SEHEMU YA 14
TULIPOKOMEA.....
Kilichomtia kiburi zaidi Kibutu ni milioni kadhaa zilizokuwa bado ndani ya begi lake ambalo hakuling’atua begani hata alipokuwa kaketi. Milioni moja aliyoitenga sasa ilikwishapungua na kubaki laki kadhaa. Hata hivyo aliamini kuwa kwa Scolastica atalainika tu, atake, asitake. Atamwomba radhi na atampa laki kadhaa za kumpoza. Atakataa? Hawezi!
Kiburi cha Kibutu kilikuwa katika ubora wake!
****ENDELEA****
“Nilishindwa kuvumilia, Scola,” alizungumza mwishoni mwa risala yake. “Ningefanya nini wakati nilikuwa nikikuhitaji sana na wewe ukawa unanipa majibu ya kuudhi? Lakini hayo tuyaache, Scola. Yamepita. Nakuomba sana radhi kwa yaliyotokea. Na siyo tu kwamba nakuomba unisamehe, bali pia nakuomba upokee kitu kidogo nilichonacho katika kuthibitisha kuwa ninakupenda na nilichokifanya nakijutia.”
Scolastica aliuinua uso na kumtazama kwa macho makali. Kisha akamuuliza, “Unataka kunipa nini?”
Tazama ya Scolastica haikuwa na amani hata chembe. Kibutu alilibaini hilo, lakini hakubabaika. Bado alikuwa na ule ujasiri uliosababishwa na milioni mbili zilizohifadhiwa ndani ya begi na laki saba na ushei zilizokuwa ndani ya mfuko mmoja wa suruali.
Alichoamini yeye ni kwamba, Scolastica ni mwanamke tu, ambaye huenda anaishi kwa kutegemea mshahara wa mwezi, huenda labda na vijisenti vya kuhongwa na hawara. Hakujua kuwa alikuwa akifanya kazi, na wala hakuwa na haja ya kujua, ila tu alijenga imani hiyo. Kwa jinsi akili yake ilivyomtuma, alihisi huenda Scolastica analipwa mshahara usiozidi shilingi lake nne au tano kwa mwezi.
Kama atakuwa analipwa kiasi hicho cha pesa, atakuwa na uwezo wa kukataa fidia ya laki kadhaa atakazokabidhiwa usiku huo? Uwezo huo hana, Kibutu aliendelea kuamini hivyo. Hivyo, akiwa hatishwi na swali pamoja na huu utazamaji wa Scolastica, alimjibu, “Nataka kukufidia kidogo.”
Scolastica aliendelea kumtazama kwa makini. Alipoyamisha macho ni pale tu alipoishika chupa ya bia na kunywa funda mbili kubwa za bia kisha akairejesha mezani. Akamrudia Kibutu.
“Sijakuelewa, ujue?”
Kibutu aliamua kukisogeza zaidi kiti chake kwa Scola. Wakawa jirani zaidi na huenda hakutaka wanachoongea kinaswe na yeyote asiyehusika. Akilini mwake aliamini kuwa shilingi laki tano zingetosha kumlainisha Scolastica. Laki tano za mkupuo kama fidia kwa tukio la zaidi ya mwezi mzima uliopita, tukio ambalo huenda hata halimtii uchungu tena mtendewa, si zitakuwa kama pesa za bure?
Akiendelea kujiamini kwa kiasi kikubwa, akasema, “Nimeona nikufidie kwa kiasi kidogo cha pesa.”
“Fidia?” Scolastica aliendelea kumkazia macho.
“No,” Kibutu alijisahihisha. “Tuseme ni kama pole tu. Ni kiasi kidogo tu Scola. Haiwezi kuwa fidia, lakini naomba tu uipokee.”
Hii harufu kali ya jasho kutoka kwa Kibutu ilikuwa ni kero ambayo Scolastica alilazimika kuivumilia. Alijua hii ni kero ya muda, itapita tu. Kimoyomoyo akawa akicheka, pia akilia.
Kumbukumbu sahihi ya ile siku isiyosahaulika kule Komakoma, ilimjia na kumfanya awakumbuke wale wenzake Kibutu, ambao mmojawao alimtamkia maneno ya dharau na kumlazimisha aondoke huku pia akiwa ameshinikizwa azivunjevunje laini za simu yake!
Sasa aliamua kumsikiliza na kwenda naye sambamba huyu Kibutu, auone mwisho wa kilichomleta hapa mezani. “Hiyo pole yako ni kiasi gani?”
Kibutu aliingiza mkono mfukoni na kuchomoa bunda zito la noti. Akatenga mafungu saba ya shilingi laki moja, moja. Akamkabidhi Scolastica shilingi laki tano kwa namna ambayo hakutaka macho yasiyohusika yashuhudie. Laki mbili akazirejesha mfukoni. Kisha kwa sauti ya chini, yenye kijimkwaruzo kilekile cha kilevi, akanong’ona, “Ni laki tano.”
