Riwaya: Ufukwe wa Madagascar

Riwaya: Ufukwe wa Madagascar

RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 31
Mtunzi: Kelvin Mponda

zilikuwa zimeniweka njia panda katika kuhusisha utekaji wake na sababu za kijeshi au za kisiasa. Bado sikuweza kuona mwanga wowote katika fikra zangu hivyo nikaendelea mbele na uchunguzi wangu. Nikauacha ule mti uliokuwa kando ya lile bwawa la kuogelea na kupotelea kwenye giza zito lililokuwa chini ya ile miti iliyokuwa eneo lile.
Mvua kubwa bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na hivyo kunipelekea nitembee kwa tahadhari ya hali ya juu. Wakati nikiikaribia kona moja ya ile nyumba nikashtuka tena baada ya kukiona kitu fulani cheusi kisichoeleweka kikiwa kimelala ardhini umbali mfupi mbele yangu. Hali ile ikanipelekea tena niikamate vyema bastola yangu mkononi na kusogea karibu zaidi ya eneo lile huku macho yangu yakiwa makini kutazama pale chini.
Mbwa mmoja mkubwa aina ya German shephered alikuwa ameuawa kwa risasi moja ya kichwani. Nilimgundua haraka baada ya kuinama na kumchunguza kwa makini mbwa yule. Kwa sekunde kadhaa nikaupisha utulivu kichwani mwangu huku kwa makini nikiyatembeza macho yangu taratibu kulichunguza eneo lile. Kulikuwa na alama za buti za jeshi kadhaa zilizokanyaga chini eneo lile hata hivyo nilipochunguza kwa makini nikagundua kuwa alama zile zilikuwa ni za mtu mmoja. Nilipoendelea kuchunguza vizuri alama zile nikagundua kuwa zilikuwa zimepotelea kwenye nyasi laini zilizopandwa kuizunguka ile nyumba. Hivyo nikahitimisha kuwa alama zile za buti za jeshi zilikuwa ni za mmoja wa watu waliohusika katika kumteka Balozi Adam Mwambapa.
Hatimaye nikauacha ule mzoga wa mbwa na kupotelea tena gizani chini ya ile miti iliyokuwa kando ya ile nyumba. Nyuma ya ile nyumba kulikuwa na tenki moja kubwa la maji na kando ya tenki lile kulikuwa na karo kubwa la kuoshea vyombo na kufulia pembeni ya sehemu maalum ya kuanikia nguo ambayo kwa wakati ule haikuwa na nguo. Nilipoendelea kuchunguza nikakiona kibanda kidogo kando ya eneo lile na niliposogea karibu na kukichunguza kibanda kile nikagundua kuwa kile kibanda kilikuwa kikitumika kama makazi ya mbwa wa ile nyumba.
Mwishowe nikaifikia sehemu ya nyuma ya ile nyumba na kuanza kupanda ngazi chache za varandani kuelekea mlango wa nyuma wa nyumba ile. Ilikuwa ni wakati huo pale nilipouona tena mzoga mwingine wa mbwa mkubwa kama yule wa awali ukiwa umelala kwenye sakafu ya ile varanda. Kando ya yule mbwa kulikuwa na michirizi kadhaa ya damu kutoka kwenye jeraha la risasi lililokuwa kifuani kwa yule mbwa. Nikasimama kidogo kuupeleleza mzoga ule kabla ya kuendelea na safari. Hatimaye nikaufikia mlango wa nyuma wa ile nyumba na kusimama kwa utulivu nikitazama huku na kule katika namna ya kuchunguza hali ya usalama wa eneo lile. Hali bado ilikuwa shwari na sikuona dalili zozote za upinzani katika harakati zangu hivyo nikausogelea ule mlango wa nyuma wa ile nyumba na kuanza kuuchunguza kwa makini.
Jambo la kustaajabisha ni kuwa ule mlango wa nyuma wa ile nyumba ulikuwa umefungwa kwa funguo na geti lake la grili lilikuwa limefungwa kikamilifu kwa kufuli kubwa la Sorex. Kushughulika na lile kufuli na kuufungua ule mlango niliona ni kazi ambayo ingenipotezea muda mwingi hivyo nikaamua kutafuta mbadala wa namna rahisi zaidi ya kuingia mle ndani. Pembeni ya ile varanda kulikuwa na dirisha moja upande wa kushoto. Nilipolisogelea lile dirisha na kuchunguza kwa utulivu nikagundua kuwa lile lilikuwa ni dirisha la sehemu ya jiko la ile nyumba kwani pamoja na kwamba pazia la lile dirisha lilikuwa limefunika kwa ndani lakini kupitia uwazi mdogo pembeni ya dirisha lile niliweza kuona mle ndani kwa msaada wa kurunzi yangu yenye mwanga mkali.
Nikajaribu kulifungua lile dirisha kwa hila lakini sikufanikiwa kwani lile dirisha lilikuwa limefungwa ndani kwa komeo. Hivyo hatimaye nikaamua kuvunja kioo cha lile dirisha kwa pigo moja la kitako cha bastola yangu mkononi. Kile kioo kilipovunjika nikapenyeza mkono na kufyatua komeo kulifungua lile dirisha. Muda mfupi uliofuata nikawa nimefanikiwa kulifungua lile dirisha na kuingia mle ndani ya kile chumba cha lile jiko nikitabaruku.
Kwa dakika chache nikatulia mle ndani ya kile chumba cha jiko huku macho yangu yakiusindikiza kwa utulivu mwanga mkali na mwembamba wa kurunzi yangu mkononi. Kile chumba cha jiko kilikuwa kimezungukwa na makabati ya vyombo yaliyojengewa vizuri ukutani na upande wa kushoto wa chumba kile kulikuwa na sinki kubwa la kuoshea vyombo lililopakana na ukuta msafi wa marumaru nyeupe. Nilipomulika chini nikaiona sakafu imara ya tarazo kabla ya kuizima kurunzi yangu.
Hatimaye nikaufikia mlango wa kile chumba cha jiko na kuufungua taratibu katika utulivu wa hali ya juu. Ule mlango ulipofunguka nikajikuta nimetokezea kwenye korido pana lakini fupi kuelekea upande wa kulia. Kabla ya kuendelea mbele zaidi nikasimama katikati ya ile korido gizani huku nikiupima vizuri utulivu wa mle ndani. Sikusikia sauti ya kitu chochote mle ndani hivyo hali bado ilikuwa tulivu. Nikaamua kuiwasha kurunzi yangu mkononi na kumulika huku na kule katika namna ya kutaka kupata picha kamili ya mazingira yale kisha nikaizima tena. Hatua chache mbele ile korido ilikuwa imepinda kona kuelekea upande wa kushoto.
Nikaifuata ile korido kwa utulivu na nilipofika mwisho nikaziona ngazi chache za kushuka chini. Bila kusita nikaanza kuzifuata zile ngazi nikishuka chini kwa tahadhari huku bastola yangu ikiwa mkononi na baada ya safari fupi nikajikuta nimetokezea kwenye ukumbi mdogo wenye meza iliyozungukwa na viti kumi na mbili. Ile meza ilikuwa katikati ya ule ukumbi mdogo na upande wa kulia kulikuwa na sinki moja lililokuwa kwenye kona. Sinki lile lilikuwa limepakana na rafu kubwa ya vyombo iliyojengewa vizuri ukutani.
Niliposogea karibu na ile meza upande wa kulia nikaliona dirisha kubwa lakini pazia la dirisha lile lilikuwa limesogezwa kando. Nikasogea pale dirishani kwa utulivu na kutazama nje kisha nikawasha tena kurunzi yangu na kuanza kumulika mle ndani. Kupitia mandhari yale haraka nikatambua kuwa ule ulikuwa ni ukumbi wa kulia chakula wa ile nyumba na hapakuwa na kitu chochote cha maana eneo lile hivyo nikaendelea mbele zaidi na uchunguzi wangu.
Nilipofika kwenye kona moja iliyokuwa upande wa kushoto wa ule ukumbi nikauona mlango na mlango ule ulikuwa umefunguliwa nusu hivyo sikuishika pale badala yake kwa tahadhari nikaingia mle ndani. Kwa kufanya vile nikajikuta nimetokezea kwenye sebule pana yenye umbo duara. Mara baada ya kuingia mle ndani nikasimama kando ya ile sebule na kuanza kumulika kwa kurunzi yangu mkononi nikiyapeleleza mandhari yale.
Ilikuwa sebule kubwa yenye samani zote muhimu za kisasa. Kulikuwa na seti mbili za makochi ya sofa ya kifahari yaliyopangwa katika mtindo wa kuizunguka ile sebule. Sakafuni kulikuwa na zulia zuri la rangi nyekundu huku katikati ya sebule ile kukiwa na meza fupi ya kioo yenye umbo la pembe tatu. Upande wa kulia wa ile sebule kwenye kona kulikuwa na runinga pana iliyofungwa ukutani huku chini yake kukikiwa na meza fupi nyeusi yenye sistimu ya muziki, deki moja ya Dvd na kinyago kidogo cha askari shupavu akipuliza tarumbeta. Nilipomulika ukutani nikaziona picha mbalimbali za Balozi Adam Mwambapa akiwa katika hafla tofauti za majukumu ya kiserikali jijini Bujumbura. Upande wa kushoto wa ile sebule kwenye kona nyingine kulikuwa na meza fupi ya mapambo iliyotenganisha jokofu na feni. Pembeni ya meza ile kulikuwa rafu kubwa iliyopangwa vitabu na majalada mengi na juu ya rafu ile kulikuwa na vinyago vya kiafrika vilivyopangwa kwa ustadi wa hali ya juu. Kutoka pale nilipokuwa nimesimama upande wa kulia nikauona mlango mkubwa wa sebuleni ile katikati ya madirisha mapana ya vioo yaliyofunikwa kwa mapazia marefu. Kulikuwa pia na mlango mwingine upande wa nyuma wa ile sebule na nilipochunguza nikagundua kuwa ule ulikuwa ni mlango wa kuelekea kwenye vyumba vya kulala vya ile nyumba.
Nilitaka kupata tathmini ya kina juu ya lile tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa mle ndani ya ile nyumba hivyo ikanibidi nisogee katikati ya ile sebule na kuanza kumulika kwa ile kurunzi yangu mkononi. Taswira iliyojengeka machoni mwangu ni kuwa kulikuwa na uharibifu mkubwa uliofanywa pale sebuleni kupitia mashambulizi ya risasi. Baadhi ya makochi ya sofa yaliyokuwa pale sebuleni yalikuwa yametobolewa vibaya kwa risasi. Kioo cha dirisha moja kilikuwa kimevunjika. Kabati kubwa la pale sebuleni upande wake mmoja ulikuwa umevunjwa na simu ya mezani iliyokuwa juu ya stuli ndefu kando ya kochi mojawapo la pale sebuleni ilikuwa imepigwa chini na kuvunjika vipandevipande. Mpangilio wa samani za pale sebuleni ukanitanabaisha kuwa kulikuwa kumetokea varangati la kukata na shoka wakati watekaji walipovamia nyumba ile.
Kwa kweli hali ya pale sebuleni ilikuwa segemnege. Nikiwa nimesimama katikati ya ile sebule nikajikuta nikivutiwa na nyaraka za kiofisi zilizokuwa kwenye kabati la pale sebuleni. Hivyo nikaanza kuzitupa hatua zangu kwa utulivu kulifikia lile kabati. Mle ndani kulikuwa na giza zito. Nilitamani kuwasha taa ya pale sebuleni hata hivyo nafsi yangu ilinionya kuwa kwa kufanya vile huwenda ningeweza kuyavuta macho ya adui ambayo yangekuwa jirani na eneo lile.
Hatimaye nikawa nimelifikia lile kabati na kwa msaada wa kurunzi yangu mkononi nikaanza kufanya upekuzi. Nilipovichunguza vile vitabu nikagundua kuwa vilikuwa ni vitabu vya kiofisi vinavyohusu masuala mbalimbali ya mahusiano ya kimataifa hivyo nikaachana navyo na kuanza kuchangamkia majalada yaliyokuwa yamepangwa sehemu ya chini ya lile kabati. Nikayapekuwa yale majalada kwa utulivu moja baada ya lingine hata hivyo nilimaliza zoezi lile pasipo kupata kitu chochote cha kunisaidia katika harakati zangu kwani ndani ya majalada yale niliambulia kukuta na ajenda za vikao vilivyopita, barua za kiofisi zilizoegemea masuala ya utendaji, vimemo vya hapa na pale na barua tofauti za mialiko ya kitaifa.
Mwishowe nikaachana na yale majalada na kuanza kufanya upekuzi katika droo za chini za lile kabati. Droo ya kwanza ilikuwa imejaa matoleo ya zamani ya magazeti mbalimbali ya nchini Burundi na mengine ya nchi za jirani. Droo ya pili ilikuwa na bahasha moja kubwa ya kaki yenye vyeti mbalimbali vya utumishi bora alivyowahi kutunukiwa balozi Adam Mwambapa wakati wa utumishi wake. Hivyo bado hapakuwa na taarifa zozote za maana za kuweza kunisaidia.
Wakati nikifungua droo ya tatu ya lile kabati ili niendelee na upekuzi wangu ghafla hisia fulani zikanijia akilini na kuniletea maradhi ya hofu. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu na hapo nikaanza kuhisi kijasho chepesi kikianza kushuka mgongoni kabla ya koo langu kukauka. Nilihisi kuwa kulikuwa na mtu aliyesimama hatua chache nyuma yangu ingawa sikuweza kuthibitisha jambo hilo kwa haraka badala yake nikaikamata vyema bastola yangu mkononi na kugeuka nyuma yangu taratibu. Sikufanikiwa kwani muda ule nikahisi chuma baridi kikitekenya kisogo changu.
“Tupa bastola yako chini komredi’’. Sauti nzito ya kiume yenye lafudhi mbovu ya kiswahili cha kirundi ikanionya kutoka nyuma yangu. Kwa sekunde kadhaa nikajikuta nimeganda kama sanamu huku maamuzi yangu yakiwa njia panda.
“Jitahidi kidogo kuwa msikivu komredi huu siyo wakati wa kuleta hila. Nimesema tupa bastola yako chini’’. Ile sauti nyuma yangu ikarudia kunionya na mara hii sikuhisi mzaha wowote hivyo taratibu nikaiweka chini bastola yangu huku nikishindwa kabisa kuamini kama nilikuwa nimejiingiza mtegoni.
“Wewe ni nani?”. Nikauliza kwa sauti ya kupwaya huku nikigeuka taratibu na kutazama nyuma yangu hata hivyo sikufanikiwa badala yake nikajikuta nikikabiliana na maumivu makali ya kofi zito la sikioni lililonipelekea nianze kuhisi kichefuchefu.
“Tulia hivyohivyo kenge mkubwa wewe”. Yule mtu akaendelea kunitahadharisha huku akisogea karibu na kuipiga bastola yangu mbali na eneo lile.
“Mko wangapi?’’. Yule mtu akaniuliza huku akinipekuapekua maungoni na namna ya upekuaji ule ulikuwa na kila namna ya kunidhalilisha.
“Tuko watatu”. Nikaamua kudanganya pasipo kufahamu kuwa uongo ule ungekuwa na madhara gani huko mbeleni.
“Muongo wewe sasa hao wenzako wako wapi?’’. Yule mtu akaniuliza kwa kisirani huku akinipekua kwenye mifuko ya nyuma ya suruali yangu huku akinipapasa makalio yangu. Kwa kweli tukio lile lilinipandisha sana hasira hata hivyo sikuwa na namna ya kufanya kwani ule mtutu wa bastola ya yule mtu ulikuwa bado ukinitazama kisogoni nyuma yangu.
“Sasa kama mimi ni muongo mbona unawaulizia hao wenzangu?”. Nikamuuliza yule mtu nyuma yangu hata hivyo sikujibiwa badala yake nikajikuta nikishushiwa kipigo cha nguvu cha ngumi kavu mgongoni na mbavuni hali iliyonipelekea nianze kuhisi kichomi huku nikihema ovyo.
“Jibu vizuri swali nililokuuliza na usilete mambo ya siasa”. Yule mtu akamalizia kwa kunizaba kofi moja la shingoni na nguvu ya mkono wake iliyotumika ikanitanabaisha kuwa nilikuwa nimeingia kwenye mikono ya binadamu mbabe mwenye nguvu za ajabu aliyekomaa mwili wake kama mti wa mninga. Kisha yule mtu akanikwida shingoni na kunigeuza katika namna ya kunifanya nimtazame. Mbele yangu alikuwa amesimama mwanaume mrefu kunizidi mimi na mweusi kama lami huku akiwa amenyoa upara na kukipelekea kichwa chake kilichosongwa na mishipa mingi ya damu iliyosambaa ovyo kama mizizi ya mmea wa mhindi kionekane vizuri. Ile njemba ilikuwa kipande cha mtu chenye misuli imara ya nguvu. Kifuani alikuwa amevaa fulana mchinjo ya jeshi iliyokibana vyema kifua chake kiasi cha kunipelekea nidhani kuwa fulana ile ingetatuka muda mfupi ujao. Yule mtu chini alikuwa amevaa suruali ya kombati na miguuni alikuwa amevaa buti ngumu za jeshi. Mkononi alikuwa ameshika bastola ambayo haraka nilipotazama kwa kurunzi yangu nikagundua kuwa ilikuwa ni aina ya 22 Caliber Revolver na hapo matumaini ya kutoka salama kwenye himaya ya mtu yule yakapotea kabisa.
“Wenzako wako wapi?’’. Yule mtu akaniuliza huku akikunja sura kama aliyeona chembe ya mavi kwenye sahani ya wali hotelini.
“Nimewaacha mjini”. Nikaongea kwa utulivu huku akili yangu ikianza kufanya kazi. Yule mtu akanitazama kwa utulivu kama ambaye anafikiri jambo kisha akaniuliza.
“Mbona tumeambiwa kuwa umekuja peke yako?”. Swali la yule mtu likanifanya niyapeleke macho yangu kumtazama usoni huku dhahiri nikionesha kushtushwa na maelezo yake...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 32
Mtunzi:Kelvin Mponda

...“Mmeambiwa na nani?”. Nikamuuliza yule mtu hata hivyo hakunijibu badala yake muda uleule yule mtu akanikwida shingoni na kiunoni kisha akaninyanyua juu juu na kunibwaga vibaya kwenye lile kabati. Lile kabati likapasuka vipandevipande na kupelekea vitabu na yale majalada kutawanyika ovyo sakafuni. Nikapiga yowe kali la maumivu huku nikijitahidi kuwahi kusimama lakini ilikuwa kazi bure kwani yule mtu aliniwahi kabla sijasimama akanikwida tena na kuninyanyua juu. Nikijitahidi kujitetea kwa kila namna nikirusha ovyo miguu na mikono lakini bado haikunisaidia kitu kwani lile jitu likanibeba mzegamzega na kwenda kunibwaga tena kwenye ile meza fupi ya kioo iliyokuwa pale sebuleni. Japokuwa nilijitahidi kwa kila namna kujihami lakini lile jitu lilikuwa na nguvu nyingi kama roboti hivyo likanibwaga juu ya ile meza kama furushi. Ile meza ikapasuka vipandevipande na baadhi ya vioo vyake vikanichanachana mikononi. Nikapiga tena yowe huku maumivu makali yakisambaa mwilini huku nikianza kuingiwa na hofu ya kudhibitiwa kikamilifu. Lile jitu likaangua kicheko cha dhihaka na kujipigapiga kibabe kifuani kama sokwe mtu.
Nikiwa nimeanza kuhisi hatari ambayo ingenikaribia endapo ningeendelea kuruhusu mashambulizi yale zaidi nikakumbuka haraka ule upande ambao bastola yangu ilikuwa imetupwa na teke la lile jitu. Hivyo nikajiviringisha kwa kasi sakafuni kuelekea ule upande ilipoangukia bastola yangu. Hata hivyo sikufanikiwa kwani lile jitu ni kama tayari lilikuwa limeshtukia dhamira yangu hivyo likaniwahi kwa kunitandika teke makini la tumbo lililonitupa kando kama paka mwizi. Sikuona tena kama kungekuwa na namna nyingine ya kujiokoa kutoka kwenye mikono matata ya lile dubwana hivyo nikawahi kujikaza na kusimama huku hasira za kudhibitiwa zikiwa zimenipanda kichwani kama mbogo aliyejeruhiwa.
Lile jitu jeusi liliponifikia nikawahi kulitupia mapigo manne ya ngumi kavu za tumbo. Jambo la kushangaza ni kuwa lile jitu halikutia jitihada zozote za kujitetea badala yake likanyanyua mikono yake juu huku likiangua kicheko cha dharau na kutikisa kichwa chake kibabe katika namna ya kunionesha kuwa mapigo yangu hayakuwa yamefua dafu. Nikiwa katika hali ya kushangazwa na tukio lile jitu likanizaba kofi moja zito likitumia mgongo mkavu wa kiganja chake. Pigo lile likanipelekea nijihisi kama niliyepigwa na kipande cha mbao kavu ya mpingo. Nikarushwa na kutupwa sakafuni huku nikihisi maumivu makali yasiyoelezeka. Kwa kweli hali yangu ilizidi kuwa mbaya na kabla sijafikiria namna ya kufanya nikaliona lile jitu likinifuata pale chini. Sasa nilikuwa makini zaidi kwani nilianza kuona hatari kubwa ya kukamatwa mzimamzima kama siyo kupoteza maisha kabisa endapo ningeendelea kupokea mkongʾoto wa lile dubwana. Hivyo nikajipanga kujihami zaidi kwa kufanya mashambulizi ya nguvu na yenye tija.
Lile jitu likionekana kunogewa na mtindo wake mmoja wa kuninyanyua juu na kunibwaga chini kama mcheza miereka mara aliponifikia pale chini akainama tena ili aninyanyue na kunibwaga. Mara hii hakufanikiwa kwani niliwahi kujibetua na kumtandika pigo moja takatifu la teke la kidevu lililompelekea ajingʾate ulimi na kuangua kilio kama mtoto mdogo huku akijishika mdomoni. Nikawahi kusimama wakati lile jitu likiendelea kupepesuka na hapo nikampelekea mapigo matatu makini ya chapuchapu ya kareti shingoni na tumboni kwake hata hivyo sikufua dafu kwani yule mtu aliyakwepa mapigo yangu kama mchezo akiyapangusia mbali.
Nikabadili mtindo wa mapigano nikitumia Kung fu na hapo nikatupa mapigo matatu makini. Hong Cha, Lei tai na Tang Soo Do hata hivyo bado sikuweza kufua dafu kwani yule mtu alikuwa mpiganaji wa kiwango cha juu huku akionekana kuwa makini sana kuzisoma nyendo zangu. Hata hivyo nilikuwa nimelipunguza kasi kwa kiasi kikubwa kiasi cha kumpelekea atumie wake muda mwingi kujihami badala ya kushambulia. Miaka sita ya mafunzo yangu ya kijasusi niliyokuwa nimeyapata nchini China katika chuo kimoja cha sanaa ya juu ya mapigano Martial Arts. Mafunzo ambayo nilikuwa nimehitimu vizuri katika alama za juu sana kiasi cha kuridhisha kuweza kukabiliana na aina yoyote ya mpiganaji. Hivyo nilipoona mapigo yangu hayaelekei kuniletea majibu ya haraka nikaamua kubadili tena namna ya upambanaji nikitumia mtindo mwingine wa mapigano wa Kung fu uitwao Zui quan au pia mtindo huo ukifahamika kama Drunken first. Mtindo mzuri wa mapigano wenye mapigo hatari kama ule wa Cao guojiu unaonifanya nionekane kama mlevi aliyechanganyikiwa huku lengo langu kubwa likiwa ni kushambulia sehemu laini za mwili wa lile dubwana huku nikimpotezea umakini katika malengo yake.
Wakati nikilikaribia tena lile jitu nikagundua haraka kuwa lilikuwa limeshtukia hila yangu ingawa halikuweza kufahamu vizuri mikakati niliyokuwa nayo. Hivyo lile jitu likaanza kutupa ngumi mfululizo kichwani mwangu lakini mara hii ilikuwa ni kazi bure kwani nilizikwepa ngumi zake kwa ulaini pasipo kutumia nguvu kubwa mwilini huku nikisogea huku na kule na kama mlevi lakini wakati huo nikiendelea kumdokoa taratibu sehemu laini za mwili wake kama mbavuni, tumboni, shingoni na kichwani.
Lile jitu likaanza kuchanganyikiwa huku likishindwa kuelewa namna ambavyo ushindi ulivyokuwa ukihamia kwangu taratibu. Lile jitu lilipoona kuwa hali inazidi kuwa mbaya likawa linajitahidi kunikwepa na kukaa mbali na mimi huku likifuatilia nyendo zangu kwa makini na kwa hakika ile ilikuwa mbinu makini iliyoninyima nafasi nzuri ya kulifikia lile jitu kirahisi. Hivyo lile jitu likawa likinishambulia zaidi kwa mateke.
Teke la kwanza lililorushwa na lile jitu niliwahi kuliona mapema hivyo nikainama chini kidogo na kuliacha likikata upepo bila mafanikio lakini wakati nikifurahia utundu wangu teke lingine likaja na kukibamiza vibaya kifuani kiasi cha kufanikiwa kunitupa nyuma huku nikiyumbayumba ovyo. Pigo lingine la teke makini la Side-snap kick nikawahi kulipangua lakini lile jitu lilikuwa na nguvu nyingi kwani pamoja na kufanikiwa kulipangua lile pigo lakini bado nilihisi maumivu makali sana mikononi huku nikipepesuka na hatimaye kuanguka chini. Lile jitu kuona vile likapata matumaini ya kuibuka na ushindi hivyo likawahi kunitandika teke lingine la mtindo wa mapigano ya kijapani liitwalo Mae geri hata hivyo nilikuwa makini kuwahi kujiviringisha kando ya eneo lile. Hata hivyo lile jitu halikunipa nafasi ya kutabaruku badala yake akanifuata na kutupa teke lingine ambalo haraka nililikwepa kwa kujitupa kando sakafuni kisha nikaizungusha miguu yangu chini kwa mtindo wa mapigano wa kibrazil itwao Capoeira nikilichota lile jitu mtama maridadi wa kiufundi uliompaisha hewani kabla ya kutua sakafuni kwa matako na hapo tusi zito likamponyoka mdomoni.
Lile jitu likawahi kusimama lakini nikiwa tayari nimejiandaa kwa tukio lile nikawahi kujibetua kwa sarakasi ya Sama soti kisha nikamchapa pigo moja takatifu la Flying kick na kumtia udhaifu mkubwa kifuani na kichwani kwake. Pigo lile likapelekea lile jitu lirudi kinyumenyume na kupepesuka ovyo huku likipiga mayowe ya hofu. Sikutaka kumkawiza hivyo nikaruka tena hewani na kumchapa pigo lingine la teke la kijapani liitwalo Mikazuki geri ambalo lilikata mzizi wa fitina kwani lile jitu hatimaye likaanguka chini kama mti wa mbuyu na kuvikalia bila kupenda vile vipande vya kioo cha ile meza kilipasuka pale chini sakafuni. Lile jitu likaguna kwa maumivu makali hata hivyo likajikaza na kuwahi kusimama kama Zombi kisha likajipukuta na kujiweka sawa halafu likaanza kunifuata kwa hasira kama Mbogo. Nikajitahidi kulikwepa bila mafanikio na liliponikaribia likatupa pigo moja makini la Kung fu kifuani kwangu lililonisababishia maumivu makali sana. Nikapepesuka na kurudi nyuma na hilo likawa kosa kubwa kulifanya kwani lile jitu likanichapa pigo la teke matata la kijapani liitwalo Yoko geri shingoni na kama nisingefanya jitihada za haraka za kulipoza pigo lile huwenda lingenivunja shingo kama siyo kunisambaratisha kabisa. Lile jitu kuona vile likanogewa na matunda ya kazi yake hata hivyo mara hii bahati haikuwa kwake kwani lilipotupa pigo lingine la teke nikawahi kulidaka na hapo nikapata nafasi nzuri ya kumtandika teke la korodani lililomsababishia maumivu makali na kumpelekea abweke kama mbwa mwizi huku akirukaruka kama aliyekanyaga kaa la moto wakati huo mimi nikijirusha upande wa pili.
Tukio lile likawa limelipandisha hasira sana lile jitu kwani nililiona likikimbia haraka kuelekea upande ule ile bastola yake ilipoangukia hata hivyo niliwahi kulizuia kwa kulisukumia kochi moja la pale sebuleni kwa mguu wangu. Lile jitu kuona vile likaanza kuokota vitu na kuanza kunirushia kwa hasira na kwa kuwa sote tulikuwa gizani ikaniwia vigumu kuvikwepa vitu vile hivyo nikawa nikihaha huku na kule. Kumbe lile jitu lilikuwa likinifanyia hila kwani wakati nikifikiria namna ya kufanya katikati ya giza lile mara nikajikuta tayari nimeenea kwenye kabari yake matata. Nikajikuta nikifurukuta bila mafanikio kwani lile jitu lilizidi kuikaza vizuri mikono yake na kuninyima kuvuta hewa kwa urahisi. Sikutaka kufa kifo laini cha kondoo anayechinjwa huku ameinamisha shingo mwenyewe hivyo nikaamua kuanzisha purukushani na mikikimikiki ya kuvuruga malengo. Hata hivyo lile jitu halikuniachia kwani mikono yangu sasa lilikuwa limeibana kisawasawa na kwa kuwa lile jitu lilikuwa na nguvu nyingi hali ikazidi kuniwia ngumu lakini hatimaye nikapata ufumbuzi.
Nilikusanya nguvu za kutosha kisha nikalitandika kichwa cha nguvu lile jitu nyuma yangu na kuupasua vibaya mwamba wa pua yake. Lile jitu likapiga yowe kali la maumivu huku likiniachia bila kupenda na hapo nikageuka na kulitupia pigo kali la kareti shingoni lililolipelekea lile jitu lipepesuke. Ulikuwa ni wakati mzuri wa kufunga kazi hivyo nikatupa ngumi mbili kavu tumboni mwake na kisha kuhitimisha ngwe ile kwa pigo makini la Jeet Kune Do, a very nice finishing kick la kichwani. Lile jitu likapiga yowe kali la maumivu wakati lilipojipigiza kichwa chake ukutani kisha likaanguka chini na kutulia kimya. Nilipolisogelea karibu kulichunguza nikagundua kuwa tayari lilikwisha kata roho huku shingo yake ikiwa imevunjika na damu ikimtoka puani na mdomoni.
Kwa sekunde kadhaa nikabaki nimesimama nikilitazama lile jitu huku nikitweta ovyo na kijasho chepesi kikinitoka usoni. Kwa kweli nilikuwa nimechomoka na ushindi mwembamba wa pambano kali la kukata na shoka. Hatimaye nikalisogelea lile jitu pale chini na kuanza kulipekua mifukoni. Sikupata kitu chochote cha maana zaidi magazine moja ya bastola iliyojaa risasi.
Sasa nilikuwa na hakika kuwa uwepo wangu pale jijini Bujumbura ulikuwa ukitambulika rasmi na kikundi cha watu hatari ambao kwa namna moja au nyingine nisingesita kuwahusisha moja kwa moja na lile tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa. Nikalikumbuka lile gari jeupe Landcruiser Hardtop lililokuwa likinifuatilia nyuma yangu muda mfupi baada ya kutoka kwenye lile jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Burundi ambalo ndani yake kulikuwa na wanajeshi. Kisha nikalitazama lile jitu pale chini ambalo lilikuwa limevaa sare za jeshi na hapo nikatambua kuwa nilikuwa nikielekea kukabiliana na watu wa namna gani katika safari yangu ya kijasusi.
Sikuwa na muda zaidi wa kuendelea kupoteza eneo lile hivyo haraka nikaanza kuitafuta bastola na ile kurunzi yangu ndogo ya kijasusi kule ilipoangukia. Ndani ya muda mfupi nikawa nimefanikiwa kuipata ile bastola na ile kurunzi hivyo nikawa nimevirudisha tena kwenye himaya yangu. Nilipomaliza nikaelekea tena kwenye lile kabati na kumalizia upekuzi wangu kwenye zile droo za chini pasipo kuambulia kitu chochote cha maana. Sikuona dalili za kupata kitu chochote cha kunisaidia pale sebuleni hivyo nikaikamata vyema bastola yangu mkononi na kuelekea vyumbani nikipitia kwenye mlango uliokuwa nyuma ya ile sebule mara baada ya kupanda ngazi chache za eneo lile. Wakati nikiendelea na safari ile nikajipa umakini zaidi hasa baada ya kulikumbuka lile tukio la uvamizi nililofanyiwa na lile jitu muda mfupi uliopita.
Ule mlango ulikuwa wazi hivyo mara baada ya kumaliza kuzipanda zile ngazi chache kutokea pale sebuleni nikajikuta nimetokezea kwenye korido pana iliyokuwa ikitazamana na milango minne. Milango miwili upande wa kushoto na milango miwili mingine upande wa kulia huku mlango mmoja ukiwa mwisho wa ile korido. Mara baada ya kuingia kwenye ile korido nikasimama kwa sekunde kadhaa nikimulika kwa kurunzi yangu mkononi katikati ya giza nene lililokuwa limetanda kwenye ile korido. Sikuona kiashiria chochote cha uhai kwani ile korido ilikuwa imemezwa na utulivu wa hali ya juu. Sauti pekee iliyosikika ilikuwa ni ile ya mvua kubwa iliyokuwa ikianguka juu kwenye paa la ile nyumba. Nikiwa nimeanza kuridhishwa na hali ya utulivu wa mle ndani nikaanza kujongea taratibu nikielekea chumba cha kwanza cha kwenye ile korido kilichokuwa upande wa kushoto. Muda mfupi uliofuata nikawa nimefika na nilipojaribu kuufungua mlango wa kile chumba nikagundua kuwa ule mlango haukuwa umefungwa hivyo nikausukuma taratibu na kuingia mle ndani.
Chumba kilikuwa kipana chenye nafasi ya kutosha. Upande wa kushoto kulikuwa na kabati kubwa la nguo la ukutani hata hivyo niliposogea karibu na kulichunguza vizuri lile kabati sikuona kitu chochote ndani yake zaidi ya suruali moja ya kiume iliyotundikwa kwenye ufito mwembamba huku ikionekana kutelekezwa kwa muda mrefu kwa namna ilivyokuwa imeshika vumbi. Pembeni ya kabati lile kulikuwa na meza ndogo ya mbao yenye miguu mitatu iliyochongwa vizuri kando ya kochi moja la sofa. Nilipogeuka na kutazama katikati ya kile chumba nikaona kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita kilichotandikwa shuka safi za rangi ya nyeupe. Kando ya kitanda kile kulikuwa na meza ndogo yenye droo mbili na juu ya meza ile kulikuwa na taa ndogo ya Lampshade. Nikaisogelea ile meza ndogo na kuzichunguza zile droo mbili hata hivyo sikuona kitu chochote mle ndani hivyo nikazifunga na kutazama sehemu ya chini ya kile kitanda ambako pia sikuona kitu chochote cha maana. Nikaendelea kupeleleza sehemu nyingine za kile chumba nikitarajia kupata kitu chochote cha kunisaidia katika harakati zangu. Sikupata kitu chochote mle ndani hivyo hatimaye nikaelekea kwenye mlango wa kile chumba na kutoka nje.
Chumba cha pili kukifanyia uchunguzi kwenye ile nyumba kilikuwa ni kile kilichokuwa kikitazamana na kile cha awali ambapo haraka nilipokichunguza nikagundua kuwa kilikuwa kikitumika kama stoo. Ndani ya kile chumba kulikuwa na vifaa vya kutunzia bustani na mazingira kwa ujumla kama jembe, reki, panga, buti za mvua na vifaa vingine vidogo vidogo. Kulikuwa pia na magunia matatu ya mpunga yaliyopangwa vizuri mle ndani na ziadi ya vile sikuona kitu kingine chochote cha maana.
Chumba kilichofuata mbele upande ule wa kulia wa ile korido kilikuwa ni chumba cha mazoezi kutokana na vifaa vya kufanyia mazoezi vilivyokuwa mle ndani huku sakafu yake ikiwa imefunikwa kwa zulia zuri la rangi nyekundu. Hivyo mle ndani bado hapakuwa na kitu chochote cha maana katika harakati zangu. Hatimaye nikakiacha kile chumba na kutoka nje nikielekea kwenye chumba kingine cha upande wa pili kilichokuwa kikitazama na kile nilichotoka.
Nilipoingia ndani ya kile chumba haraka nikagundua kuwa mazingira yake hayakuwa tofauti sana na ya kile chumba cha mwanzo. Hata hivyo niligundua kuwa kile chumba kilikuwa kikitumika na mwenyeji wake kutokana na mandhari ya mle ndani ingawa nilipochunguza...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 33
Mtunzi:Kelvin Mponda

vizuri sikuona dalili zozote za uwepo wa mtu mle ndani. Hata hivyo sikukata tamaa badala yake nikafanya upekuzi wa hapa na pale ambao pia haukuniletea manufaa yoyote hivyo mwishowe nikaamua kutoka nje ya kile chumba mikono mitupu.
Chumba kilichosalia kilikuwa ni kile ambacho mlango wake ulikuwa mwisho ukitazamana na ile korido. Nikausogelea mlango wa kile chumba kwa tahadhari huku bastola yangu ikiwa mkononi. Nilipofika karibu nikagundua kuwa mlango wa kile chumba ulikuwa nusu wazi hivyo nikanyata taratibu na kuingia mle ndani. Mara baada ya kuingia mle ndani ya kile chumba kwa sekunde kadhaa nikasimama kando ya ule mlango huku nikiupima utulivu wa mle ndani. Kupitia mwanga hafifu wa taa za nyumba za jirani kwa mbali niliweza kuona mapazia marefu na mepesi ya madirisha mawili ya kile chumba yakipepea kwa utulivu na hivyo kuiruhusu miali hafifu ya ule mwanga kupenya madirishani na kuingia mle ndani. Nikayatembeza macho yangu taratibu mle ndani nikichunguza kama kungekuwa na mjongeo wowote wa kiumbe hai mle ndani. Hali bado ilikuwa tulivu lakini haikunipelekea niamini kuwa nilikuwa sehemu salama.
Nikiwa nimeikamata vyema bastola yangu mkononi pamoja na ile kurunzi ndogo kwa tahadhari nikaanza kukatisha katikati ya kile chumba nikielekea upande mmoja wenye dirisha. Wakati nikifanya vile ghafla nikashtushwa na sauti hafifu ya mtu akikohoa mle ndani. Haraka nikageuka kwa tahadhari huku bastola yangu ukiwa tayari kufanya kazi. Ile sauti ya mtu anayekohoa ikasikika tena na mara moja nikagundua kuwa ilikuwa ikitokea kwenye kona moja ya kile chumba iliyokuwa upande wa kulia. Haraka nikawasha kurunzi yangu na kumulika kwenye ile kona na nilichokiona mbele yangu kikanishtua kama siyo kunifedhehesha.
Kijana mdogo alikuwa ameegemea kwenye kona ya chumba kile huku akihema kwa tabu sana. Alikuwa amevaa suruali nyeusi ya kitambaa na fulana nyeupe hata hivyo ile fulana ilikuwa imelowa damu chapachapa. Yule kijana alikuwa amejishika tumboni kwa mikono yake miwili katika namna ya kupambana na maumivu makali ya tumbo. Bado kulikuwa na kila dalili uhai machoni mwake hivyo nikamsogelea taratibu pale chini kwenye kona alipoketi na wakati nikimsogelea haraka nikagundua kuwa kulikuwa na michirizi ya damu iliyotokea kwenye mlango wa kile chumba hadi pale chini yule kijana alipokuwa ameketi. Sasa nilifahamu kuwa ile michirizi ya damu ilikuwa imetokana na jeraha lililokuwa kwenye sehemu ya tumbo la yule kijana. Loh! ile damu ilikuwa nyingi sana. Hatimaye nikamfikia yule kijana kwa tahadhari kisha nikainama na kumchunguza huku nikishindwa kuelewa kilichomsibu. Katika hali nisiyotarajia yule kijana akafumbua macho ghafla kisha akiniongelesha kwa sauti hafifu akinisihi.
“Sʾil vous plaît ne me tuez pas’’. Tafadhali usiniue. Namna ya uzungumzaji wa kifaransa cha yule kijana haraka ukanitanabaisha kuwa yule kijana alikuwa mtanzania mwenzangu.
“Wewe ni mtanzania?”. Nikamuuliza yule kijana kwa shauku. Yule kijana akanitazama kwa mshangao kabla ya kutabasamu kisha akanijibu kwa sauti hafifu huku akijitahidi kumeza funda la mate.
“Ndiyo!”. Yule kijana akanijibu kwa sauti dhaifu huku nikishangazwa na tabasamu lake katikati ya hali ile mbaya ya kiafya aliyokuwanayo. Nilipomchunguza vizuri yule kijana tumboni nikakiona kisu kikubwa kikiwa kimezama tumboni mwake na hivyo sehemu ya mpini tu wa kisu kile kubaki nje.
“Tafadhali naomba unipeleke hospitali vinginevyo nitafia hapa”. Yule kijana akinisihi kwa sauti hafifu iliyopoteza matumaini hata hivyo nilipomtazama kwa makini nikagundua kuwa endapo ningemchukua na kumuwahisha hospitali ni dhahiri kuwa nisingefikanaye mbali. Kulikuwa na kila dalili kuwa yule kijana angekufa katika muda mfupi sana kuanzia pale kutokana na kizidiwa na maumivu makali na damu nyingi aliyopoteza katika lile jeraha tumboni mwake. Roho yake ni kama ilikuwa ikiningʾinia kwenye uzi mwembamba sana wa pamba chakavu ambao muda wowote ungekatika. Hata hivyo sikutaka kumkatisha tamaa badala yake nikampa matumaini.
“Ondoa shaka wala hautakufa kwani nimefika hapa kukusaidia”. Nikaongea kwa utulivu huku nikikiegemeza kichwa chake mkononi mwangu huku nikimsogelea karibu ili nimsikie vizuri.
“Jina lako nani?”. Nikamuuliza
“Naitwa Sundi”. Yule kijana akaongea kwa sauti dhaifu ya mkoromo.
“Wewe ni mfanyakazi wa humu ndani?”. Nikamuuliza.
“Ndiyo”. Sundi akaitikia kwa sauti dhaifu iliyonipelekea nitege sikio langu karibu zaidi na mdomo wake.
“Balozi Adam Mwambapa yuko wapi?”. Nikamuuliza yule kijana na bilashaka swali langu lilisababisha mshtuko mkubwa usoni mwake kiasi cha kunipelekea nishindwe kumuelewa badala yake nikamuona akinishika mkono wangu taratibu huku akitabasamu. Hata hivyo nilishangazwa sana na machozi mepesi yaliyoanza kutiririka mashavuni mwake pasipo kusema neno lolote. Macho yangu yakaweka kituo kumtazama na hapo nikajikuta nikiingiwa na simanzi kwani sikuwa nimeona ishara yoyote ya furaha kiasi cha kumpelekea yule kijana atabasamu katika hali ile.
“Tafadhali naomba uniambie Balozi Adam Mwambapa yuko wapi?”. Nikarudia kumuuliza Sundi huku taratibu nikimpigapiga mgongoni katika namna ya kumtia moyo. Sundi akanitazama tena katika hali ya kukata tamaa kabla ya kuzungumza kwa tabu.
“Sifahamu alipo”. Jibu la Sundi likanipelekea nimtazame kwa mshangao hata hivyo haraka niligundua kuwa hali yake ilikuwa ikizidi kuwa mbaya kwani macho yake yalikuwa yakizidi kubadilika kwa kupoteza muono huku akihema kwa tabu kama mwanariadha wa mbio ndefu aliyekata tamaa na ushidi.
“Naomba unipe maji ya kunywa. Nasikia kiu sana’’. Hatimaye nikamsikia Sundi akinisihi kwa tabu huku akinishika mikononi wangu na kunivuta karibu yake. Ile ilikuwa ni ishara mbaya sana katika uhai wa Sundi kutokana na ile hali mbaya ya afya aliyokuwa. Sasa kinywa chake alikuwa amekiachama kama ishara ya kuhitaji maji ya kunywa kutokana na kiu kali ya ghafla aliyokuwa nayo. Ni dhahiri kuwa kifo kilikuwa kikimuhitaji Sundi kuliko wakati wowote wa maisha yake na uzoefu ukanikumbusha kuwa endapo ningempa maji mara baada ya kuyanywa hiyo ndiyo ingekuwa safari yake ya mwisho katika sayari hii. Hata hivyo nilifahamu kuwa bila kumpa Sundi maji ya kunywa basi asingeweza kuzungumza tena katika sehemu ndogo iliyosalia ya uhai wake. Hivyo taratibu nikaanza kujitoa mikononi mwake nikipanga kwenda kumchukulia maji ya kunywa kwenye ule ukumbi wa kulia chakula uliokuwa kando ya ile sebule. Hata hivyo wakati nikiwa katika harakati zile mara nikamuona Sundi akinizuia nisiondoke na nilipomtazama usoni nikagundua kuwa kulikuwa na jambo fulani alilotaka kuniambia. Hivyo nikasogea karibu yake zaidi huku nikimtazama usoni kwa shauku.
“Ukitoka hapa mtafute Padri Aloysius Kanyameza”
“Nitampata wapi?”. Nikamuuliza Sundi kwa shauku hata hivyo hakunijibu badala yake akaendelea kunitazama kwa utulivu huku akitoa sauti hafifu ya mkoromo kinywani kwake. Nilipomtazama Sundi haraka nikagundua kuwa alikuwa katika hatua za mwisho kabisa za uhai wake. Nikajaribu kumtikisa kidogo na kumuita mara kadhaa lakini Sundi hakuitika badala yake hata ile sauti yake ya mkoromo hafifu ikafifia taratibu na hatimaye kukoma kabisa huku ameacha wazi macho yake akinitazama. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu na nilipojaribu kupitisha mkono wangu mbele ya macho yake sikuona ishara yoyote ya mjongeo wa macho yake. Macho yake yakaendelea kunitazama kwa utulivu na hapo nikajua kuwa hakukuwa na uhai tena nafsini mwake. Kwa kweli roho iliniuma sana huku moyoni nikishikwa na simanzi isiyoelezeka. Sundi alikuwa amekufa kifo cha maumivu makali mno kwa pigo moja madhubuti la kisu kikubwa kilichozamishwa tumboni mwake pasipo namna yoyote ya utetezi.
Nikameza fundo kubwa la mate huku nikiyafinya macho yangu katika namna ya kukabiliana na simanzi kubwa nafsini mwangu. Sikuwa na namna tena ya kufanya katika kuukoa uhai wa Sindi hivyo nikamfumba macho na mdomo wake huku taratibu nikimkaza sakafuni. Nikasimama kwa masikitiko huku nimejishika kiuno katika namna ya kukata tamaa sana na aina ile ya unyama. Sikuwa na shaka yoyote kuwa Sundi alikuwa ameuwawa wakati alipokuwa katika harakati za kumsaidia Balozi Adam Mwambapa wakati watekaji walipokuwa katika harakati zao ingawa kwa namna moja au nyingine hisia dhidi ya tukio lile zilikuwa zimeshindwa kabisa kukamilika kichwani mwangu.
Kwanza nilijiuliza ni kwanini kisu ndiyo kilikuwa kimetumika kuupokonya uhai wa Sundi badala ya risasi kama ilivyokuwa kwa wale walinzi na wale mbwa kule nje ya nyumba. Pili nilishindwa kabisa kuelewa kuwa ni kwa nini Sundi alitabasamu wakati nilipokuwa nikimuuliza kuhusu Balozi Adam Mwambapa ingawa kicheko na tabasamu lake vilikuwa vimechanganyikana na majuto, uchungu na kilio kisichokuwa na uwiano na furaha yake ya kuigiza. Tatu nilikumbuka kuwa michirizi ya damu kutoka kwenye lile jeraha la kisu tumboni kwa Sundi ilikuwa imeanzia mlangoni ndani ya kile chumba ikielekea kwenye kona ya kile chumba hadi pale umauti ulipomfika muda mfupi uliopita akiwa mkononi mwangu.
Kwa mtazamo wa awali ni kuwa kifo cha Sundi kilikuwa kimefanyika ndani ya kile chumba na siyo nje hivyo hali ile ilimaanisha kuwa muuaji wa Sundi alikuwa ndani ya kile chumba cha Balozi Adam Mwambapa wakati alipokuwa akitekeleza mpango wake. Maswali mengine yakaendelea kuibuka kichwani mwangu wakati nilipokuwa nikizidi kufikiria. Kama Sundi alishambuliwa akiwa mle ndani ya kile chumbani cha Balozi Adam Mwambapa nilitaka kufahamu kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa wapi wakati tukio lile lilipokuwa likifanyika mle ndani. Ni kweli kuwa watekaji walikuwa tayari wamefanikiwa kumteka Balozi Adam Mwambapa wakati mmoja wao alipofanikiwa kumhadaa Sundi atoke chumbani kwake na kuingia chumbani kwa Balozi Adam Mwambapa huku akijifanya kuwa yeye ni Balozi Adam Mwambapa. Uongo uliompelekea muuaji huyo atimize adhma yake pasipo upinzani wowote?. Kwa kweli sikupata penyenye yoyote katika hisia zangu. Labda huwenda ningepata chochote cha kunisaidia katika kujibu maswali yangu kichwani kutoka kwa lile jitu hatari nililotoka kupambana nalo kule sebuleni. Lakini sasa jitu lile tayari lilikuwa limepoteza maisha baada ya kupambano nalo vikali hivyo uwezo wa taarifa kunifikia kwa wakati ule ulikuwa ndani ya mipaka.
Wakati nikiendelea kufikiri nikajikuta nikiyakumbuka maelezo ya Sundi wakati aliponitaka nikamtafute Padri Aloysius Kanyameza. Sikutaka kuyachukulia maelezo ya Sundi kama maneno yamtokayo mtu kinywani pale anapokuwa katika hatua za mwisho za kukabiliana na kifo katika namna ya kuweweseka. Nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa pamoja na jeraha kubwa la kisu tumboni mwake lakini jeraha lile lisingekuwa kigezo cha kuikoroga akili ya Sundi na kumpelekea anieleze jambo asilolifahamu. Hivyo kwa namna moja au nyingine niliamini kuwa Sundi alikuwa akifahamu jambo fulani la siri lenye kuhusiana moja kwa moja na lile tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa. Hivyo kwa mtazamo mwingine ni kuwa Padri Aloysius Kanyameza angekuwa hatua muhimu sana katika upelelezi wangu ingawa sikufahamu ni wapi ambapo ningeweza kumpata kiongozi huyo wa kiroho pale jijini Bujumbura.
Muda haukuwa rafiki kwangu vilevile sikutaka kabisa kuamini kuwa lile jitu nililopambana nalo mle ndani lilikuwa peke yake hivyo kwa namna moja au nyingine niliamini kuwa kitendo cha lile jitu kuchelewa kurudisha mrejesho kwa wenzake ingeweza kuwa ni ishara mbaya ya kuwafanya wenzake hao waje na kunikuta mle ndani kabla sijapiga hatua nyingine muhimu katika harakati zangu. Hivyo hararaka nikaanza kufanya upekuzi mle ndani.
Kile chumba kilikuwa kikubwa na chenye nafasi ya kutosha. Upande wa kushoto na wa kulia wa chumba kile kulikuwa na madirisha mapana yenye nondo na vioo yaliyofunikwa kwa mapazia marefu na mepesi. Upande wa kulia ukutani kulikuwa na kabati kubwa la nguo la mbao na kando ya kabati lile kulikuwa na meza nzuri nyeusi ya kioo. Juu ya meza ile kulikuwa na seti moja ya runinga kubwa Flat screen katikati ya spika mbili za sistimu ya muziki wa Home threatre. Kwa kurunzi yangu ndogo mkononi nikamulika kwa utulivu kwenye kabati lile na hapo haraka nikagundua kuwa upekuzi wa ovyo ulikuwa umefanyika ndani ya lile kabati. Lile kabati lilikuwa limefunguliwa na kuachwa wazi. Nguo za mle ndani zilikuwa zimepekuliwa na kutawanywa ovyo. Droo za ndani za lile kabati zilikuwa zimevunjwa na vitu vilivyokuwa mle ndani vilikuwa vimetawanywa ovyo kila mahali. Katika droo ya chini kabisa ya lile kabati niliona jozi tatu za viatu vya ngozi vya aina tofauti. Mwishowe sikuona kama kungekuwa na tija yoyote ya kufanya upekuzi katika kabati lile hivyo nikageuka na kuchunguza upande wa kulia wa kile chumba.
Kulikuwa na kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita chenye nakshi nzuri za kupendeza hata hivyo kitanda kile kilikuwa kimevurugwa. Shuka zake zilikuwa zimetawanywa ovyo na mito yake ya kuegemea ilikuwa imetupwa sakafuni. Taratibu nikakizunguka kitanda kile na kuanza kuchunguza kwa makini kabla ya kuliondoa lile godoro na kutazama chini yake. Sikuona kitu chochote cha maana hivyo nikahamishia uchunguzi wangu kwenye droo mbili zilizokuwa upande wa kushoto wa kitanda kile. Nilipozifungua zile droo ndani yake sikuona kitu chochote na hapo hisia za awali zikanitanabaisha kuwa kulikuwa kumefanyika upekuzi wa kina mle ndani.
Hatimaye nikiacha kile kitanda na kuelekea upande wa kushoto wa kile chumba. Mara baada ya kuupita ule mlango wa kile chumba upande wa kushoto nikauona mlango mwingine lakini mlango ule ulikuwa wazi. Niliposogea karibu na kuchunguza mle ndani kwa mwanga wa kurunzi yangu nikagundua kuwa ule ulikuwa mlango wa kuelekea kwenye chumba kidogo cha maliwato. Nikaingia mle ndani kwa tahadhari na kuanza kumulika kwa utulivu hata hivyo sikuona kitu chochote cha maana zaidi ya choo kimoja cha kukaa cha marumaru nyeupe na beseni kubwa la kuogea. Mle ndani ukutani kulikuwa kumeningʾinizwa mataulo mbalimbali na zaidi ya pale sikuona kitu kingine chochote cha kunivutia hivyo hatimaye nikaamua kutoka nje ya kile chumba...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 34

Upande wa kushoto wa kile chumba kulikuwa na seti moja ya makochi ya sofa nadhifu na ya kisasa juu ya zulia zuri lenye rangi za ngozi ya Pundamilia. Katikati ya makochi yale kulikuwa na meza ndogo ya mbao yenye umbo la nusu duara. Niliposogea karibu na meza ile na kuchunguza juu yake nikaona kibakuli kidogo cha majivu ya sigara, kibiriti kioja cha gesi, kasha tupu la miwani ya macho na simu ya mezani. Nikaitazama kwa makini ile simu ya mezani huku kichwani nikianza kuvuta picha namna Balozi Adam Mwambapa alivyokuwa katika harakati za kutumia simu za mle ndani katika kufanya mawasiliano na Hidaya wakati watekaji walipovamia ile nyumba. Hatimaye nikashawishika kuchukua kiwambo cha ile na kukiweka sikioni huku nikitumia kitambaa changu kidogo cha leso nikikwepa kuacha alama za vidole vyangu eneo lile. Nilipojaribu kubonyeza tarakimu kadhaa za ile simu ya mezani haraka nikagundua kuwa mawasiliano ya ile simu yalikuwa yamekatwa. Nilikuwa nikitarajia jambo la namna ile hivyo sikushangaa.
Muda ulikuwa ukienda na dakika nazo zilikuwa zikiyoyoma hivyo hatimaye nikairudisha ile simu mahala pake na kuanza kutembea kwa utulivu nikielekea sehemu ya mbele ya kile chumba. Nilipokaribia dirishani upande wa kushoto nikaona ua kubwa zuri kwenye chungu cha udongo na kando ya ua lile kulikuwa na kiti kimoja cha kupumzikia kilichokuwa kikitazamana na lile dirisha. Pembeni ya kile kiti kulikuwa na meza fupi ya mbao yenye droo mbili na juu ya meza ile kulikuwa na chupa moja tupu ya kahawa na kikombe cha dongo pembeni yake.
Bastola yangu ikiwa imetuama vyema mkononi nikajaribu kuvichunguza vitu vile kwa makini kabla ya kuhamia kwenye droo mbili za ile meza ndogo iliyokuwa pembeni ya kile kiti cha kupumzikia. Haraka nilipoanza upekuzi wangu nikagundua kuwa zile droo za ile meza nazo zilikuwa zimefunguliwa na kuachwa wazi huku zikionekana zimefanyiwa upekuzi. Watekaji bila shaka walikuwa wamechukua vielelezo vyote ambavyo vingeweza kusaidia katika kupatikana kwa Balozi Adam Mwambapa. Hivyo sikutaka kuendelea kupoteza muda wangu eneo lile badala yake nikahamia kwenye sefu mbili za chumba zilizokuwa kwenye kona ya upande wa kulia wa kile chumba. Hatimaye nikazifikia zile sefu na kuanza kuzichunguza kwa makini. Sefu ya kwanza haikuwa na kitu ndani yake. Ile sefu nyingine ilikuwa wazi huku ikionekana kuwa kulikuwa na upekuzi uliokuwa umefanyika ndani yake. Nilipoendelea kuchunguza mle ndani nikaona kuwa kulikuwa na nyaraka muhimu za kiofisi zikiwemo barua za siri zenye maelekezo fulani kuhusu masuala ya kiutendaji ya kibalozi kutoka ikulu ya Tanzania ya jijini Dar es Salaam.
Nilipoendelea kuichunguza vizuri ile sefu kwa chini nikagundua kuwa droo zake mbili zilikuwa zimevunjwa na nilipochunguza kwa makini ndani ya zile droo nikagundua kuwa kulikuwa na harufu nzuri ya pesa nyingi iliyohifadhiwa mle ndani kwa muda mrefu. Harufu ile ya pesa ikanipelekea niamini kuwa kulikuwa na kiasi kikubwa cha fedha iliyoibwa kutoka kwenye droo zile za sefu. Hali ile ikanivuta kuzidi kufanya uchunguzi zaidi na kwa kufanya vile nikaokota noti moja ya dola mia ya kimarekani. Nikaichunguzi kwa makini noti ile kabla ya kuitia mfukoni. Kwa muda mfupi uliosalia nikawa nimefanikiwa kufanya upekuzi kwenye vipenyo vyote muhimu vya ile nyumba huku nikiwa sijaambulia kitu chochote cha maana. Hatimaye nikaamua kutoka nje ya ile nyumba lakini safari hii nikiutumia ule mlango wa mbele ambao niligundua kuwa ulikuwa haujafungwa kwa funguo. Sasa nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa ametekwa na kikundi fulani cha watu wasiofahamika kwa sababu wanazozijua wao.
Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha wakati nilipokuwa nikitoka nje ya ile nyumba na kukatisha kwenye giza zito chini ya miti mikubwa ya kivuli iliyopandwa kuizunguka ile nyumba. Kwa kuhofia usalama wangu eneo lile sikutaka kuwasha ile kurunzi yangu mkononi badala yake nikaitia mfukoni na kuikamata vyema bastola yangu mkononi nikielekea kwenye geti la ile nyumba kutoka nje.
Mara tu nilipotoka nje ya lile geti nikakumbuka kuitazama saa yangu ya mkononi na hapo nikagundua kuwa nilikuwa nimepoteza muda mwingi ndani ya ile nyumba. Sikutaka kurudi kule nilikoegesha gari langu kwa kuufuata uelekeo ule niliokuja nao. Hivyo mara tu baada ya kutoka nje ya lile geti nikashika uelekeo wa upande wa kulia wa barabara ya lami iliyokuwa ikikatisha mbele ya ile nyumba kwa kuambaa ambaa na ukuta wa uzio wa ile nyumba. Muda ulikuwa umesonga sana na utulivu katika ile barabara na eneo lile lote kwa ujumla ulikuwa umeongezeka. Sauti pekee zilizokuwa zikisika zilikuwa ni sauti za mbwa waliokuwa wakibweka kutoka nyumba za jirani na eneo lile.
Niliendelea kutembea kwa mwendo wa tahadhari kandokando ya ule ukuta huku mara kwa mara nikigeuka na kutazama nyuma kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia. Sikumuona mtu yeyote hivyo hali bado ilikuwa shwari. Nilipofika mwisho wa ule ukuta nikasimama kutathmini hali ya usalama wa eneo lile na niliporidhika nikachepuka na kuvuka barabara upande wa pili. Nikiwa upande wa pili wa ile barabara nikaendelea kutembea chini ya miti iliyokuwa pembeni ya barabara ile yenye giza hafifu huku jina la Padri Aloysius Kanyameza likianza upya kuzitekenya fikra zangu huku nikijaribu kuwaza ni kwa namna gani mtumishi huyo wa kiroho alikuwa ametumbukia kwenye mkasa huu wa hatari wenye matukio ya aina yake. Jibu sikulipata ingawa hisia zangu zilinitanabaisha kuwa nilikuwa nimejiingiza kwenye mkasa hatari.
Niliendelea kutembea chini ya miti ile ya kando ile barabara pembeni ya kuta ndefu zilizopandwa kuyazunguka majumba makubwa ya kifahari huku mara kwa mara nikigeuka nyuma katika namna ya kujihakikishia usalama wangu.
Ilikuwa ni wakati nilipokuwa nikikaribia kuifikia kona ya barabara ile pale nilipoona mwanga wa taa za gari ukianza kuchomoza kwenye ile kona mbele yangu kasha ukafuatia muungurumo wa gari. Haraka nikawahi kujibanza kwenye kona moja ya ukuta wa eneo lile sehemu iliyokuwa na giza zito lililofanywa na matawi ya mti. Nikiwa nimejibanza kwenye ile kona muda uleule mara nikaliona gari dogo aina ya LandRover likichommoka kwenye ile kona na kuingia kwenye ile barabara. Mwendo wa lile gari ulikuwa wa kasi mno kiasi cha kunitahadharisha kuwa mambo hayakuwa shwari. Nilipolichunguza vizuri lile gari nikagundua kuwa lilikuwa ni gari la jeshi na nyuma yake kulikuwa na wanajeshi sita huku mikononi wakiwa wameshika bunduki zao.
Muda mfupi uliofuata lile gari likanipita kwa kasi kama gari la kikosi maalum cha uokozi wa majanga ya moto likielekea kule nyuma nilipotoka. Nikiwa bado nimejibanza kwenye ile kona nikaendelea kulitazama lile gari namna lilivyokuwa likitimua. Mara nikaliona lile gari likipunguza mwendo kule mbele na kitendo kile kikawapelekea wanajeshi watatu waruke kwa mbwembwe kutoka nyuma ya lile gari na namna ya urukaji wao ulitosha kunifahamisha kuwa kulikuwa na jambo la hatari. Nilipoendelea kuchunguza nikagundua kuwa wale wanajeshi walikuwa wameruka kutoka kwenye lile gari wakiwa wamebakisha hatua chache kabla ya kuifikia ile nyumba aliyokuwa akiishi Balozi Adam Mwambapa.
Wale wanajeshi waliporuka mara nikamuona mmoja wao akienda kujibanza mwanzo wa ukuta wa ile nyumba upande wa kushoto. Mwingine nikamuona akiuzunguza ule ukuta kwa nyuma na yule mwingine aliyesalia akaenda kujibanza kwenye kona ya ule ukuta iliyokuwa upande wa kulia. Mara baada ya wale wanajeshi watatu kuruka lile gari LandRover likaongeza tena mwendo kuendelea na safari na lilipofika mbele ya geti la ile nyumba ya Balozi Adam Mwambapa nikaliona likipunguza tena mwendo. Kwa kufanya vile nikawaona wanajeshi wengine watatu wakiruka kutoka nyuma ya lile gari katika mtindo wa kibabe kisha wakijiviringisha barabarani kama ninja kila mmoja akishika uelekeo wake kuizingira ile nyumba. Wale wanajeshi walipomaliza kuruka lile gari LandRover halikusimama badala yake likaongeza kasi mbele ya ile barabara na hatimaye kutokomea mitaani.
Nikiwa bado nimejibanza kwenye kona ya ule ukuta mara nikawaona wale wanajeshi walioruka kutoka kwenye lile gari LandRover wakielekea kwa tahadhari kwenye geti la ile nyumba ya Balozi Adam Mwambapa huku wakiwa wamezishika vyema bunduki zao mikononi. Haukupita muda mara nikawaona wale wanajeshi wakiusukuma mlango mdogo wa lile geti na kuingia mle ndani. Kwa kweli moyo wangu ulipoteza utulivu kabisa huku damu ikinichemka mwilini hali iliyopelekea kijasho chepesi kianze kunitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu. Nafsi yangu ikanitanabaisha kuwa nilikuwa nimepishana na hatari muda mfupi uliopita. Nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa kuwa wale wanajeshi walikuwa na ushirika na lile jitu hatari nililotoka kupambananalo vikali na hatimaye kufanikiwa kuliangamiza ndani ya ile sebule ya Balozi Adam Mwambapa muda mfupi uliopita.
Nilitamani sana kuendelea kujibanza eneo lile ili niweze kuwapeleleza vizuri wale wanajeshi walioshuka kwenye lile gari na kuivamia nyumba ya Balozi Adam Mwambapa lakini mara moja nafsi yangu ikanionya kuwa lile lingekuwa jambo la hatari sana. Nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa mara baada ya wale watu kunitafuta na kunikosa mle ndani ya ile nyumba wasingekubaliana na hali ile na badala yake wangeamua kupanua mipaka ya operesheni yao zaidi wakinisaka katika vipenyo na kona zote za kitongoji kile hivyo endapo ningeendelea kuzubaa eneo lile wangenifikia na kunikamata.
Kwa kweli sikutaka wale wanajeshi wanifikie hivyo kwa tahadhari nikayaacha yale maficho na kuondoka eneo lile nikiambaa na zile kuta za uzio wa zile nyumba zilizokuwa zikipakana na ile barabara ya lami. Nilipofika mwisho wa ile kona nikaingia upande wa kushoto nikiifuata barabara pana ya lami iliyokuwa ikikatisha katikati ya makazi ya watu.
Mvua kubwa bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na hivyo kupelekea barabara ile kumezwa na upweke wa kifo. Sikuweza kumuona mtu yeyote wakati nilipokuwa nikitembea kandokando ya barabara ile huku mara kwa mara nikigeuka kutazama nyuma. Kulikuwa na nyumba chache zilizokuwa zikiwaka taa katika mtaa ule huku nyumba nyingi zikionekana kutawaliwa na giza. Ilifikia wakati nikawa nasikia milio ya risasi kwa mbali hata hivyo sikuweza kufahamu kwa hakika kuwa sauti zile za majibishano ya risasi zilikuwa zikitokea maeneo gani. Hata hivyo nilijipa tahadhari kwa kuwa makini kutokana na hali ya machafuko ya kisiasa iliyokuwa ikiendelea nchini Burundi.
Niliendelea kutembea kwa tahadhari kando ya barabara ile na nilipofika mbele nikaona kuwa kulikuwa na barabara nyingine iliyokuwa ikichepuka kuingia upande wa kushoto. Nilipofika eneo lile nikaingia upande wa kushoto kuifuata ile barabara. Niliendelea kutembea katika barabara inayokatisha katikati ya majumba makubwa ya kifahari yaliyozungukwa na kuta kubwa za uzio zenye sistimu maalum za umeme wa kuzuia wezi juu yake. Kulikuwa na utulivu wa hali ya juu katika kitongoji kile hali iliyonipelekea nijihisi mpweke.
Ile barabara ilikuwa ikikatisha mbele ya mageti makubwa ya nyumba za kifahari zilizokuwa eneo lile hivyo nilipofika mbele kidogo nikachepuka na kuifuata barabara nyingine iliyokuwa ikiingia upande wa kulia. Barabara ile ilikuwa ikikatisha kati ya jengo la benki ya biashara ya Burundi na kituo kimoja binafsi cha urushaji wa matangazo ya redioni.
Kwa mujibu wa ramani yangu ndogo ya kijasusi ni kuwa mbele ya barabara ile kulikuwa na barabara nyingine ya mtaa iliyokuwa ikikatisha kwa mbele. Upande wa kushoto mbele ya ile barabara ndiyo kulikuwa na ile supermarket ndogo ambayo mbele yake nilikuwa nimeegesha lile gari langu.
Hata hivyo wakati nilipokuwa mbioni kuifikia ile barabara mara nikashtushwa na muungurumo wa gari lililokatisha haraka na kuingia kwenye ile barabara niliyokuwa nikitembea. Haraka nikawahi kuchepuka na kujibanza kwenye uchochoro mwembamba uliokuwa baina ya ukuta wa nyumba moja na nyingine na nilipochungulia kutazama nikaliona lile gari LandRover ambalo lilikuwa limenipita kwenye ile kona muda mfupi uliopita baada ya kutoka kwenye ile nyumba ya Balozi Adam Mwambapa kule nyuma nilipotoka. Hata hivyo lile gari halikuwa katika mwendo kasi kama lilivyokuwa pale awali wakati likinipita. Nikiwa bado nimejibanza kwenye ule uchochoro nikaendelea kulitazama lile gari na kwa kufanya vile nikawaona wanajeshi wawili wakiwa wameketi sehemu ya mbele ya lile gari. Sehemu ya nyuma ya lile gari hapakuwa na mtu na hali ile ilinishangaza sana.
Lile gari likaendelea na safari yake kwa mwendo wa taratibu na wa tahadhari na lilipokaribia kwenye kile kichochoro nilichojibanza mara nikaliona likipunguza mwendo na hatimaye kusimama. Tukio lile likanipelekea niingiwe na hofu. Nilipogeuka haraka kutazama nyuma ya kile kichochoro hofu ikaniingia zaidi baada ya kugundua kuwa mwisho wa kile kichochoro kilikuwa na ukomo baada ya kuuona ukuta mrefu wenye sengʾenge juu yake. Hivyo kule nyuma hapakuwa na sehemu ya kutokea endapo ningeamua kukifuata zaidi kile kichochoro. Nikiwa katika hali ile ya kutafakari nini cha kufanya mara nikauona mlango wa mbele wa lile gari ukifunguliwa kisha mtu mmoja akashuka huku mkononi akiwa ameshika bastola. Tukio lile likanipelekea nigeuke tena kutazama nyuma ya kile kichochoro huku akili yangu ikifanya kazi ya ziada ya kujihakikishia usalama wangu.
Nikiwa katika hali ile ya taharuki mara nikagundua kuwa chini ya ule ukuta mwisho wa kile kichochoro kulikuwa na pipa moja chakavu la taka. Sikuwa na namna nyingine ya kufanya hivyo kwa haraka nikalifuata lile pipa na pasipo kujishauri nikaufungua mfuniko wake na kuingia mle ndani kisha nikajifunika kwa ule mfuniko. Lile pipa lilikuwa na takataka chache na nilipolichunguza nikagundua kuwa lilikuwa likitumika kuchomea takataka hata hivyo sikuwa na budi kuvumilia harufu mbaya ya masalia ya takataka zilizokuwa mle ndani ingawa bado hewa safi kidogo iliweza kupenya kupitia matundu machache yaliyofanywa na kutu kwenye mfuniko wa lile pipa.
Muda mfupi baada ya kuingia mle ndani ya lile pipa mara nikauona mwanga mkali wa kurunzi ukimulika juu ya ule mfuniko wa lile pipa huku ule mwanga ukisindikizwa kwa sauti ya hatua hafifu za mtu akiingia kwenye kichochoro kile. Sikuona kama kuna namna nyingine ya kufanya katika kuepuka kadhia ile. Hivyo nikiwa ndani ya lile pipa nikaikamata vyema bastola yangu mkononi tayari kukabiliana na rabsha yoyote ambayo ingejitokeza mbele yangu.
Kupitia matundu machache ya kutu yaliyokuwa pembeni ya lile pipa ule mwanga wa kurunzi ya yule mtu mkononi ukaniwezesha kuangalia kule nje. Nilimuona mtu mmoja mrefu mweusi kichwani akiwa amevaa kofia ya bereti na fulana aliyoichomekea vizuri kiunoni kwenye suruali yake ya kombati na buti ngumu za jeshi miguuni huku mkononi akiwa ameshika bastola. Yule mtu alikuwa mrefu sana huku misuli ya shingo na mikono yake ikiwa imetuna kwa ukomavu. Mwonekano wake ukanitanabaisha kuwa alikuwa ni mtu anayependa matata.
Yule mtu akaendelea kutembea kwa tahadhari akilikaribia lile pipa huku akiendelea kumulika mulika huku na kule kwenye kile kichochoro. Mwenzake bado alikuwa amebaki ndani ya lile gari akisubiri. Yule mtu akaendelea kutembea kwa tahadhari akilikaribia lile pipa nililokuwa nimejibanza ndani yake na kadiri yule mtu alivyokuwa akizidi kulikaribia lile pipa ndivyo moyo wangu ulivyokuwa ukizidi kupoteza utulivu huku kijasho chepesi kikinitoka.
Hata hivyo wakati nikiwa bado mle ndani ya lile pipa la taka jambo moja likatokea na kunifurahisha sana. Ilikuwa ni wakati yule mtu alipokuwa amesaliwa na hatua chache kabla ya kulifikia lile pipa mara nikasiki akiitwa na yule mwenzake aliyekuwa amebaki kwenye lile gari kule barabarani huku yule mwenzake akilalamika kuwa walikuwa wakipoteza muda wao bure eneo lile. Yule mtu aliyekuwa akilikaribia lile pipa kusikia akiitwa kukamfanya asite kuendelea na safari ya kulifikia lile pipa nililojibanza badala yake akasimama na kulitazama lile pipa kwa makini kama mtu aliyehisi kitu fulani mle ndani ya lile pipa. Hata hivyo yule mtu hakupiga hatua zaidi badala akautembeza ule mwanga wa kurunzi yake mkononi kumulika chini ya lile pipa na huwenda alipoona mabaki ya takataka yaliyoangukia nje ya lile pipa kukampelekea azipuuze hisia zake. Hatimaye nikamuona yule mtu akiitia bastola yake kiunoni huku akimulikamulika eneo lile kabla ya kuamua kugeuza na kurudi kwenye lile gari kule barabarani mwenzake alipokuwa akimsubiri. Baada ya muda mfupi kupita mara nikasikia mlango wa lile gari ukifungwa kisha dereva wa lile gari akatia moto na kuondoka akitokomea mbali na eneo lile.
Kwa sekunde kadhaa nikiwa ndani ya lile pipa nikajikuta nikimezwa na mduwao usioelezeka huku nikishindwa kabisa kuamini kuwa nilikuwa nimesalimika na mkasa ule hatari. Hata hivyo niliendelea kujibanza ndani ya lile pipa hadi pale niliporidhika kuwa lile gari lilikuwa limetokomea mbali na eneo lile ndiyo nikauondoa ule mfuniko wa lile pipa na kutoka.
Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na hali ile ilikuwa nafuu kwangu kwani wakati nikiendelea na safari matone makubwa ya mvua ile yakawa yakiosha uvundo mwilini mwangu uliotokana na masalia ya takataka zilizokuwa ndani ya lile pipa.
Muda mfupi uliofuata nikawa nimetoka kwenye kile kichochoro na kuingia barabarani huku kwa tahadhari nikiendelea kupita kandokando ya kuta ndefu zilizoyazunguka majumba ya kifahari ya eneo lile. Mwisho wa ile barabara kulikuwa na barabara nyingine iliyokatisha hivyo nilipoifikia ile barabara nikaingia upande wa kushoto huku nikiendelea kutembea kwa tahadhari na mara kwa mara nikawa nikigeuka na kutazama nyuma kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia. Sikumuona mtu yeyote nyuma yangu hivyo hali bado ilikuwa...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 35

shwari. Ile barabara ilikuwa ikikatisha moja kwa moja mbele ya ile suparmaket niliyoegesha gari langu hivyo nilinyoosha moja kwa moja.
Wakati nikilifikia lile gari langu nikachepuka kidogo na kujibanza kwenye kona moja ya ukuta katika namna ya kuchunguza hali ya usalama wa eneo lile na niliporidhika kuwa hali bado ilikuwa shwari nikavuka barabara na kuelekea kwenye gari langu kwa tahadhari huku mkono wangu wa kushoto ukiwa umekikamata vyema kilimi cha bastola yangu kwenye mfuko wa koti langu tayari kukabiliana na rabsha yoyote ambayo ingejitokeza eneo lile. Hatimaye nikalifikia gari langu na baada ya kulizunguka kidogo kukagua usalama wake na kuridhishwa nikafungua mlango wa dereva na kuingia mle ndani. Koti langu la mvua nikalivua na kulitupia siti ya nyuma kasha bila kupoteza muda nikawasha gari na kuondoka eneo lile huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu.
Kwa namna moja au nyingine nilianza kuamini kuwa tukio la kutekwa kwa balozi Adam Mwambapa lilikuwa limetekelezwa na kikundi cha wanajeshi wachache wa jeshi la wananchi wa Burundi ingawa bado sikuweza kufahamu dhamira ya watekaji hao. Nilikuwa nimeanza kushawishika kwenda kuripoti juu ya tukio lile kwa maafisa usalama waandamizi wa nchini Burundi hata hivyo hali ile ya machafuko ya kisiasa iliyokuwa ikiendelea nchini Burundi ilinionya kuwa kwa kufanya vile huwenda ningejitumbukiza kwenye hatari ya kugharimu uhai wangu badala ya kutatua tatizo kama ilivyokuwa lengo langu.
Mvua kubwa bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na wakati nikiendelea na safari yangu mbali na kile kitongoji cha Chaussée P.L. Rwagasore nikagundua kuwa mifereji mingi ya maji iliyokuwa ikipakana na barabara za kitongoji kile ilikuwa mbioni kufurika kwa maji ya mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha. Nikaendelea kuendesha gari kwa kasi nikikitoroka kitongoji kile huku mara kwa mara nikiyapeleka macho yangu kutazama vioo vya ubavuni vya lile gari kuona kama kungekuwa na gari lolote lililokuwa likinifungia mkia kwa nyuma. Sikuona gari lolote hivyo hali bado ilikuwa shwari.
Baada ya mwendo mrefu wa safari yangu nikivizunguka vichuguu kushuka mabonde na kupanda milima hatimaye nikapita mbele ya jengo refu la ghorofa la Vaya residence apartments services. Nilipolipita lile jengo upande wa kushoto baada ya safari fupi nikakunja kona upande wa kulia nikipanda mlima mfupi katika barabara ya Chaussée P.L. Rwagasore. Mwendo wangu ulikuwa wa kasi mno hivyo baada ya muda mfupi nikawa nimeyafikia makutano ya barabara ya Chaussée P.L. Rwagasore na barabara ya Avenue Belvedere. Nilipoyafikia yale makutano nikapunguza mwendo na kuingia barabara ya Avenue Belvedere nikianza kushuka mteremko mkali wa barabara ile kuelekea mjini.

_____
Saa tano na dakika kumi usiku niliegesha gari langu katika viunga vya maegesho ya magari vya jengo la New Parador Residence kando ya barabara ya Boulevard du 28 Novembre. Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na nje ya jengo ile kulikuwa na magari machache yaliyoegeshwa.
Nilikuwa nimeyakumbuka vyema maelezo ya Hidaya kuwa siku ile ambayo hakuhudhuria kazini Balozi Adam Mwambapa alikuwa amealikwa na maafisa waandamizi wa serikali ya Burundi kuhudhuria kikao juu ya hali tete ya machafuko ya kisiasa iliyokuwa imeanza kutokea nchini Burundi. Kwa mujibu wa maelezo ya Hidaya aliyoyapata kutoka kwa Balozi Adam Mwambapa ni kuwa mkutano ule ungefanyikia katika ukumbi wa lile jengo la New Parador Residence ndiyo kisa nikawa nimefika pale.
Kabla ya kushuka kwenye gari nikatulia kwa dakika chache nikitathmini vizuri mandhari yale. Eneo la mbele la maegesho ya magari ya lile jengo kulipandwa miti mirefu ya kivuli aina ya Quercus virginiana katikati ya bustani nzuri ya maua baina ya sehemu moja ya maegesho ya gari na sehemu nyingine. Kulikuwa na taa hafifu za ardhini zilizokuwa zikimulika eneo lile na hivyo kulifanya lile eneo lipendeze.
Nilipozidi kuchunguza nikagundua kuwa kulikuwa na magari machache madogo yaliyokuwa yameegeshwa eneo lile. Mbali na magari yale madogo pia kulikuwa na basi moja la wanafunzi wa shule ya sekondari ya Eldoret ya nchini Kenya, lori moja kubwa la kubebea watalii wa masafa marefu na gari moja jeusi aina ya Nissan Caravan lililokuwa limeegeshwa upande wa kushoto mwisho wa lile jengo.
Upande wa kulia wa eneo lile kulikuwa na kibanda kidogo chenye mashine mbili za ATM za benki. Mashine moja ya ATM ya Banque de Crédit de Bujumbura na mashine nyingine ya ATM ya Banque de la République du Burundi. Kulikuwa na watu wachache katika foleni za wahitaji huduma kuelekea kwenye zile mashine za ATM na wengi wao walikuwa ya wazungu wa kutoka nje ya bara la Afrika. Pembeni ya mashine zile za ATM kulikuwa na bustani ya nyasi laini zilizokatiwa vizuri na kupendeza na katika bustani ile kulikuwa na sehemu za kupumzika zenye viti na meza chini ya miamvuli mikubwa yenye rangi za kupendeza. Nilipoyatembeza macho yangu kwa utulivu nikagundua kuwa hapakuwa na mtu yeyote eneo lile labda kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha.
Jengo la New Parador Residence lilijengwa kwa ufanisi wa hali ya juu kiasi kwamba taa nzuri zilizokuwa zikiwaka kwenye ghorofa zake zililipelekea jengo lile lionekane kama meli kubwa ya kupendeza iliyotia nanga kwenye bandari ya nchi kavu. Chini ya lile jengo kulikuwa na supermarket moja kubwa, maduka ya nguo za kisasa, ofisi za mashirika ya simu, ofisi za Dstv, Dhl na maduka mawili ya kubadilishia fedha za kigeni.
Hatimaye nikalichukua lile koti langu jeusi la mvua na kulivaa kisha nikafungua mlango wa gari na kushuka. Taratibu nikaanza kukatisha kwenye viunga vile vya maegesho taratibu nikielekea mbele wa lile jengo sehemu kulipokuwa na mlango mkubwa wa kioo na varanda pana yenye ngazi iliyofunikwa kwa kofia nzuri ya zege.
Wakati nikiendelea kutembea nikawa nikiyatembeza macho yangu kwa utulivu kutazama huku na kule kuchunguza kama kungekuwa na mtu yeyote ambaye angekuwa akizifuatilia nyendo zangu. Sikumuona mtu yeyote wa kumtilia mashaka hivyo hatimaye nikazifikia zile ngazi na kuanza kuzipanda tatatibu kisha nilipoufikia ule mlango wa kioo nikausukuma na kupotelea ndani.
Kulikuwa na vijana wawili wahudumu wa ile hoteli waliokuwa wamesimama kando ya ule mlango wa kuingilia kwa ndani. Vijana wale waliovaa sare za kazi, suruali nyeusi, makoti ya suti ya rangi nyekundu na kofia nyeupe kichwani wakanipokea kwa bashasha zote huku wakinionesha tabasamu la kirafiki kwenye nyuso zao. Nikawashukuru vijana wale kwa ukaribisho wao na kuendelea na safari yangu nikitembea juu ya kipande mstatili cha zulia jekundu kuelekea sehemu ya mapokezi ya hoteli ile huku nikiendelea kuyatembeza macho yangu kupeleleza mandhari ya mle ndani.
Upande wa kushoto mara baada ya kushuka ngazi chache chini kulikuwa na ukumbi mkubwa wenye meza nyingi za kulia chakula zenye umbo duara zilizozungukwa kwa viti nadhifu vyenye foronya laini. Meza zile zilikuwa zikimefunikwa kwa vitambaa visafi vya rangi nyeupe na juu yake kuliwekwa kadi ngumu za kupendeza zenye orodha ya vyakula na vinywaji vinavyopatika katika hoteli ile. Karatasi laini nyeupe za tishu za kufutia mikono na vifaa vyote muhimu vya kujipatia maakuli kama uma, visu na vijiko. Vikasha wiwili vidogo kimoja cha kuwekea chumvi ya mezani na kingine cha vijiti vya kuchokolea meno. Pembeni ya meza zile kulikuwa na makochi mazuri ya sofa yaliyopangwa kuzizunguka meza fupi za vioo katika mpangilio mmoja unaovutia. Nilipozidi kuchunguza mwisho wa ukumbi ule nikaiona kaunta kubwa ya vinywaji.
Madirisha makubwa ya vioo ya ukumbi ule yalikuwa yamefunikwa kwa mapazia marefu yenye rangi nzuri za kupendeza. Ukutani kulikuwa na runinga pana za flat screen zilizokuwa zikiendelea kurusha taarifa kutoka sehemu mbalimbali za jiji la Bujumbura zikielezea juu ya hali ya machafuko ya kisiasa iliyokuwa ikiendelea kufuka moshi nchini Burundi.
Nilipotazama vizuri ndani ya ule ukumbi nikaona kuwa kulikuwa na watu wachache waliokuwa wameketi mle ndani wakijipatia mlo na vinywaji huku kwa makini wakiendelea kufuatilia taarifa zilizokuwa zikirushwa kupitia zile runinga. Ukumbi ule mkubwa ulikuwa umetenganishwa na ile sehemu ya mapokezi kwa ukuta mkubwa wa kioo unaomruhusu mtu yeyote kuweza kuona mle ndani bila usumbufu wowote.
Nilipogeuka kutazama upande wa kulia nikauona ukumbi mwingine mdogo wenye nguzo mbili kubwa katikati yake. Kulikuwa na watu wachache kwenye ukumbi ule, wazungu kwa waafrika wakiendelea na maongezi yao ya hapa na pale katika makochi mazuri ya sofa yenye meza fupi za mbao. Watu wale wakijipatia vinywaji, wengine wakivuta sigara na kutazama mechi za mpira wa miguu za ligi za ulaya zilizokuwa zikioneshwa kwenye runinga tofauti zilizotundikwa ukutani. Wahudumu wa hoteli ile walikuwa wakiendelea na taratibu zao za kutoa huduma kwa wateja kama ilivyo ada.
Wakati nilipokuwa nikiifikia kaunta ya mapokezi ya ile hoteli mle ndani nikawaona vijana wawili waliovaa sare za kazi zinazofanana na za wale vijana wengine walionikaribisha kule mlangoni na wote walikuwa warefu na weusi wenye maumbo imara na miili iliyojengeka vizuri. Mhudumu mmoja alikuwa akizifuta bilauri ndefu za vinywaji kwa kitaulo kidogo kilichokuwa begani mwake na kuzipanga vizuri katika rafu ya mbao iliyokuwa ukutani eneo lile. Mwenzake alikuwa akiandika taarifa fulani kwenye kitabu kidogo kilichokuwa juu ya meza ya ile kaunta na aliponiona haraka akaacha kile alichokuwa akikifanya na kunikaribisha kwa tabasamu zuri la kibiashara na mimi bila ajizi nikawahi kumsalimia.
“Comment va le travail?’’. Habari za kazi?.
“Bien frère, je peus tʾaider?”. Salama kaka sijui nikusaidie nini?. Yule kijana akanijibu kwa bashasha zote za kirafiki huku akinitazama kwa makini huku akikunja vizuri mikono ya shati lake.
“Je suis Iʾofficien de Iʾambassade de Tanzanie ici à Bujumbura. Je veus savoir sʾil y a eu une reunion de dirigents qui a eu lieu dans votre”. Mimi ni afisa wa ubalozi wa Tanzania hapa Bujumbura. Nataka kufahamu kama kulikuwa na mkutano wowote wa viongozi wa serikali uliofanyikia hapa siku ya juzi. Nikaongea kwa utulivu huku nikiwatazama wale vijana kwa makini. Swali langu bila shaka lilimshtua kidogo yule kijana na hapo nikamuona akinikata jicho la udadisi kabla ya kugeuka na kumtazama mwenzake pale kaunta. Nikahisi jambo fulani nisilolielewa hata hivyo sikutia neno lolote. Yule kijana akageuka na kunitazama tena.
“Pardon!, nous ne sommes pas permis de donner auquʾune information, peut être allez voir notre directeur’’. Samahani!, haturuhusiwi kutoa taarifa zozote za kiofisi labda ukamuone meneja wetu.
Yule kijana akaniambia kwa utulivu huku akinitazama na kwa kweli sikuona tashwishwi yoyote usoni mwake. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku nikigeuka nyuma na kuyatembeza macho yangu taratibu katika namna ya kupeleleza sura za watu zinazostahili kutiliwa mashaka mle ndani. Sikumuona mtu yoyote akinitazama hivyo nikayarudisha macho yangu kwa yule kijana na kuweka kituo.
“Où est le bureau de votre directeur?”. Ofisi ya meneja wenu iko wapi?. Nikamuuliza yule kijana mhudumu na mara ile tena nikamuona akigeuka na kumtazama mwenzake pasipo kusema neno lolote kisha akayarudisha macho yake tena kunitazama.
“Au cinquieme niveau dans la chambre numero 302”. Ghorofa ya tano chumba namba 302. Yule kijana akaniambia kwa utulivu huku akinitazama na hapo nikakumbuka kutumbukiza ombi langu.
“Fais un coup de téléphone et dis lui quʾil ya qulquʾun qui veut le voir”. Piga simu mueleze kuwa kuna mtu anahitaji kumuona. Nikamwambia yule kijana na baada ya kusita kidogo nikamuona akinyanyua kiwambo cha simu ya mezani iliyokuwa pale juu kwenye meza ya kaunta na kukiweka sikioni kisha nikamuona akibonyeza tarakimu kadhaa. Muda mfupi uliofuata ile simu ilikuwa hewani na hapo nikajua kuwa yule kijana alikuwa akiwasiliana na meneja wa ile hoteli ingawa mazungumzo ya simu yalipoanza sikuambulia kitu chochote kwani lugha ya mawasiliano iliyokuwa ikitumika baina ya yule kijana mhudumu na meneja wa ile hoteli ilikuwa ni kirundi ambayo mimi sikuifahamu. Yale mazungumzo ya simu yaliposimama nikamuona yule kijana akigeuka na kuniuliza.
“II demande qui etes vous?’’. Anauliza kuwa wewe ni nani?.
“Dis lui que cʾest Iʾofficié de Iʾembassade de Tanzanie ici au Burundi”. Mwambie kuwa mimi ni afisa kutoka ubalozi wa Tanzania hapa nchini Burundi. Nikamwambia yule kijana huku taratibu nikivigongesha vidole vyangu juu ya sakafu ya ubao wa ile kaunta. Yule kijana akayahamishia maongezi yake tena kwenye ile simu kisha baada ya maongezi mafupi akaikata ile simu na kukirudishia kile kiwambo mahala pake. Muda uleule akageuka tena na kunitazama akivunja ukimya.
“Allez maintenant, il est dans la chambre numero 302, il vous ettend”. Nenda sasa hivi yupo chumba namba 302 anakusubiri. Yule kijana akaniambia.
“A la fin de ce comptoire du côté droit tu vas voir Iʾassacaire. Ça sera bien si vous partez vite, parcequʾil reste avec un peu de temps avant quʾil ferme son bureau cette nuit’’. Mwisho wa hii kaunta upande wa kulia utaona lifti. Itakuwa vizuri ukiwahi maana amebakiwa na muda mfupi kabla ya kufunga ofisi yake usiku huu. Yule mwenzake akasisitiza.
“Je vous remercis beaucoup”. Ahsanteni sana.
Nikawashukuru wale vijana na kuanza kuondoka eneo lile. Niliiacha ile kaunta ya mapokezi na kushika uelekeo wa upande kulia nikitembea kwa utulivu na baada ya kuipita nguzo moja kubwa ya ule ukumbi upande wa kushoto nikaiona lifti ya lile jengo. Nilipochunguza vizuri nikagundua kuwa ile lifti ilikuwa ikishuka hivyo nikasimama na kusubiri mtu aliyekuwa...ITAENDELEA
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom