Riwaya: Ufukwe wa Madagascar

Riwaya: Ufukwe wa Madagascar

RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 26
Mtunzi:Kelvin Mponda

“Hapana sikurudi nyumbani kwani hata kama ningerudi nyumbani bado nisingeweza kupata usingizi kutokana na hali yenyewe ya mambo ilivyokuwa. Kutoka nyumbani kwangu hadi hapa ofisini umbali wake siyo mrefu sana hivyo nikawa nimepata wazo la kupenyapenya mitaani na kuja hapa.
“Walinzi wa hapa ofisini waliponiona waliingiwa na wasiwasi hata hivyo niliwatoa hofu kwa kuwaambia kuwa kulikuwa na jambo la dharura lililokuwa limejitokeza na hivyo nilikuwa nimelazimika kufika hapa usiku ili kulifanyia kazi. Sikukabiliana na upinzani wowote hivyo nikafungua ofisi na kuingia ndani ndiyo nikaketi na kuandika ile Fax na hatimaye kuituma makao makuu ya idara yetu ya ujasusi jijini Dar es Salaam”
Maelezo ya Hidaya yakawa yameniingia vizuri na kwa mara nyingine nikajikuta nikimpongeza kwa kuwa msichana jasiri, mzalendo na mwenye kujali.
“Ulitoa taarifa kwa vyombo vya usalama vya hapa Burundi?”. Nikamuuliza Hidaya kwa udadisi.
“Hapana! kwani baada ya kufikiri sana niliona kuwa hilo lisingekuwa jambo jema”
“Kwa nini?”
“Jaribio hili la mapinduzi ya kijeshi hapa nchini Burundi limepelekea hali ya kutoaminiana sana tena kwa baadhi ya maafisa katika vyombo vya usalama. Hivyo niliona kuwa taarifa kama hii ya kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa huwenda kwa baadhi ya maafisa usalama wa hapa wangeipa uzito unaostahili huku wengine wakihisi kuwa ni kama niliyekuwa nimeenda kutoa taarifa za uchochezi baina ya nchi na nchi au baina ya makundi hasimu. Vilevile sikutaka serikali ya Burundi ijihusishe kwa namna yeyote katika suala hili kwa kigezo kuwa katika mazingira nisiyoyaelewa huwenda ushahidi wa tukio hili la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa ungetoweshwa na vyanzo vyake vyote muhimu vya upelelezi kufutiliwa mbali na hivyo kazi yote kuwa ngumu”. Hidaya akaweka kituo baada ya kumaliza kutoa maelezo yake na kwa kweli alikuwa amenifurahisha sana kiasi cha kulipelekea tabasamu langu jepesi lichomoze usoni taratibu kama miale ya jua la asubuhi.
“Niseme kuwa umefanya uamuzi mzuri wa busara kwa kuto kutoa taarifa hizi kwa chombo chochote cha usalama cha hapa nchini Burundi kwani hata Chifu amesisitiza kuwa jambo hili lifanyike kwa weledi na usiri wa hali ya juu. Vinginevyo serikali yetu inaweza kulaumiwa kwa kutokuwa makini na usalama wa maafisa wake”. Nikasisitiza kisha baada ya kufikicha macho kidogo nikamuuliza Hidaya.
“Kuna mtu mwingine yeyote anayefahamu habari hizi za kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa katika ofisi yenu?”
“Hapana nimelazimika kutengeneza taarifa ya uongo inayotanabaisha kuwa Balozi Adam Mwambapa amepata dharura ya kikazi hivyo hatokuwepo hapa ofisini kwa siku kadhaa. Sikupenda mtu yeyote wa hapa ofisini afahamu juu ya suala hili katika hatua ya awali kama hii”. Hidaya akaniambia kwa hakika pasina kuujutia uamuzi wake na kwa kweli hata mimi nilikuwa nimependezwa na uamuzi wake.
“Chifu analifahamu hilo?”. Nikamuuliza Hidaya katika namna ya kutafuta uhalali
“Wazo hili limetoka kwake na nimekuwa nikimfahamisha kwa ukaribu kila kitu kinachoendelea hapa nchini Burundi tangu kutokea kwa jaribio hili la mapinduzi ya kijeshi”
“Umefanya vyema sana”. Nikamwambia Hidaya kisha nikakohoa kidogo kusafisha koo kabla ya kuendelea.
“Niseme tukio la kutekwa kwa Balozi wetu Adam Mwambapa limenishtua na kunishangaza sana kwani hadi sasa nikifikiria bado sioni sababu yoyote walau ya kuhisi tu inayoweza kuhalalisha tukio la kinyama kama hili”
“Hata mimi nimeshindwa kuelewa kinachoendelea Tibba”. Hidaya akasisitiza huku akitikisa kichwa chake katika namna ya kuonesha kusikitishwa na tukio lile.
“Nitajitahidi kufanya kila liwezekanalo katika kuhakikisha kuwa Balozi wetu Adam Mwambapa anapatikana na yeyote aliyehusika na kitendo hiki cha kiharamia ataijutia nafsi yake”. Maelezo yangu yalikuwa ya hakika na kwa namna moja au nyingine yalionekana kumfurahisha sana Hidaya kiasi cha kumpelekea atabasamu na uzuri wake kujidhihirisha vizuri usoni mwake.
“Kuwa mwangalifu sana Tibba kwani huwenda hali ikawa tofauti kabisa na vile unavyofikiria”. Hidaya akaniambia na kupitia sauti yake tulivu ya kike niliweza kuhisi huruma aliyokuwa nayo juu yangu. Hata hivyo nilimtoa wasiwasi kwa kumwambia.
“Ondoa shaka Hidaya naamini kuwa Mungu atanisaidia”. Kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku kila mmoja akionekana kuzama kwenye tafakuri na wakati hali ile ikiendelea mara nikakumbuka kumuuliza Hidaya.
“Kuna mtu yeyote aliyefanikiwa kufika nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa baada ya tukio la kutekwa kwake?”
“Hakuna mtu yeyote aliyefika kwani ni kama nilivyokueleza kuwa hakuna mtu mwingine anayefahamu juu ya tukio hili hapa ofisini isipokuwa mimi peke yangu na Balozi Adam Mwambapa huko alipo. Hidaya akaongea kwa msisitizo na kwa hakika nilimuelewa vizuri. Ukimya kiasi ukapita baina yetu huku kila mmoja akionekana kuzama tena katika fikra zake na kwa kweli tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa lilikuwa limenishangaza sana.
Kwa namna moja au nyingine niliamini kuwa watu hao ambao walihusika katika kumteka Balozi Adam Mwambapa walikuwa ni watu wenye uwezo na maarifa ya juu ya medani za kijeshi kwa vile Balozi Adam Mwambapa alikuwa ni kiongozi mstaafu wa jeshi mwenye maarifa ya juu sana ya mapambano. Ingawa bado sikuweza kuhisi lengo la watekaji hao.
Mwanzoni nilihisi kuwa huwenda watekaji hao walikuwa na lengo la kujiingizia fedha haramu endapo wangejitokeza na kudai malipo kwa ajili ya kumwachia Balozi Adam Mwambapa. Lakini ni kitendo cha kuona kuwa muda unaenda pasipo watekaji hao kujitokeza na kudai fedha kilizidi kunitia mashaka. Ukimya ule ulipokuwa mbioni kushika hatamu Hidaya akaibua hoja.
“Umefikia kwenye hoteli gani hapa jijini Bujumbura?’. Swali la Hidaya likanipelekea nitabasamu kidogo kabla ya kuvunja ukimya.
“Mwenyeji wangu ameniambia kuwa anakaa nyumba namba 37 kwenye jengo la shirika la nyumba la taifa kando ya barabara ya Boulevard de Iʾndependence. Nyuma ya uwanja wa mpira wa miguu wa Prince Rwegasore Stadium hapa jijini Bujumbura”
“Mh! mara hii tu ushapata mwenyeji wa kufikia kwenye jiji usilolijua?”. Hidaya akaniuliza huku akiangua kicheko cha kimbea na kuubinua mdomo wake.
“Mwenyeji wangu anaitwa Veronica. Toto zuri la kirundi lenye vigezo vyote vya kuupoza vyema mtima wangu”. Nikaongea kwa utulivu huku nikiliruhusu tabasamu hafifu kuchanua usoni mwangu. Hidaya akaangua kicheko hafifu cha udaku huku akipiga makofi dhaifu ya kimbea.
“Mh! Tibba kwa mambo hayo tu mimi sikuwezi. Najua mtoto wa watu atakuwa amebabaishwa na uzuri wako tu vinginevyo huna lolote zaidi ya kumdanganya”
“Sasa Hidaya nifanyeje wakati mzabuni wa kunipikia chakula kitamu cha kirundi na kunipa huduma nyingine za kimwili na za kiroho keshashinda tenda hiyo moyoni mwangu tena kwa kiwango cha juu”. Nikaongea kwa utulivu huku nikiangua kicheko hafifu na bila shaka Hidaya nilikuwa nimemfikisha mahala pake kwani suala la utani ilikuwa hulka yake hali iliyompelekea azidishe kicheko huku mkono wake mmoja shavuni na mdomo wake kuachama kwa mshangao.
“Mh! Tibba kweli umeshindikana bora utafute mmoja wa kuoa utakayetulia naye kama mimi ya kaka yako. Tambua kuwa umri unaenda huo!”. Hidaya akaniambia huku machozi ya kicheko yakikaribia kubisha hodi machoni mwake.
“Kwani kuoa mwisho miaka mingapi wenzangu mliopo kwenye ndoa?”. Nikamchombeza tena utani.
“Shauri yako!. Wewe kazi yako kuwachezea warembo na kuwaacha kwenye mataa. Yaani kama ndiyo ningekuwa mimi wala nisingekubaliana na huo upuuzi wako”. Hidaya akaongea huku akiyabetua mabega yake.
“Mh! jamani kwani nimemdanganya au tumekubaliana. Kama atanifaa basi huwenda nikatangaza nia kabisa na wewe ukiwa kama wifi yake mwandamizi basi naamini kuwa hapata haribika jambo”. Maneno yangu yakamuacha Hidaya akiendelea kuangua kicheko cha udaku huku kichwani nikianza kupanga namna ya kuanza rasmi harakati zangu pale jijini Bujumbura. Kile kicheko cha Hidaya kilipokuwa mbioni kukoma akageuka na kuniambia.
“Chifu aliniambia nikuandalie sehemu nzuri ya malazi pamoja na silaha”
“Wala usisumbuke Hidaya mimi nitalala kwa mrembo Veronica na kuhusu silaha tayari nimekwishaipata moja ya kuanzia kazi”. Maelezo yangu yakapeleka mshangao wa aina yake usoni kwa Hidaya na hapo kile kicheko chake kikakoma kabisa.
“Khe! Hiyo silaha umeipata wapi?”. Hidaya akaniuliza huku kanitumbulia macho kwa mshangao.
“Nimeipata huko njiani nilipotoka”. Jibu langu likatosha kabisa kumfahamisha Hidaya nini nilichokuwa nikimaanisha hivyo haraka akamezea na kubadili mada.
“Sasa ungependa nikusaidie nini kwa sasa?”
“Nahitaji usafiri wa uhakika usiokuwa na rekodi ya kesi yoyote ya barabarani”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimtazama Hidaya usoni.
“Kuhusu hilo ondoa shaka. Nyuma ya hili jengo kuna gari moja jeusi aina ya Peugeot 504. Utalitumia kwa muda wote utakao kuwa hapa jijini Bujumbura. Chifu alinifahamisha juu ya hilo mapema wakati tulipozungumza kwa simu hivyo tayari nilikuwa nimekuandalia gari”. Hidaya akaongea kwa utulivu.
“Nashukuru sana Hidaya”
“Sema kingine” Hidaya akaniambia huku akinitazama kwa shauku.
“Ofisi ya Balozi Adam Mwambapa ipo wapi katika hili jengo?’’. Nikamuuliza Hidaya huku nikiitazama saa yangu ya mkononi.
“Nje ya chumba hiki kuna korido. Ukitoka nje upande wa kushoto mwisho wa korido hiyo utaziona ngazi. Panda hizo ngazi kuelekea ghorofa ya pili na utakapomaliza kupanda hizo ngazi utajikuta ukitazamana na korido pana inayotazamana na milango ya vyumba vya ofisi mbalimbali. Wewe nyoosha moja kwa moja hadi mwisho wa hiyo korido utauona mlango mkubwa wa kijivu. Mlango huo ndiyo wa kuelekea ofisi ya Balozi Adam Mwambapa na juu yake kuna kibao kidogo cheusi chenye maandishi meupe kinachotanabaisha cheo chake”. Maelezo ya Hidaya nikayashika vyema hivyo nikasogeza kiti changu nyuma na kusimama.
“Ofisi yake ipo wazi?”. Nikamuuliza na hapo nikamuona Hidaya haraka akijipapasa mifukoni na baada ya muda mfupi akawa amepata funguo moja na kunikabidhi mkononi. Nikaipokea ile funguo na kuitia mfukoni kabla ya kumuuliza.
“Maafisa wenzako hawawezi kunisumbua?”
“Usijali nitawataarifu kuwa wewe ni fundi wa mashine ya kudurufu iliyopata hitilafu ofisini kwa Balozi”. Uongo wa Hidaya ukanifanya niliruhusu tabasamu hafifu kuchomoza usoni mwangu kwani Hidaya alikuwa msichana mjanja sana na mwerevu.