Ulikuwa ni mnong’ono ulioyafikia masikio ya Scolastica kwa usahihi. Akawaza, azichukue au aziache? Papohapo akajiambia kuwa utakuwa ni ujinga kuziacha laki tano za bure. Akilini mwake, alipata picha kuwa Kibutu anajiona kampa pesa nyingi sana za kuweza kumfanya ababaike na kumsujudia.
*****
NUSU saa baadaye, walikuwa kama wapenzi wa muda mrefu. Laki tano zilizokuwa ndani ya mkoba wa Scolastica zilimwongezea hasira na kujiamini zaidi. Oda ya nyamachoma ikatolewa. Vinywaji vikaendelea kutua mezani.
Scolastica hakujali pale Kibutu alipodiriki kumpapasa paja. Ya nini kujali ilhali alikuwa hapo kwa malengo maalum? Hakujali kupapaswa, alichojali ni kutouruhusu ulevi kichwani mwake na kujali muda.
Kwa upande wa Kibutu, akilini mwake aliamini kwa kuwa tayari laki tano zilishaingia kibindoni mwa Scolastica, basi hakuna litakaloshindikana. Fedha ni uchawi wa kipekee, aliwaza. Hatoki mtu hapa mpaka kieleweke, alijiapiza.
Wakati akijiapiza hivyo, hakujua mwenzake alikuwa akiwaza nini. Akiwa ni mwanamke aliyejiamini kwa kiwango cha juu, Scolastica akitumia akili za darasani, akachanganya na za kuzaliwa, alikuwa mtulivu na makini katika kufuatilia kila kilichofanya na kusema na Kibutu.
Pamoja na hoja hii na ile kuzungumzwa, hata hivyo Scolastica hakuwa mbumbumbu, alijua Kibutu anakoelekea, hivyo hakushangaa alipomsikia akipendekeza kuhusu kuwa wote usiku huo hadi kunakucha.
Lilikuwa ni pendekezo lililokaribia kumchekesha Scolastica, kicheko cha wazi, lakini hakuwa, mjinga kiasi hicho. Aliendelea kucheka na kulia kimoyomoyo. Kwa kufuata zile ambazo zilishachukuliwa kama kanuni, Scolastica alipingana na pendekezo hilo. Mwananke hapaswi kukubali papohapo atongozwapo na mwanaume, vinginevyo ataonekana ni malaya.
Scolastica naye aliifuata imani au kanuni hiyo, lsakini Kibutu hakukubali; alisimama kidete. Mwanaume akabembeleza na kubembeleza, kiwangocha pombe aliyokunywa kikizidi kumwongezea morali ya kutaka kile alichokikusudia. Hatimaye, akiataka kuhakiiiksha hakosi anachokitaka, akaitupa laki moja mapajani kwa Scolastica.
Scolastica akamtazama Kibutu kwa huruma, hiyo lakini nayo ikiingia mkobani. Siachi kitu, alijisemea moyoni. Dakika chache baadaye mzizi wa fitina ukakatwa. Scolastica akatoa tamko. Kibutu akakaribia kuwehuka kwa furaha!
Wakati Kibutu akifurahia kupewa kibali kwa burudani ya usiku huo, Scolastica alikuwa akilichekea moyoni pato lake.
Laki sita kiimchezomchezo tu!
Saa nne kasoro dakika chache, Kibutu alipendekeza waondoke. Kwa jumla hakuwa na shida tena ya kuwa ndani ya hiyo baa. Alikunywa bia na pombe kali za kutosha, alichohitaji sasa ni kupata burudani na mrembo Scolastica.
Alishajiwekea utaratibu wa kutokwenda baa na teksi yake usiku. Alihofia kuzidiwa na kilevi na kushindwa kuendesha kwa ufanisi. Hivyo, hata alipokuwa hapo Mood Bar siku hiyo, alikuwa amekwishaegesha gari sehemu fulani anakolipia egesho. Alipotupa macho kule kaunta akawaona wale vijana bado wapo. Akamwita mhudumu mmoja na kumtaka akamwitie mmoja wa vijana wale.
Dakika mbili, tatu baadaye kijana mmoja alikuwa mbele yake.
“Hamidu, niko na shem wako,” alimwambia kimadaraka. “Please, kanitafutie usafiri hapo nje. Siyo bodaboda au bajaji. Tafuta teksi, tena ya maana siyo lingalangala linaloweza kufia njiani.”
Kijana yule alipoondoka, Scolastica aligugumia bia yake na kuirejesha chupa chini. Kisha akamwambia Kibutu, “Kama tunaondoka kwa nini tusichukue na bia mbilmbili za kumalizia huko kwako?”
Kibutu hakupinga, hakuwa mtu wa kupinga pendekezo lolote la Scolastica, ilimradi kishamkubalia kuumaliza usiku wakiwa pamoja! Nani kama yeye? Kwa nini asiione siku hiyo kuwa ni ya kipekee?
Wakati wakiifuata teksi nje, mfuko wenye bia nne, mbili za Scolastica na mbili za Kibutu ulikuwa umeshikwa na mkono wa kulia wa Scolastica.
Safari ya Komakoma!
***ITAENDELEA KWA HISANI YA
Madame S ***