Riwaya: Ufukwe wa Madagascar

Riwaya: Ufukwe wa Madagascar

RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 39
Mtunzi:Kelvin Mponda

...wakigeuka na kunitazama kwa mashaka wakiendelea kuzipanda zile ngazi kwa bidii. Sikugeuka tena nyuma kuwatazama badala yake nikakazana kuzitupa hatua zangu kuendelea mbele na safari.
Nilipomaliza kushuka zile ngazi nikawa nimetokezea kwenye korido ya ghorofa ya nne ambapo nilishika uelekeo wa upande wa kushoto nikielekea mwisho wa ile korido sehemu kulipokuwa na lifti ya lile jengo ili nishuke chini. Hata hivyo wakati nilipokuwa nikiikaribia ile sehemu ya lifti ya lile jengo mara ghafla nikakiona kile chumba cha lifti kikitia nanga kwenye korido ya ile ghorofa ya nne kisha mlango wake ulipofunguka akatoka mwanaume mmoja mweusi, mrefu na mwenye misuli imara ya nguvu mwilini huku akiwa amenyoa upara. Macho ya mtu yule yalikuwa yamefichwa vizuri nyuma ya miwani nyeusi. Yule mtu alikuwa amevaa suti nyeusi ambayo kutokana na ukubwa wa mwili wake wenye misuli imara suti ile ilionekana kama ambayo haimtoshi vizuri kwa namna ilivyombana katika baadhi ya maeneo ya mwili wake huku weusi wa ile suti na rangi yake vikimpelekea aonekane kama mpingo.
Kitendo cha kumuona yule mtu akija ule upande wangu kikaupelekea moyo wangu ulipuke kwa hofu huku kwa tahadhari nikiipapasa bastola yangu chini ya lile sinia nililolibeba mkononi baada ya kuanza kuhisi hali ya hatari. Yule mtu kuona vile akawahi kuupeleka mkono wake kwenye mfuko wa koti lake la suti huku akinikazia macho kunitazama kwa makini. Nikameza fundo kubwa la mate huku nikijitahidi kutabasamu hata hivyo ni kama tabasamu langu liliishia njiani kwa hofu na kunipelekea nionekane kama ninayetaka kucheka pasipo kitu cha kuchekesha. Yule mtu aliponikaribia akazidi kukaza uso wake kunitazama huku taratibu akipunguza urefu wa hatua zake huku mkono wake mmoja ukiwa bado upo kwenye mfuko wa ndani wa koti lake la suti. Haraka nikagundua kuwa alikuwa akiipapasa bastola yake mfukoni tayari kukabiliana na chochote.
Hofu ikiwa imeanza kuniingia nikapiga moyo konde na kumeza funda kubwa la mate kuitowesha hofu iliyoanza kujengeka nafsini mwangu na katika harakati za kurudisha hali ya kujiamini wakati nikipishana na yule mtu nikamuuliza huku nikilazimisha tabasamu la kirafiki usoni mwangu.
“Y at-il quelque chose de mal patron?”. Kuna tatizo lolote bosi?.
“Occupe toi de tes affaires”. Fuata mambo yako. Yule mtu akanijibu kwa jeuri huku taratibu akiutoa mkono wake mfukoni na kunipiga kumbo hafifu huku akiendelea na safari yake. Kwa sekunde kadhaa moyo wangu ukawa ni kama ulioshika ganzi huku baridi nyepesi ikisambaa mwilini mwangu. Hata hivyo nilijitahidi kwa kila namna kuimeza hofu yangu huku nikiendelea mbele na safari yangu pasipo kugeuka nyuma.
Wakati nikikifikia kile chumba cha lifti nikagundua kuwa kilikuwa kimepanda ghorofa ya juu kumpeleka mtu mwingine hivyo nikabonyeza kitufe cha kushuka chini kuiita ile lifti. Ile lifti iliposhuka na mlango wake kufunguka haraka nikaingia mle ndani na kubonyeza kitufe cha kushuka ghorofa ya chini kabisa ya lile jengo.
Wakati nikishuka chini ya lile jengo la ile hoteli mawazo mengi yakawa yakipita kichwani mwangu. Kupitia wale wanaume wawili niliopishana nao wakati nikishuka zile ngazi kuelekea ghorofa ya nne ya lile jengo na yule mtu matata niliyepishana naye muda mfupi uliopita kwenye ile korido. Sasa nilikuwa na hakika kuwa uwepo wangu kwenye lile jengo la hoteli ulikuwa ukifahamika na adui zangu lakini vilevile nilipokumbuka juu ya vile vifaa vya kijasusi nilivyovigundua kwenye miili ya wale watu niliopambana nao kule ofisini. Ilikuwa ni ishara tosha kuwa nilikuwa nimejitumbukiza kwenye mkasa hatari wa mapambano dhidi ya watu wenye ujuzi wa hali ya juu katika masuala ya kijasusi. Hivyo nafsi yangu ikazidi kunionya kuwa niwe makini sana na nyendo zangu.
Ndani ya muda mfupi kile chumba cha lifti kikawa kimefika ghorofa ya chini kabisa ya lile jengo la ile hoteli New Parador Residence. Mlango wa kile chumba cha lifti ulipofunguka nikatoka nje na kupishana na wanaume wengine wawili ambao haraka waligeuka na kunitazama kabla hawajaingia kwenye ile lifti. Mara tu nilipotoka kwenye kile chumba cha lifti sikutaka kutoka nje ya lile jengo kwa kupitia ule mlango mkubwa uliokuwa sehemu ya mbele ya ile hoteli. Hivyo haraka nikashika uelekeo wa upande wa kushoto nikipotelea gizani nyuma ya ile sehemu ya mapokezi ya ile hoteli huku nikijitahidi kutoyavuta macho ya mtu yeyote ambaye angekuwa akinitazama.
Sikuwa mwenyeji wa mazingira yale hivyo kwa kila namna nilijitahidi kuwa mwangalifu. Nyuma ya ile sehemu ya mapokezi nikatokezea kwenye korido pana yenye mwanga hafifu. Nikaanza kuufuata uelekeo wa korido ile pasipo kutambua ilikuwa ikielekea wapi huku mara kwa mara nikigeuka nyuma kutazama kama kulikuwa na mtu yoyote ambaye angekuwa akinifuatilia. Sikumuona mtu yoyote hivyo hali bado ilikuwa shwari. Nilipofika kule mbele nikagundua kuwa ile korido ilikuwa imebadili uelekeo na kufuata upande wa kulia na niliposoma kibao elekezi kwenye ile korido nikagundua kuwa ule uelekeo ulikuwa ni wa kwenda kwenye sehemu za maliwato ya wahudumu wa ile hoteli. Hivyo nikauacha ule uelekeo na kuanza kushuka ngazi zilizokuwa mbele ya kona ya ile korido sehemu yenye giza. Niliporidhika kuwa nimetokomea kabisa gizani sehemu ile nikalitelekeza chini lile sinia kisha nikazivua zile sare za mhudumu wa ile hoteli na kulivaa vyema lile koti langu jeusi la mvua. Ile chupa ya mvinyo mwekundu wa gharama wa kifaransa Château Lascombes nikaitia kwenye mfuko wa koti langu na kuzidi kushuka zile ngazi gizani.
Nilipofika chini kabisa ya zile ngazi nikashika uelekeo wa upande wa kushoto nikitembea katika uchochoro mwembamba wenye giza nene. Nilitamani kuwasha kurunzi yangu mkononi hata hivyo nilijikuta nikisita kufanya vile baada ya kuhisi kuwa mwanga wake ungeweza kumvuta mtu yeyote ambaye angekuwa eneo lile.
Baada ya safari fupi hatimaye nikaanza kuuona mwanga hafifu wa taa kabla ya kusikia maongezi ya watu eneo lile. Nilipochunguza nikagundua kuwa nilikuwa nimetokezea kwenye sehemu ya jiko la ile hoteli na wakati nikiendelea kutembea nikahisi kuwa nilikuwa nikilikaribia zaidi lile eneo la jiko la ile hoteli. Kwa mbali niliweza kuwaona wapishi katika sare zao za kazi wakiendelea na shughuli zao kwenye jiko lile. Hewa ya mle ndani ilikuwa nzito kidogo kutokana na moshi mwingi na joto kali ambalo lilikuwa likitoka kwenye ile sehemu ya lile jiko.
Niliendelea kutembea kwa utulivu na nilipokaribia lile jiko upande wa kulia nikaiona korido nyingine ambayo chini yake ilikuwa imetandazwa mabomba mengi ya maji, gesi na nyaya za umeme huku eneo lile likitawaliwa na harufu ya mnuko wa mafuta ya vyakula.
Hatimaye nikauacha ule uelekeo wa lile jiko la ile hoteli na kuanza kuifuata ile korido ya upande wa kulia kwa tahadhari huku mara kwa mara nikigeuka na kutazama nyuma kama kungekuwa na mtu yeyote akinifuatilia. Baada ya umbali mfupi wa safari yangu mara nikauona mlango mmoja wa chumba cha stoo. Nilipochunguza vizuri nikagundua ule mlango ulikuwa wazi na ndani yake kulikuwa na watu kutokana na minongʾono hafifu iliyokuwa ikisikika. Kwa tahadhari nikaupita mlango wa kile chumba na kuendelea mbele na safari yangu na baada ya hatua chache nikakutana na korido nyingine inayokatisha mbele yangu. Nilipofika kwenye ile korido nikasimama na kuanza kulichunguza eneo lile kwa makini.
Kulikuwa na giza zito eneo lile ingawa kupitia mwanga hafifu uliopenya kutoka lile eneo la jiko niliweza kuona kwa shida mandhari yale. Ile korido kwa upande wa kulia ilikuwa ikielekea kwenye tenki kubwa la maji ya akiba ya ile hoteli na nilipochunguza vizuri nikagundua kuwa hakukuwa na uelekeo mwingine baada ya ile sehemu yenye lile tenki la maji. Hivyo nikaamua kushika uelekeo wa upande wa kushoto nikitembea katikati ya korido nyembamba inayotazamana na vyumba vyenye mitambo ya umeme huku bastola yangu ikiwa imetuama vyema mkononi.
Baada ya muda mfupi nikawa nimetokezea kwenye sehemu kubwa ya wazi yenye mitambo mingine mikubwa ya umeme wa lile jengo likiwemo jenereta kubwa umeme wa dharura. Nilipofika pale nikasimama tena nikiyapeleleza vizuri mazingira yale na kwa kufanya vile upande wa kulia nikauona mlango mkubwa wa wavu na nondo za chuma kuelekea sehemu ya nyuma ya ile hoteli. Hisia zangu zikanieleza kuwa angalau nilikuwa kwenye eneo salama lenye unafuu wa kutoroka kwangu ingawa kwa namna moja au nyingine nilikuwa nikiamini kuwa mpaka kufikia wakati ule lile jengo la ile hoteli New Parador Residence lingekuwa chini ya uangalizi mkali wa watu waliokuwa wakifanya mawasiliano na wale watu niliopambana nao kule juu kwenye ile ofisi ya meneja wa ile hoteli ghorofani.