“Ngoja nikachunguze huwenda nikapata chochote cha kunisaidia”. Hatimaye nikamwambia Hidaya huku nikimkonyeza kichokozi tukio lililompelekea aangue kicheko kama ilivyokuwa kawaida yake.
“Usijali Tibba uwanja sasa ni wako unaweza kucheza utakavyo. Ukihitaji msaada wowote usisite kunijulisha mimi nitakuwa pale mapokezi nikisaidiana na wenzangu kuhudumia watu”. Hidaya akaniambia huku na yeye akisogeza kiti chake nyuma na kusimama. Nilipousukuma ule mlango na kutoka nje Hidaya tayari alikuwa nyuma yangu akanipiga ngumi hafifu ya kichokozi mgongoni kisha akashika uelekeo wa upande wa kulia kuelekea ile sehemu ya mapokezi. Nikasimama kidogo nikitabasamu huku nikimtazama Hidaya namna alivyokuwa akitembea kwa mikogo kisha nikaanza kuzitupa hatua zangu taratibu kuelekea mwisho wa ile korido sehemu kulipokuwa na ngazi za kupanda kuelekea ghorofa ya juu ya lile jengo.
Nilitembea kwa utulivu huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu na nilipozifikia zile ngazi nikaanza kuzipanda na kwa kuwa nilikuwa mgeni wa mazingira yale mara kwa mara nilijikuta nikisimama na kuweka kituo nikitazama huku na kule. Baada ya muda mfupi hatimaye nikamaliza kuzipanda zile ngazi na hapo nikajikuta nikitazamana na korido pana yenye sakafu imara ya tarazo inayotazamana na milango minne. Milango miwili ilikuwa upande wa kushoto na milango miwili mingine ilikuwa upande wa kulia na mwisho wa korido ile kulikuwa na mlango mkubwa wa rangi ya kijivu.
Kabla ya kukatisha katika korido ile nikageuka na kutazama mwisho wa ngazi zile upande wa kushoto. Kupitia dirisha jembamba la kioo lililokuwa upande ule niliweza kuona mandhari tulivu ya lile jengo yaliyozungukwa na miti mirefu ya kuvutia na bustani nzuri ya maua. Vyote vikiwa ndani ya uzio wa ukuta wenye sistimu maalum ya umeme wa kuzuia wezi. Nje ya ukuta ule niliyaona majengo mengine ya ghorofa yenye nyungo za runinga na minara ya mawasiliano juu yake.
Nikiwa nimeridhika na uchunguzi wangu wa awali nikaanza kutembea taratibu nikikatisha katikati ya korido ile kuelekea kwenye ule mlango mkubwa wa kijivu uliokuwa mwisho wa ile korido. Kwa kufanya vile nikapata wasaha mzuri wa kuitazama ile milango iliyopakana na ile korido kwa upande wa kulia na kushoto. Kwa kufanya vile nikaweza kuiona ofisi ya afisa mahusiano, ofisi za afisa mkuu anayeshughulika na masuala ya vibali vya ukaaji na pasi za kusafiria pamoja na ofisi ya afisa mkaguzi kupitia utambulisho uliokuwa juu ya milango ile. Hatimaye nikaufikia ule mlango wa kijivu uliokuwa mwisho wa ile korido na kupitia kibao cheusi juu ya mlango ule chenye maandishi meupe nikatambua kuwa ile ilikuwa ni ofisi ya Balozi Adam Mwambapa kama Hidaya alivyokuwa amenielekeza hapo awali.
Nilipoufikia ule mlango nikakishika kitasa chake na kujaribu kuufungua. Ule mlango ulikuwa umefungwa hivyo sikutaka kutia ufundi mwingine badala yake nikaingiza mkono mfukoni na kuchukua ile funguo niliyopewa na Hidaya. Nilipoupachika ule ufunguo kwenye lile tundu la kitasa na kuuzungusha kabari yake ikafyatuka na hapo nikakizungusha kidogo kile kitasa na kuusukuma ule mlango kwa ndani. Ule mlango ukafunguka na hapo kwa tahadhari nikausukuma na kuingia mle ndani kabla ya kuurudishia nyuma yangu.
Taswira iliyojengeka machoni mwangu ilikuwa ni ya mandhari tulivu ya ofisi ya kisasa yenye vitu vyote muhimu. Upande wa kushoto kulikuwa na dirisha pana la kioo dirisha hilo lilikuwa limefunikwa kwa mapazia mawili marefu ya rangi ya kijivu. Nilipoyatembeza macho yangu kwa utulivu juu ya lile dirisha nikaziona picha mbili zilizotundikwa ukutani. Picha moja ilikuwa ni ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na picha nyingine ilikuwa ni ya Balozi Adam Mwambapa akiwa katika suti nadhifu nyeusi, shati la kijivu na tai nyeusi. Macho yake tulivu katika sura yake ya umbo duara, pua pana ya kibantu na mdomo uliozungukwa na ndevu zilizokatiwa vizuri vikiongeza ziada nyingine katika wajihi wake.
Kando ya dirisha lile kulikuwa na meza kubwa ya ofisini yenye majalada mengi juu yake. Bendera ndogo mbili, moja ya taifa la Tanzania na nyingine ya taifa la Burundi. Kitabu kidogo cha katiba ya nchi ya Tanzania. Kidau cha wino, mhuri na kichupa kidogo chenye wino mweupe wa kufutia maandishi.
Nyuma ya meza ile kulikuwa na kiti kikubwa cha ofisini yenye foronya laini na kiti kile kilikuwa kimetundikwa koti jeusi la suti. Niliendelea kuyatembeza macho yangu kwa utulivu mle ndani na upande wa kulia wa ile meza nikaliona kabati kubwa nadhifu la mbao lenye droo sita. Sakafu ya ofisi ile ilifunikwa kwa zulia maridadi jekundu huku katikati likiwa na mstari mpana wenye rangi za bendera ya taifa la Tanzania.
Upande wa kushoto kulitundikwa saa kubwa ya ukutani ya mshale na pembeni ya saa ile kulikuwa kalenda moja kubwa. Kando ya dirisha lile mle ndani kulipangwa seti moja ya makochi mazuri ya ngozi laini ya sofa yaliyoizunguka meza ya kioo yenye umbo duara na chini ya meza ile kulikuwa na magazeti na majarida kadhaa tofauti ya huko siku za nyuma. Kando ya makochi yale kulikuwa na rafu kubwa ya vitabu na majalada yaliyopangwa kwa ustadi wa hali ya juu. Kiyoyozi makini kilichokuwa mle ndani kiliendea kusambaza hewa safi.
Ofisi ilikuwa ya kistaarabu sana yenye samani za kisasa na iliyopangiliwa vizuri ama kwa hakika muonekano wake uliendana kabisa na ule wa hadhi ya ofisi ya balozi. Runinga kubwa ya ukutani iliyounganishwa na chaneli tofauti za kimataifa iliyokuwa ukutani mle ndani ilikuwa imezimwa na katika kona mbili za ile ofisi kulikuwa na maua mazuri ya asili katika vyungu vyake maalum vya udongo, kazi nzuri ya mfinyanzi.
Nikiwa nimeridhishwa na mandhari nzuri ya ofisi ile yenye hadhi ya juu taratibu nikaanza kutupa hatua zangu nikianza uchunguzi kwenye yale magazeti na majarida yaliyokuwa chini ya ile meza ya kioo mle ndani iliyozungukwa na ile seti ya makochi ya sofa. Nilipofika kwenye ile meza nikaanza kufanya upekuzi. Hata hivyo nilipomaliza upekuzi wangu sikuambulia chochote cha maana kwani yale magazeti na majarida yalikuwa ni ya kawaida kabisa tena matoleo ya siku za nyuma. Hatimaye nikaiacha sehemu ile na kuhamia kwenye ile rafu ya mbao yenye vitabu na majalada chungu mzima nikaanza kufanya upekuzi wangu kwa makini huku nikipekua kila kitabu na jalada na maeneo yote muhimu katika rafu ile. Hata hivyo nilimaliza zoezi lile pasipo kuambulia chochote cha maana kwani vile vitabu na yale majalada vilikuwa ni nyaraka za wazi za sera za mahusiano ya kimataifa. Ajenda za vikao na mikutano iliyofanyika huko siku za nyuma pamoja na masuala ya sheria za kimataifa sera na mipango.
Hatimaye nikaiacha ile rafu na kuelekea kwenye lile kabati lenye droo sita lililokuwa upande wa kushoto wa ile ofisi. Nilipofika nikaanza kuzifungua zile droo moja baada ya nyingine na kuanza kufanya upekuzi makini na kwa vile droo zile hazikuwa na vizuizi vyovyote kazi ilikuwa rahisi tu. Hata hivyo ndani ya droo zile hapakuwa na kitu chochote cha maana zaidi ya picha za Balozi Adam Mwambapa akiwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wa Burundi. Picha zile zilikuwa zimepigwa katika maeneo tofauti yenye hadhi ya juu baadhi kwenye hoteli za kifahari na nyingine Ikulu ya Burundi. Hatimaye nikazifunga zile droo na kuhamishia upekuzi wangu kwenye ile meza ya ofisini.
Nilianza upekuzi kwa kupekua jalada moja baada ya jingine juu ya meza ile lakini pia sikuambulia kitu chochote katika ukomo wa upekuzi wangu hivyo nikahamishia upekuzi wangu kwenye droo tatu za meza ile ya ofisini. Mle ndani ya droo sikuambulia kitu chochote cha maana zaidi ya pini za majalada, gundi ya maji, kalamu mbalimbali za wino na karatasi mbili za kaboni zilizokuwa zimekunjwa vizuri na kuhifadhiwa vyema ndani ya bahasha ya kaki. Hakukuwa na kitu kingine cha maana ambacho kingeweza kunisaidia katika harakati zangu hivyo hatimaye nikazifunga zile droo kama nilivyozikuta. Kisha kwa makini nikayapanga vyema yale majalada pale juu ya meza huku akili yangu ikifikiria upya juu ya nini cha kufanya.
Nikiwa katika hali ile mara nikapata wazo fulani wakati nilipolitazama lile koti la suti lililotundikwa kwenye kile kiti cha ofisini. Nikasogea karibu na kulichukua lile koti na kuanza kulipekua mifukoni na wakati nikifanya vile pua yangu ikajikuta ikisumbuliwa kidogo na harufu nzuri ya manukato ya gharama yaliyopuliziwa kwenye koti lile. Lilikuwa ni koti zuri la suti lenye vifungo vinne la brandi ya daraja la kwanza kwa ubora na sikuwa na mashaka yoyote kuwa koti lile la suti lilikuwa ni la Balozi Adam Mwambapa. Hata hivyo nilipomaliza upekuzi wangu sikuambulia kitu chochote cha maana zaidi ya pakiti moja ya sigara aina ya Marlboro iliyokuwa na sigara mbili ndani yake pamoja na kibiriti kimoja cha gesi na hapo nikahitimisha kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa mvutaji wa sigara. Hatimaye nikalirudishia lile koti la suti mahala pake huku akili yangu ikianza kuhisi kushindwa.
Mwishowe nikasimama na kuitia mikono yangu mifukoni kwa utulivu huku nikianza upya kuishughulisha akili yangu. Pembeni ya ile meza ya ofisini chini yake kulikuwa na mashine ndogo ya digital ya kurudufu, printer, scanner na mashine moja ya fax. Nilijaribu kuifanyia upekuzi mashine moja baada ya nyingine nikijaribu kupekua karatasi zilizokuwa ndani yake nikichunguza kama ningeweza kupata kitu chochote muhimu cha kunisaidia. Sikupata kitu chochote cha kunisaidia na kwa kutaka kujiridhisha zaidi nikaiwasha ile kompyuta ya pale mezani ili kuchunguza kama kungekuwa na nyaraka zozote zilizokuwa zimefanyiwa kazi kupitia ile mashine ya kurudufu, printer, scanner na ile mashine ya fax. Hata hivyo jitihada zangu ziligonga mwamba kwani ile kompyuta ilikuwa imefungwa kwa password inayofahamika na mtumiaji pekee wa ile kompyuta ambaye bila shaka alikuwa ni Balozi Adam Mwambapa. Nikaanza kuhisi kuwa upekuzi wangu ulikuwa hauelekei kuniletea manufaa yoyote hivyo nikaizima ile kompyuta na kuanza kutembeatembea mle ndani katika namna ya kufikiri zaidi nini cha kufanya.
Nikiwa katika hali ile mara wazo fulani likawa limenijia kichwani baada ya kuikumbuka ile simu ya mezani iliyokuwa pale juu ya ile meza ya ofisini mle ndani. Nilipoikaribia ile meza na kuichunguza ile simu kwa utulivu nikagundua kuwa mfumo wa mawasiliano wa ile simu ulikuwa ni ule wa kizamani unaotumia sistimu ya Landline. Hali ile ikanipa matumaini hivyo nikakichukua kiwambo cha ile simu na kukiweka sikioni katika namna ya kujaribu kama ile simu ilikuwa ikitumika au lah!. Kwa kufanya vile nikagundua kuwa ile simu bado ilikuwa ikitumika.
Wakati nilipokuwa nikikirudisha kile kiwambo cha simu mahala pake ghafla nikashtuka baada ya kuuona ule mlango wa ile ofisi ukifunguliwa. Tukio lile likapelekea haraka niupeleke mkono wangu mafichoni kuikamata bastola yangu lakini kitendo cha kumuona Hidaya akiingia mle ndani kikabadili dhamira yangu na hapo nikahitimisha kwa kuweka kile kiwambo cha simu mahala pake huku uso wangu ukitengeneza tabasamu la kirafiki...ITAENDELEA IJUMAA.
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 27
Mtunzi:Kelvin Mponda

“Vipi Tibba?”. Hidaya akawahi kuniuliza huku akiurudishia vizuri ule mlango kabla ya kuanza kutembea taratibu kuja pale niliposimama.
“Poa”. Nikamwitikia Hidaya huku nikimtazama kwa sura ya kirafiki.
“Nimehisi kuwa pengine ukahitaji msaada wowote kutoka kwangu”
“Unaweza kuzungumza na opareta wa hii simu na kumuomba akupe orodha ya simu zote zilizoingia na kutoka kwa muda wa wiki mbili zilizopita?’’. Ombi langu likampelekea Hidaya anitazame kidogo kwa mshangao kabla ya kuniambia.
“Unadhani hiyo itasaidia kitu?”
“Sina hakika”. Nikamwambia Hidaya huku nikitabasamu.
“Okay! basi nipe dakika chache tu naelekea idara ya mawasiliano”. Hidaya akaniambia kisha pasipo kusubiri wazo jingine kutoka kwangu muda uleule nikamuona akielekea mahali ulipokuwa mlango wa ile ofisi kisha akaufungua na kutokomea nje. Kwa sekunde chache zilizofuata nikaendelea kuutazama ule mlango wa ile ofisi kwa utulivu huku akili yangu ikiwa mbali kabisa na eneo lile. Hatimaye nikageuka na kuelekea dirishani.
Nilipofika pale dirishani nikasogeza pazia pembeni na kupitia ukuta msafi wa kioo nikaweza kuona vizuri mandhari ya nje ya lile jengo. Ile ofisi ilikuwa ikitazamana na ile barabara iliyokuwa ikikatisha mbele ya lile jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Burundi na baada ya kuvuka ile barabara upande wa pili kulikuwa na jengo lingine refu la ghorofa. Kwa dakika kadhaa nikatulia pale dirishani huku nikilitazama jengo lile refu la ghorofa kumi na mbili na kujiuliza kuwa lilikuwa likitumika kwa shughuli gani. Nikaendelea kulichunguza lile jengo kwa utulivu huku mikono yangu nikiwa nimeigemeza pale dirishani. Chini ya lile jengo kulikuwa na magari machache yalioegeshwa katika sehemu ya maegesho ya magari ya lile jengo. Nilipoyachunguza vizuri yale magari yaliyoegeshwa pale chini nikagundua kuwa yote yalielekea kuwa ni ya watu binafsi kutokana na utambulisho wa namba zake.
Vyumba vingi vya lile jengo la ghorofa lililokuwa upande wa pili wa ile barabara vioo vyake vilikuwa vyeusi na vinavyoakisi vizuri taswira ya vitu vya nje na hivyo kutomruhusu mtu yeyote kuona mle ndani kwa urahisi. Hata hivyo bado kulikuwa na vyumba vichache katika ghorofa ya sita na ya nane ambavyo vioo vyake havikuwa vyeusi kama ilivyokuwa kwa vile vingine. Hivyo kwa kuendelea kununua muda huku nikimsubiri Hidaya arudi kule alipoenda nikapeleka macho yangu kutazama vile vyumba ambavyo vioo vyake havikuwa vyeusi na kwa kufanya vile nikaweza kuona japo kwa shida kidogo ndani ya vile vyumba vya lile jengo. Baadhi ya vile vyumba vya lile jengo madirisha yake yalikuwa yamefunikwa kwa mapazia hivyo sikufanikiwa kuona kitu chochote mle ndani. Lakini vile vyumba ambavyo madirisha yake yalikuwa hayajafunikwa kwa mapazia niliweza kuona vifaa vya ofisini kama meza na viti vyake, makabati ya kutunzia nyaraka, rafu za chuma, kompyuta na vitu vingine vidogovidogo vya kiofisi.
Ndani ya vile vyumba nikawaona baadhi ya wafanyakazi wakiwa wanaendelea na shughuli zao. Wengine wakiwa wameinamia kompyuta zao mezani na wengine wakipitia taarifa kwenye majalada ya ofisini. Alimradi kila mmoja alikuwa amezama kwenye hamsini zake na hakuna aliyekuwa akitazama pale dirishani nilipokuwa nimesimama jambo ambalo lilinipa uhuru wa kuwatazama vizuri wale watu.
Niliendelea kuvichunguza vyumba vile vya ofisi huku macho yangu taratibu yakihama kutoka kwenye floo moja ya ghorofa na kuhamia kwenye floo nyingine ya ghorofa za jengo lile. Hatimaye macho yangu yakaweka kituo kwenye chumba kimoja kilichokuwa kwenye kona ya kushoto ya floo ya nane ya lile jengo baada ya kumuona mwanaume mmoja akiwa amesimama kando ya pazia la chumba kile lililofunguliwa nusu na kuachwa wazi. Ingawa kulikuwa na umbali mrefu kiasi kutoka pale dirishani niliposimama hadi lilipokuwa lile jengo la ghorofa lakini bado niliweza kuona vizuri ndani ya kile chumba. Mtu yule mrefu alikuwa amelisogeza kidogo pazia la chumba kile huku akinitazama kwa makini pale dirishani nilipokuwa nimesimama. Macho yangu yakaweka kituo kumtazama vizuri yule mtu na nilipomchunguza kwa makini nikagundua kuwa mkononi alikuwa ameshika kitu ambacho sikuweza kukiona vizuri kutokana na vile alivyokuwa amesimama pale dirishani.
Macho yangu yakiwa yameweka kituo kumtazama kwa makini yule mtu pale dirishani taratibu fikra zangu zikaanza kuzama kwenye tafakuri ya kina nikijiuliza kuwa yule mtu ni nani alikuwa akifanya nini pale dirishani. Hata hivyo sikufika mbali kwenye uchunguzi wangu kwani mara moja moja mawazo yangu yakahamishwa haraka na tukio la mlango wa ile ofisi kufunguliwa. Nilipogeuka na kutazama pale mlangoni nikamuona Hidaya akiingia huku mkononi akiwa ameshika karatasi yenye maelezo fulani. Uso wangu ukaumba tabasamu la kirafiki huku nikimkaribisha Hidaya kwa ishara halafu haraka nikageuka pale dirishani na kurudia kutazama tena kwenye kile chumba alichokuwa amesimama yule mtu kwenye lile jengo la ghorofa lililokuwa upande wa pili wa ile barabara.
Hata hivyo uchunguzi wangu ule wa mara ya pili ukanipelekea nijikute nikikabiliana na mshtuko usioelezeka. Yule mtu kwenye kile chumba cha ghorofa la upande wa pili wa ile barabara hakuwepo tena pale dirishani kama alivyokuwa amesimama pale awali na pazia nalo lilikuwa limerudishiwa vizuri pale dirishani kiasi cha kuninyima upenyo wa kuweza kuona ndani ya kile chumba. Kwa sekunde kadhaa akili yangu ikashikwa na mduwao huku hisia mbaya zikaanza kuutafuna mtima wangu taratibu. Hata hivyo sikukata tamaa badala nikaendelea kutazama pale dirisha huku nikitarajia kuona lile pazia la kile chumba likifunguliwa na yule mtu kujitokeza tena. Baada ya kitambo kirefu kupita nafsi yangu ikaniambia kuwa nilikuwa nikijifariji bure tu kwani jambo lile lisingewezekana kutokea. Moyo wangu ukajifunza haraka kukabiliana na hali ile na nilipofanikiwa kuumeza vizuri mshtuko wangu nikageuka na kumtazama Hidaya aliyekuwa tayari amefika na kusimama kando yangu huku usoni nikiumba tabasamu hafifu la kirafiki.
“Samahani Tibba utanisamehe kwa kuchelewa kidogo”. Hidaya akavunja ukimya hata hivyo sikuona kama alikuwa amechelewa sana kama mwenyewe alivyojinasibisha.
“Usijali Hidaya kwanza nilidhani kuwa ni zoezi ambalo lingechukuwa muda mwingi zaidi ya huu ulioutumia”. Nikaongea kwa utulivu na hapo Hidaya akasogea karibu zaidi na kunionesha ile karatasi aliyoishika mkononi. Ilikuwa ni karatasi yenye rekodi zinazo onesha muda na siku ambazo ile simu ya mezani ya mle ofisini kwa Balozi Adam Mwambapa ilikuwa imetumika kupigwa na kupiga kwenda maeneo tofauti ya ndani na nje ya nchi ya Burundi kwa muda wa wiki mbili zilizopita. Kabla ya kutazama vizuri rekodi zile nikarudishia kwanza lile pazia na kufunika vizuri lile dirisha kisha nikaipokea ile karatasi mkononi mwa Hidaya na kuanza kuzipitia kwa makini rekodi zile za opareta wa idara ya mawasiliano.
Kulikuwa na simu chache zilizoingia na kutoka kwa kipindi cha juma moja lililopita na nilipochunguza kwa makini nikagundua kuwa mawasiliano yale yalikuwa yamefanyika baina ya ofisi ile ya balozi wa Tanzania nchini Burundi na kurugenzi ya mahusiano ya kimataifa ya Ikulu ya Burundi. Mawasiliano mengine yaliyofanyika yalikuwa ni baina ya ofisi ya waziri wa mambo ya nje wa nchi ya Burundi na Ikulu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.
Kupitia rekodi zile nikatafakari na kujiridhisha kuwa aina yoyote ya mawasiliano ambayo yalikuwa yamefanyika baina ya ofisi ile ya balozi wa Tanzania nchini Burundi na zile idara nyingine za serikali kwa vyovyote yalielekea kuwa ya kawaida na yalikuwa ni ya taratibu za kiutendaji za ofisi ile hivyo sikuyatilia mashaka yoyote.
Juma la pili hadi kuelekea jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi kwa kupitia rekodi zilizokuwa kwenye ile karatasi nikagundua kuwa kulikuwa na mawasiliano mengi yaliyokuwa yamefanyika kupitia ile simu ya mezani ya mle ndani ofisini kwa Balozi Adam Mwambapa. Simu za kuingia na za kutoka. Hata hivyo nilipojaribu kufuatilia mawasiliano yale yalipoishia nikagundua kuwa mawasiliano yale mengi yalikuwa ni yenye mwelekeo wa kikazi kutokana na ofisi ambazo yalikuwa yamefanyikia.
Hata hivyo wakati nikiendelea kuchunguza mara nikagundua kuwa kulikuwa na sehemu moja iliyonivuta na kuamsha upya hisia zangu ambapo simu ile ya mezani ya mle ndani ofisini ilikuwa imetumika kufanya mawasiliano. Sehemu hiyo ilikuwa ni katika hoteli moja maarufu ya kimataifa iitwayo Le Tulip Hôtel Africaine iliyokuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara mmoja wa kifaransa iliyopo pembezoni kidogo mwa jiji la Bujumbura.
Nilipoendelea kuchunguza zaidi nikagundua kuwa muda wa siku mbili zilizopita kabla ya kuelekea kwenye jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi simu ile ya mezani mle ndani ofisini kwa Balozi Adam Mwambapa ilikuwa imetumika kufanya mawasiliano mengi zaidi kuelekea Le Tulip Hôtel Africaine kuliko sehemu nyingine yoyote hali iliyopelekea kuibuka kwa maswali mengi kichwani mwangu.
“Vipi Tibba kuna jambo lolote umelishuku?”. Swali la Hidaya likanipelekea nigeuke kidogo na kumtazama huku uso wangu ukishindwa kuonesha tashwishwi yoyote. Nilimfahamu Hidaya kama mwanausalama makini na msichana aliyekuwa akiipenda sana kazi yangu ya ujasusi lakini hata hivyo sikuona kama kulikuwa na haja ya kumuelezea kila jambo juu ya hisia zangu katika tukio lile.
“Mh! kwa sasa ni mapema sana kuzungumza lolote. Nadhani kuna mambo mawili matatu nitahitajika kwanza kuyafanyia kazi ambayo huwenda yakanipa mwelekeo sahihi juu ya nini kilichojificha nyuma ya tukio hili la kutekwa kwa balozi wetu Adam Mwambapa”. Nikaongea kwa utulivu huku nikimshika Hidaya begani ingawa fikra zangu zilikuwa mbali kabisa na eneo lile.
“Nakuombea sana mafanikio katika harakati zako Tibba ili wale wote waliohusika na tukio hili wakione cha mtema kuni. Vilevile hii iwe fundisho kwa wengine wanaofikiria kufanya kitu cha namna hii”. Hidaya akaongea kwa utulivu ingawa maneno yake yalionekana dhahiri kuhifadhi chuki na hasira dhidi ya kitendo kile cha utekaji.
“Kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa ni pigo kubwa la kiusalama na udhalilishaji kwa taifa letu. Kamwe vitendo vya namna hii haviwezi kuvumilika kokote ulimwenguni”. Hidaya akaongea kwa gadhabu huku akimeza funda la mate kulitowesha donge kubwa la hasira lililomnasa kooni. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia huku kila mmoja akijitahidi kuidhibiti vyema hasira iliyokuwa ikifurukuta nafsini mwake. Ukimya ule ulipokuwa mbioni kuota mizizi mle ofisini nikageuka na kumtazama Hidaya kwa utulivu kando yangu kabla ya kamuuliza.
“Nijuavyo mimi ni kuwa balozi anapaswa kukaa kwenye nyumba yake iliyopo kwenye hili jengo. Sasa imekuwaje Balozi Adam Mwambapa akakaa nje ya eneo hili?”. Swali langu likampelekea Hidaya atabasamu kidogo kama mtu mzima aliyeulizwa swali la kitoto.
“Nyumba ya balozi inafanyiwa ukarabati hivyo serikali iliamua kukodi nyumba ya nje itakayotumika kama makazi yake hadi hapo ukarabati huo utakapokamilika”. Hidaya akaongea kwa hakika huku akinitazama.
“Nyumba ya balozi iko wapi kwenye hili jengo?”
“Juu ghorofa ya tatu”
“Naweza kuikagua?”
“Hakuna chochote unachoweza kupata”. Hidaya akaongea huku akiyabetua mabega yake.
“Kwanini unasema hivyo?”
“Ndani ya nyumba ya balozi kwenye hili jengo hakuna kitu chochote. Mafundi tu ndiyo wanaondelea na ukarabati”. Jibu la Hidaya likanipelekea nimtazame kwa kitambo huku nikitafakari. Ukimya ule ulipokuwa mbioni kushika hatamu nikanyanyua mkono kuitazama saa yangu ya mkononi halafu kama niliyeshtukia kuwa muda ulikuwa ukisonga nikavunja ukimya.
“Noamba uniruhusu niondoke Hidaya kwani tukiendelea kukaa humu ndani hatutapata majibu”. Kama ambaye ameshtushwa na wazo langu Hidaya akageuka haraka na kunitazama kwa shauku.
“Unaelekea wapi Tibba?”. Hidaya akaniuliza kwa sauti ya upweke.
“Boulevard du 28 Novembre nyumbani kwa Balozi Adam Mwambapa”
“Kuwa mwangalifu sana Tibba kwani yeyote aliyehusika na kitendo hiki haelekei kuwa ni mtu wa kawaida”. Hidaya akanionya.
“Usijali Hidaya nitakuwa mwangalifu. Utakapoongea na Chifu utamueleza kuwa tumeonana mengine tutaendelea kufahamishana pale itakapobidi”. Nikamwambia Hidaya nikishikana naye mkono wa kuagana huku tabasamu langu la kikazi likiumbika vizuri usoni mwangu. Hidaya hakusema neno lolote badala yake akaingiza mkono wake mfukoni na kutoa kadi ndogo ambayo alinikabidhi mkononi.
“Ukihitaji msaada wowote utanitafuta kupitia hii kadi”. Hidaya akaniambia kwa utulivu na bila kusema chochote nikaichukua ile kadi na kuipitishia macho kisha nikaitia mfukoni.
“Ahsante sana Hidaya”. Nikamwambia Hidaya huku nikimshika tena begani katika namna ya kumtoa hofu juu yangu kisha nikaanza kuzitupa hatua zangu kwa utulivu nikielekea kwenye ule mlango wa ile ofisi.
“Kila la kheri Tibba”
“Ahsante Hidaya tutaonana Mungu akipenda”
Nikaendelea kutembea kwa utulivu huku nikiwa na hakika kuwa macho ya Hidaya yalikuwa nyuma yangu yakinisindikiza. Hata hivyo sikugeuka nyuma badala yake nilipoufikia ule mlango wa ile ofisi nikaufungua na kutoka nje.
Akili yangu ikiwa imeanza kupata afya njema huku matendo yangu yakiwa yameanza kutawaliwa na hisia sikuona sababu ya kuendelea kupoteza muda wangu kwenye ofisi ile. Hivyo mara baada ya kutoka kwenye ile ofisi ya Balozi Adam Mwambapa nikaurudishia ule mlango nyuma yangu na kuanza kukatisha kwa utulivu kwenye ile korido kuelekea kwenye zile ngazi za kushukia ghorofa ya chini.
Muda mfupi baadaye nilikuwa nikikatisha kwenye ile kaunta ya mapokezi kuelekea nje na wakati nikifanya vile nikagundua kuwa idadi ya watu waliokuwa wakihitaji huduma kwenye ofisi zile ilikuwa imeongezeka maradufu na hivyo kupelekea msongamano mkubwa wa watu eneo lile. Nilipofika pale mapokezi nikatumia dakika chache kuwaaga wale maafisa uhamiaji ambao pale awali nilikuwa nimesalimiana nao kisha nikapenya katikati ya kundi la watu na kutoka nje.
Kitendo cha kumkumbuka yule mtu aliyekuwa akinitazama kupitia dirisha la kile chumba kilichokuwa kwenye kona ya lile jengo la ghorofa lililokuwa upande wa pili wa ile barabara iliyokuwa ikikatisha mbele ya ofisi zile za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi kikawa kimenikumbusha kuwa mwangalifu.
Kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu na magari nje ya ofisi zile za ubalozi waliofika kufuata msaada wa kidiplomasia na nilipowachunguza watu wale nikagundua kuwa wengi wao walikuwa ni raia wa nchini Tanzania waliokuwa wakiishi na kufanya kazi nchini Burundi. Nyuso zao zilionekana dhahiri kushikwa na hofu na mashaka juu ya hatima ya usalama wa maisha yao baada ya lile jaribio la mapinduzi ya kijeshi kufanyika...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 28
Mtunzi:Kelvin Mponda
Niliishusha vyema kofia kuufunika uso wangu wakati nilipokuwa nikikatisha katikati ya kundi kubwa la watu lililokuwa pale nje ya ofisi zile za ubalozi nikielekea upande wa kushoto wa lile jengo. Hata hivyo wakati nikifanya vile macho yangu yalikuwa makini zaidi kuzichunguza sura za watu na mijongeo yao. Nilipofika kwenye kona ya lile jengo nikaingia upande wa kushoto nikielekea eneo la nyuma la ofisi zile sehemu kulipokuwa na maegesho ya magari ya wafanyakazi.
Muda mfupi uliofuata nikawa nimefika nyuma ya lile jengo la ubalozi na baada ya kuyatembeza macho yangu kwa utulivu huku na kule mara nikawa nimeliona gari moja dogo na madhubuti la mtindo wa kizamani aina ya Peugeot 504 kama Hidaya alivyokuwa amenielekeza hapo awali. Gari lile jeusi lilikuwa na vioo vyeusi vinavyoweza kumuwezesha mtu aliyeko ndani kuweza kuona nje pasipo usumbufu wowote huku mtu aliyeko nje akishindwa kuona mle ndani. Gari lile lilikuwa limefungwa magurudumu mapya na madhubuti yanayoweza kuhimili vizuri mikikimikiki na rabsha za aina yeyote katika barabara korofi. Lile gari lilikuwa limeegeshwa kwenye eneo maalum lenye utambulisho wa cheo cha balozi huku kando yake kukiwa na kibao kidogo cheupe chenye maandishi meusi yanayosomeka “This Parking Lot Is Reserved For The Ambassador Only” na hivyo kupelekea gari lile kuonekana limejitenga na magari mengine yaliyokuwa yameegeshwa eneo lile.
Moyoni nikamshukuru sana Hidaya kwa kunifanyia maandalizi motomoto ya kazi yangu. Muda mfupi uliofuata nikawa nimelifikia lile gari kisha baada ya kujaribu kufungua mlango wa dereva nikafanikiwa kiulaini kwani mlango ule ulikuwa haujafungwa hivyo nikaingia mle ndani. Mara tu nilipoingia mle ndani nikakumbuka kuwa sikuwa nimechukua funguo ya lile gari kutoka kwa Hidaya lakini mara moja tu nilipochungulia kwenye swichi iliyokuwa chini ya usukani nikajikuta nikitabasamu baada ya kuiona funguo ya gari ikiwa mahala pake. Hapakuwa na muda wa kuendelea kupoteza zaidi hivyo nikafunga mlango na kuvaa mkanda wa siti. Dakika chache zilizofuata nikaitoa ile gari kwenye maegesho na kuzunguka nikielekea kule upande wa mbele wa lile jengo la ubalozi kwenye geti la kutokea. Kitu kilichonishangaza ni kuwa walinzi wa ofisi zile hawakunisimamisha na hapo nikahidi kuwa huwenda Hidaya tayari alikuwa amenisafishia njia.
Muda mfupi uliofuata nikawa tayari nimetoka kwenye lile eneo la ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi na kuingia barabarani. Mshale wa mafuta kwenye dashibodi ya lile gari ulionesha kuwa lile gari lilikuwa na mafuta ya kutosha kiasi cha kufanikiwa kunitoa wasiwasi kuwa mizunguko yangu isingekwamia njiani jambo ambalo lilinifurahisha sana.
Sikutaka kupita kwenye ile barabara niliyopita pale awali hivyo mara baada ya kuingia kwenye ile barabara iliyokuwa ikikatisha mbele ya zile ofisi za ubalozi nikashika uelekeo wa upande wa kushoto halafu baada ya mwendo mfupi wa safari yangu nikachepuka tena na kuingia upande wa kulia nikiifuata barabara ya Avenue de Gihungwe. Haikuwa barabara yenye msongamano mkubwa wa magari hivyo mwendo wangu ulikuwa wa kuridhisha. Nilipoitupia macho saa yangu ya mkononi nikagundua kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa nane mchana. Jua lilikuwa limeshamiri japokuwa hali ya hewa ya joto la jiji la Bujumbura haikuwa kama ile ya jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania.
Hatimaye nikaupeleka mkono wangu mafichoni kuipapasa bastola yangu na nilipojiridhisha kuwa bado ilikuwa mahali salama nikafyatua kofia ya kujikinga na jua juu yangu kisha nikabandika ile ramani yangu ndogo ya kijasusi ili nisisumbuke sana wakati nitakapohitaji kuitazama.
Wakati nikiendelea na safari yangu nikagundua kuwa mitaa mingi ya jiji la Bujumbura iliyokuwa na ofisi za serikali kwa muda ule ilikuwa ikilindwa na wanajeshi watiifu wa serikali ya Rais Pierre Nkurunziza. Wanajeshi wale walikuwa wamesambaa kila kona katika namna ya mkakati wa kuzima maandamano ya raia waliokuwa wakiipinga serikali iliyopo madarakani lakini vilevile katika kuhakikisha kuwa vitendo vya uvunjifu wa amani vinakomeshwa mara moja na nchi inarudi katika hali yake ya usalama haraka iwezekanavyo.
Nilipoendelea kuchunguza nikagundua kuwa kulikuwa na vikwazo vingi vya barabarani vilivyowekwa kwa makusudi na wanajeshi watiifu wa serikali katika namna ya kurahisisha upekuzi wa magari yaliyokuwa yakiingia na kutoka jijini Bujumbura tangu kutokea kwa jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi. Lengo kubwa likiwa ni kuzuia mamluki wa jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi kuingia au kutoroka jijini Bunjumbura. Hata hivyo gari langu halikusimamishwa barabarani kizembezembe na ile ilitokana na nembo ndogo ya kidipromasia yenye utambulisho wa ubalozi wa Tanzania nchini Burundi iliyokuwa imebandikwa ubavuni mwa lile gari. Hali ile ikanipelekea nikitabasamu huku moyoni nikimpongeza Hidaya kwa kuniandalia mazingira mazuri ya ufanyaji wa kazi yangu.
Baada ya safari fupi mbele kidogo nikaiacha ile barabara Avenue de Gihungwe na kuingia upande wa kushoto nikiifuata barabara ya Boulevard De la Liberte. Ilikuwa barabara pana yenye kiasi kikubwa cha magari na iliyokuwa ikikatisha katikati ya majengo marefu ya ghorofa yenye ofisi za kimataifa zenye utulivu wa hali ya juu na nje ya majengo yale magari machache yalionekana kuegeshwa katika maeneo maalum ya maegesho. Nikaendelea mbele na safari yangu huku nikifanya tathmini nzuri ya barabara ile iliyoonekana kuwa na watu wachache watembea kwa miguu.
Baada ya mwendo mfupi wa safari yangu mbele kidogo nikaiacha barabara ile na kuchepukia upande wa kulia nikiifuata barabara ya Avenue Des Euphorbes lakini mara moja nikajikuta nikishikwa na mshtuko. Mara tu baada ya kuingia kwenye barabara ile kupitia vioo vya ubavuni vya gari langu nikawa nimeliona gari moja jeupe aina ya Landcruiser Hardtop likiwa kiasi cha umbali usiopungua mita mia moja nyuma yangu. Ingawa sikuwa na hakika kama gari lile lilikuwa likinifungia mkia au lah! lakini akili yangu ilianza kupoteza utulivu taratibu kadiri nilivyokuwa nikiendelea kulitazama gari lile kupitia vile vioo vya ubavuni vya gari.
Nilikuwa nimepanga kuwa mara nitakapofika mbele ningeingia barabara ya RN 7 na baada ya kuuvuka mzunguko wa barabara hiyo ningeingia upande wa kushoto kuifuata barabara ya Boulevard du 28 Novembre ambapo mbele yake ningechepuka tena na kuingia kwenye barabara za mitaa mingine ambazo hatimaye zingekuja kunikutanisha na ile barabara kuu ya Chaussée P.L.Rwagasore hadi kwenye nyumba namba 26 yalipokuwa maskani ya Balozi Adam Mwambapa. Lakini kitendo cha kuliona lile gari jeupe Landcruiser Hardtop nyuma yangu kikanipelekea nibadili uelekeo.
Hivyo nilipoifikia ile barabara ya RN 7 sikuingia upande wa kulia kuifuata ile barabara badala yake nikakatisha na kuingia barabara ya Avenue des Chênes. Kitendo cha kuingia kwenye barabara ile kikalipelekea lile gari jeupe Landcruiser Hardtop nalo likatishe kwenye ile barabara ya RN 7 na kushika uelekeo wangu japokuwa lilikawia kidogo baada ya kusubiri magari machache yakatishe kwanza kwenye barabara ile. Tukio lile bado lisingekuwa kigezo cha kuniridhisha kuwa sasa nilikuwa nimefungiwa mkia hata hivyo kwa namna nyingine ile ilikuwa ni ishara mojawapo ya kunitahadharisha kuwa nilipaswa kuwa makini na mienendo yangu.
Mara hii nilijikuta nikilitazama lile gari kwa utulivu wa hali ya juu katika namna ya kutafuta hakika kama nilikuwa nikifungiwa mkia na lah!. Hivyo baada ya mwendo mfupi wa safari yangu nikaiacha barabara ile na kuchepuka upande wa kushoto nikiifuata barabara ya Avenue Des Mimosas. Niliendelea kuendesha gari katika barabara ile huku kijasho chepesi kikianza kunitoka usoni. Moyo wangu nao ukawa umeanza kupoteza utulivu hata hivyo kwa kila hali nilijitahidi kupambana kikamilifu na hali ile.
Akili yangu ikiwa mbioni kupoteza utulivu sasa nilikuwa makini sana kulichunguza lile gari kupitia vile vioo vya ubavuni. Hata hivyo lile gari halikujitokeza mapema hadi pale nilipokuwa mbioni kufikia mwisho wa barabara ile. Nilipenda kutafuta hakika juu ya hisia zangu hivyo nilipofika mwisho wa barabara ile nikachepuka upande wa kulia nikiifuata barabara ya Avenue Des Non Aligens. Ilikuwa barabara pana iliyokuwa ikikatisha katikati makazi ya watu na hapakuwa na msongamano mkubwa wa magari katika barabara ile hivyo niliamua kuongeza mwendo. Kwa kufanya vile haukupita muda mrefu mara nikaliona lile gari Landcruiser Hardtop jeupe likiingia kwenye ile barabara na kushika uelekeo wangu.
Bado sikutaka kujipa hakika kuwa lile gari lilikuwa likinifungia mkia hivyo kwa kutafuta hakika zaidi baada ya safari ndefu katika barabara ile hatimaye mbele nikaja kukutana na barabara ya Avenue Pierre Ngendandumwe. Nilipoifikia barabara ile nikakunja kona na kuingia upande wa kulia nikiifuata barabara ile kwa utulivu lakini vilevile nikipunguza mwendo wangu kwa kasi. Ilikuwa ni barabara yenye pilikapilika nyingi za magari na watembea kwa miguu hivyo hali ile niliipenda kwa jambo moja kwani lingekuwa ni jambo rahisi kwangu kufanya uchunguzi juu ya lile gari nililohisi kuwa lilikuwa likinifungia mkia.
Haukupita muda mrefu mara nikaliona lile gari Landcruiser Hardtop jeupe likiingia kwenye ile barabara na kufuata uelekeo wangu. Kitendo kile kikanipelekea nitabasamu kidogo baada ya kuridhishwa vizuri na tathmini za hisia zangu. Sasa nilihitimisha kuwa lile gari Landcruiser Hardtop jeupe nyuma yangu lilikuwa kazini kunifungia mkia kama nilivyokuwa nimehisi pale awali.
Nilipofika mwisho wa ile barabara ya Avenue Pierre Ngendandumwe nikachepuka na kuingia upande wa kushoto nikiifuata barabara ya Avenue de Muramvya halafu nilipofika mbele kidogo nikachepuka na kuingia upande wa kulia nikiifuata barabara ya Avenue DʾOctobre. Nilipoingia kwenye ile barabara nikaongeza mwendo lakini lile gari jeupe Landcruiser Hardtop halikuniacha nifike mbali nyuma yangu na badala yake nikaliona likiongeza mwendo kunifuata.
Sikutaka mtu au watu waliokuwa ndani ya lile gari jeupe Landcruiser Hardtop nyuma yangu wafahamu nilipokuwa nikielekea. Hivyo mara tu nilipoyapita makutano ya barabara ya Avenue des Travailleurs mbele kidogo nikaingia barabara ya Boulevard du 28 Novembre na kushika uelekeo wa upande wa kulia na hivyo kushika uelekeo wa kurudi kule nilipotoka.
Kitendo cha kuingia kwenye ile barabara ya Boulevard du 28 Novembre kikanipelekea niongeze mwendo zaidi huku akili yangu ikisumbuka katika kutafuta namna ya kukabiliana na lile gari lililonifungia mkia nyuma yangu. Baada ya kufikiri kwa muda hatimaye nikawa nimepata wazo kuwa mara baada ya kuufikia ule mzunguko wa barabara wa RN 7 ningeshika uelekeo wa upande kushoto nikiifuata barabara ya Chaussée de Gitega kuelekea eneo liitwalo Muha lililojitenga kidogo na makazi ya watu. Nikiamini kuwa nikiwa huko ningeweza kukabiliana vizuri na mtu au watu waliokuwa ndani ya lile gari. Hata hivyo mawazo yangu yalikatishwa haraka na kizuizi cha barabarani kilichokuwa katika makutano ya barabara ya Boulevard du 28 Novembre na barabara ya Avenue de Muramvya.
Haraka nikapunguza mwendo wa gari baada ya kumuona askari jeshi mmoja akijitokeza na kusimama katikati ya barabara ile akinioneshea ishara kwa mkono wake kuwa nisimame huku mkono wake mmoja akiwa ameikamata vyema bunduki yake SMG. Kwa kweli lilikuwa ni tukio la kushtukiza lakini vilevile lililoichanganya vibaya akili yangu hasa pale nilipokumbuka kuwa nyuma yangu nilikuwa nikifuatiliwa na lile gari jeupe Landcruiser Hardtop. Wakati nikipunguza mwendo kichwani nikawa nikipiga akili namna ya kujinasua kutoka katika kadhia ile bila kupoteza muda. Hata hivyo ni kama hila yangu ilikuwa imeanza kushtukiwa kwani haraka niliwaona wanajeshi wengine wawili wakiongezeka katikati ya barabara ile na kusimama nyuma ya kizuizi kikubwa cha barabarani huku nao wakiwa na bunduki zao mikononi. Loh! hila zangu ni kama zilikuwa mbioni kugonga mwamba.
Hata hivyo nikapunguza mwendo taratibu huku nikijitahidi kukabiliana na hali ile na nilipochunguza nyuma kupitia vioo vya ubavuni vya lile gari langu nikaliona lile gari jeupe Landcruiser Hardtop likitimua mbio kunikaribia. Hali ile ikapelekea kijasho chepesi kianze kunitoka maungoni. Wakati nilipokuwa nikikikaribia kile kizuizi mbele yangu nikagundua kuwa kulikuwa na magari mengine manne yaliyokuwa yamesimamishwa kando ya ile barabara yakipekuliwa na wajeshi wengine.
Hatimaye nikakifikia kile kizuizi cha barabarani na kusimama hata hivyo sikushuka kwenye gari badala yake nikashusha kioo cha dirishani kwangu na kutengeneza tabasamu la kirafiki. Wanajeshi wawili haraka wakalizingira gari langu. Mwanajeshi mmoja akaja dirishani hata hivyo hakunisemesha neno zaidi ya kunionesha tabasamu lake la kirafiki baada ya kuiona ile nembo ya ubavuni mwa gari langu iliyokuwa ikilitambulisha lile gari kuwa ni mali ya ubalozi wa Tanzania nchini Burundi. Nikawaona wale wanajeshi wakilizunguka gari langu kama ambao wanachunguza chunguza mle ndani kisha yule mwanajeshi aliyesimama pale mlangoni akanifanyia ishara kwa kichwa kuwa niendelee na safari yangu. Nikatabasamu kidogo na kumuaga yule afande kwa kumpungia mkono kisha nikatia moto gari na kuondoka eneo lile na wakati nikiondoka kupitia vioo vya ubavuni vya gari langu nikawaona wale wanajeshi wakilisimamisha lile gari jeupe Landcruiser Hardtop lililokuwa nyuma yangu likinifukuza.
Tukio la lile gari Landcruiser Hardtop jeupe kusimamishwa na wale wanajeshi kwenye kile kizuizi nyuma yangu likanipelekea nitabasamu kwani niliamini kuwa ule ndiyo ungekuwa wakati wangu mzuri wa kulitoroka lile gari na kuendelea na harakati zangu. Hata hivyo hilo halikutokea badala yake muda mfupi uliofuata nikajikuta nikishikwa na mshangao kwani wakati nilipokuwa mbioni kuuzunguka ule mzunguko wa barabara wa RN 7 upande wa kushoto nikaliona lile gari jeupe Landcruiser Hardtop likiingia kwenye ule mzunguko wa barabara kunifuata nyuma yangu. Kwa kweli nilipatwa na mshtuko wa aina yake kiasi cha moyo wangu kupoteza kabisa utulivu. Hatimaye hisia zangu zikanitanabaisha kuwa nilikuwa mbioni kukabiliana na hatari.
Sikutaka hatari ile inifikie hivyo mara baada ya kuuvuka mzunguko ule wa barabara haraka nikaingia barabara ya Chaussée de Gitega na kuongeza mwendo. Ilikuwa barabara pana ya lami iliyokuwa ikielekea mbali na jiji la Bujumbura isiyokuwa na pilika za magari wala watembea kwa miguu. Barabara ile ilikuwa ikikatisha katikati ya vichaka hafifu na miti mirefu ya kivuli na hivyo kupelekea utulivu wa hali ya juu safarini. Nikiwa katika mwendo mkali njiani nikapishana na malori mawili ya mizigo na gari moja la mtu binafsi. Sikuwa na shaka yoyote kuwa madereva wa magari yale waligeuka kunishangaa baada ya kupishana na mimi huku nikiwa katika mwendo kasi usioelezeka.
Kwa mujibu wa ramani yangu ndogo ya kijasusi iliyokuwa kwenye ile kofia ya kujikinga na jua juu yangu ni kuwa kule mbele kidogo mara baada ya kulipita jengo la kiwanda cha kuchapisha magazeti. Upande wa kulia ningevuka daraja kubwa na baada ya kulivuka daraja lile barabara ile ingekatisha katikati ya makazi ya watu. Sikupenda kuyafikia makazi yale ya watu kabla ya mpango wangu kukamilika.
Wakati nilipokuwa mbioni kulipita lile jengo la kiwanda cha kuchapisha magazeti mara nikaliona lile gari jeupe Landcruiser Hardtop likichomoza kwa kasi nyuma yangu huku likiwa limewasha taa kali za mbele. Nilielewa haraka nini maana ya tukio lile hivyo na mimi nikaongeza mwendo zaidi. Hata hivyo dereva wa lile gari Landcruiser Hardtop jeupe nyuma yangu alikuwa mwepesi wa kuishtukia haraka hila yangu hivyo hakunipa nafasi. Kufumba na kufumbua lile gari jeupe Landcruiser Hardtop likawa tayari limenifikia kando yangu ubavuni. Nikageuka haraka kulitazama lile gari na hapo wasiwasi ukaniingia mara baada ya kukiona kioo cha dereva wa lile gari kikishushwa chini kwa haraka. Wakati nikiendelea kushangazwa na tukio lile mara nikauona mtutu wa bastola ukipenyezwa katika upenyo wa dirisha lile na kuelekezwa kwangu.
Hapakuwa na muda wa kuendelea kusubiri nini ambacho kingetokea baada ya pale hivyo haraka nikaminya breki kuliruhusu lile gari linipite mbele yangu. Muda uleule nikasikia mlio mkali wa risasi iliyonikosa shabaha na kufanikiwa kuparaza boneti ya gari langu na kusababisha cheche kali. Sikuiruhusu risasi ya pili kunifikia hivyo haraka nikaichomoa bastola yangu kutoka mafichoni kisha mkono wangu mmoja ukiwa umeshika usukani nikairuhusu risasi moja kufanya kazi. Hata hivyo risasi ile ikapoteza shabaha kidogo na kukichangua vibaya kioo cha mbele cha lile gari. Risasi ya pili niliyoifyatua haraka ikakichangua vibaya kioo cha mlango wa dereva wa lile hali iliyompelekea yule dereva wa lile gari kuinama chini ili kulipisha shambulizi lile makini...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 29
Mtunzi:Kelvin Mponda

Nilipokuwa nikijiandaa kufyatua risasi ya tatu dereva wa lile gari akawa mwerevu wa kushtukia mapema hila yangu hivyo akaliwahi gari langu na kuligonga ubavuni. Mtikisiko uliotokea ukapelekea bastola yangu iniponyoke mkononi na kuangukia kwenye siti ya abiria kushoto kwangu. Nilifahamu kuwa ule ungekuwa mchezo hatari kwani lile gari jeupe Landcruiser Hardtop lilikuwa na nguvu zaidi kuliko gari langu hivyo haraka nikawa nafikiria namna ya kufanya. Nilipotazama kule mbele nikagundua kuwa tulikuwa tumelikaribia lile daraja la mto mkubwa uliokuwa ukikatisha eneo lile. Wakati nikiendelea kufikiria nini cha kufanya lile gari jeupe Landcruiser Hardtop likawa tayari limenifikia tena na kunipiga kumbo ubavuni kiasi cha kufanikiwa kunihamisha barabarani na kunisogeza kwenye uchochoro hafifu wenye nyasi fupi uliokuwa kando ya ile barabara.
Tukaendelea kufukuzana huku nikijitahidi kwa kila hali kulirudisha gari langu barabarani hata hivyo sikufanikiwa haraka mpango wangu ingawa sasa niliweza kulikwepa lile gari kila lilipokuwa likitia bidii kunipiga kumbo. Dereva wa lile gari alipoona hila yake inaelekea kushindwa akachungulia kidogo dirishani kunitazama na hilo likawa kosa kubwa kuwahi kufanywa na binadamu yule. Nilikuwa tayari nimeichukua ile bastola yangu na kaimata vyema kwa mkono wangu wa kushoto na safari ile sikufanya tena makosa kwani risasi moja niliyoiruhusu baada ya kuvuta kilimi cha bastola yangu ikapenya katikati ya paji la uso wa yule dereva na kukifumua vibaya kichwa chake.
Tukio lile likalipelekea lile gari lianze kupoteza uelekeo huku likiyumbayumba ovyo barabarani. Wakati tukio lile likiendelea mara nikamuona mtu mwingine aliyekuwa amekaa kwenye siti ya abiria kando ya yule dereva akisogea pale kwa dereva na kujitahidi kuudhibiti usukani wa gari. Hata hivyo hakufanikiwa kwani muda ule tulikuwa tayari tumelifikia lile daraja la ule mto mkubwa na sikutaka kuichezea nafasi ile. Hivyo haraka nikakanyaga pedali ya mafuta na kuanza kulifuata lile gari kushoto kwangu. Yule dereva wa lile gari jeupe Landcruiser Hardtop alikuwa tayari ameulalia usukani wa lile gari huku uhai ukiwa mbali na mwili wake na yule msaidizi wake ndiyo kwanza alikuwa akiukaribia ule usukani wa gari. Hivyo kumbo moja la nguvu la gari langu pasipo upinzani wowote lilitosha kabisa kuliondosha lile gari barabarani. Muda ule mara nikayaona magurudumu ya mbele ya lile gari jeupe Landcruiser Hardtop yakiparamia vibaya ukingo wa lile daraja tukio lililoambatana na mayowe kadhaa ya hofu kutoka kwa watu waliokuwa mle ndani ya lile gari ambao idadi yao sikuweza haraka kuifahamu.
Magurudumu ya lile gari Landcruiser Hardtop yalipoupanda ule ukingo wa lile daraja nikaliona lile gari likipiga sarakasi mara mbili zaidi hewani. Tukio lile likapelekea mlango mmoja wa lile gari ufunguke na mtu mmoja mwenye sare za kijeshi kuchomoka toka mle ndani. Haraka nikapunguza mwendo kushuhudia ajali ile ya kutisha. Muda uleule lile gari likatumbukia kwenye ule mto na kutengeneza mshindo wa aina yake eneo lile. Yule mtu aliyechomoka kwenye mlango wa lile gari akapiga yowe la hofu huku akisema maneno fulani nisiyoyaelewa wakati akiwa angani lakini hatimaye na yeye akatumbukia kwenye ule mto umbali wa hatua chache kutoka pale lilipotumbukia lile gari. Taratibu nikaendesha gari langu huku nikishuhudia tukio lile hadi pale nilipovuka lile daraja kisha nikaegesha gari langu kando ya ile barabara na kushuka nikielekea kule mtoni.
Hapakuwa na mtu yeyote eneo lile wala magari yaliyokuwa yakikatisha kwenye ile barabara kwa wakati ule na hali ile ilinipa uhuru. Kwa dakika kadhaa nikasimama kando ya ule mto nikiitazama kwa makini ile sehemu ya mto lilipokuwa limetumbukia lile gari na yule mtu pasipo kuona chochote. Hata hivyo yale maji ya mto kwa sehemu ile yalionekana kutibuka sana. Kufuatia mvua za masika zilizokuwa zikiendelea kunyesha nchini Burundi ule mto ulikuwa umefurika sana kiasi cha kuelekea kutapisha maji kwenye kingo zake. Sikuwa na mashaka yoyote kuwa ule mto ulikuwa na kina kirefu sana kwani pamoja na lile gari kutumbukia kwenye ule mto lakini bado sikuweza kuona dalili zozote za uwepo wa lile gari mle mtoni na badala yake yale maji ya mto yaliendelea kusafiri kwa utulivu huku sauti ya mzizimo wake ikituama vyema masikioni mwangu.
Nikiwa bado nimesimama kando ya ule mto nikaendelea kutazama kwenye ule mto sehemu ambayo lile gari lilikuwa limetumbukia. Muda ukazidi kusonga pasipo kuona dalili zozote za kuibuka kwa mtu watu au lile gari huku maroli mawili ya mizigo yakipita juu ya lile daraja na kuendelea na safari. Hatimaye nikakata tamaa kabisa ya kuliona lile gari lililotumbukia kwenye ule mto au wale watu waliokuwa mle ndani. Kulikuwa na kila dalili kuwa mvua kubwa ingenyesha muda mfupi baadaye kwani hali ya hewa ilikuwa imebadilika ghafla na wingu zito lilikuwa limeanza kutanda angani.
Nikiwa sasa nimekata tamaa ya kuambulia chochote mwisho nikaamua kuanza kuondoka taratibu eneo lile. Lakini ghafla wakati nikianza kuondoka nyuma yangu kwenye ule mto nikashtushwa na sauti mtu akipiga yowe kuomba msaada. Nikageuka haraka na kutazama kwenye ule mto ile sauti ilipokuwa ikitokea na hapo nikajikuta nikishikwa na mshtuko. Mwanaume mmoja alikuwa akijitahidi kuogelea kutoka kwenye lile eneo la mto lile gari jeupe Landcruiser Hardtop lilipokuwa limetumbukia huku akiomba msaada. Yule mtu alikuwa hodari sana wa kuogelea akiogelea kwa jitihada zake zote kuelekea kwenye ukingo wa ule mto kwa kihoro kikubwa kama mtu akimbiaye kifo.
Tumaini la kukipata kile nilichokuwa nikikitarajia likafufuka upya moyoni mwangu na hapo nikaanza kutimua mbio nikirudi kumfuata yule mtu kwenye ukingo wa ule mto.
Mwanzoni nilidhani kuwa mtu yule huwenda angekuwa ndiye yule aliyechomoka mlangoni wakati lile gari lililotumbukia mtoni lilipokuwa likipiga sarakasi hewani lakini wakati nikimkaribia nikagundua kuwa hakuwa yeye. Hata hivyo nilipomchunguza vizuri yule mtu nikamkumbuka kuwa alikuwa ndiye yule aliyekuwa akinitazama kupitia dirishani wakati alipokuwa kwenye kile chumba cha jengo la ghorofa lililokuwa likitazamana na lile jengo la ghorofa lenye zile ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi muda mfupi uliopita.
Yule mtu akaendelea kuogelea kwa bidii zake zote hadi alipofika kwenye ukingo wa ule mto huku akiwa hajiwezi kwa hali. Nikawahi kumfikia na kumshika mkono hata hivyo sikumtoa kutoka kwenye yale maji mengi ule ya mto hivyo akawa anaeleaelea tu kwenye ule ukingo. Bila shaka yule mtu hakuwa amenitambua haraka kuwa mimi ni nani kwani macho yetu yalipokutana nikaiona hofu iliyomwingia haraka usoni mwake kiasi cha kutaka kurudi kule alipotoka. Hata hivyo hakufanikiwa kwani tayari nilikuwa nimemkwida shingoni na nilipomchunguza vizuri nikamuona kuwa alikuwa ameningʾiniza kamera shingoni.
“Wewe ni nani?” Nikamuuliza kibabe pasipo kutaka kufahamu kama alikuwa akifahamu kuzungumza kiswahili au lah!. Kupitia ile kamera shingoni mwake nikajikuta nikimkumbuka vizuri yule mtu kwani wakati alipokuwa akinitazama kupitia kwenye lile dirisha la kile chumba kilichokuwa kwenye kona ya lile jengo la ghorofa lililokuwa likitazamana na zile ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Burundi. Nikakumbuka kuwa mtu yule alikuwa ameshika kitu fulani mkononi ambacho kutokana na ule umbali sikuwa nimekiona vizuri kitu kile. Lakini sasa kumuona mtu yule akiwa ameningʾiniza kamera shingoni nikapata hakika kuwa nilikuwa nimepigwa picha kadhaa wakati nilipokuwa nimesimama kwenye lile dirisha la ofisi ya Balozi Adam Mwambapa. Yule mtu alikuwa amevaa suruali ya kijivu na shati jeusi na umri wake haukuelekea kuzidi miaka arobaini. Mweusi na mrefu lakini mwenye macho yaliyohifadhi kila hila nafsini mwake.
“Naitwa Jean-Baptiste Nibizi”. Yule mtu akajitambulisha kwa kujiamini kana kwamba alikuwa ni mtu maarufu sana Jijini Bujumbura ambaye ni mimi tu ndiye ambaye nilikuwa simfahamu na lafudhi ya kiswahili chake ilikuwa ni ya kirundi.
“Mna shida gani na mimi?”. Nikamuuliza yule mtu huku nikizidi kumkwida shati lake shingoni.
“Sina shida yoyote na wewe”. Yule mtu akaongea kwa unyonge hata hivyo nikamchangamsha kwa kumzaba makofi mawili ya nguvu usoni.
“Sasa kwa nini mnanifuatafuata kila niendako?”
“Siyo mimi ni wale mimi nimelipwa tu pesa kwa ajili ya kuchukua picha zake”. Maelezo ya yule mtu yakanipelekea nimtazame kwa mshangao kidogo huku nikishindwa kumuelewa vizuri.
“Wale akina nani?”. Hatimaye nikamuuliza.
“Wale watu niliokuwa nao ndani ya lile gari”. Yule mtu akaongea kinyonge.
“Mlikuwa wangapi mle ndani ya gari?”
“Tulikuwa sita na mimi wa saba”
“Nipe kamera yako”. Nikamwambia yule mtu huku nikizidi kumkwida hata hivyo yule mtu hakuonesha upinzani wowote badala yake taratibu akaanza kuivua ile kamera yake kutoka shingoni na wakati akiendelea na zoezi lile nikaendelea kumhoji.
“Nani aliyekulipa pesa kwa ajili ya kuchukua picha zangu?’’. Yule mtu hakufanikiwa kujibu swali langu badala yake ghafla nikamuona akitoa macho na kuacha mdomo wake kama mjusi alikanyagwa na gurudumu la baiskeli tumboni kisha nikaanza kuona damu nyepesi ikimtoka yule mtu puani na mdomoni. Wakati nikiendelea kushangazwa na hali ile mara nikamsikia yule mtu akipiga yowe hafifu la kukata kauli na hapo nikaliona tundu dogo linaloanza kuvuja damu upande wa kushoto wa kifua chake. Haikuniwia vigumu kufahamu kuwa tundu lile linalovuja damu lilikuwa limetokana na shambulizi la risasi hali iliyonipelekea nishikwe na hofu. Yule mtu akaniponyoka mkononi na kuanza kuzama taratibu hata hivyo haraka nikawahi kuupelekea mkono wangu kuichukua ile kamera yake shingoni. Sikufanikiwa na katika muda mfupi tu nikatambua kuwa lile zoezi lisingewezekana kwani mkanda wa ile kamera ulikuwa tayari umefyatuliwa na yule mtu kabla sijaifikia hivyo ile kamera ikawahi kuangukia kwenye maji ya ule mto na kupotea. Nikashawishika kumvuta yule mtu na kumtoa nje ya ule mto hata hivyo wazo lile nikaliweka kando pale nilipojiridhisha kuwa tayari yule mtu alikuwa amekufa. Risasi ya mwisho iliyotoka mafichoni kusikojulikana ikaniparaza kidogo begani na kuacha tundu kwenye shingo ya yule mtu. Hivyo sikuwa na namna tena ya kumuokoa yule mtu badala yake nikamwachia haraka mikononi tukio lililompelekea asombwe haraka na maji ya ule mto huku mimi nikiruka na kujibanza kwenye kichaka kilichokuwa kando ya ukingo wa ule mto.
Nikiwa nimejibanza kwenye kile kichaka nikaikamata vyema bastola yangu mkononi huku nikiyatembeza macho yangu huku na kule pasipo kumuona mtu yeyote eneo lile. Kwa kweli tukio lile lilinishangaza sana kwani bado sikuweza kufahamu haraka kuwa yale mashambulizi ya risasi yalikuwa yakitokea upande gani. Hata hivyo haraka nikagundua kuwa pale kwenye kile kichaka bado sikuwa sehemu salama kwani risasi kadhaa ziliendelea kuniandama eneo lile kiasi cha kuelekea kutishia usalama wangu. Hali ile ilipoelekea kuzidi kutishia usalama wangu nikajitupa chini na kuanza kutambaa taratibu nikihamia kwenye kichaka kingine kilichokuwa jirani na eneo lile.
Zile risasi zikaendelea kurindima kwenye kile kichaka na kwa kuwa mipigo yote ilikuwa ya kimyakimya nikajua kuwa kwa vyote bunduki iliyokuwa ikitumika katika shambulizi lile ilikuwa imefungwa kiwambo maalum cha kuzuia sauti. Swali likabaki kuwa shambulizi lile lilikuwa likifanywa na nani na mtu huyo alikuwa amejificha wapi eneo lile. Niliendelea kujibanza kwenye kichaka huku nikijipa utulivu na kutazama huku na kule eneo lile. Muda mfupi uliofuata zile risasi zikakoma na eneo lile likamezwa na utulivu wa hali ya juu. Hata hivyo nikaendelea kujipa subira.
Kwa kufanya vile mara nikajikuta nikivutiwa na taswira ya kichuguu kidogo kilichokuwa kimechomoza kwenye pembe ya nguzo moja ya lile daraja chini yake. Nilipoendelea kuchunguza vizuri nikagundua kuwa kile hakikuwa kichuguu kama nilivyokuwa nimedhani ila kilikuwa kichwa cha mtu aliyekuwa akijitahidi kuchungulia kwa makini pale kwenye kile kichaka cha awali nilipokuwa nimejibanza. Nilipomchunguza vizuri yule mtu haraka nikamtambua kuwa alikuwa ni yule mwanajeshi aliyechomoka mlangoni wakati ile Landcruiser ilipokuwa ikipiga sarakasi na kutumbukia mtoni. Mkononi alikuwa ameshika bastola. Sasa nilifahamu kuwa yule mtu alikuwa amefanikiwa kuogelea na hatimaye kujiokoa kutoka kwenye ule mto.
Sikutaka kufanya papara ya namna yoyote badala yake nikajipa utulivu katika namna ya kumwaminisha yule mtu kuwa shambulizi lake lilikuwa limezaa matunda kwenye kile kichaka nilichokuwa nimejibanza pale awali. Yule alipoona kuwa hakuna mtikisiko wowote kwenye kile kichaka akajiaminisha kuwa tayari alikuwa amenilaza chini hivyo akajitokeza kwa uhuru zaidi nyuma ya ile nguzo ya daraja huku akitazama tazama huku na kule. Sikutaka kumuacha aendelee kutabaruku zaidi hivyo nikaikamata vyema bastola yangu na kumchapa risasi ya begani na hapo bila kupenda akaiachia ile bastola yake mkononi na kuangukia mtoni.
Yule mtu akapiga yowe kali la maumivu na kujishika begani huku akishangaa kuwa shambulizi lile lilikuwa limetokea uelekeo gani. Muda ule nikawa tayari nimekijaza vizuri kichwa chake kwenye jicho langu hiyo yule mtu hakupata nafasi ya kuomba maji kwani risasi yangu moja ikamchakaza vibaya na hapo akaanguka na kutumbukia kwenye ule mto akisombwa na maji.
Niliendelea kujibanza kwenye kile kichaka kwa muda mrefu katika namna ya kujiridhisha na hali ya usalama wa eneo lile hadi pale nilipohakikisha kuwa hali ilikuwa shwari ndiyo nikatoka kwenye yale maficho kwa tahadhari na kuelekea kule nilipokuwa nimeegesha gari langu. Manyunyu hafifu ya mvua yalikuwa yameanza kuanguka kutoka angani wakati nilipoitazama saa yangu ya mkononi na kugundua kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa kumi na moja kasoro robo jioni. Sikuwa na muda wa kupoteza hivyo mara tu nilipoingia kwenye gari nikaanza safari ya kurudi mjini huku jina la Jean-Baptiste Nibizi likianza kutawala fikra zangu.
Mambo yote yaliyotokea kwenye ule mto yalikuwa kama kipande cha mkasa katika filamu ndefu nisioufahamu mwisho wake. Sikuweza kufahamu watu wale waliokuwa wakinifuatilia kwenye lile gari jeupe Landcruiser Hardtop lililotumbukia mtoni walikuwa ni akina nani na walikuwa na shida gani na mimi. Hata hivyo niliamini kuwa hadi kufikia wakati ule uwepo wangu jijini Bujumbura nchini Burundi ulikuwa ukifahamika na watu fulani nisiowafahamu. Nilimkumbuka yule mtu aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Jean-Baptiste Nibizi wakati aliponiambia kuwa alikuwa amelipwa pesa kwa ajili ya kunipiga picha kwa siri na hapo nikahisi kuwa kulikuwa na mtu au kikundi cha watu waliokuwa wakitengeneza mikakati michafu katika kuhakikisha kuwa nauwawa mapema kabla harakati zangu hazijafika kokote. Nilitaka kufahamu kuwa watu hao wangekuwa akina nani hata hivyo nilitambua kuwa kwa wakati ule hilo lisingewezekana hivyo nikaendelea na safari yangu huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu.
______
Kama ilivyokuwa kwa viongozi wengi wa bara la Afrika kupenda kuishi kwenye maeneo ya mijini yenye hadhi ya juu kiuchumi na kiusalama. Makazi ya balozi wa Tanzania nchini Burundi Meja jenerali mstaafu Adam Mwambapa nayo pia yalikuwa katika eneo zuri la kifahari lenye majumba makubwa ya kisasa ya watu wakwasi yaliyokuwa yamezungukwa na kuta ndefu za uzio na mageti makubwa yenye vifaa vyote vya usalama vya kuwahakikisha wakazi wake usalama wa hali ya juu.
Eneo la Chausée P.L.Rwagasore jijini Bujumbura lilikuwa limezungukwa na makazi ya kisasa ya viongozi wa kitaifa na wa kimataifa. Vitongoji vyake vilikuwa vimeunganishwa kwa barabara nzuri za lami zenye taa za barabarani. Pilika za watu na magari zilikuwa hafifu sana huku ustaarabu wa kisomi ukionekana kuzingatiwa kwa asilimia zote. Kwa mbali ukiwa barabarani ungeweza kumuona mtu mmoja mmoja au wawili katika sehemu za kupumzikia za majengo yale ya ghorofa kwa juu wakinywa kahawa na kusoma vitabu na magazeti. Sehemu nyingine ungeona nguo zikiwa zimeanikwa kwenye sehemu maalum za kuanikia nguo. Mahali fulani ghorofani ungeweza kuwaona wapenzi wakiwa wamesimama wakitazama mandhari nzuri ya kupendeza nje ya nyumba zao za kifahari nyakati za jioni. Kwengineko si ajabu sana ungezisikia sauti kali za mbwa wakibweka ndani ya mageti yale...ITAENDELEA
 
RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 30
Mtunzi:Kelvin Mponda

Lakini kufuatia jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi taratibu za maisha ya kawaida ya wakazi wake zilikuwa zimebadilika. Majumba mengi ya kifahari katika eneo lile la Chausée P.L. Rwagasore yalionekana kubaki ukiwa kutokana na wakazi wake wengi kufunga majumba yao na kuondoka wakihofia kutokea kwa mapigano na umwagaji damu kati ya vikosi vya askari watiifu kwa serikali ya Rais Pierre Nkurunziza na vile vya waasi wanaotaka kuingʾoa serikali iliyoko madarakani.
Mvua kubwa ilikuwa imeanza kunyesha na giza nalo lilikuwa limeanza kuingia wakati nilipokuwa nikiegesha gari langu barabara ya mtaa wa pili mbele ya supermarket ndogo iliyokuwa imefungwa kwa wakati ule. Kisha nikachukua koti refu jeusi la mvua ambalo Hidaya alikuwa ameniandalia mle ndani ya gari na kulivaa. Bastola yangu ikiwa nyuma kiunoni nikashuka na kufunga mlango wa gari nikianza kutembea kuelekea mtaa wa pili yalipokuwa makazi ya Balozi Adam Mwambapa.
Pamoja na hofu kubwa ya kutokea kwa machafuko ya kisiasa nchini Burundi lakini mvua ile kubwa ya masika ilikuwa imechangia barabara nyingi za kitongoji kile kukimbiwa na watu. Hivyo wakati nikitembea nikajihisi kama kiumbe pekee niliyekuwa nimesalia kwenye sayari ya peke yangu. Sikuweza kuona gari wala mtu katika barabara za kitongoji kile ingawa hali ile haikutosha kunihakikishia kuwa nilikuwa katika mazingira salama.
Niliendelea kutembea nikizipita nyumba mbili za ghorofa upande wa kushoto hata hivyo nyumba zile zilikuwa na giza kana kwamba hazikuwa na wakazi wake kwa wakati ule. Nilipofika mbele nikaingia upande wa kulia nikiifuta barabara pana ya lami iliyokuwa ikipakana na maduka makubwa ya kisasa na ofisi ndogo ya posta. Nilipofika mwisho wa barabara ile nikachepuka na kuingia upande wa kushoto nikizipita ofisi za shirika moja la mtandao wa simu na duka moja kubwa la pombe za kisasa. Kwa kufanya vile nikajikuta nikitazamana na barabara tulivu ya mtaa wenye majumba ya kifahari yaliyozungukwa na miti mirefu na kuta zenye usalama wa uhakika. Barabara ya mtaa ule ilikuwa tulivu mno huku ikimulikwa na taa nzuri zenye mwanga mkali na hivyo kunifanya nijihisi kama niliyekuwa nikionekana vizuri na mtu yeyote aliyekuwa mafichoni akinitazama. Kwa mbali niliweza kuzisikia sauti kali za mbwa waliokuwa wakibweka katika nyumba za jirani na eneo lile bila sababu za msingi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Hidaya ni kuwa nyumba namba 26 aliyokuwa akiishi Balozi Adam Mwambapa ilikuwa ikipakana na nyumba ya makamu wa mahakama ya kikatiba ya nchini Burundi jaji Sylvere Nimpagaritse ambaye kupitia taarifa za awali zilizorushwa na kituo kimoja cha matangazo ya redio cha jijini Bujumbura zilikuwa zimeeleza kuwa jaji Sylvere Nimpagaritse alikuwa tayari ametoroka nchi na kukimbilia nchini Rwanda kwa kile alichodai kuwa yeye pamoja na majaji wenzake walikuwa wametishiwa maisha baada ya mahakama ya kikatiba kushinikizwa kumpitisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu kinyume na katiba.
Kulikuwa na miti michache ya vivuli kandokando ya barabara ile iliyofanikiwa kutengeneza giza hafifu hivyo kwa kukwepa kuonekana kwa urahisi nikachepuka na kuanza kupita chini ya miti ile.
Nyumba ya jaji Sylvere Nimpagaritse ilikuwa kiasi cha umbali wa hatua ishirini mbele yangu. Ilikuwa nyumba nzuri ya kifahari iliyozungukwa na miti mizuri ya vivuli na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatiwa vizuri. Ukuta wake kuizunguka ile nyumba ulikuwa mfupi na wenye nakshi za hapa na pale kiasi cha kumruhusu mtembea kwa miguu kuweza kuona mle ndani kwa shida kidogo. Taa zote za ile nyumba zilikuwa zimezimwa na hivyo kupelekea mandhari yake kutawaliwa na giza. Hata hivyo kupitia taa za barabarani zilizokuwa juu ya nguzo ndefu niliweza kuona sehemu tu ya mandhari yale ingawa uwepo wa giza na ukimya wa nyumba ile haikuwa kigezo tosha cha kunifanya niamini kuwa nyumba ile haikuwa chini ya uangalizi makini wa wanausalama wa nchi ya Burundi.Nilipoipita ile nyumba nikapunguza mwendo na kuanza kutembea kwa tahadhari huku mara kwa mara nikigeuka nyuma na kutazama kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia. Hali bado ilikuwa shwari hivyo nikazidi kufarijika.
Nyumba ya Balozi Adam Mwambapa ilikuwa umbali wa hatua chache mara baada ya kuipitia ile nyumba ya jaji Sylvere Nimpagaritse kwani nyumba zile mbili zilikuwa zikipakana na kutenganishwa na ukuta mrefu.
Hatimaye nikawa nimelifikia geti kubwa jeusi la ile nyumba aliyokuwa akiishi Balozi Adam Mwambapa hata hivyo ukuta mrefu uliofungwa sistimu maalum ya umeme wa kuzuia wezi juu yake haukuniwezesha kuona mle ndani. Nilipolifikia lille geti nikasimama na kushawishika kubonyeza kitufe cha kengele kilichokuwa pembeni yake lakini kitendo cha kuona viashiria vichache kuwa nyumba ile ilikuwa gizani kikanipelekea nighairi kwanza mpango wangu. Awali ya yote nilitaka kufahamu kwanza hali ya usalama wa eneo lile hivyo nikaachana kwanza na lile geti na kutembea kwa utulivu kandokando ya ukuta wa ile nyumba chini ya vivuli vya miti katika namna ya kufanya tathmini ya mazingira yale. Lakini vilevile nilitaka kuvuta uwepo wa kiumbe hai chochote ambacho kingekuwa eneo lile kikinitazama.
Hatimaye nikafika mwisho wa ukuta wa ile nyumba pasipo kuhisi uwepo wa mtu yeyote eneo lile. Hali bado ilikuwa shwari na kwa mbali niliendelea kuzisikia sauti za mbwa waliokuwa kwenye nyumba za jirani na eneo lile wakibweka japo nyumba zote za eneo lile zilikuwa zimetawaliwa na ukimya wa aina yake. Nilipoitazama saa yangu ya mkononi nikagundua kuwa ilikuwa tayari imetimia saa moja na robo usiku. Mvua kubwa bado ilikuwa ikiendelea kunyesha.
Baada ya kuridhika na tathmini yangu kwa tahadhari nikarudi tena kwenye lile geti mara hii nikiwa na dhamira moja tu ya kuingia mle ndani ya ile nyumba. Nilipolifikia tena lile geti nikasimama huku nikigeuka na kuyatembeza macho yangu huku na kule katika namna ya kujiridhisha na hali ya usalama wa eneo lile. Hali bado ilikuwa shwari na sikuweza kuhisi kitu chochote katika geti la nyumba ya jirani upande wa pili wa barabara lililokuwa likitazamana na lile geti la nyumba ya Balozi Adam Mwambapa. Hivyo nikaisogelea swichi ya kengele iliyokuwa ukutani kando ya lile geti na kubofya kitufe chake. Ile kengele ikaita kwa muda mrefu na hatimaye kukata pasipo mwitikio wa aina yoyote kutoka mle ndani. Takio lile likanipelekea nirudie kubofya tena ile swichi kwa mara mbili zaidi huku nikitarajia mtu yeyote kujitokeza na kunisikiliza lakini hilo halikutokea. Ile kengele ikaendelea kuita tena kwa muda mrefu pasipo mwitikio wowote kisha ikakata. Nikarudia zoezi lile kwa mara kadhaa kabla ya kujiridhisha kuwa nilikuwa nikipoteza muda wangu bure.
Mwishowe nikaamua kuachana na ile swichi ya kengele badala yake nikausogelea mlango mdogo wa lile geti huku bastola yangu tayari ikiwa mkononi. Lakini wakati nilipokuwa nikitaka kufanya vile mara nikashtushwa na sauti ya muungurumo wa gari lililokuwa likija upande ule hivyo nikachepuka na kujibanza kwenye kona moja ya lile geti nikiliacha kwanza lile gari lipite. Lilikuwa gari dogo aina ya Mitsubishi Wagon ya rangi nyekundu na dereva wa gari lile alipita kwa mwendo kasi uliomnyima fursa ya kutazama vizuri pale nilipojibanza na hali ile kwa kweli ilinitia faraja sana. Nikasubiri lile gari litokomee kabisa mbali na eneo lile na hapo kwa tahadhari nikausogelea tena ule mlango mdogo wa lile geti. Nilipofika nikakishika kitasa na kuusukuma ndani ule mlango taratibu kwa tahadhari ya hali ya juu. Ule mlango ulikuwa wazi tofauti kabisa na matarajio yangu na hali ile ilinishangaza sana.
Bastola yangu ikiwa mkononi sikutaka tena kurudi nyuma hivyo nikaendelea kuusukuma ule mlango taratibu katika namna ya kuuzuia usipige kelele na kumshtua mtu yoyote ambaye angekuwa mle ndani. Hatimaye nikaingia mle ndani na kuurudishia nyema yangu.
Kabla ya kufanya mjongeo mwingine wowote nikatulia pale getini nikiyatembeza macho yangu kupeleleza mandhari ya ile nyumba. Ilikuwa nyumba kubwa ya kisasa lakini siyo ya ghorofa yenye madirisha makubwa ya kisasa na baraza kubwa mbele yake iliyopangwa seti moja ya makochi ya sofa. Nje ya nyumba ile upande wa kushoto kulikuwa na banda la wazi la kuegeshea magari na nilipochunguza nikaona kuwa kulikuwa na magari matatu ya kifahari. Gari la kwanza lilikuwa ni Landcruiser V8 jeupe. Gari la pili lilikuwa ni Toyota Lexus RX ya rangi nyeusi na gari la mwisho lilikuwa ni Mercedes Benz E-class jeusi lenye milango sita ambalo niliamini kuwa lilikuwa ndiyo gari lililokuwa likitumiwazaidi na Balozi Adam Mwambapa kwa shughuli za kiofisi.
Sehemu nyingine ya mandhari ya nyumba ile ilizungukwa na miti mirefu na mikubwa ya kivuli hata hivyo matawi makubwa ya miti ile usiku ule yalikuwa yametengeneza vichaka vya giza la kutisha. Niliendelea kuitazama ile miti mikubwa kwa utulivu huku hisia zangu zikinieleza kuwa mtu yeyote mwenye hila angeweza kujibanza nyuma ya miti ile na kuitimiza adhma yake mbaya. Sehemu ya mbele ya ile nyumba ilikuwa imezungukwa na bustani nzuri ya maua ya kupendeza na katikati ya bustani ile kulitengenezwa njia nzuri ya kutembea kwa miguu kwa vitofali vidogo vinavyovutia. Njia kubwa ya gari ilikuwa imetengenezwa kwa ufundi mkubwa ikianzia sehemu ya getini hadi mbele ya ile nyumba inayomruhusu dereva ageuze gari pasipo kurudi nyuma.
Kwa sekunde kadhaa niliendelea kusimama pale getini huku nikiupisha utulivu kichwani mwangu na kitendo cha kuona taa zote za ile nyumba zikiwa zimezimwa kikaongeza ziada nyingine katika hisia zangu kuwa mle ndani ya ile nyumba hapakuwa na mtu yeyote hasa baada ya lile tukio la kutekwa kwa Balozi Adam Mwambapa. Lakini vilevile uwepo wa giza zito lililosababishwa na ile miti mikubwa iliyoizunguka ile nyumba ukanipelekea nihisi kuwa hali ile ingeweza kutumika vizuri na adui mwenye hila katika kutimiza adhma yake.
Hatimaye nikaondoka pale getini na kuzidi kusogea upande wa kulia wa lile geti sehemu kulipokuwa na kibanda cha mlinzi. Bastola yangu ikiwa imetulia vyema kwenye kiganja cha mkono wangu wa kushoto hatimaye nikakifikia kile kibanda cha mlinzi na kuanza kuchunguza mle ndani. Jambo lililonishangaza ni kuwa mlango wa kile kibanda ulikuwa wazi ingawa mle ndani kulikuwa na giza. Kwa tahadhari nikasogea karibu zaidi na kile kibanda na kuanza kuchunguza mle ndani huku mtutu wa bastola yangu ukitangulia mbele tayari kwa rabsha zozote.
Hatua moja tu niliyoitupa mbele yangu kuukaribia mlango wa kile kibanda ikapelekea pua yangu ijikute ikikabiliana na harufu nzito ya uvundo na hapo nikahisi mambo hayakuwa shwari. Hata hivyo sikusita badala yake nikausukuma mlango wa kibanda kile taratibu kwa mkono wangu mmoja huku mkono mwingine ukiidhibiti vizuri bastola tayari tayari kufanya shambulizi endapo mambo yangebadilika. Sikukutana na upinzani wowote kama nilivyodhani hapo awali lakini ile harufu ya uvundo sasa ilikuwa kali zaidi. Hapakuwa na dalili zozote za uwepo wa kiumbe hai mle ndani hisia zangu zikanitanabaisha vile hata hivyo kwa kutaka kujiridhisha zaidi nikachukua tochi yangu ndogo ya kijasusi aina ya Penlight yenye umbo kama la kalamu ndogo na kumulika mle ndani.
Taswira iliyojengeka machoni mwangu kwa sekunde kadhaa ikapelekea shughuli za mwili wangu zisimame kwa sekunde kadhaa huku moyo wangu ukiwa umepoteza kabisa utulivu. Miili ya askari wawili ilikuwa mle ndani ya kile kibanda. Askari mmoja alikuwa ameketi kwenye kiti mdomo wazi huku macho yake yakitazama juu. Mkononi alikuwa ameshika kiwambo cha simu ya mezani ambayo haraka nilipoichunguza nikahisi kuwa umauti ule ulikuwa umemfika wakati alipokuwa katika harakati za kufanya mawasiliano ya kuomba msaada. Nilipozidi kumchunguza askari yule nikagundua kuwa kulikuwa na matundu mawili ya risasi upande wa kulia wa shingo yake. Matundu yale ya risasi yalikuwa yamevuja damu nyingi na damu hiyo ilikuwa imetiririka na kuangukia sakafuni ikisambaa ovyo na kuganda.
Mlinzi wa pili alikuwa amelala chali sakafuni huku macho na mdomo wake vikiwa wazi na hivyo kumpelekea aonekane kama aliyekuwa akitazama kitu fulani kwenye dari ya kibanda kile. Mkono wake wa kulia ulikuwa umetuwama vyema juu ya bunduki yake SMG huku akionekana ni kama aliyekuwa katika harakati za kujibu shambulizi la adui wakati risasi mbili zilipomfumania vibaya na kutengeneza matundu mawili yanayovuja damu katika pafu lake la upande wa kulia.
Sasa nilifahamu kuwa harufu ile kali ya uvundo ilikuwa ikitokana na kule kuganda na kuanza kuoza kwa ile damu nyingi sakafuni. Loh! ulikuwa ni unyama wa aina yake kwani wale walinzi walikuwa wameuwawa kama kuku. Kwa sekunde kadhaa nikatulia nikijitahidi kukabiliana na taswira ile ya kusikitisha kabla ya kumeza fundo kubwa la mate kuipooza hasira iliyofurika vibaya kifuani mwangu. Hatimaye nikaanza kufanya upekuzi mle ndani hata hivyo nilimaliza upekuzi wangu pasipo kuambulia kitu chochote cha maana hivyo nikaamua kutoka nje ya kile kibanda.
Nikiwa nje ya kile kibanda nikaanza kutembea kwa tahadhari kuizunguka ile nyumba katika namna ya kupata uhakika wa hali ya usalama wa eneo lile. Giza zito lililofanywa na matawi makubwa ya miti ya vivuli iliyoizunguka nyumba ile likanipa nafasi nzuri ya kufanya mjongeo makini wa utulivu kama kivuli nikitoka mti mmoja na kuhamia mti mwingine. Nilikuwa na hakika kuwa mtu yeyote ambaye angekuwa eneo lile basi angehitaji kuwa na uzoefu wa hali ya juu wa mienendo ya sampuli ile ili kugundua uwepo wangu eneo lile.
Wakati nikikatisha chini ya miti ile nikagundua kuwa upande wa kulia wa ile nyumba kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea lililozungukwa na vitanda vizuri vya kujipumzisha chini ya miamvuli mikubwa ya kivuli. Nikaendelea kusogea zaidi na kisha kujibanza katika mti mmoja mkubwa uliokuwa jirani na lile bwawa la kuogelea huku nikiyapa macho yangu utulivu wa kufanya uchunguzi wa mazingira yale. Ingawa kulikuwa na giza zito na mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha lakini kupitia mwanga uliopenya juu ya ukuta wa uzio ukitokea kwenye nyumba ya ghorofa iliyokuwa ikipakana kwa nyuma na ile nyumba ya Balozi Adam Mwambapa niliweza kupata muono hafifu wa ndani ya lile bwawa la kuogelea.
Kulikuwa na kitu cheusi mfano wa kipisi cha gogo kilichokuwa kikielea kwenye maji ya lile bwawa. Mawazo yangu yakasimama kwa sekunde kadhaa wakati akili yangu ilipokuwa ikikazana kufikiri katika namna kutafuta tafsiri nzuri ya kitu kile kilichokuwa kikielea kwenye yale maji mengi ya lile bwawa la kuogelea. Kwa kufanya vile taswira ya Balozi Adam Mwambapa ikatumbukia katika fikra zangu haraka na kuibua mshtuko uliomezwa haraka na simanzi. Hata hivyo nikaitowesha haraka taswira ile kichwani mwangu kwa mwanga mkali na mwembamba wa kurunzi yangu ndogo ya kijasusi.
Maiti ya mlinzi mwingine wa eneo lile ilikuwa amevimba vibaya huku ikielea juu ya maji ya bwawa lile kama mzoga wa kiboko kwenye bwawa lenye kina kirefu. Nikazima kurunzi yangu haraka na kushusha pumzi taratibu huku nikiyafikicha macho yangu na kumeza funda kubwa la mate kuupooza mtima wangu. Hatimaye nikayaacha maficho yale na kuendelea na uchunguzi wangu nikikatisha katika giza zito lililosababishwa na ile miti mikubwa ya kivuli iliyopandwa kuizunguka ile nyumba.
Kwa muda mfupi tu niliyoshuhudia maiti tatu za walinzi wa ile nyumba ya Balozi Adam Mwambapa nilikuwa na kila sababu za kuyaamini vizuri maneno ya Hidaya kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa ametekwa. Kwa kweli nilisikitika sana japokuwa sikuweza kufahamu lipi lilikuwa lengo la wa watekaji hao. Kwa mtazamo mwingine ni kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa ni mwakilishi wa shughuli zote za Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na serikali yake nchini Burundi.
Hivyo niseme kuwa Balozi Adam Mwambapa alikuwa kiungo muhimu cha mahusiano baina ya nchi ya Tanzania na Burundi lakini vilevile alikuwa kiongozi mstaafu wa nafasi ya juu sana katika jeshi la wananchi wa Tanzania. Hivyo siyo tu kwamba alikuwa akizifahamu vizuri siri na mbinu nyingi za mikakati ya jeshi la wananchi la Tanzania lakini vilevile alikuwa amelitumikia jeshi hilo kwa miaka mingi ya maisha yake. Kwa hiyo nyadhifa zile mbili muhimu za uongozi wa ndugu Adam Mwambapa akiwa kama kiongozi mkubwa mstaafu wa jeshi la wananchi wa Tanzania na hatimaye kushika wadhifa wa kisiasa kama balozi wa Tanzania nchini Burundi...ITAENDELEA
 
Njoo ukichafue hukuuu kaka
Kumbe majasusi tupo wengi humu.
Lete vitu mkuu
Ila kwa uzoefu wangu wa kijasusi nimeshagundua kuwa waasi wa Burundi ndio watekaji. Ili awasaidie katika mikakati yao ya kufanya mapinduzi kwasababu balozi ni mtaalamu wa kijeshi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom