Riwaya: Ufukwe wa Madagascar

Riwaya: Ufukwe wa Madagascar

Mwamba,kimya!?
Au ndio hadi tujiunge what's sap group ukatuchanje buku buku?
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 44
Mtunzi:Kelvin Mponda
Kulikuwa na chupa kubwa ya mvinyo mwekundu aina ya Merlot ulikuwa nusu huku glasi mbili zikiwa kando yake. Kupitia zile glasi mbili pale mezani na ule mzinga wa pombe nikajiridhisha kuwa mle kulikuwa na watu wawili waliokuwa wakiyasindikiza maongezi yao kwa kile kinywaji na bila shaka mtu huyo mwingine ndiye angekuwa amehusika kumnyonga kinyama yule Padri wa kizungu mle ndani. Niliposogea karibu na kuchunguza pale juu ya ile meza nikaona kalamu na karatasi ingawa karatasi ile nilipoichunguza vizuri nikagundua kuwa ilikuwa haijaandikwa kitu chochote juu yake.
Kwa sekunde kadhaa nikasimama huku taratibu nikiyatembeza macho yangu mle ndani kupeleleza kama kungekuwa na kitu kingine cha kuziteka hisia zangu. Sikuona kitu chochote cha ziada kwani mandhari ya kile chumba hayakutofautiana kabisa na kile chumba nilichotoka. Jambo moja la kushangaza ni kuwa runinga iliyokuwa mle ndani ilikuwa ikiendelea kurusha matangazo yake kama kawaida. Kwa kweli sikuweza kupata picha kamili juu ya kilichokuwa kikiendelea mle ndani hadi kupelekea tukio la kunyongwa kwa yule padri wa kizungu. Hata hivyo kupitia ile kalamu na karatasi juu ya ile meza fupi mle ndani nilihisi kuwa huwenda yule Padri alikuwa amelazimishwa kutoa taarifa fulani na alipokataa kutoa ushirikiano mnyongaji akawa amepata sababu ya kutimiza adhma yake. Bado sikuweza kufahamu kilichokuwa kikiendelea mle ndani ingawa jina la Pierre Okongo sasa lilianza kupata nafasi kubwa ya kujadiliwa kichwani mwangu. Nikaendelea kujiuliza kuwa Pierre Okongo ni nani na yule Padri wa kizungu aliyenyongwa mle ndani alikuwa ameingiaje kwenye mkasa huu hatari usioeleweka. Bado sikupata majibu hivyo mawazo mengi bado yalikuwa yakipita kichwani mwangu.
Hatimaye nikaisogelea karibu maiti ya yule Padri wa kizungu huku nikiwa nimeziba pua yangu kwa kiganja ili kujikinga na ile harufu mbaya ya uvundo kisha nikaanza kiufanyia uchunguzi kwa kuipekua mifukoni. Nilipomaliza kufanya upekuzi wangu nikawa nimefanikiwa kupata kitabu kidogo cha sala ambapo nilipokipekua vizuri ndani yake nikaona kuwa kilikuwa kimegongwa mhuri wa kutambulisha kuwa kitabu kile cha sala kilikuwa ni mali ya kanisa la Katoriki dayosisi ya jimbo moja lililokuwa katikati ya jiji la Bujumbura. Zaidi ya pale sikuona kitu kingine cha ziada hivyo nikachukua kile kitabu kidogo cha sala na kukitia mfukoni.
Ghafla wakati nilipokuwa nikiendelea na uchunguzi wangu dhidi ya ule mwili wa yule Padri wa kizungu mle ndani mara nikasikia sauti za vishindo vya hatua za watu wakikimbia nje ya ile korido kuukaribia mlango wa kile chumba. Haraka nikahisi kuwa jambo la hatari lilikuwa mbioni kunikaribia hivyo sikutaka kusubiri badala yake haraka nikakatisha kwenye kile chumba kuelekea dirishani huku nikijipa tahadhari. Nilipofika pale dirishani nikasogeza pazia pembeni na kufyatua komeo la dirisha pana la kioo na kulifungua lile dirisha. Vile vishindo vya watu vikaongezeka kwenye ile korido na hatimaye kuja kukomea nje ya ule mlango wa kile chumba kisha ukimya mfupi ukafuata kabla ya kusikia kelele za kitasa cha ule mlango kikichokolewa kwa funguo.
Niliwahi kufungua lile dirisha haraka nikachungulia kule nje nikitazama kama kungekuwa na uwezekano wowote wa kutoroka eneo lile. Hata hivyo muundo wa jengo lile haukunipa nafasi nzuri ya kutimiza haraka azma yangu kwa kuwa hapakuwa na sehemu nzuri ya kuning’inia mbali na vijukwaa vifupi vilivyokuwa chini ya madirisha ya lile jengo. Hata hivyo nilipoendelea kuchunguza nikaliona bomba moja lililokuwa likisafirisha maji ya mvua kutoka sehemu ya juu ya paa la ile hoteli kwenda chini ya lile jengo. Lile bomba lilikuwa kiasi cha umbali wa mita kadhaa upande wa kushoto likipita kando ya dirisha la chumba kingine kilichokuwa jirani. Haraka nikawahi kujilaza pale dirishani kisha nikawihi kutanguliza miguu yangu nje ya lile dirisha. Kiwiliwili changu kilipopita nikamalizia kwa kuning’inia nje ya lile dirisha kwa mikono yangu huku nikiwahi kurudishia lile pazia na kulifunga lile dirisha kwa nje. Sasa nilikuwa nimening’inia kwenye ukingo mdogo wa lile dirisha na uzito wote mwilini ulielekea kuilemea mikono yangu.
Nikiwa bado nimening’inia pale dirishani nikageuka na kutazama kule chini na ule umbali ukanionya kuwa namna yoyote ya kukosa umakini katika kuning’inia pale dirishani kifo kilikuwa tayari kunipokea. Hata hivyo sikutaka kuondoka haraka pale dirishani kabla sijatafuta hakika ya wale watu waliokuwa kule nje mlangoni koridoni wakifanya jitihada za kuingia mle ndani.
Muda mfupi uliofuata ule mlango wa kile chumba ukasikika ukifunguliwa kwa kishindo cha nguvu kazi ya hali ya juu. Ule mlango ukafunguka kwa pupa na kujipigiza ukutani. Nikawahi kujivuta juu na kuchungulia mle ndani ya kile chumba kupitia uwazi mdogo ulioachwa na pazia la kile chumba pale dirishani. Nilipochungulia nikawaona wanaume wawili wakiingia mle ndani huku kila mmoja akiwa na bastola yake mkononi. Walikuwa wanaume warefu na weusi wenye miili iliyojengeka imara. Japokuwa watu wale hawakuwa wamevaa sare za jeshi lakini wajihi wao ulitosha kunitanabaisha kuwa walikuwa ni askari jeshi waliohitimu vizuri mafunzo ya juu ya kijeshi.
Kitu kilichonistaajabisha ni kuwa watu wale hawakuonekana kushtushwa kabisa na lile tukio la kunyongwa kwa yule Padri wa kizungu mle ndani badala yake walijikita katika kumtafuta mtu mwingine ambaye bila shaka mtu huyo alikuwa mimi. Nikamuona mwanaume mmoja kati ya wale wanaume wawili walioingia mle ndani akichepuka haraka na kuelekea kwenye chumba kidogo cha maliwato kilichokuwa kwenye kona ya kile chumba cha kulala ambapo alipofika akafungua mlango wa kile chumba kwa tahadhari na kutazama tazama mle ndani. Alipoona mle ndani hakuna mtu akarudi tena pale chumbani. Yule mwenzake akaendelea kusimama pale mlangoni huku akionekana kuchukua tahadhari za kiusalama za kila namna kujihami.
Nikiwa bado nimening’inia pale dirishani nikaendelea kuwachunguza wale watu hata hivyo haraka niligundua kuwa sura zao zilikuwa ngeni kabisa machoni mwangu. Hali ikanipelekea nijiulize maswali kadhaa kichwani mwangu kuwa watu wale walikuwa akina nani na walikuwa na shida gani. Wote walikuwa wamevaa suti nyeusi, mashati ya kijivu na tai nyeusi shingoni mwao huku kichwani wakiwa wamevaa kofia nyeusi nadhifu za pama. Yule mwanaume mmoja akaendelea kufanya upekuzi mle ndani na aliporidhika kuwa hapakuwa na mtu mle ndani nikamuona akimwonesha ishara fulani yule mwenzake pale mlangoni na hapo nikamuona yule mwenzake pale mlangoni akiwasha kifaa cha mawasiliano kilichokuwa shingoni mwake na kupelekea habari kwa mtu wa tatu ambaye sikumuona mle ndani.
Wakati yule mtu wa mlangoni akiendelea kumpasha taarifa huyo mtu wa tatu ambaye hakuwa mle ndani mara nikamuona yule mwenzake akigeuka na kutazama pale dirishani kama aliyehisi jambo fulani na kwa kutaka kuzitafutia hakika hisia zake nikamuona taratibu akipiga hatua zake hafifu za tahadhari kusogea pale dirishani nilipokuwa nimening’inia kwa nje. Kuona vile nikaamua kujidhatiti ili kukabiliana na rabsha zozote ambazo zingejitokeza. Hata hivyo mikono yangu ilikuwa imeanza kuchoka kuning’nia pale dirishani na hali ile ilizidi kunipa wasiwasi. Hata hivyo kabla yule mtu hajafika pale dirishani nikawa tayari nimekusanya nguvu za kujisogeza kando ya lile dirisha nikiendelea kuning’inia. Mikono yangu ilikuwa imeanza kutetemeka kutokana na nguvu nyingi niliyokuwa nikiitumia kuubeba uzito wa kiwiliwili changu na ingawa kulikuwa na hali ya hewa ya baridi kufuatia mvua za masika zilizokuwa zikiendelea kunyesha lakini mwilini nilianza kuhisi hali ya joto kali.
Yule mtu alipofika pale dirishani akasogeza pazia na kufungua lile dirisha akitazama tazama kule chini ya lile jengo. Hata hivyo niligundua haraka kuwa hakuwa ameniona kutokana na giza lililokuwa eneo lile na baada ya kuridhika na uchunguzi wake usio makini nikamsikia akimwambia neno fulani la kirundi yule mwenzake kule mlangoni kisha akatoa sigara kutoka mfukoni na kuiwasha akianza kuivuta taratibu pale dirishani. Kwa kweli nilikuwa nimeanza kuchoka kuning’inia pale dirishani hivyo nilianza kuona hatari ya kujiachia mzimamzima bila kupenda na hatimaye kuanguka chini ya lile jengo. Hata hivyo ule umbali wa chini ya lile jengo ulikuwa umenionya kuwa kujiachia pale ilikuwa ni sawa na kujiua kwa kifo cha aibu na woga wa kujisalimisha kwa wale watu.
Nikiwa mbioni kuishiwa nguvu pale dirishani niliponing’inia nikageuka tena na kulichunguza vizuri lile bomba la kusafirishia maji ya mvua kutoka sehemu ya juu ya lile jengo. Mara moja uchunguzi wangu makini ukabadilisha mawazo yangu kuwa sikuwa sahihi na sikupaswa kuyategemeza maisha yangu kwenye lile bomba kwani niligundua haraka kuwa lile bomba lilikuwa na udhaifu mkubwa katika baadhi ya maungio yake kutokana na kutofanyiwa ukarabati madhubuti wa mara kwa mara hivyo hofu ikajipenyeza upya moyoni mwangu.