Nilipoitazama saa yangu ya mkononi nikagundua kuwa muda ulikuwa umeenda sana hata hivyo nilihisi mafanikio kidogo katika kazi yangu. Hatimaye nikaikamata vyema bastola yangu mkononi na kuanza kulitoroka taratibu eneo lile lakini mara moja nikiwa katika harakati zile mara nikajikuta nikimezwa na mshtuko wa aina yake. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu na kupoteza utulivu huku nywele kichwani zikinicheza.
Hatua chache kutoka pale lilipokuwa lile jenereta la umeme wa dharura wa lile jengo la hoteli kulikuwa na mtu aliyesimama na sikuweza kuelewa ni kwa namna gani mtu yule hakuweza kushtukia uwepo wangu eneo lile. Ingawa kulikuwa na giza zito lakini miali hafifu ya mwanga wa taa uliopenya kutoka nje ya lile jengo uliniwezesha kumuona kwa shida kidogo yule mtu. Alikuwa mrefu zaidi yangu mwenye umbo lenye afya njema na alikuwa amevaa suti nadhifu ambayo sikuitambua haraka rangi yake kutokana na giza la ile sehemu na nilipomchunguza vizuri yule mtu nikagundua kuwa mkononi alikuwa ameshika bastola.
Yule mtu alikuwa akitazama upande mwingine wa lile eneo huku akiyatembeza macho yake huku na kule kama atafutaye kitu na hapo nikawaza kuwa huwenda yule mtu alikuwa mbali na lile eneo muda mfupi uliopita kabla ya kufika pale. Niliwahi haraka kurudi nyuma na kujibanza kwenye kona moja ya ukuta wa eneo lile huku kwa makini macho yangu yakimtazama yule mtu.
Kitambo kifupi cha ukimya kikaumeza mshtuko wangu huku nikiendelea kumtazama yule mtu kwa makini na bastola yangu mkononi. Baada ya kitambo kifupi mara nikamuona yule mtu akianza kuzitupa hatua zake kwa tahadhari kuja pale nilipojibanza huku akionekana kama aliyehisi jambo fulani. Macho yangu yakiwa makini kumtazama yule mtu nikaanza kujiandaa kumkabili. Hata hivyo kabla hajanifikia mara nikaona taa ndogo ya kijani ikiwaka kwenye sehemu ya ukosi wa koti lake la suti shingoni. Tukio lile likampelekea yule mtu asite kuendelea mbele na safari yake badala yake haraka akaupeleka mkono wake shingoni kurekebisha kifaa chake cha mawasiliano. Uzoefu wangu ukanitanabaisha kuwa kulikuwa na mtu mwingine mbali na eneo lile aliyekuwa akitaka kuwasiliana na yule mtu bahati mbaya sana maneno machache ya lugha waliotumia kuwasiliana watu wale sikuielewa ingawa nilikuwa na kila hakika kuwa ilikuwa ni lugha ya kirundi.
Muda mfupi baada ya mawasiliano kwenye kile kifaa cha mawasiliano cha yule mtu kukatika hewani mara nikamuona yule mtu akisitisha kuja pale nilipokuwa nimejibanza na badala yake haraka akabadili uelekeo akikatisha kwenye ile korido niliyotoka na kutokomea gizani. Kwa sekunde kadhaa nikaendelea kujibanza eneo lile huku nikiupisha utulivu nafsini mwangu. Ile sauti ya hatua hafifu za yule mtu taratibu ikaendelea kutokomea mbali na eneo lile na hatimaye kukoma kabisa. Sasa nilikuwa na kila hakika kuwa yule mtu alikuwa shirika moja pamoja na wale watu hatari waliokuwa wakiisaka roho yangu kwa udi na uvumba.
Kitambo kifupi cha ukimya kikapita wakati nikiendelea kufanya tathmini ya hali ya usalama wa eneo lile. Nilipojiridhisha kuwa hapakuwa na mtu mwingine eneo lile taratibu nikayaacha maficho yale kwa tahadhari na kuelekea kwenye ule mlango mkubwa wa nondo na wavu. Nilipofika na kuuchunguza vizuri ule mlango nikagundua kuwa lile geti lilikuwa limefungwa kwa mnyororo mkubwa na kufuli moja imara hata hivyo sikupata upinzani wowote kwani mfukoni nilikuwa na funguo zangu maalum kwa ajili ya kushughulika na maeneo korofi kama yale. Hivyo kwa tahadhari nikaifungua ile kufuli na kisha kuufungua na ule mnyororo. Nilipotoka nje nikaurudishia vizuri ule mlango na kulifunga lile geti kama nilivyolikuta.
Sasa nilikuwa nimetokezea sehemu ya nyuma ya lile jengo la New Parador Residence na mbele yangu niliweza kuona mabwawa matatu makubwa ya kupigia mbizi katika uwanja mkubwa wenye nyasi nzuri za kijani kibichi. Mabwawa yale yalikuwa yamezungukwa na viti maalum vya kupumzika chini ya miavuli mikubwa yenye rangi za kupendeza. Umbali mfupi baada ya ile sehemu yenye yale mabwawa ya kupigia mbizi kulikuwa na viwanja vitatu vikubwa vya michezo. Kiwanja kimoja cha mpira wa kikapu, kingine cha mpira wa mikono na kiwanja cha mwisho kilikuwa cha mazoezi ya viungo ya kawaida.
Eneo kubwa lililosalia lilikuwa ni la kiwanja cha mpira wa golf hata hivyo kiwanja kile kilizungukwa na sehemu nzuri zenye viti visivyohamishika vya kupumzika vilivyokuwa chini ya miti mirefu ya vivuli. Mandhari ile ilikuwa ni ya kupendeza sana hata hivyo nilipoendelea kulichunguza lile eneo sikuweza kumuona mtu yeyote ingawa hali ile haikuwa kigezo tosha cha kunihakikishia kuwa eneo lile halikuwa chini ya ulinzi.
Nikiwa bado nayatathmini vizuri mazingira yale kando ya ule mlango mkubwa wa wavu na nondo mara ghafla nikauona mwanga mkali wa kurunzi ikimulika mulika mle ndani kwenye lile eneo la chini la lile jengo nilipotoka muda mfupi iliopita. Haraka nikawahi kusogea kando na kujibanza huku nikichungulia na kutazama mle ndani. Kwa kufanya vile nikawaona wanaume wawili wakiwa na bastola zao mikononi huku mmoja akiwa ameshika kurunzi mkononi mwake.
Kulikuwa na mabishano hafifu baina yao ingawaje sikuweza kuambulia kitu kupitia ile lugha waliyokuwa wakiizungumza ambayo niliihisi kuwa ilikuwa ni lugha ya kirundi. Hata hivyo kupitia vitendo niliweza kuhisi kiini cha mabishano yale baina ya wale watu wawili.
Yule mtu aliyeshika ile kurunzi mkono wake mwingine ulikuwa umezishika zile sare za mhudumu wa ile hoteli ambazo muda mfupi uliopita nilikuwa nimetoka kuzivua na kuzitelekeza mle ndani gizani. Yule mtu alikuwa akimuonesha mwenzake zile nguo huku akimfokea kwa jazba dhahiri akionekana kushikwa na hasira. Kupitia tukio lile nikafahamu kuwa mpango wangu wa kutoroka kwenye lile jengo haukuwa siri tena kwani wale watu hatari tayari walikuwa wameingʾamua vyema hila yangu...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 40
Mtunzi:Kelvin Mponda

Tayari wasiwasi ukiwa umeanza kuniingia mara nikawaona wale watu wakisogea kwenye ule mlango mkubwa nondo na wavu na kuanza kumulikamulika kwenye ule mnyororo na lile kufuli huku wakionekana kushikwa na mshangao baada ya kuona ile sehemu ikiwa imefungwa vizuri. Muda mfupi uliofuata mara nikamsikia yule mtu aliyeshika ile kurunzi mkononi akimwambia jambo fulani yule mwenzake kisha akazima ule mwanga wa kurunzi mkononi mwake na hapo wale watu wakaanza kuondoka haraka eneo lile.
Nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa watu wale walikuwa bado hawajakata tamaa juu yangu na sasa walikuwa katika harakati za kubuni mkakati mwingine makini zaidi wa kunikamata kabla sijafika mbali hivyo sikutaka kuendelea kupoteza muda wangu zaidi eneo lile. Haraka nikayaacha yale maficho yangu kando ya ule mlango mkubwa na kuanza kuambaa mbaa kwa tahadhari nyuma ya lile jengo huku mara kwa mara nikiyatembeza macho yangu huku na kule kutazama kama kungekuwa na mtu yeyote eneo lile. Mvua kubwa ilikuwa ikiendelea kunyesha na huwenda hali ile ndiyo iliyokuwa imepelekea mazingira yale kukimbiwa na watu. Hata hivyo kidole cha mkono wangu wa kushoto kilikuwa kimetulia vyema juu ya kilimi cha bastola yangu ndani ya mfuko wa koti langu tayari kukabiliana na rabsha yoyote ambayo ingejitokeza mbeleni.
Wakati nikitembea ikafika sehemu mwanga wa taa za nyuma za lile jengo ukawa ukinimulika hali iliyonipelekea nichepuke haraka kando ya lile jengo na kupita chini ya miti na baada ya muda mfupi nikawa nimetokezea nyuma ya kile kibanda chenye mashine za ATM kilichokuwa kando ya lile jengo la ile hoteli hata hivyo sikumuona mtu yeyote eneo lile. Ile sehemu yenye viti na miamvuli ya kujipumzishia nyakati za jua nayo haikuwa na mtu hata mmoja bila shaka kutokana na ile mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha.
Kwa kukwepa kutiliwa mashaka na mtu yoyote nikaamua kukatisha nyuma ya kibanda cha mlinzi wa ile hoteli nikielekea kwenye lile eneo la maegesho ya magari mbele ya ile hoteli huku nikiwa makini kuchunguza kama kungekuwa na mtu yeyote eneo lile. Muda mfupi uliofuata nikawa nimelifikia lile eneo la maegesho ya magari la ile hoteli na mara moja nilipochunguza nikagundua kuwa kulikuwa na magari mawili yaliyoondoka na gari moja liliongezeka baada ya mimi kuingia kwenye ile hoteli. Nilipochunguza lile gari lililoongezeka nikagundua kuwa lilikuwa ni gari aina ya Landcruiser Vx jeupe.
Sikutaka kuendelea kupoteza muda zaidi eneo lile kwani tayari nilikuwa nimeanza kuhisi mambo hayakuwa shwari tena hivyo mara tu nilipolifikia gari langu nikalikagua haraka kisha nikafungua mlango na kuingia ndani. Bila kusubiri muda uleule nikawasha gari na kuyaacha yale maegesho huku bado nikiendelea kuyatembeza macho yangu huku na kule kuchunguza kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akizifuatilia nyendo zangu. Sikumuona mtu yoyote na baada ya muda mfupi nikawa nimetoka kabisa nje ya geti la mbele la ile hoteli.
Wakati nikiwa katika harakati za kutokomea mbali na ile hoteli mara kwa mbali nikawaona watu wawili wakitoka kwa kasi kwenye mlango wa mbele wa ile hoteli na kuelekea kwenye lile eneo la maegesho ya magari la ile hoteli. Kitendo cha kuwakumbuka wale watu wawili wenye kurunzi walioondoka ile sehemu ya chini ya ile hoteli nikahisi nini ambacho kingefuatia baada ya pale. Hivyo nikaongeza mwendo na kuzidi kutokomea mbali zaidi na eneo lile.
_____
Bado nilikuwa katika barabara ya Boulevard du 28 Novembre na mwendo wangu wa gari haukuwa wa kubabaisha. Mvua kubwa ya masika ilikuwa ikiendelea kunyesha na giza zito lilikuwa limetanda angani hali iliyopelekea magari machache kwa wakati ule kuonekana barabarani. Wakati nikiendelea na safari yangu moyoni nikawa nikiomba kuwa nisikutane na kizuizi kingine chochote cha barabarani ambacho kingenitia hatarini.
Niliendelea na safari yangu huku mara kwa mara nikitazama nyuma yangu kupitia vioo vya ubavuni vya gari ili kuona kama kuna gari lolote lililonifungia mkia au lah!. Mambo bado yalikuwa shwari kwani sikuliona gari lolote nyuma yangu hata hivyo sikupunguza mwendo. Muda mfupi baadaye nikayapita makutano ya barabara ya Boulevard du 28 Novembre na barabara ya Chaussée P.L. Rwagasore nikiiacha hoteli ya City Hill upande wa kulia. Hatimaye nikaipita barabara ya Avenue De LʾUNESCO upande wa kushoto mbele kidogo baada ya kulipita jengo la kiwanda cha sabuni.
Nilipoyafikia makutano ya barabara ya Boulevard du 28 Novembre na ile barabara ya Avenue de la Dynastie upande wangu wa kulia nikaliona gari jeupe aina ya Landcruiser kama lile nililoliona kwenye lile eneo la maegesho ya magari la New Parador Residence likiingia kwenye barabara ile na kuanza kunifuata kwa nyuma. Wasiwasi ukaniingia huku nikitafuta hakika kama gari lile lilikuwa likinifungia mkia au lilikuwa kwenye hamsini zake. Nikaendelea kulichunguza lile gari kupitia vioo vya ubavuni vya gari langu huku nikiendelea na safari kwa umbali mrefu katika barabara ile hata hivyo lile gari nyuma yangu halikuniacha.
Wasiwasi ukiwa umeanza kuniingia akili yangu ikaanza kufikiria namna ya kukabiliana na hatari ya namna yoyote ambayo ingenikabili endapo watu waliokuwa ndani ya lile gari wangekuwa na dhamira mbaya na mimi. Lakini wakati nikiwa katika harakati za kupanga mikakati ya kujihami mara nikashangaa kuliona lile gari nyuma yangu likipunguza mwendo na kuingia upande kushoto kuifuata barabara ya Aveneu du Iʾuniversite iliyokuwa ikieleke chuo kikuu cha Burundi. Mara moja nilipolichunguza vizuri lile gari ubavuni nikaiona nembo kubwa ya Université du Burundi inayolitambulisha gari lile kuwa ni mali ya chuo kikuu cha Burundi. Kuona vile nikaachia msonyo mrefu mdomoni huku taratibu utulivu ukianza kutafuta hifadhi moyoni mwangu na hapo nikaingiza tena gia na kukanyaga mafuta nikiendelea kuchanja mbuga.
Wakati nikiendelea na safari mawazo mengi yakawa yakipita kichwani mwangu yaliyokusanya mlolongo mrefu wa matukio yote yaliyotokea tangu siku ile nilipoondoka jijini Dar es Salaam kuja pale Jijini Bujumbura nchini Burundi. Hatimaye mawazo yangu yakaweka kituo na kukumbuka mambo yote yaliyotokea kwenye lile chumba 302 cha ghorofa ya tano ya lile jengo la ile hoteli New Parador Residence nililotoka muda mfupi uliopita. Nikawakumbuka vizuri wale watu niliopambananao na kufanikiwa kuwaangamiza huku wote wakijifanya kuwa ni wafanyakazi wa ile hoteli. Kwa kweli sikuweza kufahamu walikuwa wakifanya vile kwa maslahi ya nani, waliwezaje kunifahamu na kujua kuwa ningefika pale kwenye ile hoteli.
Hata hivyo nilipoyakumbuka vizuri maelezo ya yule mtu mfupi aliyejinadi kwangu kuwa ndiye meneja wa ile hoteli angalau nikapata faraja kidogo. Bila shaka ule ulikuwa ni mpango ulioandaliwa kikamilifu na watu waliomteka balozi Adam Mwambapa na huwenda walikuwa wakifahamu vizuri kuwa nilikuwa pale jijini Bujumbura kwa kazi moja tu ya kumtafuta balozi Adam Mwambapa. Nikaendelea kukumbuka vizuri maelezo ya yule mtu mfupi aliyejinadi kwangu kwa jina la Vital Desire Habonimana huku akionekana kunifahamu vizuri kiasi cha kulitaja jina langu halisi pasipo kigugumizi cha namna yoyote. Maswali mengi yakaanza kuibuka kichwani mwangu.
Mtu yule alilifahamu vipi jina langu wakati mimi na yeye hatukuwahi kufahamiana hapo kabla?. Uongozi wa ile hoteli uliwezaje kuwaruhusu watu wa namna ile kutekeleza mpango wao mchafu wa kutaka kuniangamiza?. Jambo gani lilikuwa likiendelea kiasi cha kupelekea Balozi Adam Mwambapa kutekwa?. Nikaendelea kujiuliza maswali mengi pasipo kupata majibu ingawa kwa namna moja au nyingine niliamini kuwa tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa lilikuwa limeratibiwa na kutekelezwa kwa utaalam wa hali ya juu maana Balozi Adam Mwambapa hakuwa mtu wa kuingilika kirahisi pamoja na umri kumtupa mkono. Mwishowe mawazo yangu yakahamia kwa Padri Aloysius Kanyameza ambaye yule kijana aitwaye Sundi alikuwa amenigusia na kunitaka nikamtafute.
Nikaendelea kuwaza huku nikijiuliza ni kwa namna gani mtumishi huyo wa kiroho alikuwa ameingia kwenye mkasa huu hatari. Sundi alikuwa akifahamu nini kuhusu Padri Aloysius Kanyameza na kwanini aliangua kicheko hafifu katikati ya maumivu makali ya jeraha lake kubwa la kisu tumboni wakati nilipokuwa nikimuuliza maswali machache juu ya tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa?. Majibu sikuyapata na kwa kweli hali ile ilikuwa imenipelekea nijihisi ni kama niliyekuwa nimetupwa kwenye shimo refu la msongo wa mawazo pasipo dalili ya mtu yeyote kunitupia kamba ya kuniokoa kutoka katika kadhia ile.
Mawazo yangu yaliporudi mle ndani ya gari nikashtukia kuwa tayari nilikuwa nimeyafikia makutano ya barabara ya Boulevard du 28 Novembre na barabara ya Avenue de Iʾimprimerie upande wa kushoto kando ya kiwanda kidogo cha kusindika samaki wa kutoka Ziwa Tanganyika. Kitendo cha kuyaona makutano yale ya barabara kikanipelekea nipunguze mwendo na kuingia upande wa kushoto nikiifuata barabara ndefu ya Avenue de Iʾimprimerie eneo la Ntahangwa iliyokuwa ikikatisha katikati ya makazi ya watu.
Muda mfupi baada ya kuingia kwenye barabara ile mbele yangu nikakutana na kizuizi cha barabarani cha askari jeshi wakiwa katika makoti yao marefu ya mvua na bunduki zao mkononi. Askari mmoja akaingia barabarani na kunipiga mkono wa kunitaka nisimame. Kwa kweli nianza tena kuingiwa na wasiwasi huku taratibu nikipunguza mwendo wa gari kukikaribia kile kizuizi. Wakati nilipokuwa nikiendelea kupunguza mwendo mara nikawaona askari wengine wawili wakijitokeza kando ya barabara ile na kuingia barabarani huku wakiwa na bunduki zao mikononi katika namna ya kuonesha msisitizo kuwa nilipaswa kusimama.
Sikuwa na namna ya kufanya hivyo taratibu nikaanza kupunguza mwendo huku nikivificha vifaa vyangu muhimu vya kazi na nilipoyapeleka macho yangu kutazama kwenye vioo vya ubavuni vya gari langu ghafla nikajikuta nikishikwa na mshtuko. Lile gari Landcruiser jeupe nililokuwa nimeliacha kwenye vile viunga vya maegesho ya magari vya New Parador Residence sasa lilikuwa umbali wa mita chache nyuma yangu. Niliweza kulikumbuka vizuri lile gari kupitia sahani ya namba zake na gurudumu moja la akiba lililokuwa limefungwa juu ya boneti ya lile gari. Kwa kweli nilitamani nishuke kwenye gari na kuanza kutimua mbio nikipotelea kwenye vichaka vya jirani na eneo lile hata hivyo nafsi yangu ilinionya kuwa huwenda lile lisingekuwa jambo rahisi kama nilivyodhani kwani kile kilikuwa kizuizi kikubwa zaidi cha barabarani na chenye askari jeshi wengi zaidi kuliko vizuizi vyote nilivyowahi kukabiliana navyo pale jijini Bujumbura hadi kufikia wakati ule.
Wakati nikisimama eneo lile mara nikaona kuwa kulikuwa na magari mengine mawili yaliyokuwa yamesimamishwa kando ya ile barabara eneo lile yakifanyiwa upekuzi na askari jeshi wengine walioshika bunduki zao mkononi. Nikiwa nimesimama katikati ya ile barabara mara nikamuona yule askari aliyewahi kunisimamisha pale barabarani akizitupa hatua zake taratibu kusogea pale nilipokuwa nimesimamisha gari langu huku akiwa ameikamata vyema bunduki yake mkononi. Kuona vile ikabidi nishushe kioo cha mlangoni taratibu huku nikimtazama yule askari katika uso wa mashaka. Hata hivyo sikuweza kumuona vizuri usoni kutokana na kofia ya koti lake la mvua iliyokuwa imeukinga vyema uso wake.
“Bonsoir mon commandant?’’. Habari za usiku afande?. Nikawahi kumsalimia yule mwanajeshi hata hivyo hakuitikia na wala sikuona tashwishwi yoyote usoni mwake badala yake akanikata jicho kali la hadhari. Aliponifikia akajipangusa maji ya mvua usoni kwa kiganja chake na kisha kuniambia kwa sauti ya ukali.
“Mettez votre vehicule.`a côté de la route”. Egesha gari lako pale kando ya barabara. Sikutaka kuleta ubishi wowote hivyo taratibu nikaendesha gari langu na kwenda kuegesha mbele kidogo kando ya ile barabara hata hivyo sikushuka kwenye gari.
Kitambo kifupi kilipopita mara nikamuona yule mwanajeshi akisogea taratibu pale nilipoegesha gari langu kando ya ile barabara. Alipofika akainama kidogo dirishani akichunguza chunguza mle ndani ya gari kabla ya kuniuliza kwa utulivu.
“Dʾoù venez vous cette nuit?’’. Unatoka wapi usiku huu?.
“Commandant, je viens de Iʾuniversité de Burundi”. Natoka chuo kikuu cha Burundi afande. Nikadanganya huku nikiongea kwa kujiamini kana kwamba sikuwa na wasiwasi wowote nafsini mwangu. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku yule askari akanitazama kwa makini kabla ya kuniambia.
“Montre moi votre carte”. Nioneshe kitambulisho chako. Yule askari akaniambia huku akiendelea kunitazama kwa makini. Akili yangu ikasumbuka kidogo kisha nikakumbuka kuwa katika droo iliyokuwa kwenye dashibodi ya lile gari Hidaya alikuwa ameniwekea kitambulisho feki kinachonitambulisha kama afisa wa ubalozi wa Tanzania pale nchini Burundi. Hivyo haraka nikaifungua ile droo na kuchukua kile kitambulisho na kumkabidhi yule askari. Yule askari akakipokea kile kitambulisho na kukipitishia macho haraka kisha akanirudishia huku akinitazama kwa makini kabla ya kuniuliza.
“Où allez vous?”. Unaelekea wapi?.
“Je vais à Iʾavenue de IʾOUA chez moi”. Naelekea mtaa wa OAU nyumbani kwangu. Nikamjibu yule afande huku nikijitia kutazama saa yangu ya mkononi katika namna ya kuashiria kuwa alikuwa akinichelewesha.
“Ouvrez le capot du vehicule, je veus controler”. Fungua buti ya gari nahitaji kukagua. Yule askari hatimaye akaniambia huku akijitia kutabasamu hata hivyo sikupingana na ombi lake badala yake nikavuta kabari ya buti ya lile gari chini ya usukani na hapo ile buti ya gari ikafunguka. Yule askari kuona vile taratibu akielekea nyuma ya gari langu kuchunguza kwenye buti. Nikiwa ndani ya gari nikaendelea kuomba kimoyomoyo kuwa Mungu aniepushe mbali na hatari yoyote ambayo ingejitokeza eneo lile.
Nikaupisha utulivu kichwani mwangu huku nikitazama nyuma ya gari kupitia vile vioo vya ubavuni na kwa kufanya vile mara nikashikwa na mshtuko. Niliwaona wanajeshi nane haraka wakisogelea karibu na kulizingira lile gari jeupe Landcruiser lililokuwa limenifungia mkia nyuma yangu huku wanajeshi wale wakiwa na bunduki zao mkononi. Haraka nikahisi kuwa kulikuwa na jambo la hatari lililokuwa likielekea kutokea eneo lile.
Kwa sauti ya ukali na mara nikamsikia mmoja wa wale wanajeshi mwenye cheo cha Meja akiwaamrisha watu wote waliokuwa ndani ya lile gari jeupe Landcruiser washuke chini. Hata hivyo pamoja na amri ile ya ukali bado sikuona dalili za mtu yeyote kutaka kushuka kwenye...ITAENDELEA
 
Dah Hao maafande watachazwa kwa risasi muda si mrefu....mwee...
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 41
Mtunzi:Kelvin Mponda

...Lile gari badala yake ukimya usio na majibu ukaendelea kutawala eneo lile. Wakati yale yakiendelea yule askari nyuma ya gari langu akawa amemaliza kufanya upekuzi kwenye buti ya gari akimulika kwa kurunzi yake mkononi. Hivyo akafunga haraka ile buti ya gari kule nyuma na kupitia kioo cha ubavuni nikamuona akija tena kule mbele kwa haraka na alipofika pale dirishani akainama kidogo na kuniambia.
“Dʾaccord, vous pouvez continuer avec votre voyage”. Okay, unaweza kuendelea na safari. Yule afande akaniambia hata hivyo nilisita kidogo kwa vile nilikuwa sijamsikia vizuri na macho yetu yalipokutana akanifanyia ishara kwa kichwa akinitaka niondoke eneo lile.
“Merci, bon travail”. Ahsante, kazi njema. Haraka nikamwambia yule afande huku nikiingiza gia na kuanza kuondoka sehemu ile.
“Et vous aussi”. Na wewe pia. Yule afande akaitikia huku akianza kurudi kule nyuma kando ya barabara lilipoegeshwa lile gari jeupe Landcruiser. Haraka nikalitoa gari kwenye kile kizuizi na kuingia barabarani na wakati nikifanya vile nikaanza kusikia majibizano ya risasi nyuma yangu yakifanyika kati ya wale wanajeshi wa kile kizuizi na watu waliokuwa ndani ya lile gari Landcruiser.
Lile gari lilikuwa limeanza kuondoka kwa kasi kunifuata nyuma yangu pasipo kufanyiwa ukaguzi hivyo wale wanajeshi walikuwa wakilizuia lisiondoke. Hata hivyo dereva wa lile gari alikuwa amedharau ile amri ya wale askari na hivyo kuamua kuondoka pasipo ruhusa. Lile gari halikufika mbali kwani risasi za wale askari zikawa zimefanikiwa kupasua magurudumu yake na hivyo kulifanya lile gari liende kwa mwendo wa kuyumba yumba barabara nzima kabla ya kusimama. Nikapunguza mwendo kidogo baada ya kukipita kile kizuizi nikitaka kushuhudia nini ambacho kingefuatia baada ya pale. Lile gari jeupe Landcruiser liliposimama milango yake ikafunguliwa kwa ghafla kisha wakashuka wanaume wanne na kuanza kutimua mbio wakielekea kwenye pori lililokuwa jirani na eneo lile. Muda uleule mara nikamuona mmoja wao akisombwa vibaya na kutupwa hewani kwa shambulio la risasi za mmoja wa wale wanajeshi kabla hajalifikia lile pori huku majibizano ya risasi yakiendelea. Sikutaka tena kuendelea kupoteza muda wangu eneo lile hivyo nikaongeza mwendo na kuzidi kutokomea.
_____
Baada ya muda mrefu wa safari yangu hatimaye nikawa nimeifikia barabara ya Chausseé du Peuple Murundi. Ilikuwa ni barabara pana ya kisasa kama zilivyokuwa barabara nyingi za mijini hata hivyo ile barabara ilikuwa imejitenga sana na makazi ya watu ikikatisha katikati ya vichaka vizito vya miti, mawe na nyasi ndefu. Hivyo haraka nilifahamu kuwa usalama katika barabara ile ulikuwa hafifu sana kwani baada ya mwendo mfupi tu wa safari yangu nikaanza kuziona maiti za watu zikiwa zimezagaa ovyo barabarani na kutelekezwa. Nilipoendelea kuchunguza vizuri kwenye barabara ile nikayaona magurudumu chakavu ya magari yakiendelea kuteketea kwa moto pamoja na vizuizi vya mawe makubwa katika baadhi ya maeneo ya barabara ile. Kuona vile ikabidi nipunguze mwendo na kuanza kuchagua sehemu za kupita. Sikumuona mtu yoyote katika ile barabara na hali ile ilinitia wasiwasi kidogo.
Athari za jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi zilikuwa zimeanza kujitokeza. Barabara za mitaa mingi ya jiji la Bujumbura zilikuwa zimeachwa upweke baada ya kukimbiwa na watu waliokuwa wakitafuta usalama wa roho zao. Kila eneo sasa lilikuwa likinuka harufu ya moshi wa risasi na magruneti ya kutupa kwa mkono. Maiti za watu nazo zilikuwa zimezagaa ovyo kila mahali. Hali ya amani katika nchi ya Burundi ilikuwa ikizidi kuwa tete kwa vile haikufahamika hadharani kuwa uongozi wa serikali ya nchi ya Burundi ulikuwa chini ya nani kwa wakati ule. Nilipolikumbuka lile gari jeupe Landcruiser lililokuwa limenifungia mkia kule nyuma nikaanza kuhisi kuwa wale watu waliokuwa ndani ya lile gari na wale wengine niliyopambana nao kwenye kile chumba cha ofisi ya meneja wa ile hoteli ya New Parador Residence walikuwa shirika moja katika kumteka balozi Adam Mwambapa. Nilihisi kuwa kulikuwa na jambo kubwa la hatari lililofichika katika mkasa mzima wa kutekwa kwa balozi Adam Mwambapa hata hivyo hadi kufikia wakati ule bado nilikuwa sijapata vizuri penyenye yoyote ya kile nilichokuwa nikipeleleza.
Mawazo yangu yaliporudi mle ndani nikashtuka kuwa tayari nilikwishaufikia mzunguko mkubwa wa barabara uliozikutanisha barabara kubwa tano. Katikati ya makutano yale kulikuwa na bustani nzuri ya miti ya maua iliyokatiwa vizuri ikizungukwa kwa nguzo ndefu zenye taa nzuri za barabarani. Nilipoufikia ule mzunguko wa barabara nikapunguza mwendo na kuingia upande wa kushoto na wakati nikifanya vile nikapishana na magari machache eneo lile. Muda mfupi uliofuata nikaiacha barabara ya Avenue de lʾOAU upande wa kushoto na kuingia barabara ya Boulevard Mwambutsa upande wa kaskazini nikikipita kituo cha kujazia mafuta cha EBS Petroleum upande wa kulia. Barabara ya Boulevard Mwambutsa ilikuwa barabara pana ya kisasa iliyopakana na mifereji ya maji taka iliyojengewa vizuri kando yake huku ikipakana na miti mirefu ya kivuli na hivyo kuifanya igubikwe na utulivu wa aina yake.
Nilipoitazama ramani yangu ndogo ya kijasusi nikagundua kuwa kutoka pale nilipokuwa sikuwa mbali sana na Le Tulip Hôtel Africaine ambayo kwa mujibu wa uchunguzi wangu kupitia zile nyaraka muhimu zenye orodha ya mienendo ya mawasiliano ambayo Hidaya alikuwa ameipata kwa opareta ni kuwa simu ya mezani ya ofisini kwa Balozi Adam Mwambapa ilikuwa imetumika kufanya mawasiliano mengi kuelekea kwenye hoteli ile muda mfupi kabla ya mapinduzi yale ya kijeshi.
Baada ya mwendo wa robo saa katika barabara pana ya lami iliyokuwa ikikatisha katikati ya mashamba na iliyopakana na miti mirefu na vichaka vya hapa na pale hatimaye nikaja kuiona Le Tulip Hôtel Africaine upande wa kushoto kiasi cha umbali usiopungua mita mia mbili kando ya barabara ile.
Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuiona hoteli ile hata hivyo sifa zake zilikuwa zimeyafikia masikio yangu kwa muda wa miaka kadhaa iliyopita kutoka kwa marafiki na wakuu wangu wa kazi ambao walikuwa wamebahatika kuitembelea hoteli ile huko siku za nyuma mara kwa mara wakati walipokuwa wakifika pale nchini Burundi kwa safari za kikazi. Mojawapo ya taarifa nilizokuwanazo ni kuwa Le Tulip Hôtel Africaine ilikuwa ni hoteli yenye hadhi ya nyota tano na ilikuwa ikimilikiwa na mwekezaji mmoja wa jijini Bujumbura ambaye alikuwa ni raia wa Ufaransa.
Bango kubwa lenye tangazo la hoteli ile barabarani likanipelekea nipunguze mwendo na kuingia upande wa kushoto nikiifuata barabara nyembamba kiasi iliyofunikwa kwa changarawe na kupakana na miti mirefu ya kivuli iliyozungukwa na bustani ya maua ya kupendeza yenye hewa safi ya upepo wa asili. Le Tulip Hôtel Africaine sasa ilikuwa mbele yangu na ilikuwa ni hoteli kubwa yenye mandhari tulivu ya kupendeza.
Katika bustani nzuri iliyoizunguka hoteli ile kulikuwa na mabwawa makubwa ya kuogelea, sehemu zenye viti maalum vya kupumzikia chini ya miti mizuri ya kivuli aina ya Hopea odorata pamoja na vibanda vidogo vya faragha. Ile barabara niliyoingia ilikuwa ikimulikwa kwa mwanga hafifu wa taa zilizokuwa kando ya ile barabara juu ya vinguzo vifupi vya chuma. Katika lile jengo la ghorofa la ile hoteli wakati ule wa usiku niliviona baadhi ya vyumba vikiwa vinawaka taa ghorofani. Wakati nikiwasili nje ya ile hoteli nikaiona milingoti mitano yenye bendera zinazopepea taratibu. Zilikuwa ni bendera za nchi za Afrika mashariki na bendera ya taifa la Ufaransa na Marekani na sehemu ya mbele chini ya hoteli ile kulikuwa na magari mengi yaliyoegeshwa.
Hatimaye nikawa nimefika mbele ya ile hoteli ambapo baada ya hangaika ya hapa na pale nikawa nimepata sehemu nzuri ya maegesho ya gari langu. Kabla ya kushuka kwenye gari nikatulia kidogo nikifanya tathmini nzuri ya mandhari ya hoteli ile na baada ya muda macho yangu yakaridhika kuwa ilikuwa ni hoteli nzuri mno ingawaje majengo yake yalikuwa ni ya mtindo wa kizamani kidogo. Nilipoendelea kuchunguza nikagundua kuwa nyuma ya ile hoteli kiasi cha umbali usiopungua mita mia tano kulikuwa na msitu mkubwa wa miti ya kupandwa kama ule wa Sao Hill uliopo mkoani Iringa ingawa ukubwa wa msitu ule sikuweza kuufahamu.
Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na giza nalo lilikuwa zito ingawa mara kwa mara giza lile lilitoweshwa na mwanga mkali wa radi kutoka angani. Sikuweza kumuona mtu yeyote nje ya hoteli ile mbali na walinzi wawili waliokuwa ndani ya kibanda kidogo kando ya eneo lile. Hivyo nikalichukua koti langu la mvua na kulivaa huku bastola yangu nikiitia ndani ya mfuko wa lile koti. Baada ya kujitazama kidogo kupitia kioo cha mbele chini ya paa ya lile gari na kuridhika na mwonekano wangu nikafungua mlango wa gari na kutoka nikikatisha katikati ya lile eneo la maegesho ya magari kuelekea mbele ya ile hoteli. Wakati nikitembea nikihakikisha kuwa hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia nyendo zangu eneo lile.
Nilipofika mbele ya ile hoteli nikapanda ngazi kumi na mbili za varanda yenye sakafu nzuri ya tarazo iliyoandikwa kwa ufundi mkubwa jina la hoteli ile kisha nikausukuma mlango mkubwa wa kioo na kutokomea ndani. Kama zilivyokuwa hoteli nyingi za kimataifa duniani Le Tulip Hôtel Africaine haikuwa tofauti. Sehemu yake ya mapokezi ilikuwa na umbo la nusu duara iliyozungukwa na meza nzuri ya kaunta ya mbao ya mti wa Jacaranda iliyokuwa ikitazamana na makochi meupe ya ngozi laini ya sofa.
Niliwakuta wazungu watatu eneo lile, wawili wanaume na mmoja mwanamke wakiwa wameketi kwenye yale makochi ya sofa huku upande wa pili kukiwa na wanaume wengine wawili waafrika kama mimi na kila mtu alionekana kuzama kwenye hamsini zake. Pale sehemu mapokezi nikawakuta wahudumu wawili, kaka na dada wakiwa katika sare zao nadhifu za kazi za mashati meupe yenye kola za rangi ya kijivu na suruali za rangi ya kijivu huku shingoni wakiwa wamevaa tai ndogo nyeusi zilizowapendeza. Yule mhudumu wa kiume alikuwa amejitenga kando akizungumza na mwanaume mmoja niliyemhisi kuwa alikuwa ni raia wa Nigeria kutokana na lafudhi ya kiingereza chake na aina ya mavazi aliyovaa. Yule mhudumu wa kike alikuwa akihitimisha kuongea na simu ya mezani wakati nilipokuwa nikiifikia ile kaunta ya mapokezi hivyo haraka akairudishia ile simu mahala pake kisha uso wake ukiwa umefanikiwa kutengeneza tabasamu zuri la kirafiki akageuka na kunitazama.
“Soeur, comment va le travail?”. Dada, habari za kazi?. Nikawahi kumsalimia huku usoni nikitengeneza tabasamu la kikazi na hapo nikamsikia yule dada akinikaribisha kwa sauti nyororo ya kike.
“Bien frère bienvenu, je peux tʾaider?”. Nzuri tu kaka karibu nikusaidie.
“Merci beaucoup soeur, je suis venu voir mon visiteur”. Ahsante sana dada, nimekuja kumuona mgeni wangu. Nikamwambia yule dada huku nikimtazama usoni kwa bashasha zote za kimapenzi hali iliyompelekea akwepeshe macho yake pembeni huku akiangua tabasamu lenye kimelea cha aibu na kisha kujiziba mdomo kwa kiganja cha mkono wake. Alikuwa msichana mrembo sana kiasi kwamba lile tabasamu likavipelekea vishimo vidogo mashavuni mwake kuchomoza vizuri na kuuteka vibaya mtima wangu.
“Il est dans la chambre numero combien?”. Yupo chumba namba ngapi?. Yule dada mhudumu akaniuliza kwa utulivu huku akinitazama. Tukio lile likanipelekea nikohoe kidogo na kuvunja ukimya.
“Deux jours passé jʾai appellé de lʾambassade de Tanzanie ici à Bujumbura en parlant avec quelquʾun de la réception quʾil puisse reserver une chambre pour mon visiteur. Je ne sais pas vous Iʾavais donne la chambre numero combien”. Siku mbili zilizopita nilipiga simu hapa kutoka ofisi ya ubalozi wa Tanzania hapa Bujumbura, nikaongea na mtu wa hapa mapokezi kuwa aniwekee chumba kwa ajili ya mgeni wangu. Sijui mtakuwa mlimpatia chumba namba ngapi. Nikamuuliza yule dada mhudumu wa hoteli na hapo yule dada akanitazama kwa uyakinifu kama mtu anayejaribu kuvuta kumbukumbu zake kisha nikamuona akikichukua kitabu kikubwa chenye taarifa za wageni wa ile hoteli kilichokuwa kando yake pale juu mezani. Muda uleule nikamuona akianza kufunua kurasa za kile kitabu kwa utulivu hadi pale alipoufikia ukurasa fulani ndiyo akaweka kituo akiyapitia maelezo fulani yaliyokuwa kwenye ule ukurasa. Hatimaye nikamuona akiinua tena macho yake kunitazama.
“Oh! cʾest vrai que je vois ces coordonés dans le registre de visiteurs son nom cʾest Pierre Okongo, nʾest ce pas?”. Oh! ni kweli naona maelezo ya mgeni wako yapo hapa kwenye kitabu cha wageni, jina lake anaitwa Peter Okongo, au sivyo?. Yule dada mhudumu akaniambia huku akiyapeleka macho yake kunitazama tena.
“Cʾest bien lui, il est dans la chambre numero combien?”. Huyo ndiyo mwenyewe, yupo chumba namba ngapi?. Nikadakia haraka na kuuliza huku jina la Pierre Okongo likianza kuzitekenya upya fikra zangu.
“II est dans la chambre numero 403 au sixième niveau”. Yupo chumba namba 403 ghorofa ya sita. Yule dada akaniambia kwa utulivu huku akinitazama kwa makini. Kwa kitambo kifupi nikaupisha utulivu kichwani mwangu huku nikifikiria jambo fulani kabla ya kuvunja ukimya.
“Tu peux appeller pour me confirmer sʾil est de dans à cet heure?”. Unaweza kupiga simu kunihakikishia kama yupo ndani kwa muda huu?. Yule dada akatikisa kichwa chake haraka akionesha kukubaliana na ombi langu kisha akaisogeza ile simu ya mezani pale mapokezi na kukiweka kiwambo cha simu sikioni kwake. Alipobofya tarakimu kadhaa ile simu ikaanza kuita upande wa pili na hapo yule dada mhudumu akayahamishia macho yake kunitazama tena. Ile simu iliendelea kuita hadi pale ilipokata na hapo nikamuona yule dada akiipiga tena kwa mara nyingine. Akalirudia lile zoezi mara kadhaa pasipo ile simu kupokelewa na hatimaye yule dada akaikata ile simu na kurudishia kiwambo chake mahala pake.
“Je pense quʾil nʾest pas là, parceque le téléphone de sa chambre appelle mais personne ne décroche”. Nadhani atakuwa ametoka maana simu ya chumbani kwake inaita muda mrefu bila ya kupokelewa. Yule dada mhudumu akaniambia huku akinitazama katika namna ya kunionea huruma kwa kitendo cha kupishana na mgeni wangu.
“Dʾaccord, je peux trouver la chambre à côte de celle de mon visiteur?”. Okay, ninaweza kupata chumba jirani na hicho cha mgeni wangu?”. Swali langu likampelekea tena yule dada anitazame kwa mshangao kidogo lakini hatimaye akayahamishia macho yake kuitazama tena ile kurasa katika kile kitabu cha taarifa za wageni. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita kisha nikamuona tena yule dada akiinua macho yake na kunitazama kabla ya kuniambia..ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 42
Mtunzi:Kelvin Mponda

“Toutes les chambres à côté de celle de ton visiteur sont occupés peut être celle qui est en face de sa chambre”. Vyumba vyote vya jirani na yeye naona vimejaa labda uchukue chumba kinachotazamana na chake upande wa pili wa korido.
“Jʾapprécierai”. Nitashukuru. Nikamwambia yule dada kisha nikanyanyua mkono kuitazama saa yangu ya mkononi na nilipojiridhisha na mwenendo wa majira yake nikageuka nyuma na kuyatembeza macho yangu taratibu kuchunguza kama kungekuwa na ongezeko la mtu mwingine eneo lile. Sikumuona mtu yeyote mwingine hivyo hali bado ilikuwa shwari. Baada ya kumaliza kufanya malipo ya chumba yule dada muhudumu akanikabidhi funguo ya chumba na kunielekeza sehemu kulipokuwa na lifti ya lile jengo la hoteli kuelekea juu.
Muda mfupi uliofuata nikaliacha lile eneo la mapokezi na kushika uelekeo wa upande wa kulia. Mbele kidogo nikaingia upande wa kushoto na baada ya kuupita mlango mkubwa wa kuelekea sehemu ya maliwato uliokuwa upande wa kushoto hatua chache mbele yangu nikakiona chumba cha lifti cha kuelekea ghorofa za juu za lile jengo la hoteli Le Tulip Hôtel Africaine. Kwa sekunde kadhaa nikasubiri kile chumba cha lifti kishuke chini kwa vile kulikuwa na watu wakishuka chini ya lile jengo. Kile chumba kilipofika chini na mlango wake kufungua wazungu wawili mwanamke na mwanaume wakatoka na kunisalimia huku wakishika hamsini zao. Nikawahi kuingia ndani ya kile chumba cha lifti kisha nikabonyeza kitufe kuiamuru ile lifti inipeleke ghorofa ya sita ya lile jengo. Muda mfupi uliofuata kile chumba cha lifti kikaanza kukwea juu ya lile jengo huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu.
_____
Mandhari ya ghorofa ya sita ya lile jengo la Le Tulip Hôtel Africaine jijini Bujumbura yakanitanabaisha vizuri kuwa ni kwa sababu gani hoteli ile ilikuwa imepewa hadhi ya nyota tano. Kile chumba cha lifti kilipotia nanga na kugota ghorofa ya sita na mlango wake kufunguka nikatoka nje na kujikuta katikati ya korido pana yenye utulivu wa hali ya juu. Kwa sekunde kadhaa nikasimama na kuyatathmini vizuri mandhari yale. Kulikuwa na hewa safi iliyokuwa ikisambazwa taratibu na viyoyozi viwili kimoja kikiwa mwanzo wa ile korido na kingine mwisho. Sakafu ya korido ile ilifunikwa kwa zulia jekundu lenye umbo mstatili na hapakuwa na kitu kingine cha ziada zaidi ya utulivu mkubwa wa kistaarabu. Dari ya ile korido ilitengenezwa kwa gypsum nzuri ya rangi nyeupe na katika sehemu za dari ile kuliningʾinizwa taa nzuri zilizozungukwa na vitenga maridadi vya wavu mwepesi unaopitisha mwanga.
Taratibu nikaanza kutembea katikati ya ile korido huku nikiyatembeza macho yangu upande huu na ule kutazama namba zilizokuwa juu ya milango ya vyumba vilivyokuwa vikitazamana na ile korido huku kidole changu kimoja kikiwa tayari kimetuama vyema kwenye kilimi cha bastola yangu ndani ya mfuko wa koti. Nikaendelea kutembea taratibu hadi nilipofika katikati ya ile korido na hapo nikasimama.
Nikiwa katikati ya ile korido nikagundua kuwa kulikuwa na korido nyingine ya ile ghorofa iliyoingia upande wa kushoto na hivyo kunipelekea niweze kuielewa vizuri ramani ya lile jengo kuwa ilikuwa ni katika mtindo wa herufi T. Nikaendelea kuyatembeza macho yangu eneo lile na kwa kufanya vile nikagundua kuwa kutoka pale nilipokuwa nimesimama namba za milango ya vyumba vile mbele yangu bado ilikuwa chini ya namba ya kile chumba nilichokuwa nikielekea. Hivyo hisia zangu zikanieleza kuwa chumba namba 403 kingekuwa kwenye ile korido ya upande wa kushoto wa lile jengo. Hivyo haraka nikabadili uelekeo wangu nikiacha kuifuata ile korido mbele yangu badala yake nikashika uelekeo wa upande wa kushoto nikiifuata ile korido.
Ilikuwa korido ndefu sana inayoniwezesha kuona vizuri hadi mwisho wake na korido ile ilikuwa ikitazamana na milango mingi ya vyumba kwa upande wa kushoto na kulia. Niliendelea kutembea katikati ya korido ile huku taratibu nikiyatembeza macho yangu milangoni. Nilipofika katikati ya ile korido nikapishana na mwanaume mmoja aliyetoka katika chumba jirani na eneo lile ambapo alinisalimia kwa heshima zote na kushika hamsini zake akiniacha niendelee na safari yangu.
Nilikuwa mbioni kukata tamaa wakati nilipokiona chumba namba 403 upande wangu wa kulia hatua chache kabla ya kufika mwisho wa ile korido. Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu kama niliyeona jambo la kushangaza na la hatari mno. Sikujua ni kwa namna gani hali ile ilinitokea hata hivyo niliziheshimu sana hisia zangu. Taratibu nikausogelea ule mlango na kuuchunguza kwa utulivu. Ulikuwa ni mlango mkubwa na imara wa mbao ngumu. Juu ya mlango ule kulikuwa na nafasi ndogo iliyozibwa kwa kioo chenye mawimbi kisichomuwezesha mtu yeyote aliyeko nje kuweza kuona vizuri ndani ya kile chumba. Hata hivyo kupitia kioo kile nikaweza kugundua kuwa taa ya ndani ya kile chumba ilikuwa imewashwa na hivyo kushikilia kuwa kama mwenyeji wa kile chumba hakuwa mle ndani basi huwenda alikuwa ametoka kidogo kwa safari ya fupi au hakuwa mbali na eneo lile.
Nilitaka kupata hakika kama mwenyeji wa kile chumba alikuwepo mle ndani au lah!. Hivyo baada ya kuyatembeza macho yangu kwenye ile korido na kuridhika kuwa hakukuwa na mtu mwingine eneo lile nikausogelea ule mlango na kubofya kengele ya mlangoni. Ile kengele ikaanza kuita na tukio lile ikapelekea hamasa ya kipekee nafsini mwangu na hivyo kuifanya taswira ya kufikirika ya mtu aitwaye Pierre Okongo kuanza kujengeka machoni mwangu. Maswali kadhaa yakaanza kuibuka kichwani mwangu nikijiuliza kuwa Pierre Okongo ni nani na alikuwa ametumbukiaje katika mkasa ule. Hata hivyo nilijionya na kujipa tahadhari kuwa nilipaswa kuwa makini zaidi katika nyendo zangu kwani bado sikuwa na hakika vizuri juu ya adui yangu.
Ile kengele ya mlangoni ikaendelea kuita mle ndani ya kile chumba pasipo dalili zozote za ule mlango kufunguliwa na hatimaye ikafika ukomo bila majibu. Nikarudia tena kubofya ile kengele ya mlangoni mara kadhaa hata hivyo sikujibiwa wala ule mlango kufunguliwa. Hali ile ikanipelekea niyaamini maelezo ya yule dada mhudumu wa kule mapokezi nilipotoka kuwa mwenyeji wa kile chumba huwenda alikuwa ametoka kidogo kutokana na lile tukio la simu ya kile chumba kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
Nafsi yangu ikanitanabaisha kuwa nilipaswa kujipa subira kwanza katika kutafuta hakika ya hisia zangu. Hivyo nikauacha mlango wa kile chumba na kuhamia upande wa pili wa ile korido kwenye mlango wa chumba kingine nilichokuwa nimekabidhiwa ufunguo wake na yule dada mhudumu wa mapokezi wa ile hoteli kule chini. Nilipofika nikauchukua ule ufunguo kutoka mfukoni na kuupachika kwenye tundu la kitasa cha ule mlango ambapo nilipoutekenya kidogo ule ufunguo mlango wa kile chumba ukafunguka na hapo nikausukuma taratibu kuingia mle ndani.
Nilipoingia mle ndani ya kile chumba nikaufungua ule mlango nyuma yangu na kusimama nikitathmini vizuri mandhari ya mle ndani. Kilikuwa chumba kikubwa sana na chenye nafasi ya kutosha. Mle ndani upande wa kulia kulikuwa na kitanda kikubwa cha mbao chenye godoro la foronya laini lililofunikwa kwa shuka safi za rangi nyeupe. Sakafu ya kile chumba ilifunikwa kwa zulia zuri la rangi ya kijivu lenye maua mekundu. Upande wa kushoto wa kile kitanda kulikuwa na kabati zuri la nguo la ukutani pembeni ya dirisha kubwa la kile chumba lililofunikwa kwa mapazia marefu na mepesi yanayoruhusu hewa safi kupenya mle ndani. Upande wa kulia wa kile chumba kando ya kile kitanda nikauona mlango mmoja na hapo nikajua kuwa ule ulikuwa ni mlango wa kueleke kwenye chumba cha maliwato. Kiyoyozi makini kilichokuwa sehemu fulani kwenye kona ya kile chumba kilikuwa kikiendelea kusambaza hewa safi mle ndani pasipo kuzingatia uwepo wa mtumiaji. Kulikuwa na makochi mawili ya sofa upande wa kushoto wa kile chumba nyuma ya meza ndogo fupi ya mbao yenye kibakuli kidogo cha majivu ya sigara juu yake. Makochi yale yalikuwa yakitazamana na seti moja kubwa ya runinga aina ya Sonny Blavia ya inchi 44 iliyofungwa vizuri ukutani na kuunganishwa na king’amuzi cha chaneli nyingi za kimataifa. Niliposogea karibu na yale makochi nikaiona simu moja ya mezani iliyokuwa juu ya stuli moja ya mbao yenye miguu mitatu iliyokuwa kwenye kona ya kile chumba. Pembeni ya simu ile kulikuwa na kitabu kikubwa cha rangi ya samawati chenye orodha ya majina na namba za simu za watu na makampuni mbalimbali ya nchini Burundi.
Niliwaza kuwa mle ndani ingekuwa ni sehemu tulivu ya kumsubiri Pierre Okongo mwenyeji wa kile chumba cha upande wa pili wa ile korido kilichokuwa mkabala na mlango wa kile chumba changu. Hata hivyo kabla ya kuketi kwenye kochi nikazunguka mle ndani kwa utulivu kukipeleleza vizuri kile chumba. Niliporidhika na hali ya usalama ya mle ndani nikarudi na kuketi kwenye kochi moja mle ndani.
Kwa mara ya kwanza tangu nifike pale jijini Bujumbura nikajihisi kuwa angalau nilikuwa sehemu salama yenye upweke japokuwa hali ya usalama wa mle ndani haikuwa ya hakika. Nikatulia mle ndani nikifikiria juu ya hili na lile na hatimaye mawazo yangu yakawa yamehamia kwa yule mtu mwenye jina la Pierre Okongo huku nikijaribu kuvuta picha kuwa mtu huyo angekuwa ni mtu wa namna gani. Kwa namna moja au nyingine nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa Pierre Okongo angekuwa ni msaada mkubwa katika kujibu maswali mengi yaliyokuwa yakikisumbua kichwa changu. Nilikuwa nimekumbuka kuwa kulikuwa na mawasiliano mengi yaliyokuwa yamefanywa kati ya simu ya mezani ya ofisini kwa Balozi Adam Mwambapa na sehemu ya mapokezi ya hoteli ile na sasa nilianza kuamini kuwa Pierre Okongo ndiye aliyeonekana kuwa mlengwa mkubwa wa mawasiliano yale.
Nikiwa nimeketi kwenye kochi mle chumbani mawazo mengi yakawa yakipita kichwani mwangu. Nilihisi uchovu mwingi mwilini hata hivyo sikuruhusu usingizi unichukue badala yake nikaendelea kuyatega vizuri masikio yangu kwa utulivu nikisikilizia hatua za mtu yeyote ambaye angejitokeza na kuukaribia mlango wa kile chumba 403 cha jirani kilichokuwa mkabala na kile chumba changu.
Muda uliendelea kusonga pasipo dalili za mtu yeyote kusikika akiusogelea ule mlango wa kile chumba cha jirani kwenye ile korido. Hata hivyo sikukata tamaa kamwe kwani nilikuwa nimejiapiza kusubiri hadi hapo utafiti wangu utakapozaa matunda. Muda bado uliendelea kusonga huku nikiendelea kusubiri na nikiwa katika hali ile wazo jipya likanijia kichwani baada ya kukumbuka kuwa mle ndani kulikuwa na simu ya mezani. Wazo fulani lilikuwa limenijia kichwani na kunifanya nione kuwa kulikuwa na umuhimu wa kumueleza Hidaya juu ya mambo yote yaliyojiri tangu mara ya mwisho tulipoachana.
Nikaitazama saa yangu ya mkononi na kugundua kuwa muda ulikuwa umesonga sana hali iliyonipelekea niamini kuwa kwa muda ule huwenda Hidaya angekuwa tayari ameshalala nyumbani kwake. Hata hivyo nilifahamu kuwa Hidaya alikuwa msichana makini asiyependa kuendekeza usingizi hususani katika hali tete kama ile. Hivyo nikaichukua ile kadi ndogo yenye namba za simu zilizoandikwa kijasusi kwa mtindo wa herufi na mchoro wa ramani ndogo mfano wa ua zuri la kuchora ambalo mtu yeyote wa kawaida asingeweza kuitambua ramani ile kuwa ingeweza kunifikisha nyumbani kwa Hidaya.
Ilikuwa ni ile kadi niliyopewa na Hidaya asubuhi ile wakati tulipoonana kule kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi. Nikamata kadi ile mkononi kisha nikanyakua kiwambo cha ile simu ya mezani mle chumbani na kubonyeza tarakimu za siri zilizokuwa kwenye ile kadi. Nilipomaliza tu ile simu ikaanza kuita upande wa pili hivyo nikakiweka vizuri kile kiwambo cha simu sikioni mwangu na kuanza kusikiliza. Ilikuwa ni kama bahati kwani ule mwito wa simu ulipokuwa mbioni kufika ukomo ile simu ikapokelewa upande wa pili. Hata hivyo mpokeaji wa ile simu hakuzungumza neno lolote huku dhahiri akionekana kunitegea kwa kutokuwa na hakika kuwa mpigaji wa simu ile angekuwa nani kama zilivyokuwa tabia za ujasusi.
“Hidaya…”. Hatimaye nikavunja ukimya na kuita kwa sauti tulivu ya chini lakini pia inayosikika vizuri hata hivyo Hidaya hakuitikia mapema badala yake nikasikia kelele kidogo kama mtu anayejiweka sawa baada ya kuzinduka kutoka usingizini.
“Hidaya ni mimi hapa Tibba”
“Tibba…?”
“Ndiyo ni mimi Tibba Ganza shemeji yako mwandamizi”. Nikaongea kwa msisitizo huku tukio lile la kupokelewa kwa simu yangu likinifurahisha.
“Vipi Tibba, kwema?”. Hidaya akaniuliza kwa mashaka huku akitamani kucheka.
“Ondoa hofu mimi niko salama kabisa labda wewe”
“Mimi naendelea vizuri, vipi upo kwa wifi yangu Veronica?”. Hidaya akaongea huku akiangua kicheko hafifu cha kimbea chenye kimelea cha wivu wa starehe zangu.
“Mh! si afadhali ningekuwa kwa huyo Veronica”
“Sasa upo wapi muda huu?”
“Nipo Le Tulip Hôtel Africaine ndani ya chumba kimoja kizuri cha daraja la kwanza namsubiri mwenyeji wangu”
“Mbona hukuniambia kuwa una mwenyeji mwingine hapa jijini Bujumbura?”. Hidaya akaniuliza na hapo haraka nikatambua kuwa lile lilikuwa swali la hila kwa vile alitaka kusikia mengi zaidi kutoka kwangu kama ulivyokuwa ujanja wake. Hivyo nikaikwepa haraka hoja yake kwa kumtumbukizia swali langu.
“Umewasiliana na Chifu usiku huu?’’
“Ndiyo”
“Anasemaje?”
“Nimemueleza kuwa tayari tumeonana na sasa upo kazini ukiendelea na majukumu yako”
“Umefanya vizuri sana”. Nikaongea kwa utulivu huku nikiyatafakari maelezo yale na wakati nikiwa katika hali ile Hidaya akavunja ukimya.
“Vipi Tibba ulifika nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa?’’. Hidaya akaniuliza kwa shauku...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 43

“Nimetoka huko muda siyo mrefu lakini mambo siyo shwari”
“Una maana gani?”
“Kutokana na mazingira niliyoyaona nimejiridhisha kuwa Balozi Adam Mwambapa ametekwa na bahati mbaya sana tukio la kutekwa kwake limegharimu maisha ya watu wengi wasio na hatia”
“Una maanisha kuwa kuna watu waliouawa?” Hidaya akaniuliza kwa hofu.
“Walinzi wake wote”
“Oh! my God”. Hidaya akaongea kwa masikitiko na nilipotega vizuri sikio langu kwa mbali nikamsikia akishusha pumzi katika namna ya kukata tamaa juu ya taarifa ile kisha kukafuatia kitambo kifupi cha ukimya wa tafakari.
“Balozi Adam Mwambapa alikuwa akiishi na nani nyumbani kwake?’’. Nikawahi kumuuliza Hidaya baada ya kukumbuka kiini cha mawasiliano yale.
“Zaidi ya yeye mwenyewe, walinzi wake na kijana wake mmoja wa kazi simfahamu mtu mwingine”. Hidaya akanijibu kwa hakika.
“Kijana wake wa kazi!...”. Nikajisemea moyoni huku nikimkumbuka Sundi. Yule kijana aliyekuwa na jeraha kubwa la kisu tumboni niliyemkuta chumbani kwa Balozi Adam Mwambapa muda mfupi kabla hajakata roho.
“Kijana wa kazi wa nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa anaitwa Sundi?”
“Sundi Masele”. Hidaya akaniweka bayana kisha akakohoa kidogo na kuniuliza kwa mashaka.
“Mungu wangu Sundi amefanya nini tena?”
“Ameuawa hata hivyo nilipata nafasi ya kuzungumza naye kwa kifupi kabla ya kifo chake. Alitaka nimtafute Padri mmoja wa kanisa la katoliki la hapa jijini Bujumbura aitwaye Aloysius Kanyameza. Umewahi kumsikia popote Padri huyo?”
“Sundi amekufa…!. Mungu wangu ni unyama gani huu?’’. Nikamsikia Hidaya akisononeka na kushusha pumzi taratibu katika namna ya kukata tamaa hata hivyo sikuona kama ule ungekuwa ni wakati wa majadiliano hivyo haraka nikaelekea kwenye hoja yangu.
“Niambie Hidaya, unaweza ukawa unafahamu chochote kuhusu Padri Aloysius Kanyameza?”. Hoja yangu ikapelekea kitambo kifupi cha ukimya kupita kisha kwa sauti dhaifu nikamsikia Hidaya akinijibu.
“Hapana sifahamu chochote kwani hilo jina ni geni kabisa masikioni mwangu. Kwani imekuwaje Tibba?”
“Bado nipo kwenye uchunguzi Hidaya hivyo taarifa yoyote inaweza kuwa na umuhumu kwangu. Bado sijapata uelekeo sahihi wa kile ninachokipeleleza hivyo pia sina lolote la kukwambia kwa sasa”
“Sasa kuhusu huyo Padri Aloysius Kanyameza je unadhani kuna lolote ninaloweza kukusaidia?”
“Hapana Hidaya hili lipo nje ya uwezo wako. Acha tu nitajua namna ya kufanya”
“Kama ni hivyo sawa”
“Jambo moja tu…”
“Ondoa shaka Tibba niambie tu”. Hidaya akaniuliza kwa shauku.
“Naomba kutakapo pambazuka uwatume vijana wakaiondoe ile miili nyumba ya Balozi Adam Mwambapa. Hakikisha jambo hilo linafanyika kwa usiri mkubwa nadhani unaelewa vizuri ninachomaanisha”
“Ondoa shaka Tibba nitafanya hivyo. Unadhani ni vyema kumueleza Chifu juu ya hatua uliyofikia?”
“Siyo jambo la lazima sana lakini pia siyo vibaya kumueleza kwani ni yeye ndiye atakaye shughulikia utaratibu wa kusafirisha hiyo miili hadi Dar es Salaam”
“Sawa, kuna kingine?”. Hidaya akaniuliza huku usingizi ukionekana kuwa mbali na nafsi yake.
“Ni hayo tu kwa sasa chochote kingine kitakachojiri tutafahamishana baadaye kadiri muda utakavyoruhusu”. Nikaongea kwa utulivu huku nikiitazama saa yangu ya mkononi.
“Tibba…”
“Naam nakusikia Hidaya”
“Bado hujaniambia kuwa mwenyeji wako hapo hotelini ni nani?”. Swali la Hidaya likanipelekea nitabasamu kidogo baada ya kufurahishwa na tabia yake ya kutokupitwa na jambo.
“Mtu anayefahamika kwa jina la Pierre Okongo. Kwa mujibu wa uchunguzi wangu ni kuwa huyu ndiye mtu aliyewasiliana na Balozi Adam Mmwambapa muda mfupi kabla ya tukio la kutekwa kwake”
“Kuwa mwangalifu Tibba”
“Kifo kitakapokuja hakuna wa kukizuia Hidaya ingawa nimekuwa nikipishana nacho mara kwa mara”
“Mh! kumbuka Veronica bado anakuhitaji”. Hidaya akachombeza utani huku akiangua kicheko hafifu cha umbea.
“Ushaanza mambo yako mimi nitakuwezea wapi wewe”. Sote tukaangua kicheko na kwa kuwa sikuwa na jambo lingine la maana la kuzungumza kicheko kile kilipofika ukomo nikaona nimuage kabisa Hidaya.
“Usiku mwema”
“Ahsante Tibba na wewe pia. Nakutakia kila la heri katika kazi yako”
“Nashukuru sana hata hivyo unisamehe sana kwa kukuharibia usingizi wako”
“Ondoa shaka wala usijali”
Hatimaye nikaagana na Hidaya na kisha kurudishia kile kiwambo cha simu ya mezani mahala pake. Kwa sekunde kadhaa nikatulia pale kwenye kochi huku nikiupisha utulivu kichwani mwangu. Kwa kweli sikuweza kufahamu kama nilikuwa nikipiga hatua yoyote kwenye uchunguzi wangu. Hata hivyo nilikuwa na kila sababu ya kuamini kuwa yeyote niliyekutana naye au niliyekuwa nikielekea kukutana naye alikuwa akihusika na mkasa huu. Masaa yalikuwa yakizidi kuyoyoma na mvua nayo ilikuwa ikiendelea kunyesha wakati mawazo mwengi yakipita kichwani mwangu.
_____
Sikuweza kufahamu ni kwa namna gani usingizi ulikuwa umefanikiwa kuniteka nyara nikiwa bado nimeketi kwenye lile kochi mle chumbani. Hata hivyo kitendo cha kushtuka kutoka usingizini na kujikuta bado nikiwa kwenye mazingira salama kikanitia faraja. Nikausogeza mkono wangu karibu na kuitazama saa yangu ya mkononi na hapo majira yake yakanitanabaisha kuwa nilikuwa nimeponda usingizi kwa muda wa saa moja kasoro dakika chache nikiwa bado nimeketi kwenye lile kochi. Nikajikuta nikijilaumu kwa kuwa mzembe kiasi kile kwa kuuruhusu usingizi unichukue mzima mzima. Adui mjanja angeweza kuitumia nafasi ile adimu kutimiza dhamira yake mbaya. Nikawaza huku nikipiga mwayo hafifu na kuvinyoosha viungo vyangu mwilini.
Nilipotuliza fikra zangu nikawaza kuwa muda ule nilioutumia kuuponda usingizi ningeweza kumruhusu Pierre Okongo au mtu mwingine yeyote kuweza kuufikia ule mlango wa chumba cha jirani na hatimaye kuingia mle ndani pasipo kumsikia. Hali ile ikanipelekea nishindwe kufahamu kama bado nilikuwa ndani ya muda au nje ya muda katika kumsubiri mwenyeji wangu. Mwishowe nafsi yangu ikanionya kuwa huwenda nilikuwa nikimsubiri mtu nisiyekuwa na hakika naye hivyo nikasimama na kuelekea kwenye dirisha la kile chumba. Nilipofika nikasogeza pazia kando na kutazama nje chini ya lile jengo.
Nyuma ya lile jengo kulikuwa na bustani nzuri ya maua na viwanja vya mazoezi na mbele ya viwanja vile kulikuwa na msitu mkubwa wa miti ya kupandwa. Sikuweza haraka kutambua msitu ule ulikuwa umeishia wapi kwa kule mbele hata hivyo ulikuwa umeshona sana na hivyo kuupelekea uonekane unatisha sana kwa nyakati zile za usiku wa manane. Mara moja au mbili mwanga mkali wa radi ulimulika kwenye msitu ule na kutengeneza nuru kubwa ya ghafla iliyoniwezesha walau kuona sehemu tu ya msitu ule wa kutisha. Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha hata hivyo nilihisi kuwa ilikuwa imepungua kidogo. Zaidi ya pale sikuweza kuona kiumbe chochote eneo lile na hali ile ikanitanabaisha kuwa masaa yalikuwa yameenda sana.
Mwishowe nikaliacha lile dirisha na kufunika pazia vizuri kabla ya kuelekea mlangoni. Sikuona kama kuendelea kusubiri zaidi mle ndani kungeweza kufanikisha majibu ya maswali yangu kichwani hivyo nilipoufikia ule mlango nikaufungua taratibu na kutoka. Mlango ulipofunguka nikatoka na kuchungulia kwenye ile korido. Sikumuona mtu yeyote eneo lile na ukimya ule ulikuwa kama wa kifo. Hatimaye nikatoka kabisa nje ya kile chumba na kuufunga ule mlango nyuma yangu. Kwa sekunde kadhaa baada ya kutoka kwenye kile chumba nikasimama katikati ya ile korido nikitaka kutafuta salama ya eneo lile. Sikumuona mtu yeyote hivyo hali bado ilikuwa shwari.
Nilipoyapeleka macho yangu kutazama juu ya mlango wa kile chumba namba 403 nikashangaa kuona kuwa ile taa ya mle ndani ya kile chumba ilikuwa bado ikiwaka. Tukio lile likaibua maswali mengi kichwani mwangu huku nikishikwa na wasiwasi kuwa huwenda mwenyeji wa chumba kile alikuwa bado hajarudi. Nikajiuliza kama kweli mwenyeji wa chumba kile angekuwa bado hajarudi ingenichukuwa muda gani kumsubiri mtu nisiyekuwa na miadi naye. Jibu la haraka sikulipata hivyo pia sikuona sababu ya kuendelea kusubiri badala yake taratibu nikausogelea mlango wa kile chumba na kubofya kitufe cha kengele ya mlangoni. Miito kadhaa ya ile kengele ya mlangoni ikasikika kwa mbali ndani ya kile chumba pasipo dalili za kufunguliwa kwa ule mlango. Nikarudia tena na tena kubofya kitufe cha ile kengele hata hivyo ule mlango haukufunguliwa wala mtu yeyote kujitokeza na hali ile ikazidi kunitia mashaka.
Hatimaye nikaanza kuhisi kuwa nilikuwa nikipoteza muda wangu bure kwa kufanya utafiti usiokuwa na tija. Hivyo nikaachana na lile zoezi la kubofya kile kitufe cha kengele pale mlangoni badala yake nikausogelea karibu ule mlango na kushika kitasa chake huku tayari nikiwa nimevaa glovu nyepesi mikononi ili kukwepa kuacha alama za vidole vyangu eneo lile. Nikiwa nimeridhishwa na hali ya usalama wa eneo lile taratibu nikakizungusha kile kitasa na kuusukuma ndani ule mlango. Hata hivyo jitihada zangu hazikufua dafu kwani ule mlango ulikuwa umefungwa.
Bila kupoteza muda nikaingiza mkono wangu mfukoni na kuchukua mkungu wa funguo malaya ambapo nilianza taratibu kujaribu funguo moja baada ya nyingine kwenye kile kitasa cha ule mlango. Baada ya hangaika hangaika ya hapa na pale hatimaye ule mlango ukafunguka hivyo nikachomoa funguo na kuitia mfukoni.
Nilianza kwa kuusukuma taratibu ule mlango kwa mkono wa kulia huku mkono wangu wa kushoto ukiwa umeikamata vyema bastola yangu tayari kukabiliana na rabsha za aina yoyote ambazo zingejitokeza mbele yangu. Hata hivyo sikukutana na upinzani wowote badala yake ule mlango ukatii amri kama nilivyotaka hivyo haraka nikaingia mle ndani ya kile chumba na kuurudishia ule mlango nyuma yangu.
Kwa sekunde kadhaa nikiwa nimesimama mlangoni ndani ya kile chumba nikajikuta nimeshikwa na taharuki isiyoelezeka. Moyo wangu ukapoteza utulivu kabisa huku kijasho chembamba kikianza kufanya ziara sehemu mbalimbali za mwili wangu.
Katikati ya kitanda kikubwa cha mle ndani chini ya dari ya kile chumba mwili wa mwanaume mmoja mzee wa kizungu mwenye umri wa kukadirika kati ya miaka hamsini hadi sitini ulikuwa ukining’inia kwenye waya mwembamba uliofungwa shingoni na kutundikwa darini. Kwa kweli nilistaajabu sana kwa tukio lile. Yule mzee wa kizungu alikuwa amevaa mavazi ya kitakatifu, joho refu jeupe na kofia nyeupe ya kasisi yenye alama ya msalaba mwekundu mbele yake. Sikuwa na shaka yoyote kuwa mtu yule alikuwa amenyongwa siku moja au mbili zilizopita kwani mwili wake ulikuwa imeanza kutoa harufu mbaya inayoweza kumtapisha mtu.
Chini ya lile joho yule mtu alikuwa amevaa suruali nyeusi na viatu vyeusi vya ngozi. Mkononi alikuwa ameshika kitabu kitakatifu cha Biblia kilichozungushiwa rozari na kifuani pake alikuwa amening’iniza kidani cha msalaba mkubwa uliotiwa nakshi ya madini ya shaba katika baadhi ya maeneo yake. Ulimi na macho vilikuwa vimemtoa kiongozi yule wa kiroho kutokana na ule waya mwembamba ulioikaba vibaya shingo yake kiasi cha kuuzuia mzunguko wa damu kichwani mwake.
Haikuwa maiti ya kurudia kuitazama mara mbili mbili. Yule mtu alikuwa amenyongwa tena katika mazingira ya kibabe sana. Uchunguzi wangu ukahitimisha hivyo. Hata hivyo nilihisi kuwa halikuwa jambo rahisi kwani mandhari ya mle ndani yaliashiria kuwa kulikuwa kumetokea patashika ya aina yake. Shuka za pale kitandani zilikuwa zimevurugwa ovyo na mito yake kutupwa sakafuni. Kabati la nguo la ukutani la mle ndani lilikuwa limeachwa wazi ingawa ndani yake hapakuwa na kitu chochote. Simu ya mezani mle chumbani ilikuwa imeangushwa chini ingawa haikuwa imeharibika. Droo za kitanda zilikuwa zimefunguliwa na kuachwa wazi na katika meza ndogo ya mle ndani iliyokuwa pembeni ya kitanda juu yake...ITAENDELEA
 
Hizi ndio hadithi za kusoma mwanamme,sio mwanamme mzima unakesha eti kusoma "SHEMEJI MONICA"
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom