SEHEMU YA 48
ILIPOKOMEA...
Kwa sauti alisema, "Nilivyokwambia kuwa PAK ilikuwa ikiuzwa katika maduka makubwa, makubwa tu, sikuwa na maana kuwa nayajua maduka hayo. Namaanisha kuwa thamani ya PAK siyo ndogo. Ni vigumu kwa mtu mwenye kijiduka chake cha dawa kule Manzese, kuweka PAK akitarajia kuiuza ndani ya miezi sita."
***SASA ENDELEA***
"PAK inatengenezwa Athens, Ugiriki. Mwagizaji hana budi kuagiza katoni moja au zaidi, ikitegemea uwezo wake. Katoni moja ina chupa kumi na mbili za PAK. Mwagizaji analipa shilingi elfu sitini kwa chupa, na hapo bado hatujaweka vijiushuru vya bandari. Kwa jumla zitamgharimu pesa nyingi mwagizaji, si chini ya laki nane kwa katoni moja tu! Hapo sasa nd’o maana nakwambia kuwa siyo rahisi kwa muuzaji wa daraja la kati au la chini kuweza kuagiza PAK, kitu ambacho mauzo yake yanakwenda taratibu sana. Umenielewa?"
"Nimekuelewa, dokta," Ndonya alijibu kwa unyonge. Kisha akasimama bna kuanza kutoka. Mara tu alipogusa mlango, aligeuka na kusema, "Dokta, nashukuru sana kwa msaada wako. Mungu akipenda tutaonana tena."
"Ok."
Muda mfupi baadaye Ndonya alikuwa akivuka makutano ya barabara za India na Morogoro. Akawa akitembea kwa mwendo wa kikakamavu zaidi, akizidi kutokomea katikati ya mitaa hiyo ya Uhindini.
Hatimaye, baada ya kuyadharau maduka mawili ya dawa, aliingia katika duka la dawa lililokuwa Mtaa wa Kitumbini. Lilikuwa ni duka kubwa, zaidi ya maduka mengine mtaani hapo yaliyouza dawa kwa mfumo wa rejareja na jumla.
Wateja wasiopungua kumi walikuwa wakihitaji huduma kutoka kwa Mwasia mmojja mwenye tumbo kubwa. Ndonya alisimama, akiwa ni kati ya wateja hao ambao wengi wao walionesha dhahiri kuwa ni wanunuzi wa jumla. Kulikuwa na pilikapilika nyingi, kila mteja akionesha kuwa na haraka zaidi ya mwingine.
"Nipe katoni mbili za Panadol ya Kenya!”
“Oyaa…lete katoni moja ya Dakika Tatu!” wa pili ni kama alikuwa kifoka.
Mwingine alipaza sauti, “Paracetanol zipo?" hakusubiri jibu. Papohapo alinyoosha mkono wenye noti kadhaa huku akiamuru, "Toa katoni tatu haraka!"
Ndonya alikuwa miongoni mwa walioongeza idadi dukani humo, lakini hakuwa miongoni mwa wateja wa kawaida, waliohitaji bidhaa za kawaida. Yeye alikuwa na lake jambo. Akaishia kuziona bidhaa ambazo macho yake yalikwishazizoea na kinywa kilishazikinai. Zilikuwa ni dawa za kutibu maradhi, wala hakuiona hata sumu ya kuua panya, mende au wadudu wowote warukao au watambaao.
Akaendelea kuangaza huku na kule mithili ya mteja wa kawaida kama hao wateja wa kawaida. Hatimaye akaamua kumwita kijana mmoja ambaye jukumu lake kubwa lilikuwa ni kufuata ghalani katoni zilizoagizwa na mteja.
Kijana huyo alipomsogelea, Ndonya alitamka kwa mnong’ono, "Mkifunga duka saa saba, unikute pale kwa muuza mihogo ya kukaanga."
"Pale kwenye makutano ya mitaa ya Mosque na Mshihiri?"
"Hapohapo. Utapata lunch yako ya nguvu, siyo ile mihogo. Sawa?"
"Poa."
Kichwani mwa kijana huyo hakuwa na kumbukumbu yoyote kuhusu Ndonya. Hakumbuki aliwahi kuimwona wapi. Ni shinikizo tu la moyo wake kumtaka akubaliane na wito, japo alikuwa akihitaji kuhoji zaidi. Na aliamua kutohoji zaidi kwa wakati huo kwa kile alichoamini kuwa kitendo hicho kingezua hisia tofauti kwa bosi wake, mhindi yule mwenye tumbo kubwa.
*****
KWA Ndonya, utaratibu wa kula mihogo ya kukaanga ambayo hutayarishwa sehemu mbalimbali jijini Dar, hususan kando ya barabara, alishaucha tangu alipopata ajira yenye mshahara mnono na marupurupu kibao.
Sasa yeye alikuwa ni mtu wa kuingia katika migahawa yenye gharama kubwa, migahawa amayo mamilioni ya Watanzania wengine hawathubutu hata kuisogelea.
Lakini kwa siku hii, akizingatia kuwa tayari ameshawasiliana na yule kijana wa duka la dawa,alilazimika kuzikumbuka zile enzi zake. Ili aweze kuketi hapo kwenye biashara ya mihogo, ilimlazimu kuwa mteja halisi, jambo ambalo alilifanya.
"Mihogo miwili," aliagiza.
Dakika mbili au tatu hivi baadaye alikabidhiwa sahani ya mihogo iliyopondwapondwa na kuwekwa kachumbari juu yake. Hakuonesha kushangazwa na masizi yaliyoganda hapa na pale katika sahani hiyo. Ashangae? Ashangae halafu wateja wengine wanaokula mihogo hiyo nao wamshangae? Alikandamiza moyoni mshangao wake na kukiepuka kinyaa kilichomnyemelea kwa kasi ya kutisha. Akala mihogo hiyo taratibu, akivua muda katika kumsubiri kijana huyo.
Ni saa saba na robo kijana huyo alipotokea. Na Ndonya hakumchelewesha, aklimwita kando na kumnong’oneza, “Mtafungua saa ngapi?”
“Saa tisa kamili.”
Ndonya akachomoa noti ya shilingi 5,000 na kumpatia huku, kwa mnong’ono uleule, akisema, “Kuna suala moja muhimu. Tangulia pale Kili Hotel. Ukifika agiza chochote.”
“Poa.”
Dakika tano baadaye walikuwa pamoja Kili Hotel. Makoo yao yalikuwa yakishusha soda baridi matumbini mwao.
“Sasa nadhani tusipoteze muda,” Ndonya alianza. “Kuna kitu ambacho nakihitaji, na n’nadhani dukani kwenu kipo. Na kama hakuna hapo kwenu nadhani wewe utanipa mwangaza wapi pa kukipata.”
Kijana huyo alikunja uso na kumtazama Ndonya kwa mshangao. “Ni kitu gani hicho?” hatimaye aliuliza.
“PAK,” Ndonya alishusha sauti. “PAK inayotengenezwa Athens, Ugiriki. Unaifahamu?”
Kijana huyo alikuna kichwa huku akikodoa macho mezani. Kisha akamtazama Ndonya. “Naifahamu.”
“Naiweza kuipata?” Ndonya alimdaka.
Kijana akaguna. “Ni ngumu. Si unajua serikali I’shaipiga stop?”
"Hilo nalijua sana, dogo," Ndonya aliachia tabasamu la mbali. "Lakini pia najua kuwa bado ipo kwa wauzaji ingawa haiwekwi hadharani. Mimi naihitaji sana kama vile kuuhitaji Ufalme wa Mbinguni. Naitaka kwa gharama yoyote ile!"
Yalikuwa ni maneno yaliyomwingia vilivyo kijana huyo na kuchambuliwa akilini mwake kwa umakini wa hali ya juu. Picha ya noti nyingi za shilingi elfu kumi, kumi ikamjia akilini, noti ambazo angezimiliki baada ya mtu huyo kupata akitakacho.
"Naweza kuipata?" Ndonya alimshtua.
"Unaweza kuipata," kijana huyo alizinduka na kujibu kwa kujiamini.
"Una hakika?"
"Siku tanii. Mfuko wako tu."
Tabasamu la matumaini likachanua usoni pa Ndonya. Akanyanyua chupa ya Cocacola na kuipeleka kinywani. Akanywa mafunda machache kisha akairejesha mezani. Hatimaye, huku tabasamu likiendelea kuchanua, akasema, "Kama nilivyokwambia awali, ninaihitaji PAK kama ninavyotamani kuingia Paradiso. We nipe uhakika kama unaweza kuipata leo hii!"
"Unaweza kuipata!" kijana yule alisisitiza. “Kuipata s’o tatizo. S’o tatizo kabisa. Muhimu ni mkwanja tu!”
“Kiasi gani?”
“Siyo nyingi, fanya milioni tu.”
Ndonya alitokwa macho. Mwonekano wa kijana huyu haukuwa wa mtu wa kutamka kiwango hicho. Ndonya alitarajia kuambiwa atoe labda shilingi laki moja au mbili tu. Kiwango alichotajiwa, aliona ni kikubwa sana.
"Milioni moja?!" alimuuliza kijana huyo kwa mshangao.
"Nd’o maana'ake."
"Hapana, shusha kidogo mdogo wangu. Nitakupa shilingi laki tatu."
Kijana huyo akaachia cheko la dhihaka, cheko la kujiamini. “Sifanyi biashara hiyo, kaka. Kwa laki tatu labda kazunguke kwingine, labda utabahatisha. Na ukienda kichwakichwa kuuliza kwa kila mtu, utajikuta unadakwa na askari.”
Ndonya alikunja uso kidogo. Akamtazama kijana huyo kwa makini na kuubaini msimamo mkali uliodhihirika usoni pake. “Siki’za dogo,” hatimaye alisema kwa mnong’ono uleule “Hili ni dili lako we’ binafsi. Hakuna cha mhindi wako wala nani. Upo?”
***ITAENDELEA***
Sent using
Jamii Forums mobile app