akaitikia kwa kutikisa kichwa chake huku akitabasamu na wakati alipokuwa akijiandaa kuondoka eneo lile nikakumbuka kumuuliza kitu, lengo langu likiwa ni kutaka kuisikia sauti yake nyororo ya kumtoa nyoka pangoni.
“Ҫa va prendre combien de tempʾs?”. Itachukua muda gani?.
“Juste maintenant”. Sasa hivi. Yule mhudumu akaniambia huku akitabasamu.
“Jai faim, je serais contant si tu le fait rapidement”. Nina njaa sana hivyo nitashukuru ukinifanyia haraka. Nikamwambia yule mhudumu huku nikimkonyeza kidogo kwa jicho langu la kushoto na kumpelekea azidi kutabasamu.
“Ne tʾenfait pas”. Ondoa shaka. Yule mhudumu akaniambia kisha akageuka na kuanza taratibu kuondoka eneo lile na wakati akitembea akili yangu ikajikuta ikizidi kupumbazika na mtikisiko maridhawa wa mzigo wa makalio yake chakaramu.
Nikaendelea kumtazama msichana yule kwa utulivu hadi pale alipotokomea kwenye kaunta ya jikoni ya ukumbi ule wa maakuli huku nikijisikia faraja ya kipekee kabla ya mawazo yangu kuhamia kwenye tafakuri nyingine.
Sasa nilikuwa nimeingia rasmi jijini Bujumbura nchini Burundi tayari kuanza kazi niliyotumwa na idara yangu ya ujasusi jijini Dar es Salaam. Nikiwa bado nimeketi kwenye ile kona nikaanza kukumbuka misukosuko yote niliyopitia tangu nilipoanza safari yangu kutokea jijini Kigali nchini Rwanda jioni ya jana. Kisha nikakumbuka namna nilivyomuokoa Amanda na hatimaye kupambana kikamilifu na wale watekaji wa msituni kule njiani. Kwa kweli sikuwa nimetarajia kabisa kuwa Amanda angekuja kunisaliti pamoja na fadhila zote zile nilizomfanyia. Hata hivyo ule haukuwa wakati wa kumlaumu Amanda badala yake niliona kuwa zilipaswa kujilaumu mwenyewe kwa kitendo cha kumwamini sana mtu nisiyemfahamu vizuri.
Baada ya muda mfupi kupita mara nikamuona yule dada mhudumu akirudi pale nilipoketi huku mikononi akiwa amebeba sinia kubwa lenye staftahi huku lile tabasamu lake la kibiashara usoni likikataa kabisa kwenda likizo. Yule mhudumu alipofika pale kwenye meza yangu akainama kwa utulivu akilitua lile sinia juu ya ile meza mbele yangu na kitendo kile cha kuinama kidogo kikapelekea kile kidani chake kilichojificha katikati ya mfereji wa matiti yake kitoke mafichoni na kuningʾinia kifuani mwake na hivyo kunipelekea niweze kukiona vizuri.
Kilikuwa kidani kizuri cha madini yanayongʾara sana nisiyoyafahamu chenye herufi V. Hata hivyo msichana yule mhudumu hakuonekana kupendezwa na tukio lile la kuponyokwa kwa kidani chake kile kilichonipa nafasi nzuri ya kuyachungulia matiti yake yenye mvuto wa kipekee. Hivyo haraka akakichukua kile kidani na kukirudishia katikati ya matiti yake kisha akaitengeneza vizuri blauzi yake huku akiona aibu kidogo mbele yangu.
Nikamtazama usoni mrembo yule huku nikitabasamu tukio lile likampelekea atabasamu kidogo kwa aibu huku akiyakwepesha macho yake pembeni yasikutane na yangu na tabia yake ile ya heshima ikazidi kupeleka nuru njema moyoni mwangu. Yule dada mhudumu hatimaye akaanza kuitoa ile sahani ya supu na glasi ya mvinyo mwepesi kutoka kwenye lile sinia na kuviweka mbele yangu huku akikwepa kunitazama usoni.
“Do you speak Swahili?”. Nikamuuliza yule mhudumu wakati alipokuwa akiendelea na kazi yake pale mezani. Japokuwa Burundi ni nchi inayotumia lugha ya kifaransa kama lugha rasmi ya ofisini lakini kiswahili haikuwa lugha ngeni katika nchi zilizo katika ukanda wa maziwa makuu na vilevile katika sehemu kama pale HAVANA CLUB ambapo wageni mbalimbali wa kimataifa walikuwa wakifika. Hivyo lisingekuwa jambo la kustaajabisha kwa wafanyakazi wa mle ndani kujua kuzungumza angalau lugha mbili au tatu za kimataifa katika namna ya kurahisisha utoaji wao wa huduma hivyo swali langu bado lilikuwa na mantiki. Swali langu likampelekea yule msichana anitazame kwa bashasha zote huku akitabasamu na hapo nikajua kuwa huwenda lile swali lilikuwa limemfurahisha sana.
“Unataka nini?”. Hatimaye yule mhudumu akaniuliza huku macho yake meupe makubwa na legevu yakinitazama usoni na tabasamu lake usoni likaashiria kuwa urafiki wetu ungedumu kwa muda mrefu zaidi.
“Napenda kufahamu hiyo herufi V kwenye kidani chako shingoni ina maana gani?”. Swali langu likampelekea yule mhudumu azidi kuchanua tabasamu lake usoni na hali ile ikazidi kunitia faraja moyoni mwangu.
“Herufi V ni herufi ya mwanzo ya jina langu”. Hatimaye akanijibu huku akijichelewesha pale mezani kama aliyekuwa na kiu ya kutaka kuzidi kunisikia.
“Vanessa, Vaileth, Verdiane, Vicky, Victorie...”. Nikajaribu kuotea huku nikiangua kicheko hafifu.
“Veronica”. Yule mlimbwende akanikatisha kabla sijamaliza kuotea huku akiangua kicheko hafifu kilichopelekea vile vishimo vya mashavuni mwake vionekane waziwazi bila kificho na hivyo yale meno yake meupe yaliyopangika vizuri kuongeza ziada nyingine katika uzuri wake. Loh! Veronica alikuwa msichana mzuri mno kuwahi kumuona maishani mwangu hata Amanda hakufua dafu mbele yake.
“Jina lako tamu kama asali na hakika uzuri wako umelitendea haki”. Nikachombeza utani huku nikiangua kicheko hafifu.
“Mh! nashukuru, na wewe je unaitwa nani?”. Veronica akaniuliza na nikiwa tayari nimejiandaa kukabiliana na swali la namna ile nikamdanganya huku nikitabasamu...ITENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 22
Mtunzi:Kelvin Mponda

“Naitwa Gilbert”
“Hii ni mara yako ya kwanza kufika hapa HAVANA CLUB?”. Veronica akaniuliza huku akijitia kupangapanga lile bakuli la supu na ile glasi ya mvinyo mwepesi.
“Hujakosea ingawa nimetokea kuipenda sana Club hii”
“Ni kweli kwani nilipokuona tu kwa mara ya kwanza wakati ulipokuwa ukiingia humu ndani nikajua kuwa wewe ni mgeni wa mahali hapa”. Veronica akaongea huku akinitazama na hapo nikajichekesha kidogo kabla ya kumuuliza.
“Umejuaje?”
“Kwanza sura yako ni ngeni kabisa machoni mwangu na wateja wanaofika hapa wengi huwa nawafahamu na istoshe nilikuona ukibabaika kidogo kama mgeni wa mazingira haya wakati ulipokuwa ukiingia”. Veronica akaniambia na kwa kweli nilimuona ni msichana mjanja na mwerevu kiasi cha kuweza kunishtukia mapema.
“Mh! au labda Club yenu haipendi wageni?”. Nikachombeza utani na hapo nikamsikia Veronica akiangua kicheko cha dhahiri.
“Naomba unisamehe kaka sikuwa na maana hiyo”. Veronica akaongea kwa utulivu baada ya kicheko chake kufika ukomo. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia huku Veronica akijitahidi kunisogezea karibu staftahi ile na ukaribu wake ukanipelekea niisikie harufu nzuri ya manukato yake aliyojipaka mwilini. Bila kupoteza muda nikavunja ukimya nikimuuliza kwa sauti ya chini ambayo isingeweza kumruhusu mtu yeyote jirani na eneo lile kunisikia.
“Vipi shemeji yangu hajambo?”. Swali langu likampelekea Veronica anitupie jicho la hisia kisha taratibu akatikisa kichwa chake kuonesha kuikataa hoja ile huku tabasamu lake bado lingali usoni mwake.
“Wewe ni mtanzania?”. Veronica akaniuliza huku dhahiri nikifahamu kuwa alikuwa akitia jitihada za kuyahamisha maongezi yangu.
“Ndiyo”
“Watanzania wengi tabia zenu zinafanana”. Veronica akaniambia huku akitabasamu.
“Mh! kwani watanzania tabia zetu zipoje?”
“Wacheshi na marafiki sana”
“Mh! labda kwa kuwa wewe ndiye umesema basi naamini itakuwa kweli”. Nikaongea huku nikiangua kicheko hafifu kilichomfanya Veronica azidi kutabasamu.
“Unakaa wapi hapa jijini Bujumbura?”. Hatimaye nikavunja tena ukimya na kumuuliza Veronica.
“Nakaa nyumba namba 37 kwenye jengo la shirika la nyumba la taifa kando ya barabara ya Boulevard de Iʾndependence, nyuma ya uwanja wa mpira wa miguu wa Prince Rwagesore Stadium”. Veronica akaniambia huku akiitazama saa yake ya mkononi.
“Huwa unatoka saa ngapi kazini?”
“Saa mbili usiku mara baada ya mwenzangu anayenipokea zamu kufika”. Veronica akaniambia kwa sauti tulivu huku akionesha jitihada za kutaka kuondoka baada ya kumaliza kazi yake ya kuniandalia maakuli pale mezani.
“Naomba ruhusa yako ya kuja kukutembelea usiku wa leo kama hutojali”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama Veronica machoni katika namna ya kutaka kupata hakika na jibu ambalo lingemtoka mdomoni.
“Karibu sana”. Hatimaye Veronica akaniambia huku akiniaga kwa tabasamu maridhawa huku akichukua lile sinia aliloletea zile staftahi na kuondoka zake.
Kwa sekunde kadhaa nikabaki nimeganda kama sanamu huku nikimtazama Veronica namna alivyokuwa akiondoka eneo lile na hatimaye kutokomea kabisa kwenye ile kaunta ya ule ukumbi wa chakula.
Mara baada ya Veronica kutoweka machoni mwangu nikavuta lile bakuli la supu karibu yangu na kuanza kujipatia mlo. Kwa kuwa nilikuwa na njaa sana ile supu nilifakamia kwa kasi ya ajabu hivyo baada ya muda mfupi lile bakuli lilikuwa tupu. Nikasubiri kidogo ule mlo ushuke vizuri tumboni kisha taratibu nikashushia na ule mvinyo mwekundu wa kifaransa wa Navette de Marseille na wakati ule mvinyo ukishuka taratibu kooni mwangu akili yangu nayo ikaanza kuchangamka na kuanza kufikiria ni wapi pa kuanzia kazi nzito iliyokuwa mbele yangu.
Nilipomaliza kupata ule mlo Veronica akaja pale mezani mara moja kuondoa vile vyombo na kusafisha ile meza. Alipomaliza nikamuagiza aniletee kuku wa kurosti kwa vitunguu saumu pamoja na ugali wa dona wa kuweza kunipa nguvu mwilini. Halafu nikamwambia aniongezee glasi nyingine ya mvinyo mwekundu.
Veronica aliponiletea ule mlo na kuondoka nikaanza kula taratibu huku nikipata wasaha mzuri wa kuichukua ile ramani yangu ndogo ya kijasusi ya kukunja kisha nikaifungua na kuanza kuipitia taratibu huku nikiendelea kujipatia ule mlo pale mezani.
Kupitia ile ramani yangu ndogo ya kijasusi ya kukunja niliweza haraka kufahamu sehemu ulipokuwa uBalozi wa nchi yangu Tanzania kwa pale jijini Bujumbura nchini Burundi. Ofisi za uBalozi wa Tanzania pale jijini Bujumbura zilikuwa umbali mfupi baada ya kuyavuka makutano ya barabara ya Avenue de Gihungwe na barabara ya Avenue du 18 Septembre. Kutoka pale HAVANA CLUB hadi zilipokuwa ofisi zile za uBalozi wa Tanzania nchini Burundi hapakuwa na umbali mrefu sana ingawa pia isingefaa kutembea kwa miguu kwani mitaa mingi ya jiji la Bujumbura kwa wakati ule ilikuwa imezingirwa na askari waliokuwa wakijitahidi kudumisha hali ya usalama baada ya lile jaribio la mapinduzi ya kijeshi kufanyika.
Akili yangu hatimaye ikajikita kwenye hoja nyingine juu ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Burundi Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa na kwa kweli bado sikuweza kupata hoja yoyote juu yake. Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa kama cheo chake kinavyojieleza vizuri siyo tu alikuwa kiongozi na mwakilishi mzuri wa serikali ya Tanzania nchini Brurundi lakini vilevile alikuwa kiongozi mstaatu wa kijeshi mwenye elimu ya juu ya masuala ya kijeshi na mbinu zote za mapigano ya medani za kivita.
Kiongozi wa namna yake kusikika ametekwa au kutoweka katika mazingira ya kutatanisha halikuwa jambo la kulichukulia mzaha hata kidogo. Kwa kweli nilishindwa kabisa walau kuhisi nini ambacho kingekuwa kimejificha nyuma ya tukio lile la kutoweka kwa mwakilishi wa nchi na kiongozi yule mkubwa wa kijeshi. Huku nikiamini kuwa kama ni kweli kuwa Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa angekuwa ametekwa basi mtekaji huyo asingekuwa mtu mmoja na badala yake kingekuwa labda ni kikundi cha siri cha wanajeshi na wanajeshi hao walipaswa kuwa ni watu waliofuzu vizuri katika masuala ya kijeshi. Fikra zile zikanipelekea nianze kuhisi hatari na ugumu wa kupambana na watu hao hatari endapo harakati zangu zingenikutanisha nao, iwe kwa bahati mbaya au kwa makusudi.
Hatimaye nikamaliza kupata mlo wangu wa nguvu katika mgahawa ule kisha nikachukua simu yangu kutoka mfukoni na kuandika ujumbe mfupi wa kumfahamisha Brigedia jenerali Ibrahim Gambari kuwa tayari nilikuwa nimefika jijini Bujumbura nchini Burundi. Ule ujumbe ulipoenda nikazima simu yangu na kuitia mfukoni.
Wazo fulani lilikuwa limenijia akilini. Sikutaka kufanya mizunguko yangu huku nikiwa na mzigo wowote hivyo Veronica alipokuja pale mezani kuondoa vyombo akanipa karatasi ndogo yenye bili ya ile huduma ya chakula na vinywaji. Nikaipokea ile karatasi na kuipitishia macho kisha nikafungua wallet yangu ndogo kutoka mfukoni na kuhesabu kiasi kile cha pesa na kulipa. Halafu nikachomoa noti mbili za faranga za Burundi ambazo nilimpa Veronica kama ahsante kwa kunihudumia vizuri pale mgahawani. Veronica akapokea noti zile kwa furaha na kabla sijaondoka nikamuomba nimuachie lile begi langu dogo la shanta kwa kisingizio kuwa nilikuwa na mizunguko mingi jijini Bujumbura hivyo kutembea na begi lile kwangu ingekuwa usumbufu. Veronica akanikubalia ombi langu bila kusita hivyo nikaagana naye kwa miadi ya kuonana naye tena baadaye.
Saa yangu ya mkononi ilionesha kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa tano na robo asubuhi wakati nilipokuwa nikitoka nje ya lile jengo la HAVANA CLUB na kuelekea kando ya eneo lile sehemu kulipokuwa na maegesho ya teksi.
Jua tayari lilikuwa limechomoza vizuri na hivyo kupelekea joto hafifu kuongeza ziada nyingine ya hali ya hewa ya jiji la Bujumbura. Jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi lenye lengo la kuingʾoa madarakani serikali ya rais Pierre Nkurunziza lilikuwa limeacha taharuki ya aina yake na kutengeneza hali ya hofu kwa raia wa nchini Burundi. Hofu ile ya kudorora kwa hali ya usalama nchini Burundi ilikuwa imepelekea raia wengi kuanza kuyakimbia makazi yao na kuelekea nchi za jirani kama mkoani Kigoma nchini Tanzania, Rwanda na D.R. Congo kuyanusuru maisha yao. Hivyo kwa wakati ule mitaa mingi ya jiji la Bujumbura ilikuwa mbioni kubaki ukiwa kwa kukimbiwa na watu. Hata hivyo hali ile haikuwa kwa wakazi wote kwani wapo baadhi ya raia waliokuwa wamejifungia majumbani mwao huku wakisubiri kuona hatima ya mapinduzi yale.
Dereva wa teksi kijana anayeelekeana na umri wangu, mrefu, mweusi na mwenye sura yenye bashasha zote za kirafiki akawahi kunifungulia mlango wa mbele wa teksi yake wakati nilipokuwa mbioni kuyafikia yale maegesho ya teksi nje ya HAVANA CLUB. Hata hivyo sikukubaliana na mpango wake badala yake nikazunguka na kufungua mlango wa nyuma wa teksi ile na kuingia ndani. Yule dereva wa teksi kuona vile haraka akaufunga ule mlango alionifungulia kisha haraka akazunguka na kufungua mlango wa dereva wa ile teksi na kuingia ndani na kabla hajageuka nyuma na kuniuliza uelekeo nikavunja ukimya na kumwambia.
“Prends moi à lʾambassade de Tanzanie”. Nipeleke ulipo uBalozi wa Tanzania. Yule dereva akanitazama kidogo na kutikisa kichwa chake katika namna ya kuashiria kuwa alikuwa amenielewa na nilipomchunguza nikajua kuwa hakuwa mtu wa maneno mengi.
Muda uleule ile teksi ikayaacha yale maegesho na kuingia upande wa kulia kuifuata barabara ya Boulevard de IʾUprona. Hata hivyo kabla hatujafika mwisho wa barabara ile mara nikamuona yule dereva akikata kona kuingia upande wa kulia na kuifuata barabara ya Avenue de la Mission. Ilikuwa ni barabara kama zilivyokuwa barabara nyingine za mitaa ya jiji la Bujumbura kutokana na muonekano wa mandhari yake. Tofauti pekee niliyoiona ni kuwa barabara ile haikuwa na msongamano wa waandamanaji na ilikuwa ikikatisha katikati ya majengo marefu ya ghorofa yenye ofisi za kisasa za watu binafsi na ofisi za mashirika mbalimbali ya serikali ya Burundi.
Baada ya safari fupi hatimaye tukawa tumefika mwisho wa ile barabara na hapo nikamuona yule dereva akipunguza mwendo na kuingia upande wa kushoto akifuata barabara pana ya Chaussée P.L. Rwagasore. Ilikuwa barabara pana zaidi kama zile za masafa marefu na hata idadi ya magari katika barabara ile ilikuwa kubwa na magari yale mengi yalikuwa ni ya jeshi la wananchi wa Burundi huku yakiwa yamebeba wanajeshi. Nikageuka kuyatazama magari yale ya jeshi kwa utulivu huku mawazo mengi yakipita kichwani. Hata hivyo nilipogeuka nyuma kutazama sikuliona gari lolote likitufungia mkia na hali ile ikanitia faraja.
Barabara ya Chaussée P.L. Rwagasore mbele yake ingekuja kukutana na barabara nyingine ya Boulevard de IʾIndependence. Hata hivyo kabla hatujayafikia makutano yale mara nikamuona tena yule dereva wa ile teksi akipunguza mwendo na hatimaye kuingia upande wa kulia akiifuata barabara ya Avenue du Commerce. Hata hivyo hatukusafiri sana katika barabara ile kwani kule mbele ile barabara ilikuwa imefungwa na polisi wa Burundi waliokuwa wakipambana kikamilifu na waandamanaji. Hivyo yule dereva akaingia upande wa kushoto kuifuata barabara ya Avenue du Marche na hapo mwendo wetu ukaongezeka. Yule dereva alikuwa mtu mjanja sana na anayeijua vizuri kazi yake kwani nilipomchunguza nikagundua kuwa alikuwa akiepuka zile barabara zilizokuwa na msongamano wa magari na zile zilizokuwa na waandamanaji wa kuunga mkono lile jaribio la mapinduzi la kijeshi.
Nikiwa kwenye ile siti ya nyuma ya ile teksi uchunguzi wangu ukanitanabaisha kuwa majengo mengi muhimu ya serikali kama posta, benki, hospitali na vituo vya redio kwa wakati ule yalikuwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la wananchi wa Burundi. Wanajeshi wale wakionekana kuyazingira majengo yale na bunduki zao mikononi.
Tulipoyafikia makutano ya barabara ya Avenue de LʾEnseignement na ile barabara ya Avenue du Marche nikamuona tena yule dereva akipunguza mwendo na kuingia barabara ya Avenue de LʾEnseignement upande wa kulia na hapo nikaliona jengo la Banque de Crédit de Bujumbura upande wa kulia. Hata hivyo kwa wakati ule benki ile ilikuwa imefungwa huku ikionekana kulindwa kikamilifu na wanajeshi waliokuwa wamelizingira jengo lile kikamilifu.
Tukaendelea na safari yetu na kabla ya kuifikia barabara ya Rue de La Sciénce yule dereva akapunguza tena mwendo na kuingia upande wa kushoto akiifuata barabara ya Boulevard Patrice Lumumba. Kitendo cha kuingia kwenye barabara ile kikanipelekea nilione jengo la Galerie du Progres upande wa kulia kwenye barabara ya Rue du Progres na jengo refu la ghorofa la benki ya biashara ya Kenya kiasi cha umbali wa hatua chache kabla ya kuyafikia makutano ya barabara ya Boulevard Patrice Lumumba na barabara ya Avenue Pierré Ngendandumwe.
Mwendo wetu ukiwa siyo wa kubabaisha tulipofika mbele kidogo upande wa kulia tukaipita barabara ya Avenue Des Eucalyptus kisha barabara ya Avenue du Palmier upande wa kulia na ile barabara ya Avenue Des Non Aligens upande wa kushoto. Tulipoyafikia makutano ya barabara ya RN 7 nikamuona yule dereva akiufuata mzunguko wa barabara wa RN 7 na hapo haraka nikajua kuwa yule dereva wa teksi alikuwa akifanya ujanja wa kuongeza mizunguko ili hatimaye anitoze pesa nyingi kwani vinginevyo angeweza kupunguza urefu wa safari ile kwa...ITAENDELEA
 
RIWAYA; UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU; 23
Mtunzi:Kelvin Mponda

...kuchepukia upande wa kulia ambapo mbele yake angekuja kukutana na ile barabara ya Avenue du 18 Septembre ambapo tungeshuka na barabara ile hadi sehemu lilipokuwa jengo la ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi. Hata hivyo sikutia neno lolote kwani pamoja na hila ya yule dereva kwangu ilikuwa ni starehe nyingine ya utalii wa maeneo mbalimbali ya jiji la Bujumbura.
Tulipoufikia ule mzunguko wa barabara ya RN 7 yule dereva akauzunguka mzunguko ule na kushika uelekeo wa upande wa kushoto akiifuata barabara ya Boulevard du Japan. Ilikuwa barabara pana yenye njia mbili upande wa kushoto na njia nyingine mbili upande wa kulia. Ilikuwa ni barabara yenye matunzo mazuri na miongoni mwa barabara za kisasa kabisa jijini Bujumbura. Barabara ile ikipakana na majengo marefu ya ghorofa yenye ofisi za mashirika ya kimataifa kama shirika la wakimbizi duniani UNHCR-United Nations High Commissioner for Refugees, shirika la afya duniani WHO-World Health Organisation na ofisi za wizara ya haki na sheria za nchini Burundi. Kwa hakika ilikuwa ni barabara yenye ustaarabu na utulivu wa hali ya juu kama vile zilivyokuwa barabara nyingi za eneo la Upanga lililopo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.
Mara tu tulipoingia kwenye ile barabara dereva wa ile teksi akapunguza mwendo na kuendesha gari taratibu na kwa kufanya vile nikagundua kuwa kutoka pale hatukuwa mbali sana na ofisi za uBalozi wa Tanzania jijini Bujumbura. Nilipogeuka kutazama upande wa kulia nikaliona jengo kubwa la kanisa la katoliki la Regina Mundi Cathedral. Tukaendelea na safari ile na mbele kidogo tukaja kukutana na barabara ya Boulevard de la Liberte.
Mara tu tulipoyapita makutano yale upande wa kushoto nikaliona jengo la shule ya Ubelgiji la jijini Bujumbura-Ecole Belge de Bujumbura. Hatukufika mbali sana katika safari yetu mara nikamuona yule dereva wa teksi akipunguza mwendo na kisha kuwasha taa za gari za upande wa kulia akiashiria kuwa alikuwa akijiandaa kuchepukia barabara ya Avenue du 18 Septembre kwani mbele kidogo ya barabara ile upande wa kushoto kabla ya kuyafikia makutano ya barabara ya Avenue du 18 Septembre na barabara ya Avenue de Gihungwe ndiyo lilipokuwa jengo lenye ofisi za uBalozi wa Tanzania jijini Bujumbura nchini Burundi. Sikupenda teksi ile ikanishushie mbele kabisa ya lile jengo la uBalozi hivyo kabla yule dereva hajakata kona kuifuata barabara ile haraka nikavunja ukimywa kwa kumwambia.
“Laissez-moi ici, sʾil vous plaît”. Niache hapa tafadhali. Kauli yangu ya ghafla ikampelekea yule dereva azidi kupunguza mwendo kisha akageuka kidogo na kunitazama kama mtu aliyeshikwa na mshangao. Hata hivyo hakutia neno badala yake akazidi kupunguza mwendo zaidi na hatimaye kusimama mbele ya ofisi moja ya mawasiliano iliyokuwa kwenye ile kona. Sikutaka kupoteza muda hivyo haraka nikamuuliza yule dereva gharama za usafiri hadi pale na aliponiambia pasipo mabishano nikachomoa noti kadhaa kutoka katika wallet yangu mfukoni na kumpa kiasi kile cha fedha kisha nikamshukuru huku nikifungua mlango na kushuka. Muda uleule mara nikaiona ile teksi ikigeuza na kushika ule uelekeo wa kule tulipotoka.
Ile teksi ilipotoweka kabisa machoni mwangu nikaanza kupiga hatua zangu kwa utulivu nikikatisha mbele ya zile ofisi za mawasiliano kuelekea barabara ya Avenue du 18 Septembre na nilipoingia tu kwenye ile barabara nikagundua kuwa ilikuwa ni barabara iliyochangamka kidogo kwa pilikapilika za magari. Labda kutokana na kwamba ile ilikuwa ni barabara iliyokuwa imepakana na majengo yenye ofisi nyeti za serikali ya Burundi na mashirika makubwa ya kimataifa. Wakati nikitembea upande wa kulia wa ile barabara nikauona mgahawa mmoja wa kisasa wa La Belle Fille Restaurant baada ya kuipita ofisi ya shirika la Bima la Burundi. Upande wa kushoto wa barabara ile kulikuwa na bustani ya wazi ya maua kabla ya kulipita jengo la benki ya wanawake ya Burundi.
Nilikatisha mbele ya bustani ile ya wazi na nilipolivuka lile jengo la benki ya wanawake ya Burundi nikapita mbele ya jengo refu la ghorofa lililokuwa likitumika kama makao makuu ya ofisi za ukusanyaji kodi na mapato za serikali ya Burundi. Baada ya kulipita jengo lile hatimaye nikajikuta nikikabiliana na ofisi za uBalozi wa Tanzania nchini Burundi. Mbele ya ofisi zile za Balozi kulikuwa na bustani nzuri ya miti na maua ya kupendeza yaliyokatiwa vizuri na katikati ya bustani ile mbele ya lile jengo kulikuwa na milingoti sita yenye bendera za nchi za Afrika ya mashariki zilizokuwa zikipepea kwa utulivu.
Kwa tathmini ya haraka nilipozichunguza ofisi zile za Balozi ya Tanzania nchini Burundi nikagundua kuwa kwa wakati ule zile ofisi zilikuwa mbioni kuzidiwa na pilikapilika za watu waliokuwa wamefika pale kufuata huduma. Upande wa kushoto nje ya zile ofisi kulikuwa na magari mengi yaliyoegeshwa. Idadi kubwa ya magari yale yalikuwa ni ya watu binafsi na machache yalikuwa ni ya mashirika ya kimataifa kama UNHCR, UNCEF, Amnesty International na magari ya mashirika mbalimbali makubwa ya habari duniani kama THE REUTERS, CNN, BBC na mengineyo. Nje ya ofisi zile pia niliwaona watu wengi wakiwa na mabegi yao kama wasafiri na hapo nikajua kuwa watu wale walikuwa kwenye pilikapilika za kufuata taratibu za uhamiaji kabla ya kuondoka nchini Burundi kufuatia hali ya usalama wa nchi ile kuzidi kuwa tete.
Hatimaye nikafika nje ya ofisi zile na hapo nikaanza kujipenyeza katikati ya lile kundi kubwa la watu nikielekea ndani ya zile ofisi za Balozi kuelekea eneo la mapokezi.
Mara tu nilipoingia nikagundua kuwa msongamano wa watu mle ndani ulikuwa mkubwa sana huku watu wale wakiwa wamepanga foleni kwenye mistari minyoofu kufuata huduma kwenye kauta kubwa yenye maafisa uhamiaji wanne waliokuwa wamependeza katika sare zao za kazi. Maafisa uhamiaji wale walikuwa ni wanaume watatu na dada mmoja ambaye haraka macho yetu yalipokutana akashikwa na hamaki huku tabasamu la hakika likichomoza usoni mwake. Msichana yule nilimfahamu kwa jina la Hidaya Kijuu afisa uhamiaji mwenye cheo cha Sajenti. Miezi miwili iliyopita Hidaya alikuwa amefunga ndoa na rafiki yangu kipenzi wa jeshi la wananchi wa Tanzania Kanali Mbinde Mtimkavu jijini Dar es Salaam ambapo sherehe yao ya kufana ilifanyikia kwenye ukumbi wa jeshi wa Lugalo.
“Kha! shemeji…!” Hidaya alikuwa wa kwanza kuniita kwa uchangamfu wa hali ya juu huku ameshikwa na furaha isiyoelezeka.
“Hakika ndiyo mimi shemejio. Mh! kweli waswahili hawakukosea pale waliposema milima haikutani lakini binadamu hukutana”. Nikaongea kwa utulivu huku usoni nikiumba tabasamu na nilipoifikia ile meza ya kaunta alipokuwa Hidaya nikaiegemeza mikono yangu huku nikipambana vikali na macho ya chuki kutoka kwa watu waliokuwa kwenye mstari wa foleni ya kumfikia Hidaya baada ya kuhisi kuwa nilikuwa nataka kuwazidi maarifa kwa kukwepa kupanga foleni. Wale maafisa wengine wa uhamiaji wakageuka kunitazama kwa makini huku dhahiri wakionekana kushindwa kunielewa. Hata hivyo niliwasalimia na wote wakaitikia na kugeuka wakiendelea na hamsini zao.
Hata hivyo Hidaya alikuwa mjanja sana kwa kushtukia kuwa maongezi yetu eneo lile yangeweza kusababisha kero kwa wale watu waliokuwa wamepanga foleni ya kutaka huduma kwenye kaunta yake. Hivyo haraka akanionesha ishara kuwa nizunguke nyuma ya ile kaunta na kwenda kumsubiri kwenye ukumbi mdogo wa kuta za vioo uliokuwa ndani ya lile jengo. Bila kupingana na wazo lake nikafanya vile na nilipokuwa nikiizunguka ile kaunta nikawaona maafisa wengine uhamiaji wa ofisi zile za uBalozi wakiwa ndani ya ofisi zao wametingwa na kazi. Wengine wakichambua taarifa kutoka kwenye majalada yaliyozizunguka meza zao na wengine wakifanya uhakiki wa taarifa kwenye kompyuta. Hata hivyo hakuna aliyejisumbua kunitazama wakati nilipokuwa nikipiga hatua zangu kwa utulivu katikati ya korido pana kuelekea kwenye ukumbi mdogo uliozungukwa na kuta kubwa za vioo uliokuwa upande wa kushoto wa lile jengo la ofisi zile za ubalozi.
Nyuma ya ile kaunta kulikuwa na meza na viti vilivyokaliwa na maafisa wengine wawili wa kike waliokuwa makini kuwahudumia watu na upande wa kulia kwenye kona ya ile kaunta kulikuwa na korido nyingine pana iliyokuwa ikitazamana na milango ya vyumba vitatu vya ofisi iliyokuwa wazi. Huku nje ya korido ile kukiwa na foleni nyingine ya watu katika mabenchi marefu, watu wale wakisubiri kuingia kwenye zile ofisi. Ile korido niliyoingia ilikuwa ikitazamana na milango mitatu ya ofisi na mwisho wa korido ile kulikuwa na ngazi za kuelekea ghorofa ya juu.
Hatimaye nilipofika katikati ya ile korido nikauona ukumbi mdogo wa mikutano wenye jumla ya viti kumi na mbili vilivyoizunguka meza moja ndefu ya umbo mstatili. Ukumbi ule ulikuwa umezungukwa na kuta kubwa za vioo na mapazia marefu ambayo kwa wakati ule hayakuwa yamefungwa.
Taratibu nikausukuma mlango wa kile chumba na kuingia ndani ya ule ukumbi huku nikiyatembeza macho yangu taratibu kutathmini mandhari yale. Ukiondoa ile meza kubwa ya mikutano iliyozungukwa na viti kumi na mbili na runinga pana iliyokuwa upande wa kulia wa kile chumba. Ukutani hakukuwa na ziada nyingine mle ndani zaidi ya utulivu wa hali ya juu. Nilipourudishia ule mlango nyuma yangu nikatembea taratibu nikiizunguka ile meza kisha nikavuta kiti kimoja na kuketi. Nikiwa pale nikaanza kumkumbuka vizuri Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa, Balozi wa Tanzania nchini Burundi ambaye taarifa zilizoifikia idara ya ujasusi jijini Dar es Salaam zilikuwa zimeeleza kuwa alikuwa ametekwa na watu wasiofahamika.
Dakika tano zilipokuwa mbioni kutokomea tangu nilipoingia mle ndani ya kile chumba mara nikauona mlango wa kile chumba ukifunguliwa kisha Hidaya akaingia mle ndani huku akiwa katika uso wenye tabasamu la kirafiki. Hidaya alipoingia mle ndani akaanza kuzunguka kile chumba huku akishusha mapazia katika namna ya kuyazuia macho ya watu wanaopita nje ya kile chumba kututazama wakati tukiendelea na maongezi yetu. Hidaya alipomaliza kufungua yale mapazia akaelekea ukutani na kuwasha taa iliyoleta nuru ya kutosha mle ndani kisha akaja na kuvuta kiti akiketi mbele yangu. Nilipomtazama mara moja sikuona tashwishwi yoyote usoni mwake ingawa alijitahidi kwa kila hali kutabasamu. Hidaya alikuwa msichana mzuri na mrembo mwenye umbo lenye mvuto wa aina yake lakini vilevile mcheshi na anayethamini sana utu.
“Habari za jijini Dar es Salaam Tibba?”. Hidaya akavunja ukimya akiniuliza kwa sauti nyepesi ya kubembeleza huku akinilegezea macho kabla ya kuangua kicheko hafifu cha kimahaba. Nilimfahamu vizuri Hidaya kuwa utani ilikuwa hulka yake na kwa kuwa nilikuwa nimemzoea wala sikuona tatizo lolote badala yake nikajikuta nikiangua kicheko cha furaha na kicheko kile kilipokuwa mbioni kufika ukomo nikavunja ukimya.
“Kweli kaka yangu Mbinde kapata mke. Sipati picha angekufanya nini kama muda huu angekuwa humu ndani amejibanza sehemu fulani halafu akufume unanifanyia upuuzi huo”. Nikamwambia Hidaya na kitendo cha kumuona haraka akigeuka na kuyatembeza macho yake kwa hofu mle ukumbini kikanipelekea niangue kicheko kingine.
“Mh! umenitisha sana na kaka yako jinsi alivyo na wivu ningetoka mkuku humu ndani bila ya kupenda kabla hajanifikia”. Hidaya akaongea huku akiendelea kucheka kisha akasogeza kiti vizuri na kuvaa uso wa kazi.
“Dar es Salaam ni kwema kama ulivyokuacha shemeji”. Nikaongea kwa utulivu huku tukitazamana pale mezani na hapo Hidaya akanitazama kidogo kama anayefikiri kitu cha kuongea na hatimaye akavunja ukimya akiongea kwa sauti dhaifu inayopwaya.
“Hapa mambo si shwari Tibba”
“Nafahamu na ndiyo maana nimekuja hapa Hidaya. Chifu amenigusia juu ya kutekwa kwa Balozi wetu hata hivyo maelezo yake hayakuwa na ziada yoyote nje ya maelezo yaliyokuwa kwenye faksi aliyotumiwa kutoka hapa”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama kwa makini msichana yule mwanausalama machachari.
“Jana usiku Chifu alinidokeza juu ya ujio wako kwa njia ya simu na kwa kweli nilifurahi sana niliposikia kuwa ni wewe ndiye uliyekabidhiwa jukumu hili. Kwani kwa vile ninavyokufahamu najua kazi itafanyika kwa weledi wa hali ya juu na majibu yatapatikana haraka ingawa pia sitarajii kuwa kazi itakuwa nyepesi”. Hidaya akaongea kwa sauti tulivu na nilipomtazama usoni nikagundua kuwa mzaha ulikuwa mbali kabisa na nafsi yake.
“Ina maana Chifu alikuwa akifahamu kuwa wewe upo huku?”. Nikamuuliza Hidaya kwa udadisi huku nikimtazama usoni kwa makini.
“Ndiyo alikuwa akifahamu na ni yeye ndiye aliyependekeza niletwe hapa”
“Una muda gani tangu uhamishiwe hapa kikazi?”. Nikamuuliza Hidaya huku mawazo mengi yakipita kichwana mwangu.
“Mwezi mmoja na nusu” Hidaya akanijibu huku akinitazama kwa makini.
“Sasa mbona Chifu hakuwahi kunidokezea juu ya uwepo wako hapa jijini Bujumbura?”
“Huwenda alitaka kukufanyia surprise kwa vile anajua sisi ni marafiki wa muda mrefu kama chanda na pete”. Hidaya akaongea kwa uchangamfu huku akiumba tabasamu hafifu usoni mwake. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku kila mmoja akiwaza lake na ukimya ule ulipokuwa mbioni kushika hatamu nikawekeza kwenye hoja ya msingi.
“Nini kinachoendelea hapa Burundi?”
“Baadhi ya raia wa kawaida, wanasiasa na wanajeshi hawaitaki serikali iliyopo madarakani”
“Kwa nini?” nikamuuliza Hidaya kwa shauku na hapo nikamuona akinitazama kidogo kwa mshangao.
“Taarifa zinaeleza kuwa rais wa Burundi ndugu Pierre Nkurunziza anajaribu kuipindisha katiba ya nchi hii ili aweze kugombea kiti cha urais kwa mhula wa tatu na ambapo inasemekana kuwa mpango huo ni kinyume cha katiba”
“Kweli aliyesema kuwa Afrika ni bara la giza hakuwa amekosea. Hivi hii Afrika imeingiliwa na mdudu gani kiasi kwamba kila kiongozi anayeingia madarakani aone ugumu wa kutoka wakati inapofikia wakati wa kufanya hivyo?”...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU; 24
Mtunzi:Kelvin Mponda

“Kweli haya ni maradhi ya aina yake kwani hata wale viongozi wanaoona aibu na kuondoka madarakani kwa mujibu wa katiba ukizitazama vizuri nyuso zao kwa makini utagundua kuwa mioyo yao bado inatamani kuendelea kubaki madarakani ila tu ni kwamba mazingira ya kuendelea kubaki madarakani hayaruhusu”. Hidaya aliongea kwa masikitiko.
“Unavyosema ni kweli kabisa Hidaya ingawa wapo baadhi ya viongozi wa Afrika ambao wamewafanyia mambo mengi mema na mazuri raia wao kiasi kwamba raia haohao wakaamua kuendelea kuwabakiza madarakani waendelee kuwaongoza kwa muda mrefu kutokana na wananchi wao wanavyowaamini na kufurahishwa na uongozi wao. Lakini kitu cha kushangaza ni kuwa viongozi wa namna hiyo wamejikuta wakipokea fadhila hizo kwa kiasi cha kupitiliza kiasi kwamba baadaye wanapotakiwa kuachia madaraka ya nchi huanza kuchukia na kuikataa hali hiyo na badala yake hutengeneza mikakati mikali ikibidi kumwaga hata damu za raia wasio na hatia kama siyo kuwashughulikia wapinzani wao kwa mbinu chafu ili tu waendelee kubaki madarakani na kula maisha na familia zao pamoja na ndugu jamaa na marafiki.
Kuna mifano mingi tu ya viongozi wa Afrika waliokaa madarakani kwa kipindi kirefu sana kiasi kwamba ilipofika wakati wa wananchi kuwataka waachie madaraka wao hawakuwa tayari kufanya hivyo kwa ridhaa yao.
“Ni kweli Tibba” Hidaya akaongea kwa utulivu huku akitikisa kichwa kuonesha kunielewa.
“Blaise Compaoré aliyekuwa rais wa Burkina Faso aliingia madarakani kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1987. Mapinduzi ambayo yaliingʾoa madarakani serikali ya rais wa wakati huo ndugu Thomas Sankara ambapo aliuwawa katika mazingira yasiyoelezeka. Baada ya miaka 27 ya ungozi wa rais Blaise Compaoré hatimaye wananchi wa Burkina Faso wakaonesha kutosheka naye wakimtaka aachie madaraka. Hata hivyo hakuwa tayari kufanya hivyo badala yake akajaribu kubadili katiba ili awanie urais kwa mhula mwingine. Wananchi kuona hivyo wakakasirika na kuingia mitaani wakiandamana na kupinga uhuni huo. Matokeo yake nguvu ya umma ikamshinda hivyo akalazimika kukimbilia nchi jirani ya Ivory Coast huku serikali ya mpito ikishikiliwa na jeshi.
Rais wa Equatorial Guinea ndugu Teodoro Obiang Nguema Mbasogo amekaa madarakani kwa muda wa miaka zaidi ya 35 tangu alipotwaa madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi na kuapishwa kuwa rais mwaka 1982.
José Eduardo dos Santos, rais wa nchi ya Angola amekaa madarakani tangu mwaka 1979, ikiwa ni miaka minne baada ya nchi hiyo kupata ukombozi. Wakati akisifiwa kwa sera yake nzuri ya kuinua sekta ya mafuta nchini humo, bado amekuwa akishutumiwa vikali kwa kuongoza serikali inayonuka rushwa. Wakati asilimia sabini ya raia wa nchi hiyo wakiishi chini ya dola mbili kwa siku moja mtoto wake wa kike aitwaye Isabel kupitia mianya ya kisiasa amekuwa mmoja wa matajiri wakubwa akitambulika kama bilionea mwenye umri mdogo barani Afrika.
Rais Robert Mugabe ni kiongozi mwingine aliyekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 34 huku akiendelea kukosolewa vikali na serikali za nchi za magharibi. Lakini vilevile amekuwa akipendwa sana na raia wengi wa bara la Afrika kwa misimamo yake mikali ya kuzituhumu serikali za nchi za magharibi kwa kupenda kuingilia mambo ya serikali za nchi nyingine zikiwemo nchi za Afrika.
Paul Biya rais wa Cameroon na yeye amekaa madarakani kwa miaka zaidi ya 32 hadi sasa tangu mwaka 1982 na amekuwa akijificha katika siasa za chama kimoja tangu miaka ya themanini na hatimaye kuachana na siasa za chama kimoja mapema miaka ya tisini chini ya shinikizo la kimataifa. Hata hivyo chaguzi nyingi zinazomrudisha madarakani zimekuwa zikihisiwa kuwa siyo za haki huku akiendelea kuboresha mahusiano mazuri na nchi ya Ufaransa.
Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 baada ya kuanguka kwa tawala za Iddi Amin Dada na Milton Obote. Hata hivyo amekuwa miongoni mwa viongozi walio mstari wa mbele kupinga vitendo vya kishoga lakini vilevile anasifika kwa kuinua vizuri uchumi wa nchi ya Uganda na kutengeneza mipango kabambe ya kupambana na ugonjwa hatari wa UKIMWI nchini kwake.
Kiongozi mwingine wa Afrika ni Brigedia Omar al-Bashir wa Sudan ambaye aliingia madarakani mwaka 1989 kwa mapinduzi ya kijeshi yasiyo ya kumwaga damu. Amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 25 na amechaguliwa mara tatu kuendelea kushika madaraka katika chaguzi tatu zenye kukosolewa vikali na wapinzani na umoja wa mataifa. Mwaka 2009 Omar al-Bashir alikuwa ndiye kiongozi wa kwanza wa Afrika kushtakiwa kwenye mahakama ya ICC kwa tuhuma za mauji ya halaiki, ubakaji na utesaji wa watu katika jimbo la Darfur.
Idriss Déby rais wa Chad yeye pia amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 23 tangu mwaka 1990 alipoipindua madarakani serikali ya rais wa wakati huo ndugu Hissene Habré katika mji mkuu wa nchi hiyo uitwao NʾDjaména.
Kiongozi mwingine ni Isaias Afwerki rais wa Eritrea ambaye na yeye amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 23 tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1993. Eritrea ni nchi ya mrengo wa chama kimoja tu cha siasa. Chama cha siasa cha rais Afwerki kiitwacho Peopleʾs Front for Democracy and Justice (PFDJ) ndiyo chama pekee kinachoruhusiwa kushiriki shughuli za siasa za nchi hiyo. Ndugu Afwerki amekuwa akikosolewa vikali kwa kushindwa kukuza demokrasia nchini mwake. Serikali yake imekuwa ikipambana vikali na wakosoaji wake huku akivifungia vyombo binafsi vya habari vinavyokinzana na utawala wake.
Mwingine ni ndugu Yahya Jammeh rais wa Gambia ambaye hadi sasa amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 20 tangu alipoanza kuitawala nchi hiyo tangu mwaka 1994 akiwa mwenyekiti wa chama chake cha siasa cha Armed Forces Provisional Ruling Council (AFPRC)
Denis Sassou Nguesso rais wa jamhuri ya Kongo ni miongoni mwa marais waliokaa muda mrefu madarakani katika nchi yake. Hadi wakati huu amekaa madarakani kwa muda wa zaidi ya miaka 17 tangu kuanguka kwa utawala wa rais Pascal Lisouba nchini humo. Hii ni sehemu tu ya viongozi wa Afrika wenye kasumba ya kupenda kungʾangʾania madaraka”. Nikaweka kituo na kumtazama Hidaya nikitaka kupata hakika kama alikuwa akiyasikiliza maelezo yangu kwa makini na kitendo cha kumuona akinitazama kwa utulivu kikanijulisha kuwa tulikuwa pamoja.
“Mh! Tibba kweli wewe ni mdadisi. Umeyajulia wapi mambo yote hayo?”. Hidaya akaniuliza kwa shauku huku akinitazama kwa makini.
“Haya ni mambo tunayopaswa kuyafahamu sisi wote Hidaya kwani ukichunguza utagundua kuwa matatizo ya nchi za Afrika kwa kiasi kikubwa yanafanana. Ingawa mimi binafsi wakati mwingine naona kuwa tatizo siyo kwa kiongozi kukaa muda mrefu madarakani kwani anaweza kufanya hivyo kutegemeana na katiba ya nchi husika kama itamruhusu kufanya hivyo na siyo kubadili katiba ili izidi kumuweka zaidi madarakani. Raia wengi hawana matatizo na serikali inayokaa madarakani muda mrefu kama serikali hiyo itawaletea maendeleo na kukidhi haja ya shida zao. Lakini pale unapokuta kiongozi wa nchi na serikali yake ni mzigo kwa raia, serikali inanuka rushwa huku ikiandamwa na utabaka wa kidini au ukabila na hakuna maendeleo yoyote hapo ndiyo ubaya wa viongozi wa Afrika unapoonekana waziwazi”. Nikaweka kituo huku nikiviminyaminya vidole vyangu mkononi.
“Kwa muda mfupi wa mwezi mmoja na nusu tangu nilipofika hapa jijini Bujumbura nimegundua kitu?”. Maelezo ya Hidaya yakaamsha upya hisia zangu na hapo nikamkata jicho la shauku kabla ya kimuuliza.
“Kitu gani?”
“Suala la ukabila”
“Bado sijakuelewa?”. Nikamuuliza Hidaya huku nikimtazama kwa makini.
“Burundi ni miongoni mwa nchi chache za barani Afrika zenye makovu ya ukabila na katika nadharia hiyo hali ya kuaminiana kati ya wenyewe kwa wenyewe huwa ni tete. Hii nchi inaundwa na watu wa makabila matatu. Kabila la Wahutu ndiyo kubwa kuliko makabila mengine huku likichukua kiasi cha asilimia themanini na tano ya idadi ya raia wote wa Burundi. Asilimia kumi na nne ya sehemu iliyosalia inachukuliwa na watu wa kabila la Tutsi na hivyo kupelekea asilimia moja iliyosalia kuchukuliwa na kabila dogo kabisa la Watwa. Hata hivyo msuguano mkali upo katika haya makabila mawili makubwa.
Kwa mfano ikitokea serikali inaongozwa na mhutu basi ujue hapo idadi kubwa ya watutsi hawataunga mkono serikali hiyo kinaga ubaga kwa vile aliyeko madarakani siyo wa mrengo wao. Vilevile ikitokea kuwa serikali iliyopo madarakani inaongozwa na mtutsi basi hapo ujue wahutu wengi watahisi kuwa uongozi uliopo madarakani hauwatendei haki na ndiyo maana kumefanyika mapinduzi mengi ya kijeshi katika nchi hii”. Hidaya akaweka kituo akinitazama na macho yetu yalipokutana nikagundua kuwa macho yake yalikuwa na uchovu mwingi kama mtu aliyepoteza usingizi kwa muda wa siku mbili mfululizo.
“Unadhani jeshi la wananchi wa Burundi limefanikiwa kuchukuwa udhibiti wa maeneo yote ya serikali?”. Nikamuuliza Hidaya katika namna ya kuzidi kumdadisi.
“Mh! bado hali ni tete kwani inavyoonekana ni kama mpango wa jaribio hili la mapinduzi ya kijeshi hapa Burundi ulikuwa haujaratibiwa vizuri na kupata ushawishi wa kutosha kutoka kwa viongozi waandamizi wa jeshi. Kwani baadhi ya askari watiifu kwa serikali ya rais Pierre Nkurunziza wameonekana wakipambana kikamilifu kudhibiti mapinduzi haya dhidi ya askari wenzao waasi wanaotaka kuingʾoa serikali iliyoko madarakani na hivyo kupelekea hali ya usalama wa hapa Burundi kuzidi kuwa tete”
Maelezo ya Hidaya nilikuwa nimeyapata vyema hivyo nikaanza kuyatembeza macho yangu mle ndani taratibu huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu juu ya hali ile ya usalama ilivyokuwa pale nchini Burundi. Nilitamani kumuelezea Hidaya juu ya masaibu yote yaliyonikuta tangu nilipotoka jijini Dar es Salaam hata hivyo sikuona kama ule ungekuwa wakati mwafaka hivyo hatimaye nikavunja tena ukimya.
“Kupitia maelezo yako inaonekana kuwa kuna mpasuko mkubwa ndani ya jeshi la wananchi wa Burundi?”
“Naweza kusema hivyo kwani ukiwasikiliza raia wa hapa Burundi kwa makini utagundua kuwa wapo baadhi yao wasiobariki hata kidogo jaribio la mapinduzi haya ya kijeshi huku wakidai kuwa rais Pierre Nkurunziza anakiuka sheria kwa kuvunja katiba ya nchi inayomtaka kukaa madarakani kwa vipindi vya mihula miwili tu tofauti na yeye anavyotaka kuwania urais kwa mhula wa tatu. Lakini vilevile wapo raia wa Burundi wanaoona kuwa kitendo cha rais Pierre Nkurunziza kuwania tena urais hajafanya kosa lolote na wala hajaibaka katiba ya nchi. Watu hao wanao muunga mkono rais Nkurunziza wakitumia kigezo kuwa mwanzoni rais Pierre Nkurunziza alisimikwa madarakani na sheria ya bunge la Burundi lakini kwa sasa anayo haki ya kikatiba ya kuwania urais kama walivyo wagombea wengine wa vyama pinzani na kama ukichunguza kwa makini utagundua kuwa kuna namna ya ukweli juu ya madai haya. Hata hivyo bado naweza kusema kuwa mambo ya hapa nchini Burundi tuwaachie warundi wenyewe”. Hidaya hatimaye akaweka kituo huku akinitazama kwa utulivu kama mtu aliyezongwa na fikra nyingi kichwani.
“Mambo ya Burundi kuwaachia warundi wenyewe ni jambo jema zaidi kwani hakuna nchi inayoruhusiwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Lakini ni lazima ufahamu kuwa hali yoyote ya machafuko ya kisiasa na umwagaji damu utakaotokea hapa nchini Burundi yana athari kubwa kwa nchi nyingine za jirani ikiwemo Tanzania. Kwa mfano tangu kufanyika kwa jaribio la mapinduzi haya ya kijeshi hapa Burundi kumekuwa na wimbi kubwa la wakimbizi wa kutoka hapa nchini Burundi wanaovuka mpaka na kuingia nchini Tanzania katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo mkoani Kigoma. Matokeo yake ni kuwa kumekuwa na uharibu mkubwa wa mazingira unaofanywa kutokana na ukataji mkubwa wa miti ya asili inayotumika kama chanzo cha nishati ya kupikia chakula katika kambi hiyo na mfumuko mkubwa wa magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu na homa ya matumbo.
Lakini vilevile serikali yetu imekuwa ikitumia fedha nyingi katika kutoa misaada mbalimbali kwa wakimbizi hawa kwa kuzingatia utu wa binadamu na hivyo kupunguza kasi ya maendeleo kwa taifa katika nyanja mbalimbali. Hivyo kama kutakuwa na namna ya kufanya katika kuzuia hali ya machafuko ya kisiasa hapa nchini Burundi mimi naona ni jambo jema zaidi alimradi namna hiyo ya kuzuia machafuko hayo ifanyike kwa weledi wa hali ya juu na ushirikiano wa majadiliano ya pamoja baina ya pande mbili zenye kutofautiana, wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo nchi ya Burundi ni mwanachama hai pamoja na viongozi wakubwa wa umoja wa Afrika wenye ushawishi katika masuala ya kisiasa”
“Idara yetu ya ujasusi ina mpango gani juu ya hili jaribio la mapinduzi ya kijeshi la hapa nchini Burundi?”. Hidaya akaniuliza kwa udadisi.
“Hadi wakati huu bado sijasikia chochote na naamini kuwa hatuwezi kusikia chochote hadi hapo mkutano wa viongozi wa nchi hizi za Afrika Mashariki utakapofika tamati jijini Dar es Salaam. Kilichonileta hapa ni kumtafuta Balozi wetu hadi hapo atakapopatikana au hatima yake kujulikana”. Nikamwambia Hidaya kwa msisitizo.
“Chifu tayari amekwishanieleza kila kitu juu ya safari yako ya kuja hapa Burundi wakati nilipoongea naye usiku wa jana”. Hidaya akaniambia kwa utulivu na hapo nikamtazama kwa udadisi nikizichunguza vizuri hisia zake na nilipotaka kutumbukiza hoja mpya mara nikakumbuka kumuuliza jambo katika namna ya kutaka kupata hakika.
“Nani aliyeko nyuma ya mpango huu wa mapinduzi ya kijeshi hapa Burundi?”
“Kiongozi mmoja mwandamizi wa jeshi la wananchi wa Burundi aitwaye Meja jenerali Godefroid Niyombare. Taarifa zinaeleza kuwa Meja jenerali Godefroid Niyombare akiwa na...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 25
Mtunzi:Kelvin Mponda

...viongozi wengine wa kijeshi akiwemo aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Burundi kupitia kituo kimoja binafsi cha redio kiitwacho FRANCE 24 walitangaza mapinduzi hayo ya kijeshi. Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa mapinduzi hayo ya kijeshi yenye lengo la kuingʾoa madarakani serikali ya rais Pierre Nkurunziza raia wengi waliingia mitaani kusherehekea mapinduzi hayo huku wanajeshi wengi wakionekana kulinda ofisi za serikali kikiwemo kituo cha kurushia matangazo cha redio ya taifa. Wakati huo rais Pierre Nkurunziza akiwa jijini Dar es Salaam Tanzania kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki ambapo suala la mustakabali wa amani ya hapa nchini Burundi likiwa ndiyo kipaumbele namba moja.
Taarifa zinaeleza kuwa mara baada ya kutangazwa kwa mapinduzi hayo ya kijeshi rais Pierre Nkurunziza alijaribu haraka kurudi hapa Burundi lakini ndege yake ilisemekana kugeuzia angani na kurudi nchini Tanzania. Shirika la habari la AFP la nchini ufaransa Agence France-Presse liliripoti kuwa wanajeshi waasi walikuwa tayari wameuteka uwanja wa ndege wa kimataifa wa hapa Bujumbura”.
Maelezo ya Hidaya yalikuwa yameongezea ziada nyingine katika ufahamu wangu ingawa pia hayakuwa na msaada mkubwa katika harakati zangu. Hatimaye nikapiga mwayo hafifu wa uchovu na kunyoosha viungo vyangu na nilipotulia nikaiegemeza vizuri mikono yangu juu ya ile meza na kutumbukiza hoja mpya katika maongezi yale.
“Taarifa kupitia Fax iliyotumwa katika ofisi kuu ya idara yetu ya ujasusi jijini Dar es Salaam kutoka hapa inaeleza kuwa Balozi wetu wa hapa Burundi Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa ametekwa. Una mfahamu mtu aliyetuma taarifa hiyo?”. Nikamuuliza Hidaya kwa utulivu huku nikimtazama usoni kwa makini. Swali langu likampelekea Hidaya alegeze kidogo uso wake na kutabasamu kisha akakohoa kidogo kusafisha koo lake na hatimaye kuvunja ukimya.
“Ndiyo namfahamu na mtu huyo ni mimi”. Jibu la Hidaya likapelekea fikra zangu zimezwe na mduwao wa aina yake huku kwa sekunde kadhaa nikimtazama katika namna ya kutoamini maneno yale. Loh! hatimaye nikashusha pumzi taratibu na kuulegeza uso wangu huku nikiliruhusu tabasamu jepesi kuchomoza usoni mwangu kisha nikasogeza kiti changu vizuri na kuketi.
“Kwa kweli sikuwahi kufikiria kama mtu aliyetuma Fax ile ungekuwa ni wewe Hidaya. Mh! Kweli Chifu alikuwa na maana kubwa kukuleta hapa”. Nikaongea huku nikiangua kicheko hafifu kisha kicheko kile kilipofika ukomo nikaendelea.
“Hata hivyo ni matumaini yangu kuwa huwezi kutuma Fax yenye ujumbe mzito kama ule ukiwa katika namna ya kufanya mizaha yako kama tulivyokuzoea. Hili ni jambo nyeti sana Hidaya na naamini kuwa ulifanya uchunguzi wa kutosha wa kujiridhisha kabla hujaamua kutuma Fax ile”
“Mh! Tibba yaani hata kama napenda kufanya mzaha lakini siwezi kufanya mzaha katika jambo nyeti kama hili”. Hidaya akaongea kwa kusononeka huku akionekana kutopendezwa na kauli yangu. Hata hivyo nikatabasamu kidogo kulainisha maongezi yetu kisha nikamchombeza Hidaya utani kwa kumkonyeza tukio ambalo lilimpelekea na yeye atabasamu kidogo. Utulivu uliporejea mahala pake nikavunja ukimya.
“Nataka kufahamu kuwa ni mazingira gani yaliyokufanya uamini kuwa Balozi Adam Mwambapa ametekwa”. Swali langu likampelekea Hidaya aupishe utulivu kidogo huku akionekana kufikiri jambo kisha akaniambia.
“Ilikuwa ni muda wa saa nane, usiku wa kuamkia siku ya jana, muda mfupi baada ya tukio la jaribio la mapinduzi ya kijeshi kufanyika hapa Burundi. Asubuhi ya siku ile ya kuelekea mapinduzi haya Balozi Adam Mwambapa hakufika hapa ofisini kwake kama ilivyozoeleka pasipo kutanguliza taarifa yoyote jambo ambalo lilikuwa siyo la kawaida. Ilipofika saa tano asubuhi wafanyakazi wa hapa sote tukaingiwa na wasiwasi kwani ile haikuwa hali ya kawaida na kwa kuwa taratibu za kazi yangu nazifahamu vizuri niliamua kupiga simu ya nyumbani kwake”
“Balozi Adam Mwambapa anaishi wapi hapa jijini Bujumbura?”. Nikamuuliza Hidaya huku nikimtazama usoni kwa makini.
“Chausée P.L. Rwagasore nyumba namba 26. Nadhani kadiri utakavyoendelea kukaa hapa Bujumbura utaizoea vizuri mitaa ya jiji hili”. Hidaya akaweka kituo huku akinitazama kama ambaye alikuwa akitarajia kusikia swali lingine kutoka kwangu.
“Wakati unasiliana na Balozi Adam Mwambapa wewe ulikuwa wapi?”
“Niliwasiliana naye nikiwa hapa ofisini kupitia simu ya mezani ya idara yangu”. Jibu la Hidaya lilikuwa la kweli na la hakika.
“Baada ya hapo nini kilifuata?”
“Baada ya miito kadhaa hatimaye simu ya nyumbani ya Balozi Adam Mwambapa ikapokelewa na kwa kweli tukio lile lilinitia faraja sana moyoni.
“Nani aliyepokea hiyo simu?”
“Alikuwa ni Balozi Adam Mwambapa mwenyewe na baada ya kumuuliza kama kulikuwa na tatizo lolote lililompelekea kutokufika ofisini siku ile akaniambia kuwa nisiwe na wasiwasi wowote kwani alikuwa akijiandaa kwenda kuhudhuria mkutano wa dharura ulioandaliwa na viongozi waandamizi wa serikali ya Burundi hapa jijini Bujumbura.
Maelezo ya Hidaya yakawa yamenishtua kidogo na kunipelekea nianze kuunda hoja za kila namna kichwani mwangu ingawa nilipomtazama Hidaya sikuweza kuona tashwishwi yoyote usoni mwake.
“Balozi Adam Mwambapa alikwambia kuwa huo mkutano wa dharura ungefanyikia wapi?”
“New Parador Residence. Ni hoteli moja yenye ukumbi wa kisasa wa mikutano na huduma ya malazi uliopo kando kidogo ya hili jiji la Bujumbura”
Maelezo ya Hidaya yakanipelekea nimtazame kwa utulivu huku nikiiruhusu taarifa ile kupenya vizuri kwenye fikra zangu.
“Balozi alikueleza kiini cha mkutano huo?”
“Ingawa alikuwa hajapewa maelezo ya kutosha juu ya mkutano huo lakini aliniambia kuwa taarifa za awali zilieleza kuwa mkutano huo ulikuwa ukihusiana na hali tete ya usalama wa hapa nchini Burundi baada ya jaribio la mapinduzi ya kieshi kufanyika”
“Nani aliyeitisha mkutano huo?’’. Nikamuuliza Hidaya kwa udadisi ingawa sikuwa na hakika kama angeweza kuwa na jibu moja la hakika.
“Hilo hakunidokeza labda kwa sababu nilisita kuendelea kumuuliza na hiyo ni baada ya kuona kuwa majibu yake yalikuwa ya mkato sana kama mtu mwenye haraka”. Hidaya akaongea huku akijitahidi kuvuta kumbukumbu kichwani mwake.
“Sasa ni kitu gani kilichokupelekea uamini kuwa Balozi Adam Mwambapa amatekwa?”. Baada ya kufikicha macho yangu kwa vidole na kupiga mwayo hafifu wa uchovu nikamuuliza Hidaya huku nikimtazama kwa makini.
“Saa nane ya usiku ule ambao asubuhi yake niliwasiliana na Balozi Adam Mwambapa nilishtushwa kutoka usingizini na mlio wa simu ya mezani iliyokuwa sebuleni kwangu”. Hidaya akaendelea kuongea huku akionekana kuzidi kuvuta kumbukumbu hata hivyo nilimkatisha.
“Simu kutoka kwa nani?”
“Ilikuwa ni simu ya kutoka nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa na mzungumzaji alikuwa ni Balozi Adam Mwambapa mwenyewe”. Hidaya akaweka kituo na hapo nikamtazama kwa shauku kama nyoka aliyeona kifaranga cha kuku. Maelezo yale yalikuwa yameanza kunivuta hivyo nikaegemeza vizuri mikono yangu pale juu mezani huku nikimtazama Hidaya kwa makini.
“Una hakika kuwa sauti ya mzungumzaji kwenye hiyo simu uliyopokea ilikuwa ni ya Balozi Adam Mwambapa mwenyewe?”. Nikamuuliza Hidaya katika namna ya kutaka kupata hakika.
“Nina hakika kabisa kwani sauti ya Balozi Adam Mwambapa ni vigumu kuisahau kama ilivyo kwa mlio wa risasi. Hidaya akanitanabaisha akichombeza utani.
“Mara baada ya kuipokea hiyo simu Balozi Adam Mwambapa alikueleza nini?”
“Sauti yake ilikuwa imetawaliwa na kitetemeshi cha hofu na mashaka wakati aliponieleza kuwa maisha yake yalikuwa hatarini kwani nyumba yake ilikuwa imevamiwa na watu wasiojulikana na hivyo alikuwa akiomba msaada wa haraka”. Maelezo ya Hidaya yakawa yameamsha hisia mpya nafsini mwangu hivyo taratibu nikauruhusu utulivu kichwani mwangu huku nikitafakari kwa kina juu ya maelezo yale.
“Walinzi wake walikuwa wapi wakati yeye akivamiwa?”
“Sikukumbuka kumuuliza swali hilo kutokana na haraka”. Jibu la Hidaya likanipelekea nishikwe kidogo na mshangao huku nikimkodolea macho. Hatimaye nikamuuliza.
“Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa tangu ulipowasiliana na Balozi Adam Mwambapa asubuhi ile hiyo simu ya saa nane usiku ilikuwa ni ya mara yenu ya pili kuwasaliana?”. Nikamuuliza Hidaya huku nikimtazama kwa makini.
“Ndiyo’’. Hidaya akanijibu kwa hakika huku akinitazama.
“Nini kilifuata baada ya hapo?’’
“Nilimdadisi Balozi Adam Mwambapa kwa kumuuliza kuwa ni kipi kilichokuwa kimempelekea ahisi kuwa alikuwa amefanyiwa uvamizi”
“Jibu lake lilikuwaje?’’ nikamuuliza Hidaya kwa shauku.
“Alinieleza kuwa nyumba yake ilikuwa imezingirwa na wavamizi hao wasiojulikana na nje kulikuwa na majibizano ya risasi kati ya walinzi wake na wavamizi hao”. Hidaya akaweka kituo akinitazama kama mtu afikiriaye jambo hali iliyonipelekea na mimi nianze kuibua maswali mengi kichwani mwangu juu ya maelezo yale ambayo sasa nilikuwa nimeanza kuhisi uzito wake.
“Baada ya hapo Balozi Adam Mwambapa alikueleza nini?”. Hatimaye nikamuuliza Hidaya baada ya kuhisi kuwa ukimya ulikuwa mbioni kushika hatamu mle ndani. Hidaya akageuka kwa utulivu kunitazama kisha akaendelea.
“Hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya mwisho kuisikia sauti ya Balozi Adam Mwambapa kwani wakati nilipokuwa nikijiandaa kutia neno ghafla sauti yake ilitoweka hewani ingawa simu ile haikukatwa. Nikiwa naendelea kusikilizia kupitia simu ile kwa mbali niliweze kuisikia sauti ya Balozi Adam Mwambapa ikilalamika na hatimaye kukoma kabisa na kisha kufuatiwa na sauti ya milio kadhaa ya risasi ambayo nayo pia haikudumu sana”. Hidaya akaweka kituo tena kama mtu afikiriaye jambo kwa kina na nilipomtazama usoni nikagundua kuwa uso wake ulikuwa umejawa sana na simanzi na hapo nikajua kuwa alikuwa amehuzunishwa sana na tukio lile la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa.
Sasa nilianza kushawishika juu ya maelezo ya Hidaya yaliyokuwa kwenye ile Fax aliyoituma jijini Dar es Salaam kwenye ofisi kuu ya idara ya ujasusi ikielezea juu ya tukio la kutekwa kwa Balozi wetu wa Tanzania nchini Burundi Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa. Kwa kweli nilimeza fundo kumbwa la mate baada ya kuhisi kazi ngumu ya hatari iliyokuwa mbele yangu.
“Sasa baada ya hapo ikawaje?. Hatimaye nikavunja ukimya na kumuuliza Hidaya kwa utulivu huku nikimtazama.
“Niliendelea kuiweka ile simu sikioni huku nikiita katika namna ya kutarajia kumpata mtu yeyote hususani miongoni mwa wale watekaji apokee simu ile na kuongea dhumuni za uvamizi ule. Lakini hilo halikutokea kwani muda mfupi uliofuata ile simu upande wa pili ilikatwa kabisa na sikuweza kusikia chochote.
Hofu ikiwa imenishika hatimaye nikairudishia ile simu mahala pale kisha nikaamka kutoka kitandani na kujiandaa haraka. Nilipomaliza kujiandaa nikatoka nje na kufunga mlango wa nyumba kisha nikawasha gari langu na kuelekea mtaa wa Boulevard du 28 Novembre nyumba namba 26 sehemu yalipokuwa makazi ya Balozi Adam Mwambapa”
Mara hii nikamtazama Hidaya na kumuona kuwa ni msichana jasiri sana kwa kitendo cha kuthubutu kuhatarisha maisha yake kwa kutembea mitaani usiku wa manane katika jiji lisilokuwa na usalama.
“Ulipofika nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa hali ilikuwaje?”. Nikamuuliza Hidaya kwa shauku huku nikimtazama kwa makini.
“Sikufanikiwa kufika kwani mapema tu nilipoanza safari yangu nikagundua kuwa mbele yangu nilikuwa nikielekea kukabiliana na kifo”
“Kwanini unasema hivyo?”
“Kwa sababu barabara nyingi za jiji la Bujumbura kwa wakati ule zilikuwa zimetawaliwa na majibishano ya risasi kati ya wanajeshi waasi na wale wanajeshi wanaoiunga mkono serikali ya rais Pierre Nkurunziza. Kwa hiyo unaweza mwenyewe kuhisi hali ya usalama ilikuwaje kwa wakati huo”. Hidaya akaniambia huku akinikata jicho la hadhari.
“Kwa hiyo uligeuza na kurudi nyumbani?”...ITAENDELEA
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom