NITAKUPATA TU
Sehemu ya O90
Akatulia kuwasubiri watu hawa. Kitambulisho maalum tayari kilikuwa mkononi kuwaonyesha watu hawa. Kitambulisho ambacho kingemuonyesha yeye alikuwa nani katika nchi hii. Watu wale wakasogea huku bunduki zao zikiwa tayari kwa chochote. Mmoja akasogea kwa Tahadhali mpaka dirishani mwa gari ya Mwanaharamu. Kabla Hajagonga kioo Cha Mlango wa gari, kioo kikashushwa.
"Habari yako Ndugu?. Sauti ya Mtu huyu aliyeonekana ndiye mkuu katika kundi hili akauliza. "Salama tu, habari yako!" Alijibu kisha kuuliza. "Tunaomba ushuke tuweze kupekua gari yako." Bila kujibiwa salamu yake amri ikatoka. Wakati bado akifikiria kile cha kujibu. Akashuhudia watu wale waliopembeni wakisogea. Hakutaka kuchelewa wala kuupoteza muda. Kitambulisho kikaonyeshwa. Mkuu yule akakitizama Mara mbili mara tatu. Akakirudisha huku akiomba msamaha kwa kilichotokea. Kitambulisho chake kilichomtambulisha Kama Jasusi Wa CIA kilitosha kuwaaminisha wana usalama hawa kuwa mtu huyu hakuwa mmoja kati ya waliofanya kilichotokea. Bila kujibu akapandisha kioo na kuliondoa gari kwa mwendo wa Taratibu. Tayari mipango yake ilikuwa imefeli lakini kwa kilichotokea alihisi ilikuwa njia bora ya kuwafanya watu hawa waanze kuweweseka. Ingawa nia yake ilikuwa ni kumteka mtoto wa Rais ili kumshurutisha Baba yake aitoe Betri maalum. Lakini hata hili lililotokea halikuwa baya. Halikuwa baya kwa kuwa alijua mapambano ndiyo yatakuwa magumu. Alipenda sana kupambana Kwenye uhatari. Alipenda sana kupambana kwenye ugumu. Na mwisho alipenda sana kuonyesha kuwa yeye alikuwa nani katika medani hii ya kimapambano. Gari ikatembea akipanga muda huu kwenda kuanza kufuatilia Wapi walipopelekwa watoto wa Masimba. Hakutaka kupumzika mpaka pale atakapopata taarifa ya kumuwezesha kufahamu walipo watoto. Alitembea usiku ule akipishana na Askari wa vikosi mbalimbali vya majeshi ya Ulinzi na Usalama. Moyoni kwake aliumia sana Baada ya kuwaza kuwa wanajeshi na polisi wetu walikuwa wamejiingiza katika Siasa. Taaluma yao na Sheria zao kama vyombo vya ulinzi walisahau kabisa. Sasa hivi hata Askari walikuwa ni wanasiasa. Aliendelea kuendesha gari huku akiendelea kuumizwa na hilo.
********
Alijiinamia peke yake ndani ya chumba kile cha hoteli. Alikuwa amejiinamia Akiwaza na kuwazua kila kitu alichopoteza kwa kuipigania nchi yake. Alikumbuka watu waliopotezwa na suala hili. Alimkumbuka Marehemu Asteria. Msichana ambaye aliuawa mwanzo tu mwa mkasa huu. Akamkumbuka Dee plus na mama yake mzazi. Akawakumbuka vijana ambao walikuwa wakiteseka katika hilo, vijana ambao waliendelea kuteswa na kuumizwa kwa matumizi ya madawa. Akamkumbuka Teddy kwa mara nyingine. Tukio la kumiminiwa Risasi na teddy likajirudia taratibu. Ni wazi kuwa teddy alikuwa amezamilia kumuua. Ni kweli teddy alikuwa Tayari kumuua. Kama sio kuondoka Eneo husika basi risasi zisizopungua tano zingeuchakaza mwili wake. Kufikia hapo akatulia Zaidi akifikiria. Ilikuwa lazima apambane na ilikuwa tayari aondoke usiku ule kwenda kuianza kazi. Haikuwa sahihi kwake kuendelea kukaa hapo ndani wakati tayari Betri ipo mikononi mwa Rais. Akainuka na kusimama katikati ya chumba. Lakini kitendo cha kusimama akajikuta akipatwa na kizunguzungu. Kizunguzungu ambacho kilimlazimu arudi pale kitandani. Ilikuwa wazi kuwa hawezi kupambana na hawezi kwenda mstari wa mbele. Akarudi kitandani huku akiruhusu chozi lake kushuka. Alikuwa akilia taratibu. Alikuwa akiipigania nchi yake, alikuwa akiwasaidia wananchi wasio na uwezo. Lakini kitendo cha rais kumgeuka kilimtesa na kumsumbua kichwani. Safari hii akawaza kitu ambacho hapo mwanzo hakuwahi kuwaza. Aliwaza kumuua Rais, alipanga kumuua rais sambamba na teddy. Huo ndio uamuzi ambao alioupitisha. Ni Lazima risasi itumbukie kwenye uso wa Rais. Alikuwa tayari kwa hilo. Alikuwa tayari muda wowote. Alimchukia Teddy na pia alimchukia Rais. Hakuona kama Ni kiongozi ambaye angeweza kuliongoza Taifa hili. Akajikuta hali ile ya kupoteza nguvu ikiwa tatizo kwake. Tatizo lakutokukifanya kwa wakati ule ambacho alikipanga kukifanya. Ilimuumiza sana hali ile. Kila alipokuwa akiitizama picha ya rais ambayo iliwekwa ndani ya kile chumba ndipo hapo hasira zilivyozidi kupanda. Alitamani kuinuka muda ule ule kumfuata mtu . Kitendo cha kushirikiana na majasusi wa CIA na serikali ya marekani kuwaharibu wananchi kilikuwa kitendo ambacho alikichukia. Kitendo ambacho kilitokea kumuona kiongozi huyu wa nchi kuwa hapaswi kuishi pamoja na Teddy na hata Jimmy. Wakati akiliwaza hilo pale chumbani mara akashtushwa na Taarifa kutoka kwenye TV pale chumbani. Taarifa iliyokuja kama Habari mpasuko (Breaking news) kwamba Mtoto wa Rais alikuwa ameuawa kwa kupigwa Risasi kichwani akiwa na Mpenzi wake. Habari ikaongeza kuwa muuaji aliufanya unyama huo wakati walinzi wa mtoto huyo wa Rais wakiwa ndani. Kwa Taarifa Zaidi endelea Kufuatilia HANDENI TV kukujuza kila kitakachoendelea Hakuamini macho yake na hata masikio yake. Ingawa kifo hakifurahiwi lakini kwa mara ya kwanza Masimba akatabasamu. Akatabasamu akitingisha kichwa. Akajua hii ilikuwa kazi ya mwanaharamu, alijua hii ilikuwa kazi ya mwanaharamu huyu aliyelaaniwa. Akauona ushindi kwa mbali ukijisogeza. Kumuua mtoto wa Rais ulikuwa ujumbe tosha kwa Serikali na Vibaraka wake. Hakuna Ujumbe mzuri na mtamu katika vita ya Akili kama Ujumbe wa Damu. Sasa Rais alikuwa ametumiwa Ujumbe wa kumwambia Bado mapambano yanaendelea. Akajilaza kitandani Taratibu Akiwa katika tabasamu mwanana. Alitamani apone ili amkabili Teddy, alitaka kumuua Teddy kwa Mikono yake mwenyewe. Mkono uliomuua Waziri mkuu ndio Mkono ambao utamuua Teddy. Ilikuwa ni lazima Teddy Afe. Ni lazima betri ipatikane kuwaokoa vijana wanaoendelea kupotea. Kuliwaza hilo kwa muda likamfanya aukumbuke mzigo wa madawa wa mamilioni ya Shilingi aliyoyachukua Mikononi kwa watu hawa. Ilikuwa ni lazima akauone na Kuupata. Lakini hakutaka kuwa na Haraka Zaidi ya kuivuta subira. Ni kweli alitulia ili kuivuta subira.
*****
Paja zake nzuri zilikuwa wazi zikionekana pasipo na kificho. Alikuwa ametulia pembezoni mwa ukumbi wa msasani club akipata vinywaji huku kivazi chake kifupi kikiyavuta macho ya wanaume wakwale. Macho ambayo hayakuondoka katika paja za mwanamke huyu ambaye hakujali kutizamwa. Kunawakati alikuwa akiiachia miguu yake makusudi na kusababisha hata nguo yake ya ndani kuonekana. Aliumbwa akaumbika, alipewa na kulidhika na hata kupendelewa na kukubali. Alikuwa na macho mazuri na yakuvutia katika Usiku. Midomo na Dimpoz zake unaweza kumfaninisha na mwanadada mwenye umbo tamu Kama Tumosa. Miguu yake ilipendeza na kuvutia. Bado macho ya Wanaume Wa Kwale yalikuwa Yakipita Juu ya paja zile. Wanaume ambao walikuwa wakipagana vikumbo kwa macho kumtizama mwanadada yule. Hakuwa mwingine huyu kiumbe, bali alikuwa Veronica Senka. Alikuwa hapo kwa sababu ya kumhitaji Jimmy Lambert. Alikuwa hapo akitaka kuipeleka tiketi kwa mtu huyu. Mtu huyu ambaye mkono wake ulikuwa na watu hawa. Mtu huyu ambaye aliubadilisha ubongo wa Mtoto Wa Kipare. Mwanaume huyu ambaye alikuwa jasusi wa kutupwa akitumika kama wakala wa Siri wa CIA. Alikuwa hapo akiamini mtu huyu hawezi kukosa kufika hapo. Akaendelea kujiachia akionyesha kutokujali. Kila wakati alikuwa akitizama saa yake. Wakati hilo likiendelea, punde akaonekana mhudumu wa Mahala pale Akisogea pale alipokaa. Veronica Akafanya kama hakumuona, akaendelea kumimina kinywaji kinywani. Mhudumu yule alipofika akauonyoosha mkono na kumkabidhi Veronica kikaratasi kidogo. Bila kuongea kitu Veronica akakipokea kisha kukikunjua pale pale. "Nakuomba Hapa ndani." Ni maandishi yaliyoandikwa yaliyomfanya atabasamu. "Ananiomba Niingie ndani? Lilikuwa swali ambalo hakutaka kulijibu. Akainuka na Bia zake mbili mkononi Taratibu Akasogea sehemu ambayo alitakiwa. Baada ya kufika kwenye meza hiyo ambayo alikuta imekaliwa na kijana mmoja mmoja hivi, Veronica Naye akakaa hapo muda huu akionyesha kuyumba. "Karibu Mrembo wangu karibu sana." Alitamka kijana yule akimpa mkono Veronica. Veronica Akaupokea mkono, kisha kwa sauti ya kilevi akanena. "Ahsante Sana Kijana mzuri wa Sura. Inaonekana hata kitandani uko vizuri." Maneno hayo yalimfanya kijana huyu atabasamu, tabasamu la kuvutia ama kufurahishwa na maneno yale.
"Hapana mrembo, miye kitandani nipo sifuri kabisa."akajibu tena huku akiushika mkono wa Veronica. "Mh!! Wifi ndiye anaujua ukweli." Akajibu Veronica huku kwa mara nyingine akitupia jicho kwenye Saa yake. "Naitwa ADK, ni mfanyabiashara wa Mahindi na maharage. Naishi mikocheni." Akajitambulisha Kijana Yule. "Naitwa Rehema, naishi Mwananyamala kisiwani. Akajibu Veronica Huku mara hii akiruhusu macho yake ya kurembua yamtizame Kijana huyu. Ni kweli macho yao yakaangaliana. Tofauti na kijana huyu kusema kuwa anafanya biashara, veronica aligundua kitu kingine kabisa machoni mwa kijana huyu. Alikutana na macho ya Ulaghai, macho yanayotambulisha kitu kingine kabisa. Macho yanayomwambia kuwa Mtu huyu ni Mmoja wa watu wale ambao hawakutakiwa kujulikana. Yaani alikuwa jasusi wa kutupwa. Kingine ambacho Veronica kilimvutia kwa huyu kijana ni kule kuyapeleka macho yake sehemu fulani katika namna ambayo Kama ungekuwa Mtu Wa Kawaida basi usingegundua kitu. Ni Sehemu Hiyo ambayo ilimpasa hata yeye kutizama huko. Kutizama katika namna ambayo mtu huyu hakuwez kung'amua Chochote kile. Ni hapo alipomuona Yule ambaye alimhitaji. Alimuona Jimmy Akiwa ametulia pembeni kabisa mwa ukumbi Ule. Taratibuuu Akatabasamu. Tabasamu ambalo halikugundulika machoni kwa kijana huyu aliyejipachika ufanya biashara. "Sawa bibie Rehema, naweza kusema leo nina Bahati kubwa sana kukutana na wewe." Baada ya kuongea hilo akapiga fundo moja la bia kisha kuitua glasi pale mezani, kisha akaendelea. "Licha ya kuwa na bahati hiyo, lakini naona bahati hii ni ya bosi wangu." Alipomaliza kuongea Hilo akamuangalia Veronica usoni. Kwa kujua kuwa mtego wake ulikuwa unakwenda kunasa. Veronica alikuwa amelilegeza jicho na hata miguu. Akatuliza macho yake machoni kwa kijana yule. Akamuona kijana alivyokuwa akihangaishwa. Hakujua kuwa alikuwa Akiongea na mtu hatari, hakujua kuwa alikuwa akiongea na Mtoa Roho. Vero akaruhusu macho ya kijana huyu yaendelee kukiona kile alichokikusudia. Hilo ndilo lililompa kile ambacho alikuwa akikihitaji. Punde akamuona Kijana yule akiinuka huku mambo yakiwa sio mambo.
Zijapita kama dakika mbili pasipo mtu huyu kurudi. Wakati akilishangaa hilo. Akamuona yule yule mhudumu wa kwanza akisogea pale mezani kwake. "Unatakiwa Uingie Upande Wa Nyumba ya Kulala Wageni. Nifuate." Aliongea mhudymu yule huku akigeuka kuelekea kule ndani. Veronica hakuchelewa. Muda huu alikuwa amesimama akimfuata Mwanadada yule kwa nyuma. Macho yake yalikuwa yakizunguka huku na huko kuona kama alikuwa akisindikizwa. Ni kweli alikuwa akisindikizwa, akisindikizwa na macho ya wanaume wa kwale. Katika macho hayo kulikuwa na macho mengine ambayo hayakumuangalia kama macho ya wengine. Haya yalikuwa macho maalum. Macho ambayo Yalitaka kitu tofauti zaidi ya mapenzi. Veronica hakujali. Akaongoza ndani akitembea kwa Mwendo wake Wa pozi.
********
Alisimamisha gari kwenye maegesho ya Magari Nje ya ukumbi wa Msasani. Akashuka na kuufunga mlango kisha kuongoza kuelekea pembezoni mwa ukumbi. Wakati akikaribia sehemu husika. Akamuona Veronica akiwa amejiachia. Hapo akagundua Veronica alikuwa kwenye mtego. Alikuwa kwenye mawindo. Mwanaharamu akamkwepa kwa kupitia upande mwingine. Hakutaka waonane na Veronica. Alitaka kufuatilia ama kukiona kile alichokiona veronica. Wakati akiendelea kutulia upande tofauti na Veronica. Macho yake yakamuona Jimmy akiwa sambamba na mtu mmoja pamoja na mhudumu. Hazikupita hata sekunde thelathini akamuona Mhudumu yule akisogea sehemu aliyokuwa amekaa Veronica. Mwanaharamu bado aliendelea kutulia hapo. Hata pale alipomuona Veronica akiingia kwa ndani. Hata yeye akafanya hivyo. Hata pale alipokuwa akiongea na yule kijana, bado mwanaharamu aliendelea kumuangalia tu. Wakati kijana yule alipoinuka na kumuacha Veronica pale. Hata Mwanaharamu naye akasimama. Wakati kijana yule anampita Jimmy na kumpa ishara fulani. Mwanaharamu Alishuhudia kila kitu. Akatambua kuwa Hapakuwa na Usalama upqnde Wa veronica. Ilikuwa ni lazima afanye kitu. Ni kweli alikifanya. Punde tu alikuwa akitembea sambamba na kijana yule aliyekuwa akiongea na Vero.