Kadiri hali yangu ilivyokuwa ikizidi kuwa mbaya mawazo ya kutaka kupiga kelele na kumshtua yule mtu pale dirishani ili aniokoe yakawa taratibu yakianza kuniingia akilini mwangu kwani niliamini kuwa kwa muda usiozidi dakika tano baada ya pale hata nguvu za kusogea tena eneo lile nisingekuwa nazo tena. Nikiwa katika hali ile mara nikamsikia yule mtu aliyesimama pale mlangoni akimuita yule mwenzake wa pale dirishani. Muda uleule yule mtu aliyesimama pale dirishani akasitisha starehe yake ya kuvuta sigara kisha kile kipisi cha sigara akakitupa nje lakini bila kutarajia kile kipisi cha sigara kikaangukia kwenye vidole vyangu pale nilipong’inia na kuniunguza hata hivyo sikushughulika nacho kwani nguvu zilikuwa mbioni kuniishia. Haukupita muda mrefu mara nikamsikia yule mtu pale dirishani akifunga lile dirisha na kurudishia lile pazia. Muda mfupi uliofuata nikausikia mlango wa kile chumba ukifunguliwa na kisha kufungwa baada ya pale ukimya ukafuatia.
Sikuwa na sababu nyingine ya kuendelea kusubiri kwani nguvu za mikono yangu zilikuwa mbioni kuniishia na hali yangu ilikuwa ikizidi kuwa mbaya hivyo taabu nikakusanya nguvu na kufanikiwa kuupandisha mguu wangu mmoja pale dirishani. Nilipofanikiwa kuupandisha mguu mwingine nikawahi kushika pembe moja ya lile dirisha ambapo nilijivuta kwa nguvu zangu zote hadi pale nilipofanikiwa kukaa pale juu dirishani huku nikihema ovyo. Sikutaka tena kugeuka na kutazama chini ya lile jengo kwani kizunguzungu kilikuwa kimenishika vilivyo kutokana na msukumo mkubwa wa damu kichwani mwangu. Nilipojaribu kulifungua lile dirisha nikagundua kuwa yule mtu aliyekuwa amesimama pale dirishani muda mfupi uliopita alikuwa amelifunga lile dirisha kwa ndani kwa komeo hivyo hapakuwa na namna mbadala ya kurudi mle ndani bila ya kupasua kile kioo cha pale dirishani.
Bila kupoteza muda nikaikamata vizuri pembe moja ya lile dirisha kisha nikapiga kiwiko kimoja cha nguvu pale dirishani. Kioo cha lile dirisha kilipopasuka nikapenyeza mkono na kufyatua komeo na muda mfupi uliofuata nikawa nimerudi mle ndani ya kile chumba. Sikutaka kupoteza muda tena mle ndani hivyo haraka nikaelekea kwenye mlango wa kile chumba huku kidole changu kikiwa tayari mbele ya kilimi cha bastola yangu iliyokuwa ndani ya mfuko wa koti langu. Nilipofika pale mlangoni taratibu nikaufungua ule mlango kisha kwa tahadhari nikachungulia kwenye ile korido. Sikumuona mtu yeyote kwenye ile korido hivyo hali bado ilikuwa shwari. Hatimaye nikatoka kwenye kile chumba na kuingia kwenye ile korido. Niliwakumbuka wale watu wawili waliotoka mle ndani ya kile chumba muda mfupi uliopita kuwa wangekuwa wamekwisha toweka na kushika hamsini zao hata hivyo niliamini kuwa hadi kufikia wakati ule wale watu wasingekuwa wamefika mbali sana na eneo lile. Hivyo kwa kukwepa kukutana nao mara tu nilipotoka nje ya kile chumba nikashika uelekeo wa upande kulia wa ile korido nikitembea kwa tahadhari huku mara kwa mara nikigeuka na kutazama nyuma.
Mwisho wa ile korido upande wa kushoto kulikuwa na lifti na wakati nikifika eneo lile nikagundua kuwa kile chumba cha lifti kilikuwa kipo ghorofa ya 12 ya lile jengo. Hivyo nikabonyeza kitufe kando ya ule mlango kuiita ile lifti pale nilipokuwa. Kulikuwa na muda kidogo wa kusubiri kwani kile chumba cha lifti kiliendelea na safari yake hadi ghorofa ya 14 na hapo nikajua kuwa kulikuwa na mtu kwenye ile ghorofa ya 14 aliyekuwa ameiita ile lifti akitaka kushuka chini ya lile jengo. Hivyo baada ya muda mfupi kupita kile chumba cha lifti kikaanza kushuka chini.
Wakati nikiendelea kusubiri kile chumba cha lifti kinifikie mara nikajikuta nikishtushwa na sauti ya kishindo cha hatua za mtu aliyekuwa akikimbia kuja kwenye ile korido. Wasiwasi ukiwa tayari umeanza kiniingia nikageuka na kutazama kule mwanzo wa ile korido ambapo kulikuwa na korido na nyingine iliyokatisha mbele yake. Haukupita muda mrefu mara nikawaona wale wanaume wawili hatari wakitimua mbio na kuingia kwenye ile korido kunifuata huku bastola zao wamezishika mkononi. Niliwakumbuka vizuri wale watu kuwa ndiyo wale waliokuwa wametoka kwenye kile chumba chenye yule Padri wa kizungu aliyenyongwa muda mfupi uliopita na sikuwa na mashaka kuwa mlengwa wa mbio zile nilikuwa mimi.
Wasiwasi ukiwa umenishika taratibu nikageuka na kuchunguza lile eneo kama kungekuwa na mwanya wowote wa kutoroka. Kwa mara ya kwanza nikajikuta kwenye wakati mgumu baada kuhisi kuwa hapakuwa na sehemu yoyote ya kukimbilia na wale watu sasa walikuwa wakinikaribia kwa kasi ya ajabu. Sikuwa na namna ya kufanya hivyo haraka nikaingiza mkono kwenye mfuko wa koti langu na kuikamata vyema bastola yangu tayari kuanzisha mapamana. Wale watu ni kama tayari walikuwa wameishtukia janja yangu kwani mmoja aliwahi kufyatua bastola kunilenga ila kutokana na kule kukimbia kwake akawa amekosa shabaha hivyo ile risasi ikaniparaza begani na kwenda kupasua kioo cha dirisha lililokuwa mwisho wa ile korido tukio lile likasababisha sauti kali ya mpasuko wa kile kioo. Kuona vile nikaamua kujibu mashambulizi. Risasi mbili nilizofyatua zikawakosa wale watu hata hivyo zilifanikiwa kuipunguza kasi yao ya kunifikia ingawa wale watu bado hawakukata tamaa. Tukaendelea kutupiana risasi huku kila mmoja akichepuka na kujibanza kwenye kona za milango ya vyumba vilivyokuwa vikipakana na ile korido. Wale watu hawakutaka kunipa nafasi ya kuwatoroka hivyo wakawa wakinitupia risasi nyingi lakini zisizokuwa na shabaha nami sikuacha kuwaandama wale watu kwa risasi zangu na kwa kufanya vile nikafanikiwa kumpata mmoja begani.
Nikiwa mbioni kukata tamaa mara kile chumba cha lifti kikawa tayari kimefika kwenye ile korido na mlango wake ulipofunguka nikajitupa ndani kinyume nyume huku nikiendelea kujibu mashambulizi dhidi ya wale watu. Wale watu walitamani sana nisifanikiwe kuwatoroka hata hivyo risasi zangu ziliwazuia kunifikia kwa wepesi. Hatimaye ule mlango wa kile chumba...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 45

...cha lifti ukafunga na ile lifti ikaanza kushuka chini ya lile jengo. Mle ndani ya kile chumba cha lifti hakukuwa na mtu mwingine yeyote na hali ile niliipenda. Sasa akili yangu ikaanza kujiandaa namna ya kukabiliana na hatari yeyote ambayo ingejitokeza baada ya kufika chini ya lile jengo.
Sikufanikiwa kwani wakati kile chumba cha lifti kinafika ghorofa ya tatu ya lile jengo la Le Tulip Hôtel Africaine ghafla taa ya mle ndani ikazima na kisha kile chumba cha lifti kusimama. Kwa sekunde kadhaa nikaganda kama nyamafu nikishikwa na taharuki isiyoelezeka sambamba hofu kuanza kupenya taratibu moyoni mwangu. Hisia zangu zikanitanabaisha kuwa nilikuwa nimejitumbukiza kwenye hatari nyingine na tukio lile huwenda lingekuwa ni mtego wa kuninasa mzimamzima kama siyo hitilafu ya umeme ya kawaida.
Kutokana na mfumo wa kile chumba cha lifti hapakuwa na hewa iliyokuwa ikiingia au kutoka mle ndani hivyo nilianza kuishiwa pumzi taratibu huku nikitokwa na jasho jingi mwilini. Hata hivyo nilijipa uvumilivu huku nikijipa matumaini kuwa kama lile lingekuwa ni tatizo la umeme wa kawaida basi jenereta la umeme wa dharura wa lile jengo lisingechukua zaidi ya dakika tatu kabla kuwaka na hivyo safari yangu ingeendelea kama kawaida.
Hata hivyo kile nilichokuwa nikikiwaza hakikutokea kwani ule umeme haukurudi wala kile chumba cha lifti kuendelea na safari. Kwa zaidi ya dakika mbili nikakaa mle ndani na baada ya kuona hakuna uelekeo sikutaka kusubiri zaidi kwani hewa ya mle ndani ya kile chumba ilikuwa tayari imeanza kuwa nzito kiasi cha kunipelekea nianze kuhema kwa tabu. Haraka nikaingiza mkono mfukoni kuchukua kurunzi yangu ndogo ya kijasusi yenye mwanga mkali na kuanza kumulikamulika mle ndani. Kwa kufanya vile nikakiona kifuniko kidogo kilichokuwa sehemu ya juu katikati ya kile chumba cha lifti kikiwa kimefungwa kwa skrubu.
Bila ya kupoteza muda nikadandia kuta za kile chumba kwa miguu yangu na kuanza kufungua ule mfuniko kwa kisu changu kidogo chenye mkusanyiko wa vifaa vingi muhimu kama kiberiti cha gesi, bisbisi, uma mdogo, kijiko, opena na vifaa vingine vidogo vidogo muhimu. Baada ya muda mfupi nikawa nimefanikiwa kuufungua ule mfuniko na kuuweka kando huku moyoni nikiomba kuwa ule umeme wa lile jengo usirudi haraka kabla ya kukamilika kwa operesheni yangu.
Nilipouondoa ule mfuniko nikapenyeza kichwa changu kwenye lile tundu kule juu na kuanza kumulika. Kule juu kulikuwa na nyaya nyingi zinazopishana na machuma mengi yaliyoshikilia kile chumba cha lifti. Mle ndani hewa ilikuwa imeanza kuwa nzito na joto nalo lilikuwa likiongezeka taratibu. Nilianza kuzifuatilia zile nyaya na nilipohisi kuwa zisingenifaa chochote nikaamua kuachana nazo. Nilipoendelea kuchunguza vizuri nikauona mpira mwembamba uliopenya kwenye tundu ndogo kama la pipa la maji. Nilipoufuatilia ule mpira nikagundua kuwa ulikuwa ni mpira wa kiyoyozi cha kile chumba hivyo nikachukua kisu na kuukata kisha nikaanza kuuvuta. Muda mfupi uliofuata nikawa nimefanikiwa kuunyofoa ule mpira na hapo hewa safi na nyepesi ikaanza kupenya mle ndani na hapo akili yangu ikaanza kupata afya njema huku mwili wangu ukirudi katika hali yake ya kawaida. Sasa suala la hewa safi mle ndani likawa limerudi katika hali yake ya kawaida.
Nikaendelea kukwea juu zaidi ya kile chumba cha lifti nikipenya kwenye vile vyuma vya juu vilivyoshikilia kile chumba. Kulikuwa na mitambo mingine ya kuendeshea mjongeo wa kile chumba cha lifti ambayo hata nilipojitahidi kuichunguza mitambo ile bado sikuweza kufahamu namna ya ufanyakazi wake wa kazi. Baada ya kuvipita vile vyuma juu yake nikakutana na mfuniko mwingine wa chuma chepesi ambapo kulikuwa na nyaya nyingi za umeme zilizofungwa pamoja zilizokuwa zimepenya kwenye tundu dogo lililokuwa kwenye pembe ya ule mfuniko. Niliposogea karibu na kuchungulia kwenye lile tundu dogo kule juu nikaona uwazi mkubwa. Kwa msaada wa ile bisibis nikafungua kile kifuniko na kupenya zaidi kule juu. Muda mfupi baadaye nikawa nimetokezea sehemu salama zaidi iliyokuwa juu ya kile chumba katika eneo la wazi lililoniwezesha kuona vizuri kule juu ya kile chumba cha lifti na sehemu ya nje ya lile jengo kupitia kuta safi za kioo.
Upande wa kushoto eneo lile nikaliona bomba kubwa la chuma ingawa sikuweza kufahamu kuwa lile bomba lilikuwa likielekea wapi. Hata hivyo nilishawishika kulifuata lile bomba nikihisi kuwa huwenda lingekuwa msaada mkubwa katika kulitoroka eneo lile. Hivyo haraka nikalisogelea lile bomba na kujilaza juu yake kisha nikaanza kusota kwa tumbo nikielekea kule mbele lile bomba lilipokuwa likielekea. Lile bomba lilikuwa refu sana likipenya kwenye vipenyo kadhaa vya lile jengo.
Hatimaye nikafika sehemu ambapo lile bomba lilikuwa limebadili uelekeo na kuingia upande wa kulia. Nilipofika eneo lile sehemu ya chini nikaona vyumba vingi vinavyopakana na eneo kubwa la wazi. Hisia zangu zikanitanabaisha kuwa nilikuwa nimetokezea kwenye eneo la maliwato. Nilifurahi sana hivyo nikajiachia kwenye lile bomba na kutua kwenye vyoo vya wanaume vya ghorofa ile.
Kulikuwa na vyumba vitano vya vyoo eneo lile vilivyokuwa vikitazamana na eneo la wazi lenye masinki ya kunawia na vyoo vidogo vya marumaru vya haja ndogo ukutani. Mle ndani hapakuwa na mtu na mlango wa eneo lile ulikuwa umefungwa. Nikaachana na ule mlango wa eneo lile na kaingia kwenye choo kimoja. Nyuma ya kile choo kulikuwa na dirisha dogo la kioo linaloniwezesha kupenya vizuri hivyo nikafyatua komeo lake na kufungua lile dirisha. Halafu pasipo kupoteza muda nikapanda juu ya choo cha kukaa cha marumaru cha mle ndani kisha nikakanyaga tenki dogo la maji ya kusukumia uchafu na kuanza kupenya nikitoka nje ya kile chumba. Bado lile jengo lilikuwa limegubigwa na giza kila mahali na hali ile niliipenda sana kwani yeyote aliyekuwa akinifuatilia asingeweza kuniona kwa urahisi.
Mara baada ya kutoka kwenye lile dirisha nikaning’inia kwenye jukwaa dogo la zege lililokuwa chini ya lile dirisha huku nikitafuta namna ya kushuka kule chini ingawa sasa nilikuwa na matumaini ya usalama wangu kwani ule umbali wa kule chini ulikuwa umepungua. Nilipoendelea kuchunguza upande ule nikauona mti mmoja mkubwa wa kivuli hata hivyo matawi ya mti ule yalikuwa yameishia ghorofa ya pili hivyo ingenilazimu kushuka chini kwa ghorofa moja zaidi kabla ya kuyafikia matawi ya ule mti.
Sikuwa na namna nyingine ya kufanya hivyo nikaanza kuning’inia kwa tahadhari nikitoka dirisha la chumba kimoja kwenda dirisha la chumba kingine na ndani ya muda mfupi nikawa nimelifikia lile bomba dhaifu lililokuwa likitiririsha maji ya mvua kutoka kwenye paa la juu la lile jengo la ile hoteli. Nilipolifikia lile bomba nikaning’inia kwa tahadhari nikisota taratibu kushuka chini huku nikiwa mwangalifu lisije likakwanyuka na kuniangusha chini. Hivyo baada ya muda mfupi nikawa nimefanikiwa kulifikia paa dogo la dirisha la chumba kimoja cha ghorofa ya pili hivyo nikaliacha lile bomba na kurukia juu ya lile paa dogo la lile dirisha.
Nikiwa pale juu ya lile paa nikatulia kwa muda nikayatembeza macho yangu kulipeleleza vizuri eneo lile. Sikumuona mtu yeyote hivyo hali bado ilikuwa shwari na bila kupoteza muda nikajilaza tena juu ya lile paa nikianza kusota taratibu nikilifuata tawi moja la mti mkubwa wa kivuli uliokuwa kando kidogo na lile dirisha. Hatimaye nikawa nimelipata tawi moja imara lenye uwezo wa kuubeba uzito wangu bila mashaka yoyote. Taratibu na kwa tahadhari ya hali ya juu nikaanza kukwea lile tawi nikishuka chini ya ule mti. Macho yangu bado yalikuwa makini kulichunguza eneo lile. Muda mfupi uliofuata nikawa nimefanikiwa kushuka chini ya ule mti. Hata hivyo kabla ya kuondoka eneo lile nikatulia kidogo nikipeleleza kama kungekuwa na mtu yeyote eneo lile na niliporidhika kuwa bado nilikuwa salama nikachepuka na kuanza kutembea kwa tahadhari kando ya ukuta wa Le Tulip Hôtel Africaine nikipita kwenye vichaka vya maua ya kupandwa kuelekea mbele ya ile hoteli.
Wakati nikitembea nikawa nikiwakumbuka wale watu waliokuwa wakinifuatilia kule nyuma na lile gari jeupe Landcruiser na hatimaye kuzuiliwa na kile kizuizi cha askari jeshi kule barabarani na hapo nikajikuta nikiwahusisha wale watu na hawa niliofanikiwa kuwatoroka kwenye ile korido ya ghorofa ya tano ya lile jengo la hoteli muda mfupi uliopita. Sasa nilianza kuamini kuwa mpango wa kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa usiku ule kule nyumbani kwake ulikuwa umepangwa na kutekelezwa na kikundi cha askari jeshi wachache wa jeshi la wananchi wa Burundi huku nikishindwa kuelewa lengo lao.
Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na giza zito lilikuwa limetanda kila mahali. Nilichokuwa nikiwaza kichwani ni kuondoka haraka eneo lile kabla masaibu mengine hayajanikuta eneo lile. Nikaendelea kutembea kwa tahadhari nikilizunguka lile jengo la hoteli kuelekea kule mbele nilipokuwa nimeegesha gari langu. Nilikuwa na kila hakika kuwa wale watu waliokuwa wakinifuatilia kule ghorofani wakati watakapofanikiwa kukifungua kile chumba cha lifti na kushikwa na mshangao mimi ningekuwa tayari niko mbali na eneo lile nikitokomea na jambo hilo lingenipa faraja sana.
Hata hivyo mambo hayakwenda kama nilivyokuwa nimetarajia kwani wakati nikifikia mbele ya lile jengo la hoteli mara nikaliona gari moja la jeshi aina ya Nissan Patrol likiingia kwa kasi na kuegesha katika maegesho ya mbele ya ile hoteli. Kisha kabla ya mlango wa lile gari kufunguliwa haraka nikamuona mtu mmoja akichepuka kutoka sehemu ya mbele ya ile hoteli na kulifuata lile gari. Nilipozidi kuchunguza nikagundua kuwa yule mtu alikuwa miongoni mwa wale watu wawili niliotoka kupambana nao na hatimaye kufanikiwa kuwatoroka kule juu ghorofani kwenye ile korido ingawa sikuweza kufahamu yule mwenzake alikuwa wapi kwa wakati ule. Yule mtu alipofika kwenye lile gari kioo cha dirishani kikashushwa na hapo nikamuona yule mtu akiongea na mtu mwingine pale dirishani huku akimuelekeza kwa kidole juu ya lile jengo la ghorofa la ile hoteli.
Nilihisi jambo fulani lisilo la kawaida kuelekea kutokea eneo lile hata hivyo sikuweza tena kulifikia lile gari langu pale kwenye yale maegesho kwani lile gari Nissan Patrol lilikuwa limechukua nafasi kando ya gari langu baada ya gari jingine lililokuwa pale kuondoka. Haukupita muda mrefu mara nikaona milango ya lile gari Nissan Patrol ikifunguliwa kisha wakashuka wanaume kumi na moja pamoja na mbwa wawili wakubwa aina ya German Shephered wenye urefu sawa na ule wa ndama wa kisasa. Lile gari Nissan Patrol lilikuwa dogo kuweza kuwabeba wale watu wote hata hivyo kwa kuwa ililazimishwa basi iliwezekana. Sasa nilitambua kuwa kikosi cha kunisaka kilikuwa kimeongezwa kama moja ya mkakati makini wa kuhakikisha kuwa sipati mwanya wowote wa kutoroka.
Wale watu walioshuka kutoka kwenye lile gari walikuwa wamevaa makoti marefu ya kijeshi ya mvua na mikononi walikuwa wameshika bunduki. Muda mfupi uliofuata nikawaona watu wawili wakielekea pale kwenye gari langu baada ya kuelekezwa na yule mtu wa awali. Wale watu walipofika wakalizunguka gari langu na kuanza kulikagua kwa tahadhari kisha nikamuona mmoja akitia utundu na kufungua mlango wa lile gari langu akiingia mle ndani. Sikuweza kufahamu kwa haraka kuwa lipi lilikuwa lengo la yule mtu hata hivyo nilihisi kuwa chochote ambacho kingefanyika ndani ya lile gari bila shaka kingekuwa katika moja ya mikakati yao mingi ya kutaka kunikamata kama siyo kuniangamiza kabisa.
Wakati wale watu wakiendelea kushughulika na gari langu mara nikamuona yule mtu wa awali aliyevaa suti akiongozana na watu watatu miongoni mwa wale watu walioshuka kutoka kwenye lile gari la jeshi wakielekea kwenye ile hoteli. Wale watu sita waliosalia nikawaona wakijigawa katika makundi mawili yenye watu watatu na kila kundi moja likawa likiongozwa na mbwa mmoja. Kundi moja likashika uelekeo wa upande wa kushoto wa lile jengo la hoteli na kundi jingine likashika uelekeo wa upande wa kulia wakija kwenye ile kona ya lile jengo nilipokuwa nimejibanza.
Nikiwa nimeanza kuhisi hatari ambayo ingenikabili sikutaka kuendelea kusubiri zaidi eneo lile kwani kwa namna moja au nyingine sikuona tena kama kungekuwa na uwezekano wa kuondoka pale kwa kutumia lile gari langu. Hivyo taratibu nikayaacha yale maficho yangu na kuanza kuondoka eneo lile nikirudi kule nyuma ya lile jengo nilipotoka huku nikiwaza namna ya kulitoroka eneo lile kabla wale watu hatari hawajanifikia.
Mvua kubwa ilikuwa ikiendelea kunyesha na nilitambua kuwa hali ile ingeweza kuathiri uwezo wa wale mbwa kunusa ardhini. Hata hivyo niliamini kuwa pale ambapo wale mbwa wangeniona isingewachukua muda mfupi kabla ya kunifikia na hiyo ingekuwa hatari zaidi kwangu.
Nilikumbuka kuwa nyuma ya lile jengo la hoteli kulikuwa na msitu mkubwa wa miti ya kupandwa hata hivyo kulikuwa na kipande kirefu cha uwanda kabla ya kuufikia ule msitu ambao hata hivyo nilikuwa mgeni kabisa wa mazingira yale. Nafsi yangu ikanitanabaisha kuwa ndani ya ule ndiyo ingekuwa sehemu salama ya kukimbilia katika kuisalimisha roho yangu. Hivyo mara tu baada ya kufika nyuma ya ile hoteli nikachepuka nikiliacha lile jengo kwa tahadhari na kuanza kukimbia kuelekea kwenye ule msitu. Hata hivyo kabla sijafika mbali na eneo lile mara ghafla umeme wa lile jengo la hoteli ukarudi na hivyo kupelekea taa za nyuma ya lile jengo kuwaka na kuangaza kila mahali. Kwa kweli nililaani vibaya kitendo kile cha umeme kurudi mapema kabla sijatimiza azima yangu. Nilipogeuka kutazama upande wa kushoto wa ile hoteli nikawaona watu wawili miongoni mwa wale watu watatu waliopita upande wa kushoto wa ile hoteli. Yule mwenzao mmoja aliyekuwa na yule mbwa sikumuona na wala sikuweza kutambua kuwa alikua ameshika uelekeo upi.
Wale watu wakawa kama waliosita ghafla baada ya kuniona eneo lile na mimi kuona vile hofu ikaniingia moyoni haraka na hivyo kushawishika kuwa nianze kutimua mbio. Hata hivyo nilijionya juu ya kuanza kutimua mbio za ghafla kwani kwa namna moja au nyingine nilihisi kuwa kwa kufanya vile ningeweza kutengeneza hakika juu ya hisia za wale watu dhidi yangu. Hivyo nikaamua kukazana nikiongeza urefu wa hatua zangu kuelekea kule msituni huku nikiwatazama wale watu kwa jicho la pembe. Hata hivyo baada ya kutafakari nikagundua kuwa ile ilikuwa hila dhaifu sana ya kuweza kuwahadaa watu wale kwani kitendo cha wale watu kuniona nikiharakisha kutembea kikawapelekea na wao waanze taratibu kutimua mbio wakinifuata. Kuona vile nikazidi kuchanganya miguu nikikimbia kistaarabu hata hivyo wale watu hawakuniacha kwani haraka nikawaona wakiaongeza mbio na kukatisha chini ya miti ya kivuli ya eneo lile kunifuata.
Hatimaye sikuona tena sababu ya kuendelea kupoteza muda kwa kujifanya kuwa watu wale hawakuwa na hamsini na mimi hivyo nikakusanya nguvu na kuanza kutimua mbio za uhakika nikikatisha kwenye ule uwanda kuelekea kule msituni huku nikiwa nimechukua tahadhari za kila namna. Nilipogeuka nyuma kutazama nikawaona wale watu nao wakitimua mbio...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU:46
Mtunzi:Kelvin Mponda
...Kunifukuza huku mmoja akipuliza filimbi kuwashtua wenzake. Mwendo wangu haukuwa wa kubabaisha huku moyoni nikiamini kuwa ile ndiyo ingekuwa nafasi yangu nzuri ya kuwatoroka wale watu. Hata hivyo kabla ya kufika mbali mara nikaanza kusikia risasi zikifyatuliwa nyuma yangu. Hofu ikaanza kuniingia hata hivyo sikupunguza mwendo kwani niliamini kuwa kwa kadiri nilivyokuwa nikitimua mbio kupotelea kule mbele gizani ndivyo ambavyo nilivyokuwa nikiwapotezea malengo ya shabaha ya wale watu nyuma yangu. Hata hivyo wale watu hawakuniacha badala yake wakaendelea kunifukuza huku wakiendelea kunifyatulia risasi. Nilipoona ile mvua ya risasi inazidi kuninyea nikachomoa bastola yangu kutoka kwenye mfuko wa koti langu na kugeuka nyuma nikijibu mashambulizi lakini wakati ule sote tulikuwa gizani hivyo utupaji wangu wa risasi ulikuwa ni kama wa kubahatisha.
Hata hivyo kwa kufanya vile nikafanikiwa kumtungua mmoja miongoni mwa wale watu wawili kwani ghafla nilikuwa nimesikia sauti ya mtu akipiga yowe gizani nyuma yangu huku kukifuatiwa na kukoma kwa yale mashambulizi ya risasi nyuma yangu. Hata hivyo sikupunguza mwendo badala yake nikazidi kukata upepo kwa kasi ya mwanariadha mahiri nikielekea kwenye ule msitu mbele yangu. Wakati nikiendelea kutimua mbio nikawa nikijitahidi kutazama mbele yangu katika namna ya kutathmini vizuri mandhari ya ule msitu kwa usalama wa roho yangu.
Kwa kufanya vile kiasi cha umbali wa mita zisizopungua hamsini mbele yangu nikagundua kuwa kulikuwa na uzio mrefu wa seng’enge uliotenganisha eneo la ile hoteli na ule msitu mkubwa wa kupandwa. Nikaanza kupatwa na mashaka juu ya kufanikiwa kuuvuka ule uzio wa seng’enge salama kabla ya wale watu waliokuwa wakinifukuza nyuma yangu hawajanifikia. Nikiwa katikati ya fikra zile mara nikashangaa nikipigwa kumbo la nguvu lililonitupa kando bila jitihada zozote za kujihami na nilipotua chini nikajikuta tayari nipo chini ya kifua shupavu cha mbwa mkubwa mwenye uchu na windo lake. Nikajitahidi kufurukuta pasipo mafanikio kwani ile bastola yangu ilikuwa imeangukia mbali kidogo na eneo lile na ukubwa wa mbwa yule na nguvu zake hazikunipa ruhusa ya kufurukuta. Yule mbwa akawa akipenyeza kichwa chake ili aniume shingoni. Kwa kushtukia hila ya yule mbwa nikawahi kumzuia kwa mkono wangu wa mmoja na lile likawa kosa kubwa kwani yule mbwa haraka akaudaka mkono wangu kama adakavyo mfupa. Meno yake makali yakapenya na kuikamata vyema mifupa ya mkono wangu na tukio lile likasababisha maumivu makali yasambae mwilini mwangu.
Niliendelea kufurukuta pale chini pasipo mafanikio na hali ile ikazidi kunitia hofu kwani niliamini kadiri nilivyokuwa nikiendelea kukaa chini ya himaya ya yule mbwa ndivyo wale watu kule nyuma yangu walivyokuwa wakikaribia kunifikia.
Baada ya kufurukuta kwa kitambo hatimaye nikafanikiwa kuunasua mkono wangu kutoka kinywani kwa yule mbwa. Hata hivyo ni kama niliyekuwa nimefanya kazi bure kwani safari hii yule mbwa haraka aliuachia mkono wangu na kuniuma begani huku akiunguruma kwa hasira na kujaribu kunikwaruza kwa kucha zake kifuani mwangu.
Hofu ikiwa imeanza kuniingia sikutaka kuendelea kudhibitiwa tena na mnyama yule aliyezidiwa akili nyingi na binadamu. Hivyo haraka nikaingiza mkono mfukoni na kuchukua kisu mkunjo kisha nikamchapa yule mbwa kwa pigo moja madhubuti lililolichana vibaya tumbo lake na kupelekea utumbo wake kuchungulia nje. Hata hivyo yule mbwa hakuniachia na badala yake ni kama niliyekuwa nimempandisha hasira yule mbwa kwani kwa nguvu zake zote akajitahidi kuninyofoa begani na hapo maumivu makali yakasambaa mwilini. Nilipoona kuwa yule mbwa haelekei kuniachia nikamchapa mapigo mengine matatu ya kisu kwenye koo lake nikiazimia kumtia adabu. Safari hii yule mbwa hakufurukuta tena badala yake akasimama kimya akinitazama kama anayejiandaa kuimba wimbo wa taifa lake na hapo nikajua kuwa mapigo yangu yalikuwa yamemuingia vizuri. Yule mbwa hakuwa na ujanja tena hivyo bila kupoteza muda nikamsukuma kwa miguu yangu akiangukia kando kama mzigo na kuanza kulia kwa sauti ya huruma.
Haraka nikajiviringisha kando na kuikota bastola yangu kisha nikasimama na kuendelea kutimua mbio nikielekea kwenye zile seng’enge. Nilipozifikia zile seng’enge nikaanza kuziparamia kwa fujo. Zile seng’enge zikanichana vibaya mikononi kiasi cha kunisababishia majeraha mabaya yanayovuja damu hata hivyo sikuzembea kwani niliamini kuwa ile ndiyo ingekuwa salama yangu.
Nilipokuwa nikikaribia kufika juu ya ule uzio wa seng’enge mbwa mwingine akawa tayari amenifika na kunirukia akiuma kiatu changu mguuni. Nikajitahidi kujinasua bila mafanikio na nilipoona muda unaenda nikageuka na kumchapa yule mbwa risasi moja ya kichwa iliyomtupa chini na kutulia kimya na hapo nikapandisha mguu wangu na kuangukia upande wa pili wa ule uzio. Pasipo kusubiri nikasimama tena na kuanza kutimua mbio nikipotelea kwenye ule msitu mzito wa kupandwa wenye giza la kuzimu. Sikufika mbali mara nikaanza kusikia mvua ya risasi ikinisindikiza nyuma yangu hata hivyo sikugeuka nyuma badala yake nikaendelea kutimua mbio na baada ya muda mfupi nikawa nimetokomea kabisa ndani ya ule msitu.
Sasa nilikuwa nimetomea ndani ya ule msitu na hisia zangu zikanitanabaisha kuwa nilikuwa nimeingia kwenye ulimwengu mwingine. Japokuwa nilikuwa nimetoka kukiepuka kifo cha mateso makali nyuma yangu lakini mazingira ya msitu ule yalikuwa yamenisababishia aina nyingine ya hofu nisiyokuwa na hakika nayo. Ingawa miti ya ule msitu ilikuwa imepandwa kitaalam na katika mistari minyoofu lakini giza la mle msituni lililohanikizwa na kelele za bundi liliniletea hisia mbaya. Hata hivyo sikupunguza mwendo wala kurudi nyuma badala yake nikaikamata vyema bastola yangu mkononi na kuendelea kutimua mbio nikizidi kutokomea ndani zaidi ya ule msitu.
Mvua ilikuwa ikiendelea kunyesha na manyunyu yale yalirudisha nguvu mpya mwilini mwangu. Yale majeraha ya begani na mkononi yalikuwa yakiendelea kuvuja damu huku maumivu makali yakiendelea kusambaa mwilini. Hata hivyo sikuwa na namna kwani kwa namna nyingine ilikuwa ni afadhali kukabiliana na maumivu yale kuliko kifo kilichokuwa kikinifukuza nyuma yangu.
Baada ya mwendo mrefu wa kutimua mbio hatimaye nikawa nimefika kwenye eneo la ndani zaidi la msitu ule lililonipelekea nianze kuingiwa na hisia mbaya. Nywele zikanicheza, damu ikanichemka mwilini huku mapigo ya moyo wangu yakienda mbio isivyo kawaida. Utulivu ukiwa mbioni kutoweka kabisa moyoni mwangu hatimaye nikaingiza mkono kwenye mfuko wa koti langu na kuchukua kurunzi yangu ndogo ya kijasusi kisha haraka nikaiwasha na kuanza kumulika eneo lile. Nilichokiona kikanishtua sana kama siyo kuniogopesha.
Kulikuwa na kundi kubwa la fisi waliokuwa wakigombea minofu ya maiti za watu wafu. Fisi wale wakashtuka baada ya kuuona mwanga wa kurunzi yangu mkononi. Baadhi ya wale fisi wakaingiwa na mashaka hata hivyo wengine walionekana kunipuuza na kuendelea kujipatia kitoweo kile cha aibu na fedheha kwa binadamu. Kuona vile nikaanza kuokota mawe na kuanza kuwarushia wale fisi kwa hasira hata hivyo walionitii walikuwa wachache huku wengi wao wakiacha ile mizoga ya wafu na kuanza kujikusanya taratibu wakinisogelea na kunizunguka. Kuona vile nikaamua kuitumia bastola yangu mkononi kujihami na kwa kuwa bastola yangu ilikuwa na kiwambo maalum cha kuzuia sauti kazi ikawa rahisi tu. Risasi zangu zikawaangusha fisi watatu eneo lile huku wakibweka ovyo na kuwapelekea wale fisi wengine waanze kuniogopa wakigeuka nyuma na kuanza kutimua mbio wakitokomea mbali na eneo lile. Kitendo cha wale fisi kukimbia mbali na eneo lile kikanipelekea nipate nafasi nzuri ya kuanza kulipeleleza kwa makini eneo lile.
Baada ya kumulika eneo lile kwa muda mrefu nikitumia kurunzi yangu mkononi hatimaye nikagundua kuwa kulikuwa na miili ya watu sita iliyoharibika vibaya huku ikiwa imevuliwa nguo na kufungwa kwenye miti mikubwa iliyokuwa eneo lile. Niliposogea karibu na kuichunguza ile miili nikagundua kuwa wale watu walikuwa wameuawa kwa kufyatuliwa risasi kifuani na tumboni mwao. Nilipoendelea kuchunguza nikagundua kuwa kati ya wale watu wanawake walikuwa wawili na wanaume walikuwa sita kwa idadi yao na kwa makadirio ya umri wao watu wale walionekana ni wenye umri wa kati ya miaka thelathini na tano hadi sitini.
Uchunguzi wangu ukanitanabaisha kuwa wale watu walikuwa wamepitia mateso makali kutokana na hali mbaya ya miili yao kabla ya kuuawa kinyama. Watu wale walikuwa wamefungwa sehemu tatu kwenye miili yao kwa kamba ngumu zilizokazwa huku kila moja akiwa amefungwa kwenye mti wake. Walikuwa wamefungwa miguuni, kiunoni na shingoni huku macho na ndimi zao zimewatoka kiasi cha kuogopesha kurudia kuwatazama mara mbili. Miili ya watu wale ilikuwa imevimba sana na kuanza kuharibika ikitoa harufu mbaya na sikuona dalili zozote za uhai kwa watu wale. Kwa kweli nilijikuta nikishikwa na hasira dhidi ya unyama ule usiyomithirika. Ingawa sikuweza kufahamu kuwa watu wale walikuwa wametenda kosa gani hata hivyo sikuona kama ule ungekuwa ni ujira waliostahili kupewa. Machozi yakanitoka na hapo nikafumba macho kuyazuia yasidondoke ardhini.
Niliendelea kusimama eneo lile kwa tahadhari huku nikijiuliza ni kosa gani walilolifanya wale watu hadi wastahili kufanyiwa unyama ule wa kishenzi. Wakati nikiendelea kuwachunguza wale watu nikajikuta nikivutiwa zaidi na maiti ya mwanaume mmoja mwenye umri kati ya miaka arobaini na tano hadi hamsini. Mwanaume yule alikuwa amefungwa kwenye mti wa mwisho uliokuwa upande wa kushoto huku macho yamemtoka akitazama katika uelekeo tofauti kabisa na wenzake. Kupitia macho ya yule mtu nikawa nimehisi jambo fulani lisilo la kawaida na hapo nikajikuta nikishawishika kuanza kufuata uelekeo wa macho ya yule mtu kule yalipokuwa yakitazama.
Baada ya kutembea umbali wa takribani mita zisizopungua ishirini nikaliona shimo moja jembamba lililokuwa kando ya kichuguu kidogo. Nilipomulika kwa kurunzi yangu kutazama ndani ya lile shimo nikaona kuwa lilikuwa limejaa maji kufuatia mvua kubwa ya masika iliyokuwa ikiendelea kunyesha. Nilipoendelea kuchunguza kwenye maji ya lile shimo nikaziona nguo zikielea. Nilipoendelea kuzichunguza zile nguo nikagundua kuwa zilikuwa ni mchanganyiko wa nguo za kike na za kiume tukio lililonipelekea moja kwa moja niamini kuwa zile nguo zingekuwa ni za wale watu waliouawa kinyama na kufungwa kwenye ile miti ya ule msitu. Hisia zangu zikanipelekea nihisi kuwa kulikuwa na jambo nililokuwa nikipaswa kulifahamu zaidi juu tukio lile lisiloeleweka. Hivyo nikasogea karibu na lile shimo na kuziopoa zile nguo kwa kijiti kidogo nilichokiokota kando ya dimbwi lile. Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na giza zito lilikuwa limetanda kwenye ule msitu na hivyo kuupelekea ule msitu uzidi kutisha.
Nafsi yangu ikanisukuma nianze kujihisi kuwa ni kama niliyekuwa nikipoteza muda wangu bure kwa kujishughulisha na mambo yasiyonihusu. Hata hivyo kwa kuwa sikuwa na jambo lingine zito lililokuwa likinisubiri mbele yangu kwa usiku ule sikuona kama nilikuwa nikipoteza muda wangu bure. Hivyo baada ya kuziopoa zile nguo na kuziweka kando ya lile shimo nikaanza kuzipekua taratibu. Idadi ya zile nguo na jinsia ilikuwa imeendana na ile idadi ya wale watu waliokuwa wameuawa na kufungwa kwenye ile miti pale msituni hivyo sikuwa na shaka yoyote kuwa zile nguo zilikuwa ni za wale watu.
Nikiwa nimeanza kuhisi jambo fulani lisilo la kawaida haraka nikaanza kuzipekua zile nguo huku mara kwa mara nikigeuka na kuyatembeza macho yangu eneo lile katika namna ya kujihakikishia usalama wangu. Hatimaye nikawa nimemaliza kuzifanyia upekuzi zile nguo ambapo nilipata funguo tatu za magari tofauti na funguo moja ambayo sikuweza kuifahamu haraka kuwa ilikuwa ni funguo ya kufungulia kitu gani pamoja na kitambulisho kimoja cha mfanyakazi chenye utambulisho wa jina la Jean Aristide Wamba. Kitambulisho kile chenye jina la Jean Aristide Wamba kilikuwa kimemtambulisha mhusika yule kama meneja mkuu wa Banque de la République du Burundi iliyopo Avenue Des Non Aligens jijini Bujumbura. Chini ya kitambulisho kile nikaziona taarifa nyingine muhimu kama sanduku la posta, barua pepe, nukushi na namba za simu ya ofisini. Nikaendelea kukichunguza vizuri kile kitambulisho huku nikishindwa kuelewa nini kilichokuwa kikiendelea eneo lile. Zile kelele za wale fisi zikaanza kusikika tena wakiikaribia ile mizoga ya wale watu waliofungwa kwenye ile miti baada ya kuona hakuna mwendelezo wa upinzani. Kwa kweli nilijikuta nikishikwa na hasira hata hivyo sikuwa na namna ya kufanya kwani nilifahamu fika kuwa ingekuwa ni kazi ngumu kupambana na wale fisi wasiendelee kuitafuna ile mizoga ya wale wafu.
Huzini ikaniingia na kunipelekea nifumbe macho yangu na kumeza funda kubwa la mate kuitowesha hasira iliyokuwa ikifurukuta vibaya moyoni mwangu dhidi ya unyama ule wa aibu kufanyiwa binadamu. Hatimaye nikaichukua ile funguo moja isiyoeleweka na kile kitambulisho cha kazi na kuvitia ndani ya mfuko wa koti langu. Lakini wakati nikiwa katikati ya harakati zile kwa mbali mara nikaanza kusikia kelele za vishindo hafifu vya watu fulani wakija upande ule. Nilipogeuka nyuma na kutazama nikaona miale ya kurunzi nne ikimulika kuja eneo lile. Sikuwa na mashaka yoyote kuwa watu wale wangekuwa ni wale niliyokuwa nimewatoroka kule Le Tulip Hôtel Africaine muda mfupi uliopita. Hivyo sikutaka tena wale watu wanikute pale badala yake kwa tahadhari ya hali ya juu nikaanza kuondoka eneo lile na kushika uelekeo wa upande wa mashariki wa ule msitu. Nilipofika mbele nikachanganya miguu na kuanza kutimua mbio nikiwakimbia wale watu nyuma yangu.
Mvua kubwa ilikuwa ikiendelea kunyesha na kufuatia giza nene lililotanda angani ule msitu ulikuwa ukitisha mno. Hata hivyo hatari ya wanyama wakali ambao wangekuwa kwenye msitu ule kwangu ilikuwa ni afadhali zaidi kuliko kukabiliana na wale watu hatari waliokuwa nyuma yangu.
Sikukumbuka kutazama saa yangu ya mkononi hata hivyo nilihisi kuwa nilikuwa nimetumia muda usiopungua nusu saa kabla ya kukutana na mteremko mkali ndani ya ule msitu wenye majabali makubwa katika mikingamo yake. Nilipofika eneo lile nikapunguza mwendo na kuanza kushuka taratibu na kwa tahadhari huku bastola yangu ikiwa mkononi tayari kukabiliana na hatari yoyote ambayo ingejitokeza mbele yangu.
Hata hivyo wakati nikiendelea kushuka ule mteremko nikahisi kuwa kutoka pale sikuwa mbali sana na barabara kwani mara moja au mbili niliweza kusikia kelele za muungurumo wa injini ya gari zikivuma eneo lile ingawa sikuweza kufahamu barabara ile ya magari ingekuwa upande gani kutoka pale nilipokuwa. Niliendelea kushuka ule mteremko na baada ya mwendo mfupi nikaanza kuona sehemu ya wazi iliyojitenga na ule msitu mbele yangu iliyosongwa na vichaka...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 47
Mtunzi:Kelvin Mpond
...vya miti hafifu na nyasi ndefu. Nilipofika kwenye lile eneo nikaanza kukatisha katikati ya vichaka vile na kadiri nilivyokuwa nikiendelea mbele na safari yangu ndivyo zile kelele za muungurumo wa injini ya gari ulivyokuwa ukizidi kusikika. Hatimaye nikawa nimetokezea sehemu ya wazi kabisa na mbele yangu nikaiona barabara ya lami. Huwenda magari machache yalikuwa yametangulia kukatisha eneo lile kwani kwa mbali nilisikia makelele ya injini ya gari yakiyoyoma kabla ya kukoma na hivyo eneo lile kugubikwa na ukimya.
Sikutaka kuendelea kupoteza muda eneo lile kwani nilikumbuka kuwa nyuma yangu kulikuwa na wale watu waliokuwa wakinifuatilia. Hivyo nikaanza kutembea kwa tahadhari kandokando ya barabara ile nikishika uelekeo wa upande wa kushoto baada ya kuhisi kuwa ule ndiyo ungekuwa uelekeo sahihi wa kuelekea mjini.
Wakati nikiendelea kutembea nikaanza kuhisi kuwa angalau nilikuwa kwenye mazingira salama kidogo ukifananisha na kule nilipotoka ingawa bado sikuacha kuchukua tahadhari huku mara kwa mara nikigeuka na kutazama nyuma. Wakati nikiendelea kutembea mawazo mengi yakawa yakipita kichwani mwangu. Matukio yote yaliyojiri tangu nifike jijini Bujumbura yalikuwa yameniacha hoi sana kifikra na sasa mawazo yangu yalikuwa yamejikita katika kile chumba namba 403 cha ghorofa ya sita ya Le Tulip Hôtel Africaine aliponyongwa yule Padri wa kizungu. Hadi sasa sikuweza kufahamu ni sababu gani iliyokuwa imempelekea kiongozi yule wa kiroho kunyongwa kinyama namna ile.
Nilikumbuka maneno ya mwisho ya Sundi Masele mfanyakazi wa nyumbani kwa Bolozi Adam Mwambapa wakati aliponieleza kuwa nimtafute Padri Aloysius Kanyameza kuwa ni yeye ndiye angeweza kunipa taarifa nilizozihitaji. Kwa kweli sikuweza kufahamu ni wapi ambapo ningempata huyo Padri Aloysius Kanyameza kwa pale jijini Bujumbura lakini kitendo cha kumuona Padri yule kiongozi wa kiroho akiwa amenyongwa vibaya katika kile chumba kilichosemekana kukodiwa na mtu aliyesemekana kuitwa Pierre Okongo kilikuwa kimeniacha njia panda. Nikaendelea kutafakari huku nikihisi kuwa huwenda yule mtu aliyenyongwa kwenye kile chumba ndiye angekuwa huyo Padri Aloysius Kanyameza. Hata hivyo nilikuwa nimesita katika kuamini hivyo kwani jina la Kanyameza lilikuwa limenitatiza kidogo kwa kuwa lilikuwa ni jina la asili la watu wa Burundi ambao ni waafrika weusi kama mimi na yule alikuwa ni Padri wa kizungu kwa muonekano wake. Kwa kweli fikra zangu bado zilikuwa njia panda ingawa kwa namna moja au nyingine nilijiridhisha katika kuamini kuwa kama Pierre Okongo ndiye aliyekuwa amehusika na kifo cha yule Padri kwenye kile chumba namba 403 cha Le Tulip Hôteli Africaine basi kwa namna moja au nyingine alikuwa na mahusiano ya moja kwa moja na wale watu walikuwa wakiniwinda. Pierre Okongo ni nani na anahusika vipi kwenye huu mkasa?. Nikaendelea kujiuliza pasipo kupata majibu hata hivyo niliamini kuwa ukweli ungekuja kufahamika muda mfupi mbele ya safari.
Nikiwa naendelea kutembea kandokando ya ile barabara mawazo yangu yakajikuta yakihamia kwenye ule msitu niliotoka muda mfupi uliopita. Mara hii nikajikuta nikiwakumbuka wale watu waliouawa kinyama kwa kupigwa risasi huku wakiwa wamefungwa kwa kamba kwenye ile miti ya ule msitu. Kwa kweli niliuona ni kama ulikuwa mkasa uliokuwa ukujitegemea huku nikishindwa kabisa kufahamu kilichokuwa kikiendelea. Nilipoendelea kiwaza hisia fulani zikaanza kujengeka kichwani mwangu juu ya mauaji yale. Kupitia kile kitambulisho cha kazi nilichokikuta mfukoni kwenye zile nguo za wale watu waliouawa kule msituni ambazo nilikuwa nimeziopoa kwenye lile dimbwi la maji nilikuwa nimeamini kuwa miongoni mwa wale watu wafu alikuwepo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Jean Aristide Wamba ambaye kama kitambulisho kile kilivyoeleza mtu yule alikuwa ni meneja mkuu wa Banque de la République du Burundi.
Kama zile taarifa kwenye kile kitambulisho zilivyokuwa zikieleza binafsi niliamini kuwa meneja mkuu wa benki ya taifa kama ile alikuwa ni mtu muhimu sana katika suala zima la uchumi wa nchi. Hivyo kwa namna moja au nyingine wadhifa mkubwa wa mtu yule nisiyemfahamu nikaanza kuuhusisha na sababu ya kifo chake au vifo vya wale watu na suala la kimaslahi ingawa bado sikuweza kufahamu kuwa maslahi hayo yangekuwa katika mtazamo upi. Hatimaye mawazo yangu yakahamia kwa msichana mrembo mfanyakazi wa Havana Club aitwaye Veronica. Nilikuwa nimemuahidi Veronica kuwa ningemtembelea nyumbani kwake usiku ule mara baada ya kutoka kazini saa mbili usiku lakini sasa ilikuwa ikielekea kutimia saa nane usiku kwa mujibu wa majira ya saa yangu ya mkononi. Nikaendelea kuwaza kuwa huwenda ungekuwa usumbufu mkubwa kwenda kumgongea Veronica nyumbani kwake usiku ule hata hivyo nikapiga moyo konde na kujipa matumaini kuwa baada ya kufunguliwa mlango kwa kila hali ningejitahidi kumuelewesha kwa kila hali huku nikimpa sababu za uongo zilizonipelekea kuchelewa kufika kwenye miadi kwani vinginevyo sikuwa na sehemu nyingine ya kulaza mbavu zangu kwa usiku ule.
Wakati nikiendelea na safari yangu mara nikasikia muungurumo wa gari likija na nilipogeuka nyuma yangu kutazama nikauona mwanga hafifu wa taa za mbele za gari ukichomoza. Haraka nikawahi kuchepuka na kujibanza kichakani kando ya ile barabara. Muda mfupi uliofuata mara nikaliona gari ndogo aina ya Land Rover likikatisha eneo lile na nilipochunguza kwa makini nikawaona wanaume watatu ndani ya lile gari. Nikashawishika kutaka kujitokeza na kuomba lifti hata hivyo nafsi yangu ikawahi kunionya haraka juu ya kufanya vile pale nilipofikiria juu ya hatari ambayo ingenifika endapo wale watu kwenye lile gari wangekuwa ni miongoni mwa wale wanajeshi waliokuwa wakinisaka. Hivyo nikaendelea kujibanza kwenye kile kichaka nikiliacha lile gari linipite na kutokomea mbele ya safari.
Muda mfupi baada ya lile gari kutokomea nikatoka kwenye kile kichaka na kurudi barabarani nikiendelea mbele na safari yangu.
Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na ingawa nilikuwa sifahamu jiografia ya makazi ya jiji la Bujumbura lakini nilianza kuona athari ya mafuriko makubwa kuelekea kutokea endapo mvua ile ingeendelea kunyesha zaidi. Mara kwa mara nikaendelea kutembea kandokando ya ile barabara huku nikigeuka nyuma kutazama kama ningewaona wale watu waliokuwa wakinifuatilia kule msituni. Bado sikuwaona wale watu na sikuweza kufahamu kuwa walikuwa wamekwamia wapi hata hivyo niliendelea kujipa tahadhari.
Baada ya safari ndefu ya kutembea kwa miguu mara nikakutana mteremko mkali na chini ya ule mteremko kulikuwa na daraja kubwa. Nilipovuka lile daraja nikaanza kupanda mlima. Ilikuwa ni kabla sijamaliza kuupanda ule mlima mara nikasikia tena muungurumo wa gari nyuma yangu na nilipogeuka kutazama nikauona mwanga wa taa kali za mbele za gari lililokuwa likija nyuma yangu. Uzoefu wangu wa magari ukanitanabaisha kuwa lile lilikuwa ni gari kubwa. Tumaini jipya likafufuka moyoni mwangu hivyo haraka nikachepuka tena na kujificha kwenye kichaka kilichokuwa kando ya ile barabara. Haukupita muda mrefu mara nikaliona lile gari likishuka ule mteremko kwa kasi na lilipopita tu pale darajani likaanza taratibu kupanda mlima hali iliyonipelekea nihisi kuwa lilikuwa limebeba mzigo mzito. Kadri lile gari lilivyokuwa likikaribia usawa wa kile kichaka nilichokuwa nimejibanza kando ya ile barabara ndiyo nilivyofanikiwa kuliona vizuri lile gari. Lilikuwa ni lori kubwa la mizigo aina ya Fuso.
Nafsi yangu ikaniambia kuwa ule ungekuwa wakati muafaka katika kupiga hatua nyingine zaidi katika harakati zangu. Hivyo wakati lile lori likikatisha eneo lile na kuanza kupanda ule mlima haraka nikatoka kwenye kile kichaka kando ya barabara na kuanza kulikimbilia lile lori la mizigo kwa nyuma. Kwa kuwa lile lori lilikuwa likipanda mlima taratibu hivyo ndani ya muda mfupi tu nikawa tayari nimelifikia na nilipochunguza ile sehemu ya nyuma ya lile lori haraka nikagundua kuwa ilikuwa imefunikwa kwa turubai kubwa ili kuukinga mzigo uliokuwa mle ndani usilowane na ile mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha.
Nikaendelea kulikimbilia lile lori huku mara kwa mara nikigeuka nyuma na kutazama kama kungekuwa na mtu yeyote nyuma yangu. Sikumuona mtu yeyote hivyo hali bado ilikuwa shwari. Nilipolifikia lile lori kwa nyuma nikadandia na kuanza kupanda juu ambapo nililifungua lile turubai na kulisogeza kando kiasi cha kuniwezesha kuufungua ule mlango wa nyuma wa lile lori. Muda mfupi uliofuata nikawa nimefanikiwa kuingia mle ndani huku nikiwa tayari nimechukua tahadhari za kila namna za kujihami endepo mle ndani ningewakuta watu. Hata hivyo kwa kuwa kule nyuma kulikuwa kumefungwa na kufunikwa na lile turubai hivyo matumaini ya kuwakuta watu mle ndani yalikuwa hafifu sana. Mara tu nilipoingia mle ndani haraka nikachukua kurunzi yangu kutoka mfukoni na kuiwasha nikiangaza angaza mle ndani.
Lile lori lilikuwa limebeba magunia ya vitunguu na bila shaka lilikuwa likielekea jijini Bujumbura kwenye maeneo ya masoko na hali ile ikanipa matumaini ya kufika mjini pasipo usumbufu wowote. Lile lori likaendelea kupanda ule mlima kwa mwendo wa taratibu huku injini yake ikilalamika vibaya kila gia moja ilipokuwa ikipanguliwa na gia nyingine kuingizwa kutokana na ule mzigo mzito lililoubeba. Hata hivyo baada ya safari ndefu hatimaye lile lori likamaliza kupanda ule mlima na hapo mwendo kasi ukaongezeka tena.
Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha huku mara kwa mara nikisogeza lile turubai na chungulia kule nyuma barabarani kutazama kama kungekuwa na gari lolote likilifungia mkia lile lori. Bado hali ilikuwa shwari kwani magari machache yaliyojitokeza na kulifuata lile lori kwa nyuma yalilikaribia na hatimaye kulipita yakiendelea mbele na safari zao. Bado lile lori liliendelea kuchanja mbuga likiendelea na safari na kwa vile kule mbele miinuko ilikuwa imepungua hivyo mwendo wa lile lori nao ulikuwa umeongezeka.
Moyoni niliendelea kuomba kuwa tusikutane na kizuizi cha barabarani mbele ya safari. Wakati safari ikiendelea mawazo mengi yakawa yakipita kichwani mwangu huku nikijaribu kuunganisha mlolongo wa matukio yote yaliyojiri tangu nilipoanza safari yangu ya kijasusi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania. Mawazo yangu hatimaye yakahamia kwa Veronica huku nikijiuliza kama muda ule angekuwa tayari kunifungulia mlango wa nyumba yake na kunipokea kwa furaha kama wakati tulivyoachana kwenye ule mgahawa Havana Club asubuhi ile. Uzoefu wangu ulinieleza kuwa wanawake ni viumbe wanaoweza kubadilika ghafla kutegemea na nyakati na hisia zao hivyo upo uwezekano kuwa mara ya kwanza unapo onana na mwanamke akakuchangamkia na kukufurahia lakini muda mfupi baadaye mkipoteana na kuonana tena akakupuuza haraka na kukuchukia vibaya bila sababu za msingi. Moyoni niliomba sana kuwa Veronica asiwe miongoni mwa wanawake wenye hulka hiyo.
Safari ikiwa inaendelea nikaanza kuvuta picha namna nitakavyopokelewa na Veronica kwa bashasha zote kisha kuvuliwa nguo zangu na kutayarishiwa maji ya moto ya kuoga na baadaye kuandaliwa chakula kitamu cha kirundi kilichopikwa kwa ufundi wa hali ya juu na kutiwa vikorombwezo vyote vya mapishi. Kufika pale nikajikuta nikiomba tena kimoyomoyo kuwa sebuleni kwa Veronica kusiwe na makochi ili baaada ya kuoga na kupata mlo mzuri moja kwa moja anifungulie chumba chake na kunikaribisha kitandani kwake. Picha ya kufikirika iliyofuata baada ya pale ikaniacha nikitabasamu peke yangu katikati ya giza nene lililokuwa kule nyuma ndani ya lile lori la mizigo.
Ghafla nikiwa katikati ya mawazo yale mara nikahisi dereva wa lile lori alikuwa akijitahidi kupangua gia na kupunguza mwendo wa lile lori. Mawazo yangu yakahama, moyo wangu ukapoteza utulivu huku baridi nyepesi ikipenya kifuani mwangu. Haraka nikasogea na kusogeza lile turubai pembeni nikichungulia kwa tahadhari kule nyuma barabarani. Loh! koo langu likakauka ghafla baada ya kuliona lile gari la jeshi Nissan Patrol nililoliona likiingia na kuegesha kule mbele ya Le Tulip Hôtel Africaine likiwa umbali wa hatua chache nyuma ya lile lori. Dereva wa lile gari Nissan Patrol alikuwa amewasha taa za hadhari katika namna ya kumuashiria yule dereva wa lile lori asimame haraka.
Nikiwa na hakika kuwa wale watu kwenye lile gari Nissan patrol hawakuwa wameniona nikaendelea kuchungulia kupitia uwazi mdogo uliokuwa kwenye pembe ya lile turubai la lori. Kwa kufanya vile mbele ya lile gari nikawaona wanaume wawili ambao wote niliwakumbuka haraka kuwa walikuwa miongoni mwa wale watu kumi na moja walioshuka kwenye lile gari wakati lilipowasili na kuegesha kule nje ya Le Tulip Hôtel Africaine. Sasa nilikuwa na kila hakika kuwa mlengwa wa tukio lile la kusimamishwa kwa lile lori nilikuwa mimi. Bila kusubiri zaidi akili yangu ikaanza kufanya kazi ya ziada nikifikiria namna ya kujinasua kwenye hatari ile. Kwa kweli nilikuwa nimechoshwa sana na ile tabia ya kufuatwafuatwa kila niendapo hivyo uvumilivu wangu nao ulikuwa ukingoni.
Dereva wa lile lori akaendelea kupangua gia taratibu huku akionekana kutafuta sehemu nzuri ya maegesho kwani lile eneo la barabara lilikuwa limekaa vibaya sana kutokana na uwepo wa kona nyingi na kupakana na bonde kubwa upande wa kulia. Kitendo cha dereva wa ile Nissan Patrol kuliona lile lori likikawia kusimama kikampelekea aongeze mwendo zaidi na kulipita lile lori kwa kasi huku akiwa na lengo la kwenda kuliwekea lile lori kizuizi kwa mbele. Nafsi yangu ikaniambia kuwa ile ndiyo ingekuwa nafasi nzuri ya kuitorosha roho yangu mbali na wale watu hatari waliokuwa kwenye lile gari. Hivyo wakati lile lori likipunguza mwendo na kusimama baada ya kuwekewa kizuizi cha ghafla na ile Nissan Patrol kule mbele mimi nikaitumia nafasi ile kutoka haraka nyuma ya lile lori kisha nikajirusha chini kwa mtindo wa kininja nikijiviringisha kama gurudumu la gari na hatimaye kupotelea kwenye kichaka kilichokuwa kando ya ile barabara.
Kabla ya kutoweka eneo lile nilitaka kwanza kupata tathmini ya hakika kuwa wale watu waliokuwa wakinifuatilia kwenye lile gari Nissan Patrol walikuwa akina nani. Hatua chache mbele kutoka pale niliporuka lile lori likapungua mwendo na kusimama umbali mfupi nyuma ya ile Nissan Patrol. Muda uleule nikawaona wanaume wanne wakishuka kutoka kwenye ile Nissan Patrol huku wakiwa na bunduki zao mikononi. Nilipowachunguza wale watu nikagundua kuwa hawakuwa watu wa kufanya mzaha hata kidogo. Mmoja wao akaielekeza bunduki yake juu na kufyatua risasi kadhaa katika namna ya kutengeneza hofu kwa wale watu waliokuwa ndani ya lile lori kule mbele. Haukupita muda mrefu mara nikawaona tena wanaume wawili kati ya wale wanaume wanne walioshuka kutoka kwenye ile Nissan Patrol wakichepuka na kulizunguka lile lori kwa nyuma na bunduki zao mikononi.
Mara nikamsikia mwanaume mmoja kati ya wale wanaume wawili waliobakia kule mbele ya lile lori akitoa amri ya kuwataka wale watu waliokuwa kwenye lile lori washuke chini mara moja. Muda uleule nikamuona yule dereva wa lile lori akifungua mlango na kushuka chini taratibu huku akiwa ameongozana na vijana wawili wa kiume na mwanamke mmoja. Yule mtu...ITEANDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 48
Mtunzi:Kelvin Mponda

...aliyetoa amri ya kuwataka watu wote waliokuwa kwenye lile lori washuke chini akamsogelea yule dereva na kuanza kumshushia kipigo cha nguvu huku yule mwenzake akiingia mbele ya lile lori na kufanya upekuzi. Kule nyuma ya lile lori wale wanaume wawili wenye bunduki mkononi wakausogelea ule mlango wa nyuma wa lile lori kwa tahadhari kisha mmoja akashika kamba fupi iliyokuwa ikining’inia na kukwea kule nyuma akiingia mle ndani ya lori na kuanza kufanya upekuzi. Hata hivyo kitendo cha kuukuta ule mlango wa nyuma wa lile lori ukiwa wazi kikawa kimewapa mashaka na hapo nikawaona wale watu wakijipa tahadhari na kugeuka eneo lile wakiyatembeza macho yao taratibu kulipeleleza lile eneo la vichaka vilivyokuwa kando ya ile barabara.
Nikahisi kuwa hatari ilikuwa mbioni kunifikia kwenye kile kichaka nilichojibanza kando ya barabara hivyo taratibu nikakiacha kile kichaka na kuanza kushuka kwenye lile bonde msituni kando ya ile barabara. Nikaendelea kushuka kwenye lile bonde hadi nilipofika chini na hapo nikakutana na mto mkubwa wenye mawe mengi ambao kwa wakati ule ulikuwa mbioni kufurika kufuatia mvua za masika zilizokuwa zikiendelea kunyesha. Hisia zangu zikanitanabaisha kuwa kutoka pale nilikuwa karibu sana na kitovu cha jiji la Bujumbura hivyo nikaanza kutembea taratibu kando ya ule mto nikiufuata kule mbele unapoelekea.
Baada ya safari ya kitambo kirefu hatimaye nikafika sehemu ambapo mto ule ulikuwa ukikatisha chini ya daraja kubwa lenye barabara ya lami juu yake. Nikiwa chini ya lile daraja nikayaona magari machache madogo yakikatisha juu ya lile daraja. Sikuwa na shaka yoyote kuwa sasa nilikuwa karibu sana na eneo la mjini lenye makazi ya watu hivyo nikauacha ule mto na kupanda juu ya lile daraja nikishika uelekeo wa magharibi baada ya kuliona bango kubwa la barabarani linaloelekeza majina ya vitongoji vya jiji la Bujumbura na umbali wake kutoka pale. Kulikuwa na umbali mfupi kabla ya kufika katikati ya jiji la Bujumbura hivyo nikaendelea kutembea kwa utulivu kando ya barabara ile huku mara kwa mara nikigeuka na kutazama nyuma yangu kama kungekuwa na gari au mtu yeyote akinifuatilia. Sikumuona mtu yeyote wala gari hivyo hali bado ilikuwa shwari.
_____
Teksi niliyoikodi kutoka kwenye kituo cha kujazia mafuta cha Hash Petroleum nje kidogo ya jiji la Bujumbura kando ya ghala kubwa ya kuhifadhia mafuta ghafi ikanishushia hatua chache kabla ya ilipokuwa nyumba namba 37 ya shirika la nyumba la taifa la Burundi kwenye barabara ya Boulevard de Iʾindependence nyuma ya uwanja mkubwa wa mpira wa miguu wa Prince Rwagasore Stadium. Akili yangu ilikuwa imechoka sana kutokana na pilika za kutwa nzima hivyo sikutaka kuanzisha maongezi ya aina yoyote na dereva yule badala yake nikamlipa pesa yake na kushuka.
Ile teksi iliposhika hamsini zake na kutokomea mbali na eneo lile nikavuka barabara huku nikitazama majira kwenye saa yangu ya mkononi. Mara moja nikagundua kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa nane na nusu usiku. Nikaendelea kutembea taratibu huku utulivu katika mtaa ule ukinipa hadhari ya namna yake. Nilipofika mbele nikasimama kidogo kando ya ile barabara nikiyatembeza macho yangu kwa makini kuyapeleleza mandhari yale na niliporidhika na tathmini yangu nikaanza tena kutembea taratibu huku mikono wangu mmoja ukiwa ndani ya mifuko ya koti langu umeikamata bastola.
Lile eneo lilikuwa la hifadhi ya nyumba za taifa la Burundi hivyo hata makazi yake yalikuwa yamepangwa vizuri yakitenganishwa kwa barabara nzuri za lami. Nyumba aliyokuwa akiishi Veronica ilikuwa kwenye ghorofa ya pili upande wa kushoto baada ya kuipita bustani ndogo ya maua. Uchunguzi wangu ulihitimisha vile. Muda ulikuwa umesonga sana hivyo matumaini ya kumkuta Veronica akiwa macho kwa tafsiri nyingine yalikuwa madogo sana. Hata hivyo niliona kuwa kuchelewa kwenye miadi ilikuwa ni afadhali kuliko kutokufika kabisa.
Wakati nikiendelea kutembea kandokando ya ile barabara kumbukumbu juu ya Veronica wakati nilipoonana naye asubuhi ile ndani ya Havana Club ikaanza kujengeka taratibu kichwani mwangu. Veronica alikuwa msichana mrembo sana ambaye mwanaume yeyote angejisikia fahari kuwa naye. Umbo lake matata na sauti yake nyororo vilikuwa vimeuteka vibaya moyo wangu na kunipelekea nijihisi kuwa nimekuwa mateka wa nafsi mbele yake.
Baada ya kitambo kifupi cha safari yangu nikachepuka upande wa kulia na kuanza kuifuata barabara ndogo ya watembea kwa miguu iliyotengenezwa kwa vitofali vidogo vilivyounganishwa kwa ustadi wa hali ya juu. Barabara ile ikikatisha katikati ya majengo marefu ya ghorofa ya shirika la nyumba la taifa huku kando yake ikipakana na bustani nzuri za maua. Nilipoingia kwenye barabara ile haraka nikajihisi mpweke kwani giza lilikuwa zito mno na mvua nayo ilikuwa ikiendelea kunyesha. Ingawa baadhi ya nyumba zilikuwa zikiwaka taa kwenye baadhi ya majengo ya ghorofa ya eneo lile lakini mwanga wa taa zile haukuwa na msaada wowote katikati ya lile giza nene.
Nilipoupita mstari wa kwanza wa nyumba za ghorofa macho yangu yakawa makini zaidi wakati nikiukaribia mstari wa pili. Kidole changu kikiwa kimetuama vyema kwenye kilimi cha bastola ndani ya mfuko wa koti langu wala sikuwa na wasiwasi wowote. Nilipoufikia ule mstari wa pili wa nyumba za ghorofa nikachepuka na kuingia upande wa kushoto. Mara moja nikageuka nyuma kuangalia kama kungekuwa na mtu yeyote akinifuatilia. Sikumuona mtu yeyote hivyo hali bado ilikuwa shwari.
Kulikuwa na gari moja dogo jeupe aina ya Toyota double cabin iliyokuwa imeegeshwa chini mbele ya jengo la ghorofa la kwanza. Nilipolichunguza vizuri jengo lile nikagundua kuwa taa zake zote zilikuwa zimezimwa na hivyo kuashiria kuwa wakazi wa jengo lile walikuwa tayari wamekwisha lala usiku ule.
Nilipolifikia lile jengo la pili la ghorofa nikasimama na kulichunguza kwa utulivu na umakini wa hali ya juu. Tathmini yangu ikanitanabaisha kuwa lile jengo lilikuwa na ghorofa saba na kama lilivyokuwa lile jengo la kwanza jengo lile nalo lilikuwa limemezwa na giza zito kila mahali. Taa zote za lile jengo zilikuwa zimezimwa na hivyo kuashiria kuwa wakazi wake walikuwa wamelala. Upande wa kulia chini ya lile jengo nikaziona ngazi za kuelekea sehemu ya juu ya lile jengo.
Kabla ya kupanda zile ngazi nikasimama nikizitazama kwa utulivu na nilipohisi kuridhishwa na hali ya usalama wa eneo lile nikaanza kupanda zile ngazi taratibu kuelekea ghorofa ya pili. Hali ilikuwa tulivu hivyo wakati nikipanda zile ngazi nikawa nikisikia sauti dhaifu ya hatua zangu kwa kadiri nilivyokuwa nikijongea. Nikaendelea kuzipanda zile ngazi kwa utulivu huku mara kwa mara nikisimama na kuyapa masikio yangu utulivu wa hali ya juu.
Hatimaye nikamaliza kupanda zile ngazi na kujikuta nimetokezea kwenye korido ya ghorofa ya pili. Ilikuwa korido pana na ndefu sana kiasi kwamba sikuweza kuona mwisho wake. Mara tu nilipofika kwenye ile korido nikasimama tena nikiupima utulivu wa eneo lile. Bado hali ilikuwa shwari na hapakuwa na kiashiria chochote cha uwepo wa kiumbe hai eneo lile.
Kutokana na giza zito lililokuwa limetanda kwenye ile korido sikuweza kunasa picha halisi ya mandhari yale. Hivyo taratibu nikautumbukiza mkono wangu kwenye mfuko wa koti na kuchukua kurunzi ambapo niliiwasha na kuanza kumulika kwenye ile korido. Mara moja nilipochunguza nikagundua kuwa ile korido ilikuwa ikitazamana na milango mingi iliyochorwa namba juu yake. Uchakavu wa ile milango katika baadhi ya maeneo ikawa ni ishara tosha kuwa lile jengo lilikuwa likekula chumvi nyingi pasipo kufanyiwa ukarabati wa kuridhisha. Niliyakumbuka vizuri maelezo ya Veronica asubuhi ile aliponiambia kuwa alikuwa akiishi nyumba namba 37 katika ghorofa ya pili ya jengo lile hivyo nikajipa moyo kuwa bado nilikuwa sijapotea.
Taratibu nikaanza kutembea kwenye ile korido huku nikimulika na kuchunguza zile namba za milangoni. Baada ya kitambo kirefu kupita nikilifanya zoezi lile hatimaye nikauona mlango mmoja wenye namba 37 ukiwa katikati ya ile korido. Haraka nikazima kurunzi yangu na kuitia mfukoni kisha nikausogelea ule mlango na kuupima utulivu wa mle ndani kwa kutega sikio langu kwa karibu. Niliporidhika kuwa mambo yalikuwa shwari nikaanza kugonga taratibu pale mlangoni.
Niligonga mara kadhaa bila ule mlango kufunguliwa na hali ile ikaanza kunitia wasiwasi kuwa huwenda nilikuwa nimekosea mlango. Hata hivyo nilipoyatupia macho yangu pale mlangoni na kuiona namba 37 juu ya ule mlango nikapata matumaini kuwa bado nilikuwa sehemu sahihi. Hivyo nikaendelea kugonga tena kwa kishindo zaidi. Hata hivyo ule mlango haukufunguliwa wala kuwepo kwa dalili zozote za uwepo wa mtu mle ndani. Taratibu hisia mbaya zikaanza kupenya nafsini mwangu na kunipelekea nianze kuhisi kuwa huwenda Veronica alikuwa amenidanganya. Kwa nini Veronica anidanganye na alikuwa na sababu gani ya kunidanganya?. Nikajiuliza pasipo kupata majibu na hali ile ikaniacha njia panda. Nilipokumbuka begi langu dogo la shanta la mgongoni nililomuachia Veronica nikaanza kujilaumu kwa kuwa mwepesi wa kumuamini mlimbwende yule kutokana na kubabaishwa vibaya na uzuri wake.
Sasa nilikuwa njia panda katika kuamua uelekeo. Upande mmoja wa nafsi yangu ukawa unanisukuma kuwa niondoke eneo lile na kwenda kutafuta malazi katika hoteli yoyote ambayo ingekuwa jirani na eneo lile hadi hapo kutakapopambazuka huku upande mwingine wa nafsi yangu ukinisukuma kuwa niufungue ule mlango kwa hila na kuingia mle ndani huku nikiwa tayari kukabiliana na kitu chochote cha hatari ambacho kingetokea. Hata hivyo wakati nikiwa katikati ya hali ile mara ghafla nikasikia kitasa cha ule mlango kikichokolewa kwa funguo na kisha ule mlango kufunguliwa taratibu. Mwanga hafifu kutoka ndani ya kile chumba ukasababisha mshangao wa kipekee nafsini mwangu.
Msichana mzuri Veronica alikuwa amesimamia pale mlangoni. Kwa sekunde kadhaa nikasimama pale mlangoni nikimtazama Veronica huku macho yangu yakishindwa kuamini kama kweli msichana yule mzuri alikuwa ni yeye. Alikuwa Veronica hatimaye nafsi yangu ikanitanabaisha vile. Hata hivyo hakuwa Veronica yule niliyeonana naye kule Havana Club asubuhi ile akiwa katika sare zake za kazi kwani usiku huu uzuri wake ulikuwa umeongezeka maradufu na kuzichakaza vibaya hisia zangu. Nimewahi kukutana na wasichana wengi wazuri na warembo katika pilikapilika zangu lakini niseme kuwa Veronica alikuwa zaidi yao wote. Alikuwa amevaa nguo nyepesi ya kulalia, nightdress nyeupe iliyolichora vyema umbo lake maridhawa kuwahi kutunukiwa mwanamke wa duniani na hivyo kupelekea nguo yake nyekundu ya ndani kuonekana bila kificho chochote.
Macho yake legevu yaliyotoka kupambana na usingizi wa mang’amu ng’amu yakasimama yakinitazama kwa tuo kama mtu ambaye haamini anachokiona mbele yake. Hatimaye tabasamu jepesi likaanza kuchomoza usoni mwake na kunipelekea nijihisi kuwa sikuwa nimekosea mlango.
Hisia zangu zikiwa taabani macho yangu chakaramu yakaanza kufanya ziara ya kushtukiza kifuani pake na hapo kupitia kivazi chake chepesi nikasiona chuchu zake laini zilivyosimama kwa utulivu juu ya milima miwili isiyofahamu adha yoyote ya volkano. Kitovu chake laini chenye kishimo kidogo kikitengeneza ziada nyingine ya uzuri wake. Macho yangu yalipofika kiunoni pake nikaiona nyonga yake laini yenye mifupa miteke iliyopakana na mzigo imara wa makalio yaliyotuama vyema kiasi cha kumpelekea aonekane kama aliyeficha vipande vya mikate mapajani. Wakati nikiwa katika hali ile ya mduwao mara Veronica akavunja ukimya baada ya kuitazama saa yake ya mkononi.
“Gilbert…”
“Veronica…”
“Kwa nini umechelewa?” Veronica akaniuliza huku akijitahidi kudhibiti donge la hasira ya wivu kooni mwake. Ingawa tulikuwa tukielekea kufungua ukurasa mpya wa mapenzi na mlimbwende yule lakini hisia zangu zilinitanabaisha mapema kuwa Veronica alikuwa msichana mwenye wivu mkubwa juu yangu.
“Naomba kwanza unikaribishe ndani mpenzi”. Nikamsihi kwa utulivu huku usoni nikiumba tabasamu jepesi la kirafiki.
“Karibu ndani”. Veronica akanikaribisha kwa sauti dhaifu ya kinyonge huku akinipisha pale mlangoni. Bila kutia neno nikavua koti langu na kulitundika begani kisha nikaingia mle ndani na hapo Veronica akaufunga ule mlango nyuma yangu.
Wakati Veronica akimalizia kufunga ule mlango na kugeuka mimi tayari nilikuwa nimelitupa koti langu sakafuni kisha nikamkaribia pale mlangoni na kumshika kiunoni bila ruhusa yake hata hivyo nikashukuru kuwa sikukutana na upinzani wowote. Veronica akanitazama machoni kisha tabasamu maridhawa likachomoza usoni mwake.
“Kwanini umechelewa hivi mpenzi?”. Veronica akaniuliza kwa utulivu huku akiipitisha mikono yake nyuma ya shingo yangu na kupelekea chuchu za matiti yake kukitekenya kifua changu na kupelekea joto kali la mwili wake linifanye nijisikie faraja ya aina yake. Nilipomtazama Veronica machoni nikayaona machozi ya furaha yakianza kumtoka.
Veronica alikuwa na kiu sana ya penzi langu na sikutaka kuamini kuwa nilikuwa mwanaume wake wa kwanza lakini niseme kuwa hisia zetu ziliendana kwa kiwango cha juu kabisa kwa wapenzi. Kwa kiganja changu taratibu nikamfuta machozi lakini huwenda tendo lile halikuwa na umuhimu wowote kwake kwani haraka aliuondoa mkono wangu machoni mwake kisha akanivuta karibu na hapo ndimi zetu zikakutana. Nilichoweza kusikia baada ya pale ilikuwa ni sauti nyepesi ya pumzi yake namna ilivyokuwa ikipenya kwa fujo kwenye matundu ya pua yake sambamba na miguno isiyoeleweka ya mahaba. Nilitaka kuleta pingamizi kwa vile nilikuwa mchafu nikinuka jasho la kutwa nzima lakini sikufanikiwa.
Kama mtu aliyepandwa na wazimu wa mapenzi Veronica akanivua kofia yangu na kuitupilia mbali kisha akapenyeza mikono yake kifuani mwangu na kuanza kunivua nguo kwa pupa. Nilipotaka kumzuia akaning’ata mkono.
“Gilbert…”
“Naam Veronica…”
“Ulikuwa wapi mpenzi mbona umechelewa?”. Veronica akaniuliza kama mwehu huku akiufungua mkanda wa suruali yangu kwa pupa.
“Naomba unisamehe mpenzi kwa kuchelewa”. Nikanong’ona.
“Ulikuwa wapi?”. Veronica akaniuliza na wakati nilipokuwa nikijiandaa kutunga uongo ndimi zetu zikaingia tena kazini zikitekenyana taratibu mdomoni. Ingawa nilikuwa jasusi hatari wa...ITAENDELEA
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom